Kenya sasa wananyoana, Watanzania tutie maji

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,886
Kenya sasa wananyoana, Watanzania tutie maji

Chris Alan
Tanzania Daima

YANAYOTOKEA Kenya baada ya uchaguzi mkuu ambao umesababisha machafuko ya kisiasa na kijamii kutokana na kutangazwa kwa mshindi anayedaiwa si halali, yanazidi kuwa funzo kubwa si kwa Wakenya tu, bali kwa Tanzania na dunia nzima kwa ujumla.
Awali ilionekana kwamba ghasia zilizokuwa zikiendelea baada ya Rais Mwai Kibaki kutangazwa mshindi wa kiti cha urais, zilikuwa ni za kisiasa zaidi kuliko za kiuchumi na chuki ambayo imejijenga miongoni mwa jamii ya Kenya. Lakini kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, kinachotokea ni ishara na kielelezo cha watu kuchoka.

Kuchoka kwa watu hawa kunajidhihirisha katika mambo mawili, moja; kwamba sasa imejulikana kwamba njia ya kupata haki kwa sanduku la kura si rahisi. Kwamba ni lazima miaka nenda rudi kundi fulani katika jamii lichukue madaraka ya dola. Iwe isiwe, wao ndio wa kuongoza!

Katika hali kama hiyo, hasira za aina mbili zinakuwa wazi. Kuna hasira ya kuhisi kudharauliwa na kuporwa kwa haki kwenye sanduku la kura, lakini hasira nyingine ni kufunuliwa kwa hisia za ndani za miaka mingi. Miaka mingi ya kukosa ajira, kukosa kipato, kukosa maisha ya staha sawa na hao wanaodhani wana haki ya kuwa madarakani daima, lakini hata hawana habari kwamba kuna watu wanaoishi maisha ya dhiki kuu.

Kuchoka kwa aina ya pili ni kutokana na uchovu wa kiuchumi au tuseme hasira ya kiuchumi. Uchovu huu ndiyo chimbuko la hasira kubwa zaidi. Watu wanadhihirisha kwamba kwa nini wao waishi maisha ya dhiki kuu miaka yote ndani ya nchi yao; watu hawa wanajiuliza kwamba ni kwa nini wapo wanaokula na kusaza wakati wapo ambao hata hawawezi kupata kibaba cha unga wa ugali?

Akiwa nchini Kenya wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, alisema kinachotokea Kenya kwa sasa ni matokeo ya sehemu ya jamii kujiona kwamba hawana chao katika mgawanyo mzima wa rasilimali katika nchi yao. Ghasia hizi ni kielelezo cha hisia za kuwekwa pembeni kwa jamii kubwa katika mgawanyo wa keki ya taifa.

Katika mataifa yote duniani, ghasia huwa zinaendeshwa na watu wasiokuwa na kitu. Hawa ni wale Vladimir Lenin aliwaita kundi la kimapinduzi, kundi fukara ambalo katika mapigano ya ukombozi halina cha kupoteza isipokuwa minyororo ya utumwa na udhalili wao. Kwa hali hiyo, haishangazi kuona kwamba mapigano makali zaidi katika miji kama Nairobi yanajitokeza katika maeneo kama ya Kibera.

Hapa kwetu, kwa miaka mingi wapo watu wamekuwa wakihubiri amani na utulivu. Wapo watu wamefikia hata hatua ya kusema kwamba Tanzania ni nchi ya kipekee kwa bara la Afrika, kwamba ni nchi ambayo amani imetamalaki. Haya yote ni sawa. Kweli amani imetamalaki.

Wapo wanaodhani kwamba Kenya au Uganda au DRC au Rwanda na hata Burundi ni tofauti sana na Tanzania, kwa sababu tu wao wanapigana wenyewe kwa wenyewe. Kwetu hatupigani, na kwa hiyo sisi ni watu tofauti. Hili ndilo ninataka kuzungumzia kwa leo nikioanisha na hali ya Kenya.

Nimesema kwamba kuna hasira mbili hapo juu. Hasira ya kuhisi kuibiwa kwenye sanduku la kura, na hasira ya kiuchumi, njaa, dhiki na kukataa tamaa ya kufanikiwa kimapato.

