Kesi dhidi ya JamiiForums (Kuhusu CRDB): Shahidi kutoka Makao Makuu ya Polisi Kitengo cha Upelelezi Mtandaoni ahojiwa

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,981
Kesi namba 458 ya Jamhuri vs Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media na mwanahisa wa kampuni hiyo inayohusu kuendesha mtandao (JamiiForums.com) bila kutumia Kikoa cha do.TZ na Kuzuia Upelelezi wa Polisi iliendelea Novemba 07, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu.

NOTE: Kabla ya kuhamia shtaka la pili, shahidi wa mwisho kwenye shtaka la kwanza alihojiwa hivi - Kesi namba 458 ya JamiiForums kutosajiliwa TZ yaendelea. Yapigwa tena kalenda

Itakumbukwa kuwa katika kosa la kuzuia upelelezi, Jamhuri inawashtaki Watuhumiwa kwa kutotoa ushirikiano kwa Polisi walipoambiwa watoe taarifa muhimu za Watumiaji wa mtandao wa JamiiForums waliandika kuhusu Benki ya CRDB (Ref: Kesi dhidi ya JamiiForums(Namba 458): Jamhuri yahamia shtaka la pili. Ni kuhusu Benki ya CRDB)

Taarifa za Wanachama ambazo zilitakiwa kutolewa ni IP-Address, barua pepe, Majina Halisi ya Wanachama hao. Pia ilitakiwa zitolewe post zote zinazohusu Uhalifu unaofanyika katika benki ya CRDB.

Taarifa zilizotakiwa ni za Wanachama walioanzisha mijadala inayosomeka "Charles Kimei (CRDB) jiuzulu, kashfa ya kontena, tiketi TFF, Wanafunzi na ujambazi CRDB" mjadala unaodaiwa kuanzishwa tarehe 18 Januari 2016 pamoja na "Wizi wa Benki ya CRDB part II" unaodaiwa kuanzishwa Machi 11, 2015

Siku ya leo, upande wa Jamhuri umewakilishwa na Wakili Mwandamizi Nassoro Katuga huku upande wa Utetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala kwa kushirikiana na Wakili Jeremiah Mtobesya na Wakili Jebra Kambole mbele ya Hakimu Huruma Shaidi.

Upande wa Jamhuri ulikuja na Shahidi wao mmoja ambaye ni Inspekta wa Polisi kitengo cha Upelelezi kilichopo Makao Makuu ya Polisi jijini Dar, Beatrice Majule.

*****
Shauri hilo liliendelea kama ifuatavyo;

Hakimu Huruma Shaidi anamtaka Inspekta Beatrice Majule aape na kujieleza majina yake na dini, ambapo Inspekta Beatrice anasema yeye ni Mkristo mwenye miaka 37 na kuahidi kusema ukweli mtupu.

Baada ya hapo Hakimu anamuruhusu Wakili wa Jamhuri kumuongoza Shahidi wake kwa maswali aliyoyaandaa.

Wakili Katuga: Shahidi unafanya kazi wapi?

Shahidi: Nafanya kazi Makao Makuu ya Polisi (HQ) kama Mpelelezi Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni.

Wakili Katuga: Upo tangu lini na majukumu yako ni yapi?

Shahidi: Nipo tangu 2015 na majukumu yangu ni kufuatilia upelelezi katika makosa ya kimtandao

Wakili Katuga: Hebu tuambie, unajua nini kuhusu jalada lenye kumbukumbu namba CID/HQ/05/2016

Shahidi: Ni jalada la uchunguzi lililofunguliwa baada ya muongozo kutoka kwa Afande DCI Diwani Athumani kuhusu malalamiko kutoka benki ya CRDB kwamba wamechafuliwa katika mtandao wa JamiiForum kuwa benki yao inashirikiana na majambazi kuibia wateja.

Wakili Katuga: Enhe! Baada ya taarifa hiyo uliambiwa ufanye nini?

Shahidi: Niliambiwa nifuatilie kwenye mtandao wa JamiiForum.

Nilianza kufanya ufuatiliaji kwenye mtandao huo mnamo tarehe 20/01/2016. Niliingia kwenye mtandao wa JamiiForum. Kwa kuwa alikuwa amenipa akaunti mbili ambazo zilipost hizo taarifa, akaunti hizo ni RB Expert Member na Sawana Expert Member.

