Kesho yako ipo ndani ya herufi 5 au 7!

James Hadley Chase

JF-Expert Member
Mar 25, 2020
1,578
2,664
MBWANA Samatta anaendelea kusuka rekodi za soka kwenye ardhi ya Tanzania. Anavunja dari za kioo zilizozuia wengine wasipasue anga. Anatuonesha kuwa mbingu pekee ndio inaweza kuwa ukomo wake. Yes, sky the limit!

Kutoka African Lyon mpaka Simba, akatua TP Mazembe ambao walimuuza KRC Genk. Sasa yupo Aston Villa, klabu kongwe England, yenye rekodi ya kutwaa kombe la Klabu Bingwa Ulaya. Miguu ya Samatta itashuka kila dimba la ligi ya soka maarufu zaidi duniani, Ligi Kuu England (EPL).

Ni Samatta aliyeifanya Tanzania itoe mfungaji bora Afrika mwaka 2015. Samatta huyohuyo akawa Mchezaji Bora Afrika ndani ya Bara la Afrika katika Glo Caf Awards 2015. Akawa Mtanzania wa kwanza kukipiga Uefa Champions League. Na akafunga. Aliwafunga mpaka Liverpool pale soweto kwao, Anfield. Anaitwa Samatta marekodi!

Unadhani kwa nini Samatta anapasua anga zote hizo? Kipaji? Ni kweli Samatta ana kipaji kikubwa lakini ukithubutu kujibu kwamba anabebwa na kipaji, nitakufelisha.

Juhudi? Sikatai. Samatta anajituma. Hata hivyo ukiniandikia jibu la kwamba juhudi ndizo zinamfikisha mbali Samatta, usishangae nikikupa F. Na hapa sitanii.

Nidhamu? Hakika, Samatta ana nidhamu ya hali ya juu. Katika kazi yake na kimaisha. Ni kijana safi, hana makuu, mnyenyekevu, hana zile za “mimi ndio Mbwana Samatta”, wakati ni staa wa kila staa kwenye soka Bongo, halafu ngawira anazo nyingi.

Pamoja na kukiri kuwa Samatta ana nidhamu, lakini kama ukinijibu hivyo kwenye mtihani wangu, utakuta nimekupa mviringo. Nitakunyima hata alama za kuhudhuria chumba cha mtihani.

Acha nikupe jibu mapema ili wakati mwingine tusisumbuane. Samatta amefika hapo alipo kwa sababu ya herufi tano kama utatumia Kiswahili. Na herufi saba kama unauendekeza ukoloni.

Na hizo herufi ndio huleta matokeo ya mustakabali wa kila mmoja. Ndizo zimewafanya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kuwa mastaa wa dunia leo. Ndizo zimewapa utajiri wa kidunia akina Jeff Bezos, Bill Gates, Warren Buffett na wengine.

Usiende mbali sana; hizo herufi ndizo zimemfanya Said Salim Bakhresa kuwa bilionea kama alivyo. Zilisababisha Reginald Mengi, Elvis Musiba na Ally Mufuruki, kufariki dunia wakiwa giants wa sekta binafsi Tanzania.

Maisha ni maono! Vipi unataka kuweka “maono” kwamba ndio herufi tano za Kiswahili? Usithubutu, karatasi yako ya majibu ya mtihani nitaichanilia mbali.

Kila binadamu anayo maono. Kila mtu hujiona yeye ni nani. Hujiotea, hujifikiria, hujitamania. Sasa kutimia, kufeli au kufa kwa hayo maono ndipo kwenye jibu. Ni herufi tano za Kiswahili, “Amini”. Herufi saba za Kingereza, “Believe”.

Unajiona wewe ni nani kesho? Unaamini hayo maono? Au kwa Kiingereza, do you believe? Maono yenye kutimia ni yale yenye kuchakatwa ndani ya imani. Ukiamini utajiamini, kisha utanoa makali ya kipaji chako, halafu juhudi na nidhamu vitakufikisha. Hilo ndio jibu la safari ya Mbwana Samatta.

Kipaji si mali kitu kama huna maono nacho. Yaani hujioni wewe ni nani kesho kupitia kipaji chako. Maono hayatakusaidia ikiwa huyaamini.

Kipindi Bakhresa anauza kacholi, angekuwa hajioni yeye ni bilionea wa kesho, au asingeamini katika hayo maono ya yeye kuwa bilionea, angeishia kuuza kacholi na maandazi. Jione kwanza wewe ni nani kesho, kisha amini wewe ni huyo unayejiona.

Kile unachokiamini, utakitenda kwa nidhamu na juhudi. Hivyo imani yako ndio ufunguo wa nidhamu na juhudi. Sasa, kama ni ushauri kwako, nitakwambia “amini”, ndio, just believe!

Samatta alipokuwa Simba hakucheza kama aliyefika. Aliwajibika mithili ya mwenye kutafuta njia ya kupita. Ni kwa sababu alikuwa anajiona yeye ni mchezaji mkubwa kuliko Simba. Hata alipokwenda Mazembe alionesha ari ya kwamba pale ni njiani, kisha Genk, sasa Aston Villa.

Ikiwa maono yake yaliishia kucheza EPL, sasa akacheza Aston Villa kama aliyefika, bila shaka hatafanya makubwa zaidi. Kama Samatta anajiona Aston Villa ni njiani kwake, si ajabu Watanzania wakamsherehekea tena atakapokuwa anatua kituo kingine.

Je, Samatta anayo maono ya kuchezea Manchester United? Man City? Liverpool? Real Madrid? Barcelona? Au klabu nyingine yoyote kubwa? Basi ayaamini hayo maono, halafu, sky the limit!

