Kifo siku ya harusi yangu

Kifo siku ya harusi yangu

Mkuu huna pdf yake aisee.... Napendaga sana hiz kitu
 
SEHEMU YA 12


Sharti la Farida kufaulu na kuendelea na elimu ya chuo kikuu, lililowekwa na wazazi wa Genesis ili aruhusiwe kumuoa msichana huyo, linapokelewa kwa shangwe, kila mmoja akiwa na uhakika kwamba linatekelezeka. Farida hakuwa na mashaka kabisa na uwezo wake kimasomo.

Suala la kufaulu lilikuwa la lazima na alimhakikishia kabisa Genesis kuwa hatamuangusha! Wakiwa wanawaza hayo, vichwani mwao ni kama wapofu, maana hawajui mpango hatari uliopo dhidi yao. Kilichopangwa klikuwa ni kuhakikisha Bianca anafanya kila aina ya hila, kuhakikisha Farida anayumbishwa kisaikolojia ili mwisho wa siku ashindwe kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya mwisho, huo ungekuwa mwisho wa mapenzi yao.

Likizo ilipokwisha na kurudi shuleni, uhusiano wao ukaanza kuyumba. Asubuhi ya kwanza tu, wanagombana huku Farida akieleza sababu kwamba Genesis alikuwa akitoka kimapenzi na Bianca, jambo ambalo halikuwa na ukweli kabisa.

Wakiwa wanazungumza kwa nia ya kusuluhisha, akatokea Bianca ambaye alimsalimia Farida, jambo ambalo Farida aliliona kama kejeli hivyo kuamua kuondoka zake. Si Farida wala Genesis wanaojua kilichopo nyuma ya hayo yote. Ukweli ni kwamba mharibifu wa uhusiano wao ni Bianca!

Wakiwa darasani, Farida alishindwa kuvumilia kumwangalia Genesis, kila alipokutanisha naye macho alimwaga machozi. Hali ilizidi kuwa mbaya hadi mwalimu wao wa somo la Kemia aliyekuwa darasani, Sister Adventina, akagundua na kumwuliza tatizo lililokuwa likimsumbua.
Kwa kuficha ukweli, Farida akasingizia kwamba anasumbuliwa na mafua makali pamoja na kichwa, ndiyo maana alikuwa akitokwa na machozi.

Hakuweza kumaliza siku nzima darasani, akaamua kwenda kupumzika bwenini. Baadaye Genesis anaamua kwenda kumfuata bwenini kwao, akasimama jirani na bweni lake kisha akamuomba msichana mmoja akamuitie. Akiwa anamsubiria, akatokea Bianca na kuanza kuzungumza naye, Farida alipotokea akakasirika na kuondoka. Genesis akamwita kwa sauti ya juu, lakini Farida hakuitika.

Akiwa bado amesimama eneo lile, mawazo mengi yakimsumbua kichwa chake, yule msichana aliyemuomba akamwitie Farida akatokea akiwa na barua mkononi. Ilikuwa barua kutoka kwa Farida, ni barua hiyo ndiyo iliyomchanganya kichwa chake.

Farida alikuwa tayari kuachana naye baada ya kuwa na uhakika kuwa anatoka na Bianca.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...


MACHO yake yaliendelea kutembea juu ya maandishi yale katika ile barua akiwa haamini kabisa anachokisoma! Hakutaka kuamini kama ni kweli Farida aliamua kuachana naye. Kilichomuumiza zaidi, kila alipojaribu kuvuta picha, ni kwamba hakuweza kufahamu kosa lake lilikuwa nini.

Hakujua kama kuna sumu kali inayosambazwa na Bianca akishirikiana na marafiki zake. Alianza kuwa na wasiwasi kidogo baada ya matukio mfululizo ya kukutana na Farida akiwa na Bianca.
“Au Bianca anahusika? Kwa nini inakuwa hivi?” akawaza kichwani mwake akiwa hana majibu kabisa.

Kichwa chake kilishavurugika, lakini hakutaka kabisa kuachana na Farida, alikuwa mwanamke pekee ambaye moyo wake uliridhia kuwa naye katika maisha yake, hapakuwa na mwanamke mwingine yeyote ambaye angekuwa na nafasi kubwa kama aliyokuwa nayo Farida.

Machozi hayakukoma, alikuwa ameishika ile barua mikononi mwake, bila kuelewa kwamba machozi yalikuwa yakiidondokea na kuilowanisha kabisa! Akiwa amesimama mwenye huzuni sana, akahisi mtu akimgusa begani, alipogeuka akakutana na sura ya rafiki yake Chris.

“Vipi Genesis, mbona hivi?”
“Chris niache.”
“Nitakuacha, lakini nataka kujua kitu gani kinakusumbua?” Kwanini unalia?”

“Acha tu Chris rafiki yangu, nina matatizo makubwa sana”.
“Hayo matatizo ndiyo nataka kuyajua ili nikusaidie mawazo.”
“Chukua,” akasema na kumkabidhi ile barua.

Chris akaichukua na kuanza kuisoma taratibu. Alizidi kuyatoa macho yake kwa mshangao kila aliporukia katika mstari wa chini wa barua ile, haikuwa rahisi kabisa kuamini alichokisoma kama kilikuwa sahihi.
“Ni kweli au unatania?”

“Chris yapo mambo ya kutania, lakini si haya na sidhani kama unaweza kufikiria naweza kukutania kuhusu Farida.”
“Hebu nikuulize kitu.”
“Uliza.”
“Ni kweli unatoka na Bianca?”

“Nilishakuambia kila kitu kuhusu Bianca, mimi nampenda Farida pekee Chris, kwa nini nikufiche kama kungekuwa na ukweli?”
“Kwa hiyo unanihakikishia kwamba hutoki na Bianca?”
“Sitoki naye, niamini mimi!”
“Kweli?”
“Niamini.”

“Ok! Kama ndivyo, niachie mimi hii kazi. Nitamtafuta Farida kwa muda wangu nitazungumza naye, pia Bianca nitaongea naye, kujua nini kinachoendelea, maana nahisi kama kuna mchezo mchafu!”
“Mchezo mchafu?”
“Ndiyo!”
“Kivipi?”

“Acha nifuatilie, nimekuahidi kufuatilia sasa ni vizuri ukaniachia hii kazi, nitajua la kufanya.”
“Ok! Poa rafiki yangu.”
“Naomba twende zetu mgahawani.”
“Sijisikii kula chochote.”

“Twende ukapate japo kikombe cha chai, uunguze utumbo kidogo.”
“Sawa Chris, ndiyo maana nakupenda rafiki yangu. Wewe ni zaidi ya rafiki, unanifanya nisijisikie mpweke.”
“Usijali.”

Wakaondoka pamoja hadi mgahawani, wakaagiza chai na vitafunwa, wakaanza kula huku wakizungumza mambo mbalimbali kuhusu masomo. Walishawaweka pembeni Farida na Bianca. Chris alikuwa msaada mkubwa sana kwa Genesis, mara zote amekuwa akimpa moyo na kuwa karibu anapokuwa na mawazo. Hiyo imeufanya urafiki wao uendelee kukomaa siku hadi siku.

Ilikuwa ni Jumamosi ya mwisho wa mwezi, siku ambayo wanafunzi waliruhusiwa kwenda mjini kutembea au kuchukua mahitaji yao na kurejea shuleni. Siku hiyo Chris akapanga kikao cha siri hakutaka Farida afahamu chochote.

Ni zaidi ya mwezi sasa, Farida na Genesis wamekuwa katika mkwaruzano, katika kipindi chote hicho, Farida amekuwa hataki kusikia kabisa habari za Genesis. Chris akazungumza na Farida na kukubaliana wangekwenda mjini kwa ajili ya mazungumzo.

Walichagua kwenda Mt. Uluguru Hotel, iliyopo eneo la Mlapakoro, pembeni kidogo mwa Barabara ya Boma, njia ya kuelekea kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. Farida na Chris Walifika eneo hilo mapema kidogo, Genesis akabana nje ya hoteli hiyo akisubiri kupewa maagizo ya kuingia.
“Nimependa kuzungumza na wewe Farida juu ya rafiki yangu Genesis, nataka kujua sababu ni nini hasa ya kuachana kwenu?”

“Kwani wewe hujui?” Farida akamwambia Chris kwa sauti ya ukali kidogo.
“Nimesikia ni kuhusu Bianca, lengo langu ni kutaka kujua kama kuna sababu nyingine zaidi ya hiyo.”

“Kumbe hiyo ni ndogo?”
“Sijasema ndogo, nimekuuliza kuna sababu nyingine?”
“Hakuna zaidi ya hiyo. Hivi Christopher unaona ni kitu kidogo sana?”

“Ni kikubwa lakini kitakuwa kikubwa zaidi kama utakuwa na uthibitisho.”
“Ninao!”
“Una uthibitisho gani?”

“Nimewaona kwa macho yangu mwenyewe mara mbili, nataka uthibitisho gani zaidi ya huo?”
“Kama Genesis atakuwa tayari kuthibitisha kwamba hana uhusiano na Bianca utakuwa tayari?”
“Kivipi?”

“Kama ataweza kukukutanisha wewe na Bianca na aweke wazi mbele yenu kwamba hawana uhusiano utakuwa tayari kurudiana naye?”
“Hata sasa hivi!”
“Ok!”

Chris akatengeneza tabasamu mwanana usoni mwake, kisha akachukua simu yake na kumtumia Genesis ujumbe, akimtaka aingie ndani. Dakika moja tu baadaye Genesis alikuwa anaingia ndani, macho yake yakakutana na ya Farida.
Farida akatoa macho kwa mshangao, akataka kusimama na kuondoka, Chris akamzuia.

“Acha hasira, keti tafadhali ni mimi nimemuita.”
Farida akakaa, lakini bado hakuwa na amani kabisa katika moyo wake, Genesis alikuwa mwanaume mbaya sana kwake.

“Samahani kwa kila kitu Farida, najua unanipenda lakini unaongozwa zaidi na hisia, nataka kukuhakikishia kwa vitendo kuwa Bianca si mpenzi wangu, nimeshaongea na Chris, nadhani amekuambia?”
“Ndiyo nimemwambia Genesis.”
“Naomba usinichukue, leo jioni tukirudi shule tutafanya hili zoezi.”

“Sawa.”
Wakaendelea kunywa vinywaji kwa furaha, Farida akiwa na matumaini kidogo ya kumrejesha mpenzi wake. Kikubwa kilichokuwa mbele yao ni kukutana na Bianca na kuweka mambo sawa.

***
Mchezo ulikuwa ule ule, Genesis alimuomba Bianca akutane naye jioni, jambo ambalo Bianca hakukataa akihisi kwamba huenda ndoto zake zilikuwa zinakaribia kuwa kweli. Walianza na mazungumzo ya kawaida, Farida na Chris wakiwa wamebana mahali.

Baada ya muda, Farida na Chris wakatokea, Bianca akaonekana kuingiwa na hofu kidogo.
“Mambo Bianca?” Farida akamsalimia.
“Poa, vipi?”
“Salama.”

“Chris vipi?”
“Safi!”
Baada ya salamu za hapa na pale, muda muafaka ulifika, muda wa kuwekana sawa.

“Bianca wewe ni dada yangu, familia zetu ni marafiki kiasi sasa tumekuwa ndugu, ni kweli?” Genesis akamwambia Bianca.
“Ni kweli kabisa Genesis.”
“Bila shaka unafahamu kwamba Farida ni mpenzi wangu?”
“Ndiyo, kwani kuna tatizo?”

“Bado halijawa tatizo, lakini ni kwamba sasa hivi mimi na Farida hatuna maelewano mazuri na sababu kubwa ni wewe!”
“Mimi?” Bianca akashtuka sana.

“Ndiyo, anahisi mimi nina uhusiano na wewe.”
“Si kweli.”
“Basi mthibitishie hapa mbele yetu kuwa mimi kaka yako na hakuna cha zaidi ya hapo!”

“Farida mwaya kuwa na amani, Genesis ni kaka yangu, hata kama unatuona tupo karibu ni kwa sababu ya undugu wetu, hakuna cha zaidi.”

“Kweli?” Farida akauliza akidondosha machozi.
“Niamini mimi.”

Farida hakuzungumza neno lingine lolote zaidi ya kumkimbilia Genesis na kumkumbatia. Chris na Bianca hawakusubiri kuambiwa waondoke, wenyewe wakaondoka zao. Walipoachiana, wakashangaa wakiwa peke yao.

“Darling hapa ni shule, tumejisahau sana!”
“Yaani acha tu dear, kweli mapenzi upofu.”
Wakaachiana.

***
“Farida usiwe mjinga, utadanganywa mpaka lini? Bianca na Genesis ni wapenzi, niamini mimi!” Ni maneo ya Grace akimwambia Farida, wiki moja tu, baada ya kuwekwa sawa na Genesis.
“Grace kwa nini unafuatilia maisha yangu? Niache kama nilivyo, sitaki tena kusikia mambo ya Bianca!”

“Unasema hivyo kwa sababu umekuwa kama kipofu, huoni tena, lakini nisubiri hapa hapa nikuletee uthibitisho. Wewe si unabisha, nisubiri hapa nakuja sasa hivi!” Grace akasema akikimbilia bwenini.

Farida akabaki ameduwaa, akiwa haelewi ni uthibitisho gani angeletewa na Grace. Moyo wake ukaanza kusinyaa tena kwa hofu, dalili za machozi aliyoyasahau, zilianza kunukia. Kwa vyovyote vile, angelia sana kama atagundua kwamba Bianca ana uhusiano na Genesis.
Lazima atalia!
FARIDA alisimama wima kama askari wanaokaguliwa gwaride kabla ya Amiri Jeshi Mkuu hajapita kuwakagua! Alihisi miguu kumuisha nguvu, lakini hilo halikumfanya ayumbe alipokuwa amesimama, macho yake yakiwa yanamwangalia Grace aliyekuwa akiishilia bwenini.

Kwa mbali alianza kuhisi jasho jembamba likianza kumchuruzika mwilini, moyo wake ulimwambia lazima kulikuwa na kitu kibaya kinachokuja mbele yake. Aliogopa sana.

‘Ana nini? Ana ushahidi gani ambao unaweza kuthibitisha kwamba Bianca anatoka na Genesis wangu?’ akawaza.

Haikuwa rahisi kwake kupata majibu ya maswali yake, hasa wakati ule ambao presha yake ilikuwa juu kabisa. Alichowaza yeye ni kutompoteza mpenzi wake tu! Alishindwa kuelewa ni shetani wa aina gani aliyekuwa akinyemelea penzi lake kwa kasi kiasi kile.

“Au sijapangiwa kuwa na Genesis?!!!” akazidi kuwaza.
Akiwa bado yupo katika mawazo hayo mazito, akamwona Grace akija upande wake akitembea kwa haraka sana, mkononi mwake akiwa na bahasha ya khaki! Grace alionekana kuwa na nia njema ya kumsadia Farida kuachana na Genesis ambaye kwake alikuwa mwanaume asiye mwaminifu, lakini hakujua upande wa pili wa Grace, upande ambao ulikuwa umejificha na ulikuwa mbaya wenye harufu mbaya ya kifo.

“Farida wewe ni rafiki yangu, nakupenda na ndiyo maana nafanya yote haya kwa ajili ya kuhakikisha unakuwa salama,” alianza kwa maneno hayo Grace.
“Sijakuelewa.”

“Nasema wewe kama msichana mwenzangu, sitapenda kuona unaingia sehemu yenye matatizo na mimi nikabaki kimya, lazima niseme ukweli ili wewe mwenyewe utajua cha kufanya kulingana na ukweli huo.”
“Grace acha porojo, nipe huo ushahidi!” Farida akasema kwa hasira ya wazi kabisa.

“Mbona unanikasirikia Farida? Au nimefanya vibaya kukuambia?”
“Nimesema kama una ushahidi lete, nimechoka sasa na haya maneno yenu ya uchonganishi!”
“Mimi nakuchonganisha?”
“Ndiyo!”
“Kweli?”

“Ndiyo!”
“Farida unasema kweli kwamba mimi nakuchonganisha?”
“Ndiyo, kwani kuna uongo hapo? Umesahau kwamba ni wewe ndiye uliyeniambia kwamba Bianca anatoka na Genesis na wameonekana wakiwa wanazungumza kimahaba?”

“Ndiyo nilisema, kwani niliongopa?”
“Wewe unaona ulisema kweli?”
“Ndiyo ni kweli!”
“Ukweli kwamba Genesis anatoka na Bianca siyo?”
“Ndiyo!”

“Sasa mbona Bianca kwa mdomo wake mwenyewe amekataa kwamba hana uhusiano na Genesis zaidi ya urafiki?”
“Haya bwana, lakini nina nia ya kukusaidia tena kirafiki kabisa, sasa labda nikuulize jambo moja dogo sana!”
“Uliza.”

“Wewe unaamini kwamba Bianca anatoka na Genesis au huamini?”
“Siamini kabisa.”
“Una moyo?”
“Ninao!” Farida akajibu kwa kujiamini.
“Subiri.”

Grace akafungua ile bahasha na kutoa picha moja kisha akamkabidhi Farida. Kwa dakika moja nzima, Farida alikuwa akiingalia ile picha akiwa haamini kabisa kama anaowaona ni wale anaowafahamu.

Ilikuwa picha inayowaonesha Bianca akiwa na Genesis, wamevutana na Bianca alikuwa akijiandaa kutoa ulimi wake nje; kwa haraka akajua kitendo kilichokuwa kinataka kutokea, ni wazi kwamba Bianca alikuwa akitaka kula denda na Genesis, kiashirio ambacho kililenga moja kwa moja mambo ya mapenzi!

“Siamini,” alijikuta akisema neno hilo Farida kisha mvua ya machozi ikaanza kumwagika.
“Unatakiwa kuamini, Genesis si mwanaume wa kuaminika, hana msimamo, ndiyo maana anawachanganya kama viungo kwenye mchuzi!”
“Mungu wangu, kwa nini inakuwa hivi kwangu, kwa nini?” Farida akasema kwa uchungu akiangalia juu.

Alipoyarudisha macho yake na kuangalia tena ile picha, alijikuta machozi yakizidi kumwagika kwa kasi zaidi machoni mwake, mara miguu yake ikaanza kumuisha nguvu, lakini akajikaza na kuondoka eneo lile akikimbia.
“Bado zingine, njoo uone,” Grace akamwambia Farida.

“Sitaki,” Farida akajibu akiendelea kukimbia.
Safari yake iliishia nyuma ya bweni lake, alipokaa bustanini akilia peke yake. Ni Immaculate ndiye aliyemfuata na kumtuliza.
“Unalia nini Farida, kuna tatizo gani?” Immaculate akamwuliza.
“Acha tu rafiki yangu, niache.”

“Hapana, mimi ni rafiki, lazima unieleze ukweli kama kuna kitu kinakusumbua!”
“Hapana ni matatizo binafsi!”
“Lakini nina haki ya kufahamu!”

“Mama yangu anaumwa, nimepigiwa simu sasa hivi, baba naye hali mbaya, ndiyo maana nimechanganyikiwa!”
“Pole, nyamaza kulia, machozi yako hayawezi kuwa tiba, kwa hiyo tatizo ni fedha?”
“Ndiyo, si unajua tena familia yangu haina uwezo?!”

“Pole sana, nitakusaidia laki moja umtumie mama, punguza mawazo.”
“Sasa na wewe si utaishiwa?”
“Usijali, wazazi wangu wananitumia pesa nyingi sana, wakati mwingine huwa nabakiza, sasa kama wewe rafiki yangu una matatizo, kwa nini nisikusaidie?” Immaculate akauliza.

Ukweli ni kwamba mama yake hakuwa anaumwa, wala hakuwa na shida na hizo fedha, lakini kwa kuwa Immaculate aliamua kwa moyo wake kumpa, hakuona sababu ya kukataa.
“Nitashukuru sana rafiki yangu!”
“Twende ndani nikakupatie!”
“Sawa, ahsante sana, Mungu akubariki!”

Wakaongozana hadi ndani, ambapo Immaculate alitoa fedha hizo na kumpatia Farida. Hapo akajikaza kwa nje, akionesha kwamba tatizo lake liliisha, lakini ndani ya moyo wake kulikuwa kunawaka moto ambao ulimsababishia maumivu makali sana.

****
Kila Genesis alipokutanisha macho na Farida, aliweza kuona alama mpya machoni mwake, aliweza kuona matatizo. Alishindwa kuelewa chanzo cha matatizo hayo ni nini?! Ni wiki moja tu walikuwa wameshawekana sawa na kusameheana, lakini kitendo cha kumwangalia na kukunja uso wake tofauti na tabasamu alilolizoea kila siku, kulimpa picha nyingine tofauti kabisa.

Baada ya vipindi vya asubuhi kuisha na wanafunzi kwenda mapumziko mafupi, Farida alionekana kukosa raha kabisa. Tofauti na siku nyingine alizokuwa akipenda kwenda kunywa soda na keki mgahawani, siku hiyo alijitenga na kusimama pembeni kabisa.

Genesis alikuwa anamfuatilia tangu alipokuwa akitoka darasani. Haraka akamkimbilia na kumshika begeni.
“Farida haupo sawa mpenzi wangu, halafu ni hatari maana muda si mrefu tutaanza mitihani ya mwisho.

Una tatizo gani mpenzi wangu?”
“Naomba uniache tafadhali,” Farida akasema kwa hasira.
“Nikuache?”
“Ndiyo!”
“Kivipi?”
“Nenda kwa Bianca wako.”

“Bianca?”
“Kwani nini kipya? Unajua unajifanya mwanaume hodari sana wa kuchanganya watoto wa wenzio. Hebu ngoja, hivi unadhani ni nani asiyejua mapenzi yenu wewe na Bianca wako?”
“Farida acha kuongea ujinga!”

“Naongea ujinga?”
“Ndiyo ni ujinga mtupu!”
“Ngoja...leo tutajua kama naongea ujinga au mambo ya maana,” akasema Farida kisha akaingiza mkono wake katika mfuko wa shati kisha akatoa picha aliyopewa na Grace.

Genesis akaiangalia ile picha na kumwangalia Farida, kisha akaiangalia tena, akaonekana kupigwa na mshangao wa hali ya juu sana!
“Bisha tena sasa!” Farida akasema kwa kujiamini, sauti yake ikitoka kwa kwa shida, akionekana kujiandaa kulia.

“Aaaah! Sikiliza Farida...unajua....unajua...aaaaaah! yaaaaaani,” Genesis akaonekana kushikwa na kigugumizi.
“Huna la kuongea, aibu zinakushika, sasa baki na Bianca wako, ahsante sana kwa kunipotezea muda wangu, nakuomba sana unisahau kabisa katika maisha yako!” Farida akasema kwa hasira na kuondoka akikimbia.

Genesis akabaki amepigwa na butwaa! Hakuwa na la kufanya, zaidi ya kubaki na maswali ambayo majibu yake yalikuwa na kazi kubwa sana kupatikana.
Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 13

Farida hakuwa na mengi ya kuongea zaidi ya kumwambia kwamba mapenzi yao yaishie pale na kumwonesha picha aliyopiga na Bianca. Genesis akatoa macho akiwa hana la kufanya, muda huohuo Farida akakimbia na kumuacha Genesis akiwa njia panda.

Hakujua kama mchezo mzima ulifanywa na Bianca, hiyo ilikuwa siri iliyokuwa sirini. Akabaki ameduwaa, hana la kufanya.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

BADO Genesis alimhitaji sana Farida, hakuwa tayari kuachana naye, kwake alikuwa mwanamke wa maisha yake, ambaye ndoto zake ni kuishi naye katika ndoa. Pamoja na ndoto hiyo nzuri, alishangazwa sana na ile picha na hakujua ni nani aliipiga na aliipata vipi!

Ni kweli ile picha ilimwonesha yeye na Bianca, wakiwa wamesogeleana kimahaba, hilo halikuwa na ubishi kabisa, pia alikumbuka vizuri sana siku waliyoingia shuleni, alikuwa akizungumza na Bianca na wote walishtuliwa na mwanga wa kamera!
Kwa vyovyote vile, ile ilikuwa picha yake. Fikra zake zikaenda mbali zaidi, tayari alianza kumfikiria baba yake, akamfikiria na mama yake. Hakujua hali ingekuwaje nyumbani kama zile picha zingeonekana na wazazi wake.

Kitendo cha zile picha kufika mikononi mwa Farida, kilitosha kabisa kumthibitishia kwamba zingeweza kufika hata kwa wazazi wake. Ingekuwa picha chafu sana kwa wazazi wake, lakini kubwa zaidi ambalo alilifikiria ni juu ya masomo yake!
Kulikuwa na kila dalili za kupoteza masomo yake, kama picha zile zingeonekana na Mkuu wa Shule. Alihisi kichwa kumuuma, mawazo tele kichwani mwake yakamjaa akiwa hana amani kabisa.

“Mungu wangu, kila kitu kitaharibika. Kila kitu...shule, wazazi na hata mpenzi wangu Farida. Naweza kupoteza vyote hivyo kwa sababu ya picha, kwa sababu ya Bianca. Halafu Bianca nilimweleza kabisa kwamba tunafanya jambo la hatari, lakini hakusikia, akanipuuza. Sasa mambo yameharibika, sijui nitauficha wapi uso wangu mimi!” Akazidi kuwaza Genesis.

Kitu pekee ambacho alitakiwa kufanya kwa haraka ilikuwa ni kukutana na Chris, yeye ndiye angeweza kumpa msaada wa mawazo kwa tatizo lile ambalo lilionekana dhahiri kuharibu mipango yake. Akiwa katika mawazo hayo, akashtuliwa na kengele ya kuingia darasani.

Haraka akakimbilia darasani, uso wake ulionekana hauna amani kabisa, alizidi kujisikia vibaya kila alipokutanisha macho yake na Farida ambaye naye alikuwa amekasirika sana. Mwalimu akaingia darasani kufundisha, lakini Genesis hakuelewa kabisa.
Mawazo yake hayakuwa darasani, ni Farida ndiye aliyetawala kichwa chake. Chris aliweza kuona tofauti inayoonekana machoni mwa Genesis. Kwa sababu madawati yao yalikuwa jirani, Chris akachana karatasi ndogo na kuandika kisha akampa mtu aliyekuwa amekaa jirani na Genesis ampatie.

“Kaka una nini, mbona kama haupo sawa?” Macho ya Genesis yalitembea juu ya maneno hayo yaliyoandikwa kwenye karatasi kutoka kwa Chris.

Genesis akachana kikaratasi kingine na kuandika: “Ni kweli nina matatizo kaka, lakini tutaongea baadaye.”
Kama kawaida akampatia aliyempa na kumwomba amfikishie Chris, wakapasiana hadi kikaratasi hicho kikamfikia Chris. Naye mara moja akajibu na kumtumia.
“Hapana, niambie kuna nini?”

Genesis akakisoma tena na kumuandikia, muda mfupi baadaye wakawa wanawasiliana kwa njia hiyo, Genesis anaandika na kumtumia Chris, naye anamjibu.
“Farida!”
“Amefanyaje tena?”

“Hataki tena kuendelea na mimi!”
“Kwani umemfanya nini tena?”
“Ni kuhusu Bianca, anasema eti natoka naye!”

“Hilo si tulishalimaliza?”
“Kaka acha tu, ndiyo maana nimekuambia tutaongea kipindi kikiisha nina mengi ya kukueleza, lakini kifupi ni kwamba amenionesha picha nikiwa na Bianca kimahaba!”
“Kimahaba?”

“Ndiyo!”
“Kwa hiyo kweli unatoka naye?”
“Hata wewe unajua siyo kweli.”

“Sasa hizo picha za kimahaba zimetokea wapi?”
“Kaka subiri kipindi kiishe nitazungumza na wewe vizuri!”
“Poa!”

Baada ya vipindi vya asubuhi kuisha, kengele ya chakula cha mchana ikapigwa, wanafunzi wote wakatoka nje na kujiandaa kwa ajili ya kwenda chumba cha chakula. Muda huo ukawa muafaka kwa Genesis na Chris kuzungumza kuhusu Farida.
“Unajua sikukuelewa vizuri, hebu sasa nifafanulie, ilikuwaje?” Chris akamwuliza Genesis.
“Ni kweli ile picha ni yangu, lakini sikupiga kwa hiyari yangu!”

“Kivipi, mbona unanichanganya?”
“Nilikuwa katika mazungumzo na Bianca, lakini ghafla tukaona mwanga wa kamera, wote tulishangaa, tukajua labda ni mtego wa shule, sasa leo nashangaa Farida anayo picha!”

“Hiyo picha inaweza isiwe tatizo, tatizo ni hayo mahaba unayozungumzia. Sasa ilikuwaje ukawa unazungumza na Bianca katika pozi la kimahaba?”
“Si kimahaba hasa Chris rafiki yangu!”

“Bali?”
“Tukiwa tunakaribia kumaliza mazungumzo yetu, Bianca aliniambia kuwa kuna kitu anataka kuniambia, kwa hiyo nimsogezee sikio kwa sababu alitaka kuzungumza kwa sauti ya chini.

“Nikafanya hivyo, lakini kinyume na matarajio yangu, Bianca alinibusu, muda huohuo nikaona mwanga wa kamera. Ni muda mrefu sasa umepita, nashangaa leo ananionesha picha, sijui amezipata wapi na wala sijui itakuwaje kama zikifika kwa Mkuu wa Shule,”

Genesis akaongea kwa sauti ya chini inayotia huruma sana.
“Lakini na wewe kwa nini ulikubali kufanya hivyo? Huoni sasa kila kitu kinaharibika? Shule, nyumbani na hata kwa mpenzi wako Farida. Unadhani nitazungumza nini mimi Farida anielewe? “

“Si wakati wa kulaumiana Chris rafiki yangu, kumbuka kwamba nakutegemea sana wewe katika mambo yangu, unatakiwa kunishauri kaka, kama ni kosa tayari limeshatokea, cha msingi ni namna ya kukabiliana nalo.”
“Twende tukale kwanza!”

“Hata hamu ya kula sina, kwa mambo haya ndugu yangu? Niambie kwanza, nini kitafanyika ili kuzima haya mambo?”
“Tukale basi kwanza!”
“Chakula hakitakuwa na ladha, kama sijajua mustakabali wa haya mambo, naomba msaada wako ndugu yangu!”

“Nitafanya uchunguzi, nipe muda, kwanza nitaanza kuongea na Farida nijue alipopata picha, halafu nitakuambia kinachoendelea.”
“Sawa, lakini unadhani zitakuwa hazijafika kwa Mkuu wa Shule kweli?” Genesis akauliza akionekana kuingiwa na woga sana.
“Hilo mimi na wewe hatujui, sidhani kama tunatakiwa kulizungumzia sana!”

“Poa.”
Wakaenda kula.
****

Farida alikuwa amekaa sehemu ya peke yake akiangalia wenzake wakicheza mpira wa pete jioni hiyo shuleni kwao. Wote walikuwa wakifurahia mchezo ule, lakini yeye alikuwa tofauti, macho yake yalikuwa uwanjani, lakini mawazo yake yalikuwa kwa Genesis.
Ni mwanaume ambaye alimteka sana akili yake, lakini aliumizwa sana na jinsi anavyounyanyasa moyo wake kila wakati. Hakustahili kudhalilishwa kiasi kile, kuteswa kiasi kile na kufanyiwa mabaya kama yale. Akilini mwake aliamini Genesis alikuwa anafanya makusudi kwa sababu ya umasikini wake.

Akiwa yupo kwenye mawazo tele, akimuwaza Genesis, akahisi mtu akimgusa bega, akainua uso wake haraka kumuangalia. Alikuwa ni Chris.
“Vipi Farida?” Chris akamsalimia.

“Unasemaje?” Farida akamjibu kwa ukali sana.
“Punguza hasira Farida, najua kila kitu, najua...natambua pia jinsi ambavyo unaumia. Lakini unatakiwa kufahamu kwamba, siku zote, matatizo huwa hayakimbiwi, yanatakiwa kutafutiwa suluhisho, si kuyakimbia.”
“Unamaanisha nini?”

“Najua unayo picha inayomwonesha Bianca amepiga na Genesis katika pozi la kimapenzi, si kweli?”
“Kweli!”
“Unadhani Bianca na Genesis ni wapenzi?”

“Swali gani hilo? Hata mtoto mdogo anaweza kukujibu kama akiona hiyo picha.”
“Unafikiri ni rahisi Genesis apige picha na Bianca, wewe ukiwa unamtuhumu kuwa na uhusiano naye, huku yeye akiendelea kukataa kila siku, tena hata Bianca mwenyewe alikataa mbele yako, unadhani inawezekana?”
“Imeshawezekana!”

“Hapana Farida, usiseme hivyo, mimi nataka kuwasaidia wote kwa wakati mmoja, kikubwa ni ushirikiano wenu tu, katika hili. Naamini unatambua kwamba mimi sipati chochote kama nyie mkitimiza ndoto yenu, kikubwa ni kwamba napenda kuwaona mkiwa pamoja, hiyo ndiyo furaha yangu.

“Hebu naomba uniambie, ni nani aliyekupa hiyo picha ya Bianca na Genesis? Tafadhali usinidanganye, nataka kujua ukweli ili nijue nitaanzia wapi uchunguzi wangu. Nahisi kuna mchezo mchafu unaendelea hapa.”
“Ni Grace!”
“Nani?”

“Grace!”
“Aaaaahaaaa Grace....” Chris akasema akitingisha kichwa akionekana kuwa na jambo fulani alilokumbuka ghafla baada ya kusikia jina hilo.
“Kwani vipi?”

“Usijali, nimeshajua kinachoendelea!” Chris akasema akijiandaa kuondoka, lakini kabla hajafanya hivyo, Grace akatokea.
“Nadhani sasa umeamini kwamba Genesis si mwanaume bali ni tapeli tu wa mapenzi. Ni bora hata ungekuwa na Chris, hebu ona mlivyopendezea. Kijana mtanashati, mpole, anayejali, mwenye akili na sifa nyingine kibao. Nahisi kama mngekuwa pamoja mngevutia sana,” akasema Grace akiwa amesimama wima, mikono yake ikiwa kiunoni.
Chris alikuwa kimya, Farida akabaki anamkodolea macho kwa mshangao.

NAWA KATA KIU KAMA KAWAIDA EH

KWA namna alivyokuwa akizungumza Grace, alionekana dhahiri kama anafanya kampeni ya wazi kabisa kuhakikisha Farida na Genesis hawawi wapenzi, hilo liliweza kujidhihirisha hata baada ya kuanza kutoa mapendekezo yake kwamba ni bora Chris
ndiye angekuwa naye kuliko yeye!

Chris aliweza kusoma kitu fulani kupitia kwa Grace, lakini kwa Farida bado kulikuwa na giza nene, maana alikuwa na mawazo tele akimuwaza Genesis na namna walivyokuwa wamepiga ile picha. Isingewezekana Genesis akawa amelazimishwa kupiga picha ya pozi la kimapenzi kama ile, lazima kulikuwa na kitu kinachoendelea kati yao.

“Grace!” hatimaye Chris akaita.
“Sema handsome boy!” Grace akaitika akicheka.
“Weka utani pembeni, tuzungumzie kuhusu jambo hili muhimu!”
“Sawa nakusikiliza!”

“Kwa nini unasema mimi namfaa Farida na si Genesis?”
“Naomba mnapendezea zaidi?”
“Kivipi?”
“Jamani mnafaa kuwa mtu na mpenzi wake!”
“Na Genesis?!”
“Hafai yule!”

“Kwa nini?”
“Wewe uko wapi Chris? Genesis anatoka na Bianca na kila mtu anajua!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”

“Lakini unatambua kwamba pia ana uhusiano na Farida?”
“Najua!”
“Kwa nini unadhani ni bora Farida ajitoe na si Bianca?”
“Basi tu!”
“Unaonekana unafamu mambo mengi sana kuhusu Bianca na Genesis, hebu tueleze vizuri!”

“Sijui zaidi ya hivyo!”
“Wewe umejuaje?”
“Picha zimezagaa shule nzima!”
“Wewe umezipata wapi?”
“Unajua maana ya kuzagaa? Picha zimezagaa!”

“Kama zimezagaa, mbona hazijafika mikononi mwangu?”
“Swali hilo naona ni gumu kidogo kwangu,” akasema Grace akionekana kuwa na aibu kidogo.
“Sasa nimeshapata jibu, wewe ni mmoja wa watu wanaochangia ugomvi kila siku katika uhusiano wa Farida na Genesis wake, hilo nimeshaligundua!”

“Hayo ni mawazo yako potofu!”
“Mawazo potofu vipi, wakati kila kitu kipo wazi?”
“Sasa na hizo picha walizopiga unataka kusema mimi ndiyo niliwalazimisha wapige?”

“We’ Chris vipi? Nakuona muelewa sana kumbe wapi, hakuna kitu!” akasema Grace akiondoka.
Chris aliweza kugundua kitu kupitia macho yake, kwamba alikuwa anaona aibu,
lakini kwa Farida bado iliendelea kuwa kweli, kulikuwa na kazi ngumu sana ya kumwelewesha Farida aamini kwamba ule ulikuwa mchezo.

Ilikuwa vigumu sana!
“Farida nisikilize kwa makini sana...” akasema Chris akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Farida.
“Una kitu gani kipya cha kuniambia?”
“Tuliza jazba kwanza, nipe nafasi nizungumze na wewe!”
“Ok! Sema.”

“Bado kuna haja ya kufuatilia zaidi kuhusu Bianca na Genesis, lakini kwa inavyoonekana ni dhahiri kwamba kuna mchezo unachezwa, hilo unatakiwa
kulielewa!”

“Naona wewe unanipotezea muda wangu bure,” akasema Farida na kuondoka zake.
Chris akabaki anamsindikiza kwa macho, bado alikuwa na msururu wa maswali mengi kichwani mwake, akishindwa kuelewa ni kweli Genesis alikuwa anatoka na Bianca au lah!

****
Aliachia tabasamu pana alipoona jina lile kwenye kioo cha simu yake iliyokuwa
ikiita. Akabonyeza kitufe cha kijani, kuruhusu simu kuingia na kuanza kuzungumza na mtu wa upande wa pili!
“Shikamoo mama,” akasema mara baada ya kupokea simu.

“Mar-haba mwanangu, habari za masomo?”
“Nzuri mama!”
“Nzuri au nzuri sana?”
“Mama jamani, nadhani unanijua mwanao!”
“Enheee!”

“Nzuri!”
“Tutarajie ngapi?”
“Kama nilivyoahidi itakuwa hivyo hivyo, hapa ni Division One tu mama!”
“Na Farida?”
“Ajiandae na sifuri ya masikio!”

Wakacheka wote. Alikuwa ni Bianca akizungumza na mama yake Genesis. Mpango wao mkubwa ulikuwa ni kuhakikisha Farida anafeli mitihani yake ya mwisho, ambapo kama angekosa alama za kuendelea na elimu ya chuo kikuu, basi ungekuwa mwisho wake na Genesis!

Hata siku moja, Genesis hakuwahi kufikiria kwamba, Bianca alikuwa na mawasiliano ya karibu kiasi kile na mama yake, lakini ukweli uliendelea kuwa huo, walikuwa wakiwasiliana kila mara na wakati mwingine ni yeye ndiye aliyekuwa akimpa mbinu mpya za kutumia ili kumfanya Farida achanganye masomo yake.

“Lakini unatumia mbinu zinazokupa mwanangu?” mama Genesis akauliza.
“Mie tena mama, nadhani unanijua!”
“Safi sana, naamini lazima utafanikisha, sitaki hicho kinyago kwenye familia
yangu, wewe ndiye unayestahili kuwa katika familia yangu na si vinginevyo.”

“Sawa mama, nakuahidi nitafanya kila niwezalo, akili zangu unazijua, kwa hiyo usiwe na wasiwasi!”
“Sawa mwanangu, nakutakia kila la heri mama, sawa?”
“Ahsante mama, tena hivi ninavyokuambia huku hakukaliki, tayari nimeshalikoroga, hakuna amani kabisa! Farida hataki kusikia mtu anayeitwa Genesis!”

“Safi sana, umetumia njia gani?”
“Ile ya picha!”
“Oooh! Safi sana, ndiyo maana nakupenda. Wewe ndiye mkwe unayetakiwa. Nimefurahi sana kusikia hivyo!”
“Ahsante sana mama, nakupenda sana mama!”
“Hata mimi pia!”

Wakakata simu zao. Bianca akatabasamu tena akijiona mshindi, alikuwa amefikia hatua ya mbali sana, Farida alikuwa na asilimia nyingi sana za kufanya vibaya katika mitihani yake. Tayari akili zake ameshazihamishia kwenye matatizo ya uhusiano wake na Genesis na siyo masomo tena.

Hayo yalikuwa mafanikio makubwa sana kwa Bianca. Nia yake iliendelea kuwa ile ile, kumweka Genesis mikononi mwake.
“Atakuja tu, mimi ndiye Bianca,” alisema Bianca akijipiga-piga kifuani huku akitabasamu.

***
Uwezo wa Farida darasani ukaanza kupungua taratibu, alikuwa akitumia muda mwingi zaidi, kumwaza Genesis badala ya masomo yake, mitihani ya majaribio ya wiki ikaanza kumshinda, hakuwa na uwezo tena darasani.

Jambo hilo liliwashangaza sana walimu pamoja na wanafunzi. Wakati yeye akianza kuporomoka, Bianca na Genesis walikuwa wanapanda uwezo wao kila kukicha, wao ndiyo walikuwa vinara wa kidato cha sita shule nzima!

Genesis aligundua kilichokuwa kikimsumbua Farida, alijua kabisa yeye ndiye chanzo cha Farida kufeli, lakini pia alikumbuka jambo moja la muhimu sana.

Pamoja na kwamba walikuwa kwenye ugomvi, alifahamu kwamba lolote linaweza kutokea mbeleni ikiwemo kurudiana, lakini wasingeweza kuishi pamoja kama angefeli mitihani yake ya mwisho, hilo likamfanya afungue mdomo wake kuzungumza naye tena.

“Farida najua huniamini, lakini nataka kuzungumza na wewe kidogo, naomba unipe nafasi tafadhali,” Genesis alimwambia Farida, siku moja mchana wakati wa mapumziko ya kupata chakula cha mchana.
“Unataka kuniambia nini Genesis?” Farida akasema kwa hasira.
“Ni kuhusu masomo, naona unashuka sana!”
“Kwani hujui sababu?”

“Naijua, ndiyo maana nataka tuwekane sawa!”
“Haya niweke sawa sasa!”
“Acha hasira Farida, nataka unisikilize, hivi ni kwa nini huamini kama mimi sina
uhusiano na Bianca?”

“Unataka nini kitokee ili niamini zaidi ya picha niliyoiona?”
“Hapana mpenzi nahisi kama kuna mchezo ulikuwa umepangwa!”
“Mchezo wa kukulazimisha kupiga picha yenye pozi la kimapenzi na mtu ambaye si mpenzi wako siyo?”

“Siyo hivyo!”
“Bali?!” Farida akauliza akionekana kuzidi kukasirika.
Genesis hakuwa na kitu cha kuongea, ni kweli ana uhakika hana uhusiano na Farida, lakini picha zilikuwa zinambana. Pamoja na hilo, alichanganyikiwa zaidi na jinsi Farida alivyokuwa akishuka kimasomo, ile ilikuwa tiketi tosha ya kuachana kwao.

Hata kama wangeamua kusameheana, lakini kitendo cha kufeli mitihani yake ya mwisho kingetosha kabisa kuwaachanisha! Ilibaki miezi miwili tu kabla ya kufanya mitihani hiyo, hilo lilikuwa tishio kwa Genesis! Alikuwa na wasiwasi sana na Farida kufaulu!

Je, nini kitatokea? Farida atabadilisha uamuzi wake? Je, atafanya vizuri kwenye mitihani yake ya mwisho?
 
SEHEMU YA 14


Huo unakuwa mtihani mkubwa sana kwake, lakini anachanganyikiwa zaidi na
kuporomoka kwa Farida kimasomo, kwani kama angeendelea kushuka zaidi, ni wazi asingekuwa na matokeo mazuri ya mtihani wake wa mwisho na huo ungekuwa mwisho wa mapenzi yao kwa namna alivyokubaliana na wazazi wake.
Jambo hilo linamchanganya sana Genesis kichwa chake.
Je, nini kitatokea? Genesis atafanya nini? SONGA NAYO...

GENESIS alitulia kwa muda akimwangalia Farida usoni. Moyo wake ulikuwa umepondeka, Farida alikuwa mwanamke muhimu sana katika maisha yake. Ni kweli alikuwa katika ugomvi naye, lakini bado alikuwa akiwaza juu ya kupatana kwao baadaye.Kupatana kwao kusingekuwa na maana kama angekuwa amefeli mitihani yake ya mwisho, kwani huo ndiyo ulikuwa mtihani mkubwa zaidi ya kupatana kwao.

Akamwangalia Farida kwa macho ya kusihi asikilizwe, lakini Farida hakuwa na dalili hiyo hata kidogo.
“Farida!”
“Unasemaje?”

“Nipe nafasi Farida!”
“Nafasi ya nini?”
“Nijieleze mpenzi wangu, kwanini unataka kuamua mambo bila kunipa nafasi ya
kujieleza?”

“Haya jieleze!” Farida akasema akimtazama kwa macho yanayoonesha dhahiri kwamba alikuwa akimkejeli.
“Sikia Farida...”

“Nakusikiliza vizuri sana, umesema unataka nafasi ya kujieleza nimekupa, unataka nini tena?”

“Punguza basi hasira mpenzi wangu, unajua ni nini? Mimi naona wazi kwamba kuna mchezo unachezwa ili mimi na wewe tugombane, hilo nimeliona wazi kabisa.”
“Mchezo?”

“Ndiyo!”
“Nimeshakuuliza tangu awali, huo mchezo ni pamoja na kukulazimisha wewe kupiga picha za mapenzi na Bianca siyo?”

“Sijasema hivyo!”
“Bali!”
“Nisikilize kwanza mpenzi wangu!”

“Hebu achana na blablaa zako zisizo na mbele wala nyuma. Mimi natambua kwamba ni masikini wa kutupwa na hapa nasoma kwa msaada wa shirika la kidini, sina msaada wowote na sina thamani yoyote kwako. Najua kwamba hata wazazi wako hawanipendi

katika ukoo wenu… alisema Farida huku machozi yakilimlenga lenga.
Kisha akaendelea kusema “Natambua kabisa kwamba naonekana kinyaa kwenu, hata kama hivyo ndivyo lakini wewe hukupaswa kunionyesha uchafu tena waziwazi kiasi hicho. Hiyo ni dharau kubwa sana Genesis ambayo ilipaswa kuoneshwa na mtu mwingine na si wewe. Umefanya vibaya sana Genesis!” Alisema Farida akianza kudondosha machozi machoni mwake.

“Najua ni kiasi gani ni vigumu wewe kunielewa, lakini inakupasa unielewe mpenzi wangu, sikuwa na taarifa yoyote na ile picha.”
“Taarifa?”

“Ndiyo Farida!”
“Umeona wapi mtu akafumaniwa kwa taarifa?”
“Kwani nilifumaniwa mpenzi wangu?”
“Kwahiyo kupigwa picha zenye viashiria vya mapenzi bila taarifa unadhani si
kufumaniwa?”

“Hapana!”
“Lakini hebu tuachane na yote hayo, wewe unataka mimi nijifunze nini kupitia zile picha? Kwamba mlikuwa kwenye pozi la dada na kaka au….?”

“Ndiyo maana nimekuambia unipe nafasi nijieleze.”
“Hiyo nafasi nimekupa lakini unaonekana huitaki kuitumia, sasa sijui unataka
nafasi ya aina gani tena?”

“Sikia Farida, kama nilivyokuambia awali, Bianca alinisogelea ghalfa tu, akidai kwamba anataka kuninong’oneza jambo, muda mfupi baadaye nikashangaa kuona mwanga wa kamera, nikajua huenda ni viongozi wa shule walikuwa wametupiga!”

“Ujinga huo unaweza kumdanganya mtoto mdogo pekee.”
“Siyo ujinga ni ukweli mpenzi wangu.”
“Ni hivyo tu?”
“Ndiyo!”

“Tafuta uongo mwingine, huo nimeushtukia.”
“Hapana Farida wangu, usiseme hivyo!”
“Unataka niseme nini?”

“Lakini nina kitu kingine cha kukuhakikishia kwamba sina uhusiano na Bianca.”
“Nini?”
“Sema kwanza kama upo tayari nikupe.”
“Nipo tayari.”

“Jumapili asubuhi, leo tuendelee na masomo kwanza.”
“Huna lolote,” Farida akasema akiondoka kwa hasira.
Genesis akabaki amesimama kama mlingoti, bado alikuwa na kazi kubwa sana ya kuhakikisha Farida anamuelewa. Kazi ambayo ilikuwa kubwa kuliko kawaida. Hata hivyo hakujali ukubwa wa kazi hiyo, kichwani mwake kulikuwa na jambo moja tu, ushindi. Aliamini kwa vyovyote vile, lazima ataibuka mshindi.

“Naam, nitashinda. Lazima nishinde na inanipasa nishinde. Mimi ndiye Genesis!”
Akawaza Genesis akianza kupiga hatua za taratibu kuelekea darasani.

Hofu kubwa, iliyoendelea kumsumbua kichwa chake ni Farida kufeli mtihani.
***

Sister Adventina aliingia darasani akiwa na mitihani ya majaribio ya wiki
mkononi mwake, uso wake ulikuwa umekunjamana kwa hasira, alionekana kukasirishwa sana na matokeo ya wanafunzi wake.

“Bado mwezi mmoja tu, mfanye mitihani yenu ya mwisho, lakini matokeo ya jaribio la wiki hii yanazidi kutia kichefuchefu,” alisema Sister Adventina aliyekuwa amesimama mbele ya darasa akiwa hana furaha kabisa.

Wanafunzi wote walikuwa kimya wakimsililiza. Sister Adventina, alikuwa mwalimu wa somo la kemia katika darasa la akina Bianca, Farida, Genesis, Chris na wengineo.

Alifundisha vizuri sana na alipendwa na wanafunzi wote. Darasa zima lilikuwa kimya kutaka kujua matokeo yao.
“Mbaya zaidi, wanafunzi ambao walikuwa tegemeo langu na shule kwa ujumla, wamefeli zaidi!”

Akaendelea: “Hongera sana Genesis, umeendelea kuonesha uwezo wako kwenye majaribio ya wiki na safari hii pia umeongoza kwa kupata alama A. Hongera sana, ongeza bidii zaidi. Bianca umekuwa nyuma ya Genesis lakini matokeo yako safari hii si mazuri sana, umepata B badala ya A uliyoipata wiki iliyopita.

“Majina yanayofuata ni waliopata alama B. Brigite, Christopher, Lucas, Beatrice,
Suzan, Linus, Sostenes na Lilian, mnaofuata wote mmepata chini ya B. Haya ni matokeo mabaya sana kwa shule yetu ni viashiria tosha kwamba hampo tayari kwa
mtihani wa mwisho na hata kama mpo tayari mtafeli vibaya sana,” akasema Sister

Adventina akitembeza macho yake katika darasa zima.
Ukimya wa muda mfupi ukapita darasani, baadaye Sister Adventina akasema: “Farida simama juu!”
Mara moja Farida akasimama.

“Wiki ya tatu sasa unaendelea kufanya vibaya katika majaribio ya wiki, mbaya zaidi kila wiki unaendelea kushuka chini na wiki hii umekuwa wa mwisho kabisa na siyo kwenye theory pekee yake, hata practical pia umefanya vibaya. Umepata S

Farida, hali ambayo ni hatari sana kwako. Naomba baada ya kipindi uje ofisini kwangu kwa mazungumzo zaidi,” akasema Sister Adventina.
“Sawa Sister!” alijibu Farida kwa unyonge.

***
“Nini kinachokushusha kwenye masomo yako?” Sister Adventina akamwuliza Farida ambaye alikuwa amekwenda ofisini kwake kuitikia wito.
Farida akanyamaza kimya.
“Mbona unanyamaza kimya?”

“Nisamehe sister!”
“Suala si kukusamehe, tatizo ni nini?”
“Nitajirekebisha sister!”

“Farida, inaonekana una matatizo ya msongo wa mawazo, nieleze maama mimi ni kama mzazi wako hapa shuleni, hebu sema nini tatizo nikusaidie?” Sister Adventina akasema kwa sauti ya upole sana.

Farida hakujibu kitu chochote zaidi ya kuanza kulia. Alinza kwa sauti ya taratibu lakini kila nukta moja ilipoondoka, ndipo alipozidi kumwaga machozi

usoni mwake. Dakika moja baadaye, mashavu yake yalikuwa chapachapa kwa machozi, macho yakishindwa kufunguka.
“Yesu wangu, lazima atakuwa na matatizo makubwa huyu mtoto,” Sister Adventina akawaza, akisimama na kuzunguka upande wa pili aliokuwa amekaa Farida.

SISTER Adventina aliyajua vizuri maisha ya Farida, alifahamu vyema kabisa historia yake, kwa hiyo maendeleo yake mabaya aliyahusisha moja kwa moja na matatizo ya kifamilia. Farida alikuwa mmoja wa wanafunzi waliotegemewa sana kidato cha sita!

Walimu walijua kabisa kati ya wanafunzi ambao wangefanya vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho ni pamoja na yeye. Taratibu Sister Adventina akasimama na kuzunguka upande wa pili, akaanza kumpigapiga begani na kumbembeleza.

“Huna sababu ya kulia Farida, nayajua maisha yako. Hebu niambie ni nini kinakusumbua?”
“Mmmh! Mmmh!” Farida akasema akitingisha kichwa kuonesha kwamba hana tatizo lolote.

“Hapana Farida, mimi nakufahamu vizuri sana, hupaswi kufeli kiasi hiki katika majaribio ya wiki, huko tunapokwenda ni pagumu zaidi. Najua si kawaida yako na wala huwezi kufeli kwa kiwango hiki, najua lazima kuna tatizo. Hebu niambie ni nini kinakutatiza?”
“Hakuna kitu Sister!” Farida akaitikia kwa upole.

“Lakini unadhani kukaa kimya na tatizo kutakusaidia kitu?”
“Hapana.”
“Sasa kwa nini hutaki kusema, wakati dalili zinaonekana wazi kuwa una tatizo?”
“Ngoja niseme ukweli,” hatimaye Farida akasema.

“Enhee, hebu niambie ni nini kinakusumbua?”
“Baba...”
“Baba yako amefanya nini?”
“Ameibiwa vifaa vyake vya kazi!” akadanganya Farida.

Ilikuwa lazima adanganye, hakuwa na kitu kingine chochote cha kuzungumza ili aeleweke, uongo pekee ndiyo ungekuwa ngao yake kwa wakati huo. Lazima Sister Adventina angeeendelea kumbana zaidi, hivyo aliona njia pekee ya kujitenga na maswali ni kuongopa.
“Pole sana,” Sister akasema.

“Sijapoa, maana hivyo ndiyo tegemeo la familia yetu.”
“Kwani huwa anafanya kazi gani?”
“Ni fudi seremala!”
“Poleni sana!”

“Nashukuru Sister, unajua ni mwezi sasa hafanyi kazi yoyote, kila nikikumbuka hilo nachanganyikiwa kabisa. Mama amenitumia barua juzi na kusema yeye ndiyo amekuwa kila kitu kwenye familia, baba ni kama amechanganyikiwa na sasa ameamua kuwa anashinda kwenye vilabu vya pombe tangu asubuhi mpaka jioni, yaani nimechanganyikiwa kabisa.”

“Pole usijali, Mungu yupo na atafanya kitu kwa ajili ya familia yenu, nakuomba ujitahidi kwenye masomo maana wewe ndiye utakuwa mkombozi wa familia yenu.

“Unajua Mungu amekuchagua wewe usome ili baadaye uje kuwasaidia wazazi wako, huu ni wakati wako wa kusoma kwa nguvu zako zote, hutapata muda mwingine tena zaidi ya huu, jitahidi sana Farida,” Sister akamwambia Farida.

“Nitajitahidi sister, ahsante sana kwa kunipa moyo!”
“Sawa lakini nataka uniahidi kwamba utasoma kwa bidii zaidi na matokeo ya wiki hii yatakuwa mazuri.”
“Nitajitahidi sister!”
“Sitaki kusikia hivyo, nataka ahadi yako!”

“Nakuahidi.”
“Masomo mema.”
“Ahsante sister!”
Farida akasimama na kutoka ofisini kwa Sister Adventina, safari yake ikaishia darasani kwao. Wanafunzi wote walikuwa wanamwangalia yeye akiingia darasani. Hakuna aliyejua siri ya kushuka kimasomo kwa Farida.

Watu wanne pekee ndiyo waliojua kinachoendelea, Chris, Genesis, Bianca na Grace. Wakati akiingia alikuwa akiwatazama wanafunzi wote kwa zamu, alipomfikia Bianca, akaonekana kutabasamu na kumkonyeza, ile ilikuwa na maana kubwa sana. Ni kama alikuwa akishangilia kilichotokea au alikuwa akifahamu nini kingetokea.

Farida hakumwangalia sana, akaachana naye na kuyapeleka macho yake kwa Genesis, yeye alionekaa kuwa na huzuni sana, hakufurahishwa na sura ya Farida iliyojaa makunyanzi na kupoteza kabisa nuru, moyo wake ulimuuma sana. Alijua wazi kuwa kufeli kwa Farida kulikuwa na maana ya mapenzi yao kuishia njiani! Hilo hakutaka kabisa litokee.

Wakati Genesis akimwangalia Farida kwa jicho la huruma ambalo liliongeza machungu aliyonayo moyoni mwake, Farida alimkazia macho na kwenda kuketi kwenye kiti chake kimya, muda mfupi baadaye akalala juu ya meza yake na kuinamisha uso wake chini. Akaanza kulia. Machozi pekee ndiyo yangeweza kuwa mfariji wake kwa wakati huo.

****
“Lakini Farida wangu nilishakumbia kwamba, naweza kuthibitisha kwamba Bianca si mpenzi wangu, kwa nini hutaki kunipa nafasi hiyo?” Genesis alimwambia Farida jioni hiyo wakiwa wamekaa kwenye chumba cha kujisomea.

“Nafasi ipi zaidi ya ile niliyokupa awali na ukashindwa kuitumia?”
“Lakini baby, wewe si unasema kwamba nina uhusiano na Bianca?”
“Siyo nasema ni hali halisi!”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Niseme nini wakati kila kitu kipo wazi.”

“Hapana mpenzi wangu, naomba ukubali nimwite kwa mara nyingine Bianca, yeye atasema ukweli.”
“Hata mara ya kwanza ulimwita na akakanusha, lakini baadaye picha zikawaumbua.”

“Unadhani ni rahisi Bianca kuwa na mimi na aruhusu niendelee kuwa na wewe kwa wakati mmoja? Unataka kusema kwamba Bianca hana wivu? Hebu jaribu kutumia akili mpenzi wangu.

“Naamini yeye ndiye atakayeweza kuweka sawa haya mambo, sitaki tuachane kwa makosa madogo hivi mpenzi wangu. Mimi nakupenda, ingawa ni kweli hiyo picha si kiashiria kizuri kwako, ila amini kwamba hakuna kitu chochote kinachoendelea.”

“Kweli Genesis?” Farida akauliza kwa sauti ya taratibu kabisa.
Kwa kiasi kikubwa, Farida alishaanza kulainishwa kidogo na maneno ya Genesis. Genesis ilibidi atumie maneno ya ushawishi mkubwa ili aweze kumrudisha Farida wake tena.

“Niamini mpenzi wangu!”
“Upo tayari tumwite Bianca hapa aje akanushe uhusiano wenu?”
“Hata sasa hivi!”
“Fanya hivyo!”

Lilikuwa jambo dogo sana kwa Genesis, mara moja akatoa simu yake na kumpigia Bianca ambaye muda mfupi baadaye alifika sehemu waliyokuwa wamesimama.
“Mambo Farida?” Bianca akasalimia.

“Poa vipi?”
“Salama!”
“Bianca samahani kwa usumbufu. Najua kuna wakati nilishakuita kwa jambo kama hili, lakini hapa kuna tatizo kidogo. Kama utakumbuka tulipofungua shule jioni ile tulikuwa tunazungumza pale karibu na kantini, halafu ghafla mwanga wa kamera ukaonekana, nadhani unakumbuka?” Genesis akamwambia Bianca.

“Nakumbuka Genesis!”
“Inaonekana kuna watu walifanya mchezo mchafu, maana zile picha zimeanza kuenea, Farida ameonyeshwa moja, tena anayo. Sasa hilo limesababisha aendelee kuamiani kwamba mimi na wewe bado tuna uhusiano wa mapenzi, jambo ambalo si la kweli.”
“Farida mpenzi,” Bianca akasema kwa sauti ya taratibu sana.

“Abee...”
“Najua ni kiasi gani unampenda Genesis wako, hilo nalitambua lakini ukiyapa mapenzi nafasi kubwa sana kichwani mwako hasa kwa muda huu wa kujiandaa na mitihani ni hatari sana.

“Genesis ni kaka yangu, kama nilivyosema mwanzoni, familia zetu ni marafiki kwa hiyo ukaribu wetu usikupe mashaka, hata mimi moyo wangu una nyama, kama ningekuwa na uhusiano naye, nisingekubali wewe uwe naye. Amini ninachokuambia, halafu achana na maneno ya watu.

“Ni kweli siku ile tuliona mwanga wa kamera na kusema ukweli ulitushtua sana, kumbe kuna watu walitupiga picha. Naomba kwa hilo utusamehe, maana hata sisi wenyewe tulichanganyikiwa tukijua ni viongozi wa shule, lakini kumbe siyo kweli.

“Acha kusikiliza maneno ya watu, kuwa na msimamo na maisha yako. Niamini mimi ninachokuambia hakuna kitu kinachoendelea kati yangu na Genesis!” Bianca akasema kwa sauti ya taratibu sana.
Maneno yale yalimwingia vizuri sana Farida aliyekuwa kimya akiwasikiliza kwa makini.
“Kweli Bianca?” Farida akauliza kwa upole.

“Sina sababu ya kukudanganya Farida.”
“Ahsante sana Bianca, nashukuru sana!” Farida akasema akimfuata Bianca na kumkumbatia.
Baada ya hapo alimkimbilia Genesis na kujitupa kifuani mwake!
“Umenisamehe?” Genesis akamwuliza.

“Wewe ndiyo unatakiwa kunisamehe mimi!” Farida akamwambia Genesis.
“Basi tusameheane mpenzi wangu!” Genesis akasema.
“Haya basi, TUMESAMEHEANA!”
“Ahsante sana!”

“MWONE VILE, UNAJIFANYA KING’ANG’ANIZI SANA, UNADHANI WEWE PEKE YAKO NDIYE UNAYEJUA KUPENDA. HUWEZI KAMWE KUWA NA GENESIS, UTAKUWA NAYE WAKATI MIMI NIKIWA NA JINA LINGINE...NAAM! NIKIITWA MAREHEMU BIANCA NDIYO ITAKUWA NAFASI YAKO KUWA NA GENESIS, LAKINI KWA SASA MAPAMBANO BADO YANAENDELEA...” Aliwaza Bianca akiwaangalia Farida na Genesis waliokuwa wamekumbatiana.

Hicho kilikuwa kiapo kutoka moyoni mwake, kwamba lazima asambaratishe penzi lao. Hilo alijiahidi kulitimiza, hata hivyo hakuwa mwenyewe katika vita hiyo, wazazi wake na wazazi wa Genesis walikuwa upande wake, hivyo ushindi ulikuwa ni wa lazima!

Je, nini kitatokea? Nani ataibuka mshindi kati ya Bianca na Farida?
 
SEHEMU YA 15


Haraka anamfuata na kumrukia akimkumbatia kwa furaha sana. Wakati tendo hilo linafanyika, Bianca alikuwa akiwaangalia kwa hasira huku ndani ya nafsi yake kukiendelea kuwa na nia ya kuhakikisha anasambaratisha penzi lao. Hilo linaendelea kuwa siri iliyojificha katikati ya moyo wa Bianca pekee, lakini alijiapiza kuhakikisha kwamba yeye anakuwa mke wa Genesis!
Je, nini kitatokea? Nini mwisho wa mpambano huu wa mapenzi? SONGA NAYO...



“HAKUNA anayekutaka katika familia yao, kwanini unajipendekeza? Kwanini usitafute mafukara wenzako? Watu wengine bwana, sijui wameumbwaje? Unajifanya mzuri, mzuri utakuwa wewe? Hata kama ni kweli mzuri, lakini uwe na pesa sasa, siyo uzuri wa bure, unanuka shida mpaka kwenye nywele,” Bianca aliendelea kumimina maneno makali ya kashfa ndani kwa ndani!

Kama maneno hayo angeyasema kwa sauti kubwa na Farida akasikia, hali ingekuwa mbaya sana, maana yalikuwa maneno ya kashfa na dharau kubwa sana kwa Farida. Aliendelea kuwakazia macho wakiwa wamekumbatiana, moyo wake ukamuuma sana.

“Lakini hata hivyo wameshachelewa, kwa muda uliobaki, ni muujiza tu, utokee ndiyo utamfanya Farida afaulu, lakini nina uhakika huyu lazima afeli, hawezi kwenda Chuo Kikuu huyu! Kikubwa akamsaidie mama yake kuosha vyombo,” kashfa zinazidi kumtoka kichwani mwake Bianca.

Kama angekuwa na uwezo wa kumuua, angefanya hivyo ndani ya sekunde chache sana, kwake Farida alikuwa sawa na kichefuchefu! Alimchukia sana na alimwona kama nuksi katika maisha yake. Yeye ndiye alikuwa kikwazo cha Genesis kukataa kuwa naye!

“Shiiit, lakini bado nina kitu cha kufanya, siwezi kuwaacha muendelee kuwa wapenzi. Mimi ndiye Bianca, mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wakwe zangu ni wahadhiri wakubwa nchini! Si li-Farida lisilo na mbele wala nyuma,” aliendelea kuwaza huku akiwa ameuma meno kwa hasira.