Kwa bahati mbaya sana, viongozi wa Tanzania mara nyingi wameshindwa kutambua kwamba hasira ya kiuchumi, yaani watu kukosa kipato, ajira na uhakika wa kupata kibaba cha unga, ipo Tanzania.

Viongozi wetu wanadhani hasira hiyo haipo na wanaoishi maisha ya kubangaiza hawajui kwamba wapo watu wanaokula fedha za umma bila huruma.

Viongozi wanadhani watu wenye hasira ya uchumi hawaoni mabilioni yanayochotwa Benki Kuu kama kashfa ya EPA; kwamba wenye njaa hawaoni mikataba ya mawengewenge ikisainiwa na watu wenye dhamana za ofisi za umma; kwamba njaa ya watu hawa inavumilika na hakuna siku italipuka.

Ninakumbuka Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, mara nyingi amekuwa akisema jambo moja la msingi kwamba kama umezungukwa na watu wenye njaa waliopoteza matumani na wewe ni tajiri, hakika huna amani, kwani kuna siku watakuja kuchukua hicho ulicho nacho. Njia ya kuishi kwa amani na kufurahia utajiri au kipato chako ni kwa kuhakikisha kwamba walau na masikini naye ana kibaba cha unga!

Hii ni dhana ngumu sana kueleweka kwa wanasiasa, si wa Tanzania tu, bali wa bara lote la Afrika. Viongozi wa kisiasa mara nyingi hawana uwezo wa kufikiria nje ya madaraka yao. Viongozi wetu wengi upeo wao wa kufikiri unaishia kuwaza nyumba za kifahari walizopewa na serikali kwa jasho la wananchi; wanawaza magari ya kifahari waliyopewa na ofisi za umma, wanawaza ukwasi kwa kutumia ofisi za umma.

Matokeo yake hata hawana muda wa kufikiri kwamba wakati wao wakiendesha magari ya kifahari ya umma na wakiishi nyumba za kifahari na kula na kusaza, wapo watu wasiokuwa na matumiani ya kuishi, na hawa kwa taarifa yao ni wengi. Hawa ni zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa taifa hili.

Katika kundi hili, zaidi ya asilimia 90 ni vijana. Hawa ni vijana tunaoona kila siku wakikimbizana na mgambo mijini wakinyang'anywa vitu vyao wanavyochuuza; hawa ni wakulima wanaokopwa mazao yao na vyama vya ushirika; hawa ni wafugaji wasiokuwa na pa kulisha mifugo yao wala pa kuwanywesha maji. Hawa ni wachimbaji wadogo wadogo wa madini wanaoswagwa kama wanyama wakishurutishwa kuwapisha wawezekezaji wakubwa wa kigeni wenye mitaji na teknolojia ya kisasa ya kuchimba madini. Hawa ni wengi kila mahali!

Kwa hiyo, kama ilivyo kwa Kenya, kundi hili la hasira ya kiuchumi likipata kichocheo kidogo kama hiki cha hasira juu ya kutokuheshimiwa kwa sanduku la kura, litalipuka bila kujali kwamba eti Tanzania ni nchi ya amani.

Ndiyo maana watu wenye ofisi za umma wanaposema eti hawana cha kujifunza kutoka yaliyotokea Kenya, wanasahau kitu kimoja, kwamba lipo bomu kubwa la watu wenye hasira ya kiuchumi, wasio na ajira, waliokata tamaa, wasiojua leo itapita vipi. Watu wanaoishi katika dhiki hii wanaambiwa eti BoT sh bilioni 133 zimeyeyuka, wanaambiwa eti ni lazima ndege ya rais inunuliwe hata kama ni kwa wananchi kula nyasi; wanaambiwa kwamba maisha bora yanawezekana kwa kila Mtanzania wakati kila uchao maisha yanazidi kuwa magumu.

Kwa hiyo, ya Kenya si funzo tu, yanatukumbusha mtihani mkubwa ulioko mbele ya watawala, kuwaondolea wananchi hasira ya kiuchumi. Hili likifanyika, amani yetu inaweza kuwa ya kweli. Amani iliyojikita kwenye mwamba wa kweli, bila kufikiriwa hili kwa makini, hakika sisi na Kenya, Burundi, Rwanda na DRC hatuna tofauti yoyote, ipo siku tutalipuka tu na hapo hatasalimika mtu.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom