Kesi ya kina Mungai yapigwa tena kalenda

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,112
Mungai%283%29.jpg

Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai



Kesi ya kutoa hongo katika mchakato wa kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai, imeahirishwa tena na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Iringa.
Kesi hiyo ilitajwa tena Mahakamani hapo Septemba 25, mwaka huu.
Mungai (66) na makada wengine wawili ambao ni Katibu wa Umoja wa vijana wa CCM wa Wilaya ya Mufindi, Fidel Cholela (39) na Moses Masasi wanakabiliwa na mashtaka 15 ya rushwa kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 na sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.
Watuhumiwa hao kwa pamoja, kwa mara ya kwanza walipandishwa kizimbani Agosti 11, mwaka huu na kusomewa mashtaka hayo na kuyakana. Mwendesha mashitaka wa Takukuru, Imani Nitume, alisema mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza pingamizi la awali la kisheria kutoka upande wa utetezi lakini hakimu anayesikiliza shauri hilo, Marry Senapee, ni mgonjwa hivyo wanaomba siku nyingine.
Upande wa utetezi unaoongozwa na mawakili Alex Mgongolwa wa Excellent Attorneys na Basil Mkwata wa Mkwata Law Chambers, hawakuwa na pingamizi na maelezo hayo, lakini wakaomba kesi hiyo irejee mahakamani hapo Oktoba 15, kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hilo la awali la kisheria.
Pande zote mbili zilikubaliana ambapo Hakimu Mkazi wa Mkoa aliyeendesha kesi hiyo kwa muda, Gladies Bath, alisema shauri hilo litarejea mahakamani Oktoba 15, mwaka huu, kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hilo huku akisema dhamana na masharti yake yanaendelea kama yalivyo.
Inadaiwa kuwa Julai 08, mwaka huu, katika kata ya Ihalimba, Wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombea ubunge Mufindi Kaskazini, walitoa hongo ya Sh. 10,000 kwa Mwenyekiti wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa zoezi la upigaji wa kura za maoni.
Katika shtaka la pili, inadaiwa kuwa siku na katika eneo hilo walitoa hongo ya Sh. 10,000 kwa Konjesta Kiyeyeu ambaye alihudhuria kikao cha kamati ya CCM Kijiji cha Vikula.
Katika shtaka la tatu, nne, tano na sita, wanadaiwa kutoa hongo ya Sh. 10,000 kwa Aldo Lugusi, Ezekiel Mhewa, Tulaigwa Kisinda na Jiston Mhagama kwa lengo hilo.
Katika shitaka la saba, wanadaiwa kutoa hongo ya Sh. 20,000 kwa Maria Kihongosi na shtaka la nane kutoa Sh. 5,000 kwa Lurent Mdalingwa wakati shtaka la tisa wanadaiwa kutoa hongo ya Sh. 20,000 kwa Victory Kalinga ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kijiji cha Ugessa.
Katika mashtaka namba kumi hadi 12 washtakiwa wote wanadaiwa walitoa hongo ya Sh. 2,000 kwa Francis Chonya, Alfred Kisinga na Issac Tewele wakati shtaka la 13 wanadaiwa walitoa Sh.10,000 kwa Sosten Kigahe.
Katika shitaka namba 14 wanadaiwa kutoa Sh. 10,000 kwa Raphael Lutumo na shitaka la mwisho walitoa hongo ya Sh. 20,000 kwa Andrew Mkiwa.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom