Wakati akiongea na wazee wa Mji wa Maswa na Malampaka, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amenukuliwa akisema "Uongozi ni kutanguliza hekima na busara katika kufikia uamuzi, uongozi si Magereza na hata Magereza wafungwa wana haki zao, Tundu Lissu amekuwa nani katika nchi hii
anaongea kama kasuku hafanyi utafiti anakurupuka na kuongea na kutoa matamko? Mie nitamtaka athibitishe tuhuma anazozitoa dhidi yangu. Nasema Chadema si baba wala mama yangu," alisema.
Alisisitiza kuwa amechoka kusikia hukumu dhidi yake kila siku kupitia vyombo vya habari kutoka kwa viongozi wake wa Chadema, huku akitoa mfano kuwa alipounga mkono nyongeza ya posho ya Bunge, aliitwa Msaliti, lakini leo wabunge wote wakiwemo wa Chadema waliogomea wanachukua posho hiyo.
"Wazee wangu niliposema bungeni posho iongezwe, niliitwa mie Msaliti na wabunge wa Chadema lakini leo kila mmoja muulizeni hata huyu Kasulumbayi (Sylvester, Mbunge wa Maswa Mashariki, Chadema), ambaye tunaye hapa kwenye kikao kama hachukui posho hizo.
Hata huyo Tundu Lissu anayeongea sana anachukua, hata Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa Chadema) alikataa gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lile la Serikali lakini hadi leo analitumia
mbona yeye haitwi Msaliti? Alihoji Shibuda.
Akizungumzia uhusika wake katika kundi la Ukawa, Shibuda alisema kuwa yeye si sehemu ya kundi hilo na wala hajawahi kuelimishwa kuhusu kundi hilo, bali anakumbuka kuwa kupitia viongozi wa juu wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wa vyama hivyo watoke bungeni na wasishiriki vikao hivyo.
"Muislamu hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo saba za Uislamu na pia huwezi kuwa Shekhe bila kupitia Madrasa na hata katika Ukristo, huwezi kuutetea Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho
na mie siwezi kuwa Ukawa wakati sijaelimishwa kuhusu kundi hilo, alisema.
Alisema kuwa aliingia katika chama hicho kwa hiari yake baada ya kukataa dhuluma alizodai kufanyiwa na CCM na kudhani ndani ya Chadema kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini alichokikuta ni tofauti kwani kila siku amekuwa akipata misukosuko kutoka ndani ya chama hicho.
"Mie niliingia Chadema kwa hiari yangu baada ya kuona dhuluma zilizokuwa ndani ya CCM, chama kilichonilea kisiasa, nikaona heri niende Chadema ambako nilidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini nilichokikuta humo ni tofauti'' alisema.
Kwa hisani ya Hbarileo.