Kamati ya Bunge yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya uviko pori la akiba Wami mbiki

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
Na. Beatus Maganja

Kamati ya kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii imeeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa miradi ya mpango wa Taifa wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO - 19 iliyotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ndani ya Pori la Akiba Wami Mbiki Mkoani Pwani.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mzava amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake wa kutafuta fedha na maelekezo aliyoyatoa juu ya matumizi ya fedha za UVIKO ambazo zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii.

"Kwa mazingira na hali tuliyoiona (Pori la Akiba Wami Mbiki) nadhani tutaungana sote kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Nchi yetu lakini hasa kwa ubunifu mkubwa alionao wa kutafuta fedha lakini pia maelekezo aliyoyatoa Juu ya matumizi ya fedha za UVIKO "

Mhe. Timotheo Mzava ameelekeza pia pongezi za Kamati yake kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kusimamia miradi hiyo ambayo iligharimu zaidi ya TZS bilioni mbili.

Sanjari na pongezi hizo, Kamati hiyo imetoa wito kwa TAWA kuongeza mikakati ya kibiashara na ya kimasoko ikiwa ni pamoja na kutangaza hifadhi hiyo ili miundombinu iliyotengenezwa iweze kutumika kama ilivyokusudiwa na Serikali kupata tija inayotarajiwa

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Malialisi na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amesema Wizara imejipanga kuhakikisha inaongeza jitihada katika kutangaza hifadhi hiyo ili kuongeza idadi ya wageni ikiwa ni pamoja na kutafuta wabia wa kushirikiana nao katika kuendesha shughuli za utalii na uwekezaji

Awali akifafanua hoja zilizoibuliwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu mikakati ya TAWA katika kuchechemua utalii katika hifadhi ya Wami Mbiki, Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema TAWA imekuja na mpango mahsusi wa kufufua hali ya hifadhi hiyo kwa kumtafuta mwekezaji ambaye atawekeza kituo cha kuokoa na kulea Wanyamapori wenye mahitaji maalumu (Wildlife Rescue and Rehabilitation Centre).

Amesema tayari TAWA imekwisha saini mkataba na mwekezaji huyo ambao unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa Wanyamapori wenye mahitaji maalumu kama vile wagonjwa, yatima, walionusurika katika matukio ya ajali na wanyamapori wanaotelekezwa na wazee wanaohitaji uangalizi maalumu.

Aidha amesema uwepo wa kituo hicho katika hifadhi ya Wami Mbiki utakuza utalii wa ndani na wa nje kupitia program mbalimbali zitakazoendeshwa ikiwemo program ya watalii wa kujitolea, utalii wa matukio lakini pia mwekezaji ameahidi kuleta wageni kati ya 30 mpaka 50 Kila mwezi jambo ambalo litachagiza utalii katika hifadhi hiyo.

Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii katika ziara hiyo ni pamoja na barabara yenye urefu wa kilometa 47.2, mabanda ya kulala wageni, lango kuu la kuingilia wageni linalojumuisha maduka ya kuuza bidhaa za utalii (Curio shops), jengo la kupumzikia wageni, jengo la kutoa taarifa kwa wageni (Visitors' Information Center), kituo cha mauzo, vyoo pamoja na nyumba za kuishi Maafisa na Askari watakaokuwa wakihudumia wageni.
IMG-20240111-WA0011.jpg
IMG-20240111-WA0007.jpg
IMG-20240111-WA0009.jpg
IMG-20240111-WA0010.jpg
IMG-20240111-WA0006.jpg
IMG-20240111-WA0005.jpg
IMG-20240111-WA0008.jpg
IMG-20240111-WA0004.jpg
IMG-20240111-WA0003.jpg

IMG-20240111-WA0012.jpg
 
Back
Top Bottom