Ni maono kisha imani ya maono yake, ndicho kilimpa ubunge kijana maskini, John Mwirigi, katikati ya ubabe wa siasa za vyama na matumizi makubwa ya fedha.

Watu walimuona Mwirigi maskini, yeye alijiona mbunge. Wengi walimdharau kwa vile hakuwa hata na pesa za kampeni, yeye aliyaamini maono yake ya kuwa mbunge.

Mwirigi aligombea kama mgombea binafsi, jimbo la Igembe Kusini, mkoa wa Meru mwaka 2017. Alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 23, mwanafunzi asiye na fedha kabisa. Fedha ya kulipia fomu ya kugombea, Sh10,000 ya Kenya, sawa na Sh215,000 ya Tanzania, zililipwa na wananchi wa Igembe Kusini waliomtakia mema.

Hakuwa na uwezo hata wa kumudu kukodi gari la kumzungusha kufanya kampeni, hakuweza kuandaa mikutano ya hadhara, hivyo Mwirigi akabuni njia yake ya kufanya kampeni na akajiamini kwayo. Mwirigi alitembea kwa miguu akigonga hodi mlango kwa mlango na kunadi sera zake uso kwa uso.

Mwirigi alizungukia watu kwenye biashara zao na kunadi sera zake. Mwisho alishinda na kuweka rekodi ya aina yake. Kijana mdogo na maskini mno kuwa mbunge.

Baada ya kushinda ubunge, Mwirigi alifanya mahojiano na televisheni ya KTN, akaulizwa uwezekano wa kununua gari. Alijibu alitamani kumiliki gari kubwa lenye kuendana na hadhi ya ubunge wake, lakini alipitia maduka mbalimbali ya magari na kukuta bei ni kubwa. Hivyo aliamua kutulia.

Siku chache baada ya Mwirigi kusema hayo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimnunulia Toyota Prado TX Land Cruiser (J120). Makabidhiano yalifanyika kwenye Hoteli ya Sagana State, iliyopo Nyeri. Mwirigi akamshukuru Rais Uhuru na kumwahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuwatumikia wananchi waliomchagua.

Matokeo ya kimaisha ni herufi tano “Amini” ni herufi saba za Mkoloni “Believe”. Facebook isingekuwa ilivyo bila Mark Zuckerberg na masela wenzake waliochangia bweni Harvard University, Eduardo Saverin, Andrew McCollum, Dustin Moskovitz na Chris Hughes, kuwa na maono, kisha kuyaamini.

Nyuma ya mafanikio ya kila taasisi na kila mtu, yapo maono yaliyoaminiwa. Hivyo, amua leo kuyaamini maono yako. Unajiona nani kesho? Unaionaje biashara yako kesho? Unaitazama vipi kazi yako kesho? Amini hayo maono. Kisha imani itakuelekeza uwe na nidhamu na juhudi.

Lazima ujiamini mwenyewe, ndio, you should believe in yourself! Maana wewe ndio mmiliki wa mustakabali wako. Hata waje manabii gani wakuhubirie, kama wewe mwenyewe huamini maono yako, hiyo ni kazi bure.

Amini katika ndoto za mkeo, mumeo, mtoto wako, nduguyo, rafiki yako. Mwisho kabisa, akifanikiwa, kitakachokupa fahari ni ile imani yako uliyomwonesha na ukampa sapoti kadiri ya uwezo wako.

Usimvunje moyo anapofuata maono anayoyaamini. Usimkimbie sababu ya changamoto za kuyafuata maono anayoyaamini. Wewe amini, ndio, just believe!

Wakati Ellen Johnson Sirleaf, akihangaika kusoma, mume wake, James Sirleaf ‘Doc’, hakuamini katika ndoto za mkewe. Akawa anampiga. Akamlazimisha aache chuo. Wakaachana. Kisha, Ellen akawa Rais wa kwanza mwanamke Afrika, halafu mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel na ya MO Ibrahim kwa uongozi uliotukuka.

Pale Samatta alipofikia kuna watu waliamini katika maono yake. Hata Ismael Aden Rage aliamini, ndio maana alihakikisha kwenye mkataba wa Simba kuwauzia Mazembe, kunakuwa na kipengele cha Simba kunufaika na mauzo kama klabu iliyomkuza, kila Samatta anapouzwa.

Aliamini angefika mbali. Na leo Simba wanaendelea kuvuta mpunga. Samatta alipouzwa Genk kutoka Mazembe, Simba walivuta chao. Genk kwenda Aston Villa, Msimbazi ni neema tupu. Hata Villa wakimuuza kwingine, mpunga utaingia.

Amini. Ndio, just believe!
 
Huwa na kereka Sana na watu wanaoanza na story af point haieleweki au ipo mwishoni , inatosha kusema umeandika pumba tupu
 
Ushahidi mwingine Kuna madaktari katika hospital Flani nchini marekani walitengeneza Unga Unga sijiui ni wa ngano wakaeka na sukar kidogo ili ilete ladha wakawaaminisha wagonjwa kua ni kidonge yaani dawa wakinywa watapona na kweli walopona aisee Kuna nguvu kubwa sana kwenye Kuamini
 
Namba 5 & 7 Hazijaelezewa kiundani ni blah blah blah blah Tupu .... Ni nguvu ya maono Au nguvu ya namba hizo shwain
 
Kama watu wanavyotofautiana kwenye huu uzi, ndivyo na fursa zinavyotujia tunatofautiana kuzifanyia kazi, kufanikiwa au kutofanikiwa inabaki kwa hatua gani unachukua na umatafsiri vipi taarifa unazozipata.

Wengine wataona haya maelezo ni pumba na kuna watu pumba hizi hizi zitabadilisha maisha yao kabisa.

Niwatakie siku njema
 
Back
Top Bottom