Kampuni ya Landfall Universe Limited yapitisha Sh 1.4 trilioni haramu

Simon Martha Mkina

Investigative Journalist
Sep 5, 2020
17
75
fincen2.JPG


Na Simon Mkina

Mamlaka za usajili na taasisi za kibenki Tanzania hazitambui kampuni ya Landfall Universe Limited, ambayo imefanya miamala yenye thamani ya Sh. trilioni 1.4 (Dola za Marekani milioni 620) kupitia kwenye akaunti yake ya benki kwa miaka mitatu mfululizo kati ya 2013 na 2016.

Kampuni hiyo inadai kusajiliwa Dar es Salaam, Tanzania na kwamba inafanya kazi zake nchini.

Upekuzi wa nyaraka na mtandao wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) hauonyeshi taarifa zozote juu ya kampuni ya Landfall Universe Limited na hakuna mahali popote jina hilo la kampuni linalokaribiana na hilo. Ugunduzi huu umeibua shaka kwamba kampuni hiyo ni “hewa,” ilianzishwa kwa kazi maalum; kutakatisha fedha.

Habari hii ni matokeo ya uchunguzi maalum wa miezi 16 uliopewa jina la FinCEN Files, baada ya Jumuia ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ) na shirika la habari la BuzzFeed News, Marekani, pamoja na washirika wake wengine kutoka nchi 88 duniani kuona nyaraka za benki zenye miamala yenye shaka.

Uchunguzi wa mwandishi unaonyesha kuwa Landfall Universe Limited ilituma au kupokea jumla ya Dola za Marekani 620,347,859 kutoka miamala 182 kupitia inayodaiwa kuwa Benki ya Standard Chartered ya Tanzania. Mtiririko huu wote wa pesa ulitokea tangu Julai 25, 2013 hadi Januari 11, 2016.

Benki ya Standard Chartered ya Tanzania (maarufu; Stanchart Tanzania) imekana kufanya biashara na kampuni ya Landfall Universe Limited wakati wowote tangu ilipoanza biashara zake Tanzania. Benki hiyo ilianzishwa nchini 1917.

Stanchart Tanzania ilionyeshwa akaunti za benki zilizotumika kupitisha kiasi hicho kikubwa cha fedha, lakini ilikana kuzitambua akaunti hizo na kueleza kwamba haijawahi kuhudumia akaunti zozote za aina hiyo. Akaunti za benki zilizoonwa na mwandishi wa habari hii ambazo zilihusika kupitisha fedha hizo zinaanza na sifuri saba (0000000).

Imebainika kuwa namba za akaunti za Stanchart Tanzania zinaanza na tarakimu mbili; “01” kwa akaunti ya Shilingi za Tanzania na tarakimu - “87” kwa akaunti ya Dola za Marekani, kila akaunti ikiwa na jumla ya tarakimu 13.

Uchunguzi kupitia nyaraka za benki unaonyesha Stanchart Tanzania ilipokea na kutuma fedha kwa benki dada ya Hong Kong, katika Jiji la Victoria, umbali wa maili 5,000 kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Benki ya Standard Chartered Hong Kong inajulikana kama SCBHK.

Baada ya kuulizwa, SCBHK ilikiri kupokea na kutuma fedha kwa niaba ya Landfall Universe Limited, lakini haikuweza kutambua lolote kuhusu uhalali wa kampuni hiyo inayodai kusajiliwa Tanzania.

Je, benki yenu iliendeshaji akaunti bila kuwa na nyaraka za usajili wa kampuni? Majibu ya SCBHK: “Hata sisi hatujui, kimetokea nini.”

Baada ya kubanwa zaidi, benki hiyo ilionyesha nyaraka ilizokuwa nazo kuhusu kampuni hiyo na zilioyesha ilikuwa imesajiliwa Tanzania. Benki hiyo ilikiri kufanya uzembe wakati wa kufungua akaunti hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizoonyeshwa na SCBHK, ofisi za kampuni ya Landfall Universe Limited ziko katika jengo la Palm Residency, Namba F10 - Pot 45/46, Barabara ya Chimara, Dar es Salaam, Tanzania.

Mwandishi wa habari hii alitembelea jengo hilo kubwa lenye ghorofa 18 na kuthibitisha kwamba chumba namba F10 ambacho kinadaiwa kuwa makao makuu ya kampuni ya Landfall Universe Limited, ni vyumba vya makazi tu na siyo ofisi. Kwa jumla, jengo zima lina vyumba vya makazi vipatavyo 72.

Meneja wa jengo hilo, Nehra Clo, alimwambia mwandishi kwamba ghorofa ya 10 yote ilitengenezwa kuwa vyumba vya makazi na haijawahi kukodishwa kuwa ofisi kwa mtu yeyote tangu kuanza kupangishwa.

Mwandishi wa habari hii alibaini kuwa chumba namba F10 kina sifa zote za makazi ya familia ambamo kuna vyumba vidogo vitatu vya kulala; kimoja ni ‘master’ na vingine viwili vidogo - kila kimoja na kitanda chake, kuna viti na kabati za kutunza nguo, jiko la kisasa, na sebule pana iliyokutwa na sofa kubwa nne.

Mwandishi alifahamishwa kwamba, raia mmoja kutoka China amekuwa mpangaji wa nyumba hiyo kwa muda mrefu.

Kwa miezi kadhaa, mwandishi alijaribu kuwasiliana na mpangaji huyo kwa simu aliyoipata, lakini kila wakati mpangaji huyo alipoombwa miadi, alikataa kukutana. Lakini, alipoulizwa ikiwa alifanya kazi na Landfall Universe Limited, mpangaji alikataa, akifafanua kuwa yeye anafanya kazi katika kampuni ya ujenzi ambayo hakuitaja. Pia alikataa kutaja jina lake, lakini ukaguzi wa mwandishi ulibaini kwamba nambari ya simu anayoitumia imesajiliwa kwa jina la "Fundi Bomba."

Kitengo cha uchunguzi wa fedha haramu nchini (FIU) kilichopo Dar es Salaam, kinasema kimefanya jitihada kuipata kampuni ya Landfall Universe Limited na wamiliki wake, bila mafanikio hadi sasa, hivyo kuthibitisha kuwa kampuni hiyo haipo.

Kazi ya msingi ya FIU ni kudhibiti utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi nchini. Kwa hiyo, ni jukumu lake kuchunguza miamala ya fedha yenye shaka.

Anwani feki
Mtaalamu wa shughuli za kibenki nchini, Salum Machibya, alisema – kwa mujibu wa maelezo, Landfall Universe Limited ni kampuni hewa, ilitumia anwani ya uongo kufungua akaunti katika Benki ya Stanchart Hong Kong, bila kuwa na uthibitisho.

"Kawaida, benki zinahitaji nyaraka kadhaa kabla ya mtu au kampuni kuruhusiwa kuwa na akaunti; hizi ni pamoja na pasipoti, anwani zilizothibitishwa na hati zingine muhimu za utambulisho," akaongeza.

Alisema kwa uhakika kampuni ya Landfall Universe Limited haikufungua akaunti zake nchini Tanzania, ilikuwa ni kampuni ya uongo, ingawa alishangaa namna ilivyoanza kazi na hatimaye kufanikiwa kutuma na kupokea kiasi kikubwa cha fedha.

fincen.graph1.png

Kampuni nyingine
Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa kuna kampuni nyingine ilipokea fedha kutoka Landfall Universe Limited, kampuni ya Sichuan Hongda Group Company Limited (SHG). Kampuni ya SHG imeitambua kampuni ya Landfall Universe Limited kama wakala wake wa biashara kwa bidhaa za chuma.

SHG imetambuliwa kuwa kampuni tanzu ya Hanlong Group, iliyoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Shanghai, China. Taarifa za kibenki zilizoonekana zinaonyesha kuwa SHG ndio mnufaika wa zaidi ya Dola za Marekani 350,000,000 kutoka kwa Landfall Universe Limited.

SHG ni miongoni mwa kampuni zingine ambazo zilipokea malipo makubwa kutoka kwa Landfall Universe Limited, ambayo ilitoa fedha kwa SHG kupitia miamala zaidi ya 100. Malipo haya yalikuwa kati ya dola 135,000 hadi zaidi ya 18.4 milioni, baadhi ya miamala ikipokelewa au kutumwa ndani ya tarehe moja.

Taarifa za benki zinaonyesha kuwa Landfall Universe Limited ilifanya miamala minne tofauti ambayo ni jumla ya dola milioni 10 kwenda SHG, Machi 6, 2014. Pia, Landfall Universe Limited ilifanya miamala minne tofauti ambayo ni kati ya dola milioni 12 hadi SHG - Agosti 5, 2014.

Pia, Landfall Universe Limited na SHG zilifanya miamala yenye jumla ya zaidi ya dola milioni 11.5 inayohusisha kampuni ya Best Metals Resources Limited. SHG ilipokea takriban dola milioni 1.5 kutoka Honours International Hong Kong Limited. SHG baadaye ilipokea zaidi ya dola 600,000 kutoka Gold Spring Company Limited.

Uthibitisho wa taarifa za biashara na vitambulisho vya kampuni zilizobainika kufanya kazi na Landfall Universe Limited haukuweza kupatikana kabisa kutoka kwa vyanzo vyetu vya habari.

Pia, SHG ilipokea malipo kupitia miamala 115 kutoka Landfall Universe Limited ikiwa inahusisha jumla ya dola 350,092,639 na miamala hii ilitokea kati ya Oktoba 30, 2013 hadi Machi 11, 2015.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Hanlong Group, Liu Han, tajiri wa madini wa China na ofisa wa zamani wa serikali ya nchi hiyo, alihukumiwa kuuawa Februari 2015 na mahakama ya China baada ya kutiwa hatiani wa makosa ya kutakatisha fedha, uhaifu wa mitandaoni, mauaji na kuendesha makundi ya uhalifu.

Sichuan Hongda ndiyo kampuni iliyosaini mkataba wa dola bilioni 3 na Serikali ya Tanzania ili kuanza kuchakata makaa ya mawe na madini ya chuma. Mkataba huo ulisainiwa Septemba 22, 2011. Mkataba huo ulihusisha makubaliamo mengi ikiwamo kuchimba makaa ya mawe Mchuchuma, ujenzi wa kituo cha umeme megawati 600 na kuhuisha uzalishaji wa chuma Liganga.

Katika mkataba huo, Sichuan Hongda inamiliki asilimia 80 ya mradi wa ubia, huku Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Kitaifa la Serikali (NDC), itakuwa na hisa 20 zilizobaki kwa niaba ya serikali.

Hata hivyo, hadi sasa, baada ya miaka 9, mchakato wa kuanza kwa shughuli huko Liganga na Mchuchuma, mkoani Njombe, bado haujaanza. Hii ni kwa sababu ya uchunguzi unaofanywa na serikali baada ya kuwepo kwa hisia za rushwa katika mchakato wa kuwapata wawekezaji.

Kampuni nyingine, Eagle Metal International Limited, inadaiwa kupokea fedha mara moja kwa Landfall Universe Limited, ikiwa ni jumla ya dola 13,551 Septemba 19, 2014.

Nyingine ni Mercuria Energy Trading, inayodai kuwa na Jiji la Singapore, Singapore - ilituma fedha mara 18 kwenda kwa Landfall Universe Limited, ikiwa ni jumla ya dola 110,622,043 na miamala hiyo ilitokea kati ya Januari 21, 2014 hadi Januari 5, 2015. Kampuni hii inaonekana kuwa na uhusiano wa karibu wa kifedha na kampuni ya Trafigura AG.

Kampuni ya Trafigura AG ilitoa fedha mara tisa kwa Landfall Universe Limited, ikiwa ni jumla ya dola 71,169,790.56 na miamala hiyo ilitokea kati ya Oktoba 24, 2013 hadi Mei 21, 2014, wakati kampuni ya Trafigura PTE ilianzisha miamala ya fedha mara kumi na tatu kwenda kwa Landfall Universe Limited yenye jumla ya dola 36,578,932, na shughuli hizo zilitokea kati ya Oktoba 31, 2013 hadi Machi 13, 2015.

Kampuni ya Ausinmet ilitoa fedha mara tatu kwa Landfall Universe Limited ikiwa ni jumla ya dola 21,172,374 na shughuli hizo zilitokea kati ya Novemba 21, 2013 hadi Desemba 9, 2013.

Kampuni ya Best Metals ilituma fedha mara nne kwa Landfall Universe Limited ikiwa ni jumla ya dola 9,524,330 na miamala hiyo ilifanyika kutoka Oktoba 23, 2015 hadi Januari 11, 2016.

Kampuni hizi, hazionekani kuwa na anwani za uhakika wala hazioneana katika mtandao wa intaneti. Ni kampuni ya Trafigura pekee mbayo ina wavuti, ikionyesha kuwa kampuni hiyo, yenye makao yake Singapore, inahusika katika biashara ya bidhaa mbaimbali na kuwa ilianzishwa mnamo 1993.

Barua pepe zilizotumwa kwa Trafigura kusaka ufafanuzi wa uhusiano wake na Landfall Universe Limited zilijibiwa kwa maneno mawili tu, "hakuna maoni," kutoka kwa msemaji wake, Victoria Dix.

Baadaye ilibainika kuwa kampuni ya Trafigura iko nchini Tanzania kupitia kampuni yake tanzu iitwayo Impala Terminals Dar es Salaam, ambayo ni wasafirishaji wa bidhaa anuwai.

Ofisa wa Impala alikana kuifahamu kampuni ya Landfall Universe Limited. "Sijawahi kusikia jina kama hili katika biashara yetu, hatujawahi kufanya biashara yoyote na kampuni ya Landfall," akaongeza, akipendelea kukaa bila kujulikana.

Serikali yapoteza kodi
Endapo kampuni ya Landfall Universe Limited ingekuwa kampuni yenye uhalali na endapo miamala hii ingekuwa imefanyika kupitia benki iliyoko Tanzania, serikali ingepokea kodi ya kampuni ya asilimia 30, ambayo ni zaidi ya Dola za Marekani 186,000,000 ikiwa ni sehemu ya Dola za Kimarekani 620,347,859 zilizosafirishwa.

Kiasi hiki kingetosha kujenga mabweni 100 ya kisasa yenye samani, umeme na maji ya bomba, na kwamba yangechukua zaidi ya wanafunzi wa sekondari 5,000 hivyo kupunguza changamoto kwa wanafunzi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo anasema ikiwa kiasi hicho kingelipwa kwa serikali, hivyo kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kiasi kikubwa.

Tanzania dhidi ya fedha haramu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema ikiwa hakuna kumbukumbu za Landfall Universe Limited katika ofisi zote za usajili wa kampuni, basi ni wazi kuwa ni kampuni ya ‘mkobani’ ambayo inahitaji kuchunguzwa.

Taasisi hiyo imesema inafahamu kuwepo kwa wawekezaji wasiokuwa waaminifu na raia wanaofanya biashara haramu, lakini hakuna uwezekano wa kuiweka Tanzania katika kundi la nchi zenye historia ya mazoea ya kutakatisha fedha na ufisadi wa kiwango cha juu.

Takukuru inadai kuwa uchunguzi wake wenye mbinu za kisasa, umefanikisha kukamata zaidi ya Sh. bilioni 190, ikiwa ni fedha na mali za watuhumiwa wa makosa ya kifisadi. Tayari Rais John Magufuli ameamuru kutaifishwa kwa fedha na mali hizo.

Wakili Nyaronyo Kicheere, akitoa maoni yake kuhusu namna ya kukomesha utakatishaji wa fedha alisema njia bora ya kupunguza hatari zaidi ni kuwepo juhudi pana na zilizoratibiwa kisayansi zaidi kati ya benki, mitandao ya malipo, wasimamizi na vyombo vya usalama.

“Kudhibiti fedha haramu ana yake ni kuimarisha usalama wa fedha na uchumi,” amesema wakili huyo na kushauri Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya uchunguzi mara kwa mara kwa taasisi za fedha ili kubaini upungufu kwenye utendaji na kuchukua hatua mapema.
 

kolola

JF-Expert Member
Apr 26, 2020
2,204
2,000
Kumbuka issue ya chuma ya mchuchuma na liganga ambalo mgombea fulani alikishadidia at JPM hayupo makini kuingilia kati
 

eddy

JF-Expert Member
Dec 26, 2007
13,794
2,000
Kampuni ime operate 2013 hadi 2016, uchafu ulikuwa unalindwa na serikali ya JK, JPM asingeonyesha umakini na kumaanisha tangu mwanzoni hawa watu wasingefunga biashara zao 2016.
yule jamaa anayelalamika biashara zimekufa atkuwa na mkono kwenye hii biashara
 

TUJITEGEMEE

JF-Expert Member
Nov 6, 2010
17,198
2,000
Sijui nimeipitia kwa haraka mno taarifa hii...!? Naona kuna vitu vingi vinakosa muunganiko. Nitarudia kuisoma baadaye. Kwa uchache, huyo "Fundi Bomba" ambaye hajulikani kwa mwenye nyumba, hiyo namba ya simu si imesajiliwa kwa kitambulisho cha NIDA!? Huyo, Mchina aliyehukumiwa kifo huko China, huku hiyo ilitekelezwa lini!?
 

Nazgur

JF-Expert Member
Apr 19, 2020
2,840
2,000
Mkuu hongera kwa kazi nzuri, nakuomba utumie utaalam wako utuambie hii kampuni ya Mayanga Construction ni ya nani? Kwa siku za karibuni imekuwa ikitajwa kwa namna isiyo pendeza

Sent using Jamii Forums mobile app
Mayanga wapo na wapo kazini hapa tanzania, nenda kawaulize wewe mwenyewe, na wako brela ukiwakosa huko njoo uanzishe uzi hapa.
Kama wewe mwenyewe hutaki kutafuta ukweli basi utulie ulishwe matango na bosi wako Tundu Lissu.

Usitegemee vya kuambiwa tafuta ukweli wewe mwenyewe.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom