Kifo siku ya harusi yangu

Kifo siku ya harusi yangu

SEHEMU YA 33


Profesa Mshana akiwa amechanganyikiwa kabisa, akaamua kumpigia simu Dk. Rwegoshora ili wajaribu kucheza na sheria waweze kuwatoa wake zao pamoja na Genesis, lakini majibu aliyopewa na Dk. Rwegoshora yalimchanganya sana, alimwambia kila mmoja ahangaike na msalaba wake mwenyewe!

Hilo lilimchanganya Profesa Mshana lakini halikutosha, simu ilikatwa akiwa bado anajaribu kumshawishi! Kitendo cha kukatiwa simu, kikazidi kumtibua na kuzidisha giza nene katika wazo la kumtoa mwanaye pamoja na mkewe kwenye mkono wa sheria.
Je, nini kitatokea? Genesis na mama yake, mama Bianca, Dulla, Festo, Patrick na Farida watatoka? SONGA NAYO...

“AMENIKATIA simu?” Profesa Mshana akatamka kwa sauti kubwa.
“Haiwezekani!” Akajijibu tena mwenyewe.
Tukio lile lilimchanganya sana kichwa chake, likatoa taswira mpya kabisa katika safari yake ya kumtoa mwanaye pamoja na mkewe jela! Kitanzi kilionekana waziwazi mbele ya familia yake, jambo ambalo hakutaka kuliruhusu litokee.

“Lazima nifanye jambo fulani hapa,” akawaza tena.
Ni kweli ilikuwa lazima afikirie jambo fulani la kufanya kwa ajili ya mkewe na mwanaye. Yeye kama baba wa familia, alitakiwa kuumiza kichwa ili aweze kuiondoa familia yake katika hatari ambayo ilikuwa wazi kabisa.

Ubongo wake ukafanya kazi zaidi ya kawaida, hapo akawaza sana lakini mwisho wa kikomo cha mawazo yake ukagonga kwa Dk. Rwegoshora ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwamba yeye ndiye kila kitu.

Kama ni kweli alitaka kufanikiwa kuwatoa mtoto wake pamoja na mkewe ndani, lazima muunganiko wao ufanye kazi sawasawa, vinginevyo ingekuwa ndoto kwake kufanikiwa!
“Lazima nizungumze naye...” akawaza.

Wazo lake lilikuwa na nguvu sana, kitu pekee alichoona kinafaa kufanyika ilikuwa ni kumpigia simu. Mara moja akanyanyua simu yake haraka na kubonyeza tena namba za Dk. Rwegoshora. Simu iliita kwa muda mfupi sana, ikapokelewa.
“Sema nakusikiliza!” Alikuwa ni Dk. Rwegoshora akizungumza kwa sauti iliyosoma majonzi na kisasi.
“Ndugu yangu tuliza hasira!”

“Hasira?”
“Ndiyo naona una hasira sana!”
“Unahisi sikutakiwa kuwa nazo siyo?”
“Sijasema hivyo Rwegoshora ndugu yangu. Unajua kama ni maji kumwagika yameshamwagika, sasa tuangalie namna ya kuwatoa hawa watu kwenye matatizo.”
“Tunawatoa akina nani?”

“Tuliza moyo ndugu yangu, naamini unajua nazungumzia akina nani, lakini hasira ndiyo inakufanya unijibu hivyo!”
“Sikiliza Mshana, sina muda wa kuendelea kupoteza kwenye simu, nina mambo mengi sana muhimu ya kufanya. Kikubwa ambacho unatakiwa kufahamu, juu ya suala hili, kila mmoja ahangaike kivyake!”

“Sisi ni ndugu lakini?”
“Undugu wetu ndiyo usababishe mwanangu afe?”
“Hapana!””Mke wangu awekwe ndani?”
“Hayo yameshatokea, tunatakiwa kuangalia mbele kwa sasa.”
“Sina mbele nyingine na wewe, naona hata huo urafiki wetu wa kinafiki uishie hapa, kila mtu ahangaike kivyake!” Akasema Dk. Rwegoshora kwa kumaanisha.

“Lakini sikikiliza rafiki yangu, unajua...” akasema Profesa Mshana hata hivyo hakusikia dalili yoyote ya Dk. Rwegoshora kuwa hewani.
“Halooo...halooo...” alikuwa akiita, lakini baadaye akagundua kwamba Dk. Rwegoshora alikuwa amemkatia simu.

Hili ni tukio la pili la aina hiyo kufanywa na Dk. Rwegoshora, rafiki yake mkubwa ambaye walishibana. Hakuhitaji mtu yeyote wa kujitokeza kumwambia kwamba harufu ya urafiki wao kufikia tamati ilikuwa inanukia. Kila kitu kilikuwa wazi kabisa, kwamba hasira ya Dk. Rwegoshora zilikuwa kali na hakuona taabu yoyote kuvunja urafiki wao.
“Si neno, nitajua cha kufanya...ni mwanaume, mwenye elimu, siyo lazima kila kitu kitafanikiwa kupitia kwake. Nitatumia uzoefu wangu kuhakikisha hili tatizo linaisha. Najua nitaweza!” Akajipa moyo Profesa Mshana.

***
Simu ya mezani kwake iliita kwa muda mrefu sana, bila kuipokea. Kwa kawaida, OCID Wambura kila anapoingia ofisini kwake asubuhi, hujiandaa kwa ajili ya kikao na Waandishi wa Habari kwa lengo la kuwapa matukio yote yalitokea kwa saa 24 zilizopita.
Ilikuwa ni saa 3:35 za asubuhi, ikiwa ni dakika 25 tu, kabla ya kikao chake na waandishi, simu ile ilikuwa na usumbufu mkubwa sana kwake. Akaamua kuipokea baada ya kujishauri kwa muda.

“Ofisini kwa OCID hapa, naomba nikusaidie!”
“Ni mimi Zena afande!” Sekretari wake Zena akazungumza kwenye chombo kwa sauti laini sana.
“Zena mara hii umesahau ratiba yangu ya asubuhi?”
“Sijasahau afande ila kuna simu muhimu sana kutoka Makao Makuu!”
“Wapi?”
“Central!”

“Niunganishe tafadhali!”
“Ok!” Zena akasema kisha akapotea hewani.
Sekunde kadhaa zikapita hewani muziki ukisikika kutoka upande wa pili, kisha sauti nzito ya kukwaruza ikasikika.
“Haloo!”
“Haloo!”

Sauti aliyoisikia kwenye simu, bila kujitambulisha, OCID Wambura alishaitambua kwamba alikuwa akizungumza na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ben Kitalilo.
“Jambo?” Kamanda Kitalilo akasema.
“Jambo afande!”
“Hao watuhumiwa wa madawa ya kulevya kutoka Saudi Arabia, wahamishie huku makao makuu asubuhi hii!”

“Nimekusoma afande!”
“Lazima nione ripoti nzima ya mwenendo wa hilo sakata kutokea Saudi Arabia hadi hapo ofisini kwako!”
“Umesomeka afande.”
Simu zikakatwa. Bila kupoteza muda OCID akaamua kumpa kazi ya kuzungumza na waandishi wa habari msaidizi wake, yeye akaagiza watuhumiwa wote watolewe selo kisha wakaingizwa kwenye gari na safari ya kwenda makao makuu ya polisi ikaanza, yeye akifuatia nyuma kwa gari lake.

***
Saa 3:45 asubuhi, Dk. Rwegoshora alikuwa akiingia ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ben Kitalilo baada ya kuruhusiwa na sekretari wake. Alipokelewa na tabasamu la kutengeneza na Kamanda Kitalilo.
“Karibu bwana!”
“Ahsante!”
“Najua unafahamu ni kwanini nipo hapa. Shida yangu ni kuona unafanya jambo fulani kwa gharama yoyote, mke wangu atoke kwenye hii kesi ya madawa ya kulevya ya Farida Mbaraka!”

“Farida Mbaraka?”
“Ndiyo, yule binti aliyekamatwa Saudi Arabia na Genesis kwenda kumuokoa huko!”
“Aisee sitaweza!”
“Kwanini? Tusaidiane tafadhali, sitaki mke wangu aozee ndani!”

“Lingekuwa limefika kwangu kama mtu wa mwisho, ningejua cha kufanya, lakini limetokea kwa IGP mwenyewe, amesisitiza nihakikishe nasimamia hili suala kikamilifu. Nakushauri ucheze na sheria, tafuta wanasheria wasimame mahakamani, lakini lazima wawe wazuri kweli kweli, maana ni kesi ngumu sana!” Akasema Kamanda Kitalilo.

Maneno ya Kamanda Kitalilo yalimkatisha tamaa kabisa Dk. Rwegoshora, kwa vyovyote vile, hakuwa na msaada wowote kwake. Hakusema chochote zaidi ya kusimama na kutoka nje ya ofisi.
Akiwa anatoka nje, kwenye ngazi akawaona mke wake, mke wa rafiki yake Profesa Mshana, Genesis, Farida na vijana watatu wakiwa chini ya ulinzi wa polisi wakipanda ngazi nyuma yao mitutu ya bunduki ikiwasindikiza!

Akawatazama wote kwa zamu, lakini macho yake yalipofika kwa mkewe, yaligota hapo! Mkewe akaanza kulia kwa uchungu! Macho ya Dk. Rwegoshora yakabadilika rangi na kuwa mekundu kabisa!

ILIKUWA ni sawa na sinema ya kusisimua iliyofikia sehemu ambayo mtazamaji asingeweza kubanduka kwenye kiti kuiacha ikiendelea. Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika ulimwengu mwingine kichwani mwa Dk. Rwegoshora.

Kwa hakika alitamani sana kile alichokiona kiwe ndoto lakini haikuwa hivyo, kila kitu kilikuwa ni kweli na halisi. Mke wake aliendelea kulia huku askari wakiwasukuma kuwapandisha ngazi haraka kwenda kituoni.

Dk. Rwegoshora hakuwa na la kufanya zaidi ya kushuka ngazi huku akigeuza shingo yake akimshuhudia mkewe akipelekwa msobemsobe. Moyo ulimuuma sana lakini hakuwa na la kufanya. Kitu pekee kilichokuwa mbele yake ilikuwa ni kwenda haraka sana ofisini kwa IGP.

Akaingia kwenye gari lake kisha akawasha na kuingiza gia namba moja, akaliondoa kwa kasi sana kama gari lililoibiwa! Alikuwa anakwenda kwa IGP. Mke wake alikuwa na thamani kuliko kitu kingine chochote katika maisha yake.
***
“Genesis ndiye yupi hapa?” IGP aliuliza kwa sauti nzito iliyoonesha ukali.
“Ni mimi Mkuu,” Genesis akasema kwa kujiamini.
“Yaani kijana mzuri namna hii unaweza kufanya vitu vya ajabu kama hivi?”

