KENYA: Mahakama ya EAC ishughulikie pia kesi za uhalifu dhidi ya binadamu: | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

KENYA: Mahakama ya EAC ishughulikie pia kesi za uhalifu dhidi ya binadamu:

Discussion in 'Kenyan News and Politics' started by BabuK, May 3, 2012.

 1. BabuK

  BabuK JF-Expert Member

  #1
  May 3, 2012
  Joined: Jul 30, 2008
  Messages: 1,847
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 145
  KENYA imefanikiwa kupenyeza ajenda zake kadhaa katika mkutano wa viongozi wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo ya kupanua wigo wa mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki ya kushughulikia kesi za uhalifu dhidi ya binadamu.
  [​IMG]

  Mkutano huo wa viongozi wakuu wa nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulimalizika Jumamosi ya Aprili 28 katika Hoteli ya Ngurdoto nje kidogo ya mji wa Arusha ukihudhuriwa na marais wanne.
  Viongozi walihudhuria mkutano huo wa siku moja ni Rais Jakaya Kikwete (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Mwai Kibaki (Kenya) wakati Burundi iliwakilishwa na Makamu wa kwanza wa Rais Therence Sinunguruza.
  Taarifa za kutoka ndani ya mkutano huo kabla ya kutolewa kwa taarifa ya pamoja zinaeleza kuwa Kenya ilikuwa na ajenda yake kuu ya kuwashawishi viongozi wa nchi wanachama wakubali ushauri wa kupanua wigo wa Mahakama ya Afrika Mashariki kusikiliza kesi za uhalifu dhidi ya binadamu.
  Nyuma ya ajenda hiyo ambayo sasa imekubaliwa na wakuu wa nchi zote tano inaeleza kuwa lengo ni kuisaidia Kenya kuhamisha kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu inayowakabili Wakenya wanne katika Mahakama ya Kimataifa yaani ICC ili ishughulikiwe na Mahakama ya Afrika Mashariki.
  Wakenya wanaokabiliwa na kesi katika ICC yenye makao yake The Hague, Uholanzi ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Uhuru Kenyetta, Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Rutto, Katibu Mkuu kiongozi wa Ikulu ya Kenya Francis Muthaura na mwandishi wa habari Joshua Arap Sang.
  Wakenya hao wanne wanatuhumiwa kuhusika na vurugu zilizotokea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Desemba mwaka 2007 uliomweka madarakani Rais Kibaki.
  Uhuru na Rutto ambao ni wanasiasa mashuhuri nchini humo, tayari wameshatangaza nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika kati ya mwezi Desemba mwaka huu au mwezi Machi mwakani.
  Vurugu hizo zilizua mauaji ya watu 1,133 na wengine 650,000 wakikosa makazi na hadi sasa wengi bado wanaishi katika makambi ya muda yaliyotengenezwa na serikali.
  Taarifa zaidi zinaeleza kuwa serikali Kenya ilikuwa inacheza karata yake ya mwisho ya kuwashawishi viongozi wa nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kesi dhidi ya raia wake hao isiendeshwe The Hague, badala yake iletwe katika Makahama ya Afrika Mashariki.
  Katika hoja zao maafisa wa Kenya katika kikao cha awali cha Baraza la Mawaziri walijenga hoja kuwa hatua ya kufanyia kesi hiyo The Hague ilikuwa sawa na kujidhalilisha kama taifa uhuru na pia itajenga mazoea siku za usoni iwapo kutatokea matatizo katika nchi nyingine kwa watuhumiwa wake kupelekwa The Hague kufunguliwa mashitaka.
  Hoja hiyo pia iliibuka wakati wa kikao cha viongozi wakuu ambapo Rais Kibaki aliwashawishi wenzake juu ya umuhimu wa kesi hiyo kusikiizwa na Mahakama ya Afrika Mashariki ambayo hata hivyo kwa mujibu wa mkataba wa Afrika Mashariki haina mamlaka ya kusikiliza kesi za jinai.
  Wiki iliyopita wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki waliokuwa wanakutana mjini Nairobi walizungumzia suala hilo nakuptisha azimio kwa nchi wanachama kuipa mamlaka ya kisheria Mahakama ya Afrika Mashariki ili isikilize pia kesi za jinai.
  Taarifa zinaeleza kuwa Kenya imekuwa ikifanya juhudi za kidiplomasia kwa muda mrefu kuhakikisha kuwa kesi hiyo inafanyika nchini mwao na hofu ya serikali ya nchi hiyo inajengwa juu ya msingi kuwa hata Rais Kibaki anaweza kufunguliwa mashitaka mara baada ya kumaliza kipindi chake cha utawala.
  "Suala la watuhumiwa hao kufunguliwa mashitaka The Hague limekuwa suala tete na kama unakumbuka hivi karibuni zilivuja taarifa za siri katika nyaraka zinazodaiwa kuwa zimetoka Ubalozi wa Uingereza kuwa Rais Kibaki ni mmoja watuhumiwa na atafikishwa katika mahakama hiyo baada ya kumaliza kipindi chake," kilieleza chanzo chetu.
  Kwa makubaliano hayo marais hao sasa wameliagiza Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki kufanya mabadiliko ya mkataba unaounda Jumuiya hiyo kabla ya Mei 30 mwaka huu ili kupanua wigo wa mamlaka ya mahakama hiyo.
  "Baada ya mawaziri kukamilisha kazi hiyo wataitisha kikao cha dharura cha wakuu wa nchi wanachama ambao nao watabariki marekebisho hayo na kuyapitisha kuwa sheria kamili," ilisomeka sehemu ya maazimio ya mkutano huo wa pamoja.
  Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja iwapo jumuiya ya kimataifa itakubaliana na maamuzi hayo ya kutaka kesi dhidi ya watuhumiwa hao ihamishwe na kusikilizwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki mjini Arusha.
  Kesi hiyo inayosikilizwa na mahakama ya ICC tayari imefikia hatua ya kusikilizwa pamoja na kwamba watuhumiwa wote ambao wako nje kwa dhamana wamekata rufaa dhidi ya shauri la awali baada ya kuelezwa kuwa wana kesi ya kujibu mbele ya Mahakama hiyo.
  Ajenda nyingine ambayo inaoenakana kuwa ni ya kuinufaisha Kenya ni ile ya mkataba wa ushirikiano katika masuala ya ulinzi ambapo sasa nchi zote zitalazimika kupeleka majeshi ya ulinzi pale nchi mojawapo itakapoingia vitani au itakaposhambuliwa na maadui wa nje ya eneo la Afrika Mashariki.
  Kenya ndiyo inayodaiwa kulete ajenda hiyo tangu mwaka jana mwishoni baada ya kuingia vitani dhidi ya kikundi cha magaidi cha Al-shabab cha nchini Somalia ambapo hadi sasa majeshi ya nchi bado yapambana na magaidi hao.
  Katika mkutano wa mwisho uliofanyika Burundi mapema mwaka jana, Tanzania ilikataa mkataba huo wa ushirikiano katika ulinzi lakini sasa taarifa zinaeleza kuwa imelegeza msimamo wake kuhusu suala hilo.
  Aidha, katika hatua nyingine, wakuu hao wameweka "kiporo" maombi ya nchi changa ya Sudan Kusini ya kutaka kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi hapo mchakato wa kujidhiridhisha utakapokamilika.
  Viongozi hao wameliagiza Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanza uhakiki wa maombi ya Sudan ya Kusini na wametaka taarifa hiyo iwafikie katika mkutano ujao utakafanyika Novemba mwaka huu.
  Viongozi hao pia wametoa wito kwa viongozi wan nchi za Sudan Kusini na Sudan ambazo ziko katika mapigano ya kugombea mpaka na visima vya mafuta, kuacha mapigano na zirejee katika meza ya mazungumzo.
  "Tunawaasa viongozi wa nchi hizo mbili warudi katika meza ya mazungumzo na kutafuta njia ya amani ya kumaliza masuala yaliyobaki katika mkataba wa amani," ilisomeka taarifa hiyo.
  Viongozi hao walisistiza katika taarifa yao pamoja kuwa wataendelea na wajibu wa kutafuta amani katika nchi hizo mbili na nyingine zinazopakana na nchi za jumuiya hiyo.

  Chanzo: Raiamwema
   
Loading...