Kila Pahala ni Ulaji. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kila Pahala ni Ulaji.

Discussion in 'JF Chit-Chat' started by Mwazange, Jun 14, 2012.

 1. Mwazange

  Mwazange JF-Expert Member

  #1
  Jun 14, 2012
  Joined: Nov 16, 2007
  Messages: 1,051
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  KWAMBA kila mtu `hula' mahala pake pa kazi, hilo halikuwa geni, hususan ofisini kwetu.
  Tangu `mnene' wa kwanza, mpaka `kapuku' wa mwisho, kila mmoja huketi mkao wa kula kwenye `wigo' unaomkinga asionekana na `vishingo' wasiokawia kuweka `mikingamo' ya kujaza michanga kitumbua cha mtu.
  Ukitilia maanani mishahara-njiwa na marupurupu njaa yenye kupigwa ‘paranja’ na wale watoza-ushuru wasio na simile, sera ikawa ni kutumia `bongo' katika nchi ya Ruksa, mradi tu usidakwe.
  Madhali mtu umekabidhiwa ofisi na meza - na ruzuku au tuseme, kasma, hasa iliyonona, hukuwa na haja ya promosheni, wala ya kwenda shule eti kuongeza `unga.' Huo unga au mchele wa nyongeza unaugema na kuumega mumo humo - mradi tu penye unyonge upenyeze matonge, au penye udhia watupia rupia!
  Kwa mtaji huo, wale ambao `ofisi' zao zilikuwa kavu, kwa maana ya kukosa pa kuchota, au cha kugema, walifanya kila namna ya kupata `transfa' ndogo ndogo huku na kule kwenye ofisi, bora mkono uende kimiani.
  Kwa upande wangu, nilionekana kupendelewa zaidi. Hata madereva wenzangu wakati mwingine waliniambia bayana wakati tukisogoa.
  "Mwenzetu unakatiwa mapande ya ulaji tu," alisema Bwana Mapepe, dereva wa bosi mkuu. "Miye kila wakati nipo na kingunge-mkuu wa ofisi! Nitaiba saa ngapi? Gari yenyewe V8. Roho juu kila wakati kuogopa majambazi. Hata `kusanya' siwezi!" Alilalama.
  Wakati huo mimi naendesha gari la maji machafu. Nikipiga tripu mbili za kampuni, napiga tano za kwangu. Na kwa kuwa gari lile ni la kubeba (ashakum) kinyesi, wanene wa kampuni hawakutupa macho yao kwangu. Mradi ilikuwa ni ulaji mtupu wa kimyakimya. Hata madereva wenzangu hawakushtuka.
  Machale yalianza kuwacheza waliposikia nimesimamisha `banda' pale bondeni. Nikahamishiwa kwenye `kijiko' - gari la kuchimbia na kung'oang'oa - kwa imani sitakuwa na cha `kuhamisha.' Wakati huo mtindo wa kutumia `nyoka' - mipira ya kutolea petroli na dizeli - ulikuwa umedhibitiwa. Lakini huwezi kumdhibiti mwanadamu, hasa ngurumbili huyo anapokuwa wa ‘Bongoland’. Ulaji wa kwenye `kijiko' ukawa mkubwa zaidi, maana katika masaa ya kazi, nusu nayatumia nikiwa `kontrakta bubu.'
  Mpaka walipostuka, nilishavuna vya kutosha. Siku nilipohamishiwa kwenye gari la kubeba wafanyakazi, wenzangu walijua wazi chizi limepewa manati, sokoni!
  "Au mwenzetu unakula na wakubwa?" walinitania.
  "Kwenda zenu! Nani asiyegema mahala pake pa kazi?" Niliwajibu kwa masikhara.
  "Ah! Lakini wewe mwenzetu unawekwa kwenye vitengo vya ulaji tu!"
  Na kweli. Kwenye gari hili la abiria kulikuwa na pesa za nje-nje tu.
  Mara ya kwanza nilikuwa naogopa kuligeuza daladala-bubu (sanyasanya), hususan asubuhi, kwa vile "wanga wengi." Lakini kadiri nilivyoshika hatamu za uongozi wa basi lile, ndivyo nilivyozidi kujiamini.
  "Kwanza wanene wote wa kampuni wanakaa uzunguni. Halafu wote wana magari. `Dili' zao zote na wazito wenzao. Huku uswahili watatafuta nini? Nyumba ndogo?"
  Ikawa desturi.
  Nikitoka kazini, baada ya `kuwatupa' wafanyakazi wenzangu, nilianza awamu mpya ya kupiga tripu za daladala ...
  Hapakuwa na tatizo. Japo konda, ambaye pia alikuwa ndiye mpiga-debe na mpambe, alikuwa `anapiga panga.' Makusanyo, bado chuma cha siku lilikuwa la kuvutia.