“Mkuu kila kitu kina sababu, unaweza kushangazwa na kitu nilichokifanya, lakini nimekifanya kwa sababu.”
“Kwani umefanya nini?”

“Aaaah! Afande mara hii umesahau kwamba nimeua?” Akajibu Genesis akitabasamu.
Jibu lile liliwashtua wote mle ofisini, IGP na wenzake wakaangaliana.
“Hivi umeua?”
”Ndiyo nimeua afande!”

“Umemuua nani?”
“Mtoto wake na yule pale...” akasema Genesis akisonta kidole alipokuwa amekaa mama Bianca.
“Huyu?” Insp. Sebastian akamuuliza akimgusa bega mama Bianca.
“Ndiyo!”

“Bi. Rwegoshora ni yupi?”
“Ni mimi!”
“Bi Mshana?”
“Nipo!”
“Festo?”

“Afande!”
“Patrick!”
”Mkuu!”
”Dullah!”
“Afande!”

“...bila shaka Farida ni wewe!” Aliuliza IGP akimtulizia macho Farida.
“Ndiyo afande!”
Baada ya hapo kilichofuata ilikuwa ni kila mmoja kuandika maelezo katika karatasi maalum. Kitu cha kushangaza Genesis alikuwa akiropoka hovyo na kusisitiza kwamba ni kweli alimuua Bianca na alifanya hivyo baada ya kugundua njama aliyofanya kwa kushirikiana na watu waliokuwa wamekamatwa ili kumpa kesi Farida.

“Genesis hebu njoo huku,” alimwita Insp. Sebastian akiondoka huku Genesis akimfuata nyuma.
Safari yao iliishia kwenye chumba maalumu cha mahojiano.
“Genesis kumbuka kwamba ukweli wako ndiyo ambao utakutoa katika haya matatizo.”
“Nafahamu Mkuu!”

“Sasa hebu naomba uwe mkweli, unajua nini kuhusu kesi hii?”
“Maelezo yangu ni yale yale sidhani kama kuna sehemu nitabadilisha. Siogopi kusema ukweli huu na nipo tayari kufa kwa kuusimamia. Ukweli ni kwamba nimemuua Bianca siku ile ile ya ndoa kwa kumchoma na kisu kifuani mwake.

“Kikubwa kilichosababisha nimuue ni baada ya kugundua mchezo mchafu uliofanyika. Mama yangu hafai kabisa na hata huyu mama yake Bianca. Ni hatari maana wanalazimisha yafanyike wanayoyataka kwa kutoa uhai wa mtu.

“Sikuwa tayari kuona Farida anakufa, mwanamke ninayempenda kuliko wote duniani. Nikaamua kwenda Saudi Arabia kumuokoa, nashukuru nilifanikiwa kumuondoa katika mikono ya kifo. Najua pesa inaweza kutumika kumrudisha Farida kwenye matatizo lakini mimi ninao ushahidi wa kutosha na nipo tayari kuwaonesha.”

“Ushahidi gani huo?” Insp. Sebastian akamuuliza akionekana kumsikiliza kwa makini sana.
“Ipo anwani ya barua pepe ambayo ina kila kitu, inaonesha mchezo mzima ulivyofanyika.”
“Ni ya nani?”
“Marehemu Bianca!”

“Unadhani hawawezi kufuta hayo maelezo?”
“Sidhani maana Bianca mwenyewe ameshafariki na ni yeye ambaye angeweza kufuta.”
“Uko tayari kunionesha sasa hivi?”
“Nipo tayari.”

Muda ule ule wakaongozana hadi kwenye chumba cha mtandao wa Internet, kisha Genesis akataja anwani ya barua pepe ya Bianca kisha akaingiza maneno ya siri, akamuonesha mawasiliano na maelezo yote ya jinsi mchezo mzima ulivyofanyika.
“Mungu wangu!” Akashtuka Insp. Sebastian.

“Usishtuke huo ndiyo ukweli wenyewe, naomba kwanza u-save huo ukurasa kwenye kompyuta yako halafu pia uchape ili ushahidi usipotee.”
“Usinifundishe kazi kijana, hebu twende huku.”
Wakaongozana tena hadi walipokuwa watuhumiwa wengine ambapo wote kwa pamoja waliingizwa selo.
***
Katika chumba hiki kidogo chenye meza ya kioo walikuwa wamekaa wapelelezi watatu kwenye kikao cha dharura wakijadili namna ya kupambana na kesi ya akina Genesis. Wote walikuwa na mafaili mikononi mwao tayari kwa kuanza kikao.

“Nadhani kila mmoja ameona hali ilivyo, bila shaka tuna mahali pa kuanzia,” alisema Insp. Sebastian ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao.
“Ndiyo Inspekta, lakini lazima nikiri kwamba sijawahi kukutana na kesi ngumu kama hii.”
“Lakini kwa kuwa ni kazi yetu tunapaswa kuikabili. Nahitaji mawazo yenu... ni akina nani tunaweza kuwaengua kwenye hii kesi?”

“Kwa ripoti ya Saudi Arabia, Farida hana cha kujibu,” alisema Insp. Mchele.
“Ni kweli kabisa, ushahidi wote mimi ninao, nadhani Farida atabaki kuwa shahidi lakini ni lazima tumtoe.”

Wakakubaliana kwa pamoja na hicho ndicho kilichotokea. Muda mfupi baada ya kikao kuisha Farida aliachiwa huru, lakini katika hali ya kushangaza alikataa kuondoka.
“Kwa nini hutaki kuondoka? Unataka kuozea jela?” Askari alimuuliza Farida.
“SIWEZI KUONDOKA BILA GENESIS WANGU, NIPO TAYARI KUFA NAYE KAMA YEYE ALIVYOKUWA TAYARI KUFA KWA AJILI YANGU, SIONDOKI!” Alisema Farida akionekana kumaanisha kilichotoka kinywani mwake.
***
IGP alikuwa makini sana kumsikiliza Dk. Rwegoshora. Kwa namna alivyokuwa akimsikiliza alionekana wazi kuwa na nia ya kumsaidia lakini cha ajabu Dk. Rwegoshora alipomaliza kuzungumza aliongea maneno ya kukatisha tamaa kabisa.

“Lipo nje ya uwezo wangu, hili suala lipo mezani kwa waziri mwenyewe.”
“Kwa waziri?”
“Ndiyo ni yeye ndiye aliyeagiza nisimamie.”
“Acha nikamuone!”

Dk. Rwegoshora akaondoka moja kwa moja hadi ofisini kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Silvanus Misiga. Katibu muhtasi wake alipomuona hakuwa na haja ya kumchelewesha, akamruhusu aende ofisini kwa waziri. Alimkuta waziri akiwa ametulia ofisini kwake. Bila kupoteza muda akamueleza kilichompeleka.

“Tafadhali sana najua hili lipo ndani ya uwezo wako naomba unisaidie. Nampenda mke wangu kuliko kitu chochote na sipendi heshima yangu iharibike!”
“Kwa masikitiko makubwa rafiki yangu napenda kukwambia kwamba hili suala lipo nje ya uwezo wangu, rais amesema nilisimamie kikamilifu.”

Dk. Rwegoshora alishtuka sana, ilikuwa ni vigumu sana kuonana na Rais hasa katika suala linalogusa maslahi ya taifa kama lile, alimuona kabisa mke wake akiwa amevaa nguo za jela akitumikia kifungo chake!

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 34


ILIPOISHIA

Dk. Rwegoshora, anaendelea kuhangaika ili mkewe atoke ndani, lakini kila anapokwenda anakwama. Alianzia kwa Mkuu wa Kituo cha Oysterbay, baadaye kwa OCID wa Kinondoni ambaye alimwambia aende Central kwa vile shauri la mkewe lilihamishiwa mezani kwa Kamanda.

Alipofika akaambiwa aende kuonana na IGP, lakini alipokwenda kwake akaambiwa kuwa ni vizuri akaonane na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kuwa ndiye aliyeagiza. Huko ndipo alipochanganyikiwa, maana aliambiwa kwamba kesi ile ilikuwa ni agizo la Rais! Dk. Rwegoshora akachanganyikiwa.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

ALIHISI moyo wake kufa ganzi, maneno yale yalikuwa mazito sana na hakujua namna gani angeweza kukabiliana na tatizo lililokuwa mbele yake. Kikubwa alichohitaji ilikuwa ni kuhakikisha mke wake anatoka kwenye mikono ya sheria. Jambo hilo lingewezekana kama lingekuwa halijafika kwa Rais!

Alikuwa na nafasi kubwa sana kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hiyo angeweza kufanya chochote kile kwa ajili ya mke wake, lakini kwa Rais, tena kwa kesi ambayo imetoka nje ya nchi na dunia nzima ipo macho ikiangalia kitu kitakachotokea, ilikuwa vigumu sana!
“Mungu wangu, nimeshampoteza mke wangu hivyo,” akawaza Dk. Rwegoshora.

Kitu pekee ambacho alihisi kingeweza kumsaidia kwa wakati huo ni kumtafuta tena Profesa Mshana na kushauriana kwa pamopa. Kitu pekee ambacho kilitakiwa kufanyika ilikuwa ni kutafuta jopo la mawakili wenye uzoefu mkubwa hata kama ni kutoka nje ya nchi ili waweze kuwasaidia.

“Inabidi nilegeze msimamo wangu, lazima nimtafute Profesa Mshana. Hili suala sitaweza kulikamilisha peke yangu, lazima nipate nguvu nyingine kutoka nje,” akawaza Dk. Rwegoshora.
“Nitafanya hivyo,” sasa akasema kwa sauti kisha akaenda alipoegesha gari lake na kuingia, safari ya kwenda nyumbani kwake ikaanza.

***
“Hivi wewe una kichaa?” Mmoja wa wapelelezi akamwuliza Farida ambaye alikuwa akilia kwa uchungu akigoma kabisa kuondoka.
“Sina kichaa.”
“Bali?”
“Namtaka Genesis wangu!”

“Kwani hufahamu kwamba ana kesi ya kujibu au unataka tukurudishe ndani?”
“Nipo tayari kurudi kama hamtamruhusu Genesis wangu. Yeye ndiyo kila kitu katika maisha yangu. Kama mnataka kunitoa lazima na yeye pia atoke, kama haiwezekani nirudisheni,” alisema Farida akilia kwa uchungu.

