JUKATA: Tumekuja na sheria za mfano kufanikisha mchakato wa katiba mpya

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) limetoa sheria mbili za mfano kwa ajili ya mchakato wa kufanikisha Katiba Mpya ambapo wamedai kuwa uandaaji wa sheria hizo ulihusisha makundi mbalimbali kwenye jamii ili kupata maoni.

"JUKATA inatangaza kutoa Sheria mbili za mfano, sheria mfano ya marekebisho ya Katiba na sheria mfano ya kura ya maoni pamoja na nyaraka mbili zinazotoa ufafanuzi juu ya sifa za upatikanaji wa kamati ya wataalamu pamoja na namna bora ya usimamizi na utatuzi wa migogoro inayoweza kutokea katika mchakato wa Katiba mpya" taarifa ya Jukata imeeleza

Taarifa ya wadau hao imeeleza kuwa Sheria mfano ya mchakato wa Katiba imetoa hatua za mchakato, upatikanaji wa kamati ya wataalamu, majukumu yake pamoja na maswala mengine ikiwemo pia kuainisha namna migogoro inavyoweza kutatuliwa na kusimamiwa na kamati ya mchakato, imependekeza masuala ya kibajeti na vitu gani vinaweza kufanyika katika hatua za mpito wa kupata Katiba mpya.

Katika mchakato wa kuandaa sheria hiyo wadau hao wamedai kuwa walipata fursa ya kukutana na makundi mbalimbali kwenye jamii wakiwemo wanasiasa, wanahabari, wanazuoni, viongozi wa dini, Asasi za kiraia, Kamati ya Bunge ya Katiba na sheria pamoja na wadau wengine.

Akifafanua baadhi ya mambo ambayo wameyaanisha kwenye nyaraka hizo za mfano Dk. Ananilea Nkya amedai kuwa wameonesha utaratibu ambao umeuita 'marekebisho madogo' ambao unaweza kutumika kama mbadala kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024 endapo Katiba mpya itakuwa bado haijapitishwa kuanza kutumika, amedai kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuepusha baadhi ya changamoto.

Hata hivyo wadau hao wamesisisitiza tena kuwa hawaungi mkono kauli ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbalo kuhusu kutaka kuanza mchakato wa kutoa elimu juu ya Katiba iliyopo kwa miaka mitatu, badala yake wanadai elimu ijielekeze kwenye mchakato wa Katiba mpya wakitolea mfano mchakato walioufanya wa kutoa sheria za mfano.

Akisoma taarifa hiyo leo Agosti 31, 2023 mbele ya wanahabari, Mkurugenzi wa JUKATA, Bob Wangwe amesema kuwa mchakato wa Katiba mpya unahitaji uwepo wa sheria zinazoendana na wakati na mahitaji ya sasa.

Aidha wametoa wito kwa Waziri mteule wa Katiba na Sheria, Pindi Chana kutoa ratiba za mchakato wa Katiba mpya ili kuondoa sintofahamu ambayo imetawala miongoni mwa wadau wa Katiba na watanzania kwa ujumla.

Katika wito wao mwingine wadau hao wanaitaka Serikali kuona umuhimu wa kutumia Sheria hizo za mchakato wa Katiba katika kutunga na kurekebisha sheria za mchakato wa Katiba wa Katiba wakidai kuwa zimezungatia mahitaji ya sasa ya Nchi pamoja uzoefu wa mchakato uliokwama mwaka 2014.

Ikumbukwe kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo harakati mbalimbali za wadau ikiwemo baadhi ya Asasi za kiraia, Wanaharakati, Vyama vya siasa na wadau mbalimbali kushinikiza mamlaka kuendeleza mchakato wa Katiba mpya.

Hata hivyo Rais Samia Suluhu Hassan tayari amechukua hatua mbalimbali zinazohusu mchakato huo japo baadhi ya wadau wamekuwa wakijitokeza na kudai kuwa mchakato huo unaenda kwa kusuasua hali ambayo inaibua baadhi ya maswali kwa baadhi ya wadau kama mchakato huo utaweza kufanikiwa kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 pamoja na uchaguzi Mkuu 2025.
IMG-20230831-WA0006.jpg
 
Back
Top Bottom