Wakili Katuga:
Akaunti za nini hizi? Unasema akaunti, akaunti!

Shahidi: Ni za wanachama wa JamiiForum (akimaanisha JamiiForums).

Wakili Katuga: Okay, baada ya kuziona hizo akaunti ulifanya nini na kuona nini?

Shahidi: Nilifungua hizo akaunti……(Samahani Mheshimiwa, naruhusiwa kujikumbusha?)

*****
Hakimu Shaidi anamruhusu Shaidi kujikumbusha, lakini Wakili Kibatala anatoa hoja kuhusu suala hilo

Wakili Kibatala: Mheshimiwa, tunaruhusiwa kuona na sisi anachojikumbusha?

Hakimu Shaidi: Sawa

Wakili Kibatala: Mheshimiwa Hakimu kilichopo humu (kwenye kijikaratasi alichokuwa ameshika mkononi shahidi) ni ushahidi sio kujikumbusha sasa, tunajua ana haki ya kujikumbusha ila huu ni ushahidi

*****
Shahidi anaendelea sasa;

Shahidi: Ninaweza kukumbuka (bila kutumia kijikaratasi) ila sio sawa na ilivyoandikwa, nakumbuka "Kimei jiuzulu", "Ujambazi CRDB", nyingine "Wizi wa benki CRDB part II"

Wakili Katuga: Hizi zote ni headings?

Shahidi: Ndio, zilipostiwa na hizo akaunti mbili. Humo nilivyosoma ndio wameelezea kuwa CRDB inashirikiana na majambazi kuibia wateja wao. Pia, wanashirikiana na TPA na TRA na kusababisha hasara kubwa.

Wakili Katuga: Hasara kubwa maana yake nini?

Shahidi: Iliishia hivyo tu. Na nyingine ilikuwa inasema “CRDB Benki inakatisha tiketi za kieletroniki na kusababisha hasara kubwa”. Na nyingine, “CRDB imefungua tawi Burundi”

Wakili Katuga: Baada ya kuziona ulifanya nini?

Shahidi: Niliandika Barua kwenda JamiiForum mnamo tarehe 26/01/2016

Wakili Katuga: Uliandika barua ulikuwa unafahamu ofisi zilipo au nini?

Shahidi: Nilikuwa na namba ya simu ya Maxence Melo. Niliandika barua ili aweze kutupa taarifa muhimu, kama namba za simu za wateja wao, ambao ni RB na Sawana

Wakili Katuga:
Ulikuwa unataka taarifa za wateja kwa ajili ya nini?

Shahidi: Kuwahoji, kujua hizo taarifa wamezipata wapi na watupe ukweli ili tuweze kuendelea na upelelezi

Wakili Katuga: Uliwaandikia barua JamiiForum, kwanini ulikuwa na namba ya Maxence Melo?

Shahidi: Kwa kuwa nilikuwa najua yeye ni Mkurugenzi wa hiyo media

Wakili Katuga: Baada ya kuandika barua?

Shahidi: Niliwasiliana na Maxence Melo ili atuelekeze ofisi zao zilipo siku hiyo hiyo ya tarehe 26 ili tuweze kupeleka barua

Wakili Katuga: Ulimpata?

Shahidi: Aliniambia kama mna barua zetu kuna mtu anakuja kuchukua

Wakili Katuga: Ulikuwa ukifahamiana naye kabla(Maxence Melo) maana unasema ulikuwa na namba zake?

Shahidi: Ndio, maana alikuwa akija pale ofisini. Baada ya muda mfupi baada ya kuwasiliana naye alikuja mtu anaitwa Muganyizi, pale ofisini Makao Makuu ndio nikamkabidhi hiyo barua

Wakili Katuga: Huyu Muganyizi alijitambulisha kama nani?

Shahidi: Nilimuuliza Maxence akasema ni Mwanasheria wake

Wakili Katuga: Unaposema umeandaa barua, utaratibu wa barua kutoka nje unakuwaje?

Shahidi: Lazima kiongozi wangu aipitie na kuisaini baada ya hapo ndio inaenda sehemu husika. Lakini anayeiandaa ni mimi mpelelezi

Wakili Katuga: Unakumbuka nani aliisaini?

