Katiba Mpya na hatma ya Taifa letu

Environmental Security

Senior Member
May 21, 2020
181
261
Siku moja nikiwa kijiweni kwetu na vijana wenzangu tukipiga stori mbili-tatu asubuhi. Mwenzetu mmoja ambaye ni fundi wa bajaji aliniuliza swali lililofanya nifike mbali sana kuhusu hali za mataifa yetu ya kiAfrika, huku nikimshukuru Mungu kwa hali ambayo bado tunayo Tanzania kama Taifa.

Jamaa aliuliza alisema.."Hivi ni kweli marekani, umoja wa mataifa, umoja wa Africa na mataifa wameshindwa kabisa kuwamaliza vikundi kama bokoharam, alshabab, IS-msumbiji, vikundi vya wapiganaji congo maana nimesikia watoto wakike wanafunzi wametekwa Naijeria?"

Baada ya kutafakari nikamjibu juu ya ukweli huu muhimu sana kwa uimara wa Taifa na hatma ya taifa kwa ujumla nikamwambia hivyo vikundi ni vyepesi sana kuvimaliza, lakini kutokana na mazingira flan flan katika mataifa husika inakuwa ngumu kuvimaliza na ili uvimalize inategemea kwa zaidi ya salimia 90 hali ya taifa husika ndipo asilimia zinazobakia mataifa mageni au taasisi za kimataifa zinaweza kusaidia. Vitu muhimu sana kwa ambavyo lazima taifa lizingatie ni kama ifuatavyo.

1. Usawa ktk mgawanyo wa keki ya taifa. Kwa kiasi kikubwa taifa lijitahidi kuhakikisha kuwa mgawanyo wa keki ya taifa unazingatia sana maeneo yote ya nchi, yaani kusiwepo na gap kubwa sana. Inawezekana baadhi ya maeneo yakasonga zaidi kutokana na vipaombele kama taifa lakini walau gap lisiwe kubwa kiasi cha kudhihirisha upendeleo wa wazi kwa baadhi ya sehemu, na sehemu nyingine kubaki nyuma sana au kusahaulika kabisa hadi kufanya watu wa maeneo hayo kuanza kufikiria namna za kujijomboa wenyewe maana hawazingatiwi. Mf. Watu wa niger delta nchini Naijeria wanaona wanatoa mafuta lakini wanabaki nyuma hivyo kuanzisha vikundi vya upiganaji kama MEND - Movement for Emancipation of Niger Delta. Vikundi vinapata wepesi ktk kupata wapiganaji wenyeji kwakuwa wengi wana manung'uniko juu ya serikali yao.

2. Kuwekeza katika ujenzi wa jamii yenye uzalendo na kuimarisha umoja wa Taifa. Yaani kuua chembechembe za vitu kama udini, ukabila, kanda flan kujiona zina nguvu kuliko nyingine, uchama usiojali taifa n.k

● Udini ukiachwa huwa ni rahisi kwa watu wenye nia ovu kupandikiza itikadi zao ovu kwa kisingizio kuwa tunatetea dini. Wengi wanapigana kwa kisingizio cha dini lakini ndani wana ajenda kama kutaka madaraka au kuvuna rasilimali nk

●Ukabila na ukanda pia haufai kwakuwa unaweza kutumika kupenyeza ajenda ovu kwa kisingizio cha kutetea maslahi ya kabila au kanda kumbe lengo ni jingine kabisa

●Vyama ni muhimu lakini taifa ni muhimu zaidi kwani bila taifa hakuna vyama. Ruksa kutofautiana katika msimamo, itikadi ajenda lakini linapokuja suala la umoja wa taifa tunaweka pembeni tofauti zetu na kutanguliza maslahi ya taifa kwanza. Vyama vingi vimegeuka makundi ya waasi na vingine vimetumiwa na maadui wa Taifa kuvuruga amani.

▪Jukumu la kuhakikisha uzalendo si, tu, la serikali, bali pia sisi wananchi maana sisi ndio tuna dini, tuna vyama tuna makabila na kanda, tusikubali kushiriki katika kuvuruga amani kwa kisingizio cha dini, chama, kabila au kanda. Zipo njia nyingi za kutatua changamoto kwa amani tuzitumie hizo zaidi na ukichunguza sana utagundua wengi wanaotumia makundi haya wana ajenda za siri na ni rahisi kurubunika na maadui

3. Demokrasia, maendeleo na utawala bora. Kwa ulimwengu ulipofikia hivi vitu havikwepeki na lazima viambatane ili taifa libaki na amani na umoja

● Usithubutu kukandamiza demokrasia kwa kisingizio cha kuleta maendeleo

● Uwekezaji ktk maendeleo ni vema uende sambamba na uwekezaji ktk demokrasia. Ndio maana nchi kama marekani, uingereza nk, mataifa yao yanasonga mbele kimaendeleo wakati huo huo haki zote za kidemokrasia zinazingatiwa kama ukomo wa vipindi vya urais, njia za kidemokrasia za kudai haki, uchaguzi unaofuata misingi ya kidemokrasia, mahakama huru na mabunge huru kwa mujibu wa katiba.

■ Nchi kama Libya pamoja na maendeleo makubwa iliyokuwa imefikia, yalikuja kupukutika ndani ya muda mfupi kutokana na ukosefu wa demokrasia. Tunaweza kusema ni njama za watu wa magharibi kupitia NATO lakini tusisahau kuwa hao wote kazi yao ilikuwa rahisi sana sababu tayari wananchi walikuwa wamegawanyika. wengine wameuchoka utawala wa muda mrefu na wengine wameridhika, kumbuka watu wa Bengazi.

■ Kumbuka Mugabe alifanya mengi makubwa lakini kelele ilitokana na kumchoka na uminywaji wa demokrasia hasa nyakati za chaguzi

\■Kuna nchi hapa Africa, wengine ni jirani zetu, wanapiga hatua sana kimaendeleo lakini wameminya sana demokrasia. siwezi kuguarantee maendeleo yao kwakuwa joto linazidi kupanda toka ndani na nje ya nchi kupinga tawala hizo zisizo za kidemokrasia na za muda mrefu, siku kamba ikikatika pabaya ndipo na maendeleo yote yatapukutika kwa machafuko.

4. Ufisadi uliokithiri hadi kudumaza mifumo yote ya nchi na kuongeza gap kati ya wenyenacho na wasionacho. Hili limesababisha baadhi ya mataifa kuingia ktk machafuko kwakuwa wanufaika wa rasilimali za nchi ni wachache wenye nguvu na fedha na mifumo ya kudai haki au kuleta maendeleo nayo imeathiriwa na ufisadi hivyo watu kushindwa kupata haki wala maendeleo kama huna chochote cha kutoa ili upate au connection na wenyenacho.

Kutokana na mifumo kuharibika kwa rushwa na ufisadi, hupelekea vitu kama uingizwaji wa silaha kuwa rahisi maana unahonga wahusika mambo yanaenda. Mwisho wa siku mnajikuta kuna vikundi vyenye silaha ndani ya nchi na vina nguvu mf. IS-msumbiji, cabo delgado

Kwa case ya msumbiji imefikia hatua mataifa rafiki yanashindwa kuingia kusaidia kwasababu mifumo imeathiriwa na ufisadi kiasi kwamba kunakuwa na hofu ya kuwa ukienda kusaidia taarifa zako zote na mikakati itavuja kwa waasi kwa urahisi kwakuwa unaoshirikiana nao wana strong ties na waasi through hongo

● Nirudi kwenye hoja ya mataifa ya magharibi au yakigeni kuingilia mataifa na kuvuruga amani. Hili lina ukweli sana lakini ili lifanikiwe linategemea sana hali ya taifa husika hasa katika maeneo niliyoyaelezea hapo juu. Kama kuna nyufa mojawapo kati ya hizo ni rahisi sana kwa mataifa hayo kupenyeza maslahi yao na kupata wanavyotaka kwa njia ovu.

● Taifa likianza kutengeneza nyufa litarajie kuna vitu vya nje vitaanza kupenya kuingia ndani.

● Nyongeza: mataifa makubwa na mengineyo ya jirani ili yeweze kupenyeza ajenda zao ovu kama kuzing'oa serikali madarakani, kupora rasilimali, au kuchafua amani.

● Moja kati ya golden chance wanazotumia sana ni michakato ya uchaguzi ndani ya nchi target, michakato ya kutunga sheria mpya za kulinda au kuvuna rasilimali mf. Madini na zaidi mchakato wa kuandika katiba mpya.

● Kama kweli waTanzania tunaitaka katiba mpya, basi ni wakati ambao tunatakiwa kuwa wamoja na wazalendo kuliko wakati uliopita. Maana tukiruhusu mgawanyiko au ufa wowote tutaruhusu kupenyezwa kwa vitu vya hatari kwa ustawi wa Taifa au tunaweza kuiweka rehani amani ya taifa letu.

■ Hii michakato inayoendelea ya kutaka katiba mpya iendelee lakini katika namna ambayo inatanguliza maslahi ya taifa letu kwanza. Kutofautiana ni jambo la kawaida lakini tusiweke misimamo ambayo itahatarisha taifa letu. Ifike hatua ambapo kila kundi liweza kuweka maslahi ya taifa mbele iwe ni wafanyabiashara, wanasiasa, wataalam mbalimbali, watu wa dini, wakulima, wafugaji, diaspora n.k

Tusiruhusu tofauti zetu kutugawa. Aliye taratibu tumweleweshe twende pamoja, tusifanye kama ni hitaji la kundi flan tu au tutaipata kwa hisani ya flan, tusing'ang'ane na itikadi zetu. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ukiona mwenzako au kundi lako linataka kushirikiana na wageni kataa hata ikibidi kutoa taarifa, lengo tufike pamoja na tufike tukiwa salama sio tumegawanyika.

● Itasikitisha sana kuona kauli au matendo ya kubaguana na kugombana kwa kisingizio cha katiba. Katiba yetu iwe ni zao la maridhiano

● Najua watu wa nje wenye maslahi yao wanatazama kwa makini ili kuona kama watapata golden chance ya kupenyeza maslahi yao kwetu na hasa kwa kupitia waTanzania wenzetu. TUSIWAPE NAFASI

● Sio kwamba katiba mpya haitakiwi au inaogopwa na watu flan. HAPANA, ni kwamba, unaangaliwa umakini na utayari wa watu wote ili isije ikawa chanzo cha kuumiza taifa, bali iwe chanzo cha kustawisha taifa. Kwahiyo wote tuoneshe utayari wetu na umoja wetu na kuchukuliana tofauti zetu ili hatimaye iwezekane kupata katiba mpya yetu sote. Wote ni wa muhimu na Tanzania ni ya muhimu sana pia.

#PAMOJA TUJENGE TAIFA LETU
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRICA
ASANTENI SANA
 
Katiba mpya bila utawala bora na uzalenda mambo yatakua yale yale...
 
Back
Top Bottom