Elections 2010 Katika kuunda serikali, Rais azingatie haya

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
jkwaza.jpg
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete

Kazi kubwa inayomkabili Rais Jakaya Kikwete baada ya siku chache zilizopita kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha pili cha miaka mitano, ni kuunda serikali yenye kukidhi viwango, mategemeo na matazamio ya wananchi. Rais anakabiliwa na kazi ngumu sana, kwani siyo siri kwamba wananchi walio wengi kwa kiasi kikubwa hawakuridhishwa na kiwango cha utendajikazi wa mawaziri wengi katika baraza lake la mawaziri katika miaka yake mitano aliyokuwa Ikulu. Katika kipindi kilichopita, tuliona baadhi ya mawaziri wakimwangusha Rais Kikwete kwa kukosa uadilifu au kukabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, hivyo kulazimika kujiuzulu. Katika kipindi hichohicho, tulishuhudia pia baadhi ya mawaziri na watendaji wake wakuu wakijiuzuru kutokana na kuwajibika baada ya kushindwa kudhibiti vitendo viovu vya baadhi ya maafisa wao katika mamlaka walizokuwa wakiziongoza

Lakini pia sote tuliona baadhi ya mawaziri wakikaa katika baraza hilo la mawaziri mithili ya watalii na kazi yao kubwa ikiwa tu ni kukaa maofisini na kufanya safari zisizokuwa na tija. Kwa tafsiri yoyote ile, viwango vya utendaji wa kazi zao vilikuwa chini kiasi cha kutisha na bahati mbaya waliendelea kukalia viti hivyo pasipo kunyooshewa vidole au kuondolewa na mamlaka husika. Kwa kweli, mawaziri hao si tu walizitia aibu mamlaka zilizowateua kushika nafasi hizo bali pia walichangia kwa kiasi fulani kufifisha imani ya wananchi kwa serikali ya Rais Kikwete.

Hata hivyo, tunaposema hivyo hatuna maana kuwa baraza hilo la mawaziri halikuwa na mawaziri wachapakazi au waadilifu. Baraza hilo hakika lilikuwa na baadhi ya mawaziri ambao walikuwa mabingwa wa kuongoza kwa kuonyesha njia, kutafuta suluhisho la matatizo mengi yaliyokuwa yanawakabili wananchi na kusimamia sheria, sera na kanuni zilizowekwa katika uendeshaji wa masuala ya kiserikali.

Tumeainisha yote hayo ili kumsaidia kiongozi wetu, Rais Kikwete, ateue mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya walio makini na bora zaidi katika serikali anayotazamia kuiunda katika wiki mbili hivi zijazo. Tunasema pasipo kupindisha maneno kwamba baadhi ya wateule wake katika kipindi chake cha kwanza katika nafasi tulizozitaja hapo juu na nyingine nyingi, walikuwa mzigo mkubwa kwake usioweza kubebeka. Mbali na kutokuwa waadilifu, baadhi yao walikuwa wazembe wa kutupwa na wengine walikuwa hawana karama ya kuongoza hata kidogo.

Ni kwa sababu hiyo tungependa kushauri kwamba katika ngwe hii ya mwisho, Rais Kikwete awatunuku wananchi baraza dogo la mawaziri na viongozi wengine katika nyadhifa mbalimbali ambao ni wachapakazi na waadilifu.

Kwa kuwa Watanzania ni wamoja na kwa kuwa wanataka wapunguziwe kodi itokanayo na gharama zinazotokana na uendeshaji wa serikali iliyo kubwa na isiyokuwa na tija, Rais Kikwete aunde wizara chache ambazo zina ulazima, pasipo kuumiza kichwa sana katika kuangalia mambo ya uwiano wa kimikoa, nakadhalika. Sote tulikuwa mashuhuda wa jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alivyoteua watendaji bila kwanza kuangalia kabila, dini au jinsia ya mtu aliyemteua.

Tunachokisisitiza hapa ni umuhimu wa sisi kama Watanzania kurudia matendo na uasilia wetu uliotufanya tuwe wamoja na kuifanya nchi yetu iwe kisiwa cha amani na utulivu. Waasisi wa taifa letu walitanguliza upendo, uadilifu, utendaji haki na kuheshimu sheria na katiba pamoja na mambo mengine ya msingi katika kufanya uteuzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali za kitaifa. Sera za udini, ukabila, umajimbo na mambo mengine ya utengano kamwe hayakupewa nafasi.

Sisi tunadhani kwamba Rais Kikwete katika kufanya uteuzi azingatie tu uwezo, uadilifu na unyenyekevu wa kila mtu atakayemteua kuanzia kwa wakuu wa wilaya na mikoa, makatibu wakuu, mawaziri na wengineo. Tunategemea pia kwamba waziri mkuu mpya si tu atakuwa mchapakazi wa mfano bali pia atakuwa mtu wa wote, wakiwamo wabunge wa kambi ya upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Chanzo. Gazeti la Mwananchi
 
Back
Top Bottom