  Mungu akupe nini! Labda gunia la chawa, Man'ake huo usiku `serikali inakuwa imelala' - hamna matrafiki, walau huko kwenye njia za uswahlini. Ukiona `tageti' waendea kwa wakati wako!
  Na hapo sikutaka `kuchezea wakati'. Ukipata tumia, ukikosa jutia. Hata kitambi kikaanza kuchomoza.
  Hicho pengine ndio kilichonisaliti. Maana maneno yakaanza `kutembea' chini chini. Tena madereva wenzangu wale wale! Utafikiri wao `hawali' kwenye magari yao! Mswahili bwana! Kwa kuchukia `maendeleo' ya mtu, Utasema na yeye hayataki maendeleo hayo!
  Sikujali.
  Wembe ni ule ule!
  Siku moja nikaamua kumchukua `dei waka' dereva wa daladala fulani iliyo juu ya mawe. Siku hiyo kondakta nikawa mwenyewe - ili kuzuia `kupigwa panga' pesa zinazokusanywa.
  Sanyasanya iliendelea kama siku zote. "Sanyasanya Trans" kama ilivyojulikana mtaani, iliendelea kudunda uswahilini. Na pesa nilizokusanya siku ile zilinifanya nijue ukubwa wa `panga' lililokata pesa siku zote.
  Ni wakati wa tripu ya mwisho, ya kupata pesa za kujazia mafuta, kizungumkuti kilipoanza.
  Wakati `nawachuna' abiria nauli, abiria aliyeketi kwenye kona kiti cha nyuma akakataa kulipa.
  "Siti ya mwisho, bado mmoja!" nilisema. "Halo we mwenye kapelo leta `uchache' huo!"
  Lakini yule jamaa aliyekuwa amevaa kofia iliyofunika uso staili ya `ukitaka kumuua nyani" alikuwa anapuuza kelele zangu.
  Nilipojaribu kufikiri ni kitu gani ananiringia, nikahisi labda kitambi!
  "Halo usiku unauweka! Ikiwa ni ubosi ni huko huko ofisini kwako, hii ofisi ya mtu mwengine bwana!"
  Lile jamaa lilinitazama tu.
  Au linavuta bangi? Hata likivuta! Shauri yake! N'nachojali ni mdako tu!
  "Halo usitutishe na kitambi chako cha mapuya! Tumbo hilo la mataputapu linakufanya ujione booosi! Nakwambia hapa umefika." Nilifoka.
  Abiria wengine walitukodolea macho. Tayari wengine walishaanza kuambukizwa `ufyatu' wa yule jamaa.
  "Asipolipa yule na sisi hatulipi." Walidai.
  Hapo ndipo wazimu wote ukanipanda kichwani. Mtu huyu hawezi kunifanyia mapuuza kwenye gari `langu' halafu nikamucha vivi hivi tu!
  Nahisi hata yeye alibaini sasa yatakuwa mengine. Ndiyo maana akatoa noti ya nauli kabla sijaongea zaidi. Nikamrudishia chenji, pungufu ya shilingi mia tano.
  "Na mimi nikikunyima chenji hii utajisikiaje?"
  Hakusema kitu.
  Nikanyoosha mkono nimpe hela yake.
  Mara, Lo!
  Akatoa miwani ya jua aliyovaa usiku ule. Kisha akainua kofia aliyovaa.
  Mama yake na mama!
  Kumbe ni bosi, `mnene mkuu' wa ofisi!!
  "Hizi zitakuwa ni fitna za watu!" niliwaza.
  Nilihisi kutaka kwenda haja papo hapo. Sijui gavana iliyookoa jahazi ilitoka wapi! Vinginevyo ingekuwa simulizi.
  Nilichanganyikiwa.
  Hata abiria wengine sikuweza kuchukua nauli zao.
  Kesho yake niliitwa ofisini kwa mkuu.
  "Kijana, maisha unayapeleka vibaya! Ungekuwa japo unaendesha mwenyewe, pengine ningeelewa, japo kidogo. Kosa ulilofanya unastahili adhabu kali!"
  Ama kweli. Siku ya kutembea uchi ndiyo unayokutana na mkweo!
  Hivi ninapokumegea stori bosi bado 'anafikiria' adhabu ya kutoa. Sijui bosi atatoa adhabu gani? Sijui atanihamishia ofisi yenye meza bila kasma? Au atanipeleka kusoma? Kunifukuza hawezi - maana ni urasimu mkubwa - ndiyo ‘raha’ ya ajira ya umma. Mwenzenu niko roho juu! Naombeni ushauri !
   
 2. Shine

  Shine JF-Expert Member

  #2
  Jun 14, 2012
  Joined: Feb 5, 2011
  Messages: 11,514
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0
  Ndefu sana ntarudi baadae!
   
Loading...