Kalamu Yangu
JF-Expert Member
- Dec 21, 2016
- 1,093
- 1,027
Siihitaji kamusi,kuipata tafsiri,
Ninaiota harusi,na haitokuwa siri,
Siyo mbio za mjusi,ukingoni kusubiri,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Kila ninaposikia,sauti yako kipenzi,
Sipendi kwona walia,sababu yangu mpenzi,
Na kwangu umetulia,tena enzi na enzi,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Nitakijaza kitabu, kuzitoa zako sifa,
Lakini isiwe taabu,nilishakupa wadhifa,
Mola atupe thawabu,atujaze maarifa,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Uzuri uvutiao,mola amekujalia,
Haufanani na wao,hilo nalishuhudia,
Pesa huifanyi ngao,mengi wayavulimia,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Wafanya nijiamini,nikatuna kila kona,
Na wakora wa mjini,hawaishi kunong'ona,
Eti unanipa nini,wanahamu ya kuona,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Na unapokuwa mbali,zile njozi hazinishi,
Nazikumbuka asali,picha hazikinaishi,
Ninaishia kusali,rohoni kwangu uishi,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Pia nakumbuka mbali,kipindi tunayaanza,
Nyimbo nilizikubali,hivyo ndivyo tulianza,
Zilivuka majabali,ulizipanga stanza,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Sitoisahau siku,ile siku twaonana,
Si mchana si usiku,sura yako niliona,
Yeyote hatokupiku,wala sitopiga kona,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Unapopata tatizo,waniita Morry wako,
Ninapokupa liwazo,watamani nije kwako,
Mpenzi wanipa tunzo,na daima niwe kwako,
Wewe maana ya penzi,ninakupenda muhibu.
Mpenzi wanithamini,kwa maneno na vitendo,
Huna roho ya kwa nini,unachojali upendo,
Laziz nakuamini,wala huhitaji lindo,
Wewe maana ya pendo,ninakupenda muhibu.
Napita kifua mbele,sina hofu abadani,
Wala sihofu kelele,nitazihofu kwa nini,
Wangoje vigelegele,kuvipiga kanisani,
Wewe maana ya pendo, ninakupenda muhibu.
Nitayasema mengi, siku ile ikifika,
Japo neno halijengi, kwetu linahitajika,
Wambea hatuwatengi,nao tunawaalika,
Wewe maana ya pendo, ninakupenda muhibu.