Joseph Butiku: Taifa hili lina Watu wengi waoga, na wasomi walio wengi waoga zaidi

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, amesema kuwa Taifa limekuwa na watu wengi waoga katika kulinda haki zao kutokana na kuepuka madhara binafsi.

Akizungumza leo Novemba 23, 2023 kwenye mdahalo wa kitaifa wa kumbukizi ya miaka 75 ya Tamko la Haki za Binadamu Duniani, ambao umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania, amesema kuwa uoga huo unakumba makundi mbalimbali kwenye jamii ikiwemo wasomi hata Wazee.

“Kuna adui wa haki uoga, nani si muoga huku anyooshe mikono juu? . Muoga asiyependa kuona nafsi yake isipate madhara, kila mtu anataka nafsi yake isipate madhara binafsi, lakini haki za umma na haki zako huwezi kuzilinda kama ni muoga. Taifa hili lina watu wengi waoga na wasomi walio wengi waoga zaidi na wazee wengine ni waoga kabisa,” amesema Mzee Butiku.

Butiku ambaye ni mwanasiasa wa muda mrefu amewataka wananchi kuunganisha nguvu katika kuhakikisha kuwa haki zao zinalindwa.

“Msipojenga nguvu za umoja watawanyonga hata nyie, jengeni nguvu za umoja ili kuweza kujitetea katika haki zenu. Umoja ni sharti la kimsingi kabisa katika kutetea haki,”amesema Butiku.

Amewakumbusha wadau kuwa "Haki za binadamu sio kitu cha hewani ni utu wako na utu wa mtu mwingine na heshima yako na heshima ya watu wengine"

Pia meeleza kuwa zipo changamoto za rushwa ambazo wadau katika mdahalo huo ametaka wazijadili ambazo ni kikwazo cha haki akitolea mfano mchakato wa kuomba mikopo pamoja na haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

“Kusoma lazima ukope, unakopa kwa kufuata taratibu au uhonge ndiyo upate mkopo. Mwaka kesho tunachagua, haki ya kuchagua na kuchaguliwa sasa wakati inafika nakuja kwako kuomba kura unasema usipo nipa hela sikupi kura hiyo ni haki sio haki? Katika nchi tuna shida ya haki katika uchaguzi,” amesema Mzee Butiku.

Aidha Mwanaharakati wa haki za binadamu kwa zaidi ya miaka 20 nchini Tanzania,Dkt. Helen Kijo-Bisimba ambaye amewai kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu akizunguza katika mdahalo huo amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambazo zimekuwa zikiingia mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa lakini kumekuwepo na changamoto ya utekelezwaji wa makubaliano hayo.

Mwanaharakati huyo ametolea mfano kesi mbalimbali ambazo wadau wameshinda kwenye vyombo vya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia kutekeleza makubaliano, miongoni mwa mambo aliyotaja na Haki ya mgombea binafsi suala ambalo Tanzania inatakiwa kuwajibika kulitekeleza kulingana na uamuzi ambao ulitolewa, suala lingine ni mabadiliko ya sheria ya ndoa.

Lakini kwa upande wa Serikali kupitia Mkurugezi wa Kitengo cha Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Nkasori Sarakikya amesema kuwa Tanzania imekuwa ikijumuika na wadau wa haki za binadamu katika masuala mbalimbali ikiwemo kuandaa shughuli za wadau wa haki za binadamu.

Amewapongeza wadau wa haki za binadamu kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kwenye baadhi ya mambo akidai kuwa kutokana na mazingira rafiki Tanzania imeweza kuwa Kituo cha Ofisi za taasisi mbalimbali za haki za binadamu za kimataifa, ikiwemo Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu pamoja na Mahakama ya Afrika Mashariki ambapo ofisi zao zipo Arusha.

Kwa niaba ya waandaaji wa mdahalo huo wa siku mbili ambao umeanza leo Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema hali ya utetezi wa haki za binadamu nchini katika kipindi cha miaka ya karibuni unaonekana kushuka kutokana na vijana kutoandaliwa mapema kutimiza jukumu hilo.

“Tunaendelea kusisitiza pamoja na kwamba tunafanya kazi nzuri lakini ni jukumu la THRDC kuona watu wengi wanatetea haki za binadamu. Tunasikitika kuona hali ya utetezi na ulinzi wa haki za binadamu inazidi kushuka chini katika makundi yote sababu tumeshindwa kuwaandaa vijana vizuri,” amesema Olengurumwa.

Amesema kuwa miaka kadhaa ya iliyopita, vyuo vikuu vilikuwa mstari wa mbele katika kuwafundisha vijana misingi ya haki za binadamu, ikiwemo kwa kuandaa makongamano na midahalo, lakini hivi sasa utamaduni huo umepungua.

“Nadhani ni muda wetu kutafakari zaidi kuona tunatokaje hapa kama nchi, tunaamini taifa litasonga mbele kama taasisi kama hizi za elimu zitatoka kushauri nchi sio katika haki za binadamu peke yake lakini kwenye maeneo mengine kuona namna gani tunasonga mbele,” amesema Olengurumwa.

Ameshauri kuwa "Inabidi kurudisha hali ya zamani ambayo vyuo vimezalisha watetezi wengi sana, THRDC imetokana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo wahadhiri waliona umuhimu wa kuwa na taasisi ya haki za binadamu. Chuo hiki kimekuwa msaada mkubwa katika kukuza haki za binadamu.”

Akizungumza kuhusu hoja hiyo, Mkuu wa Kitivo Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Boniventure Rutinwa, alikiri uwepo wa changamato za taasisi za elimu ya juu kupunguza midahalo ya kujadili haki za binadamu.

Prof. Rutinwa alisema katika uongozi wake atahakikisha midahalo na makongamano hayo yanarejea ili kuandaa wanafunzi watakaojua misingi ya haki za binadamu pamoja na kuzilinda.

"Wakati nasoma Kila Jumatano asubuhi ilikuwa ni off Kwa ajili ya kuwaona wanafunzi nafasi ya kushiriki lakini Kwa sasa tumerudi nyuma lakini hivi karibuni tutarejesha huo utaratibu," amesema Prof. Rutinwa

Prof. Rutinywa amesema kuwa ni fursa kwa washiriki kuchambua na madhumuni ya azimio hilo ili kuangalia namna ya kuboresha haki za binadamu nchini.

Ambapo maadhimisho hayo yamekwenda kwa kauli mbiu ya kutafakari wakati uliopita, uliopo na ujao katika kuimarisha haki za binadamu Tanzania.

images%20(71)_1.jpg
 
Usiombe ukutane na mkono wa chuma. Wazee wa task force na TISS au wazee wa maelekezo kutoka juu.

Ishi low key life.
 
Back
Top Bottom