Naomba kuwasilisha mawazo yangu, kwa heshima na taadhima. Hili swala limenigusa sana. Nampongeza sana Mwl. Paul Mhozya kwa hatua aliyochukua. Nadhani ni wengi tunaonung'unika chini chini tu. Tanzania, nchi ambayo raia tumezingirwa na upepo wa ahadi hewa na maneno ya asali kutoka kwenye vinywa vya miungu watu, eti nchi yetu ina amani na utulivu wakati haki zetu za msingi za kiraia zinaendelea kupuuzwa kila kukicha. Vilio vyetu vinapuuzwa, mbaya zaidi wanatukejeli raia na kutukana bila woga. Sisi sio muhimu, na kura zetu hazina maana? Sio walimu tu, au polisi na wafanyakazi wengine. Ki-mantiki, mlipa kodi yeyote ni mfanyakazi wa serikali. Serikali sio tu Rais, Mawaziri, Wabunge au vyombo vyake vya kutunga sheria na kuzisimamia. Serikali sahihi ni watu. Viongozi wanasimamia tu kwa mamlaka tuliyowapa sisi, au waliyopewa kwa niaba yetu na watu tuliowachagua. Ni waajiriwa wetu. Wanajibu kwetu. Wakiharibu tunawatoa au sio? Hiyo ndio maana halisi ya serikali ya demokrasia! Tatizo ni nini sasa? Mimi nadhani maana ya neno "Serikali" tafsiri yake imehujumiwa na watu wachache. Ni dhahiri kwamba Taifa letu la Tanzania linahitaji mapinduzi ya kweli, hasa ya kifikra. Amani? Utulivu? Mshikamano? Hivi ni vitu muhimu katika kuendeleza Taifa. Lakini hauwezi ukasema nchi ina amani wakati watu wengi tu wanalala na njaa. Sio tu kuwa ni njaa ya chakula, bali njaa ya maendeleo. Njaa ya haki. Hauwezi ukawa na mikakati ya kujenga taifa wakati wasimamizi wa ujenzi huo wanawaza tu kubomoa na kujijenga wao na familia zao. Biashara ndogondogo na ajira zetu zinahujumiwa. Rasilimali zetu muhimu hazitujengei maisha bora. Nenda leo sokoni ongea na muuza nyanya, halafu safiri kamsikilize na mkulima wa hizo nyanya. Nenda kamsikilize mwanafunzi wa shule ya kata, kamsikilize na mwalimu wake. Kamuulize na mfanyakazi yeyote wa umma, au kwa ufupi, mtanzania yeyote wa kawaida aliye karibu nawe. Muulize kama ana furaha. Ukishayatafakari majibu yote utakayoyapata, au ambayo unayo tayari sasa hivi, rejea tena kwenye barua ya Bw. Paul Mhozya hapo juu. Weka kando ushabiki wa kisiasa, urafiki au ubishi tu usio na maana. Jiulize tumetoka wapi na tunakwenda wapi? Nilimsikia Dr. Mohammed Ghalib Bilali juzi kwenye Hamza Kassongo hour, kipindi cha Channel Ten. Alijitahidi sana kujibu maswali tena kwa upeo mkubwa tu, akanivutia nimsikilize. Kuna jambo moja alihoji ambalo nadhani ni la msingi. Kwamba, Tanzania ipo moja tu na ndiyo nchi yetu pekee na wala hatuna pengine pa kwenda. Hivyo basi, na mimi nahoji, kama kweli serikali inaundwa na sisi wananchi, watanzania tunaoongozwa na katiba, sheria na taratibu tulizojiwekea, hatutaweza kuendelea kamwe katika Taifa hili endapo tutaendelea kubweteka tu na kunung'unika chini chini tukamwachia kazi Bw Paul Mhozya na wengine wachache wajaribu peke yao kutetea haki zetu. Tuwaunge mkono sio tu wanaotufaa, bali wanaofaa kwa maendeleo ya kweli ya Taifa hili. Hizi sio nyakati tulizozizoea, Dunia ya leo siyo ya jana. Inabidi tubadilishe mtazamo wetu wa kifikra. Kesi hii nadhani iwe chanzo tu cha mabadiliko hayo. Ahsanteni.