Elections 2010 Kimfaacho JK ni asasi za hisani, si urais!

Jan 16, 2007
721
176
Kimfaacho JK ni asasi za hisani, si urais!


Mwandishi Wetu
Oktoba 6, 2010

KATIKA miezi ile ya mwanzo baada ya kuingia Ikulu, Rais Jakaya Kikwete aliwashangaza wengi alipoitangazia dunia kwamba haelewi ni kwa nini Tanzania ni masikini.

Huo ukawa ndiyo mwanzo wa mfululizo wa kutoa kauli tata ambazo zimeacha baadhi yetu tuingiwe shaka na uwezo wake wa uongozi.

Kwa hakika, kauli ile ya kwamba haelewi ni kwa nini Tanzania ni nchi masikini iliibua mjadala mkubwa, kwenye mitandao, ndani na nje ya nchi; huku baadhi wakijiuliza ni vipi angeweza kuiondoa nchi katika umasikini ikiwa yeye mwenyewe hajui ni kwa nini nchi ni masikini.

Wengine walikwenda mbali zaidi na kuhoji ni vipi aliamua kugombea urais ikiwa hata sababu za umasikini wetu hazijui. Kocha anawezaje kupewa kazi ya kuifundisha timu kama hata udhaifu wa timu yenyewe haujui?

Hiyo ilikuwa miaka mitano iliyopita. Leo, ukizisikiliza ahadi ambazo Jakaya Kikwete anazitoa kila anakopita mikoani kwenye kampeni zake, unaweza kupatwa na mshtuko kama ule uliotupata baadhi yetu tulipoisikia kauli yake ile ya mwanzo kabisa kwamba hajui kwa nini tu masikini.

Hebu fikiria: Rais ambaye serikali yake ilishindwa ku- fix uchumi katika miaka mitano ya utawala wake, anawezaje leo kuwaahidi Watanzania kwamba atajenga reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa itakayotumiwa na treni za kisasa zinazokwenda kasi?

Kama vile hiyo haitoshi kukuacha hoi kwa mshangao, Kikwete akaongeza tena kwamba mradi huo wa kujenga reli mpya, itakayotumiwa na treni za kisasa ziendazo kasi, ataukamilisha ndani ya miaka mitano tu ya awamu yake ya mwisho ya uongozi!

Lakini mradi huo mkubwa na ambao lazima ni wa mabilioni ya dola si pekee ambao Kikwete ameahidi kuukamilisha ndani ya miaka yake mitano ya uongozi iwapo atachaguliwa tena kuwa rais oktoba 31.

Ipo mingine kabambe kama vile kujenga barabara za juu Dar es Salaam (fly-overs), kupeleka maji ya Ziwa Victoria hadi Tabora, kununua meli kubwa na za kisasa Lake Victoria na Nyasa, kujenga bandari kubwa na za kisasa huko Bagamoyo, Tanga (Mwambani) na Mtwara, na pia kujenga uwanja mkubwa wa ndege huko Kigoma.

Lakini pia upo utitiri wa ahadi nyingine kama vile kujenga kwa viwango vya lami barabara kadhaa ndefu nchini, kujenga chuo kikuu Shinyanga nk nk! Na bado anaendelea kutoa ahadi nyingine katika kampeni zake huko mikoani. Sijui zitafika ngapi ifikapo Oktoba 29.

Sasa, sisemi kwamba haiwezekani kabisa miradi hiyo yote kukamilishwa katika kipindi cha miaka mitano (ingawa sikumbuki Wajerumani walichukua miaka mingapi kujenga reli ya Dar –Kigoma). Hakika, kama nchi ni tajiri na ina mabilioni ya pesa za kigeni katika hazina ya taifa, hiyo yawezekana kabisa.

Lakini ninachojiuliza mimi, na ninachohoji ni kuhusu wapi mabilioni yote hayo ya pesa ya kukamilisha miradi hiyo mingi yatapatikana katika kipindi cha miaka mitano tu ijayo ya utawala wake kama atashinda uchaguzi Oktoba 31.

Najiuliza hivyo nikizingatia kwamba hata bajeti yenyewe ya Serikali ya CCM ina kawaida ya kuwa na nakisi ambapo 2009/2010 ililazimika kukopa benki ya biashara – Standard Charter).

Najiuliza hivyo nikizingatia pia kwamba hata uchumi wenyewe wa nchi haukui kwa kasi ile tuliyoahidiwa mwaka 2005; achilia mbali ukweli kwamba yetu ni nchi ambayo bado ina raia wanaoshindia mlo mmoja kwa siku kwa sababu ya umasikini.

Najiuliza hivyo nikizingatia pia kwamba mwakani serikali itaingia gharama nyingine kubwa ya ziada ya kuendesha wilaya mpya 21 ambazo serikali yake imeziunda, na ambazo zitaanza kazi rasmi Julai mwakani.

Ni wapi, basi, ambako Jakaya Kikwete, ghafla, amevumbua hazina itakayomwezesha kukamilisha miradi mikubwa kama hiyo ya mabilioni ya pesa katika kipindi kifupi cha miaka mitano tu?

Ni muhimu kujiuliza swali hilo, kwa sababu kama hatoi ahadi hizo kwa ‘kucheza usanii’, basi, bila shaka, anaweka mategemeo yake kwa ‘donors’ (wahisani). Na kama ni hivyo, ni dhahiri, basi, rais wetu huyu bado hajawaelewa Wazungu, na bado anashindwa kusoma maandiko ukutani.

Kabla sijalifafanua hilo, napenda kueleza kidogo tathmini yangu mimi ya Kikwete kama nilivyomuona katika miaka mitano ya utawala wake. Kwangu mimi huyu ni rais tegemezi (kifikra na kiutendaji) kuliko marais wengine wote waliomtangulia. Ni rais anayeamini katika dhana ya misaada kama njia ya kutoka matatizoni.

Sijui asili ya hulka yake hiyo, lakini nadhani ni kitu ambacho kipo kichwani mwake (au damuni) siku zote. Huyu ni rais ambaye akiombwa samaki na mwananchi anayeishi pembezoni mwa ziwa, hatampa mwananchi huyo msaada wa nyavu; bali atakwenda kwa jirani mwingine kumwombea mtu huyo samaki!

Huyu ni rais ambaye akilalamikiwa shida ya maji na wanavijiji wanaoishi katika eneo ambalo maji ardhini hayapo mbali (water table), hatawaonyesha njia ambayo wanaweza wenyewe kujichimbia kisima; bali atawaahidi serikali kuwajengea kisima!

Katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake tumeiona hulka yake hiyo ya kupenda kuombwa na wananchi misaada isiyostahili, na kupenda pia kugawa misaada isiyostahili kugawiwa na rais. Imefika hatua wananchi wanamwomba awasaidie hata katika mambo waliyo na uwezo nayo wenyewe kama vile kujinunulia mashine ya kusaga nk! Na yeye anaona ni sawa tu.

Hulka hiyo ya kuchekelea misaada ilijitokeza tena, hivi karibuni, huko Makete (Iringa) ambako Kikwete alijisifu kwa wananchi aliokuwa akiwahutubia kwamba amepigiwa simu na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, kumwarifu kwamba Rais Obama ametamka huko New York, Marekani, kwamba ataendelea ‘kuimwagia’ Tanzania misaada.

Kwa rais muumini wa dhana ya kujitegemea, jambo kama hilo lisingekuwa la kujivunia mbele ya wananchi unaowaongoza. Lakini si Kikwete. Yeye aliona hiyo ni sifa kubwa na ‘mtaji’ wa kisiasa!

Lakini pia hatujasahau kauli yake nyingine ya kutamba kwenye mkutano wa kampeni kwamba yeye anakwenda Marekani mara kwa mara kuhemea, na kwamba anaporudi hurudi na ‘vibaba’.

Kauli hiyo ameirudia tena mwishoni mwa wiki iliyopita huko Tabora, na kudai kwamba kama si safari zake za mara kwa mara za kwenda nje kuhemea, Watanzania wangekufa na njaa!

Ndugu zangu, rais tunayemhitaji si yule ambaye ni hodari wa kuzunguka huku na huko duniani akitembeza bakuli la ombaomba; bali ni yule atakayetuwekea misingi ya kujitegemea kama Taifa.

Kwa mfano, badala ya Rais Kikwete kwenda kila mara nje ya nchi kutuombea chakula (kama alivyodai), angekuwa anakwenda vijijini, mara kwa mara, kuhimiza kilimo kwa namna ambayo Nyerere na Sokoine walifanya zama zao.

Huo ndio ufumbuzi wa kisayansi wa kumaliza tatizo la uhaba wa chakula nchini, na si kila mara kukimbilia Marekani kuomba chakula. Si wanasema mtegemea misaada hufa masikini?

