UTEUZI wa nafasi za makamanda wapya wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa wa Arusha umekumbwa na "mauzauza" na malalamiko kutoka kwa wanachama wa jumuiya hiyo kwa kile kindachodaiwa kuwa viongozi kuwateua makamanda hao kwa malengo yao ya kisiasa.
Tayari uteuzi huo umezua mgogoro mkubwa ndani ya jumuiya hiyo mkoani hapa ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakionekana kupingana hadharani na maamuzi ya kamati ya utekelezaji ya mkoa.
Wanaolalamikia uteuzi uliofanywa katika nafasi hizo ni wanachama, wajumbe wa Baraza Kuu na baadhi ya viongozi wa kamati za utekelezaji za wilaya na mkoa ambao wanadai hawakushirikishwa katika maamuzi hayo.
Viongozi hao pia wanadaiwa kukiuka baadhi ya taratibu na kanuni katika uteuzi huo bila kufanya vikao vinavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Uteuzi unaolalamikiwa na vijana hao ni nafasi ya makamanda wapya kwa wilaya za Arumeru, Arusha na pia uteuzi wa nafasi hiyo kwa Mkoa wa Arusha.
Katika Wilaya ya Arumeru, jumuiya hiyo imemteua Goodluck Ole Medeye kuchukua nafasi ya mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi, Elisa Molell aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Elisa Molell
Medeye, ambaye ni Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), imeelezwa kuwa atawania nafasi ya ubunge katika jimbo la Arumeru Magharibi, na tayari anaendesha kampeni za chini kwa chini kuhakikisha kuwa Mollel harudi katika kiti hicho.
Hata hivyo, Medeye bado hajapitishwa na Baraza Kuu la vijana wa wilaya hiyo ambalo tayari limeandika barua ya malalamiko kwenda makao makuu ya Jumuiya ya Vijana wakilalamikia kukiukwa kwa kanuni na taratibu za kumteua.
Habari ambazo, hata hivyo, hazikuthibitishwa zilieleza kuwa Makao Makuu ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana tayari wameandika barua na kuwaelekeza viongozi wanaohusika kuanza upya mchakato wa kumtafuta kamanda wa wilaya.
Mbunge wa Arusha mjini, Felix Mrema
Uteuzi mwingine unaolalamikiwa ni wa nafasi ya ukamanda wa wilaya ya Arusha ambapo viongozi wa wilaya hiyo wamemteua Diwani wa Kata ya Olorien, Gaudance Lyimo kuchukua nafasi ya Felix Mrema.
Vijana hao pia wanalalamikia uteuzi wa Anoj Shah mwenye asili ya Kiasia kuwa Kamanda wa Mkoa wa Arusha na kumtosa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abrahman Kinana aliyekuwa kamanda kwa miaka 10.
Wakizungumza na Raia Mwema mwishoni mwa wiki, kundi la vijana hao kutoka wilaya za Arusha na Arumeru ambao waliomba majina yao yahifadhiwe kwa sasa, walieleza kuwa viongozi wa jumuiya hiyo katika wilaya hizo na wale wa mkoa wamekiuka taratibu na kanuni katika uteuzi.
Wakitoa mfano, vijana hao walieleza kuwa katika wilaya ya Arumeru, Katibu wa UV-CCM, Yasin Said Yasin aliteua jina la Medeye kwa maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Arusha, James Ole Millya bila ya kuwashirikisha viongozi wengine.
"Hata Mwenyekiti wa UV-CCM wilaya ya Arumeru, Esther Maleko hakushirikishwa katika uteuzi huo na jina la Medeye lilipelekwa moja kwa moja makao makuu; huku viongozi wakikata jila la Elisa Mollel", alieleza mmoja wa vijana hao.
"Viongozi wameondoa majina ya wabunge wawili (Felix Mrema, Elisa Mollel) kwa malengo ya kisiasa ili kuwanufaisha kisiasa wapinzani wao wanaotaka kugombea ubunge katika majimbo hayo mawili", alieleza.
Mwanachama mwingine alidai kuwa viongozi hao wamefanya uteuzi huo kwa lengo la kuwaridhisha viongozi wa kisiasa na uteuzi huo pia umelenga kuwajenga kisiasa walioteuliwa ambao wana nia ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
"Maamuzi haya yamefanyika bila kuzingatia maslahi ya vijana ila kwa lengo la kuwaridhisha viongozi wa kisasa katika mkoa wa Arusha ambao ndiyo wamekuwa wakiwafitini wenzao", alisema mjumbe huyo huku akisita kuwataja viongozi hao.
Aidha, vijana hao pia wamelalamikia uteuzi wa nafasi ya Kamanda wa Mkoa wa Arusha ambapo habari zinadai kuwa nafasi hiyo amepewa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya utengenezaji vyandarua na bidhaa mbalimbali za plastiki, Anoj Shah mwenye asili ya Kiasia.
Kinana, Mjumbe wa Kamati Kuu
"Haingii akilini eti umwondoe Mzee Kinana ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na ana uzoefu mkubwa katika masuala ya Chama na kisha kumteua mfanyabiashara ambaye inawezekana hata si mwanachama wa CCM……sijui chama chetu kinaelekea wapi"?, alihoji mmoja wa vijana hao.
Vijana hao pia wanamlalamikia Mwenyekiti wao Millya kuwa anatumiwa na baadhi ya wanasiasa wenye majina makubwa kuvuruga jumuiya hiyo kwa malengo ya kisiasa.
Wanasema kwamba ili kufanikisha malengo yake amekuwa akiwatisha vijana wanaohoji masuala mbalimbali kuwa atawafungulia kesi polisi.
"Hivi karibu Millya aliwatishia wajumbe wa wilaya ya Arumeru kuwa wale wanaopinga uteuzi wa Medeye watachukuliwa hatua za kisheria na wengine wataitwa kuhojiwa na kamati ya utekelezaji na kuchukuliwa hatua za kinidhamu…. sasa hapa demokrasia iko wapi", alisema kijana huyo kwa masikitiko.
Akizungumzia malalamiko hayo, Katibu wa UV-CCM wilaya ya Arumeru, Yasin Said Yasin alieleza kuwa wanaolalamika hawana hoja za msingi kwa kuwa wao walifuata taratibu zote katika kufanya uteuzi wa Medeye.
Akifafanua taratibu hizo, Yasin alieleza kuwa viongozi walipendekeza majina matatu ambayo ni ya Medeye, Mollel na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Jeremiah Sumari ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi.
"Majina hayo matatu ndiyo yaliyojadiliwa na Kamati ya Utekelezaji na kupelekwa mkoani ambao nao waliyapeleka Umoja wa Vijana Taifa na baada ya kuchujwa jina la Medeye ndilo lililorudishwa na kwa sasa tunasubiri Baraza Kuu likae ili limpitishe rasmi kuwa Kamanda wa Wilaya", alisema Katibu huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UV-CCM Mkoa wa Arusha, James Ole Millya alieleza kuwa mgogoro huo unakuzwa na baadhi ya wanachama wakorofi, na kwamba uteuzi wote ulipita kwenye vikao halali vya jumuiya hiyo.
"Kama viongozi wanaolalamika wana hoja za msingi, basi wawe jasiri na wajitokeze hadharani na sisi tutawajibu kwa hoja; kwani tunaamini kuwa tulizingatia vigezo vyote muhimu katika uteuzi", alisema Millya.
Millya, ambaye ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Simanjiro linaloshikiliwa na Mbunge machachari, Christopher Ole Sendeka alisema kwamba Kamanda aliyeteuliwa kushika nafasi ya mkoa pia ana uwezo mkubwa.
"Tumemwondoa Kinana kwa kuzingatia majukumu mengine mazito aliyonayo katika chama na anaweza kukosa muda wa kuhudumia vijana kutokana na majukumu hayo, na huyu tuliyemteua tunaamini ana uwezo mkubwa", alisema.
Hata hivyo, wakati Millya akisema kuwa Kinana ana majukumu mengine na anaweza kukosa muda wa kuwahudumia vijana wa mkoa wa Arusha, Shah ambaye ni mfanyabiashara maarufu mjini Arusha, mara nyingi huishi nje ya nchi na amekuwa akitumia muda mwingi katika shughuli zake za kibiashara.
Wanaoteuliwa kuwa makanda wa jumuiya za vijana mara nyingi huwa na majukumu ya kusadia kifedha shughuli mbalimbali za vijana na pia kusuluhisha migogoro inayotokea ndani ya jumuiya na kuimarisha CCM katika ngazi zote.
Nafasi hizo pia zina ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana; hasa nyakati za kampeni za uchaguzi wa nafasi mbalimbali za ndani ya chama na ile ya ubunge, na ndiyo maana uteuzi unaofanywa huleta malalamiko na hata vurugu katika maeneo mengine.