Shahidi: Alisaini Afande Joshua Mwangasa, nahisi

Wakili Katuga: Ukiiona barua utaikumba?

Shahidi: Ndio. Kwanza ina tarehe 26/01/2016 na kumbukumbu namba CID/HQ/PE/05/2016 na tulihitaji taarifa za memba, RB Expert Member na Sawana. Tuliomba watupe namba zao za simu, barua pepe taarifa ambazo zingetusaidia kuwapata

*****
Wakili Katuga anamuonesha hiyo barua na Shahidi anaitambua. Kisha Shahidi anaomba barua hiyo ipokelewe kama kielelezo Mahakamani

Wakili Kibatala: (Anaiangalia barua ile kwanza) Kwa upande wetu Mheshiwa hatuna pingamizi

Wakili Katuga: Shahidi tunaomba usome tujue kilichomo kwenye hii barua

Shahidi anaisoma. Katika hiyo waliomba, barua pepa, mada zote walizoweka kuhusu CRDB, Majina halisi ya memba hao na IP-Address zao

*****
Wakili Katuga: Baada ya kupokelewa kwa barua nini kiliendelea?

Shahidi: Majira ya mchana (siku hiyo hiyo) tulipata majibu yaliyokuja kwa njia ya barua. Barua ya tarehe 26/01/2016. Barua iliyotoka kwa Mwanasheria wa Jamii Media

Wakili Katuga: Nani alipokea majibu hayo na yaliwahi kufika kwako?

Shahidi: Ndio yalifika kwangu na yalipokelewa Masijala

Wakili Katuga: Ukiona hiyo barua ni kitu gani kitakachokufanya ukumbuke kuwa ndio hiyo?

Shahidi: Walirejea barua yetu na wakatujibu kuwa "Tunatambua sheria za nchi" hivyo wakataka “kujua jinai iliyopo kwa wateja wao na mlalamikaji ni nani”

*****
Shahidi anapewa barua ambayo inadaiwa ni majibu ya Jamii Media na kusema ni yenyewe na kuomba Mahakama iipokee kama ushahidi

Wakili Kibatala anaipitia barua hiyo na kusema hakuna pingamizi kwenye hilo pia

*****
Wakili Katuga: Baada ya kupokea hayo majibu. Je, vipi kuhusiana na majibu yako na vile ulivyokuwa unavitaka?

Shahidi: Tulichokitaka hakikupatikana ila niliwajulisha viongozi wangu kuhusu majibu hayo. Nilimjulisha Afande Mwangasa na DCI Diwani.

Wakili Katuga: Mpaka wewe ulipoomba hizo taarifa hebu eleza Mahakama jinai ilikuwa nini?

Shahidi: Mnamo tarehe 04/02/2016 tuliandika barua ya kujibu kuwa hakuna jinai na hili ni jalada la uchunguzi

Wakili Katuga: Ukiiona hiyo barua mliyoandika, utaitambua?

Shahidi: Ndio. Nitakumbuka kumbukumbu ya jalada lenyewe na tarehe ambayo ni 04/02/2016 na kuwa ilikuwa inajibu barua ya JamiiForum

*****
Shahidi anapewa inayodaiwa kuwa ndio barua hiyo ambayo ilijibu barua ya JamiiForum na kusema anaikumbuka na anaomba Mahakama itumie kama kielelezo

Wakili Kibatala: Mheshiwa Hakimu, pamoja kuwa tunataka kesi iende haraka ila kwa hili hatuna budi kupinga. Barua hii ni nakala(Photocopy) na Wakili wa Serikali hakurejea chochote kuhusu hilo wala hakuweka ‘ground work’ kuhusu nakala hiyo. Aidha, si shahidi wala Wakili wake aliyetimiza matakwa ya kielelezo hicho kupokelewa kisheria kama ilivyo katika kifungu cha 67 (Cha CPA)

Wakili Katuga: Nimesikiliza upande wa utetezi na ni kweli barua hii ni nakala na Mheshimiwa Hakimu awali kama Mahakama itakumbuka tuliwahi kutoa ‘notice’ mnamo tarehe 25/10/2018 na Mheshimiwa tuli-file notice to produce chini ya kifungu cha 68 na ukisoma ‘notice’ hiyo inasema ‘further notice to fail to produce original so Government shall use secondary evidence(Photocopy)’