Naomba sasa nifafanue kauli yangu ile kwamba Rais wetu Kikwete hajui vizuri hulka za Wazungu, na bado hayajasoma maandishi ukutani kuhusu misaada yao. Naihusisha kauli hiyo na tambo yake hiyo ya Makete kwamba kapigiwa simu na Balozi wa Marekani na kuahidiwa misaada na Obama.

Ninaposema kwamba yaelekea Kikwete hawajui vizuri Wazungu, ninamaanisha kwamba yeye Kikwete anaamini kuwa Wazungu wana nia ya kweli ya kuliendeleza Bara la Afrika na Waafrika.

Anapasawa kuelewa kwamba kama Wazungu wanaisaidia Afrika, ni kwa sababu inawabidi, na si kwa sababu wanawapenda Waafrika kiasi hicho.

Chukulia, kwa mfano, Marekani. Kama Marekani inaimwagia misaada Tanzania (vyandarua na dawa za HIV!), ni kwa sababu ya maslahi yake ya kimkakati (strategic interests), na si kwa sababu inampenda sana Kikwete au Tanzania.

Na strategic interest ya Marekani katika Tanzania, kwa sasa, ni suala la ugaidi ambalo linahusu zaidi usalama wa taifa la Marekani. Marekani inafahamu fika kwamba Tanzania imekuwa moja ya vituo vya Al Qaeda, na hasa mji wa Arusha ambako majuzi tu walikamatwa watu walioshiriki katika njama za shambulizi la kigaidi lililofanyika Kampala, Uganda wakati wa fainali za Kombe la Dunia.

Katika mazingira kama hayo, ni lazima Marekani ihakikishe kuwa inafanya urafiki na rais anayetawala Tanzania (awe Kikwete au mwingine yeyote) ili iweze kufuatilia vyema kikachero nyendo za Al Qaeda na matawi yake kama vile Al Shabab ya Somalia.

Ni kwa msingi huo, Rais Obama alikubali Rais Kikwete awe rais wa kwanza wa Afrika kumtembelea Ikulu ya Marekani baada ya kuapishwa. Ni kwa msingi huo huo Marekani ‘inaitupia’ Tanzania misaada kidogo hapa na pale.

Ni kwa msingi huo pia Balozi Lenhardt alimpigia simu Kikwete akiwa Makete kumwambia kwamba Rais Obama ameahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika hotuba yake UN.

Ilibidi Obama aisifu Tanzania kwenye hotuba yake kumtuliza Kikwete kwa sababu (Obama) alitoa hotuba kali kwenye mkutano wa UN wa kujadili Malengo ya Milenia (MDG). Katika hotuba hiyo aliyoitoa Septemba 22, Obama alizionya nchi masikini zinazobweteka na kutegemea misaada kujiendeleza.

Akitangaza mwongozo mpya wa Marekani wa kutoa misaada unaoitwa New US Global Development, Obama alisema hivi: “Nations should take control of their own destiny”. No proud leader in this room want to ask for aid. Aid alone is not development” (nchi masikini zijisimamie zenyewe na kuamua mustakabali wao. Hakuna kiongozi aliye makini katika chumba hiki anayependa kuomba misaada. Misaada peke yake haiwezi kuleta maendeleo).

Sina hakika kama Rais wetu Kikwete aliisoma hotuba hiyo ya Obama, lakini nisisitize tu hapa kwamba Obama hakuishia hapo; bali aliendelea kusema kwamba chini ya sera hiyo mpya ya New US Global Development, Marekani itazisaidia tu zile nchi zenye nia ya kweli ya kujiendeleza, na si zile zinazobweteka tu kupokea misaada.

Nina hakika hotuba hiyo kali ya Obama ilizishtua nchi nyingi masikini zinazotegemea misaada ya Marekani kama Tanzania, na nadhani ndiyo sababu ilibidi Obama ‘amtulize’ Kikwete kwa kupachika aya hiyo ya kuisifu Tanzania kwenye hotuba yake. Obama alifanya hivyo kwa sababu ya kulinda strategic interest ya Marekani katika Tanzania ambayo, kama nilivyosema, ni vita dhidi ya ugaidi.

Tofauti na Kikwete, rais visionary angeyaona maandiko ukutani; nayo ni kwamba misaada hiyo ya Marekani itakoma pale strategic interests zao kwa Tanzania zitakapokwisha. Kwa hiyo, angeng’amua kuwa ahadi ya misaada ya Obama si kitu endelevu hata kidogo cha kujivunia kwa wapiga kura wako.

