Katiba Mpya chini ya saa 100! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Katiba Mpya chini ya saa 100!

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by maggid, Apr 8, 2011.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Apr 8, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Ndugu Zangu,


  TUMEONA na kusikia kwenye taarifa ya habari TBC1 jana usiku, Waziri wa Sheria Na Katiba Bibi Celina Kombani akitamka; kuwa utaratibu wa kukusanya mawazo ya wadau juu ya mapendekezo ya Muswaada wa Sheria itakayosimamia mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya utachukua siku tatu!


  Na ulianza jana, Dodoma na Dar es Salaam. Leo zimekuja taarifa, imeongezwa siku moja zaidi. Utachukua siku nne, saa 96. Naam. Chini ya saa 100! Ina maana , kuwa baada ya saa 96 za kukusanya maoni ya wadau Muswaada utarudi tena bungeni na kujadiliwa na waheshimiwa wabunge.  Na ukipitishwa, basi, mchakato unaendelea ukimruhusu Rais kuanzisha mchakato kwa kuwateua wajumbe wa Kamati itakayoratibu mchakato na mengineyo. Na tafsiri kuu hapa ni hii; Watanzania tutakuwa tumepewa Katiba Mpya tunayoililia chini ya saa 100. Na lifuatalo nina hakika nalo, kuwa Watanzania HATUTARIDHIKA nayo. Kwanini? Fuatilia ninachoandika, utanielewa.


  Ni juzi tu nimeandika kupitia safu yangu kwenye Raia Mwema, kuwa; ” Nauona, mwelekeo mbaya wa upepo wa kisiasa nchini mwetu. Nina shaka kubwa. Naamini, tuko wengi wenye mashaka na mwelekeo wa nchi yetu tunayoipenda.” ( Mraba Wa Maggid, Raia Mwema, Aprili 6, 2011 )


  Kwenye makala yangu ile niliweka wazi, kuwa katika hili la mchakato wa kupata Katiba Mpya tumeanza na mguu mbaya. Tumeyaona Dodoma na Dar es Salaam jana. Sikuhitaji kuwa na Elimu ya Unajimu kubaini hilo. Tulishaziona ishara.


  Hakika, ikitaka, Serikali inaweza kurudi nyuma na kuanza upya. Wahenga walitwambia, ni heri nusu shari kuliko shari kamili. Katiba ni ya Watanzania, kwanini usiwepo ’ Mchakato Kivuli’- Shadow process utakayojumuisha makundi mbali mbali ya kijamii. Wajadili kwa uhuru kabisa, yote. Kisha nao waje na mapendekezo yao. Ingeepusha shari kamili.


  Haiyumkini suala nyeti kama la Muswaada wa Mapendekezo ya Sheria itakayosimamia mchakato wa Katiba likajadiliwa na wadau kwa siku nne tu. Ndio, chini ya saa 100. Maana, Katiba ya nchi ni kitabu nyeti chenye kuhusu maisha ya kila siku ya Mtanzania. Hauingii akilini, utaratibu wa wadau kujadili Muswaada huu kwenye kumbi za Msekwa Dodoma na Karimjee Dar. Halafu ikawa basi, imetosha. Urudishwe kwa Wabunge, waujadili, kisha waupigie kura, na zaidi kuupitisha.


  Watanzania tuko zaidi ya milioni 42. Ni vema na ni busara kukawepo na wigo mpana zaidi wa kuwafikia Watanzania wengi zaidi kadri inavyowezekana. Hivi, inatoka wapi, ’ghafla’ na ’dharura’ hii ya wadau kutakiwa kutoa maoni yao ndani ya saa 96? Maana, hili ni suala nyeti kwa Watanzania na lenye kuhusu mustakabali wa nchi. Kwa nini tusipewe muda zaidi wa kutafakari?


  Na wahusika wana nafasi ya kujisahihisha na kuokoa sura zao. Maana, tukubali, kuwa mchakato unaoendelea hautasaidia kupata Katiba itakayowapa imani Watanzania kuwa italinda maslahi ya taifa lao na yenye kukidhi matakwa ya wakati tulionao. Hayo ni mashaka ya kweli ya Watanzania walio wengi, yasipuuzwe. Na Watanzania wanajua, kuwa wanachokitafuta sasa walikuwa nacho, walikipoteza, kwa bahati mbaya.


  Na kuna kisa kutoka Uganda. Milton Obote, mbali ya mambo mengine, anakumbukwa na Waganda kwa tukio la kihistoria la ’ Kuchakachua’ Katiba ya nchi hiyo kwa kuifanyia mabadiliko kinyemela. Ilikuwa Aprili 15, 1966. Ilikuwa aubuhi moja. Wabunge wa Uganda, kabla ya kikao, walielekezwa kwenye masanduku yao ya makabrasha bungeni wakachukue ’ Muswaada wa dharura’ wa Marekebisho ya Katiba.  Muswaada ule wa Marekebisho ya Katiba ukajadiliwa ’ kishabiki’ na kupitishwa ndani ya saa moja. Unakumbukwa kwa jina maarufu la ’ Pigeon-hole’ Constitution- Katiba ya Sanduku la Makabrasha. Ni kitendo kile cha Obote, ndicho kilichopelekea Uganda kupitia wakati mgumu kwa miaka miaka mingi zaidi baadae.


  Si tunajua, kuwa Obote alikuwa na ugomvi na chama cha KY- Kabaka Yekka. Hivyo basi, alikuwa na ugomvi na Mfalme Fredrick Kabaka na WaBaganda. Katiba mpya ikampa nguvu nyingi Obote na UPC yake- Chama chake. Kabaka na WaBaganda walimtambua haswa Obote. Aliwanyanyasa kwa kuwafunga na hata kuwaua. Ndio, aliwanyamazisha, kwa muda.


  Lakini naye, Obote, hakubaki salama. Idi Amin akaja akampindua na kushangiliwa sana na WaBaganda wa Kampala na kwengineko. Kosa alilofanya Obote ni hili; kubadilisha Katiba kukidhi mahitaji yake na ya Chama chake katika wakati uliokuwepo. Obote hakuiangalia Uganda ya miaka 50 hadi 100 iliyofuata. Na hilo ndilo tatizo la viongozi wetu wengi Afrika.


  Tukirudi hapa kwetu, kwa kuusoma Muswaada ule wa sheria inatoa tafsiri hii; kuwa ndani ya saa 96 zilizopangwa za kupokea maoni ya wadau zitakuwa zimeweka msingi wa Watanzania kupatiwa Katiba Mpya wasiyoitaka, lakini, itakuwa imehalalishwa, kwa taratibu za Kibunge.  Kwani, haitarajiwi Wabunge wa CCM walio wengi kuukwamisha Muswaada huo. Na ikitokea wakafanya hivyo, kwa maana ya Wabunge hao wa CCM wakaukwamisha Muswaada huo wa sheria, basi, Wabunge hao wa CCM watakuwa wameanza kazi ya ’ Chama kujivua magamba’ na baadhi yao kunusurika na adhabu ya wapiga kura ifikapo 2015.


  Ni ukweli, kuwa Nchi yetu iko njia panda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ’ kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi, wakiwamo viongozi, wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo. Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi.

  Watanzania tuna kiu kubwa ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo.
  Kwa viongozi watakaochangia kutupitisha kwenye njia ya kwanza, nahofia, kuwa hao watakumbukwa kwa dhamira yao hiyo mbaya kwa Watanzania.


  Kwa wale viongozi watakaochangia katika kutupitisha kwenye njia ya pili, basi, hao hawatasahaulika mioyoni mwa Watanzania. Watakuwa ni wanadamu walioamua kuachana na ubinafsi na kutanguliza maslahi ya taifa. Ni imani yetu, kuwa hata Wabunge wengi wa CCM wanaweza kuingia katika kundi la viongozi hao. Kutupitisha kwenye njia ya pili.


  Na kama Bunge letu litabariki azma ya Serikali kuendelea kutupitisha katika njia hii ya kwanza kwenye mchakato huu wa Katiba, basi, ni dhahiri, kuwa tuendako kuna giza zaidi kulipo hapa tulipoanzia. Kuna watakaoikumbuka Katiba yetu ya sasa.


  Na hiki ni kipindi kigumu sana Nchi yetu inakipitia tangu tupate Uhuru wetu.
  Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.


  Maggid,
  Dar es Salaam
  Ijumaa, Aprili 8, 2011
  MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
   
 2. Ng'wanangwa

  Ng'wanangwa JF-Expert Member

  #2
  Apr 8, 2011
  Joined: Aug 28, 2010
  Messages: 10,180
  Likes Received: 897
  Trophy Points: 280
  the sound of patriotism.
   
 3. T

  Tovu Member

  #3
  Apr 8, 2011
  Joined: Oct 21, 2010
  Messages: 8
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  CCM walijenga nchi chiini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere na sasa tunakoelekea ni kuibomoa sababu wanataka kuwafanya watu kuwa hawana elimu ya kujitambua wao ni wakina nani katika nchi yao na ndio maana wanatufanyia haya hivi hii katiba ni ya kwao! mimi nahisi ni mali yao na ndiyo maana hawataki kuwapa wananchi vita haipo Tanzania lakini naona sasa inalazimishwa iwepo kwa hili tu. wacha wachakachue lakini Tanzania itakuwa si sehemu salama tena na hii ni kusudi tu.
   
 4. L

  Losemo Senior Member

  #4
  Apr 8, 2011
  Joined: Mar 30, 2010
  Messages: 183
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kwa namna yoyote ile nchi haiwezi kuwa na katiba ya masaa 96 na ikabaki salama. Tuikatae sasa ili mbele ya safari tupate kuwa salama. Bunge liache ushabiki lifanye kazi ya kulinusuru taifa. Tumeanza na mabomu ya kutoa machozi, Baadaye yatakuja mabomu ya kutoa damu. Mungu tuepushe na hili janga
   
 5. T

  Tovu Member

  #5
  Apr 8, 2011
  Joined: Oct 21, 2010
  Messages: 8
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Unajua mtu anekuuchokoza na kukuangalia utafanya nini ni serikali yatu ndivyo inavyofanya hivi wao hawajui watu wanadai katiba kwa sababu ya matatizo gani yaiyoko kwenye katiba? mpaka mambo ambayo ni muhimu kuyajadilii kwenye katiba wao ndio wanaema hayajadiliki hii kali na haya ni malekebisho ya katiiba na sio katiba mpya.
   
 6. Shalom

  Shalom JF-Expert Member

  #6
  Apr 8, 2011
  Joined: Jun 17, 2007
  Messages: 1,315
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Ulichokuwa unashabikia wakati wa uchaguzi kwani ulitegemea nini?
   
 7. Mpevu

  Mpevu JF-Expert Member

  #7
  Apr 8, 2011
  Joined: Nov 23, 2010
  Messages: 1,816
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Maggid,

  Hakika mtazamo wako ni wa kina hasa, ni angalizo lenye kheri mbeleni. Nionacho, NCHI IPO TETE KWA SASA NA HATUNA BUDI KUJITOLEA MHANGA KUNUSURU TAIFA.
   
 8. Dingswayo

  Dingswayo JF-Expert Member

  #8
  Apr 8, 2011
  Joined: May 26, 2009
  Messages: 4,011
  Likes Received: 86
  Trophy Points: 145
  Wakati mwingine nakua na wasiwasi na viongozi wetu kama kweli wanatumia busara zavyo ipaswavyo. Katiba nzuri, inayogusa masuala yote nyeti, ni kama msingi mzuri wa nyumba. Ukijenga msingi mzuri, una uhakika kuwa nyumba yako itakuwa imara. Ukijenga msingi mbovu na kwa haraka haraka, hakika utakuwa na kazi za kuziba nyufa, kama sio kujenga kuta nzima.

  Viongozi wetu wanasahau kuwa Watanzania wa sasa sio wale wa miaka 10 iliyopita. Wamebadilika sana katika mitazamo yao kisiasa na hata vile kijamii. Viongozi wakumbuke kuwa, ni rahisi sana kwao kuondolewa na wananchi, kuliko wao kuwaondoa wananchi. Kwa bahati nzuri tumeona mifano ya hivi karibuni ambapo viongozi wengi wmwondolewa na wananchi, na hakika hii kasi itaendelea popote pale ambapo wananchi wataona kuwa haki zao za kijamii na kisiasa zinakiukwa. Hali hii pia inaweza kutokea Tanzania. Tunachotakiwa kufanya sasa, na fursa tunayo, ni kujiwekea katiba ambayo italinda uhuru na maisha ya kila Mtanzania kwa kuzingatia haki na usawa.

  Jana niliona kwenye ITV mambo ambayo sikutegemea kuyaona Tanzania. Kitu kimoja ambacho nilikuja kuona baadae ni kuwa, ingawa nilistushwa na niliyoyaona, sikushangazwa nayo, maana nilikuwa nahisi kwa siku nyingi tu kuwa haya yatatokea. Niliyoyaona ni yale mauaji yaliyofanyika kule Tegeta. Niliona mtu anacharazwa mapanga, mithili ya picha nilizoziona live CNN na BBC za kule Rwanda miaka ya 1994, kama sikosei.

  Nawaomba viongozi wetu waache kuwa na uchu wa madaraka, wafikirie zaidi taifa hili na vizazi vya baadae. Uchu wa madaraka ni wa ki binafsi, faida zake kwa mtu hudumu muda mfupi na madhara yake ni makubwa kwa anayehusika na taifa kwa ujumla. Mapenzi kwa taifa badala yake yana faida ambayo itadumu milele.
   
 9. Najijua

  Najijua JF-Expert Member

  #9
  Apr 8, 2011
  Joined: Nov 5, 2010
  Messages: 1,029
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Tatizo la viongozi wa taifa hili ni kujishau na kushindwa kuwaheshimu wanao waongoza wakati wao wakitaka wapewe heshima zao kwa gharama zozote zile. Hawajui kuweka maslahi ya wananchi mbele daima wanaweka ya kwao na chama mbele.

  Kwa hakika na tabiri kama haya yanayifanyika kuhusu katiba mpya yataendelea hivi mwaka huu hautoisha bila nchi kuingizwa katika vurugu zisizo na sababu na zinazoweza kuzuilka mapema kabisa

  Tuendelee kuyasemea haya na kuzidi kuwaonya viongozi waache haya kuepusha yanayoweza kuepushika kwa sasa
   
 10. The Finest

  The Finest JF-Expert Member

  #10
  Apr 8, 2011
  Joined: Jul 14, 2010
  Messages: 21,709
  Likes Received: 43
  Trophy Points: 145
  Hapo kwenye red napatwa na wasiwasi sana, kwenye bluu nashindwa kuelewa ni kwanini makundi mbali mbali ya kijamii hayajashirikishwa ili na wao waje na mapendekezo yao.
   
 11. T

  Tanganyika Member

  #11
  Apr 8, 2011
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 67
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Tatizo la viongozi wengi wa Kiafrika hawajui kusoma alama za nyakati na kama wanajua basi madaraka yanawalevia mpaka wanapoteza fahamu stahili!! angalia bwana gBagbo alivyobembelezwa aachie Ikulu akakataa.....mpatanishi Raila Odinga alimshauri aaichie Ikulu apate hifadhi halali na hifadhi ya mali zake lakini bado akawa mbishi.......sasa anaelekea wapi??? heri nusu shari badala ya shari kamili, Kikwete ameshaona hali ya kisiasa nchini ilivyo lakini yeye na washauri wake bado wanataka kuchakachua Katiba ambayo ni mali ya wananchi na si ya viongozi kama walivyochakachua Uchaguzi..........hili halitakubalika kamwe hata kama wabunge wa CCM watalipitisha, sidhani kama wabunge wa ccm ni wengi kuliko raia!! Kikwete umetawala TZ kwa miaka 5 umeshajijengea sifa na umeshachota cha kukutosha wewe na familia yako.........angalia hii miaka 4 na nusu iliyobaki isije akaja kuwa fedheha kwako hata kile ulichochota ukakosa kukifaidi, Kumbuka kilichotokea au kinachoendelea kutokea kwa wenzako hata kwako kinaweza kutokea dakika yoyote na sekunde yoyote.......nakushauri achana na washauri wabovu/wabinasfi kwani mambo yakiharibika hayatakula pande yao bali itakula pande yako. KATIBA YA MASLAHI YA MTU MMOJA/WATU WACHACHE AU CHAMA FULANI HATUTAIKUBALI KAMWE.........HII NCHI MUNGU ALIWAPA WA-TZ WOTE NA SI KIKUNDI CHA WATU FULANI!!!MUNGU TUSAIDIE . AMEN.
   
 12. T

  Tanganyika Member

  #12
  Apr 8, 2011
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 67
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ni bora tukutane na mabomu ya kutoa damu tukaokoa nchi yetu kwa ajili ya watoto na wajukuu wetu kuliko kuogopa hayo mabomu na watoto wetu wakaja kuendelea kuteseka na kufanywa watumwa ndani ya nchi yao............unafikiri hao waliyopigwa risasi na mabomu huko tunisi, misri, libya na ivory coast hawakujua au hawajui adhari za risasi na mabomu?? Walitambua na wantambua lakini walisema ni bora kufa kuliko kuendelea kuwa mtumwa ndani ya nchi zao.

  "changes are around the corner" god be with us.......amen.
   
 13. T

  Tanganyika Member

  #13
  Apr 8, 2011
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 67
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kikwete ni jinsi gani unavyowadharau Watanzania........eti kwa kuwa wanataka katiba mpya basi umekubali kuwaridhisha unafanya unavyotaka ili mradi katiba mpya imepatikana hata kama haina maslahi kwa wa -TZ........hapo umepotea njia my friend, wa -TZ wanataka katiba kwa ajili ya maslahi yao na si maslahi ya viongozi wao. Hivyo waachie wajitengenezee katiba yao wenyewe, penda usipende katiba kwa ajili ya maslahi ya watanzania itapatikana kwa amani au ikibidi kwa kwa gharama zingine zozote!! na ukae ukijua isipopatikana kwa amani.........hiyo njia nyingine itakugharimu wewe!! MUNGU TUSAIDIE - AMEN.
   
Loading...