Farida na Genesis wakawa wamejisahau kabisa, hawakukumbuka kama wapo shule, waliendelea kukumbatiana hadi dakika mbili baadaye walipoachiana. Walikuwa wamezama kwenye dimbwi zito la bahari ya mapenzi. Farida alikuwa amelowana uso mzima kwa machozi ya furaha. Kwake Genesis alikuwa kila kitu katika maisha yake.

Alikuwa mwanaume wa maisha yake, hakutamani wala kusikia kuwa na mwanaume mwingine yeyote zaidi yake. Kurudiana naye kwa mara nyingine, alihisi moyo wake kuingiwa na ubaridi mkali, furaha ya ajabu ikabubujika ndani kwa ndani akiwa na amani ya moyo!

“Hongereni mwaya, Farida acha kusikiliza maneno ya watu, Genesis ni wako, acha presha!”
“Ahsante sana Bianca kwa ushauri wako!” Farida akasema.

“Siyo ahsante pekee, ni lazima uniahidi kulifanyia kazi!”
“Nakuahidi Bianca!”
“Nina jambo lingine!”

“Lipi tena Bianca rafiki yangu, niambie tu nakusikiliza, sisi sasa ni marafiki wa kweli!”
“Kwanza batilisha kauli yako, mimi si rafiki yako!”
“Kumbe nani?”

“Mimi ni wifi yako, kumbuka Genesis ni kaka yangu, kwahiyo mimi nabaki kuwa wifi yako na wewe pia.”
“Oooh! Jamani ahsante sana Bianca, nimefurahi kusikia hivyo wifi yangu! Enhee kuna jambo ulikuwa unataka kuniambia, ni nini hicho?’

“Ni kuhusu masomo, unashuka sana siku hizi, najua sababu ni Genesis, sasa achana na mawazo, nimeshakuhakikishia kwamba sina uhusiano naye, basi unatakiwa kuhamishia akili yako kwenye masomo, sawa wifi yangu?”
“Nimekuelewa vema.”

“Kaka Genesiss, kuwa makini na wanafiki, utakuja kumpoteza mpenzi wako bure!”
“Yaani acha tu Bianca, nachanganyikiwa sana mimi, siwezi kuishi bila Farida wangu. Nipo tayari kupoteza kila kitu lakini si Farida wangu, huyu ni mwanamke wangu, nampenda sana na natamani sana aendelee kuwa wangu milele yote. Naamini nikiishi naye, furaha yangu itakuwa ya kipekee!”

“Ni kweli kabisa.”
“Bianca nakushukuru kwa kila kitu, bila shaka utakuwa mshauri wangu namba moja kuanzia sasa!”
“Bila shaka Farida!”
“Sasa jamani?!” Genesis akasema.

“Nini?”
“Muda, hebu tuondokeni tukajisomee, hatuna muda wa kupoteza tena.
“Poa,” Bianca akaitika.

Wote wakatawanyika wakiwa na furaha ya ajabu mioyoni mwao. Ni Bianca pekee ndiye alikuwa na furaha ya kinafiki, kwa nje alionekana kuwa na furaha lakini ndani ya moyo wake kulikuwa na vitu tofauti kabisa. Alimchukia Farida kuliko kitu kingine chochote duniani.

Bado alikuwa kwenye mapambano. Hakutakiwa kumpa nafasi Farida aongeze juhudi kwenye masomo yake, anamfahamu vizuri sana Farida, anajua kichwa chake kilivyo chepesi kunasa mambo, kwahiyo kama angelegeza uzi kidogo tu, Farida angepanda kimasomo na mwisho wa siku angempoteza Genesis. Jambo hilo hakutarajia litokee akiwa hai, huenda lingetokea, lakini akiwa ndani ya jeneza!

***
Zilibaki siku saba tu, kabla ya kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita, bado Genesis alikuwa na wasiwasi sana na Farida, hakuamini kama kweli alikuwa ameshajisomea vya kutosha kuweza kumudu kufanya mitihani.
Jambo hilo lilimuumiza sana, kwani Farida alitumia muda mwingi zaidi kumfikiria yeye kuliko masomo na hivyo kuharibu mustakabali mzima wa masomo yake. Alikuwa ana mawazo sana, akiwa amejilaza chini ya mti jioni hiyo akijiandaa kuanza kufanya mazoezi.

Akiwa katika hali ya mawazo, simu yake ya mkononi ndiyo iliyomnasua! Alipotupa macho kwenye kioo, akakutana na jina ‘Ma Mumy’, alikuwa ni mama yake mzazi anampigia. Mara moja akabonyeza kitufe cha kupokea na kupeleka simu sikioni mwake.

“Shikamoo mama,” ndiyo neno la kwanza kutamka baada ya kupokea simu.
“Mar-haba mwanangu, habari za masomo?”
“Nzuri mama, za hapo nyumbani?”
“Huku ni nzuri kabisa, lakini nilipenda kufahamu maendeleo yako, maana bado wiki moja, uanze mitihani yako!”

“Nipo sawa mama, naamini unanifahamu vizuri, nyie anzeni kunitafutia vyuo vya nje mama, najua nitafanya vizuri mama’ngu!”
“Basi, ni vema kama ndivyo, nilitaka kusahau, vipi kuhusu mwenzako, kuna matumaini?”
“Nani Farida mama?”

“Ndiyo, kwani una mwenzako gani tena zaidi yake?”
“Aaaaah kuhusu Farida mamaaaa....unajua alikuwa na matatizo kidogo hapa katikati, kwahiyo ninachoweza kusema mama ni kwamba...” Genesis hakuweza kuongea kinachoeleweka, alibaki kujiuma-uma bila kuongea chochote cha maana.

“Naaminisha anaweza kufanya vizuri kwenye mitihani yake?” Mama yake akamkatisha.
“Bila shaka mama,” akajibu haraka, lakini moyoni mwake alikuwa na mawazo sana.
“Sawa, Mungu awatangulie, nilitaka kufahamu hilo tu!”
“Ahsante mama, jioni njema, msalimie sana baba!”

“Namba yake unayo!”
“Lakini nataka hizi salamu uzifikishe wewe mama, kwani ni vibaya?”
“Haya mwanangu usijali nitamwambia unamsalimia na wewe pia msalimie Farida na dada yako Bianca!”
“Zimefika!”

Genesis aliitoa simu sikioni kama vile anashusha mzigo mzito kichwani, alikuwa hana amani kabisa. Simu ya mama yake ilimchanganya sana. Alijua ni kiasi gani alikuwa katika mtihani wake wa mwisho wa kumpata Farida, kama angefeli ni wazi kwamba asingeweza kupata nafasi ya kuwa naye tena katika maisha yake, jambo ambalo hakutaka kabisa kuliruhusu litokee.
Bila kutarajia, machozi yakaanza kumiminika machoni mwake kama maji, alikuwa na uchungu mwingi sana.

***
Ilikuwa Jumatatu saa 2:30 Asubuhi, wanafunzi wote wa kidato cha sita, nchi nzima walikuwa wanaanza kufanya mitihani yao ya mwisho. Miongoni mwao alikuwa Farida, ambaye kwake mtihani huo ulikuwa zaidi ya kipimo cha maarifa yake, alikuwa akifanya mtihani wa mwisho utakaoamua au kupinga kuendelea kuwa katika uhusiano na Genesis.

Aliketi kwenye kiti chake ndani ya chumba cha mtihani akiwa na mawazo tele kichwani, mtihani wa kwanza ukiwa ni Biology - Paper One (Baiolojia - Mtihani wa Kwanza). Kama yalivyo maelekezo katika katatasi yake ya maswali, yaliyomtaka kusoma maswali yote kwanza kwa makini kabla ya kuanza kuyajibu, alifanya hivyo!

Alihisi kutetemeka mwili mzima, maswali mengi yalikuwa ni yale aliyoyafahamu vizuri, lakini alishasahau kabisa jinsi ya kuyajibu! Kabla ya kuanza kufanya ule mtihani, tayari alishajua amepoteza asilimia sabini! Hiyo ilikuwa na maana kwamba, kama angefanya maswali yale aliyoyafahamu vema alikuwa na uhakika wa kupata asimilia thelathini ambayo ingekuwa daraja S, kama angepata chini ya asilimia ishirini na tano, ilikuwa na maana kwamba angepata F, matokeo ambayo kwa hakika yalikuwa mabaya!

Ulikuwa mwanzo mbaya wa kuharibu kwanza maisha yake, lakini pili na muhimu zaidi kwake kwa wakati huo ni MPENZI WAKE GENESIS! Farida akajikuta akianza kulia. Alianza kwa sauti ya chini, lakini baadaye akazidisha kilio, msimamizi wa mtihani akamfuata haraka!

“Una nini binti?” Akamwuliza kwa mshangao.


NDOTO zake zote zilikuwa zinaelekea ukingoni, kila kitu kilikuwa kinakwenda kuharibika. Mtihani ule wa kwanza, ulikuwa kielelezo tosha kwamba, hata mingine iliyokuwa imesalia, angefanya vibaya sana.

Msimamizi wa mtihani aliyekuwa amesimama mbele yake, ni kama alikuwa hajamuona, alihisi moyo wake kwenda mbio na taswira za kufanya vibaya zikiwa wazi kabisa. Wakati ule hakuwaza sana kuhusu kufeli maisha yake, aliwaza zaidi juu ya Genesis wake, maana tayari alishapewa taarifa kwamba ili wazazi wake wamkubali angalau apate nafasi ya kuendelea na elimu ya chuo kikuu, ambapo angalau angeambulia shahada ya kwanza ambayo kwa familia ya Genesis, wangeona afadhali!

“Binti, una matatizo gani?” yule msimamizi aliendelea kumuuliza, lakini Farida hakujibu kitu.
“Binti si nazungumza na wewe!”
“Enheee...” Farida akashtuka mawazoni baada ya msimamizi yule kumgusa begani.”
“Una nini?”

“Nipo sawa!”
“Mbona unalia?”
“Kichwa kinaniuma sana, nahisi kama kinauma upande mmoja.”
“Pole sana, hebu subiri nifanye mawasiliano na watu wa huduma ya kwanza!”
“Hapana sina hali mbaya sana, nikipata hata maji nikajimwagia kichwani, nitakuwa sawa.”

“Sawa, lakini wanaoweza kukusaidia ni hao watu wa huduma ya kwanza, umesahau kwamba unafanya mtihani wa taifa?”
“Najua!”
“Au kuna ujanja unataka kufanya?”
“Ujanja? Hapana!”

“Basi subiri kwanza, nifanye nao mawasiliano watakuja kukuchukua. Kila kitu utafanya chini ya uangalizi wao, lakini jitahidi kwenda na muda, maana muda wa kumaliza mtihani unazidi kusogea.”
“Nimekuelewa vizuri.”
Mara moja yule msimamizi akafanya mawasiliano na watu wa Huduma ya Kwanza ambao walifika mapema sana na kumchukua Farida.

“Pole sana binti, usijali utakuwa sawa!”
“Ahsante!”
Wakaongozana naye hadi kwenye chumba maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya utolewaji wa huduma ya kwanza, akapewa maji ya kunywa, akanywa kisha akapewa na dawa za kutuliza maumivu na kukandwa kwa maji ya baridi kwa ajili ya kupunguza joto ambalo mwenyewe alisema alikuwa akihisi kichwani mwake.

Baada ya dakika kumi na tano, Farida alirudishwa kwenye chumba cha mtihani akiwa ana nafuu kidogo. Muda ulikuwa unazidi kusonga mbele, hivyo aliketi kwenye kiti chake na kuanza kujibu maswali aliyokuwa na uhakika wa kuyapata kwanza.

Baada ya hapo, Farida akaanza kupambana na maswali mengine magumu, ambayo kwa asilimia kubwa hakuwa na uhakika wa kuyapata. Muda wa kumalizika mtihani ulifika, kengele ikalia na wanafunzi wakaanza kutoka nje. Farida alikuwa na uso uliokunjamana maana hakuwa na matumaini ya kufanya ule mtihani vizuri.

***
Jioni, Farida alikutana na Genesis kwenye mgahawa wa shule. Uso wa Genesis ulionekana kuwa na furaha sana, lakini Farida alikuwa na mawazo sana. Hilo Genesis hakuweza kulifahamu mara moja.

“Niambie mpenzi wangu, naamini mtihani wa leo utakuwa umefanya vizuri, umekuja kama vile tumetungiwa na walimu wetu. Ulikuwa mwepesi sana, naamini kama huna A pale basi B safi inapatikana!” Genesis akamwambia Farida akitabasamu.

“Genesis!” Farida akaita kwa huzuni.
“Bee!”
“Ule ni mtihani mwepesi?”
“Hakika, pale najua nina A yangu safi kabisa!”
“Genesis!!!”

“Kwani vipi?”
“Pale nategemea S au F!”
“Usiseme hivyo mpenzi wangu, lazima ujipe moyo, achana na kauli za kujikatisha tamaa!”
“Siyo kujikatisha tamaa Genesis, mimi ndiyo nimefanya huo mtihani, najua nitakachokipata!”
“Matokeo hayatabiriki!”

“Mbona wewe umejitabiria A?”
“Kwa sababu niliufanya vizuri na ninaamini nitapata alama hiyo kutokana na jinsi mtihani ulivyokuja.”

“Hata kwangu pia ni vivyo hivyo, naona ugumu wake ndiyo maana natabiri matokeo hayo.”
“Lakini umeshasau sharti walilotoa wazazi wangu juu ya penzi letu?”
“Najua ndiyo maana nahuzunika.”

“Sikiliza, acha paniki, mitihani mingine bado inakuja. Jitahidi kutulia, unaweza kufanya vyema na kupata nafasi ya kuendelea na chuo. Isitoshe Farida, kichwa chako nakifahamu vizuri sana, kwa nini ufeli?”

“Kwani napenda Genesis? Ni jinsi mtihani wenyewe ulivyo!”
“Nakuomba kwa sasa utulie, acha kuwa na mawazo ili uweze kufanya vizuri katika mitihani iliyobakia!”
“Nitajitahidi mpenzi wangu.”
Wakaagana.

***
Kila Farida alipokuwa akitoka kwenye chumba cha mtihani alionekana kuwa na mawazo mengi sana, hakuwa na matumaini kabisa ya kufanya vizuri. Mpaka anamaliza mitihani yote, matumaini yake yalikuwa kidogo sana.

Alikuwa na huzuni kubwa sana moyoni mwake, si kwa sababu anakwenda kufeli mitihani yake, lakini kwa sababu anakwenda kumkosa mpenzi wake ambaye alimpenda kwa moyo wake wote. Hilo ndilo lilikuwa tatizo kubwa zaidi kwa Farida.

Baada ya kumaliza mitihani yao, wanafunzi wote wa kidato cha sita walirejea majumbani mwao! Tayari walikuwa wameshamaliza elimu ya kidato cha sita. Shule ya St. Thomas ilisifika kwa ufundishaji mzuri, hivyo asilimia kubwa ya wanafunzi walirudi majumbani mwao, sura zao zikiwa zimejaa tabasamu, maana walikuwa na uhakika wa kufanya vizuri na kusonga mbele katika elimu ya chuo kikuu.

Farida hakuwa na amani kabisa, matumaini yake yalikuwa hafifu sana, alijua kwa vyovyote vile, isingekuwa rahisi kufaulu, kutokana na jinsi alivyojibu maswali yale. Alipokelewa nyumbani kwao Mtoni Kwa Aziz-Ali, jijini Dar es Salaam kama shujaa aliyetoka vitani, matumaini ya wazazi wake yakiwa makubwa sana.

“Tunaamini mwanetu, utakuwa umefanya vizuri mitihani yako. Wewe ndiyo mkombozi wa familia hii, Mungu amekuchagua ili uje utusaidie, ni imani yetu kwamba utafaulu,” alikuwa baba yake mzazi, akimwambia Farida wakati akiingia sebuleni ya nyumba yao chakavu ya kupanga.
“Pole mama, karibu sana, karibu sana mama,” mama yake naye alidakia akichukua begi lake na kuliingiza chumbani.

“Enhee za masomo?” baba yake akauliza.
Farida hakujibu kitu zaidi ya kubaki anamkodolea macho baba yake. Baba yake akashangaa sana, alishindwa kuelewa sababu ya mwanaye kukosa furaha kiasi kile.
“Mbona upo kimya?” baba yake alimwuliza, lakini Farida hakujibu.

“Kuna tatizo?” baba yake akauliza tena lakini pia aliendelea kubaki kimya.
Mama yake akatoka chumbani alipokuwa amekwenda kuhifadhi begi, uso wake ukionekana kupambwa na tabasamu pana, lakini alipowapiga macho mume wake na mwanaye, akaona huzuni zimewatawala.
“Baba Farida, kuna nini?” mama akauliza, lakini hakujibiwa.

“Mbona mnanichanganya? Farida nini kinaendelea?” mama akamwuliza mwanaye.
Mara ghafla macho ya Farida yakazungukwa na machozi, ni baada ya taswira ya Genesis wake kuonekana mbele yake huku matumaini ya kumpata yakizidi kufifia! Hapakuwa na mwanaume mwingine duniani ambaye angekuwa na hadhi ya kuishi naye zaidi ya Genesis!

Ni mwanaume huyo pekee ndiye aliyepanga kumpa zawadi ya usichana wake, ambayo aliitunza kwa muda mrefu sana kwa ajili ya mumewe. Mawazo hayo yakasababisha Farida azidishe kilio chake kwa sauti ya juu! Bila kujua kilichokuwa kikimliza mwanaye, mama yake naye akaanza kulia.

NA MALIZIA PART MOJA KWAJILI JANA TULIKOSA

KULIKUWA na kila dalili za tatizo kubwa katika familia yao, kama watu wangepita nje na kusikia sauti zile za kilio, wangejua lazima kulikuwa na msiba au taarifa mbaya katika familia hiyo! Farida alikuwa analia kwa uchungu maana alijua wazi kwamba angefeli mitihani yake, lakini mama yake alijikuta akilia kwa huruma ya mwanaye!
Farida alijua jinsi wazazi wake walivyomtegemea, alifahamu vyema jinsi ambavyo walimchukulia kama kila kitu kwao, tegemeo la familia nzima ya kimasikini. Aliumizwa na mapokezi ya wazazi wake, ni mapokezi ambayo kwake yeye aliona kama hastahili kabisa kupewa!

Tayari alikuwa na uhakika na majibu mabaya ya mitihani yake, kwa nini apewe heshima kubwa kiasi kile? Aheshimiwe kiasi kile? Hakika hakutaka kupongezwa maana alijua kwamba tayari alishaharibu! Pongezi zile zilikuwa ni kumzidishia maumivu zaidi moyoni mwake.

Kufeli mitihani yake kungeweza kuwa jambo la kawaida, kama Genesis angeendelea kuwa wake, lakini tafsiri ya yeye kufanya vibaya ni kwamba, kwanza alipoteza mustakabali wa maisha yake, lakini pia alimpoteza mpenzi wa moyo wake, mwanaume ambaye alimpa hifadhi ndani ya moyo wake; Genesis!
Baba alibaki anawashangaa wote mama na mwana wanavyolia kwa uchungu bila kufahamu sababu.
“Mama Farida, mbona sikuelewi, kuna nini?”

“Huoni mtoto analia,” mama Farida alisema akiendelea kuangua kilio.
“Kwa hiyo mtoto akilia na wewe unalia bila hata kujua sababu.”
“Sababu sio muhimu sana mume wangu, midhali mtoto analia, maana yake ni kwamba ana matatizo, kama unavyojua, matatizo ya mtoto ni yetu wote, ndiyo maana unaona nalia.”

“Acha ujinga, hebu zungumza na mwanao umwulize tatizo ni nini sio kuungana naye kwenye kulia, bila kujua tatizo!” baba akamwambia mkewe.

“Sawa.”
“Tatizo ni nini mwanangu?” mama Farida akamwuliza mwanaye.
“Mitihani mama!”

“Ilikuwaje?”
“Mama karibu yote, sijafanya vizuri.”
“Kwa nini?” baba yake akadakia.

“Nilikuwa sijisikii vizuri, kizunguzungu kilikuwa kinanisumbua karibu siku zote nilizokuwa nafanya mitihani yangu, nashindwa kuelewa baba.”
“Kwa hiyo hakuna mategemeo tena?” baba yake akauliza akionekana kukata tamaa kabisa.
“Yapo, lakini...”

“Lakini nini mwanangu? Inaonekana uliacha kilichokupeleka na kuanza kufanya ujinga. Kwa nini unasema lakini!” baba yake akauliza kwa ukali kidogo.
Ni mtoto huyo ndiye alikuwa tegemeo lao la kuokoa familia yao, kitendo cha kuanza kusita juu ya matokeo yake, kilimnyima raha kabisa.

“Baba nilikuwa nasoma sana, lakini nashindwa kuelewa, sijui kwa nini mtihani ulikuwa mgumu kiasi kile, lakini hata ile hali ya kizunguzungu ilinichanganya pia baba, lakini mimi naomba tumuombe Mungu, tutulie mpaka matokeo yatakapotoka, unaweza kutokea muujiza.”

“Hakuna muujiza katika kitu ulichokifanya mwenyewe mwanangu, kama ulifanya madudu hayawezi kubadilika na kama ulifanya vizuri itakuwa hivyo,” baba yake akasema.
“Ndiyo maana nasema tusubiri matokeo yakitoka ukweli utajulikana, ingawa mimi naamini lolote linaweza kutokea,” Farida akasema kwa unyonge.

Furaha ya wazazi wake ikayeyuka ghafla, walimwamini sana mtoto wao, lakini majibu aliyokuja nayo, yaliwasononesha sana, matumaini yao yote kuwa angekuwa mkombozi wa familia, yakayeyuka kama barafu!

***
Gari la kifahari aina ya Toyota VX lilikuwa likiingia katika geti jeusi, kwenye nyumba kubwa nzuri ya kuvutia, eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam. Alikuwa ni Genesis anarejea nyumbani akitokea Morogoro baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha sita akiwa na dereva ambaye alikwenda kumchukua shuleni.

Baada ya gari kuingia, Genesis alishuka na kuanza kutembea taratibu kufuata lango la kuingia sebuleni. Kazi ya kushusha mizigo yake aliiacha kwa dereva ambaye alijua kazi yake ipasavyo. Sebuleni akakutana na sura za wazazi wake zikiwa zimepambwa kwa tabasamu mwanana.

“Karibu nyumbani mwanetu, bila shaka mambo yalikwenda vizuri,” Profesa Mshana, baba wa Genesis alisema akitabasamu.
“Baba...hata salamu?!”
“Karibu nyumbani,” mama yake naye akasema.

“Ahsanteni sana wazee wangu. Shikamooni,” akasalimia Genesis akiachia tabasamu usoni mwake.
“Mar-haba!” Wote wakaitikia kwa pamoja.
“Naamini njia ya kwenda chuoni umeitengeneza,” Profesa Mshana akasema.

“Bila shaka baba.”
“Vizuri sana mwanangu, vipi lakini mitihani yako?” mama naye akaongeza.
“Matarajio ni makubwa sana mama, naamini nitafanya vizuri.”

“Vipi mwenzako?” mama yake akauliza kwa sauti ya utulivu sana.
“Aaah! Chris naye atafanya vizuri, nilizungumza naye. Kwa ujumla matumaini ni makubwa karibu kwa wanafunzi wote, mtihani haukuja vibaya sana.”
“Sizungumzii Chris!”

“Kumbe nani mama?”
“Mwenzako Farida.”
“Naye atafanya vizuri!” akasema Genesis kwa kujiamini.

Ndani ya moyo wake hakuwa na matumaini makubwa ya Farida kufaulu, lakini aliamua kusema hivyo kwa nia ya kujiridhisha yeye mwenyewe! Farida hakuwa na uhakika wa kufaulu, lakini alitaka kuwanyamazisha wazazi wake.
Jibu lake liliubadilisha kabisa uso wa mama yake, ambaye alionekana kuanza kuwa na mawazo kidogo. Ni kama hakupenda kusikia kauli hiyo ya mwanaye.

“Umesema Farida...” baba yake akauliza tena.
“...Atafanya vizuri baba, naye nilizungumza naye baada ya mitihani yake.”
“Sawa, nadhani unafahamu kwamba huo ndiyo mtihani wake wa mwisho, huo utaamua kwamba atakuwa na wewe au lah!”

“Najua baba, ndiyo maana nilimwambia ajitahidi kusoma kwa nguvu.”
“Sawa basi nenda chumbani ukabadili nguo upumzike; karibu sana nyumbani Genesis,” baba yake akasema akilazimisha tabasamu usoni lakini ndani ya nafsi yake alikuwa amechukia sana.

Genesis akaondoka taratibu akielekea kwenye korido kuingia chumbani mwake. Alipoingia tu kwenye korido, Profesa Mshana akamgeukia mke wake haraka na kumwuliza.
“Kwa hiyo Bianca alikudanganya?” akauliza kwa hadhari na sauti ya taratibu kabisa.

“Sijui...sasa nini cha kufanya?”
“Hakuna cha sasa, kifupi Genesis anatakiwa kumuoa Bianca na si vinginevyo. Huyo Farida afaulu asifaulu, lakini lazima uamuzi wetu uwe huo!” akasema Profesa Mshana kwa sauti yake kali ya kumaanisha.

“Kweli?”
“Ndiyo hivyo!”
“Sasa tutafanyaje?”

“Nitajua cha kufanya, lakini awali ya yote nadhani mpigie Bianca aje nyumbani Jumamosi ijayo, tuzungumze naye kwanza kabla ya kuingia katika hatua ya pili. Sitaki matatizo katika familia yangu, sitaki mikosi ya kimasikini hapa,” akasema Profesa Mshana kwa hasira akisimama na kwenda zake chumbani.
Muda huohuo mama Genesis, akachua simu yake na kumpigia Bianca.

“Vipi mama za shule?” akasema baada ya Bianca kupokea.
“Salama, shikamoo mama.”
“Mar-haba mwanangu, pole na mitihani!”

“Nimeshapoa mama.”
“Vipi kuna matumaini?”
“Makubwa sana mama.”

“Vipi kazi uliyokuwa unaifanya, nayo ina matumaini ya ushindi?”
“Ipi mama?”
“Farida.”

“Unanijua vizuri sana mama, hiyo nimeishughulikia safi sana na imekwenda vizuri kuliko kawaida.”
“Kweli?”
“Niamini mama.”

“Nakuamini mwanangu... sasa Jumamosi tulitaka uje hapa nyumbani, tunahitaji kuzungumza na wewe kidogo.”
“Sawa mama.”
“Haya, siku njema, tutaonana Jumamosi.”
“Usijali mama, nawe pia!”

“Ok! Wasalimie wazee hapo nyumbani.”
“Sawa mama, lakini sijawakuta, wote wamekwenda kazini.”
“Wakirudi!”
“Sawa mama.”

Wakakata simu zao. Sekunde mbili tu baada ya mama Genesis kukata simu, mara Genesis akafungua ghafla mlango wa kioo, unaotokea kwenye korido za kuingia vyumbani. Alipofungua alisimama kama mlingoti mlangoni akimwangalia mama yake kwa jicho la hasira.
Ni wazi kwamba kuna kitu kibaya kilichokuwa kikiendelea ambacho hakukipenda. Ilionekana wazi kuwa alikuwa akifuatilia kwa makini mazungumzo ya mama yake na Bianca kwenye simu.

“Una nini?” mama yake akamwuliza, lakini Genesis hakujibu.
Aliendelea kumwangalia mama yake kwa jicho la hasira, akionekana kuanza kulengwalengwa na machozi.
“Kwa nini mama mnanichagulia maisha yangu? Kwa nini?” Genesis akafungua kinywa na kuuliza kwa hasira sana.

Mama yake hakujibu, alibaki kumwangalia akiwa haamini kama maneno yale yalitoka kinywani mwa mwanaye, kwa mara ya kwanza alishuhudia Genesis akimkaripia! Wakabaki wametoleana macho. Haikuwa rahisi kuamini kwamba walikuwa mama na mwana!

Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 16


Ni kama ameumbwa kwa ajili ya kuteseka katika dunia hii; penzi lake kwa Genesis lizidi kukua kwa kasi ya ajabu sana, lakini Farida yupo kwenye vita ambavyo hata yeye mwenyewe havifahamu.

Kikubwa kinachotakiwa ni yeye kufeli mitihani yake ili kumpa nafasi Bianca kuwa na Genesis jambo ambalo hakulijua kabisa. Kilichosababisha mambo kumwendea vibaya kwenye mitihani yake ni mawazo ya kumkosa mpenzi wake Genesis.

Kwa namna alivyofanya mitihani yake, alikuwa na uhakika kabisa kwamba lazima angefeli.

Amerudi nyumbani kwao na kilio, ambacho wazazi wake wanashindwa kuelewa kinapotokea! Farida analia, lakini chanzo ni wazazi wa Bianca kwa ushirikiano mkubwa na wazazi wa Genesis. Hilo hakulijua kabisa.

Wazazi wake wanashangazwa na jinsi alivyo na huzuni, alipoulizwa alibaki kusema kwamba, mitihani ilikuja tofauti na matarajio yake, kwamba ilikuwa migumu na muda mwingi aliokuwa akifanya mitihani yake alikuwa akisumbuliwa na kichwa.

Genesis yeye hana mashaka na mitihani yake, yupo tayari kabisa kuingia chuo kikuu kwa jinsi alivyofanya mitihani yake kwa kujiamini na kwa uhakika zaidi.

Alipokelewa nyumbani kwao kwa shangwe, lakini hali ilibadilika pale aliposema kwamba mpenzi wake Farida anaendelea vizuri na hata mitihani yake ameifanya kwa usahihi na kwamba ana uhakika wa kufaulu.

Hilo linawaudhi sana wazazi wake, ambao nyuso zao zilibadilika na kuwa zilizokunjamana, lakini Genesis hajali, anaingia ndani na kuwaacha wazazi wake sebuleni, ambao wanabishana kwa muda kabla ya Profesa Mshana, baba mzazi wa Genesis, kuondoka.

Muda mfupi tu baada ya Profesa Mshana kuondoka, mama yake Genesis anapiga simu kwa Bianca na kutaka kujua maendeleo ya Farida kwa namna alivyoona, Bianca akamjibu kwamba ana uhakika hatafanya vizuri kwenye mtihani huo kwa jinsi alivyokiharibu kichwa chake.

Wanakubaliana kwamba afike nyumbani kwao kwa ajili ya mazungumzo zaidi, lengo hasa likiwa ni kuhakikisha Farida haolewi na Genesis!
Mapenzi motomoto kati ya Farida na Genesis yanaendelea.

Genesis anafunga safari hadi nyumbani kwa kina Farida na kutaka kuondoka naye, malumbano yanakuwa juu ya mwenendo wa uhusiano wao.

Farida anaonesha wazi wasiwasi wake juu ya wazazi wa Genesis ambao wanaonekana hawamkubali kabisa.

Hata hivyo, Genesis anamwambia kwamba asijali, kwa kuwa yeye ndiye ambaye angemuoa! Genesis anawasha gari haraka akitaka kuondoka, lakini Farida anamwuliza wanapokwenda akionekana wazi kuwa na mashaka kidogo!
Je, nini kitatokea? Nini hatma ya mapenzi hata? Nani ataibuka mshindi kati ya Farida na Bianca? SONGA NAYO...

FARIDA aliyatoa macho yake kwa mshangao, hakujua mahali ambapo Genesis alitaka waende. Kwanza bado hakuridhishwa na majibu yake kuhusu wazazi wake kuwa kipingamizi cha wao kufunga ndoa, lakini sasa anataka kuwasha gari na kuondoka.

Ilikuwa lazima ashangae na kwa kweli alikuwa na hali ya kushang

azwa na kitendo kile. Alitakiwa kujua wanapokwenda kabla ya kuwasha gari na kuondoka. Farida akauliza kwa mara nyingine, safari hii akiwa na sauti ya unyenyekevu kidogo!
“Genesis wangu!” Farida akaita kwa upendo.

“Yes baby!” (Ndiyo mpenzi)
“Where are we going to?” Tunakwenda wapi?)
“Utajua baadaye!” akasema Genesis akianza kuondoa gari taratibu.
“Sitakiwi kujua?”
“Utajua tu mpenzi wangu.”

“Kwa nini isiwe sasa?”
“Ninazo sababu, lakini hutakiwi kujua sasa.”
“Nitajua saa ngapi?”
“Baadaye.”
“Kwa nini lakini?”
“Kwa sababu lazima tutafika, basi pia ni lazima utapafahamu.”
“Nahisi hunitendei haki mpenzi wangu.”
“Sikutendei haki?”
“Ndiyo.”