Na tulivyoileta kwa kipindi hicho upande wa utetezi haukusema chochote

Wakili Kibatala: Mheshimiwa, Mimi nilidhani wakati anamuongoza shahidi wake angemuuliza mwishoni original iko wapi? Maana hawa ndio wanao-prosecute na hiyo ina maana yake. Haiwezekani wakawa na barua mbili wanazodai wao kuwaandikia hao JamiiForum Media lakini moja wanatoa kopi na kwa upande mwingine wanatoa original! Halafu, vile vile Mheshimiwa hakuna mtu anaweza kuwazuia ku-file notice

Hakimu Shaidi: Wakili wa Serikali naona ali-relax baada ya kuona kuwa mlikubali awali. Hakujua kama siku na mawazo yanabadilika. Hivyo Wakili Katuga unatakiwa kutengeneza msingi wa nakala hiyo (laying foundation). Haya tuendelee!

*****
Wakili Katuga anamwambia Shahidi aendelee (wanajenga msingi);

Shahidi: Baada ya barua ya pili nilimpigia simu Maxence kuwa kuna barua yao na alinambia kuwa kuna Mwanasheria wake alikuwa maeneo ya pale ofisini, anaitwa Benedict(nadhani walikuwa na kikao cha Wanasheria pale ofisini). Mwanasheria huyo nilimkabidhi kwa dispatch

Wakili Katuga: Dispatch ni nini?

Shahidi: Kitabu kinachohusika kukabidhi barua zinazotoka nje ya ofisi

Wakili Katuga: Ukiona hiyo barua uliyokabidhi kwa dispatch na kuiona dispatch utaitambua?

Shahidi: Ndio nitavijua vyote

******
Anakabidhiwa dispatch na kuomba Mahakama iitumie kama kielelezo. Aidha, Wakili Kibatala anakubali dispatch hiyo ipokelewe na hakuna pingamizi

******
Wakili Katuga: Hebu iambie Mahakama, mnapoandika barua kutoka nje vipi kuhusu kumbukumbuku zenu?

Shahidi: Zinakuwepo nakala tatu za barua na zote zinasainiwa

Wakili Katuga: Huko barua inapotakiwa kwenda, mnapeleka nakala ngapi?

Shahidi: Nakala moja tu

Wakili Katuga: Ieleze Mahakama, baada ya kukabidhi barua ya 04/02/2016 kwa dispatch….

Shahidi: Tunabaki na nakala moja kwenye jalada la upelelezi na nyingine kwenye jalada la ofisi

Wakili Katuga: Nini kinatokea kwa hizo nakala nyingine mbili mlizobaki nazo?

Shahidi: Ya kwenye jalada la upepelezi ilipelekwa kwa ZCO na ya kwenye jalada la ofisi haikuwepo hivyo tukabaki na kopi. Ile iliyoenda kwa ZCO niliifuatilia lakini na wenyewe kule wakawa hawaioni walibakiwa na kopi tu.

Wakili Katuga: Sasa unaiomba nini Mahakama kuhusiana na kopi (nakala) hiyo?

Shahidi: Naomba itumike kama ushahidi

******
Wakili Kibatala: Mheshimiwa Hakimu, hii ni kesi inayoendeshwa kwa misingi ya sheria lakini nikimsikiliza Shahidi hapa ‘grounds’ zake ni mbili kwamba ya kwanza nakala halisi imepotea na nyingine ipo kwenye jalada la ZCO. Mengine aliyoyasema kuhusiana na hiyo nyaraka hiyo ni ‘hear-say’ kwa kuwa yeye sio ZCO na sio Muhifadhi wa ZCO wala hayupo ofisini kwa ZCO.

Kwa hiyo, mimi nilitegemea kutoka na kifungu cha 67 ama aje ZCO au mmoja wa Wapelelezi wanaofanya kazi kwenye ofisi ya ZCO. Hivyo Mheshimiwa, tunasisitiza kuwa masharti ya kielelezo bado hayajatimizwa

Wakili Katuga: Mapingamizi nimeyasikia na hoja ya kwanza Wakili Kibatala yupo sahihi kabisa, kwamba nakala halisi ya Makao Makuu imepotea na kifungu cha 67(c) kimetolea ufafanuzi. Pia, nakubaliana kuwa mengine ni ‘hear-say’ lakini Shahidi amejitambulisha yeye ni Polisi kutoka Makao Makuu na anatoka ofisi ya DCI ambayo ni kurugenzi kuu ya upelelezi na ZCO yupp chini ya DCI

Kwa maana halisi, ufuatiliaji wa Polisi sio ‘hear-say’ ni taarifa inayotoka kwa Polisi na kwa kuwa barua ipo kwa ZCO na Makao Makuu ndio walipeleka walikuwa na mamlaka ya kuchukua na walipeleka kwa kupitia jalada.