Kwa ndani walimwonea huruma sana, maana alionekana kuwa na mapenzi ya ndani yanayotoka katikati ya moyo wake kabisa. Hata hivyo sheria haikusema hivyo, yeye ndiye ambaye alionekana hana cha kujibu, kwa hiyo ilikuwa lazima atoke mwenyewe na isingewezekana kurudishwa ndani wakati kesi yake iliishia pale.

“Hebu njoo huku,” yule mpelelezi akasema akimvuta.
Wakaongozana hadi kwenye chumba cha mahojiano kisha akakabidhiwa kwa mpelelezi mwingine, halafu yeye akaondoka na kwenda kumtoa Genesis.
“Sikia mwenzako hana kesi ya kujibu, kwa hiyo tumemwachia.”
“Sawa, ni furaha yangu, maana ni kweli hana cha kujibu.”
“Lakini tatizo si hilo Genesis.”

“Kuna tatizo kwani afande?”
“Ndiyo lipo.”
“Gani?”
“Hataki kuondoka.”
“Kwa ini anakataa?”

“Anasema hawezi kuondoka bila wewe, ama na yeye arudishwe au na wewe utolewe.”
“Sasa?”
“Jambo hilo halitawezekana...sikia tunahitaji msaada wako katika hili. Naamini kinachomsumbua hapa ni mapenzi tu. Unatakiwa kuzungumza naye, ukimhakikishia kwamba hii kesi ni ndogo na utatoka hivyo yeye aondoke bila wasiwasi na kwamba ushahidi wake ndiyo ambao utakutoa wewe kwenye matatizo.

“Ni imani yetu kwamba baada ya kusikia kauli yako atakubali kuondoka. Tafadhali naomba utusaidie katika hili,” akasema mpelelezi huyo, macho yake yakionekana kumaanisha alichokisema.
Ni kweli alikuwa anahitaji msaada wa Genesis, lakini kilichokuwa ndani yake ni kuona Farida anaondoka, ndiyo maana akabuni njia hiyo ambayo aliamini ilikuwa nyepesi zaidi. Genesis hakutaka kukubaliana na jambo hilo haraka.

Alitumia muda mrefu kidogo kutafakari, kisha baadaye akafungua kinywa chake na kuzungumza.
“Najua mimi sitatoka, maana nakiri wazi kwamba nimeua, ila sitaki Farida wangu aendelee kupata matatizo hapa, nitazungumza naye.”
“Ahsante sana, nifuate.”

Wakaongozana hadi katika chumba alichokuwa amekaa Farida. Alipomuona Genesis tu, akaanza kulia.
“Zungumza na Genesis huyu hapa, ana maneno anataka kukuambia, sisi tunawapisha.”
“Sawa.”
Wale maaskari wakatoka nje ya chumba kile na kuwaacha wawili tu, robo saa baadaye waliporudi walikuta wakiwa wamekumbatiana.

“Vipi?” Mpelelezi mmoja akawauliza.
“Baki salama mpenzi wangu, nitakutetea mpaka mwisho, haki itataendeka, sitakubali kuolewa na mwanaume mwingine zaidi yako. Nitaendelea kujitunza kwa ajili yako maana wewe ndiye mwanaume wangu ninayekupenda kwa dhati,” akasema Farida akiwa hasikilizi maneno ya yule askari.

“Ahsante sana kwa maneno yako ya faraja Farida, Mungu atafanya kitu, nitatoka.”
“Nimefurahi kusikia hivyo, sipendi kukuona ukiwa katika hali ya unyonge.”
Hapakuwa na kitu kingine tena zaidi ya Farida kutolewa. Kwa bahati nzuri wazazi wake walikuwa tayari wapo nje wanamsubiri.
“Pole sana mwanangu,” mama Farida akamwambia mwanaye akiwa amemkumbatia.

“Ahsante mama.”
“Pole mama,” baba yake mzee Mbaraka akasema.
“Nashukuru baba.”
Kamera zote za vyombo mbalimbali vya habari zikahamia kwao. Hawakutaka kusubiri sana, Farida hakuwa tayari kusema chochote kwa waandishi wa habari. Waliondoka eneo lile haraka, wakatembea kwa miguu hadi Posta walipopanda daladala za Kwa Aziz-Ali na kwenda zao nyumbani. Furaha ikawa imerejea tena katika familia yao.

***
Muda mfupi baada ya Farida kutolewa, Profesa Mshana alifika katika Kituo Kikuu cha Polisi akiwa na mawakili wawili. Walipofika pale, akaomba kuzungumza kidogo na mke wake pamoja na mwanaye walioko selo.
Kwa umaarufu wake, jambo hilo halikuwa gumu kufanyika. Mara moja wakaitwa. Mmoja akaenda kuzungumza na mke wake na mwingine akaenda kuongea na Genesis yeye akiwa nao akiwasikiliza. Ni upande wa Genesis ndiyo ulikuwa mgumu zaidi maana ulihusisha mauaji.

“Genesis hujambo?” Profesa Mshana alianza kumsalimia mwanaye.
“Sijambo shikamoo baba!”
“Marhaba.”
“Shikamoo...” akamsalimia na yule wakili ambaye mpaka wakati huo alikuwa hajafahamu ni nani hasa.
“Marahaba kijana, pole na matatizo.”

“Ahsante sana.”
“Usiogope, nipo hapa kukusaidia, kila kitu kitaisha.”
“Genesis kutana na bwana Samson Johnson, huyu ni wakili kutoka J&P Advocates jijini Nairobi, Kenya. Yupo hapa kwa ajili yako, sasa lazima uwe mkweli, ili ajue namna ya kukusaidia.”

“Kunisaidia?”
“Ndiyo!”
“Ameshachelewa.”
“Kwanini?”
“Nimeshawakubalia askari kwamba nimemuua Bianca.”
“Kwani ni kweli?” Baba yake akamwuliza kwa mshangao.

“Ni kweli kabisa baba, hakuna uongo hapo na chanzo cha yote hayo ni ninyi na wewe baba unajua vizuri kuhusu hili. Ndoto zangu zote zinaishia gerezani, lazima nifungwe kama sitanyongwa!”
“Usiseme hivyo mwanangu, tuliza moyo wako kwanza.”

“Genesis nimeshakutana na kesi nyingi sana maisha mwangu, asilimia kubwa nimeshinda. Usijali, hata kama umeshakubali kuwa umeua tutashinda. Kikubwa hapa, endelea kusisitiza kuwa umeua hata ukipelekwa mahakamani sema umeua!” Wakili Samson akasema.
Profesa Mshana akabaki amepigwa na butwaa, alishindwa kuelewa ingewezekanaje mtu aliyekiri kosa akashinda kesi, alimwangalia Wakili Samson kwa jicho la maswali kisha akamwangalia mwanaye, roho ikamuuma sana.

Akiwa katika hali ile ya mshangao, simu yake ikaanza kuita. Alipotupa macho juu ya kioo cha simu yake, akakutana na jina ambalo hakulitegemea kabisa; DK. RWEGOSHORA NDIYE ALIYEKUWA AKIMPIGIA SIMU! Akaiangalia kwa muda, kisha akaikata kwa hasira.

“Si alishasema kila mtu ahangaike kivyake? Sitaki msaada wala ushirikiano naye wa aina yoyote ile, kila mtu ajihangaikie mwenyewe!” Akajikuta anatamka kwa sauti kubwa.
“Vipi Profesa mbona sikuelewi?” Wakili Samson akamwuliza Profesa Mshana, lakini hakumjibu.

KIMYA cha dakika nzima kilitawala katika chumba kile, Profesa Mshana akionekana kuwa na hasira. Hilo liliweza kusomeka katika uso wake uliokunja ndita. Si wakili Samson wala Genesis walioelewa kilichokuwa kinaendelea.
“Mzee kuna nini?” Wakili Samson aliuliza.
“Hapana.”

“Lazima kuna kitu. Ni nani anayakupigia simu?”
“Ni Dk. Rwegoshora, naye mkewe yupo katika kesi hii lakini alijitoa akasema kila mtu ashughulikie suala lake mwenyewe.”

“Sasa kwa nini usimpokelee ukamsikiliza?”
“Hapana tuachane naye.”
“Lakini...” kabla hajamalizia sentensi yake tayari askari alifika eneo lile.
“Muda umeisha naomba muondoke.”
“Tunaomba robo saa zaidi.”

“Kama dakika ishirini hazijawatosha haitawezekana zaidi ya hapo. Hata hivyo utaratibu wetu ni robo saa tu, naomba muondoke,” askari yule aliendelea kusisitiza.

Hawakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuondoka. Walikwenda moja kwa moja kwenye gari la Profesa Mshana kisha wakaelekea katikati ya jiji katika mgahawa maarufu wa Steers walipokaa na kuagiza vinywaji.

“Kesi mnaionaje?” aliuliza Profesa Mshana.
“Naona kama kuna ugumu fulani hivi,” alisema Wakili William Stanley kwa upole.
“Ugumu? Ugumu gani?” aliuliza Profesa Mshana akionekana kuingiwa na wasiwasi kidogo.
“Tatizo kuna watu watatuharibia.”
“Kivipi?”

“Kwa mujibu wa Mrs, wenzake hasa wale vijana wanakubali kufanya biashara ya madawa ya kulevya. Pia wanakiri kuhusika moja kwa moja na kuweka madawa yale kwenye begi la Farida, mbaya zaidi kuna mtu anaitwa Patrick ambaye yupo airport, kitengo cha ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka naye anakiri kushiriki katika hilo dili. Tutatokaje hapo?” alisema kwa mtindo wa kuuliza Wakili William Stanley huku uso wake ukionesha wasiwasi wa kushindwa.

“Ha!Ha!Ha! Mara hii umesahau ile kesi ya Kampala? Hilo ni tatizo dogo sana, kila kitu kitakwenda sawa na ninakuhakikishia hii kesi tutaimaliza,” alisema Wakili Samson Johnson.
“Oh, Yes! Nimekumbuka, nadhani tutatumia mbinu zilezile,” Wakili William Stanely alisema huku akionesha tabasamu.

Uso wake ulionesha matumaini mapya na kwa hakika aliiona kabisa njia ya kuimaliza ile kesi. Pamoja na hayo kwa Profesa Mshana ni kama alikuwa katika msitu mnene tena usiku kukiwa na giza wakati hana hata tochi.

Hata hivyo, hakuuliza kitu chochote tena, kikubwa alichoomba ni kuhakikishiwa familia yake itakuwa huru tena jambo ambalo Wakili Samon Johson alimpa asilimia mia moja.
***

Usingizi ulikuwa mgumu sana kupatikana, usiku huo Profesa Mshana aliifanya pombe kama maji ya kunywa. Kwanza aliingia nyumbani kwake saa 5:30 za usiku akiwa amelewa chakari jambo ambalo si kawaida yake.

