Kikwete aikwamua Twiga Stars
Friday, 11 June 2010 04:36
Na Amina Athumani
RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuipa zaidi ya sh. milioni 53, timu ya soka ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' kwa ajili ya fainali za mashindano ya wanawake ya Mataifa ya Afrika, yatakayofanyika nchini Afrika Kusini Oktoba mwaka huu.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana, wakati akiipongeza timu hiyo kwa kupata nafasi ya kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza Rais Kikwete, alisema fedha hizo atazitoa kwa ajili ya kugharamia kambi ya wachezaji katika kipindi chote cha maandalizi yao.
"Nitasaidia kwa upande wa kambi, chakula na malazi kwa wachezaji ikiwa ni pamoja na kuwapa posho katika kipindi chote mtakachokua kambini, ninawataka mfanye mazoezi kwa bidii, ili msonge mbele zaidi," alisema Rais Kikwete.
Alisema kwa upande wake atawasaidia wachezaji pekee na kwamba suala la makocha na viongozi wa timu hiyo, amewataka viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kubeba jukumu hilo la kuwalipa viongozi hao katika kipindi chote cha maandalizi.
Rais pia aliwataka wachezaji hao, kuhakikisha wanafuzu kucheza michuano ya Dunia, itakayofanyika nchini Ujerumani mwakani ampano nchi mbili zitakazoshika nafasi za juu kwenye fainali hizo za Afrika Kusini, ndizo zitakazoshiriki katika michuano ya Dunia.
Naye Rais wa Chama cha Mpira wa Wanawake Tanzania, Lina Mhando alisema timu hiyo inahitaji sh. milioni 300 kwa ajili ya gharama za kambi, michezo ya kirafiki, posho za wachezaji, vifaa, chakula, kutembelea mikoa kwa ajili ya kutafuta vipaji pamoja na kufanikisha kushiriki katika fainali hizo.
"Tunakushukuru Rais kwa kuweza kuona umuhimu wa kuwalipia wachezaji hawa gharama za kambi, tunaahidi msaada huo utatumika vizuri na vijana wetu watajituma, ili kuweza kuwa moja ya nchi za Afrika, zitakazoshiriki kombe la Dunia la wanawake hapo mwakani," alisema Lina.
Twiga Stars ilifuzu kucheza fainali hizo za Mataifa ya Afrika baada ya kuwatoa Ethiopia katika mzunguko wa kwanza kwa jumla ya magoli 4-2 na kwenye mzunguko wa pili, ilifanikiwa kuitoa Elitrea kwa mabao 11-4 na kuifanya kuwa timu pekee ya Afrika Mashariki inayoshiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza.
Mbali na Tanzania kufuzu kucheza fainali hizo za wanawake pia zipo timu kutoka Nigeria, Ghana, Cameroon, Algeria, Guinea na wenyeji Afrika KUsini ambapo pia matokeo kati ya Namibia na Eguatorial Guinea ambao ni mabingwa wa kombe hilo bado hayajapatikana na mshindi kati yao ataungana na timu hizo katika fainali hizo.