“Kwa kutokuambia tunapoelekea?”
“Ndiyo, kwani wewe unaona unatenda haki?”
“Sikiliza mpenzi wangu, wakati mwingine mapenzi yanahitaji kulelewa, naamini hata tunapokwenda bila kujua, inaweza kuwa njia ya kunogesha mapenzi.”
“Kivipi?”
“Kwani huniamini mpenzi wangu?”
“Nakuamini sana.”
“Basi tulia, tutafika na utajua ni wapi!”
“Ok!”
Genesis akazidi kukanyaga mafuta, wote wakawa kimya kabisa. Farida hakuuliza kitu chochote tena baada ya pale.
***

“Huku ni Masaki lakini,” alisema Farida wakati Genesis akikata kushoto eneo la International kuifuata barabara inayoelekea Coco Beach.

“Ni kweli?”
“Tunaelekea kwenu?” Farida akauliza akionekana kuwa na wasiwasi mwingi sana.
“Kwani hupendi?”
“Siyo sipendi!”
“Bali?”
“Sipendwi.”

“Sina la kuzungumza zaidi kuhusu hilo, lakini kikubwa nilichokuambia ni kwamba, kuhusu tunapokwenda ni siri yangu.”
“Haya bwana, acha ninyamaze.”

Ukimya ukatawala tena. Kila Farida alipokuwa akiangalia walipokuwa wakielekea alikuwa na uhakika kabisa kwamba wanaelekea nyumbani kwa akina Genesis. Kama matarajio yake yalivyokuwa, Genesis aliendesha gari hadi nyumbani kwao.

Akaingiza gari ndani na kuegesha sehemu nzuri kisha akashuka na kuzunguka upande wa pili, akamfungilia mlango Farida ashuke. Farida akashuka akionekana kuwa na wasiwasi mwingi sana.

“Kwa nini lakini umenileta hapa?” akauliza Farida macho yake yakisoma woga wa wazi kabisa.
“Kwa nini mimi nilikuja kwenu?” Genesis naye akamwuliza.
Lilikuwa swali zito sana, ambalo maana yake ni kama lilijibu moja kwa moja swali lake. Hakuwa na swali lingine baada ya Genesis kumjibu vile. Genesis akamwongoza Farida hadi bustanini ambapo waliketi kwenye viti vya plastiki vilivyokuwa bustanini hapo.
“Ngoja nikalete juisi,” akasema Genesis.
“Sawa, usichelewe.”

“Sichelewi mpenzi, unapenda juisi ya matunda gani?”
“Maembe.”

“Hata mimi hiyohiyo, halafu kwa bahati nzuri ndani ipo nyingi sana.”
“Sawa, enhee baba na mama wapo?”
“Ndiyo wapo, unawaogopa?”
“Nimeuliza tu.”

“Wapo, shaka ondoa, mimi ndiyo wako, hutakiwi kuwa na wasiwasi wowote.”
“Sawa mpenzi wangu.”
“Karibu sana.”

“Nimeshakaribia mpenzi.”
“Haya nakuja,” Genesis akasema akisimama na kujiandaa kuondoka kwenda nyumbani kuchukua juisi.

Kabla hajaondoa mguu wake pale bustanini, akashangaa mlinzi anafungua mlango na gari kuingia ndani. Ndani ya gari lile alimuona Bianca mwenyewe akiendesha, akaegesha kwenye maegesho kisha akashuka na kuanza kupiga hatua za taratibu kabisa!
Wote wakamwangalia kwa mshangao mkubwa.

Siku zote Farida hakumwamini kabisa Bianca. Genesis ndiyo zaidi, hakuwa na imani kabisa na Bianca! Ghafla akiwa anatembea kuelekea mlango mkubwa wa kuingia ndani, akakutanisha macho yake na Farida akiwa na Genesis!
Akashtuka sana!
“Vipi?” Genesis akauliza.

“Safi!”
“Bila taarifa?”
“Usijali, nimetumwa na wazee kuja kuonana na wazee wako.”
“Kuna usalama?”
“Mkubwa sana, kuna kitu nimetumwa nilete.”
“Poa.”

“Haya bwana, nawaona mmepumzika kidogo,” akasema Bianca akionekana kuwa na woga.
“Ndiyo, tutaenda wapi tena, wakati ndiyo hivyo tunalea mapenzi yetu?”
“Haya...Farida mambo?”
“Poa.”

“Miye nawaacha, ngoja niingie ndani, sijui wapo?”
“Utawakuta!”
“Ok! Poa.”

Bianca akaingia ndani, muda mfupi baadaye Genesis naye akafuata, akawakuta sebuleni wakizungumza kwa utulivu sana, hakuwasemesha zaidi ya kwenda kwenye jokofu na kuchukua juisi kisha kutoka zake nje.

“Amefuata nini hapa?” Farida akamwuliza Genesis.
“Nadhani ulimsikia akijieleza mwenyewe.”

“Ni hivyo tu?”
“Kama kuna zaidi sijui, lakini nahisi kuna kitu ametumwa.”
“Sijui kwa nini simuamini!”
“Wasiwasi wako, achana naye bwana.”

Wakiwa wamekaa pale nje, baada ya robo saa tu, Bianca alitoka na kuwaaga kabla ya kuingia kwenye gari lake na kuondoka zake.

Walikaa pale bustanini hadi jioni kabisa, Genesis akamrudisha nyumbani kwao Mtoni Kwa-Azizi Ally.

Wakati wanaagana, Farida akaonekana kuwa na jambo alilotaka kumwambia Genesis. Alikuwa mtulivu sana, lakini akionekana kuwa na jambo kubwa na muhimu sana.
“Genesis unanipenda?” Farida akauliza kwa upole.
“Uliza swali lingine.”

“Jibu kwanza hili.”
“Nakupenda.”

“Kama kweli unanipenda, naomba ulipokee hili kama lilivyo. Sijui kwanini simwamini kabisa Bianca, nahisi kuna kitu anafanya, tena kwa kushirikiana na wazazi wako. Samahani kama nitakuwa nimekukosea, lakini huo ndiyo ukweli.

Jaribu kuufanyia kazi!”
“Paaaaa....” kibao kikali kikatua shavuni mwa Farida.
Uso wa Genesis ukakunjamana kwa hasira, alionekana dhahiri kukasirika sana.
“Unanipiga Genesis?”

“Paaaaa...” kibao kingine kikatua tena kwenye shavu lile lile la awali.
Farida akaanguka chini akianza kulia kwa uchungu. Genesis hakuwa na muda wa kusubiri, akafungua mlango na kuingia kwenye gari lake, akawasha na kuondoka kwa kasi. Akamuacha Farida akiugulia maumivu pale chini.

FARIDA alijuta kumwambia mama yake kuhusu Genesis. Tayari alikuwa ameshaingia kwenye vita ya pande mbili; kwanza hakuwa na imani hata kidogo na Bianca, wazazi wa Genesis na sasa Genesis mwenyewe ambaye ndiye alikuwa tegemeo lake, amethubutu hadi kumpiga!

Hilo lilitosha kabisa kuthibitisha kwamba mapenzi yao yalikuwa yanafikia ukingoni. Mbaya zaidi, sehemu ambayo alitarajia kupata suluhisho, pia anapigwa! Mama yake kumpinga ni kama hakuwa na sehemu nyingine yoyote ya kupata msaada.

Alikuwa tayari kufanya kila kitu lakini asimkose Genesis, alikuwa tayari kukosana na kila mtu lakini Genesis aendelee kuwa mikononi mwake. Alikuwa mwanaume ambaye moyo wake uliridhika kwa dhati kabisa.

Jibu alilompa mama yake kwamba hataweza kuachana na Genesis, lilimpandisha zaidi mama yake hasira, ambaye alikuwa amekunja uso wake.
“Unajifanya kiburi siyo?”

“Siyo kiburi mama!”
“Sasa kama si kiburi ni nini?”
“Mama nitakusikiliza kwenye kila kitu lakini si kuhusu Genesis wangu, siwezi kuachana naye mama, siwezi

“Hivi unapata wapi huo ujasiri wa kuniambia hivyo? Nani amekuzaa? Au una mama mwingine unayemfahamu?”

“Sijasema hivyo mama, lakini Genesis siwezi kuachana naye!”
“Sasa nasema hivi achana na huyo kijana wa watu, sitaki matatizo katika familia yangu.”

“Haiwezekani mama, kikubwa ni kwamba tunapendana na sitaweza kuachana na Genesis wangu ingawa leo amenipiga!” akasema Farida akianza kulia.
“Amekupiga?” mama yake akauliza kwa mshangao mkubwa.

“Najua sababu mama, najua...” akasema Farida akiendelea kulia.
“Unajua sababu?!! Ni sababu gani hiyo ya kupigwa?” mama yake akauliza akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Farida.

Hakuwa na la kujibu, alinyamaza kimya kabla ya muda mfupi baadaye kusimama na kuingia ndani. Kitambo kidogo akasikia sauti ya baba yake nje.

Hakutaka afahamu kilichotokea, akafuta machozi haraka kisha akatoka nje kutenga chakula kwenye mkeka. Wakala pamoja na wazazi wake.

“Hayo mafua kweli leo yamekuonea sana, naona macho yako yanazidi kuwa mekundu,” akasema baba yake.

“Ni kweli baba, lakini nitameza dawa kabla ya kulala.”
“Inabidi ufanye hivyo mwanangu!”

Baba yake hakujua kwamba kulikuwa na kitu kingine nyuma ya pazia, mama yake naye hakutaka mumewe ajue kinachoendelea, maana alimfahamu vizuri asivyopenda matatizo na watu. Alijua wazi kuwa kumwambia kungeweza kusababisha kipigo kwa Farida.
Akayamaza kimya.
***
Kwenye meza ya chakula, walikuwa wamekaa Profesa Mshana, mkewe na Genesis na dada yake wakila chakula cha usiku. Wote walikuwa wanakula kwa furaha huku mazungumzo yakiwasindikiza. Kwa Genesis ilikuwa tofauti kabisa, alionekana kuwa na mawazo mengi sana kichwani wake.

Tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua ni kitendo cha kumpiga vibao Farida nyumbani kwao. Picha ya tukio lile ilikataa kabisa kufutika kichwani mwake, kila alipopeleka kijiko cha chakula kinywani alimuona Farida mbele yake akilia.

Hilo lilimuumiza sana, muda ulivyozidi kwenda mbele ndivyo Genesis alivyozidi kuonekana wazi kuwa na tatizo. Baba yake, Profesa Mshana ndiyo alikuwa wa kwanza kufahamu kwamba mwanaye hakuwa katika hali yake ya kawaida.
“Wewe una nini?”
“Hakuna kitu baba!”

“Hapana, kuna kitu kinakusumbua kichwani.”
“Ni kweli!”
“Ni nini?”

“Sijisikii vizuri tangu mchana baba, hata hamu ya kula sina!”
“Hiyo ni malaria tu, kula kwanza, halafu tutampigia simu daktari aje kukuona!”
“Sijisikii kula baba,” akasema Genesis na kusukuma sahani yake pembeni kisha akasimama na kuondoka zake.

“Genesis...” mama yake akaita, lakini Genesis hakujibu.

Safari yake iliishia chumbani mwake, ambapo alijifungia na kuanza kulia. Aligundua kwamba, kilichosababisha ampige Farida ilikuwa ni hasira kali, maneno yake yalionekana kugonga kabisa katika kichwa chake.

“Ni kweli sielewi kabisa huu ukaribu wa wazazi wangu na Bianca na ni Bianca huyo huyo aliyekuwa akisema ananipenda, halafu hata wazazi nao waliniambia kwamba yeye ndiye atakayenifaa. Hapa lazima kuna mchezo unaendelea na Farida amegundua.

“Masikini mpenzi wangu, hana hatia Farida wangu, nimemuonea bure. Lazima nifanye kitu kwa ajili ya mpenzi wangu, lazima nifanye kitu. Siwezi kumuumiza kiasi kile!” aliwaza Genesis akiendelea kulia.

Moyo wake uliingiwa na ubaridi mkali sana, akiwa hana amani kabisa. Alijiona mkosaji sana kwa mpenzi wake, kitendo alichokifanya kilimuumiza sana moyo wake, akaendelea kuteketea ndani kwa ndani.

“Nitamnunulia kadi na kwenda kumuomba msamaha,” akawaza Genesis.
Akiwa anaendelea kuelea katika lindi la mawazo mazito, mlango wake ukagongwa. Mara moja akafuta machozi yake na kusogea mlangoni.
“Nani?”
“Mimi!” ilikuwa sauti ya dada yake.

“Unasemaje?”
“Hebu fungua mlango!”
“Hapana, siwezi kufungua kama hutasema unachotaka.”
“Nataka kuzungumza na wewe kidogo!”
“Juu ya nini?”
“Kuhusu yanayokusumbua!”

“Haya mambo niachie mimi, nitayamaliza mwenyewe.”
“Huna lolote, najua lazima itakuwa ni huyo Farida wako, sijui ameshakupa limbwata la Uswahili!” akasema dada yake na kuondoka.

Maneno yale yalizidi kumuumiza moyo Genesis, haikuwa rahisi tena kwake kulala. Akaamka kutoka kitandani, akapita sebuleni akiwaacha wazazi wake wakiangalia runinga.

Akaenda mpaka nje alipoingia kwenye gari haraka, akawasha na kupiga honi getini, mlinzi akamfungulia.

“Acha niende kwa Farida, lazima nizungumze naye usiku huu!” akawaza Genesis akiondoa gari kwa kasi.

Usiku huo haikuwa rahisi tena kupata duka lililokuwa wazi kwa ajili ya kununua kadi, akaamua kwenda kwa ajili ya kuomba msamaha hata wa mdomo tu.

Alitamani sana kuwa na amani na mpenzi wake. Foleni hazikuwa nyingi sana barabarani usiku huo, tayari ilishafika saa 2:45 za usiku.

Aliendesha gari kwa kasi sana, nusu saa baadaye alikuwa ameshafika kwa Aziz-Ally, akaingia kwenye mtaa wa akina Farida, mbele ya duka aliloliona mbele yake, akaegesha gari lake na kwenda hadi dirishani.

“Habari yako?” akamsalimia kijana aliyekuwa dukani hapo.
“Nzuri kaka, karibu!”
“Ahsante, naomba Coca Cola baridi!”

Mara moja yule kijana akatoa chupa ya soda na kumpatia, Genesis akaipeleka kinywani haraka.

Hakuwa na lengo la kunywa soda, kikubwa alichotaka kufanya ni kuacha gari lake pale, kwani kwa muda ule ilikuwa vigumu kwenda nalo pale, akihofia kukutana na baba yake.

“Samahani kaka,” Genesis akasema akirudisha chupa baada ya kumaliza soda yake.
“Bila samahani.”

“Hivi huwa unafunga saa ngapi?”
“Saa 4:30 wakati mwingine hadi saa 5:00 inategemea na wateja. Kwa nini umeuliza hivyo?”

“Nataka kufika hapo bondeni mara moja, ndani ya nusu saa nitakuwa nimerudi, kuna mtu namwona mara moja, nilitaka niache gari langu hapa kwako!”
“Sawa lifunge vizuri, hakuna tatizo katika hilo!”
“Usijali, nimeshalifunga!”
“Poa basi mimi naenda!”
“Sawa kaka, hakuna tabu.”


Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 17


Usiku huo huo Genesis akatoka nyumbani kwao Masaki na kwenda kwa akina Farida Mtoni, Kwa Azizi-Ally. Akaegesha mahali na kuomba aangaliziwe na muuza duka ili aweze kwenda kuoana na Farida wake, lengo lake kubwa likiwa ni kuomba msamaha!
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

ILIKUWA lazima azungumze na Farida usiku uleule ili aweze kupata usingizi ipasavyo, kulala akiwa hana amani moyoni, ni jibu tosha kwamba usingizi kwake siku hiyo ungekuwa kitendawi! Genesis akaingia mtaa wa akina Farida, akatembea kwa mwendo wa taratibu kabisa hadi alipoikaribia nyumba yao, akasimama chini ya mti na kusoma mazingira kwanza.

Kwa mbali aliweza kuona watu watatu wakiwa wameketi kwenye mkeka chini, alipoangalia kwa makini akagundua kwamba, mmoja alikuwa mwanaume na wawili wanawake. Hakuwa na haja ya kusumbua ubongo wake kufahamu kwamba wale walikuwa baba yake Farida, mama yake na Farida mwenyewe!

“Nitafanyaje?” akawaza bila kupata jibu.
“Nimeshajua cha kufanya!” baada ya mfupi akajijibu mwenyewe.
Alichokifanya ni kutoa simu yake mfukoni, kisha akapiga namba za Farida na kupeleka simu sikioni.
“Inaita...” akajisemea akitabasamu.

Lilikuwa tabasamu la nje, lakini ndani ya moyo wake alikuwa na mawazo sana, usiku ule usingeweza kupita vyema bila kuomba msamaha kwa mpenzi wake. Moyo wake ulimuuma sana, akajiona mkosaji mkubwa kwa Farida. Simu iliendelea kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
“Ana nini? Mbona hapokei?” akajisemea taratibu akiumia moyoni.

***
“Mbona hupokei hiyo simu?” baba yake Farida alimwuliza, baada ya kuona simu yake inaita kwa muda mrefu, lakini hapokei.
“Achana naye!”
“Ni nani?”
“Baba achana naye, kwanza nakula,” Farida akasema akijikaza kuficha hisia zake, lakini ukweli ni kwamba ile simu ilimuumiza sana.

“Hebu lete hiyo simu hapa...” baba yake akasema na kumnyang’anya ile simu huku ikendelea kuita.
Farida akaogopa sana. Alitetemeka kwa hofu, alijua mambo yalikuwa yameshaharibika. Kama baba yake angepokea ile simu, basi kulikuwa na kila dalili za kumpoteza moja kwa moja Genesis wake. Farida akasimama na kuzunguka upande aliokuwa amekaa baba yake, kisha akataka kumnyang’anya simu yake.

Baba yale alimwangalia kwa hasira, akiendelea kuangalia jina la mpigaji huku akijiandaa kupokea. Akiwa anataka kubonyeza kitufe cha kupokea ili aweze kuzungumza na mtu wa upande wa pili, Farida akaunyakua mkono wa baba yake akitaka kuichukua simu yake.

“Pumbavu kabisa, nitakurarua sasa hivi, unataka kupambana na mimi? Unataka kupambana na mimi?” akauliza baba yake akiwa na hasira sana.
“Naomba simu yangu baba...” Farida akasema akiwa ameung’ang’ania ule mkono.

“Puuuu!” Ulikuwa mlio wa kishindo, Farida alipoanguka pembeni, baada ya baba yake kumpiga kofi kubwa usoni.
Alihisi kuona nyota mbele yake, akaanza kulia kwa uchungu. Hapo mama yake hakukaa kimya, akaona anatakiwa kuingilia ili mwanaye asiumie zaidi.

“Mume wangu, mwache mtoto.”
“Unamtetea siyo?”
“Hapana mume wangu, huyu ni binti mkubwa sana sasa mume wangu, kama ni adhabu napaswa kumpa mimi, si wewe tena mume wangu!”

“Sasa mbona unamwangalia tu? Unadhani mimi nafurahishwa na tabia yake ya kipuuzi?”
“Kwani ana tabia gani mume wangu?”
“Ana tabia gani? Hivi unafikiri ni kitu gani kinamzuia kupokea simu yake kama siyo ujinga?”

“Unayosema mume wangu, yanaweza kuwa na ukweli, lakini wakati mwingine lazima upime maneno yako baba Farida. Huwezi kujua labda ni rafiki zake ambao hataki sisi kama wazazi wake tusikie mazungumzo yao!”
“Sasa nahisi na wewe unataka vibao ndiyo utaelewa nazungumza juu ya nini siyo?”

“Tusifike huko mume wangu!”
“Paaaa...” kikatua kibao usoni mwa mama Farida.
“Mume wangu unanipiga?”
“Kumbe umeona nimefanya nini? Wewe na mwanao wote lenu moja, pumbavu kabisa.

Mimi nahangaika kutafuta pesa, halafu mnaniletea tabia za kipuuzi hapa? Mimi naondoka, nikirudi nahitaji kujua aliyekuwa akipiga simu ni nani...” akasema baba Farida kwa hasira na kumtupia Farida simu yake.
Akasimama na kuanza kupiga hatua za haraka. Alikuwa anaelekea mitaani.

***
Alipopiga simu mara ya pili, moyo wake ulikuwa kama umepigwa na ubaridi mkali, alitamani sana kusikia sauti ya mpenzi wake, alikuwa na neno la kumwambia, alijiona mkosaji sana, alitakiwa kumwambia samahani, hakika maisha kwake yasingekuwa chochote bila ya Farida wake.

Lakini akiwa anasubiria simu yake ipokelewe, akasikia kishindo kikuu, hapo akashtuka na kukaza macho yake upande waliokuwa wamekaa akina Farida. Pamoja na mwanga hafifu aliweza kuona Farida anapambana na baba yake, aliweza kujua hayo kutokana na sauti ya kilio cha Farida.

Mwanzoni hakujua chanzo cha mzozo ule, lakini alipofuatilia kwa makini, aliweza kusikia simu ikitajwa sana, hapo akajua ugomvi ulikuwa unamhusu yeye. Alizidi kuumia moyo wake, maana mpenzi wake alikuwa anapigwa kwa sababu yake.

“No! Natakiwa kufanya kitu fulani kwa ajili yake, anaumizwa mpenzi wangu, nateswa!” akawaza kichwani mwake.

Pamoja na kuwaza hayo, hakujua anaanzia wapi au alitakiwa kufanya jambo gani. Haikuwa rahisi yeye kwenda nyumbani kwao, tena usiku kama ule. Akaamua kutulia pale pale akiendelea kuwaza, macho yake yakiwa upande waliokuwa akina Farida.

Akiwa pale, aliweza kumuona baba yake akisimama na kuendelea kufoka kabla ya muda mfupi baadaye, kuanza kutembea akienda uelekeo wa mahali alipokuwa amesimama. Akapiga moyo konde, akaendelea kusimama palepale, alipomfikia akaamua kumsalimia.

“Shikamoo mzee,” akasalimia Genesis.
“Marhaba kijana wangu, mzima wewe?”
“Sijambo mzee vipi, mbona kama unaongea mwenyewe?” Genesis akamwuliza.
“Matatizo mwanangu!”

“Hapana mzee wangu, unajua matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, usiruhusu mawazo hadi kufikia kuzungumza peke yako barabarani, maisha ni mapambano!”
Genesis aliposema maneno hayo, baba Farida akaamua kusimama kabisa, ni kama alianza kuguswa kidogo na maneno yake.

“Unayosema ni sahihi kabisa kijana wangu, lakini unapokuwa na matatizo, halafu na familia yako nayo ikakuchanganya, lazima uchanganyikiwe zaidi. Kijana, tumia umri wako vizuri kutafuta na kutunza fedha, kama unaweza, jiendeleze sana kielimu, kwani ndiyo chanzo cha matatizo yangu!

“Baadaye ukiwa mkubwa, utajua nazungumza nini, lakini kwa faida yako, ukioa na kujaliwa watoto, hakikisha wanao wanasoma kwa bidii sana. Elimu ndiyo mwanga wa maisha, ndiyo chanzo cha mafanikio. Bila kuwa na elimu, kila kitu mbele yako kinakuwa sawa na giza nene!” alisema baba Farida akimwangalia kwa makini sana Genesis.

“Nimekuelewa mzee wangu, lakini nahisi kama una jambo unanificha zaidi!”
“Ni kweli, lakini hata kama nikikuambia hutakuwa na cha kunisaidia, nilichokifanya mimi ni kukusaidia wewe mawazo kwa ajili ya maisha yako ya baadaye!”
“Ahsante, samahani lakini mzee wangu!”
“Bila samahani!”

“Maneno yako yamenigusa sana, naweza kukusaidia kiasi kidogo cha pesa kama ahsante yangu!”
“Unasemaje?” baba Farida akauliza akiwa haamini masikio yake.
“Samahani kama nitakuwa nimekukosea, sina nia mbaya zaidi ya kukupa ahsante mzee wangui!”

“Hujakosea baba, nitakushukuru sana kijana wangu!”
Genesis akatoa pochi yake mfukoni na kutoa noti kumi za elfu kumi-kumi! Zilikuwa laki moja na kumkabidhi.
“Ahsante sana kijana wangu, nashukuru sana.”
“Usijali mzee wangu, wewe ni sawa na baba yangu kabisa.”
“Lakini sura yako ni kama ngeni kabisa, wewe unaishi wapi hapa?”

“Kweli mzee hunifahamu, mimi ni mgeni, huwa nakuja kumtembelea rafiki yangu, ni yeye ndiye namsubiri hapa amekwenda nyumbani kwao mara moja. Anaitwa Rajabu, anakaa mbele kuleee...” akasema Genesis akisonza kidole kuonesha mtaa uliopo mbele ya nyumba ya baba Farida.

“Mimi nakaa pale, kwenye kile kibanda pale, naishi na mke wangu na mwanangu wa kike, anaitwa Farida. Ni hivi juzi tu amemaliza kidato cha sita, anasubiri majibu. Yeye ndiye tegemeo letu!”
“Usijali baba, atafaulu na bila shaka atakuwa msaada kwa familia.”

“Haya mimi nakwenda!”
“Sawa baba, acha mimi niendelee kumsubiri hapa!”
“Sawa.”
Baba Farida akaondoka na kumwacha Genesis peke yake.

Maneno ya baba yake Farida yalimwingia sana, lakini alimwonea sana huruma, maisha yao yalikuwa ya shida sana. Hata hivyo alifurahi sana kukutana na baba mkwe wake, tena wakapata muda wa kuzungumza na kuonekana kumkubali, kubwa zaidi, ameweza hata kumsaidia pesa kidogo.

“Mwanzo mzuri!”
Bado alikuwa hajakamilisha kazi yake ya msingi iliyompeleka Kwa Aziz-Ally usiku ule. Alichokifanya ni kuchukua simu yake kisha akampigia tena Farida. Simu ikaita kwa muda mrefu sana bila kupokelewa, akarudia tena kwa mara ya pili, ya tatu na hatimaye ya nne ikapokelewa. Genesis akaachia tabasamu pana, akiikimbiza simu yake sikioni.

“Halooo,” sauti ya kike upande wa pili ikasikika.
“Najua nimekukosea sana Farida mpenzi wangu, lakini naomba kuchukua nafasi hii kukuomba msamaha. Nimeshindwa kabisa kulala, nimeama kuja huku kwa ajili ya kuzungumza na wewe. Nipo hapa karibu kabisa na kwenu, naomba uje tuzungumze kidogo, tuweke haya mambo sawa.

“Hujui ni kiasi gani naumia moyo wangu, yaani sina amani kabisa, lazima tuweke haya mambo sawa mpenzi wangu. Sawa mpenzi wangu?” alisema Genesis mfululizo, lakini Farida hakujibu kitu.

“Mbona umenyamaza mpenzi, najua nimekukosea, ndiyo maana nimekuja kwa ajili ya kumaliza haya mambo. Najua shetani halali usingizi kuhakikisha mimi na wewe tunaachana, lakini penye mapenzi ya kweli hakuna anayeweza kuharibu!” akaendelea kusema Genesis, lakini Farida alibaki kimya.

“Baby...” Genesis akaita simuni.
“Umemaliza?!” sauti ya ukali kutoka upande wa pili ikasikika.
“Ndiyo mpenzi wangu!”

“Ndiyo mpenzi wangu!!! We’ kijana, nakuomba sana tena sana. Achana kabisa na mwanangu, sitaki umchanganye mwanangu kwenye maisha yake. Bado ana safari ndefu sana, anatakiwa kusoma ili atuokoe, kama una njama za kumfunga, sisi wazazi wake tumeshajua na nakuomba sana achana naye!” sauti upande wa pili ikatamka.

Hapo Genesis akaduwaa, alielewa wazi kwamba lazima alikuwa ni mama yake, lakini alitaka kuhakikisha.
“Naongea na nani?”
“Mama Farida!”

Genesis alihisi kuishiwa nguvu. Alishindwa kuelewa azungumze nini. Macho yake yakiwa makavu barabarani, kichwani alikuwa amechanganyikiwa kabisa.

Midomo ikitetemeka, akitaka kujitahidi kutamka chochote, lakini ulimi ukikataa kabisa! Aliona dalili za wazi za kumpoteza mpenzi wake, Farida, mwanamke wa maisha yake!

KICHWA chake kilikuwa kizito sana, alishaona ukungu mbele ya penzi lake na Farida, kitu ambacho Genesis hakukipenda kabisa. Alitamani sana kuishi na Farida wake, ndani ya moyo wake alikiri kumpenda sana kwa moyo wake wote! Hakuwa tayari kumpoteza kwa namna yoyote ile.

Aliendelea kuyaacha macho yake yakitembea juu ya dari huku mawazo tele yakizidi kumzonga!

“Lakini nampenda nitafanyaje?” akawaza. Haikuwa rahisi kuwaza jambo lolote kwa wakati ule na kupata jibu, kila kitu kilikuwa sawa na giza nene mbele yake.

Thamani ya maisha yake ingeendelea kuonekana kama angekuwa na Farida wake, ni mwanamke ambaye moyo wake uliridhia kuwa naye kwa dhati kabisa. Akiwa katika mawazo hayo, akapata kitu cha kufanya.

“Acha nijaribu kumpigia tena simu!” akawaza na kuchukua simu yake, kisha akatafuta namba za Farida na kubonyeza kwenye kitufe cha kupiga. “Inaita...” akajisemea baada ya kusikia simu ikiita.

Ilikuwa usiku sana, kiasi cha saa sita na dakika zake za usiku! Simu iliita kwa muda mrefu kabla haijakatika. Akapiga tena, ikaendelea kuita kabla ya muda mfupi baadaye kusikia sauti ya kike kutoka upande wa pili.

“Farida...” akaita Genesis kwa woga, bado aliamini mama yake alikuwa na ile simu. “Ndiyo Genesis, unasemaje usiku huu? Halafu umeshanisababishia matatizo makubwa sana kwa wazazi wangu!” “Najua Farida, lakini nisingeweza kulala bila kusikia sauti yako mpenzi!” “Si tayari umeshaisikia?” “Ndiyo!” “Ok! Usiku mwema.”

“Hapana Farida!” “Kuna kingine?” “Kipo mpenzi wangu.” “Ni nini?” “Nataka kukuambia kwamba, yale niliyofanya naomba unisamehe mpenzi wangu, moyo wangu unaungua, nakosa amani kabisa.

Najutia kitendo kile, naomba unisamehe Farida, mimi ni wako mpenzi. Tafadhali usichukie!” “Naomba tuongee kesho Genesis, hapa nimetoka nje kidogo nimejifanya naenda msalani, ndiyo nimeweza kupokea simu yako.

Hebu tuishie hapa kwa leo, tutaongea zaidi kesho!” “Sawa, lakini napenda kujua kama umenisamehe!” “Kesho Genesis!” “Farida!” “Abee!” “Fahamu kwamba siwezi kulala, msamaha wako ni kitu cha maana sana kwangu, nimekuwa nikihangaika sana leo, hebu naomba kwanza ukubali kunisamehe, halafu hayo mengine tutazungumza kesho!” “Ndiyo maana nimesema kila kitu tutazungumza kesho Genesis!” “Farida kwa hiyo hutaki kunisamehe?” “Sijasema hivyo.”

“Bali?” “Tutazungumza kesho, ninayo maswali nataka kukuuliza kabla sijapitisha msamaha wangu kwako, unajua nimeshaumia sana kwa ajili yako.

Umefika wakati wa kufanya maamuzi sahihi Genesis, ndiyo maana unaona nakuwa mgumu kidogo kukusamehe haraka, kesho tutajua kila kitu!” “Nakuomba Farida wangu, sema tu umenisamehe nilale!” “Naona hunielewi...” Farida akasema akionekana kuwa na hasira kidogo. “Haloo..haloo...” Genesis aliita, lakini baadaye akagundua kwamba alikuwa akiongea wakati simu ilishakatwa! Farida alikuwa ameamua kumkatia simu Genesis.

Moyo wake uliumia sana, pale pale kitandani alianza kulia kwa uchungu huku akijaribu kumpigia simu Farida, lakini safari hii haikupatikana kabisa. “Amefikia hatua ya kunizimia simu? Mimi Genesis?” akazidi kuwaza akionekana kuwa na mawazo sana kichwani mwake.

Ilikuwa kazi kubwa sana Genesis kupata usingizi, lakini alilazimika kulazimisha, usiku sana akapitiwa na usingizi mzito. *** Genesis aliamka mapema sana siku hiyo, haikuwa kawaida yake kuamka kabla ya kuchomoza kwa jua, hasa ukizingatiwa hakuwa na mahali pa kwenda.

Baada ya kuoga na kuvaa, akaamua kwenda sebuleni kupata kifungua kinywa. Kichwa chake kiilikuwa na mawazo tele juu ya Farida wake, mwanamke wa maisha yake, ambaye alimpenda kuliko kitu chochote! Akiwa anafungua mlango wa kioo wa kutokea kwenye korido na kukanyaga kwenye ngazi fupi za kuingia sebuleni, akakutana uso kwa uso na baba yake aliyekuwa ameketi kwenye moja ya masofa yaliyokuwa pale sebuleni.

Uso wake ulionesha kabisa alikuwa anamsubiri yeye au alikuwa akijiandaa kwenda kumuasha kwa ajili ya kumuuliza jambo fulani ambalo si jema sana. Baba yake alionekana kukaa kishari kabisa. “Shikamoo baba...,” akasalimia Genesis. “Acha ujinga mwanangu, shikamoo pekee haiwezi kutambulisha heshima iliyopo ndani yako!” “Kwanini umesema hivyo baba.” “Mimi ni baba yako?” “Ndiyo!” “Kwanini hutaki kusikiliza maagizo yangu.”

“Naamini nakusikiliza baba, lakini kama mtoto, kama binadamu wengine, nina madhaifu yangu na huwa nakosea. Naamini mara zote ninapofanya hivyo huwa naomba msamaha baba!” “Hebu nisikilize kwa makini sana.” “Nakusikiliza baba.” “Naomba uachane na yule mtoto wa kiswahili!” baba yake akamwambia kwa kumaanisha. “Nani baba.” “Hujui namzungumzia nani?” “Farida baba?” “Huyo huyo?” “Lakini kuhusu hilo tulishakubaliana baba, kwamba majibu ya mitihani yake ndiyo yataamua.” “Kwahiyo akiwa amefeli hutaendelea naye, siyo?” “Ndiyo baba.”

“Haya mchana mwema,” akasema Profesa Mshana na kuinuka kisha kushika njia ya nje na kwenda nje alipoingia kwenye gari lake na kwenda zake ofisini. Genesis alisimama na kumwangalia baba yake mpaka alipoishia mbele ya macho yake, akajishika kiuno akiwa na mawazo mengi sana kichwani mwake. Hamu ya kunywa chai ikayeyuka ghafla. Akaamua kurudi zake chumbani.

Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kumpigia tena Farida. Jambo hilo pekee ndilo lililokuwa ni faraja yake, hata kama angekuwa katika hali gani, siku zote sauti ya Farida imekuwa ikimpa furaha kwa upya kabisa. Simu iliita mara moja tu na kupokelewa. “Vipi Genesis?” “Poa mambo vipi?” “Salama.” “Vipi afya yako?”

“Namshukuru Mungu kwakweli nipo sawa!” “Mbona asubuhi yote hii?” “Naamini unajua kwanini nimekupigia mapema yote hii.” “Bila shaka Genesis!” “Niambie basi mpenzi wangu.” “Ratiba zako leo zikoje?” “Siwezi kuwa na ratiba yoyote kabla sijaweka mambo yangu na wewe sawa mpenzi, kwanza niambie kuhusu mimi na wewe halafu ratiba nyingine zitafuata.”

“Haya sema tunakutana wapi, saa ngapi?” “Saa sita kamili nakuja kukuchukua nyumbani, halafu twende lunch pamoja, mambo mengine yatajulikana huko!” “Usifike nyumbani tafadhali, utaishia barabarani, mimi nitakufuata.” “Sawa.”

“Ok!” “Nimefurahi sana Farida, naamini mambo yetu yanakwenda sawa sasa!” “Usijali!” *** Saa 6:05 mchana Genesis alikuwa ameegesha gari mbele kidogo ya kituo cha daladala cha Kwa Aziz-Ally, nyuma kidogo ya kituo cha kuuzia mafuta ya magari. Dakika tano kabla hajafika hapo alikuwa ameshaongea na Farida na alimwambia kwamba tayari ameshatoka nyumbani. Akaamua kumpigia.

“Uko wapi?” “Hapa kituoni!” “Sasa njoo mbele kidogo, kama unaelekea sheli.” “Hata hivyo nipo mbele kidogo, lakini sioni gari lako!” “Leo sijatumia gari yangu, nimechukua ya sister, nipo na Prado nyeusi!” “Basi nimeshakuona,” akasema Farida na muda mfupi baadaye alikuwa kwenye mlango wa mbele ya gari la Genesis. Mara moja akamfungulia mlango.

Akaingia na kuketi, Genesis akamwangalia kwa macho yaliyojaa mahaba mazito. Akamsogelea kidogo na kumbusu kwenye shavu lake. Farida alishindwa kuyazuia machozi yake, akaanza kulia. “Nakupenda sana Farida, naomba ukubali kunisamehe!”

“Nimeshakusamehe mpenzi wangu!” “Unasema?” Genesis akauliza kama vile hakusikia jibu la Farida. “Nimeshakusamehe Genesis wangu, lakini usirudie tena, uliniumiza sana mpenzi!” “Huwezi kuamini, pamoja na kwamba mimi ndiye niliyekupiga, lakini mimi pia nilipata maumivu tena makali zaidi yako!”

Safari yao ikaishia katika mgahawa mmoja katikati ya jiji na kupata chakula cha mchana pamoja kwa furaha. Kila kitu kilishapita, Farida alimsamehe kabisa Genesis. Hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kumsamehe, alikuwa mwanaume aliyempenda sana na isingekuwa rahisi moyo wake kumkubali mwanaume mwingine zaidi yake. Akamsamehe kwa moyo wake wote!

***

Mama Genesis alikuwa ametulia ofisini kwake, kichwa chake hakikuwa sawa kabisa, alikuwa akimuwaza mwanaye Genesis. Mtazamo wake kuhusu mwanamke wa kuoa, ulimchanganya sana. Alitamani sana mwanaye akubali kumuoa mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bianca na siyo Farida mtoto wa Fundi Seremala! Hilo lilimuumiza sana kichwa chake. Akiwa kwenye mawazo hayo, mara simu yake ikaita. Alipoangalia kwenye kioo cha simu, akakutana na jina la Bianca.

“Haaah! Bianca ana nini tena? Ngoja nipokee!” akawaza na kubonyeza kitufe cha kupokelea. “Shikamoo mama!” Bianca akasalimia lakini akionekana kuwa na kihoro cha kusema jambo. “Vipi, mbona hivyo, kuna usalama?” “Usalama mama upo...nilitaka kukuambia matokeo yametoka!” “Nini?” “Matokeo yametoka mama.”

“Enhee umepata ngapi?” “Zaidi ya One nitapata nini kingine mama?” “Umeangalia na ya Genesis?” “Ndiyo!” “Ngapi?” “Division One!” “Vipi kuhusu Farida?” “Division Three!” akasema Bianca akicheka. “Safi kabisa!” mama Genesis akasema akiinuka juu na kushangilia. Majibu ya mtihani mgumu kuliko yote kwa Genesis yalikuwa yametoka.

Kwa namna yoyote, isingekuwa rahisi kwa Farida kupata nafasi ya kusoma Chuo Kikuu! Hiyo ilitosha kabisa, kumtenganisha na mwanaye.

Je, nini kitatokea? Genesis atakubali kuachana na Farida?
 
SEHEMU YA 18


ALIYASIKIA maneno yale vizuri sana kutoka katika kinywa cha Bianca, lakini alihisi kama yalipitia pembeni. Genesis alikaa kimya kwa muda akimwangalia Bianca bila kusema neno lolote. Bianca naye hakuonekana kuwa na wasiwasi kabisa. Aliyaamini sana maneno yake, hakuwa na mashaka kwamba amekosea!

Macho ya Genesis yalidhihirisha wazi kuwa ama hajasikia vizuri, hajaelewa vyema au anataka ufafanuzi zaidi. Bianca aliweza kusoma hayo kupitia macho yake. Ni hapo alipofungua kinywa chake na kuanza kuzungumza.
“Genesis!”
“Nakusikia!”
“Mbona umekuwa kimya!”

“Nakushangaa!”
“Unashangaa nini sasa?”
“Umesema unataka kulala na mimi au nimesikia vibaya?”
“Umesikia vizuri sana, ni kweli nataka kulala chumbani kwako.”
“Umechanganyikiwa Bianca?”
“Kwanini?”
“Wewe msichana, mimi mvulana, sasa tutawezaje kulala chumba kimoja?”

“Acha uswahili wako bwana, kwani kuna kipi cha ajabu. Unajua tatizo ni kwamba wewe umepeleka hili jambo mbali sana, umefika sehemu ambayo mimi sijaifikiria kabisa. Uwe na amani Genesis, ni kulala pamoja tu, kama kaka na dada yake, heshima itachukua nafasi yake!” Bianca akasema kwa kujiamini sana.

Maneno yake yalimpa Genesis wakati mgumu sana. Haikuwa rahisi kwake kumuelewa. Katika maisha yake, hakuwahi kulala na mwanamke chumba kimoja, siyo kulala tu, hata kimapenzi! Siku zote alijua watu wa jinsia tofauti wanapolala chumba kimoja, lazima kinachotokea baadaye huwa ni mapenzi. Hakumwamini kabisa Bianca.
“Kwahiyo umesema ni kulala tu?”
“Ndiyo kulala tu...hakuna kingine zaidi.”
“Lakini sijui kwanini moyo wangu hautaki kuamini kirahisi.”

“Kwani wewe unawaza nini?”
“Hata wewe unajua ninachowaza, sina ulazima wa kusema kitu ambacho nina imani unakijua.”
“Basi mimi nakuomba acha kuwaza hayo mambo.”
“Unaniahidi?”
“Nakuahidi Genesis!”
“Ok!”

Genesis akamuomba Bianca amsubiri kwanza aingie bafuni. Bianca akakubaliana naye. Kwake ilikuwa siku ya furaha sana maana alikuwa na uhakika anakwenda kufungua ukurasa mpya wa mapenzi. Kiasi cha robo saa, Genesis alirudi akiwa ameshaoga na kuvaa mavazi ya kulalia.
“Vipi, hatuli?” Bianca akauliza.
“Kwanini?”
“Naona upo tayari kwa kulala.”

“Ni kweli, lakini nilitaka kujiandaa kabisa.”
“Poa, sasa na mimi nataka kuoga!”
“Ingia bafuni hakuna tabu.”
“Ok!”
Bianca akainuka na kuingia chumbani, huko ndipo kulipokuwa na bafu. Akavua nguo zake kisha akavaa taulo na kuingia bafuni. Lilikuwa zoezi lililochukua dakika ishirini nzima, akioga vizuri na kufanya usafi wa kila idara, maana alikuwa na mategemeo makubwa ya kukutana na mwanaume anayeuchanganya mtima wake kwa muda mrefu sana.

“Lazima nitampata,” akawaza Bianca akiwa bafuni.
Alipomaliza kuoga akatoka hadi chumbani, akajikausha na kuvaa nguo zake, akatoka sebuleni alipokuwa amekaa Genesis.

“Naona tayari!” Genesis akasema akitabasamu.
“Ni kweli, lakini sijawa kama wewe bado.”
“Kivipi?”
“Ngoja niende chumbani kwangu nikavae nguo za kulalia.”
“Poa.”

Bianca akatoka na kwenda chumbani kwake, vyumba vitatu tu kutoka chumba cha Genesis. Alijua alichotakiwa kufanya; alivaa gauni jepesi lenye kuonesha kila kitu ndani ya mwili wake, huku ndani akiwa amevaa nguo ya ndani aina ya bikini ambayo ilionekana bila tabu juu ya gauni lake.

Akasogelea kioo kilichokuwa mbele yake na kujiangalia. Akaachia tabasamu la ushindi, akarudi kwenye begi lake na kutoa manukato mazuri yasiyokera puani, akajipulizia, kisha akafunga mlango wake kwa kadi na kutoka nje akipiga hatua za kivivu kwenda kwa Genesis.

Alipoingia tu chumbani kwa Genesis, chumba kizima kilinukia manukato yake. Genesis alipoinua macho akakutana na sura nzuri ya mwanamke mrembo ambaye hajawahi kukutana naye kabisa! Bianca alikuwa mpya, ni kama hawakuwahi kukutana kabla. Katika hali ya kushangaza sana, Genesis alimuona Bianca katika upya kabisa!

Hakutegemea kama Bianca alikuwa mwanamke mrembo wa kiwango kile. Umbo lake lilionekana kama lilivyo; alikuwa na kiuno chembamba kama cha nyigu, hipsi pana ambazo zilimchanganya kabisa Genesis. Makalio ya Bianca yalidhihirisha kwamba ni kweli yeye alikuwa mwanamke.

Kifua chake kizuri kilichobeba matiti madogo kama kifuu cha nazi, nayo yalizidi kumtia wazimu Genesis.
“Mungu wangu, sijategemea kama Bianca ni mzuri kiasi hiki,” akawaza Genesis kichwani mwake.

Bianca alikuwa katika upya kabisa, hata yeye alijishangaa kwa jinsi alivyochanganywa na uzuri wake. Bikini iliyoonekana ndani ya gauni jepesi ilipandisha moto wa mapenzi wa Genesis ambao kwa muda mrefu sana ulikuwa umetulia.

“Yes Genesis,” akatamka Bianca kwa kuremba kidogo, akazidi kumtibua Genesis.

“Karibu...” akajibu Genesis lakini akiona haya sana.
Bianca akakaa kwenye sofa kwa mtindo wa kuangaliana na Genesis. Haikuwa kazi rahisi kwa Genesis kuyatuliza macho yake kwa Bianca muda wote. Alikuwa akiangalia chini kwa kuona haya.

“Hivi Genesis, tutakula saa ngapi? Nadhani tungetumia muda huu kwenda Mgahawani kupata chakula.”
“Hapana, nimeshaweka oda, tutaletewa humu ndani.”
“Umeweka oda?”
“Ndiyo!”

“Sasa wewe unajuaje chakula ninachopenda kula?”
“Najua utakipenda.”
“Ni nini?”
“Wali samaki.”
Bianca akacheka sana.
“Ni kweli, umepatia kabisa, ni aina ya chakula ninachokipenda!”

Muda mfupi baadaye chakula kililetwa, wakaingia mezani pamoja na kuanza kula. Mazungumzo yao yalikuwa juu ya masomo ya chuo, lakini Genesis hakuwepo pale kabisa, umbo la Bianca lilimchanganya kabisa kichwa chake. Alikuwa pale mwili tu, akili yake haikuwa mahali pale kabisa, alikuwa akiwaza uzuri wa Bianca.

Alianza kujishangaa, taratibu moyo wake ulianza kuvutiwa na Bianca, lakini alipojaribu kutafakari kwa kina, alishindwa kupata jibu la moja kwa moja kwamba ni moyo wake ulikuwa unapenda au ni tamaa za mwili wake.

Walipomaliza kula, waliamua kwenda chumbani kulala.
Huko ndipo kulipokuwa na kizaazaa, wote waliingia ndani ya shuka moja, lakini Bianca alimuomba Genesis amkumbatie, jambo ambalo Genesis hakukubaliana nalo kabisa.

“Hapana Bianca, kwani umeshasahau makubaliano yetu?”
“Nakumbuka!”
“Sasa?!”
“Kukumbatiana ndiyo kufanya mapenzi? Acha ushamba bwana.”

Bianca akamzidi Genesis kwa ushawishi, akajikuta anamsogelea na kumkumbatia. Joto kali la Bianca likamchanganya Genesis, hilo Binaca alilijua, akafanya utundu wake wote na muda mfupi baadaye, kwa mara ya kwanza Genesis alijikuta amelala na mwanamke!
Ulikuwa usiku wa ajabu sana kwa Genesis, hakuwahi kufikiria kama mapenzi yalikuwa na raha aliyoisikia kutoka kwa Bianca. Ahadi kedekede akazitoa, akamuahidi kuwa mpenzi wake wa kweli.

“Nakupenda sana Bianca!”
“Nakupenda pia Genesis.”
“Naomba uniahidi kwamba hutaniacha.”
“Sitakuacha mpenzi wangu.”

Usiku kucha mchezo uliendelea kuwa huo, wote walifurahia mapenzi, lakini walikuwa na tofauti moja, Genesis ilikuwa mara yake ya kwanza kukutana na mwanamke, wakati Bianca alikuwa mzoefu. Hata Johnson alipofika asubuhi walitoa hudhuru wakidai kwamba wangeenda kufanya manunuzi siku inayofuata.

Ndivyo ilivyokuwa, siku iliyofuata walikwenda kufanya manunuzi ya mavazi na vitu vingine vya thamani jijini London, muda wote walikuwa wameshikana mikono kama wapenzi wa muda mrefu. Walipumzika Uingereza kwa wiki nzima kabla ya kurejea Tanzania wakiwa wapenzi.

Ndoto ya Bianca ikatimia, alikuwa amempata mwanaume wa maisha yake. Genesis alikuwa mwanaume aliyemchanganya sana, hakutegemea kumtia mikononi mwake, safari ya Uingereza kwake ilikuwa zaidi ya zawadi ya kufanya shopping, ilikuwa safari ya kwenda kufungua ukurasa mpya wa mapenzi na mwanaume aliyemuota siku zote, Genesis!

MOYO wake ulilipuka, akajihisi mkosaji mkubwa, alihisi kitu kingine kipya zaidi ya alivyokuwa akifikiria awali. Ni kweli uzuri wa Bianca ulimchanganya sana. Ni kweli alifikia hatua ya kumuona kwamba anamzidi uzuri Farida, lakini sasa aligundua kitu kingine kipya kabisa.

Bianca hakuwa mzuri kama Farida, ni mavazi yake ndiyo yaliyomchanganya…ndiyo! Mavazi yaliyotibua nyongo ya mapenzi baada ya kumtamani kwa kutazama maungo yake katika nguo ya kulalia aliyokuwa amevaa. Hivyo hakumpenda Bianca, alimtamani tu!

Hapo akagundua kwamba, moyo wake bado unamtaka Farida wake, mwanamke ambaye alimpenda sana. Akagundua kwamba alifanya makosa makubwa sana kumsaliti Farida. Aliendelea kusoma yale maneno katika simu yake na kuzidi kuchanganyikiwa.

“Hapana, nimefanya kosa kubwa sana, sikutakiwa kumsaliti mwenzi wangu. Hapana nimekosea sana, Farida hakupaswa kufanyiwa hivi, nimemkosea mpenzi wangu,” akaendelea kuwaza Genesis.

Akaamua kuendelea kusoma meseji nyingi za Farida, alizidi kuhisi anaungua ndani ya moyo wake, Farida aliandika maneno makali sana katika kila meseji aliyoituma.

“Kumbuka siku ya kwanza macho yetu yalipokutana, unakumbuka nini? Nakupenda sana Genesis, sitaweza kuishi bila wewe, nitajitahidi kutafuta chuo ili wazazi wako waridhike, lakini sipo tayari kabisa kukukosa…wewe ni muhimu sana kwangu!” Meseji moja ilisema.

“Kumbuka kwamba uliniahidi hutanisaliti, tuliahidiana kuoana hata kama kuna ukuta unaotutenganisha, uliahidi kunipenda kama nilivyo. Tafadhali usiniache mpenzi wangu!” Nyingine tena ilisema.

“Naomba ukirudi Dar unitafute, lazima tuzungumze kidogo kuhusu penzi letu, hata kama unataka kuniacha, lakini lazima nizungumze na wewe mpenzi, nakuomba sana urudishe moyo wako nyuma, usiniache tafadhali,” ilisema nyingine.

“Mengi yalitokea tulivyokuwa shule, lakini kwa asilimia kubwa nahisi kama kuna mkono wa mtu, kuna mpango unaoendeshwa kimya kimya, lazima tuchunguze mpenzi wangu tutaujua ukweli!” Hiyo nayo ikawa moja ya meseji hizo.

Zilikuwa meseji zilizomchoma sana, maneno yake yalikuwa makali yaliyozidi kuutibua kabisa moyo wake. Hakutaka kufanya kitu chochote usiku huo, alihisi kama hana cha kufanya zaidi ya kulala. Akaweka simu yake pembeni na kujitupa kitandani.

Akiwa kitandani, akasikia simu yake ikiita, akainuka na kwenda kuangalia kwenye kioo cha simu, alikuwa Farida ndiye anampigia. Moyo wake ukalipuka, lakini hakuwa na kitu kilichomzuia kupokea.

“Farida…” ndiyo neno la kwanza kutamka Genesis baada ya kupokea simu.
“Genesis!”
“Vipi?”
“Salama.”
“Pole na safari, umeingia leo?”
“Ndiyo!”
“Saa ngapi?”
“Usiku huu, lakini nilipelekwa The Atriums Hotel, wazee walikuwa wameniandalia party!”
“Hongera.”
“Ahsante sana.”

“Umesoma meseji zangu, maana naona ndiyo zinanirudishia delivery report kwamba umesoma.”
“Nimezisoma!”
“Bado una msimamo ule ule mpenzi wangu?”
“Msimamo gani?”
“Wa kuniacha?”

“Naomba tuongelee hilo kesho, leo niache nipumzike kwanza, nimechoka sana, lakini unatakiwa kufahamu kwamba meseji zako zimenichoma sana. Nipe muda nifikirie zaidi.”
“Sawa, kwa hiyo kesho tutaonana?”
“Nadhani hivyo, acha usiku uche kwanza, nitakupigia.”
“Sawa.”

Genesis akakata simu na kuizima kabisa, akaiweka mezani na kuishilia usingizini.
***
Kwenye meza ya chakula, walikuwa wamekaa watu watatu tu; Genesis na wazazi wake wakiwa wanakunywa chai asubuhi hiyo. Wote walikuwa na furaha sana, hasa Profesa Mshana ambaye alikuwa anatabasamu muda wote.
“Genesis!” Profesa Mshana akaita.
“Daddy!”

“Naamini ume-enjoy!”
“Ndiyo baba, nawashukuru sana wazazi wangu!”
“Usijali baba, sisi tupo kwa ajili yako, unapofanya vizuri inakuwa ni jukumu letu sisi kukupongeza kwa namna mbalimbali ikiwemo kukutoa nje ya nchi kwa mapumziko, umetufurahisha sana. Naamini unakwenda kufanya degree yako ukiwa mpya kabisa.”
“Ni kweli baba!”

“Hongera kwa mara nyingine, maana nimepata taarifa za kufurahisha sana kutoka kwa mama yako!”
“Taarifa?!” Genesis akatamka kwa mashangao kidogo.
“Ndiyo, mama yako kuna kitu ameniambia, nimefurahishwa sana na uamuzi wako, huo ndiyo uanaume.”
“Nini tena baba?”

“Ni kuhusu Bianca!”
Genesis akashituka sana, akahisi kuchanganyikiwa, tayari kichwani mwake alikuwa na maamuzi mengine, hakuwa na mawazo tena kuhusu Bianca, alishajua kwamba alifanya makosa na sasa akili yake ilikuwa kwa Farida.
“Vipi, mbona kama umepoteza furaha?” Baba yake akamwuliza.

“Ni kweli jana nilizungumza na mama lakini…” Genesis akasema.
“Lakini nini tena?”
“Nimebadilisha mawazo.”

“Yamekuwaje?”
“Baba nimeshindwa kuacha kumpenda Farida, nitakuwa kwenye uhusiano wa utumwa, nataka kumuoa Farida.”

“Hebu acha ujinga wewe mtoto, hivi huyo Farida amekuwekea nini? Kwa nini unachanganyikiwa sana juu yake? Sasa sisi kama wazazi wako, hatutaki kusikia habari za Farida. Hata kama humtaki tena Bianca, lakini hatutaki kusikia habari za Farida hapa nyumbani.

Nimemaliza…” akasema Profesa Mshana kwa hasira.
Muda huo huo wazazi wake wote wakasimama na kumuacha akiwa amekaa peke yake. Hakupoteza muda, akasimama na kwenda zake chumbani kwake, akachukua simu yake na kumpigia Bianca.

“Bianca naomba unisikilize kwa makini sana!”
“Nakusikiliza mpenzi wangu.”
“We! We! We! Tena acha kuniita mpenzi wako!”
“Kuna nini tena?”

“Hesabu kwamba kilichotokea Uingereza ilikuwa ni bahati mbaya tu. Hatuwezi kuwa wapenzi, naomba futa fikra hizo kabisa!”
“Kwanini umesema hivyo?”
“Moyo wangu umeamua, sitaki maswali zaidi.”
Alipomaliza kusema maneno hayo, akakata simu na muda huo huo akabonyeza namba za Farida. Muda mfupi baadaye alikuwa akiongea naye.

“Farida uko wapi?”
“Nyumbani!”
“Naomba ujiandae, baada ya nusu saa nitakuwa hapo, nakuja kukuchukua!”
“Kwani wewe uko wapi?”
“Nyumbani, ndiyo najiandaa kutoka!”
“Sawa dear, acha nijiandae haraka. Ahsante sana mpenzi wangu!”

“Ok!”
Farida hakuamini kabisa kilichotokea, hakutegemea kama ingekuwa rahisi Genesis akubali kukutana naye tena. Alikuwa na matumaini makubwa kwamba Genesis alikuwa amebadilisha mawazo, jambo ambalo siku zote alikuwa akiomba litokee.

Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 19


Pamoja na Genesis kukubali kufungua ukurasa mpya wa mapenzi na Bianca wakiwa Uingereza, meseji za Farida alizozisoma kwenye simu yake mara baada ya kurejea nchini, zimemchoma na kumfanya kubadili uamuzi wake.

Akiwa kwenye meza ya chakula na wazazi wake, baba yake anamuuliza kuhusu mpango wake na Bianca, Genesis anakataa kabisa, anasema kwamba hawezi kuishi bila Farida wake. Jambo hilo linawaudhi sana wazazi wake ambao wanatoa maneno makali na kuondoka sebuleni.

Muda huo huo, Genesis anakwenda chumbani na kumpigia simu Bianca na kumweleza kwamba amebadilisha uamuzi wake wa kuwa naye na anamuonya kwamba asimuite tena jina la mpenzi.

Baada ya zoezi hilo kinachofuata ni Genesis kumpigia simu Farida na kumueleza kwamba anataka kukutana naye. Farida haamini masikio yake, haraka anaanza kufanya maandalizi ya kukutana na mpenzi wake Genesis!
Je, nini kitatokea katika mvutano huu? SONGA NAYO...

HAKUWA na muda wa kupoteza, alichokifanya Genesis kilikuwa ni kufungua kabati la nguo kisha akatoa nguo alizoona zinafaa na kuvaa. Hakuwa na muda wa kusogelea meza ya kujipodoa, aliinuka na kutoka nje moja kwa moja kisha akaingia ndani ya gari lake na kuanza kuondoka nalo.

Mlinzi alifanya kazi yake ipasavyo, mara moja alifungua geti na Genesis akaliondoa gari kwa kasi sana. Aliposhika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, alikata kulia na kunyoosha moja kwa moja hadi kwenye mataa ya Morocco, ambapo alisubiri taa zimruhusu kabla ya kuondoka akiifuata barabara hiyo inayoelekea Bagamoyo.

Magari hayakuwa mengi sana, hivyo aliweza kuendesha vizuri sana, dakika tatu baadaye alikuwa kwenye mataa ya Bamaga, ingawa taa zilimtaka asimame, kwakuwa hapakuwa na magari akaamua kuunganisha hadi alipofika kwenye taa nyingine za Mwenge, ambapo hapo alikata kushoto akaishika Barabara ya Sam Nujoma.

Safari yake iliishia katika eneo la Mlimani City, aliposimama getini na kuchukua kadi kwa askari wa getini kabla ya kuingia na kutafuta sehemu nzuri ya kuegesha.

Alishuka haraka, kisha kwa mwendo wa kijeshi aliingia ndani na kaunza kuzunguka kwenye maduka ya nguo. Hakuchukua muda mrefu kuchagu nguo zilizomfaa mpenzi wake Farida, akanunua manukato na nguo. Akaenda mapokezi kulipa.

“Samahani dada,” Genesis akatamka akilipa pesa Mapokezi.
“Ndiyo!”
“Kuna kitu kimoja cha kukamilisha mzigo wangu!”
“Ni nini?”
“Kadi, sijui kama mnazo?”

“Hapana...”
“Naweza kupata wapi maeneo haya?”
“Ipo Stationery hapo nje, duka la nne kutokea hapa kwetu, wana kadi nzuri sana!”
“Ahsante dada, lazima nichukue na kadi!”

“Hongera mwaya, inaonekana unajua sana kupenda, sisi wengine tumekutana na wanaume weanaojijali wao wenyewe. Hongera yake huyo mpenzi wako!”
Genesis hakujibu kitu, aliishia kutabasamu na kuondoka zake. Akaingia kwenye duka la kadi, lakini akasimama kwenye sehemu ya kufanyia malipo, alipokuwa amekaa dada mmoja mrembo sana.

“Habari dada!”
“Salama.”
“Nahitaji kadi!”
“Umepata, nenda kule ukachague kisha uje nayo hapa nikupe bei!”

“Dada nina haraka sana, naomba unichagulie kadi nzuri sana kwa ajili ya mpenzi wangu, najua wewe unazijua vizuri kuliko mimi mteja wako, naomba unisaidie kwa hilo!”
“Sawa, hakuna shida, unataka ya nini?”
“Ya kuomba msamaha!”

Yule dada akamwangalia Genesis kuanzia juu hadi chini, alionekana kuwa na uso wenye simanzi, lakini aishangazwa na jinsi kijana huyo alivyokuwa akihangaikia penzi lake, wanaume wengi si watu wa kuhangaikia sana mapenzi hata kama wao ndiyo wakosaji.

“Vipi?”
“Nakwenda kukuletea usijali!”
“Naona umeniangalia sana.”
“Ni kweli, lakini ninachotaka kukuambia kaka yangu, endelea na moyo hup huo. Ni vizuri kuwa na usawa katika kutafuta amani ya wapenzi wetu. Wanaume ni wazito sana kwa hilo, wewe ni mfano mzuri kwa wengine!”
“Mh!” Genesis akaguna.

“Kwanini unaguna?”
“Nakushangaa tu, nahisi kila mmoja ana haki ya kupenda na kulinda penzi lake, ndicho ninachokifanya hapa.”
“Sawa, unahitaji ya bei gani?”
“Iwe kadi nzuri, bei si tatizo.”

“Ok!”
Yule dada akainuka na kuanza kupiga hatua za kivivu kwenda kutafuta kadi. Hakuchukua muda mrefu sana alifika akiwa na kadi kubwa mkononi mwake.
“Hii ni nzuri sana, bila shaka itamfaa, ina maneno mazuri sana!”
“Kiasi gani?”

“Elfu ishirini tu!”
“Usijali!” Akasema Genesis na kutoa pochi yake mfukoni kisha akamlipa.
Akachukua kadi yake na kuondoka zake hadi nje, akawasha gari na kuliondoa taratibu, getini alirudisha kadi ya kuingilia ndani kisha akavuka hadi upande wa pili, akaifuata barabara ya kuelekea Ubungo.

Kwenye mataa ya Ubungo aliendelea kunyoosha akiifuata Barabara ya Mandela, aliendesha gari hadi Tazara alinyosha moja kwa moja hadi Temeke na baadaye kurudi katika Barabara ya Kilwa, muda mfupi baadaye alikuwa ameegesha gari lake mbele kidogo ya kituo cha daladala cha Kwa-Aziz Ali. Akatoa simu yake na kumpigia Farida.

“Nimeshafika mama.”
“Hata mimi pia, mbona sikuoni?”
“Umesimama kwa wapi?”
“Hapa kituoni.”

“Mh! Jamani Farida, sasa unadhani nitaingia kituoni kwani hii ni daladala? Njoo mbele kidogo ya kituo, nipo nyuma ya sheli karibu na keep left hapa!”
“Ok! Naja.”

Kupitia kioo cha pembeni cha gari lake, Genesis aliweza kumuona Farida akitembea kwa madaha kumfuata alipokuwa ameegesha gari. Alipofika, alifungua mlango wa upande wa abiria, akaingia.

Genesis akashindwa kuzuia hisia zake, akamsogelea na kumbusu mashavuni mwake, hiyo haikutosha, akautoa ulimi wake kisha akautumbukiza kinywani mwa Farida, naye akaupokea, kisha zoezi la kubadilishana mate likachukua nafasi. Ni Farida ndiye aliyemtoa Genesis dakika mbili baadaye.

“Inatosha dear, si mahali pake!”
Genesis hakujibu kitu, alitingisha kichwa kuashiria kwamba amekubaliana na mawazo yake, akawasha gari na kuondoka taratibu eneo la Kwa-Aziz Ali.

***
Gari liliingia taratibu kwenye geti lililokuwa na bango lenye maandishi makubwa Chadibwa Beach Hotel, iliyopo Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Genesis aliendesha taratibu hadi kwenye maegesho.

Akashuka na kuzunguka upande wa pili, alipomfungulia mlango Farida naye akashuka.Kilichofuata ilikuwa kwenda kaunta, wakachukua vinywaji na kushikana mikono kuelekea ufukweni. Upepo mzuri ulikuwa ukivuma kwa kasi ukitokea baharini kuelekea nchi kavu. Walikuwa na furaha sana!

“Farida sina cha kusema, lakini kubwa zaidi ni kwamba nataka kukuambia kwamba, tusahau yote yaliyopita tugange yajayo. Mimi nakupenda sana, hayo mengine tuyaache yapite kama yalivyo, sisi tuangalie penzi letu!” Genesis akasema kwa hisia kali sana za mapenzi.

“Ahsante mpenzi wangu, nimefurahi sana kusikia hivyo, nakupenda sana. Ilikuwa vigumu sana kuishi bila wewe. Bila kukupenda, bila kupendwa na wewe. Bila sisi kupendana. Maisha yalikuwa machungu sana, ingawa ni kwa muda mfupi sana!”

“Naomba unisamehe mpenzi wangu!”
“Nimeshakusamehe!”
Wakakumbatiana kwa furaha. Genesis alikuwa na furaha sana. Alikuwa yupo na mwanamke ambaye siku zote moyo wake ulimsisitiza kwamba ndiye chaguo lake. Hakutaka kusikia habari za mwanamke mwingine yeyote zaidi yake. Penzi lake lilikuwa kwa Farida pekee.

Wakiwa wameng’ang’aniana kwa nguvu, simu ya Genesis ikaita. Wakaachiana na kuangalia aliyekuwa akimpigia, alikuwa ni baba yake, Profesa Mshana.
“Upo wapi?” Ndiyo swali la kwanza Profesa Mshana kuuliza baada ya Genesis kupokea simu.

“Kigamboni.”
“Kigamboni?”
“Ndiyo baba.”
“Nakuhitaji nyumbani sasa hivi.”
“Hapana baba,labda baadaye kidogo, nipe angalau masaa matatu kutokea sasa.”

“Kitu gani cha muhimu unachokifanya huko hadi unipe masaa matatu?”
“Baba kuna mtu nazungumza naye, naomba unikubalie baba yangu!”
“Ni nani muhimu kiasi hicho?”

“Lazima niwe mkweli baba, nipo na Farida huku beach, halafu ndiyo kwanza tumeingia ndiyo maana nakuambia ni vigumu kuja nyumbani sasa hivi!”
“Unasemaje Genesis?”
“Nipo na Farida!”

“Hivi umefikia hatua ya kunidharau kiasi hicho? Sasa kama mimi ni baba yako, nasema njoo nyumbani sasa hivi...” akasema kwa hasira Profesa Mshana na kukata simu.

Genesis akabaki ameduwaa, mawazo tele kichwani, akiwa hana la kufanya. Aende nyumbani au abaki na Farida? Hilo liliendelea kuwa swali lisilo na jibu lililousumbua sana ubongo wake.

“UKO nyumbani?” Ndiyo neno la kwanza kuongea mama Bianca baada ya mama Genesis kupokea simu yake.
“Vipi mwenzangu, hata salamu?”
“Nasema hivi, upo nyumbani?”
“Nipo, bado sijatoka!”
“Na mzee?”
“Ametoka!”
“Si neno sana, nakuja hapo sasa hivi, naomba unisubiri!”
“Kuna nini?”
“Mama Genesis nisubiri, tutakuja kuongea vizuri nikija hapo!”
“Sawa!”
Mama Bianca alikuwa amevimba kwa hasira, aliumizwa sana na jinsi mwanaye alivyokuwa akilia, ni siku moja tu baada ya kutoka Uingereza ambapo tayari Genesis alishasema kwamba amekubali kuwa na Bianca na hana mpango tena na Farida.
“Nyamaza mwanangu, jiandae tuondoke!” Mama Bianca akamwambia mwanaye ambaye bado alizidi kulia.
“Mama lakini mimi nampenda sana!”
“Najua mwanangu, ndiyo maana nataka kukusaidia. Kila kitu kitakuwa sawa mama, hutakiwi kuwa na presha!”
“Lakini amenipigia yeye mwenyewe na kusema kwamba kilichotokea Uingereza ni bahati mbaya na hana mpango na mimi!”
“Lakini mimi si ni mama yako?”
“Ndiyo mama!”
“Basi nitajua cha kufanya, nenda kajiandae!”
Bianca akaingia bafuni kuoga kisha akavaa na kutoka sebuleni alipomkuta mama yake akiwa tayari ameshajiandaa. Maneno ya Genesis yalimchoma sana moyo wake, hakuwa tayari kuwa na mwanaume mwingine yeyote zaidi yake, moyo wake ulimuuma sana, alimpenda sana Genesis na hakutaka kujiingiza katika uhusiano na mtu mwingine yeyote.
Tayari furaha aliyokuwa akiisaka kwa muda mrefu sana ilikuwa ipo moyoni mwake, lakini kitendo cha Genesis kukataa ghafla kuendelea naye, kwake ilikuwa maumivu makali sana. Ni yeye ndiye asliyesababisha Farida afeli ili aweze kuwa naye, iweje leo hii amkatae? Aliumia sana moyoni mwake.
“Nipo tayari mama!”
“Naona mwanangu, tangulia kwenye gari nakuja!”
“Sawa!” Akajibu Bianca akianza kuchanganya miguu kutoka nje.
Akaingia kwenye gari kama alivyoagizwa na mama yake, muda mfupi baadaye mama yake akatokea, akaingia kwenye gari na kuwasha, safari ya kwenda Masaki nyumbani kwa akina Genesis ikaanza.
***
Alipiga honi mara moja tu, mlinzi alikuwa ameshafungua mlango, akaendesha taratibu hadi sehemu ya maegesho, akaegesha na kushuka, Bianca naye akashuka. Wakaongozana kwenda hadi ndani, walipomkuta mama Genesis akiwa ametulia sebuleni.
Macho ya Bianca yalipogongana na ya mama Genesis akajikuta amepata msisimko wa ajabu na kuanza kulia.
“Kwanini unalia Bianca? Hebu tulia mwanangu! Kaa hapo,” akasema mama Genesis kwa huruma.
Tayari alishajua kilichowaleta, ni Genesis tu ndiyo sababu ya wao kufika nyumbani kwake asubuhi hiyo tena Bianca akiwa anamwaga machozi.
“Vipi mwezangu, za utokapo?”
“Mbaya!”
“Kuna nini tena mwenzangu?”
“Kama unavyoona, mwanangu amekuwa wa kulia tena!”
“Mama kuna nini eti?”
“Genesis!” Bianca akasema kwa sauti ya kukatakata akizidi kulia.
Mama Genesis akabaki kimya kwa muda kama aliyemwagiwa maji ya baridi. Akamwangalia mama Bianca kisha mwanaye na kuonekana kuwa na uchungu sana moyoni mwake. Hata yeye alikuwa akitamani sana mwanaye amuoe Bianca. Hakutaka kumsikia kabisa Farida.
“Kuna kitu nataka kufanya, lakini lazima Profesa Mshana awepo!”
“Ni nini?”
“Nataka Genesis aje hapa, kwasasa hayupo, lakini kwanza nataka kumpigia baba yake aje!”
“Sawa, lakini kikubwa ni kupata msimamo, mwanangu asihangaike!”
“Sawa, nisubirini kidogo!” Akasema mama Genesis akiingia chumbani.
Huko alienda kumpigia mume wake na kumweleza kuhusu ugeni uliofika nyumbani asubuhi hiyo. Profesa Mshana alihuzunika sana.
“Mtoto wa watu analia, anaonekana kabisa amempenda sana Genesis, lakini ndiyo hivyo huyu mtoto anataka kutuangusha!”
“Yupo hapo nyumbani?”
“Nani?”
“Genesis!”
“Hayupo.”
“Sasa umeshajaribu kumpigia simu?”
“Hapana, lakini nilitamani sana zoezi hilo lifanyike mbele yako!”
“Siyo mbele yangu, mimi ndiye nitakayempigia mwenyewe. Nipe nusu saa nitakuwa hapo nyumbani!”
“Sawa dear!”
“Ok!”
Wakakata simu zao. Mama Genesis akapitia jikoni alipochukua bilauri kubwa lililojaa maji ya matunda kisha akatoka na glasi tatu hadi sebuleni, akamimina na kuwakaribisha, naye akachukua glasi yake na kisha akaketi kwenye moja ya masofa pale sebuleni.
“Karibuni sana...nimeshaongea na Profesa, kasema anakuja!”
“Ok!” Mama Bianca akajibu.
Kiasi cha dakika arobaini hivi, Profesa Mshana alikuwa anaingia nyumbani kwake. Mara moja akaegesha gari lake kisha akashuka na kuanza kutembea haraka hadi sebuleni.
“Habari yako shemeji?”
“Nzuri tu, shem za hapa?”
“Salama kabisa!”
“Shikamoo baba!” Bianca akasalimia.
“Marahaba binti yangu, vipi hali yako?”
“Salama baba!”
“Si salama!”
“Kwanini?”
“Salamu nilizozipata inaonekana kabisa si salama, lakini nitahakikisha habari inakuwa salama. Acha nimpigie Genesis aje hapa sasa hivi!” Akasema Profesa Mshana akitoa simu yake kisha akabonyeza namba za Genesis na kuweka simu sikioni.
Ni hapo ndipo Genesis aliposema kwamba hawezi kufika nyumbani kwakuwa alikuwa mbali na alikuwa akizungumza na mtu mambo muhimu. Baba yake alipombana zaidi akamweleza ukweli kwamba yupo na Farida.
Profesa Mshana akafura kwa hasira na kumtaka afike nyumbani haraka sana. Alikata simu akiwa amechukia sana.
“Vipi?” Mkewe akamwuliza.
“Eti ana mazungumzo muhimu!”
“Na nani?”
“Farida!”
“Pumbavu kabisa huyu mtoto, anaweza kukujibu upumbavu kama huo, amepata wapi huo ujasiri wa kujibu utumbo kiasi hicho! Ngoja nimpigie na mimi!” Akasema mama Genesis akipiga simu yake.
“Shikamoo mama!” Sauti ya Genesis ikasikika kutoka upande wa pili.
“Sitaki shikamoo yako...sikiliza maagizo yangu, kama wewe ni mwanangu, ambaye umelala miezi tisa tumboni mwangu, naomba uje nyumbani sasa hivi!” Akasema mama Genesis kisha akakata simu.
Hakutaka kusikia kauli ya Genesis, alikuwa amekasirika kuliko kawaida. Kwao ilikuwa kukataa kuwa na Bianca ni aibu kubwa sana kwao.
“Lazima atakuja, hakuna namna!”
“Ngoja tuone!”
Msimamo wa wazazi wa Genesis uliwafurahisha sana Bianca na mama yake, walianza kuona mwelekeo mzuri wa uhusiano huo kuendelea kuwa hai.
***
Genesis alionekana kupoteza furaha ghafla baada ya kumaliza kuzungumza na simu mbili pale ufukweni. Farida alihisi kuna tatizo lililomtokea mpenzi wake. Kama mpenzi wake, alitakiwa kujua ni tatizo gani ili kama kuna uwezekano aweze kumsaidia mawazo.
“Vipi, mbona kama huna raha? Mama amesemaje?”
“Simu ya kwanza ilikuwa ya baba, amefuata na mama tena, wote wanakuwa wakali kwangu!”
“Kuhusu nini?”
“Wanasema niende nyumbani haraka!”
“Kuna nini?”
“Sijui, lakini wanasisitiza niende haraka!”
“Kama wanasema hivyo mpenzi wangu inabidi uende, kwani wale ni wazazi wako, hutakiwi kukaidi maagizo yao!”
“Sawa!”
Wakaenda hadi kwenye gari, Genesis akampa Farida zawadi zake, nguo na ile kadi. Farida akafurahi sana, akamkumbatia kwa furaha.
“Ahsante sana mpenzi wangu!”
“Usijali mpenzi wangu, nakupenda sana, siwezi kuishi bila wewe!”
“Hata mimi pia!”
“Kuna jambo nataka nikuombe!”
“Nini?”
“Naomba tukifika Feri, nikuache pale nitakupa pesa ya teksi ili niwawahi wazee nyumbani!”
“Hakuna shida.”
Genesis akawasha gari na kuliondoka kwa kasi, muda mfupi baadaye walikuwa kwenye foleni ya magari ya kuingia kwenye kivuko. Zamu ilipofika wakaingia, kama walivyokubaliana, ng’ambo Farida alishuka na kuchukua teksi, Genesis akaendelea na safari yake hadi nyumbani kwao Masaki.
Alipoingia sebuleni, macho yake yalikutana na mama yake akiwa amekunja uso kwa hasira, baba yake naye akimwangalia kwa uchungu, mama Bianca na Bianca mwenyewe! Picha nzima ya kilichokuwa kikiendelea ikamjia.
Alitakiwa kuwa na jibu moja, ingawa moyo wake tayari alishampa Farida, lakini shinikizo la wazazi wake lilimchanganya sana kichwa chake.
“Njoo huku...” Profesa Mshana akasema akionekana kukasirika sana, akasimama na kuelekea kwenye mlango wa kioo wa kuingia kwenye korido.
Genesis akamfuata, kwa mbali akasikia kama vishindo vya mtu akitembelea nyuma yake, alipogeuza shingo, akakutana na macho makali ya mama yake, naye alikuwa anawafuata. Jasho jembamba likaanza kumchuruzika mgongoni!
“Leo kazi ipo!” Akawaza akifungua mlango wa kuelekea kwenye korido.
Je, nini kitatokea? Genesis ataendelea kuwa na msimamo wake au atawasikiliza wazazi wake?
 
SEHEMU YA 20


baye anamwambia kwamba anamuhitaji nyumbani haraka sana, alipofika anashangaa kuwakuta Bianca na mama yake wakiwa sebuleni. Baba yake anamwita ndani, anasimama na kumfuata.

Akiwa anatembelea kuelekea ndani, anasikia vishindo nyuma yake, alipogeuza shingo yake kuangalia, anamuona mama yake naye akimfuata kwa nyuma!
Genesis anashtuka sana, anaamini kabisa kwamba siku hiyo kulikuwa na kazi kubwa sana na wazazi wake. Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

BIANCA akamuangalia mama yake ambaye alikuwa kimya akiwaangalia Genesis na mama yake wakiishia ndani. Ulikuwa mwanzo wa matumaini ya mwanaye kumpata Genesis tena. Alitamani sana mwanaye aolewe na Genesis. Sababu kubwa hapo ilikuwa ni familia.

Hawakupenda kabisa mtoto wao aharibiwe na watoto wengine ambao wanatoka katika familia duni. Kwao, kigezo cha kwanza kabisa cha mwenzi bora kilikuwa ni familia anayotoka. Kama akiwa anatoka familia ya kimasikini, ambayo majina ya wazazi wake hayaanzi na Dokta, Profesa, Mheshimiwa n.k hakuwa na thamani kabisa.

Mama Bianca akaachia tabasamu, kuoenesha kwamba tayari matumaini mapya yalikuwa yameshaanza kuonekana kwa binti yake.
“Vipi mama, mbona unatabasamu?”
“Nimefurahi mama!”
“Na nini?”

“Huoni kwamba wazazi wake wanaonekana wana msimamo sana?”
“Kwani hiyo inasaidia nini mama, kama mtu mwenyewe hanipendi?”
“Hapana...wazazi wana nguvu zao kama wazazi mwanangu. Wana uwezo wa kufanya chochote Genesis akakukubali, kwanza wao, halafu Genesis baadaye. Halafu usijali mwanangu, nitakufundisha namna ya kumshika vizuri akatulia na wewe.

“Wanaume nawajua mwanangu, hawanipi tabu. Sema huyo Farida unayemsema, anaonekana anajua sana mambo ya mapenzi, ndiyo maana Genesis hataki kubanduka kwake. Si unajua tena watoto wa uswahilini? Lakini hiyo haisaidii kitu, nitakufundisha cha kufanya mwanangu, wala usiwe na wasiwasi!”

“Sawa mama, nitafurahi sana!”
“Anza kufurahi mwanangu!”
Waliendelea kuzungumza pale sebuleni kwa zaidi ya dakika kumi na tano.

Baadaye kupitia mlango ule ule walioingilia, waliwaona wakitoka mmoja baada ya mwingine, lakini sura zao zikiwa tofauti kabisa na walivyoingia.
Alianza kutoka Profesa Mshana akitabasamu, baadaye akafutia mkewe ambaye sura yake ilikuwa imepambwa na shangwe kabla ya Genesis kumalizika, naye akionekana kuwa na furaha.

Kila mmoja akatafuta sehemu yake ya kuketi na kukaa. Bianca na mama yake hawakuelewa kilichotokea ndani, lakini ghafla mama Genesis, alisimama na kumuonesha ishara Bianca asimame. Akasimama.

Bianca aliposimama, akamgeukia Genesis na kumuonesha ishara ile ile, kwamba asimame. Genesis naye akasimama. Mama Bianca na mwanaye wakabaki wanashangaa wakiwa hawajui kilichotaka kutokea.
Uso wa Genesis ulikuwa umepambwa na tabasamu muda wote, pamoja na Profesa Mshana ambaye aliyaacha meno yake nje kwa furaha alipokuwa akishuhudia tendo lile.

“Mwanangu, tunaamini kwamba umetusikiliza kwa makini sana sisi wazazi wako na utafuata maagizo yetu. Kumbuka kwamba, hakuna anayekulazimisha wewe kufanya kitu ambacho hukipendi, isipokuwa sisi kama wazazi wako, tunazingatia zaidi maisha yako ya baadaye, ambayo tunatamani sana kuyaona yakiwa mazuri.

“Kama tulivyozungumza ndani, ubora wa maisha yako utakuwa kwa Bianca. Yeye ndiye atakuwa taa yako. Mwongozo wako, kwakuwa wote mtakuwa wasomi na mliozaliwa na wazazi wasomi. Kwenda katika familia fukara, wasiosoma ni kuunganisha ukoo wetu na laana ya maisha ya kifukara.

“Ni imani yetu kwamba utakuwa umeelewa na utashika maagizo yetu. Sasa tunakuomba uoneshe kile kilichopo moyoni mwako. Fanya hivyo kwa uhuru, maana tunaoshuhudia ni wazazi wako!” Akasema mama Genesis akitabasamu.
Genesis akatulia kwa muda, kisha akapiga hatua za taratibu kabisa hadi alipokuwa amesimama Bianca. Akamsogelea zaidi na kumvuta kifuani mwake. Akamkumbatia.

“Nakupenda sana Bianca. Kuanzia sasa nimejiachia kwako kikamilifu. Ni kweli nilikuwa nampenda sana Farida, lakini wazazi wangu wamenipa sababu za msingi za kwanini niachane naye na niwe na wewe.

“Najua nimekukosea, nachukua nafasi hii mbele ya wazazi wetu, kukuomba msamaha wa dhati kutoka ndani ya moyo wangu na ahadi yangu kwako ikiwa ni kutokusaliti wala kukuumiza tena. Nakupenda sana Bianca!” Akasema Genesis machozi yakimtoka machoni mwake.

“Nakupenda pia Genesis. Nimekusamehe kwa kila kitu. Tafadhali usinitese tena. Nipe moyo wako tafadhali!”
“Nimekupa mama!”
Wazazi wakaondoka mmoja baada ya mwingine na kuwaacha peke yao sebuleni. Walipoachiana, walishangaa kujikuta wakiwa peke yao sebuleni.
“Vipi?” Bianca akamuuliza Genesis.

“Sijui vipi, naona wameamua kuondoka!”
“Wameenda wapi na kwanini watuache?”
“Huenda hawakutaka kusikia yale maneno!”

“Safi sana, karibuni kwenye ukumbi wa vinywaji!” Sauti ya mama yake Genesis ikasikika ghafla akitokea kwenye korido pale sebuleni.
Genesis akamshika mkono Bianca na kuongozana naye hadi kwenye ukumbi wa vinywaji ndani ya nyumba hiyo ya kifahari. Kilichofuata hapo ilikuwa kunywa na baadaye kula. Ilikuwa sherehe kubwa sana kwa familia hizo.

***
Farida aliingia nyumbani kwao akiwa na furaha sana, ilikuwa mshangao mkubwa kwa mama yake, maana karibu wiki mbili hakuwa katika hali ya kawaida. Kwanza alichota maji na kuhakikisha yamejaa kwenye vyombo vyote.

Akaanza kumsaidia mama yake kuandaa chakula kwa ajili ya kwenda kijiweni kuuza jioni. Mama yake alizidi kushangaa hasa kutokana na uso wake kuwa wenye tabasamu karibu muda wote tangu alipofika nyumbani.
“Vipi mwenzetu, mbona uchangamfu wako umerudi ghafla?” Mama yake akamuuliza.

“Mama naye? Kwani nilikuwa nimenuna?”
“Haukuwa sawa kwa karibu wiki mbili nzima, mbaya zaidi nikikuuliza unasema ni masomo. Lakini mimi kama mtu mzima nilijua kuna tatizo lingine ambalo hukutaka kulisema, haya vipi...limeisha?”

“ Jamani mama...haya inaonekana unataka sana kujua?!”
“Sana, nisipotaka kujua mimi mama yako, nani sasa ajue?”
“Mama ni Genesis!” Akasema Farida kwa sauti ya chini.

“Amefanyaje tena? Nimeshakuambia uachane na yule kijana. Si saizi yetu, tena mtu ambaye anayemtaka ni rafiki na familia yao.
Wamesoma, wana uwezo tena umesema baba yake ni mwanasheria, tutawezaje kupambana nao mwanangu? Hebu naomba usinitafutie balaa bure...sitaki kabisa kusikia mambo ya huyo mtoto!”

“Mama nimeshazungumza naye, tena leo hii. Na ni yeye ndiye aliyenitafuta, amenipa msimamo wake na amesema atakuwa tayari kuwa na mimi hata kama sijafanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu!”
“Una uhakika?”

“Ndiyo!”
“Hebu mpigie simu, tena nataka kuzungumza naye mwenyewe nisikie anasemaje?”
“Sawa mama, kazi rahisi sana hiyo!”

Farida akatoa simu yake kisha akabonyeza namba za Genesis. Simu ikaanza kuita kwa muda mrefu sana, lakini haikupokelewa. Akajaribu tena, bado haikupokelewa. Farida aliendelea kupiga zaidi ya mara sita, lakini simu yake haikupokelewa.

Mama yake aliyekuwa amesimama mbele yake, alibaki anamkodolea macho kwa mshangao.
“Vipi, hapatikani?”
“Anapatikana!”
“Sasa?!”

“Hapokei!”
“Nilikwambia nini....? nilikuambia nini Farida....!”
“Ngoja mama, labda atapokea...” Farida akasema akijaribu kumpigia tena.
“Amepokea...” hatimaye Farida akasema kwa sauti ya chini, kisha akaanza kuongea.

“Vipi Genesis mpenzi wangu?!”
“Samahani Farida, siwezi tena kuwa na wewe, sitaki maswali katika hili. Ni maamuzi yangu binafsi ambayo hayawezi kubadilishwa na mtu yeyote!”
“Kuna nini tena mpenzi?”

“Ulivunja ahadi yetu, naona unataka kunigombanisha na wazazi wangu wewe!”
“Ahadi gani?”
“Inamaana hujui kuwa umefeli? Nitakupeleka wapi kama mtu mwenyewe umefeli? Hizo nguo ni zawadi yangu ya mwisho kwako. Naomba usijaribu kunipigia simu wala kuniandikia meseji, sitaki tena kuwa na wewe. Naomba uelewe...” akasema Genesis na kukata simu.

Kitu pekee kilichoonekana kwa Farida ilikuwa ni kutiririka kwa mvua ya machozi mashavuni mwake. Mama yake aliyekuwa bado amesiamama mbele yake hakuwa na sababu ya kuuliza kilichotokea, kama mtu mzima alikuwa ameshajua kabisa jambo gani lilikuwa likiendelea.

“Mpaka akuue ndiyo utaridhika, shida yako unataka tufungwe tukaozee jela familia nzima,” mama Farida akasema kwa sauti kubwa akionekana kuwa na hasira sana.
Hakuwa na muda tena wa kumbembeleza mwanaye!

YALIKUWA maneno mazito sana kwa Bianca, yenye maumivu yasiyoweza kufananishwa na kitu chochote. Ni kama alikuwa hajasikia vizuri maneno yale, akamuangalia Genesis usoni akitegemea huenda Genesis angejisahihisha, lakini haikuwa hivyo Genesis alionekana kutamka maneno yale kwa kudhamiria na si kwa bahati mbaya!

“Genesis!” Bianca akaita akiendelea kulia.
“Sema mama!”
“Nimekusikia vibaya au ndivyo!”
“Kwamba?”
“Hujali machozi yangu!”

“Bianca tatizo wanawake wengi huwa hampendi kuambiwa ukweli, lakini mimi nitasimamia ukweli siku zote za maisha yangu, kwanini nikudanganye? Kwanini nijitese? Huo ndiyo ukweli wenyewe!”
“Kwahiyo hunipendi Genesis?”

“Hilo mimi sijasema, labda useme wewe. Nakupenda, lakini nimekuambia ukweli kwamba ni vigumu sana kumsahau Farida!”
“Kwahiyo bado unampenda!”

“Yupo moyoni mwangu bado, lakini kwa kuwa nimeshaamua kuwa na wewe, inakubidi uhakikishe unafanya mambo mengi kama yeye, ili niweze kumsahau na kuendelea na wewe moja kwa moja!”

Maneno ya Genesis yaliendelea kuwa maumivu makali sana moyoni mwa Bianca. Yalikuwa maneno mazito sana tofauti na Genesis mwenyewe alivyofikiria! Kilichoonekana kwa Genesis ni kushindwa kuzuia hisia zake za ndani, kwani maneno yale yalikuwa yanatokea ndani kabisa mwa moyo wake.

“Lakini Genesis wangu, hebu niambie unahitaji nikufanyie nini ili uache kumuwaza yule mpumbavu?”
“Hilo ndiyo swali la maana la kuuliza!”
“Nijibu basi dear!”

“Rahisi sana, nipende, nijali, niheshimu na usinisaliti!”
“Hayo tu?!”
“Hakuna kingine...unajua Bianca ilikuwa lazima nikueleze ukweli ili na wewe ujue jinsi ya kunishika. Naamini sasa penzi letu litakuwa zuri zaidi na zaidi!”

“Ni kweli, lakini please naomba uwe unapima maneno yako kabla ya kuniambia, mengine yananiumiza sana!”
“Usijali mpenzi wangu!” Genesis akasema akimbusu Bianca mashavuni mwake.

Waliendelea kuzungumza mambo mbalimbali ya mapenzi yao, baadaye wakaamua kuingia ndani ya maji na kuogelea. Waliondoka Bagamoyo usiku wa saa mbili kurejea nyumbani. Kwanza Genesis alimpeleka Bianca nyumbani kwao Mikocheni kisha naye akaenda nyumbani kwao Masaki.

“Ulikuwa wapi baba?” Profesa Mshana akamuuliza Genesis alipokuwa akiingia sebuleni usiku huo.
“Baba...hata kabla sijakusalimia?!” Genesis akasema akitabasamu.
“Mh! Haya mzima mwanangu?”
“Salama baba, shikamoo!”

“Mar-haba...enhee sasa niambie ulikuwa wapi?”
“Bagamoyo!”
“Bagamoyo kufanya nini tena?”
“Bianca alitaka nimpeleke huko, nikawa sina ujanja!”

“Sawa, lakini lazima uwe mwangalifu, bado wiki mbili muende chuoni!”
“Hilo baba nalitambua na ahadi yangu itaendelea kuwa ile ile!”
“Kuwa lazima uwe Profesa kama baba yako, si ndiyo?” Profesa Mshana akasema kwa majigambo.

“Ndiyo baba, tena nataka niwe na mke msomi kama mama!” Genesis akasema akicheka.

Wote wakabaki wanacheka pale sebuleni. Genesis aliongea maneno yaliyowafurahisha sana wazazi wake. Katika familia ya Profesa Mshana, elimu ilikuwa ndiyo kitu cha kwanza!

***
Hatimaye siku ya kwenda chuoni ilifika, Genesis na Bianca walipangiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani). Ilikuwa siku ya furaha sana kwa familia hizo mbili; familia ya Dokta Rwegoshora na Profesa Mshana.

Wazazi wa pande zote mbili walikuwa pamoja kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao chuoni. Kwao ilikuwa zaidi ya siku ya kwanza ya kuelekea Chuo Kikuu. Ulikuwa mwanzo mzuri kwa watoto wao kushikamana pamoja na kuwa wapenzi wa kudumu. Kwao ilikuwa fahari kubwa sana.

“Genesis!” Dk. Rwegoshora akaita.
“Naam baba!”
“Unatakiwa kufahamu kwamba mmekuja hapa chuoni kusoma. Mnatakiwa kusaidiana kwa kila hali katika masomo yenu ili muhakikishe mnafaulu na kuwa wasomi kama sisi wazazi wenu. Hatuamini kama mtatumia nafasi hii vibaya.

“Ni matumaini yetu kuwa mtasoma kwa bidii zaidi ili mfanye makubwa zaidi ya yale mliyotuonesha kwenye matokeo yenu ya kidato cha sita!” Akasema Dk. Rwegoshora.
“Tunakuahidi baba!”
“Bianca!” Mama Genesis akaita.

“Abee mama!”
“Mimi sipo mbali sana na baba yenu, nawasisitiza mzingatie masomo. Tunafahamu uhusiano wenu na tunaubariki, lakini msiegemee kwenye mapenzi mkasahau masomo. Kilichowaleta hapa ni masomo na mkae mkijua kwamba mnatengeneza maisha yenu ya baadaye. Sasa hamtaweza kuyatengeneza kama mtaamua kuegemea zaidi kwenye uhusiano wenu!”

“Nimekuelewa vizuri sana mama!”
Baada ya hapo wakakumbatiana kwa pamoja kisha wakatoa mizigo yao kwenye gari na kuanza kuelekea kwenye ofisi za chuo kwa ajili ya kupata maelekezo mengine.

***
Chuo kizima walijua uhusiano wa Genesis na Bianca, kwa muda wa miezi minne tu tayari walikuwa maarufu chuoni. Jambo lililowafanya wakajulikana kwanza ni uzuri wao, Genesis alikuwa mtanashati kuliko kawaida na urembo wa Bianca ukawa tishio chuo kizima.

Mbali na hilo, kuna kubwa zaidi ambalo lilizidisha umaarufu wao chuoni, fedha! Walikuwa wanafunzi wenye matumizi makubwa zaidi ya fedha kuliko wengine. Waliongozana muda wote kama kumbikumbi, mapenzi yao hayakuwa siri kabisa.

Uhusiano huo ulimfurahisha sana Bianca, ambaye ndiye aliyesababisha wanafunzi wengi kufahamu uhusiano wao kabla ya kusambaa chuo kizima, tofauti na Genesis ambaye pamoja na kukubali kuwa na Bianca bado moyoni mwake kulikuwa na Farida akiendelea kumtesa.

Jioni moja wakiwa wamekaa chini ya mti wakijisomea, ghafla Genesis akaonekana amebadilika. Furaha yake ikatoweka na kuonekana ana mawazo sana. Bianca aligundua jambo hilo haraka sana, akaamua kumuuliza.
“Vipi Genesis una tatizo?”

“Hapana, kwanini umeniuliza hivyo?”
“Nahisi haupo sawa!”
“Ni kweli kichwa kinagonga!”
“Kama ni hivyo basi nenda ukanunue Panadol dukani umeze!”
“Hapana...” akasema Genesis akijikuta akianza kudondosha machozi.
“Una nini?”

“Nimekuambia kichwa!”
“Ndiyo ulie?!” Bianca akamuuliza tena akiwa haamini kama ni kichwa tu ndicho kinamsumbua mpenzi wake.
“Niambie basi baby, una nini?”

Genesis hakuweza kujibu kitu, hisia nzito za mapenzi dhidi ya Farida zilimzidi moyoni mwake, haikuwa rahisi kuachana naye. Alihisi kupoteza kitu kikubwa sana katika maisha yake.

“No! Siwezi kuishi na mateso haya, lazima nimfuate Farida sasa hivi!” Akawaza Genesis akiinuka na kuacha vitabu vyake pale chini.
“Vipi?”

“Natoka kidogo!”
“Unaenda wapi?”
“Nimekwambia natoka!”

Genesis akasimama na kuondoka mbio pale chini ya mti, alikuwa anakwenda kumfuata Farida nyumbani kwao Kwa-Azizi Ali.

Je, nini kitatokea? Farida atakubali kumpokea Genesis?
 
SEHEMU YA 21


Pamoja na Genesis kukubali kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Bianca, bado mzimu wa penzi la Farida unamwandama. Mara kadhaa amejitahidi kumsahau bila mafanikio.

Penzi lake na Bianca sasa limekuwa la ugomvi kila wakati. Hata hivyo, Bianca anaamua kumtumia mama yake Genesis kuweka mambo sawa.Ikiwa ndiyo kwanza wanakutana muda mfupi baada ya Bianca kumpigia simu mama yake Genesis, simu ya Genesis inaita, alipoitazama kwenye kioo akagundua aliyekuwa akipiga ni Farida.

Genesis akatafuta sababu na kuondoka ili akazungumze na Farida jambo ambalo lilifanyika. Hata hivyo, tofauti na matarajio yake, Farida alikuwa mkali na alimtaka akome kumfuatilia kwani amechoka kuumizwa moyo wake.

Kitu pekee ambacho Farida aliona kinafaa kilikuwa ni kuswali swala tano. Kingine ni kutuma maombi katika vyuo mbalimbali duniani akitafuta udhamini.

Siku moja akapata wazo la kuanzisha biashara, jambo ambalo mama yake alilifurahia na kumpa msingi wa shilingi elfu kumi.
Mara moja akaanza biashara ya kuuza matunda kwa mtindo wa kutembeza kwenye beseni mitaani.

Genesis na Bianca wakiwa ndani ya gari jua kali likiwaka, wakielekea nyumbani kwa akina Genesis, Genesis anamuona Farida akiwa na beseni la matunda pembeni mwa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, nyuma kidogo ya Mataa ya Bamaga. Moyo ukamuuma sana, akamuomba Bianca amruhusu wampe lifti Farida.

Bianca alipingana na jambo hilo na kumwambia kama anataka kumpa lifti basi ni bora yeye akashuka ndani ya gari hilo. Genesis akamwambia ashuke.
ULIKUWA mtihani mkubwa sana kwa Bianca ambaye alitumia sekunde kadhaa kumwangalia Genesis kama angebadilisha uamuzi wake. Alikuwa anajidanganya sana, Genesis alionekana kudhamiria kile alichokiongea.

Akapunguza mwendo na kuegesha gari pembeni katika Kituo cha Daladala cha Bamaga, mbele kidogo ya Baraza la Mitahani la Tanzania (NECTA).
“Haya shuka sasa!” Genesis alisema akionekana hana masihara na alichokiongea.

“Unasemaje?”
“Acha wivu wa kijinga wewe... yule nimeshaachana naye lakini ni binadamu mwenzetu, kumbuka tumesoma naye anateseka na jua wakati sisi tukipulizwa na kiyoyozi. Hakuna ustaarabu kama huo, ni lazima tumpe lifti!”

“Nimekuambia kama yule kinyago wako ataingia kwenye hili gari, mimi nitashuka!”
“Sikutegemea kama una akili ndogo kiasi hicho!” Alisema Genesis kwa dharau.

“Unamanisha nini?” Bianca aliuliza akibenua mdomo.
“Yaani hujui ni kwa nini nimesimama hapa? Ni kwa sababu mbili tu, Farida aingie kwenye gari wewe ukiwepo au ukiwa umeshuka!”
Bianca hakuongea neno lolote zaidi ya kuufungua mlango na kuubamiza kwa nguvu. Akapiga hatau za haraka akiifuata barabara inayoelekea Mwenge.

Genesis hakujali, ni kama alikuwa ametua mzigo mzito kichwani mwake.
Kwake Farida alikuwa na thamani kubwa sana kuliko Bianca. Aliona umuhimu wake katika shida ya Farida. Alichokifanya ni kufungua mlango wa gari kisha akaufunga, akaanza kupiga hatua kuelekea alipokuwa Farida.

Kazi yake kubwa ikawa ni kuangaza macho na kumtafuta Farida. Alikuwa akikazana sana, akapita Mataa ya Bamaga akiendelea kumuangalia bila Farida mafanikio.

“Yuleee...” akajisemea akisonza kidole chake mbele ya Sheli ya Bamaga.
Akaangalia magari, alipoona kuna usalama, akavuka na kwenda moja kwa moja hadi mahali alipokuwa amesimama Farida.
“Farida vipi?” Akasalimia Genesis akionekana kutetemeka kidogo.
“Salama!”

“Vipi unaelekea wapi?”
“Nipo kwenye biashara kwani we huoni?”
“Ok! Sasa aa...u-unajua nilikuwa nafikiri nikupe lifti!”
“Hivi una akili wewe? Nimekuambia nipo kwenye biashara, hiyo lifti yako sasa ni ya nini?”

“Najua Farida lakini nataka nizumgumze na wewe kidogo, hebu twende kwenye gari nina maongezi na wewe!”
“Maongezi gani na mimi? Eeeh!”
“Ni vizuri ukanisikiliza kwanza, unajua mimi nakupenda sana naaa....” Farida hakumpa nafasi ya kumalizia sentesi yake, akamkatisha.

“Achana na hizo habari Genesis kama ni kunitesa umenitesa zamani na sasa nahitaji kupumzika. Endelea na Bianca wako, tajiri mwenzako, niache na umasikini wangu!” Farida alisema akishindwa kuzuia machozi yake.

Kwa watu waliokuwa jirani na eneo lile, ilikuwa ni sinema ya bure, wakaanza kujisogeza na kufanya umati mkubwa kuwaangalia.
“Jamani nisaidieni, nampenda huyu mwanamke, nilikosana naye kidogo tu, siwezi kuishi bila yeye, nisaidieni jamani!” Alisema Genesis akiwatazama watu waliokuwa eneo lile.

“Muongo huyu ana mpenzi wake anaitwa Bianca ambaye wazazi wake wanampenda, mimi sipendwi kwa sababu ya umasikini wangu. Mwacheni aondoke, mimi sitaki kumuona,” alisema Farida huku akiendelea kulia.

“Sikiliza Farida, huwezi kuamini nimemshusha Bianca kwenye gari kwa sababu yako, tafadhali nipe nafasi nikueleze kilichopo moyoni mwangu, punguza hasira mpenzi wangu.”

“Shut up (nyamaza)! Naomba uondoke nataka kufanya biashara yangu au unataka kunikwamisha tena hata katika kibiashara changu hiki kidogo?”
“Siyo hivyo mpenzi wangu sasa anyway...sikia ...” Akasema Genesis akifungua pochi na kutoa noti mbili za elfu kumi kumi na kumkabidhi Farida ambaye alizipokea.

“Nimefurahi sana kwa kukubali kuzipokea, nakubaliana na hisia zako lakini ukiwa na tatizo wakati mwingine usisite kuwasiliana na mimi. Kumbuka bado nakupenda!” Akasema Genesis uso wake ukichanua kwa tabasamu.

Bila kutarajia, Farida alizikusanya zile fedha, akazifinyafinya kiganjani mwake kisha akamtupia Genesis. Uso wake ulizidi kuchakazwa na machozi.
“Sina shida na fedha zako, natafuta riziki yangu na inanitosha. Nimeshakumbia sikutaki tena Genesis!” Akasema Farida kwa hasira akisimama na kubeba beseni lake kisha akatimua mbio.

Watu wakabaki wanashangaa, Genesis aliduwaa akiwa hana la kufanya; hapo hapo akaanza kuangaza macho yake akimtafuta Bianca lakini hakumuona. Kwa aibu, Genesis akaondoka hadi kwenye gari lake, moyo ukiwa unamuuma sana.
“Farida naye anaringa sana, anajiona mzuri, ngoja nimpigie Bianca,” akasema Genesis akimpigia simu Bianca.

Katika hali ya kushangaza sana, simu ya Bianca haikupatikana. Jambo hilo lilimhuzunisha sana, akiwa anataka kuondoa gari, simu yake ikaita. Alipotupa macho kwenye kioo cha simu yake alikutana na jina ‘Ma Mom’ (my mother) likimaanisha mama yake.

“Wee mpumbavu njoo nyumbani.”
“Ndiyo nakuja sasa hivi mama niko njiani.”
“Haraka.”

“Ndiyo mama, kwani kuna nini?”
“Nimesema njoo nyumbani sasa hivi!”
“Sawa mama nakuja.”
Wakakata simu zao.

Genesis alijua kwa vyovyote vile tayari Bianca ama alimpigia mama yake simu au alikwenda nyumbani kumueleza kilichotokea. Jambo hilo lilimhuzunisha sana, akijua lazima angegombana na mama yake.

“Vyovyote itakavyokuwa bwana, ngoja nikamsikilize.”
Genesis akaondoa gari na kuelekea nyumbani kwao, kichwa chake kilikuwa kimejaa mawazo tele, Farida akiwa ndiye anayemsumbua zaidi.

***
Alishuka kwenye gari kisha akaanza kupiga hatua za taratibu kuufuata mlango mkubwa wa kuingia ndani kwao. Moyo wake ulikuwa ukienda kasi, akiamini lazima kulikuwa na ugomvi mkubwa kati yake na mama yake.

Alipoingia sebuleni, mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni Bianca! Mapigo ya moyo wake yakaongezeka mara dufu.
Kwenye sofa kubwa alikuwa ameketi mama yake, uso ukiwa umekunjamana.
“Shikamoo mama!”

Mama yake hakuitika, Genesis akahisi labda hakusikia, akamsalimia kwa mara nyingine.
“Mama nakusalimia shikamoo.”
“Sina shida na shikamoo yako. Hivi ni lini utaacha kumtesa mwenzako? Hilo li-Farida lako limekupa nini?” Mama Genesis alisema kwa hasira.

“Mama ni lazima tuzungumze, hatujaonana kwa muda mrefu, hata huijui hali yangu, kwa nini mama?” Genesis aliongea kwa sauti ya chini huku akionesha simanzi.

“Una lipi la kuniambia? Huna lolote, kazi ni kumnyanyasa mwenzako tu!”
Yalikuwa maneno makali yaliyomuumiza moyo Genesis, alihisi kama ananyang’anywa haki yake ya kupenda. Ni kweli alimheshimu sana mama yake lakini kwa suala la kumchagulia mchumba, aliona bora heshima ivunjike.
Genesis akasimama, akionekana kuumia sana moyoni mwake, akapiga hatua za taratibu kuufuata mlango mkubwa wa kutokea nje.

“Wee Genesis unaenda wapi?” Mama yake akamuuliza kwa hasira.
“Niache mama, naona leo Bianca amekuwa na thamani kuliko mimi mwanao wa kunizaa. Nakwenda zangu.”

Mama yake pamoja na Bianca hawakuamini maneno ya Genesis lakini walichoshuhudia ni Genesis kubamiza mlango kisha wakasikia muungurumo wa gari. Wakabaki wanaangaliana.

Alichokifanya mama Genesis ilikuwa ni kumpigia mwanaye simu lakini cha kushangaza Genesis hakupokea hadi simu ikakatika. Aliporudia mara ya pili simu ilikuwa imezimwa kabisa!!!

“Genesis kwa nini unanitesa mwanangu?” Mama Genesis alitamka maneno hayo kwa sauti.

Bianca alikuwa amechoka zaidi na machozi yakazidi kumtapakaa katika mashavu yake. Hakujua mahali alipokwenda Genesis, mwanaume anayeutesa moyo wake lakini penzi lake likiwa limeangukia kwa mwanamke fukara Farida.

MSIMAMO wa Genesis ukazidi kumshangaza sana mama yake, alishindwa kuelewa ni kwa nini mwanaye alikuwa hampendi kabisa Bianca ambaye kwao alikuwa mwanamke mwenye thamani kubwa.



Bianca aliheshimiwa na kupewa nafasi ya kwanza kwa sababu kubwa mbili; uwezo wa familia yao kifedha na kielimu pamoja na msichana huyo kuwa na uwezo mkubwa kimasomo.

Mama Genesis aliamini kama mwanaye asingemuoa Bianca, basi angeangukia kwa Farida, mwanamke kutoka familia masikini, mama yake akiwa Mama Ntilie na baba Fundi Seremala.



Kwa familia ya Profesa Mshana ilikuwa aibu au kuitia familia nuksi! Hawakutaka kusikia kabisa habari za Farida. Walikuwa tayari kufanya chochote kwa ajili ya kuwaachanisha Farida na Genesis.



Ubongo wa mama Genesis ulifanya kazi kwa kasi kuliko kawaida, hakuamini kama mwanaye wa kumzaa angeweza kumzimia simu!

Akiwa bado anatafakari cha kufanya, akayarudisha macho yake kwa Bianca aliyekuwa amekaa kwenye sofa lingine upande wa pili, akakutana na kitu cha ajabu sana!



Bianca alikuwa analia na macho yake yalikuwa yamezingizwa na machozi kila kona. Mashavu yalikuwa chapachapa!



Mara moja akainuka na kwenda kuketi pembeni yake, kinywa chake kilionekana kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kutoa maneno matamu sana ya kumfanya Bianca atulie. Punde akaanza kuzungumza.

“Binti yangu, huna sababu ya kulia, tafadhali futa machozi yako!” Akasema mama Genesis akimwangalia Bianca usoni.



“Mama naumia, mama...naumia, hata mimi moyo wangu una nyama!”

“Najua binti yangu, unajua tunatakiwa kwenda taratibu sana, hili siyo jambo la kulikatia tamaa mapema, bado tunayo nafasi ya kuweka mambo sawa. Tafadhali, nakuomba utulie kwanza!”



“Nimechoka mama...halafu lazima utambue kwamba nampenda sana Genesis, haya yote ni kwa sababu nampenda na siwezi kufanya chochote bila yeye. Naomba unisaidie mama. Nisaidie mama, bila yeye siwezi. Nitafeli mama,” alisema Bianca akizidi kulia.

Kazi kubwa kwa mama Bianca ikawa ni kumfuta machozi yake na kumbembeleza.



“Nyamaza mwanangu!”

“Jaribu tena kumpigia mama, nataka nirudi naye chuoni, sitaki kwenda peke yangu!”

“Sawa mwanangu, ngoja nijaribu kumpigia kwa mara nyingine, hata mimi napenda sana kuwaona mkiwa pamoja.



“Napenda sana uwe mwali wangu na nitahakikisha hilo linatokea. Mimi ni mtu mzima, kama ni mbinu sasa hivi ndiyo kwanza tupo kwenye asilimia tano ya kwanza, kwa hiyo bado zingine 95, huoni ni nyingi sana?” Akasema mama Genesis akionekana kuwa na nia ya kumtia moyo Bianca.



“Sawa mama, ngoja tuone!”

“Usijali, kwanza ngoja nijiandae nikupeleke chuoni!”

“Nitafurahi sana mama.”

“Ok!”



Mama Genesis akaondoka na kumuacha Bianca peke yake sebuleni. Robo saa baadaye, alirudi akiwa amejiandaa kikamilifu.

“Tunaweza kwenda binti yangu!” Akasema mama Genesis akimtazama Bianca.



Bila kupoteza muda, Bianca akainuka pale sofani na kuanza kupiga hatua za kivivu kuelekea nje. Mama Genesis akaenda sehemu wanayoegesha magari na kuangaza macho yake akifikiria gari la kutumia.



Akaridhika na Toyota Prado, hapo akarudi ndani na kuchukua funguo kisha akatoka tena nje alipoungana na Bianca hadi kwenye gari.

“Tuliza moyo, tena nataka tukifika tumtafute niweze kuzungumza naye kabla sijarudi nyumbani.”



“Hilo lilikuwa ombi langu kabla hujatamka mama, ila umeniwahi tu!”

“Vizuri sana binti yangu.”



Mama Genesis, akawasha gari na kuliondoa taratibu kabisa pale kwenye maegesho akilielekeza getini. Martin, mlinzi wa getini alijua vizuri kazi yake, hakuhitaji kufundishwa kwamba bosi wake alikuwa akitaka kuondoka, akafungua geti haraka, mama akapita akiwa na mwali wake!

***



Farida alijiona mwenye mikosi katika maisha, kila kitu kilikuwa kimeharibika, masomo kwake ilikuwa ndoto, lakini hata mapenzi ndiyo alikuwa kwenye hali mbaya zaidi.



Alipotoka pale alipokuwa akizungumza na Genesis alikimbia mbio akifuata Barabara ya Shekilango, aliporidhika kwamba Genesis hawezi kumuona tena, akaanza kutembea taratibu pembeni mwa barabara hiyo, uso wake ukiwa unasoma huzuni aliyokuwa nayo.

“Ndizi...” sauti hiyo ilimnasua mawazoni Farida.



Alipoangalia mahali sauti ile ilipotokea, alimuona kijana mmoja akimuoneshea ishara ya kumuita kwa mkono, akiwa amesimama kwenye Mgahawa uliokuwa unaangaliana na geti la Chuo cha Ustawi wa Jamii.



Farida akaishawishi miguu yake kukazana na kumfikia yule kijana aliyekuwa amesimama eneo lile. Kwa mwonekano wake, haikuwa vigumu kugundua kwamba alikuwa mwanafunzi.

“Mambo?” Yule kijana akasalimia.



“Poa, karibu. Unahitaji ndizi, tango au chungwa?” Farida akasema kwa sauti ya upole sana.

“Nataka kula ubwabwa, sasa wewe fikiria kwa chakula hicho natakiwa kununua tunda gani?”



“Kila mtu ana chaguo lake, naweza kusema nikumenyee chungwa, kumbe wewe unapenda tango, naomba uchague mwenyewe!”

“Siku nyingine ukiulizwa swali kama hilo, usiwe na wasiwasi, jibu lake ni jepesi sana, ubwabwa mwezie ndizi mbivu!” Akasema yule kijana akicheka.



Farida naye akajilazimisha kucheka, ingawa kicheko chenyewe kilitoka kwa tabu kidogo.

“Unataka ngapi?”



“Kwanza unauza bei gani?”

“Shilingi mia tu!”

“Sawa, nipatie tatu!” Yule kijana akasema akitoa noti ya shilingi mia tano.



Farida akawa anajiandaa kutoa chenji ili amrudishie yule kijana, lakini akashangaa anakataa.



“Kwa nini hutaki chenji yako?”

“Unamuona yule mshkaji pale, mpelekee ndizi mbili!”

“Sawa!”



Farida akachukua ndizi mbili na kumpelekea yule kijana aliyeagizwa. Watu wengine wakapenda matunda yake na kuanza kununua.



Muda ulivyozidi kwenda ndiyo, alivyozidi kuuza matunda yake, saa moja baadaye, beseni lake lilikuwa tupu! Akamshukuru sana Mungu kwa muujiza ule.



Hakutegemea kama biashara ingekuwa nzuri kiasi kile. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda na njaa kumuuma sana, akaamua kununua chakula pale, alipomaliza kula akalipa na kutaka kuondoka.



“Napenda sana wasichana wanaojishughulisha kama wewe, hongera sana,” mama mwenye Mgahawa ule akamwambia.

“Nashukuru sana mama.”



“Wewe ni sawa na binti zangu waliopo nyumbani, sasa nahitaji kukusaidia kidogo katika biashara yako!”

“Nitashukuru sana mama.”



“Si kwa kukupa fedha ila kukupa sehemu ya kudumu ya kufanyia biashara yako. Kuanzia kesho, ukishachukua mzigo wako, njoo moja kwa moja hapa, uuzie hapa maana naona wateja wangu wamependa sana matunda. Kama unavyoona hapa wateja wetu wengi ni wanachuo wa hapo Ustawi, kwa hiyo kuna uhakika wa kufanya biashara yako kila siku.”



“Ahsante sana, Mungu akubariki sana, naona sasa sitaungua tena na jua. Nashukuru sana.”

“Usijali.”



Farida akaondoka akiwa na furaha sana, akaanza safari ya kwenda kituoni kwa ajili ya kutafuta usafiri wa kwenda kwao Kwa Aziz-Ali. Moyoni akijiona mshindi!

***



Alipofika katika geti la kuingia eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akitokea Mlimani City, mama Genesis alipunguza mwendo na baadaye kusimama kabisa kupisha askari wafanye ukaguzi!



Zoezi hilo lilipokamilika, aliondoa gari kwa mwendo wa taratibu kabisa, baada ya mwendo mfupi, alikata kulia na kuingia kwenye Baa ya UDASA iliyopo ndani ya chuo hicho. Akatafuta sehemu nzuri na kuegesha.



“Kipi kianze, tumtafute Genesis au tukae kwanza kwa ajili ya vinywaji?” Mama Genesis alimuuliza Bianca.



“Tuanze kumtafuta kwanza Genesis, halafu mambo ya vinywaji baadaye, tena nitafurahi sana kama tutajumuika naye mezani kupata kinywaji!”

“Sawa, tunaanzia wapi?”

“Twende kule anapoegesha gari.”

“Sawa!”



Wakatoka pamoja na kuanza kutembea taratibu sana, sehemu anayoegesha gari lake hapakuwa mbali na walipokuwa, hivyo baada ya muda mfupi sana, walifika na kulikuta gari lake, hiyo ilitosha kabisa kuwadhibitishia kwamba Genesis alikuwa pale chuoni.



“Sasa mimi narudi pale baa, wewe mtafute kwa hali na mali, ukimpata mwambie namuita mimi, najua hawezi kukataa.”

“Sawa mama!”



Bianca akaondoka kumfuatilia Genesis na mama Genesis akashika njia, akirudi kwenye ile baa aliyoegesha gari lake. Safari yake iliishia moja kwa moja chumbani kwa Genesis.



Kwa bahati nzuri, alimkuta Genesis akiwa amekaa nje na rafiki yake Greyson. Alipomuona Bianca akakunja uso kwa hasira.



“Najua una hasira Genesis lakini nakuomba sana utulize moyo wako, nina ujumbe wako muhimu sana.”

“Kutoka kwa nani?”

“Mama!”



“Sitaki kuusikia, tena nakutuma, mwambie kabisa sitaki kusikia sauti yake akisema chochote kuhusu maisha yangu ya mapenzi!”

“Siyo hivyo Genesis mpenzi wangu!”



“Umeniitaje? Wewe mimi siyo mpenzi wako na nakuomba sana, acha kuniita hilo jina...naomba uondoke!”

“Mama anakuita yupo pale UDASA!”

“Hapa chuoni?”

“Ndiyo!”



“Amenifuata mimi kwa mazungumzo kuhusu wewe?”

“Ndiyo!”



“Nenda kamwambie sitaki na sipendi tabia yake ya kuingilia maisha yangu. Nina haki ya kuamua mambo yangu mweyewe. Potea...” akasema Genesis kwa kumaanisha akisimama na kumfukuza Bianca ambaye alitimua mbio kwa woga!

Mama yake atapokeaje taarifa za Genesis?

Nini kitatokea katika uhusiano wa vijana hawa wadogo?
 
SEHEMU YA 22


Genesis ameendelea kushikilia msimamo wake wa kumkataa Bianca na kutaka kuendelea na Farida. Pamoja na mama yake kumfuata chuoni, lakini alikataa kwenda kuonana naye.

Bianca naye amechanganyikiwa kabisa kutokana na msimamo wa Genesis, hakuweza tena kuendelea kubaki chuoni, akaamua kutoka na kwenda zake nyumbani kwao, ambapo alitumia muda mwingi kwenye kioo akijikagua kama anavutia au la!

Majibu aliyoyapata yalisema kwamba yeye ni mwanamke mrembo sana, hapo akawaza sababu za Genesis kumkataa, lakini hakuzipata.

Genesis ameitwa na baba yake, Profesa Mshana na kumruhusu aendelee na uhusiano na Farida kwa madai kwamba wanaheshimu hisia zake. Uamuzi huo umemfurahisha sana Genesis, ambaye haamini kabisa kilichotokea.

TABASAMU pana lilichanua usoni mwa Genesis kama mwanga wa jua changa la asubuhi linavyotaka kutoka kupishana na giza ili liangaze dunia! Ilikuwa siku mpya kwa Genesis, moyo wake ulijaa furaha na hakuwa tayari kuamini kirahisi kama wazazi wake wameamua kumruhusu kurudiana na Farida.

Akawaangalia wazazi wake kwa zamu akiwa haamini kabisa kilichotokea, macho yake tayari yalishaanza kunyemelewa na unyevunyevu ambao ungeruhusu machozi baada ya muda mfupi.
“Baba!” Genesis akaita.

“Nakupenda sana baba….nakupenda baba. Ahsante sana kwa kuamua kunikubalia kilio changu cha siku zote. Sasa nawaahidi kusoma kwa bidii na nitawashangaza sana!” Genesis alisema kwa hisia kali sana.

“Nami pia nakupenda mwanangu. Najua ujana, najua maumivu ya kupenda. Unajua kama mimi nisingekuwa nampenda mama yako, leo hii nisingekuwa naye, lakini kwa sababu moyo wangu uliamua kuwa naye bila shinikizo kutoka sehemu yoyote ndiyo maana unaona nimedumu naye na kuwazaa wewe na dada yako!”

“Ahsante sana baba… ni jambo lililokuwa likiutesa sana moyo wangu, lakini sasa nina amani!”

“Usijali tumeona ni vyema kuangalia hisia zako. Tumeamua kwa moyo mmoja, kama nilivyokuambia sasa hivi Farida yupo huru, hapa ni kwake na kwao ni kwenu, sawa mwanangu?!” Mama yake Genesis alisema.

Ilikuwa kama yupo kwenye ndoto ndefu ya kutisha, lakini haikuwa ndoto, ni ukweli ambao ulikuwa yakinifu kabisa.

Genesis akasimama akainua mikono yake, akiwaonesha wazazi wake ishara ya kuwataka wasimame, wote wakasimama na kukumbatiana kwa pamoja. Genesis akatokwa na machozi ya furaha.

“Usijali mwanangu….lakini sasa pamoja na maamuzi hayo, lipo sharti moja muhimu sana!” Profesa Mshana akasema.
“Sharti?” Genesis akauliza kwa mshangao.

“Ndiyo, lakini siyo kubwa, usishtuke sana.”
“Ni nini tena baba?” Akauliza Genesis akijinasua kutoka katika mikono ya wazazi wake.

“Hebu keti kwanza.”
“Umenishtua sana baba,” akasema Genesis akikaa kwenye sofa.
“Kama unavyojua sisi ni wasomi, tumekubaliana na uamuzi wako wa kumpenda Farida, lakini fanya juu chini, uhakikishe anapata chuo ili usioe mwanamke gunia!

“Tunapenda sana mafanikio yako ya baadaye, kwa hiyo angalau awe na sifa hiyo tu kwanza. Sisi tutakuwa tayari kukusaidia hata fedha, lakini Farida apate chuo, asome kama wewe ili muweze kujenga familia bora yenye muunganiko wa vichwa viwili vyenye akili.”
“Sawa baba, hilo ni dogo sana, nitahakikisha nalisimamia na litakuwa sawa.”

“Basi ni vyema, sasa unaweza kurudi chuoni!”
“Hapana, sina vipindi asubuhi hii, halafu leo nina kipindi kimoja tu, saa 11 jioni.”

“Kwa hiyo utashinda hapa nyumbani siyo?”
“Ndiyo, lakini itabidi nitoke!”
“Wapi tena?” Mama yake akadakia.

“Lazima niende nikampe Farida habari hizi njema kwetu.”
“Sawa, siyo vibaya.”
“Haya Genesis, acha sisi twende zetu kazini.”
“Sawa, nawatakieni kazi njema.”
“Nawe ubaki salama.”

Profesa Mshana na mke wake wakatoka nje, wakaenda moja kwa moja hadi kwenye maegesho, uso wa Bi. Mshana ukiwa umepambwa na tabasamu muda wote.
“Vipi?” Mumewe akamuuliza.

“Kazi imeisha.”
“Lakini mke wangu, unajua umeniambia niongee maneno yale, lakini sijajua kabisa lengo lako hasa ni nini?”

“Usijali mume wangu, nimekuambia Genesis tumemzaa sisi, hajaja mwenyewe duniani kwa hiyo hawezi kutushinda hata kidogo.

Kwa sasa nyamaza kwanza, muda kidogo utajua maana yangu!”
“Haya bwana, nitafanya nini basi kama si kukukubalia?” Alisema Profesa Mshana akiingia kwenye gari lake.

Mkewe naye akaingia kwenye gari lake, baada ya hapo akatangulia mama Genesis kutoka getini kisha Profesa Mshana akafuata nyuma yake.

Safari ya kwenda kazini ikaanza.
***
Macho yake yalishangazwa sana na gari aliloliona limesimama kwenye maegesho yao. Bi. Rwegoshora aliyatoa macho yake akiwa haamini alichokiona. Ni gari la mwanaye Bianca!

Alihisi mwanaye amepatwa na tatizo. Wazo hilo lilivamia ubongo wake kwa sababu Bianca hakusema kama angekuja nyumbani, hivyo kuliona gari lake pale nyumbani ilikuwa ni ishara ya matatizo.

Akasogeza gari lake na kuliegesha vizuri kisha akaanza kukagua lile gari la Bianca. Lilikuwa zima kabisa, maana tayari alikuwa ameshaanza kufikiria kwamba huenda alipata ajali.

Akapiga hatua za haraka hadi getini alipomkuta mlinzi wake aitwaye Musa.

“Musa vipi?”
“Salama shikamoo mama.”
“Mar-haba, lile gari la Bianca nani amekuja nalo?”
“Dada mwenyewe.”
“Amekuja saa ngapi?”

“Muda kidogo, tangu saa 10.”
“Amekuja peke yake?”
“Ndiyo!”
“Yupo ndani?”

“Tangu amefika, sijamuona akitoka na muda wote nilikuwa hapa getini mama!”
“Haya kazi njema.”
“Ahsante sana mama.”

Bi. Rwegoshora akaondoka zake kuelekea ndani. Alitegemea kumkuta Bianca sebuleni, lakini haikuwa hivyo, hapo akajua kwa vyovyote vile angekuwa amekwenda chumbani kwake. Akamfuata.
Hakugonga, aliusukuma mlango na kuingia moja kwa moja.

Alimuona Bianca akiwa amelala kitandani, macho yake yakiangalia juu.
“Vipi baby, una tatizo gani?” Ndiyo neno la kwanza Bi.

Rwegoshora kutamka baada ya kuingia chumbani kwa mwanaye.
Swali la mama yake lilikuwa kama limemchochea Bianca kulia. Akaanza kulia kwa sauti ya chini, lakini mama yake alivyozidi kumuuliza, ndivyo alivyozidisha sauti yake.

“Lakini machozi hayatasaidia kitu, niambie kuna nini?”
“Mama ni Genesis...”
“Genesis tena?”

“Ndiyo mama, ananifanyia vituko sana. Sioni thamani yangu mama, sioni sababu ya kuendelea kuishi tena.”
“Hapana, usiseme hivyo mwanangu, ngoja niwasiliane na mama yake, ataniambia kinachoendelea...” akasema Bi. Rwegoshora kwa sauti iliyojaa huzuni.
“Sawa.”
“Nisubiri nakuja sasa hivi.”
“Sawa mama.”

Bi. Rwegoshora akatoka na kwenda chumbani kwake, huko ndipo alipoona angeweza kuzungumza na Bi. Mshana vizuri. Alimpigia simu na kumuuliza kilichotokea.

Walizungumza kwa muda mrefu sana, mwanzoni Bi. Rwegoshora alikuwa akizungumza kwa ukali, lakini baadaye alipogundua kwamba Bi. Mshana alikuwa upande wake, akawa mpole kama maji ya mtungini.

“Sasa ninalo wazo!” Bi. Mshana akasema.
“Wazo gani mwenzangu?”
“Naona tumruhusu Genesis aendelee na Farida wake!”
“Aendelee naye?”

“Ndiyo!”
“Halafu Bianca?”
“Usijali, nitakueleza sababu, unajua...” mama Genesis akaanza kumueleza mama Bianca mpango mzima wa yeye kuamua kumruhusu Genesis aendelee na Farida.

Mwisho kabisa, mama Bianca alimuelewa na kukubaliana naye. Muda huo huo, akarudi chumbani kwa mwanaye akiwa na uso wenye tabasamu pana.

Alizungumza na Bianca kwa robo saa tu, naye akaanza kutabasamu kwa furaha. Kwa maelezo ya mama yake, Bianca alikubali kuachana kabisa na Genesis na kumruhusu aendelee na uhusiano wake na Farida.

“Sawa mama nimekuelewa!” Bianca akasema akitabasamu.
“Kwa hiyo kesho unarudi chuoni?”
“Ndiyo mama, tena asubuhi kabisa!”

“Sawa basi, mimi nipo chumbani kwangu!”
“Sawa mama, mimi naenda zangu sebuleni kuangalia filamu kidogo, hivi hakuna filamu yoyote mpya mliyoinunua?”
“Ipo moja, tena imetoka wiki hii!”
“Filamu gani?”

“Tears on Valentine Day, ni nzuri sana, wasanii wako wote unaowapenda wamecheza!”
“Mh! Mama...ngoja nikaiangalie.”
“Oke!”

Bi. Rwegoshora akaenda chumbani kwake, Bianca akatoka kwenye korido na kwenda sebuleni kwa ajili ya kuangalia filamu mpya.
***

Ilikuwa kama Genesis amefunguliwa kutoka kwenye gereza alimofungwa kwa zaidi ya miaka ishirini. Dakika tano tu, baada ya wazazi wake kuondoka, alitoka nje haraka na kuingia kwenye gari lake kisha akawasha na kuanza safari ya kwenda Mtoni Kwa Aziz-Ally.

Alikuwa na hamu sana ya kukutana na Farida ili amueleze juu ya habari mpya ya kufurahisha. Kwa mwendo aliokuwa akiendesha, alitumia nusu saa kutoka nyumbani kwao Masaki hadi Kwa Aziz-Ally.

Hakutaka kwenda na gari hadi kwa akina Farida. Akaliegesha juu kidogo, kisha yeye akashuka na kwenda mpaka karibu. Akasimama chini ya mti kisha akatoa simu yake na kumpigia Farida.

Tofauti na matarajio yake, simu yake ilipokelewa haraka.
“Farida nina habari njema mpenzi wangu...naomba ukubali kukutana na mimi nikueleze!” Akasema Genesis akiwa na furaha.

“Habari njema zilikuwa zamani, siyo sasa...kwanza elewa kwamba nipo kazini na ninahangaikia riziki yangu, sina haja na wewe mharibifu wa maisha yangu!”

“Najua Farida, najua kwamba nimeharibu sehemu kubwa ya maisha yako, lakini sasa nipo tayari kuitengeneza...nakuja kwako kwa ajili ya kutengeneza na siyo kubomoa tena. Naomba uje mara moja mpenzi wangu, nipo hapa kwenye mti mkubwa, karibu na kwenu!”

“Karibu na kwetu unafanya nini? Nenda na utajiri wako Genesis, sikuhitaji katika maisha yangu. Umeshaharibu vya kutosha, sasa inatosha, sikutaki tena.

“Moyo nao unatambua kutendwa, sasa umechoka kuendelea kukufurahisha wewe, wakati ukiniacha nalia. Elewa sikutaki tena katika maisha yangu, sina haja na wewe. Tafadhali koma kunipigia simu!” Akasema Farida kwa hasira na kukata simu.

Genesis akabaki ameganda kwenye mti, akiwa haamini kilichotokea. Alitakiwa kumpata Farida kwa gharama yoyote ile. Alimpenda sana msichana huyo, aliyeingia moyoni mwake.

“No! Nitampata tu Farida wangu, nitampata. Sitakata tamaa mpaka atakaporudi tena mikononi mwangu!” Akawaza Genesis akianza kupiga hatua kuelekea alipoegesha gari lake.


KUFUMBA na kufumbua, Bianca alikuwa mwenye tabasamu muda wote, makunyanzi yaliyokuwa yamejengeka usoni mwake yalifutika kabisa na kuwa na ngozi nyororo kama ya mtoto mdogo aliyezaliwa miezi miwili tu iliyopita!

Mama yake alimwambia maneno matamu sana ambayo kwa hakika yaliweza kufuta machozi ndani ya moyo wake na kumfanya kugubikwa na furaha isiyo na kifani.

Alipiga hatua za kivivu hadi sebuleni ambapo aliketi kwenye sofa baada ya kuweka filamu ya Tears on Valentine Day na kuanza kuangalia.

“Ndiyo sasa nipo tayari kwa lolote, sina hofu tena...” akawaza akiwa anaendelea kuangalia filamu hiyo.
Alikuwa na matarajio ya kurejea chuoni akiwa mwenye furaha siku inayofuata tofauti na alipoondoka akiwa na huzuni kubwa moyoni mwake.

***
Kichwa chake kilikuwa kizito sana, kwa kiasi kikubwa alijiona kama mwanaume mwenye mkosi kuliko wote. Tayari wazazi wake walikuwa wameshamkubalia kuwa na Farida wake, lakini Farida ndiye aliyekuwa hataki kusikia chochote kuhusu yeye.

Hilo lilikuwa sawa na kuchomwa na mwiba ndani ya moyo wake. Kwa unyonge akaingia ndani ya gari lake, akawasha na kuingiza gia namba moja tayari kwa safari ya kurudi zake chuoni.

Barabara nzima alikuwa na mawazo, mara kwa mara alikuwa akikosakosa kusabisha ajali. Mpaka anaingia kwenye geti la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akitokea Ubungo, alikuwa haamini kama amefika salama.

Moja kwa moja alikwenda kwenye maegesho. Alikuwa na mawazo sana. Baada ya kupaki gari, alichokifanya ni kumpigia simu rafiki yake Greyson haraka sana.
“Kaka vipi?” Ilikuwa sauti ya Genesis akiongea na Greyson.
“Poa, mbona hivyo?”
“Vipi?”

“Nakusikia kama haupo sawa.”
“Ni kweli, sipo sawa ndugu yangu, mapenzi yananinyanyasa kaka!”
“Uko wapi?”
“Ndiyo naingia sasa hivi!” Akajikuta anaropoka Genesis.

“Sijakuuliza kama umeshafika, nakuuliza kwa sasa uko wapi?”
“Kweli nimechanganyikiwa...nipo hapa Utawala kaka!”
“Nisubiri hapo nakuja!”
“Poa.”

Genesis akajiegemeza kwenye ukuta wa matangazo akionekana mnyonge . Greyson hakuwa mbali na eneo lile, baada ya dakika kumi tu alikuwa ameshafika.
“Enhee nini tena ndugu yangu?”

“Kaka huwezi kuamini, wazee wameshaamua kuniruhusu kuwa na Farida, lakini Farida mwenyewe hataki!”
“Hataki?”
“Ndiyo!”
“Unajuaje? Umeongea naye?”

“Siyo kuongea naye, nimetokea kwao sasa hivi, amesema nisihangaike kumpigia simu hata siku moja!”
“Sababu hasa anasema ni nini?”

“Eti hataki kuumizwa tena...ana mashaka kwamba naweza kumuumiza na kumsababishia machungu tena katika moyo wake. Rafiki yangu sina ujanja zaidi ya Farida, yeye ndiye mwanamke ambaye moyo wangu unampenda kwa dhati.

“Sitarajii kumpata mwanamke mwingine zaidi yake, sijui nitafanya nini jamani... Greyson wewe ni rafiki yangu siyo?!”
“Ndiyo!”
“Una uhakika?”
“Sana!”

“Ndugu yangu, kama kweli sisi ni marafiki, hili suala utalichukulia kama letu sote...”
“Bila shaka!”
“Nahitaji msaada wako katika hili.”

“Usijali Genesis bila shaka naweza kukusaidia, lakini si kwa sasa hivi, lazima niuachie ubongo wangu nafasi ufikirie vyema juu ya jambo hili!”

“Kaka nateseka ndugu yangu, hakuna cha kufikiria kuhusu hili wakati mimi naendelea kuumia. Unatakiwa kunisaidia kumrudisha Farida mikononi mwangu baaasi!”

“Hata mimi pia lengo langu ni kukusaidia ili uweze kumrudisha tena Farida mikononi mwako, lakini si kwa haraka, nipe muda!”
“Muda? Kiasi gani?”
“Kesho asubuhi nitakuwa na jibu!”
“Poa kaka.”

“Lakini hutakiwi kuwa na mawazo kaka, unatakiwa kujikaza!”
“Nitajitahidi ndugu yangu, lakini si jambo rahisi kama unavyofikiria. Moyo wangu unaumia sana, sina namna tu!”
“Usijali piga moyo konde, wewe ni mwanaume.”

Siku hiyo aliendelea kuwa mnyonge na aliamua kubaki na Greyson hadi usiku kabisa, walipokwenda kulala. Greyson alijitahidi kumfariji rafiki yake asahau matatizo aliyokuwa nayo.
Ilikuwa kazi ngumu sana, lakini alihakikisha Genesis anapunguza mawazo na kuwa katika hali ya kawaida.

***
Asubuhi walikwenda kwenye mgahawa wa chuo pamoja kwa ajili ya kupata kifungua kinywa. Wakiwa huko, Genesis alikuwa wa kwanza kumkumbusha Greyson kuhusu msaada wake ili aweze kumrejesha tena Farida mikononi mwake.

“Mh! Kweli umepania ndugu yangu,” alisema Greyson akimwangalia Genesis machoni mwake.
“Lazima iwe hivyo ndugu yangu, bila Farida maisha yangu si kitu kabisa. Hebu niambie umefikia wapi?”
“Umesema kwa sasa Farida anapatikana wapi?”
“Hapa hapa Dar!”

“Muda mwingi zaidi anakuwa wapi, hapo namaanisha anafanya kazi labda au yupo tu nyumbani?”
“Anafanya biashara ndogondogo mitaani!”
“Ok, basi kazi itakuwa rahisi sana. Fanya hivi, nunua line mpya ya simu, halafu iweke kwenye simu yako kisha tumalize kazi asubuhi hii!”

“Ni rahisi kiasi hicho?”
“Sana! Kwani anafanya biashara gani?”
“Anauza matunda.”
“Kazi inazidi kuwa nyepesi zaidi!”
“Basi ngoja nikahangaikie hiyo line!”
“Poa.”

Genesis akatoka mbio na kwenda dukani kununua line mpya, akaweka vocha na kurudi. Akiwa njiani kurudi mgahawani, simu yake ikaita. Kwenye kioo cha simu yake, jina la Bianca likatokea.
Genesis akavimba kwa hasira hakutaka kabisa kuona simu ya Bianca ikiendelea kumsumbua. Akaingalia ikiita mpaka ilipokatika yenyewe! Baada ya muda ikaanza kuita tena, safari hii akaamua kuipokea.

“Unasemaje Bianca?” Genesis aliongea akionesha kuwa na hasira.
“Acha hasira Genesis, mwanaume unayependwa lakini hupendeki!”
“Unamaanisha nini kusema hivyo?”
“Sina hata huo muda wa kukuambia kitu, lakini nataka kukueleza kwamba, kuanzia leo uwe huru, sitaki tena uhusiano wa mapenzi na wewe. Kama utapenda tuendelee kuwa marafiki wa kawaida sawa, lakini siyo mapenzi.

“Nimechoka sasa na mambo yako. Kama ni huyo Farida wako mfuate, sitaki tena kuumizwa na visa vyako vya mapenzi visivyoisha,” akasema Bianca huku akionesha huzuni.

“Hata mimi ni hivyo hivyo, kweli sina haja na wewe.”
“Sawa ni vizuri, nimechoka kuwa mtumwa wa mapenzi!”
“Siyo utumwa, ulikuwa unajipendekeza!”
“Nimegundua hilo, ndiyo maana nachukua uamuzi sahihi wa kukupa uhuru wa kuamua utakavyo!”

“Poa!” Akajibu Genesis na kukata simu.
Akachanganya miguu hadi alipomfikia Greyson. Akampatia ile line.
“Andika namba zake hapa!” Greyson akasema akimpa Genesis simu ambaye aliandika namba za Farida na kisha kumrudishia tena baada ya kuandika namba kwa usahihi.

Greyson akampigia simu Farida, simu ikaita kwa muda mrefu, kabla haijakatika, Farida akapokea.
“Habari yako Farida?” Greyson akamsalimia.
“Salama, nani mwenzangu?”
“Naitwa Salim!” Greyson akadanganya.
“Sina namba yako lakini!”

“Ni kweli, kuna mtu amenipatia namba yako. Mimi namiliki mgahawa wangu hapa Kinondoni. Nataka kukupa tenda ya kutuletea matunda ya elfu kumi kila siku, sijui upo tayari kwa hiyo ofa?”
“Sijakuelewa, naleta halafu naanza kuuza hapo mgahawani au naleta na kuondoka?”

“Kazi yako ni kuleta matunda asubuhi kisha unapatiwa pesa yako, halafu unaendelea na biashara yako!”
“Mungu wangu! Ahsante sana kaka Salim, nashukuru sana jamani, sijategemea kupata ofa kubwa kiasi hicho!” Akasema Farida akionekana mwenye furaha sana.

Kwake ilikuwa bahati kubwa, kupata tenda ya kupeleka matunda ya elfu kumi kila siku alikuwa na uhakika wa kupata faida ya shilingi elfu nne, nje ya biashara yake pale kijiweni kwake Shekilango!

“Sawa, hifadhi namba yangu, nitakupigia baadaye ili nikuelekeze tuweze kukutana ofisini kwangu!”
“Sawa kaka Salim, ahsante sana!”
“Karibu!”
Wakakata simu zao.
“Kazi imeisha!” Greyson akamwambia Genesis.

“Kivipi?”
“Niachie mimi!”
“Halafu huo mgahawa utaupataje?”
“Kaka shida yako mgahawa au Farida?”
“Namtaka Farida!”

“Basi umeshampata, tena kesho mbali sana, atakuwa mikononi mwako!”
“Kweli?”
“Huwa sikosei katika mambo ambayo naamini yapo ndani ya uwezo wangu. Mara hii umesahau kozi ninayosoma?” Akasema Greyson akiangua kicheko.

Genesis alikuwa na hamu ya kumpata tena Farida wake. Aliweka mategemeo yake yote kwa Greyson.

Je, nini kitatokea? Genesis atafanikiwa kumpata Farida? Greyson atatumia mbinu gani?
 
SEHEMU YA 23


Wazazi wa Genesis wameshamkubalia mtoto wao aendelee na uhusiano na Farida. Ni jambo la kushangaza kidogo ambalo Genesis lilimtia mashaka lakini furaha yake inakuwa ni kubwa zaidi.

Anajaribu kumfuata Farida nyumbani kwao Mtoni, Kwa Aziz-Ally, lakini mwanamke huyo anakataa kukutana naye, Genesis anaumia sana. Farida alikuwa ndiye pekee aliyeuteka moyo wake.

Aliporudi chuoni, alimwelezea rafiki yake Greyson kisa chote, naye akawa tayari kumsaidia. Tayari mikakati ya kumpata Farida imeshaanza,

Greyson amempigia simu Farida na kumpa tenda ya kumletea matunda! Haijulikani anataka kutumia mbinu gani, lakini Greyson amemhakikishia Genesis kwamba lazima atampata Farida.
Je, atatumia mbinu gani? SONGA NAYO...

“LAKINI rafiki yangu kwanini hutaki kuniambia mbinu unayotaka kuitumia?” Genesis akamwuliza Greyson.
“Nikuulize swali?”
“Uliza!”
“Umewahi kuumwa?”
“Ndiyo!”

“Pia umewahi kwenda hospitalini kutibiwa baada ya kuugua?”
“Maswali gani tena hayo?”
“Jibu tu, mwisho wake utaelewa ni kwanini nakuuliza maswali haya!”

“Hakuna mtu ambaye hajawahi kuugua na kwenda hospitalini.”
“Umejibu vizuri sana, sasa kwani huwa unamchagulia daktari dawa za kukutibu au daktari mwenyewe huamua kukutibu kwa dawa anayoiamini?”

“Daktari ndiye hutoa dawa ya kutumia.”
“Kama ndivyo, basi suala la utampata vipi Farida, niachie mimi, lakini nakuhakikishia utampata.”

Genesis hakuwa na jibu zaidi ya kucheka.
“Unacheka nini sasa?” Greyson akamwuliza Genesis.
“Huoni kuwa unachekesha sana?”
“Tuachane na hayo, leo una kipindi jioni?”
“Hapana.”

“Basi jiandae saa 10 jioni tutatakiwa kwenda Kinondoni kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kumalizana na Farida.”
“Sawa.”

Genesis alikuwa na hamu kubwa ya kumrejesha mpenzi wake mikononi mwake. Greyson alimpa matumaini, lakini yeye hakuweza kujua ni kwa namna gani angefanikiwa katika zoezi hilo.
Hata hivyo, hayo hayakuwa na umuhimu sana kwake, shida yake kubwa ilikuwa ni kumpata Farida wake tu, hilo tu ndilo lililomtatiza!
***
Saa 10:00 za jioni, Genesis alikuwa akiegesha gari nje ya mgahawa mmoja maeneo ya Kinondoni B, mgahawa huo ulikuwa na maandishi makubwa mlangoni yaliyosomeka Burudika Cafe.

Greyson akashuka na kumwacha Genesis ndani ya gari, aliingia ndani ya mgahawa ule na kukaa humo kwa muda wa nusu saa, alipotoka alikuwa anatabasamu.
“Vipi kaka?”

“Mambo yanakwenda poa!”
“Poa?!”
“Ndiyo kila kitu kipo sawa, acha nimpigie Farida.”
“Poa.”
Greyson akatoa ile simu yenye line mpya na kumpigia Farida ambaye alipokea haraka sana alipoona jina la Salim kwenye simu yake.

“Habari ya muda huu Farida?”
“Salama kaka Salim!”
“Naona muda umekwenda sana, lakini si neno, si lazima sana tukutane leo, cha msingi kesho asubuhi saa tatu lete hayo matunda!”

“Umesema mgahawa wako unaitwaje?”
“Burudika Cafe hapa Kinondoni B, ni barabarani kabisa. Si rahisi kupotea. Ukishuka kituoni, muulize mtu yeyote atakuonesha hapa!”
“Sawa ahsante sana kaka Salim!”
“Usijali!”

“Nilete matunda gani?”
“Kwa kuanzia, kesho lete ndizi mbivu.”
“Sawa.”
Wakakata simu zao.
Greyson akamhakikishia Genesis kwamba kila kitu lazima kitakuwa sawa.
“Kweli?”

“Niamini mimi, mbinu ninayoitumia ni ya kipekee. Kesho akileta hayo matunda yake, nitamalizana naye na wewe utakuwa naye kuanzia kesho.”
“Unadhani ni rahisi kiasi hicho?”
“Kaka wanawake wanajua kupima mapenzi, kwanza akijua kama umetumia mbinu zote hizi kwa ajili ya kumpata yeye atajisikia vizuri sana, atazidi kukupenda kwa sababu unavyomhangaikia!”
“Tutaona.”

“Amini kuwa inawezekana ndugu yangu!”
“Poa.”
Kilichofuata ilikuwa ni kuwasha gari na kurudi zao chuoni, kidogo Genesis alikuwa na amani, maana dalili za kumpata Farida wake zilianza kuonekana.
***

Farida hakuwahi kuwa na furaha tangu alipoanza biashara yake ya kuuza matunda kama siku hiyo. Aliona kama amepata bahati ya ajabu, tenda ya kupeleka matunda kwenye mgahawa halafu aendelee na biashara yake kijiweni kwake, ilikuwa kubwa sana.

Alipofika nyumbani kwao, alihakikisha anafanya usafi vizuri wa nyumba nzima, kisha akaoga na kumfuata mama yake gengeni anapouza chakula.

“Vipi mwanangu?”
“Nimekuja kukusaidia mama yangu!”
“Hapana binti yangu, kutwa nzima umeshinda kwenye jua, najua ni kiasi gani utakuwa umechoka, nenda kajipumzishe nyumbani.”

“Usijali mama, kwanza leo nina furaha isiyo na kifani, kwahiyo nina haki ya kukusaidia kazi, kama njia mojawapo ya kuonesha furaha yangu!”

“Furaha ya nini tena mwanangu? Umeokota pesa?” Mama yake akamwuliza huku akicheka.
“Hapana.”

“Umeitwa chuoni?”
“Hapana mama, bado sijapata chuo kama unavyojua tena, ilivyo vigumu!”
“Sasa ni nini?”

“Haraka ya nini mama? Si bado tupo? Utajua tu, wala usijali mama, nitakuambia!”

“Usije kuniambia kuhusu huyo bwana wako, sijui Genesis ?”
“Hapana... siyo hilo, mi’ nitakwambia tu mama.”
“Haya sawa!”

Siku hiyo Farida alimsaidia mama yake kazi akiwa mwenye uso wa tabasamu muda wote, aliwachangamkia wateja vizuri kiasi mama yake alifurahia sana hali hiyo. Kichwani mwa mama yake, alijua huenda mwanaye alipata mwanaume mwingine wa kumuoa!

Hakuwaza juu ya kitu chochote zaidi ya hicho, mawazo hayo yalikuwa mbali sana na ukweli wenyewe, ingawa kwa upande wa pili yalikuwa yanaukaribia ukweli. Waliendelea na bishara hadi muda wa kufunga ulipofika, wakabeba vyombo na kurudi nyumbani.
“Haya sasa niambie, maana umeniweka roho juu mama yako kwa muda wote huo!”

“Mama nimepata tenda ya kupeleka matunda kwenye mgahawa. Kila siku nitakuwa napeleka ya shilingi elfu kumi. Cha kufurahisha zaidi, napeleka na kuondoka kwenda zangu kijiweni. Kwa maneno mengine nitakuwa napata kipato mara mbili!” Akasema Farida akitabasamu.

“Hongera sana mwanangu, Mungu amesikia kilio chako mama. Lazima umshukuru sana, kuwa makini na hakikisha unatunza pesa zako!”
“Kwa hilo mama usijali!”

Furaha ya Farida, kwa mama yake ilikuwa mara mbili yake. Wote wakafurahia sana ofa hiyo kwa pamoja.
***

Tangu saa 2:30 za asubuhi, Genesis na Greyson walikuwa wameshafika Burudika Cafe, walikaa sehemu tofauti, Genesis akakaa meza ya kwanza kutokea kaunta na kuupa mgongo mlango wa kuingia na Greyson akakaa meza ya kwanza kabisa mlangoni.

Walifanya hivyo ili wakati Farida anaingia asimuone Genesis. Muda mfupi baadaye, simu ya Greyson ikaita, alipoangalia kwenye kioo cha simu yake, akakutana na jina la Farida.
“Nimeshafika, nipo hapa nje!”

“Ingia ndani, meza ya kwanza kushoto kwako, ndiyo nimekaa.”
“Sawa.”

Farida akaingia akiwa na mfuko wenye ndizi, kwa maelezo aliyopewa, Greyson aliweza kumuona alipokuwa akiingia. Moyo wa Greyson ulipuka sana baada ya kumuona Farida. Alikuwa mwanamke mrembo kuliko kawaida.

“Nipo hapa, karibu!” Akamkaribisha Greyson, akiendelea kumkagua Farida.

“Ahsante sana!” Sauti laini ya Farida ikasikika wakati akikaa.
“Genesis ana haki ya kuchanganyikiwa juu ya huyu mtoto, ni mzuri sana!” Akawaza Greyson akimwangalia usoni Farida.

“Sina shaka ndani ya huu mfuko kuna hayo matunda!”
“Ndiyo!”
Bila kupoteza muda Greyson akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti moja ya shilingi elfu kumi, kisha akampatia.

“Nashukuru sana kaka Salim, kesho utapenda nilete matunda gani?” Farida akasema akionekana kutaka kuinuka.

“Mbona una haraka sana Farida?”
“Natakiwa kurudi tena sokoni kwa ajili ya kuchukua mzigo mwingine nielekee kijiweni!”
“Sawa, lakini kuna jambo lingine zaidi lililosababisha nikuite hapa!”

“Jambo lingine?”
“Ndiyo!”
“Jambo gani?”
“Usijali nitakuambia...kwanza nataka kukutoa wasiwasi, usije ukanifikiria vibaya na wala sina nia mbaya na wewe!”
“Unamaanisha nini?”

“Inawezekana labda unadhani nataka kukutongoza au kukuvunjia heshima, mimi siyo mwanaume wa aina hiyo, lakini nataka kuzungumza kidogo na wewe kuhusu maisha yako!”
“Kuhusu maisha yangu kivipi? Kwani unanifahamu?”
“Ndiyo, tena nakufahamu vizuri sana.”

“Unanifahamu vipi?”
“Unaishi Mtoni, Kwa Aziz-Ally, ulikuwa unasoma Kilakala Girls lakini baadaye ukahamia St. Thomas uliposoma hadi kidato cha sita. Ukiwa hapo shuleni ulikuwa na uhusiano na kijana mmoja anayeitwa Genesis ambaye kwa sasa anasoma Mlimani...” akasema Greyson akimwangalia Farida usoni.

“Kwani wewe ni nani? Na umejuaje habari zangu, halafu kwanini umeniambia haya yote?” Farida akauliza akionesha kupigwa na mshangao mkubwa usoni pake.

ALIENDELEA kumkazia macho akiwa hamuelewi kabisa Greyson ambaye alijitambulisha kwake kwa jina la Salim. Hakuwahi kumuona mahali popote, lakini vipi ajue mambo yake kiasi kile?

Hilo lilikuwa swali ambalo lilizunguka kichwani mwake bila kupata majibu yakinifu. Greyson alikuwa amemtonesha kidonda, alikuwa amemkumbusha machungu ambayo alishaanza kuyasahau kabisa!

Moyo wa Farida ulikuwa ukichuruzika damu, ukiwa na maumivu makali,ulikuwa ni wakati wa kumsahau kabisa Genesis, hakutaka kutumia muda wake kujaribu kumkumbuka, kwake alikuwa mwanaume mbaya na zaidi ya shetani!

Aliharibu maisha yake na kumfanya awe mtu wa kulia kila wakati. Hakupenda kabisa kusikia jina la Genesis. Anazidi kumkazia macho Greyson huku midomo yake ikitingishika.
“Nimekuuliza lakini hujanijibu kaka Salim?” Akasema Farida akitetemeka.

“Usijali utanijua tu, kwanza kabisa mimi siitwi Salim kama nilivyokuambia awali, jina langu ni Greyson. Mwanaume ninayependa maisha yako ndiyo maana nayajua yote haya.

“Kuna mtu anaweza kubadilisha maisha yako, akayafuta machozi yako na kukufanya uwe mwenye furaha siku zote. Najua huwaamini tena wanaume, lakini huyu ninayemzungumzia, atakuwa mkweli kwako!”

Farida akashtuka sana!
“Mwanaume?” Akauliza kwa taharuki.
Hakuelewa alichokuwa anamaanisha Greyson.
“Ndiyo mwanaume. Yupo mwanaume mwema kwako, ambaye atakufuta machozi yako!”

“Unamaanisha nini?”
“Najua kwamba Genesis alikuumiza na kukutesa sana, alikuharibia mipango yako na ni yeye ndiye chanzo cha wewe kufeli, lakini yupo mtu ambaye anaweza kurekebisha yote hayo na ukayasahau kabisa!”

Yalikuwa maneno mazito sana kwa Farida, ambayo yaligoma kabisa kuingia kichwani mwake. Hakuwaamini kabisa wanaume, alishindwa kuelewa ni mwanaume gani huyo ambaye angeweza kuyafuta machungu yake, hasira zake na maumivu yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.

Haikuwa rahisi kwake kusema chochote, akabaki kimya akimwangalia machoni, akiwa hana la kuzungumza kabisa.

“Mbona upo kimya Farida? Au hujapenda? Nina nia njema sana na maisha yako kama nilivyokuambia awali na ninakuhakikishia utafurahi na maumivu yote yatafutika kabisa. Niamini mimi!”
“Greyson umesema?!”

“Ndiyo naitwa Greyson!”
“Kwanza ni kwanini ulinidanganya jina lako?”
“Sikuwa na nia mbaya juu ya hilo, ndiyo maana nilipokutana na wewe nimekueleza ukweli!”

“Ok! Hebu niambie, huyo mwanaume unayemzungumzia hapa ni nani? Maana nashindwa kabisa kukuelewa!”
“Utanielewa tu na ninaamini utampenda sana!”
“Ni nani na yuko wapi?”
“NI GENESIS!”

“Genesis tena?” Farida akahamaki.
“Ndiyo Genesis...ni mtu mpya, nataka kukuambia kitu kimoja ambacho ulikuwa hukijui. Genesis anakupenda sana, sasa ameachana na Bianca na wazazi wake wamekubali awe na wewe!”

Maneno hayo yalikuwa makali sana kutoka kwa Greyson na moja kwa moja yaliingia katikati ya moyo wa Farida na kumchoma. Pale pale, akashindwa kujizuia, hasira zake zikaanza kuyeyuka taratibu, akajikuta akiwa na kiu ya ghafla ya kumrejesha tena Genesis moyoni mwake.

“Kweli?” Farida akauliza akiwa ameyatoa macho yake.
“Niamini!”
“Unanihakikishia kwamba sitaumia tena?”
“Nakuhakikishia!”
“Sitalia tena?”

“Nakuhakikishia!”
“Sitateseka tena?”
“Hilo halitatokea!”

“Nipe muda wa kufikiria zaidi kuhusu hili Greyson, lazima nitulize kichwa kwanza!”
“Hapana, mapenzi hayafikiriwi, najua hata wewe unatambua kwamba moyo wako upo tayari kuwa na Genesis, unachelewa nini?” Akasema Greyson kisha akageuka nyuma na kumuita Genesis...

“Genesis...njooo...” kilikuwa kitendo cha sekunde tano tu, Genesis alikuwa amesimama mbele ya Farida.

Farida hakuamini macho yake. Genesis hakujali macho ya watu, pale pale kwenye ule mgahawa, akapiga magoti chini huku akilia, Farida akashindwa kuvumilia, naye akajikuta akianza kulia kwa uchungu uliochanganyikana na furaha.

“Nisamehe Farida wangu, nakupenda mama, sitakuumiza tena, nipe nafasi nyingine mpenzi wangu, nakupenda sana Farida. Nataka kukuhakikishia kwamba, safari hii penzi letu litakuwa ni la milele.

“Siwezi kubadilika tena, isitoshe wazazi wangu wameshakubali mimi niwe na wewe na niachane na Bianca. Wameamua kukubaliana na hisia zangu. Tafadhali usiseme hapana mpenzi wangu!” Genesis akasema uso wake ukiwa umechakazwa na machozi.

Farida akainuka na kumshika mikono Genesis, kisha akamwonesha ishara asimame, alipofanya hivyo, akamvuta karibu yake na kumkumbatia. Watu wote ndani ya mgahawa wakaacha kila walichokuwa wakikifanya na kuyaelekeza macho yao kwa Farida na Genesis.

“Nakupenda sana Genesis!”
“Nakupenda pia Farida!”
“Tafadhali usinitese tena, nipe nafasi kikamilifu ndani ya moyo wako!”

“Usijali mama, wewe ndiye malkia wangu, sina mwingine zaidi yako!”
“Ahsante sana mpenzi wangu, nimefurahi sana!”

Walikumbatiana kwa dakika kadhaa, huku wote wakishindwa kabisa kuzuia machozi yao. Hawakujali macho ya watu, ndani ya mioyo yao kulikuwa na hisia kali za mapenzi ambazo zilikuwa vigumu sana kuzizuia!

Baadaye wakaondoka pamoja na kwenda kuingia kwenye gari. Genesis akawasha gari, Farida akiwa amekaa upande wa abiria.
“Tunaenda wapi?” Farida akauliza.
“Kwanza nataka tukafanye shopping halafu mambo mengine yatafuata!”

“Kwa jinsi nilivyo?”
“Kwani ukoje?”
“Ah! Hapana bwana, sipo sawa, siwezi kutoka na nyie!”

“Usijali mimi nipo huru kwenda na wewe popote pale kwa namna yoyote utakayokuwa, mimi nakupenda Farida kama ulivyo.”
“Najua mpenzi, lakini lazima niende kijiweni!”
“Achana na mambo ya kijiweni kwako tena, nitakutafutia kitu cha kufanya!”

“Sawa, lakini kwa leo naomba nirudi nyumbani kwanza, tukutane Jumamosi!”
“Haya bwana, kama ndiyo umeamua, lakini sasa naomba nikurudishe nyumbani.”

“Sawa.”
Genesis akaondoa gari, wakielekea Mtoni Kwa Aziz-Ally. Hakumfikisha mpaka nyumbani kabisa, waliishia barabarani. Farida akashuka akiwa na furaha sana, wakaagana na Genesis akageuza gari kurudi zake chuoni.

“Kaka wewe ni noma, ahsante sana ndugu yangu, umenisaidia sana!” Genesis alisema akionekana kuwa mwenye furaha sana.

“Lakini nilikuhakikishia kwamba hili suala ni dogo sana kwangu!”
“Nimekubali, sasa kaka nitachana sana darasani, sina mawazo ya Farida tena, ila nina zawadi yako, utaipenda!”
“Poa kaka.”

***
“Lakini na wewe una akili sana, umetumia mbinu kali sana kunipata!” Alikuwa ni Farida akimwambia Genesis, wakiwa kwenye bustani, nyumbani kwao Masaki.

“Kwa sababu nakupenda, ilikuwa lazima nitafute mbinu yoyote kuhakikisha unarudi mikononi mwangu!”
“Lakini hivi mama yako akitokea hapa itakuwaje?” Farida akauliza akionekana kuogopa.

“Itakuwaje kivipi wakati wazazi wangu wote wameshaniruhusu mimi kuwa na wewe? Jaribu kujiamini, hakuna kitakachotokea, hapa ni kwako!” Genesis akasema kwa kujiamini.

“Haya bwana!” Farida akasema akionekana kukata tamaa.
Punde kidogo, wakasikia honi getini, wote wakanyamaza kimya. Mlinzi alipofungua mlango, gari la mama yake Genesis liliingia. Farida akakumbwa na hofu.

“Mungu wangu, sijui itakuwaje?”
“Usiwe na wasiwasi, nimeshakuambia mama hana tatizo na wewe!”
Mama Genesis akaendesha gari hadi kwenye maegesho kisha akashuka na kuanza kupiga hatua za taratibu kuelekea pale bustanini. Uso wake ulionekana tofauti kabisa na matarajio ya Farida.

Uso wake ulikuwa ang’avu, alionekana kuwa na furaha na tabasamu pana likichanua. Wote kwa pamoja wakasimama na kumsalimia.
“Marahaba wanangu! Vipi mbona mpo nje?” Mama Genesis akaitikia salama na kuwauliza.

“Tupo hapa tunapunga upepo!” Genesis akajibu.
“Hapana...Farida mwanangu hapa ni kwako, hebu twende ndani mwanangu. Naomba usahau yote yaliyopita, hapa sasa ni kwako, sisi tupo radhi na uhusiano wenu!” Akasema mama Genesis akimshika mkono Farida.

Moyo wa Farida, ulizizima kwa furaha, haikuwa rahisi kuamini kilikuchokuwa kikiendelea. Akatabasamu na kumwangalia Genesis.
“Ahsante sana mama, nampenda sana Genesis!” Akasema Farida.

“Vizuri sana, nisingependa mpendane pekee, nataka kuona mnafunga ndoa, sawa?” Mama Genesis akasema.
“Sawa mama!”

Kila kilichotokea, kilikuwa sawa na ndoto, lakini haikuwa hivyo, kila kitu kilikuwa kweli. Farida, Genesis na mama yake wakaingia sebuleni.

Je, nini kitatokea? Ni kweli mama Genesis ameamua kuwaacha vijana hao waoane au kuna kitu nyuma ya pazia?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom