UAMUZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwavua uanachama madiwani wake watano wa Arusha, umesifiwa kama mfano wa kuigwa na serikali na vyama vingine vya siasa katika kuchukua hatua nzito.
Wananchi kadhaa waliohojiwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha walisema CHADEMA imeonyesha mfano wa uongozi unaochukua hatua, huku baadhi ya makada wakisema hii ni ishara kwamba kinajiandaa kuchukua dola.
Wengi walisema ingawa CHADEMA haikuwa na uhakika wa kushinda tena uchaguzi katika kata hizo, haikujali kuchukua hatua dhidi ya madiwani watovu wa nidhamu, kwa sababu lilikuwa suala la msingi.
Mjini Arusha, miongoni mwa wananchi 50 waliohojiwa, 48 walisifu uamuzi na hatua ya CHADEMA na walisema wanasubiri kwa hamu uteuzi wa wagombea wapya utakaofanywa na CHADEMA ili wachague wawakilishe wengine.
Karim Abdalah, mkazi wa Kaloleni ambaye alijitambulisha kama mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema, "Kamati Kuu ni kikao cha juu kimaamuzi katika chama chochote cha siasa. Agizo lake likipuuzwa na mwanachama au kiongozi yeyote, halafu chama kikashindwa kuchukua hatua, kinakuwa dhaifu. Hawa waliofukuzwa walistahili kufukuzwa."
Aliyejitambulisha kuwa mkereketwa wa CCM, John Meddah, mkazi wa Sekei, ambaye anatetea dhana ya wagombea binafsi, alisema, "Ingawa ni maamuzi yanayozingatia sheria zilizopo sasa, huu utaratibu wa vyama kuwavua uanachama au kuwaondoa kwenye nyadhifa zao viongozi waliochaguliwa kwa kura za wananchi ambao baadhi hawana vyama unakandamiza demokrasia. Lazima sheria hii ibadilishwe. Ni sheria kandamizi."
Ombeni Mbise, mkazi wa kata ya Kaloleni, "Hawa madiwani walipitishwa na chama tukawachagua, wasifikiri wakiwa nje ya CHADEMA tutakuwa nao tena. Naunga mkono uamuzi wa kamati kuu."
Ephraim Kimaro, mkazi wa kata ya Kimandolu, alisema, "Madiwani hao wameshindwa kutambua kuwa viongozi wa juu wa chama wana kesi ya kujibu mahakamani ambayo chanzo chake ni kupinga mchakato wa uchaguzi wa Meya wa Arusha. Ni utovu wa nidhamu. Kama kweli walikuwa madiwani walipaswa kuheshimu viongozi wao."
Wananchi wengi wa Arusha walisema wanasubiri kwa hamu mkutano wa hadhara wa kesho utakaohutubiwa na viongozi wa kitaifa wa CHADEMA kufafanua hatua ya chama hicho kuwatimua madiwani hao.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema hatua ya CHADEMA imezingatia matakwa ya sheria na katiba ya chama, na kwamba anaunga mkono hatua hiyo kwa kuwa chama chochote cha siasa kinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni.
"Kama uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia kanuni na katiba ya chama pamoja na vikao ni mzuri. Huwezi kuendesha chama chochote cha siasa bila kuzingatia kanuni na taratibu.
"Lakini hilo ni fundisho pia kwa vyama vingine vya siasa nchini.
Kama wanachama au viongozi wasipotii kanuni na taratibu, lazima maamuzi magumu yachukuliwe" vyama vingine viige uzoefu wa CHADEMA," alisema Dk. Bana, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
"Ni jambo la ndani ya chama, hizo ni taratibu zao na sera zao ndani ya chama kwani mambo kama hayo hutegemeana na masharti ya chama husika," alisema mwanazuoni maarufu nchini, Profesa Issa Shivji, wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu na kukataa kuendelea kuzungumza zaidi.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema, "Sifahamu vizuri uhalali wa madiwani hao kufukuzwa, lakini athari za uamuzi huo kwa wananchi ni matokeo ya Katiba mbovu ya nchi inayovipa vyama mamlaka ya kufukuza wawakilishi wa wananchi.
"Tungekuwa tumepitisha sheria ya mgombea binafsi, vyama vingebaki na mamlaka ya kuchukua kadi tu lakini sio uongozi wa uwakilishi" watu walio kwenye vyama ni asilimia 10; wapo wengi waliopiga kura lakini hawana vyama, ndiyo maana tunahitaji Katiba itakayoviondolea vyama mamlaka ya kuamua hatma ya uwakilishi vibaki na mamlaka ya kuchukua kadi kwa mwanachama aliyekwenda kinyume cha misimamo ya chama," alisema Kafulila ambaye pia aliwahi kuwa mwanachama wa CHADEMA.
Madiwani hao walitimuliwa baada ya kugomea agizo la Kamati Kuu ya CHADEMA iliyowataka kujiondoa kwenye mwafaka bandia wa kugawana madaraka na CCM katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Wachache waliipinga hatua ya CHADEMA. Miongoni mwa waliopinga ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, ambaye alisema, "Ni tafsiri rahisi sana kwamba viongozi wa CHADEMA wanajali zaidi maslahi yao na chama badala ya wananchi wanaowaongoza"madiwani ni watu wa karibu sana na wananchi wanawajibika kuona kuwa wana Arusha wanaishi kwa amani na utulivu.
"Kitendo cha kuwashinikiza madiwani hao wakatae muafaka ni vurugu, na sisi tunajua kwamba vurugu hizo ziko ndani ya CHADEMA sio halmashauri"Napenda kumwambia meya, madiwani na wanachama wote wa CCM Arusha kwamba waendelee na shughuli zao za kawaida kwa maslahi ya wana Arusha," alisisitiza Nape.
Nape aliyasema hayo huku akiongoza harakati za CCM kushinikiza makada wake watatu Rostam Aziz, Andrew Chenge na Edward Lowassa, wafukuzwe katika uongozi wa CCM kwa tuhuma za ufisadi. Tayari Rostam ameshajiuzulu ujumbe wa Halmashauri Kuu na ubunge wa Jimbo la Igunga, na kulazimu ufanyike uchaguzi mdogo mwanzoni mwa mwezi ujao.
"Hivi Nape anataka kusema yeye aliposhinikiza Rostam Aziz na wenzake wajiondoe hawakuchaguliwa na wananchi? Mbona hazungumzii ubinafsi wa CCM katika hilo?" alisema mchambuzi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mchambuzi mwingine ambaye alijitambulisha kama mwana CCM na kuomba jina lake lisitajwe, alisema, "Tofauti ya wazi kati ya CCM na CHADEMA ni kwamba chama kimoja kinatumia muda mrefu kutangaza kwa umma kwamba kinataka kuwafukuza fulani na fulani, lakini kinashindwa kuwafukuza, na kingine kinafanya uamuzi palepale na kuchukua hatua. CHADEMA imeonyesha uongozi."
Chanzo: Tanzania Daima