Hivyo basi, ni mfumo wa ndani wa upelelezi lakini kesi bado ipo chini ya DCI na barua kwenda kwa ZCO sio kwamba walimuagiza.

Aidha, kwa kutumia kifungu cha 68(1) tuliwaomba wenzetu watupe nakala halisi na kwa kukubali kupokelewa kwa dispatch hawapingi kupokea hicho kielelezo(barua) na kwa kifungu cha 67(a) aya ya kwanza tunaona kuwa ‘secondary evidence’ inakubalika kutumika kwa kuwa upande wa utetezi wanayo nakala halisi.

Pia, naomba twende zaidi kwenye ‘merits’ na sio ‘procedure’ na vilivyosemwa na utetezi visiwe kikwazo.

Wakili Mtobesya: Kifungu 67(a)(1) ukikisoma vizuri, wenzetu wamekitumia kinyume kwa kuwa hii inahusu - Mfano: JamiIForums wangekitumia, hiki ndio kifungu hiki kingefanya kazi. Kwa sababu barua ni ya kwao(Jamhuri) na wao ndio Watunzaji

Hakimu Shaidi: Nimeangalia mlivyosema wote na Mahakama itaangalia vyote mlivyosema na kueleza wakati inatoa uamuzi ila kwa sasa Mahakama inapokea kielelezo hiki kama ushahidi

******
Wakili Katuga: Shahidi, iambie Mahakama baada ya kuwafikishia hii barua nini kiliendelea?

Shahidi: Walitujibu barua mnamo tarehe 12/02/2016 lakini sisi tuliipokea tarehe 16/02/2016 na majibu yao yaliendelea kusisitiza kuwa waelezwe jinai gani iliyofanyika

Wakili Katuga: Ukioneshwa barua yao ya majibu, utaikumbuka?

Shahidi: Ndio, kwa kuangalia baada ya wao kutujibu kwa kurejea barua yetu na pia kwa kuangalia kilichopo ndani yake

*****
Shahidi anapewa barua na kuisoma kuona kama ndio barua yenyewe waliyojibiwa. Anasema anaikumbuka na kuomba Mahakama iitumie kama kielelezo

Wakili Kibatala anasema hakuna pingamizi, na barua inapokelewa kama kielelezo

*****
Wakili Katuga: Baada ya kupoka barua hiyo nini kilitokea kuhusiana na kile ulichokuwa unakihitaji?

Shahidi: Sikupata nilichokuwa nakihitaji na kumwambia DCI kuwa sijapata nilichokihitaji hivyo siwezi kuendelea na upelelezi. DCI aliniambia niachane na hilo suala la JamiiForums na kuwa atampa Afande Msuya aendelee nalo

Wakili Katuga: Mpaka leo unatoa ushahidi, ulishawahi kupata ulichokuwa unataka?

Shahidi: Hapana

>>>>
Wakili Katuga anasema mbele ya Mahakama na Hakimu Shaidi kuwa amemaliza kumuongoza Shaidi wake. Hakimu Shaidi anaukaribisha upande wa Utetezi kumuuliza maswali Shahidi

Wakili Kibatala anaanza kumuuliza Shahidi maswali

>>>>
Wakili Kibatala: Umesoma sheria hata kidogo?

Shahidi: Kidogo

Wakili Kibatala: Kiasi cha kutekeleza majukumu yako ya msingi?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Unafahamu kuwa takwa la kisheria likielekezwa kwa mfano; Kwangu au kwa Mwanasheria wangu, amri hizo hazina uzito sawa?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Mnamo tarehe 26/01/2016 kuna vitu mliomba kwa hao mnaowaita JamiiForum Media mliandika kwa kifungu gani?

Shahidi: Criminal Procedure Act kifungu cha 10(a)

Wakili Kibatala: Unafahamu Washtakiwa wanashtakiwa kwa kifungu cha sheria gani?

Shahidi anaonekana kutoelewa ni sheria gani lakini anaeleza kuwa anadhani ni ya Makosa ya Mtandao.

Wakili Kibatala: Hiyo tarehe 26/01/2016, barua mlimuandikia nani?

Shahidi: Mwanasheria

Wakili Kibatala: Mlikuwa mnataka taarifa kutoka kwa nani?

Shahidi: Jamii Media

Wakili Kibatala: Na kwa taarifa zako unasema ulikuwa unajua Maxence Melo ndiye Mkurugenzi (Tufanye ndivyo ilivyo) lakini ninyi mkamuandikia Mwanasheria?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Taarifa mlikuwa mnataka kutoka kwa nani?

Shahidi: Maxence Melo kupitia kwa Mwanasheria

Wakili Kibatala: Unasema malalamiko yalikuwa yanatoka benki ya CRDB, nani hasa aliyaleta? Maana CRDB ni Taasisi

Shahidi: Alikuja kulalamika Mkurugenzi, Tully Mwambapa

Wakili Kibatala: Huyo Tully, anapatikana hapa Dar es Salaam au yupo wapi leo ukiwa unatoa ushahidi hapa?

Shahidi: Hapana, sijui

Wakili Kibatala: Mahakama na mimi tunataka kujua alipo huyo Tully ili aje kuthibitisha kuwa alikuja kulalamika, tutampataje?

Shahidi: Sijui

Wakili Kibatala: Hizi tuhuma mnazosema zilielekezwa kwa CRDB? Au Charles Kimei au Tully Mwambapa?

Shahidi: Kwa Benki ya CRDB

Wakili Kibatala: Unafahamu kuwa Kimei amejiuzulu miezi mitano kabla ya muda?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Unafahamu sababu?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Unafahamu kwamba huenda kilichoandikwa JamiiForums ndio chanzo?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Unafahamu chochote kuhusu wizi ndani ya CRDB kwa kushirikiana na Charles Kimei?

Shahidi: Sifahamu

Wakili Kibatala: Mlikuwa mnachunguza lakini mkasema (katika barua iliyotumiwa kama kielelezo mahakanani) mnamtaka mhusika na kumtia hatiani kwanini? Wakati mlikuwa hamjui chochote. Kumpata mtu ili kumtia hatiani na ili aweze kuwasaidia kunafanana?

Shahidi: Hapana, hakufanani

Wakili Kibatala: Mwambie Hakimu, huyo Mwanasheria mlimtaja (kwenye Barua), ni Mwanasheria wa chombo gani?

Shahidi: JamiiForums Media

Wakili Kibatala: Unafahamu uwepo wa kisheria kama ipo au haipo hiyo JamiiForums Media?

Shahidi: Ndiyo

Wakili Kibatala: Hii barua ya tarehe 04/02/2016 huyu aliyeiandika unamfahamu mpaka unatoa ushahidi hapa leo? Anapatikana?

Shahidi: Sijui kama yupo

Wakili Kibatala: Na haujafanya juhudi zozote kujua?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba mtoa huduma kama vile Jamii Media(Huyu namtaja mimi sasa, achana na huyo mliyemsema “JamiiForums Media”) ana jukumu la kutunza faragha (privacy) za wateja wake na anatakiwa kuweka uwiano wa matakwa ya sheria ya wateja wake na masuala ya mamlaka ili asije kushtakiwa kote kote?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Unaona ni muhimu au si muhimu kumpata huyu mtu aliyepokea kwa dispatch ili aje kuthibitisha?

Shahidi: Muhimu

Wakili Kibatala: Ukilinganisha saini katika kielelezo P4 na P5 unaona zinafanana?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Uliwahi kufanya uchunguzi kuhusu ulinganifu wa saini kitu ambacho kinaweza kuisaidia Mahakama?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Katika hii dispatch, kuna muhuri wa huyo Wakili Benedict?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Kwenye barua kuna muhuri na saini ya Wakili Benedict Ishabakaki?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Ni kweli au si kweli kwamba kielelezo P4 mliekeza kwa Mwanasheria wakati amri alitakiwa kuifanyia kazi Maxence?

Shahidi: Kweli

Wakili Kibatala: Kwenye kwenye kielelzo P4 na P6 kuna sehemu ametajwa Mshtakiwa wa pili Micke William?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Hivyo Mahakama inaweza kuachana na Mshtakiwa wa pili? (Ingawa najua mwendesha mashtaka atasema huhusiki na kutengeneza mashtaka)

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Wakati unaomba kutoa kielelezo P6, hoja ilikuwa nakala halisi imepotea na hii kopi inaonesha kuwa imeandikwa tarehe 04/2/2016 ila kwenye barua kuna maandishi upande wa kulia juu ni ni maadishi ya kalamu ya wino halisi au kopi?

Shahidi: Ni ya kalamu halisi

Wakili Kibatala: Hayo maneno yanamtaja nani?

Shahidi: ASP Malima

Wakili Kibatala: Yameandikwa na nani?

Shahidi: Sifahamu kwa kweli

Wakili Kibatala: Haya, sema yameandikwa lini?

Shahidi: Tarehe 13/12/2016

Wakili Kibatala: Hivyo ni baada ya tarehe 04/02/2016

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Ulivyofuatilia kwa ZCO na ofisini walikuambia lini walianza kutoiona nakala halisi ya barua?

Shahidi: Hawakusema

Wakili Kibatala: Hivyo hujui ni lini imeanza kutokuonekana?

Shahidi: Sijui

Wakili Kibatala: Uliikabidhi lini kwa ZCO hiyo barua?

Shahidi: Sikumbuki tarehe ila ni mwezi wa 12 mwaka 2016

Wakili Kibatala: Sasa hii kopi nani aliitengeneza na lini?

Shahidi: Nilikiwa nayo na sikumbuki lini nilitoa kopi ila ni mwaka 2016

Wakili Kibatala: Ni wakati nakala halisi ipo?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Hayo maelezo yaliyotolewa kwa ASP Malima tulitegemea yawepo kwenye nakala halisi au kopi uliyokuwa nayo wewe kwa ajili ya shughuli zako nyingine?

Shahidi: Kwenye nakala halisi

Wakili Kibatala: Hao Maafisa wa Polisi ulioongea nao unawafahamu huko kwa ZCO?

Shahidi: Ndio, Inspekta Peter Kayumbi na Inspekta Monica

Wakili Kibatala: Walikujibu kwa barua?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Hii barua ya kuomba maombi kwa mara ya kwanza kabisa ipo nakala halisi lakini iliyopotea ni nakala halisi ya majibu kwa Wakili baada ya kuomba kuelezewa jinai, ni kweli au si kweli?

Shahidi: Kweli

Wakili Kibatala: Hizi barua za Wakili Ben zilikuwa zinaelekezwa kwako au kwa nani?

Shahidi: Kwa Ofisi ya DCI

Wakili Kibatala: Hebu iambie Mahakama kwamba kile kielelezo P6 umesema umeanza kuitafuta wiki iliyopita sasa kuweka rekodi sawa, hebu sema tarehe kabisa

Shahidi: Sikumbuki tarehe, ni kama wiki iliyopita au mbili zilizopita

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba kwenye barua zote hizo walizojibu walisisitiza kuwa wako tayari kutoa ushirikiano lakini tu wasaidiwe kisheria kujua jinai ni nini?

Shahidi: Ndio

Wakili Kibatala: Lakini wameshitakiwa kuwa ‘intentionally and unlawfully’ walikataa kuisaidia Polisi. Je kwenye barua unaliona hilo?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Wakati unatoa ushahidi, ulitaja majina ya hao memba nitakuwa nakuonea nikikuuliza kuhusu hayo majina?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba ulisema wanaitwa RB Expert Member na Sawana Expert Member? Mwambie Hakimu kama kwenye kielelezo P5 na P6 yanafanana na ulivyosema

Shahidi: Yanafanana

Wakili Kibatala: Kwenye ushahidi wako ulisema RB JF expert member?

Shahidi: Hapana

Wakili Kibatala: Kwa hiyo tunaona majina hayafanani. Huyu Muganyizi uliyesema amekuja kuchukua barua anaonekana kwenye kielelezo chochote kuanzia P3 hadi P7?