Hakutaka mazungumzo yoyote na mlinzi wake Juma wala binti yake, akaingia moja kwa moja chumbani kwake kulala. Akiwa anaitafakari siku yake iliyopita ambayo ilikuwa ngumu kuliko kawaida, alifikia mahali akaikumbuka simu ya rafiki yake ambaye kwa sasa ni adui yake Dk. Rwegoshora.

Alimfikiria sana mtu huyo, pamoja na kwamba hakujua alitaka kumwambia nini lakini alihisi alikuwa na jambo zito la kumweleza. Taratibu akaanza kujilaumu kuacha kupokea simu yake.

Ni hapo sasa ndipo alipowasha simu na kutulia kisha akaanza kusoma meseji zilizoingia mchana mzima wa siku hiyo. Aliendelea kusoma, mara ujumbe mfupi ukaingia alipoutazama akagundua kwamba umetoka kwa Dk. Rwegoshora. Akaamua kuusoma.

“Najua una hasira lakini kumbuka sisi ni marafiki. Ni kweli mimi ndiyo chanzo cha uadui ulioingia kati yetu. Ni chanzo cha nyongo iliyomo ndani yako hivi sasa. Lakini lazima ufahamu kwamba urafiki wetu una thamani kubwa zaidi ya tatizo lililopo mbele yetu.

“Urafiki huu ungeweza kuwa ngao na mwongozo katika tatizo lililopo mbele yetu. Tafadhali legeza moyo wako, utakaposoma ujumbe huu unipigie na utambue kwamba mimi rafiki yako nimegundua kosa langu na ninahitaji kushirikiana na wewe ili tuweza kuzitoa familia zetu matatani.

“Kumbuka wewe na mimi tuna majina na heshima kubwa nchini, kushitakiwa pekee ni doa na kama unavyoona tayari magazeti yameshabadilisha habari, kila chombo ni sisi tu.

Tunahitaji kukutana na kuzungumza. Wewe ni mwanaume na mimi naamini utakubali kukutana na mimi na kuweka haya mambo sawa. Asante sana kwa kunielewa.” – Dk. Rwegoshora.

Profesa Mshana alihisi pombe ikumruka kichwani, ilikuwa ni meseji ndefu yenye ujumbe wa kumuumiza sana moyo wake na kwa hakika alisisimka na kuuona umuhimu wa kukutana na mwenzake ili kumaliza tatizo lililokuwa mbele yao.
Alivuta shuka na kulala usingizi lakini moyoni alijiahidi kitu cha kwanza kufanya siku inayofuata ni kukutana na Dk. Rwegoshora kwa ajili ya kumaliza tatizo linalowakabili.
***

“Nimefurahi sana ulivyokubali wito wangu, sasa tushughulikie suala la familia zetu,” alisema Dk. Rwegoshora akiwa na Profesa Mshana katika hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.

“Asante kwa kutambua ulipokosea. Hili suala ni letu sote hatuna budi kulishughulikia, siku zote wawili ni wawili tu. Labda nikuulize wewe umefikia wapi?”
“Kwa kweli hakuna nilipofikia, hali ni ngumu maana hii kesi imetoka mezani kwa Rais.”
“Rais?”

“Rais ndiyo, alitumiwa barua na Rais wa Saudi Arabia akamweleza kila kitu yaani hapa nimechanganyikiwa kabisa.”

“Kwa kweli kwa msimamo wa Rais wetu asiyependa rushwa wala kupindishwa sheria kutakuwa na tatizo kidogo lakini kuna njia nyingine ambayo kama hatutashindwa basi itapunguza angalau ugumu wa kesi.”

“Njia gani hiyo?”
“Tayari mawakili kutoka Nairobi katika Kampuni ya J&P Advocates wapo hapa nchini kwa ajili ya hii kesi, nadhani waishughulikie tu yote.”
“Ni wakali? Wataweza kweli?”

“Bila shaka unakumbuka ile kesi ya Waira Wamboi wa Kakamega?”
“Yeah! Si yule aliyekamatwa na kontena la madawa ya kulevya Kenya?”
“Huyo huyo.”

“Unakumbuka kesi yake iliishia wapi?”
“Nilisikia sikia kwamba eti ushahidi haukukamilika, baada ya hapo kimya mpaka leo.”
“Kwa taarifa yako ile kesi iliisha na walioimaliza ni J&P Advocates.”
“Basi watatufaa.”

Kikao kikafungwa wakiwa wamekubaliana kuwakabidhi kesi hiyo mawakili wa Kikenya.
***
Watu walikuwa wamefurika katika Mahakama Kuu ya Tanzania iliyopo jijini Dar es Salaam. Ilikuwa ni kesi iliyovuta hisia za watu wengi. Wengine walikosa nafasi na kusimama nje wakitaka tu kumshuhudia huyo Genesis.

Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliweka kamera zao sawa kumsubiri Genesis wakati akitoka na kuingizwa kwenye karandinga ili waweze kupata picha za kuuzia magazeti.
Ilikuwa ni kesi yenye utata sana, Patrick, Festo na Dulla wote walikubali shitaka lakini Mama Genesis na Mama Bianca pekee ndiyo waliokana shitaka. Hali ilikuwa tete zaidi baada ya Genesis ambaye ndiye kiunganishi mkuu wa kesi hiyo kupanda kizimbani na KUKIRI KUMUUA BIANCA!

Farida alipiga kelele mahakamani, maaskari wakamtoa nje. Hakuwa tayari kumpoteza mwanaume aliyempenda kuliko wote katika maisha yake. Hakujua nyuma ya majibu yale kulikuwa na kauli ya Wakili Samson Johnson. Hata hivyo, kesi ilikuwa imekaa vibaya.

Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 35


ILIPOISHIA

Siku ya kesi kutajwa ilifika, watu walifurika katika mahakama kuu hadi nje. Ilikuwa ni kesi iliyovuta hisia za watu wengi sana jijini Dar es Salaam. Kijana wa mjini Dulla, Patrick mfanyakazi wa uwanja wa ndege kitengo cha ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka na Festo mtaalam wa teknolojia ya mawasiliano, wote kwa pamoja walikubali kuhusika na madawa ya kulevya wakiwa wameagizwa na mama Genesis pamoja na mama Bianca ambao walikana shitaka.

Katika hali ya kushangaza sana, Genesis ambaye ndiye alikuwa kiungo wa kesi hiyo alipopanda kizimbani alikubali kumuua Bianca na kwamba mchezo mzima wa madawa ya kulevya aliujua na kuwa alikuwa na ushahidi. Mahakama nzima ilipigwa na butwaa.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

MAHAKAMA nzima ilizizima, kila mmoja akimshangaa Genesis. Kitendo cha kukubali kumuua mkewe Bianca kiliwashtua watu wengi maana ni kama alikuwa amekubali kufungwa. Alipokutanisha macho na mama yake mzazi, macho yao yalianza kutokwa na machozi.
Hata hivyo, Genesis alikuwa akilizwa na kitu kingine kabisa. Alikuwa akiumizwa sana na mpenzi wake Farida kutoka nje huku akipiga kelele. Alijua ni kiasi gani alikuwa anaumia lakini hakuwa na jinsi ya kukwepa maana aliona wazi kuwa lazima angefungwa kama siyo kunyongwa.

Kwa Genesis kufungwa au kufa kwa ajili ya Farida ambaye hakuwa na hatia katika kesi ya madai ya kutengenezwa, ilikuwa ni furaha kubwa. Hakujutia kifo chake, alikuwa tayari kufa muda wowote.
Hata hivyo, kwa mama yake hali ilikuwa tofauti, kwa maana aliona kama mwanaye anataka kumkandamiza katika kesi ile hatari. Baada ya washitakiwa kujibu tuhuma hizo, hakimu aliahirisha kesi hadi wiki mbili baadaye.

Watuhumiwa wote wakatolewa nje ya mahakama wakisindikizwa na polisi. Waandishi wa habari waliweka kamera zao tayari kupata picha nzuri za kuuzia magazeti. Genesis ndiye aliyepata wakati mgumu zaidi baada ya waandishi kumgombea ili kupata picha yake.
Kila Genesis alipokutanisha macho yake na Farida alikuwa akilia kifuani mwa mama yake akisikia uchungu sana moyoni mwake lakini hakuwa na la kufanya.
“Mpenzi wangu jamani unakwenda jela kwa kosa ambalo si lako, nitabaki na nani mimi?” Farida alitamka maneno hayo huku akilia.

“Tulia mwanangu, kila kitu kina sababu zake, Mungu atafanya kitu kwa ajili yako,” alisema mama Farida huku akiendelea kumbembeleza mwanaye.
Ilikuwa vigumu sana kwa Farida kumuelewa mama yake, machozi ndiyo yalikuwa faraja yake ya pekee iliyobakia, muda wote aliendelea kulia hadi Genesis alipopanda kwenye karandinga na kuondoka mahakamani hapo.

***
“Huu mwanzo unauonaje?” Profesa Mshana alimwuliza wakili Samson Johnson.
“Mzuri!”
“Mzuri vipi?”
“Kwa sisi wanasheria ni mwanzo mzuri sana tena nakuhakikishia tunashinda kesi.”
“Itawezekana vipi ikiwa wengi wanakubali shitaka? Kumbuka ni mke wangu na mke wa Rwegoshora pekee ndiyo waliokataa. Sasa unadhani tutashindaje?” Aliuliza Profesa Mshana akionesha wasiwasi mkubwa.

“Usiwe na wasiwasi, mimi nakuhakikishia ushindi.”
“Wiki mbili si nyingi!”
“Ni kweli, ni siku kumi na nne tu. Lakini naendelea kusisitiza ushindi ni wetu,” alisema wakili Johnson Samson.
“Ok!”

***
WIKI MBILI BAADAYE
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilifurika watu kama kawaida yake. Wengi walifika kwa ajili ya kushuhudia kesi ya Genesis ambayo ilikuwa gumzo jijini Dar es Salaam.
Kilichofanyika baada ya upelelezi zaidi ushahidi wa mawasiliano kati ya Bianca na Festo ulipelekwa mahakamani hapo na hakimu kuoneshwa. Kwa ushahidi huo kesi ilikuwa imekaa pabaya sana.

Kila mmoja aliyekuwa mahakamani aliamini kitu ambacho kingefuata kingekuwa ni wote kuozea jela. Mama Bianca na mama Genesis walipooneshwa ushahidi huo walishtuka sana. Wa kwanza kupandishwa kizimbani alikuwa ni Festo mtaalam wa teknolojia ya mawasiliano.
Wakili wa upande wa serikali, Dismas Tsengoma alisimama mbele ya kizimba alichokuwemo Festo na kuanza kumuuliza maswali.

“Bila shaka wewe ndiye Festo Linus?”
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Naamini umeona nakala ya mawasiliano iliyoletwa na shahidi wa upande wa serikali inayoonesha mawasiliano yanayodaiwa ni kati yako na marehemu Bianca.”
“Ndiyo mheshimiwa.”

“Unayatambua?”
“Ndiyo mheshimiwa.”
“Kwamba ni kweli ulikuwa unawasiliana naye?”
“Mheshimiwa labda nifafanue zaidi ni kweli zile nakala nilizituma kwenye e-mail ya marehemu Bianca ambaye alitakiwa kuolewa na Genesis lakini mawasiliano hasa yalikuwa ni kati yangu na mama Genesis.”
“Unaitambua au huitambui?”

“Naitambua.”
“Ni yako?”
“Bila shaka.”
“Sina maswali zaidi mheshimiwa.”
Mwendesha mashitaka akamwamuru Festo ashuke kizimbani kisha mama Genesis akaitwa. Alipopanda wakili namba mbili wa upande wa serikali alifika na kuanza kumhoji maswali.
“Tunayo nakala inayoonesha Farida kuitwa katika Chuo Kikuu Huria cha Riyadh, Saudi Arabia. Inaelezwa wewe ulimwagiza Festo aghushi, unaiambia nini mahakama kuhusu hilo?”
“Mheshimiwa siitambui hiyo nakala.”

“Lakini Festo anakubali kwamba yeye ndiye aliyetengeneza na kwamba ulimlipa fedha kwa kazi ya kughushi barua ya wito wa kujiunga katika chuo hicho ili wewe uweze kufanya njama za kumwekea madawa ya kulevya kwenye begi lake ukiwa tayari umeshakubaliana na Patrick aipitishe uwanjani.

“Hata hivyo, katika kesi hii Patrick amekubali kufanya jambo hilo kwa malipo ya fedha mlizokubaliana, bado unaendelea kukataa?”
“Ndiyo mheshimiwa, sikubaliana na hilo. Unajua mheshimiwa naomba mahakama hii isiwaamini hawa watu maana kinachoonekana ni kwamba wamepandikizwa ili wanichafue jina langu pamoja na mume wangu hasa ukizingatia tuna mafanikio makubwa na umaarufu nchini.”
“Lakini unamfahamu Farida?”

“Ndiyo mheshimiwa.”
“Unamfahamu vipi?”
“Alikuwa rafiki wa mwanangu, tangu wakiwa shuleni Morogoro malengo yao yalikuwa ni kuoana.”
“Walioana?”
“Hapana.”
“Kwa nini?”

“Sijui kilichotokea lakini walitofautiana wenyewe baada ya kupata habari kwamba eti alipokwenda chuoni Saudi Arabia alikutwa na madawa ya kulevya hapo ndipo Genesis alipobadilisha mawazo na kutangaza nia ya kutaka kumuoa marehemu Bianca.”
Mahakama nzima ikaangua kicheko, alikuwa akiongea kwa huruma sana lakini alionekana wazi kujichanganya mwenyewe. Maelezo yake yalipinda na kulikuwa na kila dalili kwamba alihusika na njama za kumwangamiza Farida.

Maneno yale yalikuwa machungu, yaliyomchoma sana Farida moyoni mwake, alipogonganisha macho yake na Genesis alianza kulia. Wakili akasema kwamba hana maswali zaidi ndipo mama Genesis alipotakiwa kushuka kisha Genesis kupandishwa kizimbani.

Kabla ya kuulizwa swali lolote tayari Genesis alianza kulia kwa uchungu kisha akasogelea kipaza sauti na kupiga kelele: “MAMA ACHA KUIDANGANYA MAHAKAMA, UNAJUA KILA KITU, NINA USHAHIDI WA KUTOSHA NA WALA HUWEZI KUKWEPA KITANZI. NAJUA NITAKUFA, LAKINI NITAKUFA KISHUJAA NIKIWA NA FURAHA MAANA FARIDA WANGU ATAKUWA NJE NA MALENGO YENU YA KIPUUZI YATAKUWA YAMESHINDWA.”
Wakili Samson Johnson na William Stanley wakaangaliana kisha wakarudisha macho yao chini. Kesi ilikuwa bado mbichi! Njia ya kuwanasua ikaonekana kusonga, kukawa na giza nene mbele yao.


GENESIS alikuwa na hasira sana, ni kama alikuwa amechanganyikiwa. Alimchukia sana mama yake, kwake hakuwa na thamani tena. Aliamini kama si yeye angekuwa amemuoa Farida na matatizo yote haya yasingetokea.

Alikuwa tayari kwa chochote, aliona gereza mbele yake lakini hakujali. Furaha yake ilikuwa ni Farida awe huru. Alitamani sana mama yake pamoja na mama yake Genesis wote waozee jela, aliamini hiyo ndiyo ingekuwa dawa pekee na funzo kwao.
“Genesis taratibu, hii ni mahakama jaribu kuiheshimu,” mwendesha mashitaka alimwambia Genesis akimkazia macho.

“Moyo unaniuma hafai huyu mama kabisa,” alisema Genesis huku akiendelea kumwaga machozi.
“Wakili upande wa serikali...” mwendesha mashitaka aliita, kisha Wakili Dismas Tsengoma akasogea mbele.
“Maswali ya kuhoji,” alisema mwendesha mashitaka.
“Wewe ndiye Genesis?”

“Bila shaka.”
“Unafahamu nini juu ya kesi hii?”
“Nimeshatoa maelezo yangu tangu polisi yapo vile vile sina cha kubadilisha.”
“Genesis mahakama inataka kusikia sauti yako hebu tuambie hata kama umeshatoa maelezo.”
“Ninachojua ni kwamba Farida alibambikiziwa madawa ya kulevya.”
“Na nani?”

“Mama yangu, mama yake Bianca akishirikiana na wale pale,” akasema akionyesha mkono walipokaa kina Patrick na wenzake.
“Je, ni kweli kwamba ulimuua Bianca?”

“Kwa asilimia mia moja tena kwa mkono wangu mwenyewe. Kwa taarifa yako nilimuua kwa kumchoma kisu kifuani,” alisema Genesis kwa kujiamini.
Wakili Tsengoma alishangaa sana, katika maisha yake hakuwahi kukutana na mtuhumiwa anayekubali kosa kirahisi kama Genesis. Mahakama nzima ilikuwa ikimhuzunikia, kulikuwa na kila dalili kwamba kesi ile ingemwelemea.

“Unafahamu kwamba kwa kosa la kuua unaweza kunyongwa?”
“Tena ndiyo furaha yangu, sioni sababu ya kuvuta hii kesi, kama inawezekana jambo hilo lifanyike haraka sana.”

Majibu ya Genesis yaliwashangaza wengi mahakamani, hakuogopa kufa, hakuogopa kesi ile kabisa. Alikuwa tayari kwa lolote.
“Sina maswali zaidi mheshimiwa,” alisema Wakili Tsengoma ambaye aliiwakilisha serikali mahakamani hapo.

“Wakili upande wa utetezi,” alisema mwendesha mashitaka.
Muda huo huo Wakili Samson Johnson alisogea mbele akiwa amevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai fupi nyeusi iliyoishia kwenye kola. Uso wake ulionyesha wazi kuwa na matumaini makubwa tofauti kabisa na matarajio ya wengi ambayo yalionyesha kwamba Genesis na wenzake wangeshindwa kesi ile.

“Nakaribisha maswali kutoka kwa wakili,” mwendesha mashitaka alisema.
“Genesis Mshana...” aliita Wakili Samson Johnson.
“Naam.”
“Unafahamu umesimama wapi?”
“Uliza maswali yenye akili.”

“Naomba ujibu swali langu Genesis.”
“Yeah! Hapa ni mahakamani.”
“Unafahamu una kesi gani ya kujibu?”
“Ndiyo.”

“Ni nini?”
“Ni kuhusu Farida.”
“Hebu toa maelezo yanayoeleweka Genesis. Hiyo kesi inamhusu vipi Farida wakati hayupo hapa mahakamani?”
“Yupo.”

“Yuko wapi?”
“Yuleee,” alisema Genesis akionyesha kidole mahali alikokaa Farida.
“Simaanishi sehemu aliyokaa, ila nazungumzia kuhusu uwepo wake katika hii kesi. Unafahamu kwamba yeye ni shahidi namba moja wa hii kesi na wala si mshitakiwa?”
“Sifahamu!”

“Unamfahamu Bianca?”
“Ndiyo.”
“Ni nani?”
“Aliwahi kuwa mke wangu, ndoa iliyodumu kwa saa chache kabla hajafa.”
“Hivi alikufa?”

“Ndiyo.”
“Ilikuwaje?”
“Nilimuua mimi, tena nafurahi hayupo tena duniani, najisikia amani sasa.”
“Unafahamu mimi nimesimama hapa kwa kazi gani?”
“Wewe si mwanasheria?”

“Hakuna yeyote aliyeko mahakamani hapa asiyejua kwamba mimi ni mwanasheria, lakini nataka kujua wewe unafahamu nini juu ya uwepo wangu katika hii kesi?”
“Uliza maswali ya msingi hayo si maswali ya kuuliza.”
“Na labda nikuulize Genesis, unafahamu jinsia yako?”
“Hayo tena sasa matusi.”

“Sina maswali zaidi mheshimiwa.”
Wakili Samson Johnson aliondoka akiwa anatabasamu na kurudi sehemu yake aliyokuwa amekaa. Kilichofuata kilikuwa ni shahidi wa kwanza Farida Mbaraka kutoa ushahidi wake alipomaliza naye alishuka na kwenda kukaa.

“Tumepitia vipengele vyote kwa umakini mkubwa, ningetamani kumaliza hii kesi leo, lakini natoa nafasi moja kwa ambao wana maelezo zaidi au pingamizi kabla sijatoa hukumu ya kesi hii,” alisema hakimu wa kesi hiyo Francis Mutabuzi.

Wakili Samson Johnson akanyoosha mkono na kuruhusiwa kusogea mbele. Alionekana kujiamini sana, ni kama alikuwa na hoja za msingi.

“Mheshimiwa hakimu, kutokana na maelezo ya mteja wangu naomba nikiri kwamba sikubaliana naye. Hata maelezo ya washitakiwa wengine wanaohusika katika kesi hii yanaonekana kukinzana.
“Mheshimiwa hakimu kama unafuatilia majibu ya maswali yake yote yaliyoulizwa katika kesi hii hususan nilipomwuliza mimi ambaye hapa natambulika kama wakili upande wa utetezi, inatia mashaka.

“Nina mashaka na afya yake, ninahisi ana tatizo katika ubongo wake. Yawezekana hajaua, lakini pia inawezekana akawa ameua ila majibu yake yanaonyesha kwamba kinachotoka kinywani mwake hakina ukweli maana mara kadhaa amekuwa akipindishapindisha.

“Kwa maelezo hayo basi, naomba mahakama yako tukufu ikubali ombi la kumpeleka mteja wangu katika hospitali kubwa inayotambuliwa na serikali kwa usimamizi wenu wenyewe ili apimwe na kugundua kama ubongo wake uko sawasawa. Asante sana mheshimiwa hakimu!” alisema Wakili Samson Johnson kwa sauti ya utulivu sana.

Mahakama nzima ilikuwa kimya, wengi walionekana kumhurumia Genesis. Pamoja na kwamba walichukizwa na uamuzi wake wa kumuua Bianca, wengi walionekana kuwa upande wake kutokana na uamuzi ule kuonekana kwamba ulisababishwa na mama Genesis na mwenzake mama Bianca.
“Mahakama imekubali ombi la wakili upande wa utetezi, kwa maana hiyo watuhumiwa watarudi mahabusu, taratibu zote juu ya Genesis kufanyiwa vipimo zitafanyika.

“Baada ya mwezi mmoja kesi hii itakapotajwa tena, hati kutoka hospitalini itasomwa mahakamani hapa kabla ya hukumu kutolewa. Naahirisha kesi hii hadi mwezi mmoja ujao,” alisema hakimu Mutabuzi.

“Koooorti!” ilisikika sauti ya kuahirisha mahakama.
Watu wote wakasimama, hakimu akatoka katika chumba cha mahakama, watuhumiwa wakatolewa nje, kisha watu wengine nao wakatoka nje ya mahakama. Kesi bado ilikuwa ngumu.
“Vipi mzee mwenzangu?” Profesa Mshana alimuuliza Dk. Rwegoshora.

“Sasa naanza kuwaamini J&P Advocates!” alisema Dk. Rwegoshora akitabasamu.
“Kuna matumaini?” Profesa Mshana akauliza tena.
“Tena makubwa sana!” Dk. Rwegoshora akajibu.
Wakatoka nje wakiwa wameongozana.

Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 36



ILIPOISHIA

Kabla ya hukumu kutolewa, wakili Samson Johnson alitoa hoja kwamba, ana wasiwasi na afya ya mteja wake, hasa kutokana na kupishana naye, akiwa amesimama kama wakili upande wa utetezi; hoja hiyo ilikubaliwa na hakimu.

Kesi ikaahirishwa hadi mwezi mmoja baadaye, ambapo hakimu alisema kwamba, hati ya hospitalini itafikishwa mahakani hapo kabla ya hukumu kutolewa.

Profesa Mshana alionekana kuingiwa na wasiwasi kidogo na hoja ya wakili Samson Johnson, wakiwa wanatoka nje, akamwuliza Dk. Rwegoshora kuhusu mwenendo wa kesi hiyo, akamjibu kwamba mwelekeo ni mzuri kabisa, jambo lililomshangaza sana.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

PROFESA Mshana aliona kama ndoto ya kushangaza, kushinda kesi ile ingawa aliwaamini sana J&P Advocates wakiongozwa na Wakili Samson Johnson. Aliongozana na Dk. Rwegoshora hadi nje, ambapo walisimama mahali na kuendelea kubadilishana mawazo.
“Bado naona giza kidogo mbele yetu!” Profesa Mshana akamwambia Dk. Rwegoshora akimtazama usoni.

“Hakuna giza ndugu yangu!”
“Kwa nini?”
“Kipo kitu cha kufanya.”
“Lakini vipi kuhusu kauli ya wakili?”
“Ni nzuri sana, ndiyo maana nimekwambia naanza kuwaamini zaidi ya awali.”
“Unadhani Genesis ataonekana ana kichaa?”
“Vipimo havitaonesha hivyo, lakini pesa itaongea.”

“Mh!”
“Mbona unaguna?”
“Najaribu kuona jinsi mtiririko ulivyo mgumu.”
“Ni mwepesi kama kunywa maji vile.”
“Kwa nini?”
“Ingia kwenye gari twende, nimeshaongea na mawakili, wanajua pa kutukuta.”
“Sawa.”

Wote wakaingia kwenye magari yao, Dk. Rwegoshora akatangulia, Profesa Mshana akamfuata kwa nyuma. Aliendesha akimfuata, mpaka alipoingia kwenye jengo moja refu, ambalo alilifahamu vizuri sana.
Walikuwa wakiingia katika geti la Hospitali ya Rufaa ya Ilumina, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Hapo akaanza kuhisi jambo.

Dk. Rwegoshora alipoegesha gari lake, Profesa Mshana naye akaenda kuegesha jirani yake. Akiwa ndiyo kwanza anashusha mguu wa kwanza ardhini, gari la kukodi wanalotumia mawakili wa J&P Advocates liliingia hospitalini hapo na kuegesha sehemu ile ile waliyoegesha.
“Vipi?” Profesa Mshana akasema akimwangalia Dk. Rwegoshora.

“Usiogope, najua kila kitu kwako ni kipya, lakini labda kwa kukufahamisha tu ni kwamba, tumeja hapa kwa ajili ya kukutana na Mganga Mkuu, ambaye atatusaidia kuhusu vipimo vya Genesis!”
Hapo kidogo Profesa Mshana akaanza kupata mwanga wa kilichokuwa kikiendelea.
“Unataka kuniambia kwamba, tumekuja kwa ajili ya kutengeneza majibu?”
“Ndiyo!”

“Dah! Hapo mtakuwa mmecheza.”
“Kazi ndogo sana hii.”
“Lakini tuna uhakika gani kwamba lazima watamleta hapa kwa vipimo?”
“Uhakika hakuna, lakini hii ni hospitali kubwa kabla ya kufikiria Muhimbili, hivyo kama ikitokea wakampeleka sehemu nyingine, huyu dokta atatushirikisha.”
“Sawa.”

“Ok! Twende.”
Wote wakaongozana hadi kwenye mgahawa wa hospitali hiyo, wakaagiza vinywaji kisha wakatulia kwa muda, kabla ya muda mfupi baadaye, Dk. Rwegoshora kutoa simu yake na kumpigia. Iliita kwa muda mfupi sana, akapokea.
“Ndiyo Dk. Rwegoshora,” ilikuwa ni sauti ya upande wa pili ikipenya kwenye sikio la Dk. Rwegoshora.

“Habari yako Dk. Lyatuu?”
“Salama, bila shaka mmeshafika?”
“Ndiyo!”
“Ok! Naombeni mje moja kwa moja ofisini kwangu.”
“Sawa, baada ya dakika bili tu, tutakuwa hapo.”
“Karibuni sana.”

Hawakuwa na muda wa kuendelea na vinywaji tena, cha muhimu ilikuwa ni kukutana na Dk. Lyatuu. Wakainuka vitini na kuanza kutembea kwenye korido kwenda ofisini kwa Dk. Lyatuu.
“Karibuni sana.”
“Tunashukuru sana dokta.”
“Jamani huyu ndiye Dk. Lyatuu,” akasema Dk. Rwegoshora akiwataza wote kwa zamu.
“Tunashukuru sana!” Wote wakaitikia.

“Kutana na Profesa Mshana, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Global Engineering, huyu ni rafiki yangu wa siku nyingi, mkewe na mwanaye wapo katika ile kesi niliyokuambia.”
“Ok! Karibu sana profesa.”
“Nashukuru.”

“Hawa ni Samson Johnson na William Stanley kutoka J&P Advocates ya Kenya, ambao ndiyo wanaotutetea katika kesi hii.”
“Sawa, karibuni sana.”
“Tunashukuru.”

“Hatuna mazungumzo zaidi, kikubwa ni kwamba tumekuletea mzigo wako, kazi ipo mikononi mwako. Sikufundishi namna ya kufanya,” akasema Dk. Rwegoshora akifungua mkoba wake na kutoa bahasha ya khaki na kumkabidhi Dk. Lyatuu.
“Ahsante sana,” akashukuru akiipokea ile bahasha.
“Mambo yamekwenda vile vile, ombi letu limesikilizwa na Genesis atapelekwa hospitalini kwa ajili ya vipimo.”

“Lipo ndani ya uwezo wangu.”
“Tunashukuru sana, hiyo fedha ni yote.”
“Sawa, ahsante kwa yote. Nawashukuru sana.”
“Ok!”
Wakaondoka hospitalini hapo wakiwa na matumaini makubwa ya kuelekea kushinda katika kesi ile.

***
MWEZI MMOJA BAADAYE
Mahakama ilikuwa imefurika sana siku hiyo, ilikuwa ni siku ya hukumu, hivyo kila mmoja alikuwa na hamu ya kusikia hatma ya kesi hiyo ingekuwa ni nini. Tayari shughuli za mahakama zilikuwa zimeshafunguliwa.
Hakimu alikuwa kimya kwenye kiti chake, baadaye Wakili wa Serikali akatoka mbele baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mwendesha mashitaka.

“Mahakama inatarajia utakuwa umefika na ushahidi wako wa mwisho juu dhidi ya watuhumiwa.”
“Bila shaka mheshimiwa!” Akasema Wakili Tsengoma.
“Unaweza kuusoma?”
Wakili Tsengoma akasoma ushahidi wake, zilikuwa ni karatasi zilizoonesha mawasiliano yaliyotoka kwa Festo kwenda kwa Bianca, jinsi mwenendo mzima wa mchoro wa kumjibu maombi feki ya kuitwa katika Chuo Kikuu Huria cha Riyadh, Saudi Arabia.

Ushahidi ambao ulikubaliwa na Genesis, Farida aliyekuwa shahidi pamoja na Festo. Baada ya hapo, mwendesha mashitaka alimtaka Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kanda ya Dar es Salaam, kutoa majibu ya vipimo vya Genesis.
Dk. Titus Kabitus alisoma hati ya hospitali ambayo ilonesha kwamba, Genesis alikuwa na matatizo ya afya ya akili; akisumbuliwa na mfadhaiko.

