Kagera: Watu wanne wamefariki na wengine watano walazwa kwa ugonjwa wa kipindupindu

Bull Bucka

Member
Oct 5, 2023
34
46

Watu wanne wamepoteza maisha yao na wengine watano wamelazwa kwa matibabu baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Kijiji cha Buchurago, Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera.

Taarifa hii imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Bukoba leo, Desemba 4, 2023.

Kwa mujibu wa Mwassa, mlipuko huo wa ugonjwa uligunduliwa tangu Novemba 29, 2023, katika Kijiji cha Buchurago, Kata ya Bugorola, Wilaya ya Misenyi. Alibainisha, "Mlipuko huo umegundulika tangu Novemba 29, 2023, katika kijiji cha Buchurago baada ya watu wawili kutoka nchi jirani ya Uganda kuingia kijijini hapo. Hadi sasa, watu wanne wamepoteza maisha yao na wengine watano wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kajunguti wilayani Misenyi."

Mkuu huyo wa Mkoa amewaonya wananchi wa Kagera kuchukua tahadhari kwa kuchemsha maji ya kunywa, kunawa mikono kwa sabuni, kuosha matunda kabla ya kula, na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Mkazi wa Manispaa ya Bukoba, Savera Mutimavu, ameiomba Serikali siyo tu itoe elimu kwa umma kuhusu kujikinga dhidi ya ugonjwa huo, bali pia ihakikishe inawaweka katika hali ya tahadhari wataalam wa afya ili kukabiliana na milipuko katika maeneo mengine ndani na nje ya Mkoa wa Kagera kutokana na muingiliano uliopo.

"Hatuna budi kuhakikisha kwamba dawa, vifaa tiba, na wataalam wanapatikana kwa haraka kulingana na mahitaji yanayojitokeza," amesisitiza Halima Said, mkazi wa Hamugembe, Manispaa ya Bukoba.
 
Back
Top Bottom