Isitoshe; licha ya tulizo hilo la Obama kwa Kikwete, kuna kila dalili kuwa misaada hiyo itapungua sana kwa sababu Obama mwenyewe hivi sasa anakabiliwa na matatizo chungu nzima ya kiuchumi nchini mwake. Ukosefu wa ajira umekuwa mkubwa (asilimia 9.60) kushinda kipindi kingine chochote tangu mwaka 1948. Katika hali hiyo, hawezi kuwa na mapesa mengi ya kuiendeleza Tanzania; hata kama strategic interests za taifa hilo zitakuwa hatarini. Sana sana tutapewa vyandarua, dawa za HIV na ujenzi wa barabara ndogo mbili au tatu hivi ambao, hata hivyo, utafanywa na makampuni yao wenyewe!

Nimeizungumzia Marekani, lakini hali ni hiyo hiyo huko Uingereza, Ufaransa na hata nchi za Scandinavia ambako sasa wananchi wameanza kuhoji ni kwa nini kodi zao ziendelee kuzisaidia nchi kama Tanzania kwa nusu karne sasa; ilhali zimeshindwa kujikomboa kwenye umasikini!

Nirudie tena kusisitiza kwamba kiongozi visionary hawezi kutegemea misaada ya Wazungu kuiendeleza nchi. Na ninashangaa ni Kikwete tu asiyeliona hilo.

Hata Rais Mstaafu Mkapa na Rais Meles Zenawi wa Ethiopia waliliweka wazi hilo katika mkutano wa kimataifa wa kiuchumi (World Economic Forum) uliofanyika Dar es Salaam Mei 5-7, 2010, walipotamka kwamba Wazungu hawana nia ya kweli ya kuiendeleza Afrika.

Hata Rais Kagame wakati akizungumza na vyombo vya habari mwanzoni mwa mwezi uliopita alisema hivi: “Msikubali mtu yeyote awadanganye. Watu hawa (wafadhili) hawataki Waafrika waondokane na umasikini wao. Hawataki sisi tuondokane na umasikini kwa sababu wanataka tuendelee kuwa tegemezi kwao.”

Inakuaje, basi, kina Mkapa, Zenawi na Kagame wawe na msimamo huo kuhusu dhana ya kutegemea misaada ya Wazungu, lakini Kikwete yeye awe na mtazamo tofauti? Jibu pengine ni kwamba dhana ya kutegemea misaada amekuwa nayo, kifikra na kiutendaji, tangu akiwa kijana mdogo. Huwezi leo kumbadilisha ghafla!

Vyovyote vile; mtu mwenye hulka hiyo hawezi kuwa kiongozi mzuri; kwa sababu kiongozi mzuri ni yule anayeonyesha njia ya namna ya kuzitumia vyema raslimali nyingi ambazo Mungu ametupa kujitatulia wenyewe matatizo yetu na kujiletea maendeleo, na si yule anayefurahia kutembeza bakuli la ombaomba.

Wapendwa, najua wapo watakaosema (mmh!); hata Nyerere alikuwa akiomba na kupokea misaada ya Wazungu na Wachina. Ni kweli kabisa, lakini yeye Nyerere alifanya hivyo kwa uchungu mkubwa mno, na ni uchungu huo uliomsukuma kujenga misingi ya Taifa ya kujitegemea; tofauti na Kikwete ambaye huipokea huku akichekelea na kutamba kwa wapiga kura. Anaona ni sawa, na ndio urais!

Ndiyo maana ungeniuliza leo ni kazi gani inamfaa Jakaya Mrisho Kikwete, ningekujibu haraka kwamba ni uongozi katika asasi yoyote ya kimataifa ya misaada ya hisani (international charity organasation).

Kimsingi, kazi kubwa ya asasi hizi za kimataifa za misaada ya hisani si kuzalisha au kuonyesha njia za kutatua matatizo; bali ni kwenda huku na huko duniani kuomba misaada kwa matajiri, na kisha kuigawa misaada hiyo kwa wenye shida (the needy) kama vile Durfur nk. Nadhani hiyo ndiyo kazi inayomfaa zaidi Kikwete, na si urais.

Tafakari.








Mwanzo Toleo Lilopita Hifadhi Matangazo Tuwasiliane
Copyright 2007 - 2010, Raia Mwema Publications All Rights Reserved.
 
Tutaendelea na utegemezi (dependency syndrome) hadi lini? Mwisho tutauzwa pamoja na nchi.
 
Back
Top Bottom