Vijana 363 katika jimbo la Arumeru Mashariki, wilayani Arumeru, wameandaliwa kwa ajili ya kumlinda mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (CHADEMA), katika kampeni za ubunge Arumeru Mashariki kutokana na tishio la wazee wa kimila wa kabila la Wameru (Washiri).
Hatua hiyo imefikiwa siku chache baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kumtaka Lema awaombe radhi wazee wa Washiri kwa madai kuwa aliwaudhi wakati wa mazishi ya Jeremiah Sumari.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, vijana hao kupitia viongozi wao, walisema kuwa licha ya kuchukua hatua hiyo ya kumlinda Lema pia wanasubiri kuona Jeshi la Polisi litachukua hatua gani dhidi ya wazee hao kwa kutishia kuua.
Walisema kuwa kama polisi haitamchukulia hatua mwenyekiti wa Washiri, aliyetoa tamko hilo, wao watawapiga marufuku wabunge wote wa CCM na viongozi ambao hawaishi Meru, kuonekana katika jimbo hilo kuanzia Machi 9 mara kampeni zitakapoanza.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Yohane Kimuto (51) mkazi wa Sing'isi Meru, alisema kuwa ili kumhakikishia ulinzi Lema, tayari wameandaa kundi la vijana (Morani wa Kimeru) wapatao 363, kwa ajili ya kumlinda kila atakakopita wakati wote wa kampeni.
Kimuto alisema kuwa maandalizi ya vijana hao yamekamilikana wako tayari kwa ulinzi wa mbunge wao, ambaye wanamhitaji kwa hali na mali kwenye kampeni za Arumeru Mashariki.
Alisema kinyume na hapo kampeni hizo hazitakuwa salama, kwa sababu tayari kutakuwa na makundi mawili ya kumlinda Lema na lingine linalotaka kumuua na hapo amani itatoweka.
"Lazima ikumbukwe Meru tumekuwa kwenye vita tangu wakati wa vile vya kidini walipouawa wamisionari na ikajirudia tena mwaka 2009, katika mashamba ya Madira na watu kuswekwa gerezani na wengine kupoteza maisha, hili sasa hatutaki lijirudie," alionya Kimuto.
Aliongeza kuwa kwa niaba ya Wameru wenzake wanamtaka mwenyekiti wa Washiri, aliyetoa tamko hilo ajiuzulu mara moja, kwa sababu anafanya kazi ya siasa na kuacha kazi yake ya kuratibu mila na jadi za Kimeru.
Akizungumzia sakata hilo Kaimu Kamanda wa Polisi, Akili Mpwapwa, alisema mpaka sasa hawana wa kumchukulia hatua kwani hakuna mtu aliyekwenda kushtaki kutishiwa maisha.
"Ninachofahamu mimi ni kuwa mtu anapotishiwa maisha lazima atoe taarifa polisi ili apatiwe ulinzi na hivyo hadi sasa hakuna aliyetoa taarifa kuhusiana na vitisho vya Washiri," alisema Mpwapwa.
Source:Tanzania Daima