“Tatizo hilo, huwapata watu ambao wamepata au kugundua taarifa za kushtusha, ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaharibu mustakabali wa mipango yao au kugharimu maisha yao.
“Mgonjwa mwenye tatizo hili, kama hatakuwa chini ya uangalizi mzuri, anaweza kufanya matukio makubwa ya kutisha kutokana na msukumo wa hali yake, lakini mwisho wake hujuta hasa baada ya kupata matibabu na hali yake kurejea.

“Nashukuru sana mheshimiwa, hiyo ni hati ya hospitali baada ya kuchukua vipimo kutoka kwa mgonjwa Genesis Mshana kwa amri ya mahakama yako. Ahsante sana, naomba kuwasilisha,” akasema Dk. Kabitus akipeleka hati kwa mwendesha mashitaka ambaye alimpatia hakimu.
“Baada ya maelezo hayo kutoka kwa wakili wa serikali na hati ya Mganga Mkuu kutoka Hospitali ya Kanda ya Dar es Salaam, mabibi na mabwana. Tumepitia kwa uangalifu mkubwa shauri hili.

“Aidha, tumezingatia vipengele vyote, kuanzia ushahidi uliowasilishwa kutoka katika pande zote mbili, matokeo ya hospitali, kutokana na mamlaka niliyopewa na serikali, natoa hukumu katika kesi hii kama ifutavyo; Dulla na Patrick nawahukumu kifungo cha miaka kumi kila mmoja jela, kwa kosa la kuhusika na dawa za kulevya,” akasema hakimu Francis Mutabuzi na kuwageukia mama Bianca, Genesis na mama yake.
Akaanza kuzungumza tena...

MAHAKAMA nzima ilikuwa kimya kabisa kumsikiliza hakimu ambaye alikuwa anatoa hukumu. Kila mmoja alikuwa na hamu ya kusikia hatima ya Genesis, mama yake na Bi. Rwegoshora. Hakimu Mutabuzi aliteremsha miwani chini kidogo kisha akaanza kuzungumza tena:

“Festo ambaye katika kesi hii unatajwa kuhusika katika kutengeneza hati bandia za Farida kuitwa chuoni Saudi Arabia, mahakama imeridhishwa na ushahidi ulioletwa lakini pia umezingatia maelezo yako na hivyo umekutwa na hatia.

“Kwa mamlaka niliyopewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikiwa kama hakimu wa mahakama hii kwa amri ya Katiba ya nchi kwa kuzingatia vifungu vyote vya sheria nakuhukumu kwenda jela miaka saba ili liwe fundisho kwako na kwa wengine wenye tabia kama yako.”
Mahakama ikawa kimya kusikiliza hatma ya wengine waliobakia.

“Bi. Rwegoshora na Bi. Mshana ninyi ni wanawake hatari sana. Kwanza mmeshindwa kutambua hisia za vijana wenu na kuanza kupandikiza chuki ili muweze kutimiza malengo yenu. Mmefanya njama kwa kuwahadaa hawa vijana ili watengeneze njama za kumwekea Farida madawa ya kulevya na baadaye kukamatwa nchini Saudi Arabia.

“Lengo lenu lilikuwa baya, mlitaka auawe maana mlijua sheria za huko. Na kwa hakika kama sio Genesis leo hii Farida angekuwa amekufa na dunia nzima ingeamini alikuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya jambo ambao si kweli.

“Kwanza mna shitaka la dawa za kulevya lakini pia mmeghushi nyaraka jambo ambalo lilitaka kugharimu maisha ya binti mdogo Farida. Baada ya kupata maelezo ya pande zote mbili, ushahidi uliwasilishwa mahakamani hapa pamoja na utetezi wa mawakili wenu, mahakama imewakuta na hatia na lazima mhukumiwe kwa mujibu wa sheria.

“Kwa mamlaka niliyopewa, kupitia mahakama hii nawahukumu miaka kumi na tano jela kila mmoja ili liwe fundisho kwenu na kwa watu wengine wenye tabia kama zenu. Ninyi ni wazazi wabaya sana,” alisema Hakimu Mutabuzi.

Kauli hiyo ilikuwa mwiba kwa Dk. Rwegoshora na rafiki yake Prof. Mshana ambao walishindwa kujizuia na kuinamisha vichwa vyao chini wakijifunika kwa vitambaa, ni dhahiri walikuwa wakilia.

Genesis alikuwa anahema kwa kasi, bado hakujua hatma yake ingekuwaje. Alitamani kuwa huru maana alimpenda sana mpenzi wake Farida. Alitamani kutoka ili aweze kumuoa.
Masikio yake yalikuwa kwa hakimu akitaka kujua adhabu yake.

“Genesis Mshana, tumezingatia vipengele vyote katika shauri hili. Ni kweli umepatikana na hatia ya kumuua Bianca lakini kwa namna moja ama nyingine mauaji haya uliyafanya kwa kusababishwa.

“Hata hivyo, utetezi wa wakili wako na hati kutoka Hospitali ya Kanda ya Dar es Salaam kwamba una matatizo katika ubongo wako unatufanya tuamini wakati wa tukio hilo hukuwa na akili zako timamu. Hata hivyo, maelezo kutoka katika hati ya hospitali inaonesha kwamba bado hujapona.

“Hivyo basi mahakama imezingatia yote hayo na kutambua mchango wako wa kumwokoa Farida ambaye alibambikizwa kesi ya madawa ya kulevya na washitakiwa wanaotajwa katika shauri hili.

“Kutokana na hayo yote, Genesis nakuhukumu kwenda jela miaka mitano ili iwe fundisho kwako na wengine wanaoweza kujichukulia sheria mkononi kama wewe,” alisema Hakimu Mutabuzi huku akigonga meza.

“Kama mahakama ilivyoamua!” mawakili upande wa serikali walisimama na kusema hayo.
Huo ukawa ndiyo mwisho wa kesi. Vilio vikatawala mahakamani hapo. Farida alikuwa akilia kwa furaha. Miaka mitano kwake haikuwa mingi, aliamini baada ya kipindi hicho angetoka na angefunga naye ndoa.

Baada ya hayo, akina Genesis walitolewa nje kisha wakapelekwa ofisini, walipokamilisha taratibu zote walipakiwa kwenye karandinga kwa safari ya kwenda kuanza maisha mapya gerezani.

Kamera za waandishi wa habari ziliwaelekea wao. Kila mwandishi alitaka kupata picha nzuri kwa ajili ya kuuzia gazeti lake siku inayofuata. Ilikuwa ni kesi iliyovuta hisia za watu wengi jijini Dar es Salaam na nchi nzima.

***
“Hongera sana,” alisema Dk. Rwegoshora akimpa mkono Wakili Johnson Samson kutoka J&P Advocates.
“Nashukuru sana mzee.”
“Hongereni, mmejitahidi kwa kiasi kikubwa sana!”

Wakati hayo yakitokea Prof. Mshana alikuwa kimya akiwaangalia mawakili kwa hasira. Alimshangaa sana mwenzake kuwapongeza maana watuhumiwa wote walifungwa.
“Vipi ndugu yangu mbona umekunja uso?” aliuliza Dk. Rwegoshora.
“Nakushangaa unawapa hongera za nini wakati kesi wameshindwa? Kumbuka tumewapa pesa nyingi sana hawa mabwana!” alisema kwa hasira Prof. Mshana.

“Sifurahii wake zetu kufungwa lakini pia sikulaumu kwa hili maana hauifahamu sheria vizuri. Acha nikuambie, kama si hawa mabwana, kama wake zetu wasingenyongwa basi wangeozea jela.

“Miaka kumi na tano ni michache sana, kumbuka nipo katika kitengo nyeti, naweza kufanya kitu fulani baada ya muda na wote wakatoka kwa msamaha wa rais. Tushukuru kwa yote lakini tutakuwa tumejifunza kitu fulani,” alisema Dk. Rwegoshora akimuangalia Prof. Mshana.
Prof. Mshana alikuwa kimya kabisa, hakusema neno lolote, alikuwa na uchungu sana na mkewe pamoja na mwanaye Genesis.

“Piga moyo konde rafiki yangu, lazima ukubaliane na ukweli. Fahamu kwamba kama si hawa mawakili ingekuwa kesi mbaya sana kwa familia zetu lakini imekuwa afadhali kidogo kwa hukumu iliyotolewa.”

Ilikuwa vigumu sana kwa Prof. Mshana kuelewa lakini kadri Dk. Rwegoshora alivyozidi kuzungumza naye ndivyo naye alivyoendelea kumwelewa taratibu. Waliendelea kusimama pale nje mpaka waliposhuhudia wakina Genesis wakipandishwa kwenye karandinga na kupelekwa gerezani. Kamera za waandishi zikafanya kazi yake.

Dk. Rwegoshora na rafiki yake Prof. Mshana hawakuwa na kitu cha kusubiri zaidi, wakaongozana na mawakili wao hadi nyumbani kwa Prof. Mshana, Msasani, huko wakawalipa kiasi cha fedha kilichosalia na kupongezana kwa jinsi walivyoitetea kesi ile na kupunguza idadi ya miaka ya kifungo.

***
“Afadhali mama, sasa nitaishi kwa furaha,” alikuwa ni Farida akimwambia mama yake muda mfupi baada ya kutoka mahakamani.
“Kwa nini mwanangu?” Mama yake akamwuliza kwa sauti ya upendo.
“Kesi imeisha leo na Genesis amefungwa miaka mitano tu. Huwezi kuamini mama!”
“Kwa hiyo?”

“Mama huoni kwamba atatoka mapema, aje kunioa?”
“Bado una mawazo na huyo kijana mpaka leo, unataka mpaka akuingize kaburini siyo?” Mama yake akamwuliza kwa sauti ya ukali.
“Siwezi kuacha kumpenda Genesis wangu, yeye ndiye mwanaume wa maisha yangu, niliyemchagua kwa moyo wangu wote,” Farida alimwambia mama yake kwa kujiamini sana.

Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 37



Bi. Rwegoshora na Bi. Mshana walihukumiwa kifungo cha miaka kumi na tano kila mmoja jela baada ya kupatwa na hatia ya kula njama za kutengeneza wito bandia, kujihusisha na madawa ya kulevya na kusababisha kifo cha Bianca.

Genesis Mshana, kutokana na hati ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kanda ya Dar es Salaam, Dk. Titus Kabitus, iliyoonesha kuwa wakati akifanya tukio la mauaji alikuwa na matatizo ya akili, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

Hiyo ikawa furaha kwa Farida ambaye alirudi nyumbani kwao na kumweleza mama yake nia yake ya kuolewa na Genesis. Mama yake hakuwa tayari, akakasirika sana, lakini Farida aliendelea kusisitiza kwamba kwa kuwa alimpenda Genesis kwa moyo wake hataacha kumpenda milele.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO katika sehemu hii ya mwisho...

ZILIKUWA hisia kali kutoka ndani ya moyo wa Farida ambazo kwa hakika zisingeweza kubadilishwa na kitu chochote. Alikiri ndani ya nafsi yake kwamba alimpenda Genesis na isingekuwa rahisi kumuacha!

Alimwangalia mama yake kwa macho yaliyoonesha kilichomo ndani yake, alikuwa mwenye huzuni na uchungu mwingi kutokana na kauli ya mama yake kupingana na mapenzi yake kwa Genesis.
“Nimekwambia sitaki kusikia habari za huyo kijana tena. Kumbuka sisi ni masikini hatuna chochote, hatutaweza kupambana nao. Mpaka sasa umeshasababisha matatizo katika ile familia.

“Bianca ameuawa, yote hiyo ni kwa sababu yako, mama yake amefungwa, huyo Genesis wako pamoja na mama yake nao wapo jela. Ni kwa sababu yako. Unadhani watanyamaza? Inawezekana wakanyamaza, lakini vipi kama watagundua kwamba bado una nia na mtoto wao? Unataka tuuawe?” alisema mama Farida kwa sauti ya uchungu.

“Mama... kwa nini unakuwa na mawazo potofu kiasi hicho? Nani wa kutuua? Nani wa kutufunga? Hakuna mtu aliye juu ya sheria mama. Kama fedha ingekuwa ndiyo sheria, basi wasingefungwa!

“Kilichofanyika mama ni sheria kutenda haki. Kumbuka kama siyo Genesis, leo tungekuwa tunazungumza mengine. Nisingekuwepo mama. Ningeshauawa na Waarabu, nilikuwa tayari nipo kwenye mti, nimefungwa kamba na kitambaa cheusi usoni.

“Kilichokuwa kinasubiriwa ni hesabu kutimia kisha risasi zianze kuingia mwilini mwangu, hivyo tu! Lakini baada ya Genesis kutokea, ndiyo maana leo hii naongea na wewe. Ni Mungu tu, naamini hakutaka mimi nife na bila shaka ana mpango na maisha yangu na Genesis.

Naomba uniamini na ubadilishe mawazo yako tafadhali!” alisema Farida kwa sauti ya uchungu huku macho yake yakilengwalengwa na machozi.
“Haya bwana, tutaona. Ni lazima uzungumze na baba yako lakini sidhani kama atakuelewa,” alisema mama Farida.

***
Walikuwa wamekaa nje kwenye mkeka wakipata chakula cha usiku. Mzee Mbaraka, baba yake Farida alionekana kuwa mwenye furaha ingawa haikujulikana furaha yake ilitokana na nini hasa. Wakiwa wanaendelea kula, mama Farida akaanzisha mazungumzo.

“Baba Farida, umesikia ya huko mahakamani?”
“Ndiyo, nimesikia kwenye redio. Si kuhusu hukumu?”
“Hiyo kila mtu anajua, tayari vyombo vya habari vimeshaanza kutangaza lakini kuna hoja ya mwanao!”

“Hoja ya nini tena?”
“Eti bado anawaza kuolewa na Genesis!”
“Sitaki kusikia upuuzi kama huo. Shukuru Mungu amekusaidia umekiepuka kifo. Kwa taarifa yako, amepatikana mfadhili ambaye atakulipia chuo, tayari ameanza kukutafutia nafasi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii.

“Sitaki kusikia mambo ya huyo Genesis tena, sasa hivi unatakiwa uelekeze akili yako kwenye masomo tu. Hivi karibuni utaanza kusoma, si vinginevyo!” Mzee Mbaraka alisema kwa sauti ya mamlaka.

Hakuna aliyepinga wala kuchangia kauli yake. Wakaendelea kula. Kilichofuata baada ya hapo kilikuwa ni kuingia ndani kulala. Kama kawaida Farida alilala sebuleni, wazazi wake wakalala chumbani.

***
Kama alivyoahidiwa ndivyo ilivyokuwa, mwezi mmoja baadaye mipango yote ya Farida kuanza chuo ilifanyika na kukamilika hivyo akajiunga na Chuo cha Ustawi wa Jamii kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam ambapo alisomea Stashahada ya Mambo ya Jamii.

Akili yake yote aliielekeza kwenye elimu, baada ya kuanza masomo alianza kuishi katika hosteli za chuo, hivyo akawa huru kupanga mambo yake mwenyewe. Alijitahidi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kwenda kumuona Genesis katika Gereza la Segerea.

“Pole sana Genesis utatoka tu, mimi nipo kwa ajili yako na napenda nikuahidi kwamba sitautoa mwili wangu kwa mwanaume yeyote zaidi yako. Nakupenda sana na hiki ni kipimo cha mapenzi yangu kwako,” Farida alimwambia Genesis siku moja alipokwenda kumtembelea gerezani.

“Asante kwa kunipenda, nitaendelea kukupenda daima. Nitafurahi kama ndoto yangu ya kuishi na wewe itatimia. Moyo wangu haujawahi kumpenda mwanamke mwingine yeyote kama ninavyokupenda!”

“Ndiyo furaha yangu, kwa bahati nzuri kuna mfadhili ananisomesha. Nipo Ustawi wa Jamii, baada ya miaka miwili nitamaliza Stashahada yangu, naweza nikafanya kitu fulani ukatoka!”
“Nitafurahi sana.”

Waliongea mengi, kubwa ilikuwa ni Farida kumpa moyo Genesis. Mwisho Farida alimwachia zawadi mbalimbali yakiwemo matunda, sabuni na dawa ya meno. Ilikuwa faraja kubwa sana kwa Genesis.

***
Haikuwa rahisi kwa Dk. Rwegoshora na Prof. Mshana kuwatoa wake zao pamoja na Genesis kama walivyotegemea. Kila mahali walipojaribu kutafuta msaada walikutana na giza nene. Ilikuwa lazima wote wamalize vifungo vyao.

Walitumia mbinu nyingi lakini haikuwezekana, walijaribu kupandikiza magonjwa ya muda mrefu lakini serikali ilikuwa makini na kugundua kwamba hakuna aliyekuwa mgonjwa. Wote waliendelea kutumikia vifungo vyao sawa sawa na hukumu iliyotolewa na Hakimu Mutabuzi.

Baadaye wakagundua ugumu ulipotokea, rais alikuwa macho, akiwataka kuhakikisha sheria haipindishwi. Hawakuwa na namna zaidi ya kusubiri wakamilishe vifugo vyao sawa na hukumu walizopewa.
***
MIAKA MIWILI BAADAYE
Farida alimaliza masomo yake katika Chuo cha Ustawi wa Jamii na kutunukiwa Stashahada ya Mambo ya Jamii. Katika mahafali yake walihudhuria watu watatu tu; wazazi wake na mwanaume mmoja ambaye baadaye alitambulishwa kwa Farida kwa la Mohammed Bakari.

“Mwanangu huyu ndiye Mohammed, aliyekuwa akikulipia kila kitu kwa muda wote wa masomo. Lazima ujue kitu kimoja, alifanya yote hayo kwa sababu maalum, anakupenda na alikuwa anakuandaa ili uwe mke bora kwake!” alisema Mzee Mbaraka kisha akatulia kwa muda.

“Tena mwanangu, Mohammed ni kijana wa Kiislam, ana tabia njema na amekulia katika maadili yote ya kidini. Ni muda mrefu alikupenda lakini kwa kuzingatia heshima alikuja kwetu na kueleza dhamira yake, tukamkubalia. Naomba usituangushe,” alisema mama yake Farida.

“Hapana mama, hapana wazazi wangu. Siwezi kuolewa na mwanaume yeyote tofauti na Genesis, huo ndiyo msimamo wangu ambao hauwezi kubadilika.”

“Usilete upumbavu wako hapa, ni nani atakayemlipa gharama zake zote? Miaka yote miwili ni yeye amekushughulikia, ni nani atakayemrudishia ada aliyokulipia? Sitaki ujinga lazima uolewe na Mohammed uwe unataka au hutaki!” alisema Mzee Mbaraka kwa sauti ya ukali.

“Kuna faida gani kuolewa na mtu ambaye simpendi? Atapata faida gani kwangu? Mohammed, nashukuru kwa msaada wako wote lakini kwa unavyoonekana wewe ni mwanaume mwenye akili na unayefahamu maana ya hisia.

“Hivi utajisikiaje kumuoa mwanamke ambaye hisia zake zipo kwa mwanaume mwingine? Hujisikii vibaya kweli? Naweza nikakubali kwa sababu nimelazimishwa. Lakini hiyo ndoa itakuwa ya aina gani isiyo na maridhiano?” aliongea Farida kwa sauti ya uchungu sana.

Wote walikaa kimya, kila mmoja alionekana kuingiwa na maneno yake. Baada ya muda macho ya Farida yalionekana kujaa machozi, alikuwa analia. Punde akaanza kuzungumza:
“Mohammed ahsante kwa kunisomesha, naamini Mungu atanisimamia nitapata kazi, naomba unipe muda nitakurudishia gharama zako zote lakini tu usinioe.”

“Nimemsikiliza kwa makini sana huyu binti, ni kweli nampenda lakini naomba nisikilize hisia zake. Siwezi kumlazimisha anipende, nimemruhusu aendelee na maisha yake lakini siku yoyote akiwa tayari kurudi kwangu milango iko wazi. Sidai chochote, nimesamehe kila kitu!”

Wote walipigwa na butwaa, haikuwa rahisi kuamini kama Mohammed angeridhika kwa urahisi kiasi kile. Msimamo wa Farida ukabaki kuwa ule ule, kwamba lazima aolewe na Genesis mwanaume wa maisha yake.

Miezi kadhaa mbele, Farida akapata kazi katika shirika moja lisilo la kiserikali (NGO). Ratiba yake iliendelea kuwa ile ile, kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi alimtembelea mpenzi wake Genesis ahadi yao ikiendelea kuwa ile ile.

“Mpenzi wangu naendelea kukuahidi sitakusaliti mpaka utakapotoka hapa. Nitajitunza kwa ajili yako, nitafurahi ukinioa!” Farida alimwambia Genesis siku moja alipomtembelea gerezani, miezi michache kabla ya kumaliza kifungo chake.

“Nashukuru kwa uaminifu wako mpenzi nitakupenda milele!” alisema Genesis akidondosha machozi ya furaha.
Farida naye alilia. Alisubiri kwa hamu siku ya mpenzi wake kutoka, ndoa ndiyo ilikuwa kitu cha muhimu zaidi kwao.

Mwisho
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom