Kesi ya akina Mramba yakwama tena
Imeandikwa na Regina Kumba; Tarehe: 18th April 2011 @ 23:20 Imesomwa na watu: 48; Jumla ya maoni: 0
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imezidi kukwamisha kesi inayomkabili waziri wa zamani wa fedha, Basil Mramba, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja.
Kesi hiyo iliahirishwa kwa mara nyingine katika mahakama hiyo na Hakimu Mfawidhi, Ilvin Mgeta, baada ya kusema mwenendo wa kesi hiyo haujawa tayari kwa ajili ya kupewa mawakili wa pande zote mbili, ili kujiandaa kuwasilisha majumuisho.
Hakimu Mgeta alisema mwenendo huo uko katika hatua ya mapitio na hivyo kupanga kesi hiyo kuja kuangalia kama itakuwa tayari Mei 6 mwaka huu.
Mara ya mwisho kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mustapher Siyani, akisema mahakama imekwama kuchapisha mwenendo wa kesi hiyo, kutokana na tatizo la umeme linaloendelea, alisema pamoja na tatizo hilo, mahakama inafanya jitihada kuhakikisha unakamilika.
Kesi hiyo ni ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara Serikali.
Wanatuhumiwa wanadaiwa kuisamehe kodi kinyume cha sheria, kampuni ya M/S Alex Stewart Government Business Corporation na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.
Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 na wako nje kwa dhamana.