Shahidi: Hapana

>>>>
Wakili Kibatala anamaliza kumuuliza maswali yake Shahidi na Hakimu anamruhusu Wakili Jeremiah Mtobesya kuuliza maswali yake kama anayo

*****
Wakili Mtobesya: Nitakuwa sahihi nikisema hilo jalada la uchunguzi lilikuwa linahusu taarifa za kwenye mtandao?

Shahidi: Ndio

Wakili Mtobesya: Nikisema 25/05/2015 tulikuwa na sheria ya masuala ya kimatandao nitakuwa sahihi?

Shahidi: Ndio

Wakili Mtobesya: Naamini unaelewa angalau kwa uchahe ni kipi kinafanyika kwenye masuala ya upelelezi kwenye masuala ya kimtandao…

Shahidi: Ndio

Wakili Mtobesya: Mnafahamu kuwa iwapo mtu akikataa mnatakiwa muende Mahakamani ili kumlazimisha atoe taarifa?

Shahidi: Ndio

Wakili Mtobesya: Na kuwa iwapo mmeenda Mahakamani na kupewa amri na huyo mtoaji akakataa ndipo unaweza kusema ameshindwa kutoa ushirikiano?

Shahidi: Ndio

Wakili Mtobesya: Kuna wakati wowote kabla ya kumfikia mnayemuita ‘Mwanasheria wa JamiiForum Media’ mlimpa amri ya Mahakama na akawakatalia?

Shahidi: Hatukufikia huko

Wakili Mtobesya: Wakati unafanya upelelezi wako na wao kukuandikia barua mbili kuomba kuelelezewa ujinai. Ulienda kuangalia uhusiano wa hao wamiliki na wateja wao kwenye suala ya ‘disclosure of information’?

Shahidi: Hapana sikwenda

>>>>
Wakili Mtobesya anasema amemaliza kuuliza maswali yake. Hakimu Shaidi anamuuliza Wakili wa Jamhuri kama anahitaji kumuongoza tena Shahidi wake(Re-examination), Wakili Katuga anasema anahitaji kufanya hivyo na anapewa nafasi hiyo

*****
Wakili Katuga: Mimi nataka ufafanuzi kwa yale uliyokuwa unajibu. Wakili amekuuliza kuhusiana na mashtaka waliyoshtakiwa nayo washtakiwa. Mahakama ingependa kujua uhusika wako wewe na kuandaa mashtaka

Shahidi: Sijahusika kuandaa

Wakili Katuga: Pia, Wakili Kibatala amekuuliza kuhusiana na kwamba hizi barua zote zimekuwa zikiandikwa kwenda kwa Wanasheria. Hawa Wanasheria uliokuwa unawaandikia ni kwa maelezo kutoka wapi au ulimfahamu vipi?

Shahidi: Tuliwahi kuongea na Maxence na akatuambia tuwe tunamuandikia Mwanasheria wake

Wakili Katuga: Nani aliwatajia huyo Mwanasheria?

Shahidi: Yeye mwenyewe Maxence

Wakili Katuga: Wakili Kibatala pia amekuuliza kuhusu ‘JamiiForum Media’. Hebu sema, umeipata wapi?

Shahidi: Niliiona kwenye mtandao

Wakili Katuga: Pia, amekuuliza kuna sehemu yoyote wewe umemtaja Micke William, ukasema hapana na ukaulizwa kama aachiwe huru ukasema ndio. Je, unajua huyu kashtakiwa na mashtaka yepi?

Shahidi: Sijui

Wakili Katuga: Umeelezwa kuhusu Vielelezo P3 na P6. Je, kuhusu majina uliyoyataja na uliyoandika kama ni sawa ulisema ni sawa. Ukaulizwa kuhusu JF. Je, hii JF ilikuwa inahusu nini?

Shahidi: JamiiForum

>>>>
Wakili Katuga anasema amemaliza kumuongoza Shahidi wake kwa mara nyingine na kuomba Mahakama iahirishe shauri hili kwa kuwa siku hii hakuwa na Shahidi Mwingine

Hakimu Huruma Shahidi anasema sawa na kuahirisha shauri hilo hadi Novemba 15, 2018


Kujua zaidi kuhusu muendelezo wa Kesi dhidi ya JamiiForums | Tembelea Muendelezo wa Kinachojiri Kisutu: Kesi za Jamhuri dhidi ya JamiiForums - JamiiForums
 
Back
Top Bottom