Jitahidi uwe na kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura na cheti za kuzaliwa. Hivi vitu ni muhimu kuliko unavyofikiria

Sep 6, 2021
24
111
Na Elivius Athanas.
0745937016.

Salamu kwenu Watanzania.
Leo nimeamua kuandika makala yenye lengo la kuhamasisha Watanzania, kufuatilia na kupata Kitambulisho cha Taifa, Kitambulisho cha mpiga kura na Cheti cha kuzaliwa.
Msukumo wa kutumia mda na kuandika makala haya, unachagizwa na ukweli ulio "uchi" kuwa, vitambulisho hivi ni vitu vya muhimu sana licha ya baadhi ya Watanzania kutokuwa na vitambulisho hivi.
Hivyo, kupitia jukwaa hili la uandishi wa mtandaoni wenye kuleta mabadikiko yaani "Stories of Change", ninazo sababu bilioni za kuwaeleza na kuwahamasisha Watanzania kuhusu namna ya kupata vitambulisho hivi na umuhimu wake.

UTAPATAJE KITAMBULISHO CHA TAIFA?

Kitambulisho cha Taifa kinatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kupitia zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa, lililofanyika Nchi nzima.
Kama Mtanzania hukupata nafasi ya kupata kitambulisho cha Taifa katika zoezi hilo, bado una nafasi ya kupata kitambulisho cha Taifa.
Nenda kwenye Ofisi za Serikali ya Mtaa au Kijiji chako, utapewa fomu ambayo utatakiwa kujaza taarifa zako muhimu kisha peleka hiyo fomu kwenye Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) iliyo karibu na wewe (Wilaya).
Huko utapokewa fomu yako na utaandikishwa. Baadae utapata namba ya kitambulisho itakayofuatiwa na kitambulisho halisi.

UTAPATAJE KITAMBULISHO CHA MPIGA KURA?

Kitambulisho cha mpiga kura kinatolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupitia zoezi la uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura na zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura, mazoezi haya yalifanyika Nchi nzima.
Kama Mtanzania hukupata nafasi ya kupata kitambulisho cha mpiga kura katika mazoezi hayo, bado una nafasi ya kupata kitambulisho hicho kwa kusubiri mazoezi yajayo.

UTAPATAJE CHETI CHA KUZALIWA?

Unaweza kupata cheti cha kuzaliwa katika Wilaya uliyozaliwa au katika Ofisi za Msajili Mkuu, Makao makuu ya RITA.
Utatakiwa kujaza fomu BD 15 halafu utaambatanisha kiambatanishi kimoja kati ya hivi:
Kadi ya kliniki, kitambulisho cha kupiga kura, pasi ya kusafiria, cheti cha kuhitimu elimu ya msingi au Sekondari (Leaving Certificates) au cheti za ubatizo ~ Afisa wa RITA.

JE, UMUHIMU WA KUWA NA VITAMBULISHO HIVI NI UPI?

Zipo faida milioni ambazo Mtanzania atazipata akiwa na kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura na cheti cha kuzaliwa.

1. Kitambulisho cha mpiga kura, kitakupa tiketi ya kutimiza haki yako ya msingi ya kupiga kura na kuchagua viongozi unaowataka.
Kama huna kitambulisho cha mpiga kura, utapoteza haki yako ya msingi na Kikatiba ambayo hutokea mara moja baada ya miaka mitano (5).
Huoni kuwa ni hasara!
Hivyo, utaendelea kuongozwa na viongozi ambao hujawachagua mpaka pale utakapopata kitambulisho cha mpiga kura.
Hasara ilioje!

2. Kitambulisho cha Taifa, kitakusaidia kusajili namba ya simu kwa ajili ya mawasiliano ya simu na kadhalika.
Namba zote za simu kwa sasa, zinasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole ambapo unatakiwa uwe na namba ya "NIDA" ili uweze kusajili namba yako ya simu.
Hivyo, kukosa kitambulisho cha Taifa, kutakusababishia wewe kufungiwa namba zako za simu na kukosa umiliki wa namba ya simu.

3. Vitambulisho hivi vitakutambulisha kuwa, wewe ni raia wa Tanzania hivyo kukusaidia kupata huduma sehemu tofauti tofauti.
Sehemu nyingi za ofisi za Serikali na ofisi za Mashirika binafsi, zinahitaji vitambulisho hivi kama kigezo cha mtu kupata huduma.
Taasisi nyingi za kifedha (Benki), zinahitaji vitambulisho hivi ili mtu aweze kufungua akaunti ya benki.
Taasisi nyingi za kifedha (Benki) na Taasisi nyingi za mikopo, zinaviorodhesha vitambulisho hivi kama moja ya nyaraka za kuambatanisha ili mtu aweze kupewa mkopo.
Bado huoni umuhimu wake?
Kuna baadhi ya ofisi nimewahi kwenda hapa Jijini Dar es Salaam, nilipofika getini, nikaambiwa nionyeshe kitambulisho kimoja kati ya hivi ili niweze kupita getini na kuingia kuhudumiwa. (Nisije nikawa mkimbizi nikafanya ujinga kama Hamza).

Siyo maeneo hayo tu, vitambulisho hivi vinaweza kumtambulisha mtu pindi anapopata ajali ya kujeruhiwa au umauti.
Ukigongwa na gari ukafariki, ukiwa na vitambulisho hivi mfukoni, itasaidia sana wewe kutambulika.
Hivyo kupitia jukwaa hili, nawakumbusha Watanzania kutembea na moja ya vitambulisho hivi ili kusaidia itakapotokea dharura. Dharura ni kama kikohozi, ikija haipigi hodi!
Faida ziko nyingi mno, nikiamua niendelee kuziorodhesha na kuzifafanua zote, tutakesha kama popo.

MWISHO. Ni wajibu wa Serikali na vitengo vyote vinavyohusika na utoaji wa vitambulisho hivi, kutoa elimu, utaratibu rafiki na matangazo mengi ili kuhakikisha, idadi kubwa ya Watanzania wenye sifa na vigezo vya kupata vitambulisho hivi, wanavipata bila usumbufu.
Utolewaji wa vitambulisho hivyo kwa Watanzania, utaisaidia sana Serikali kubaini na kutambua idadi ya Watanzania.

Nawatakia utekelezaji uliotukuka.
 
Dosari za uandishi (typing error).
Ni cheti cha kuzaliwa badala ya cheti za kuzaliwa.
Nawezaje kuhariri kichwa cha mnakasha (thread)? Nisaidieni.
 
Shida ni Mamlaka husika hasa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa ofisi za RITA huku wilayani.Kuna changamoto kubwa sana unaenda kuomba cheti cha kuzaliwa na ukiwa umeambatanisha na kila kitu wanachohitaji halafu unaambiwa usubiri mpaka mwezi mmoja. Kwa speed hii sidhani kama kweli kila mtanzania atapata cheti cha kuzaliwa labda Ofisi za RITA huku wilayani wabadilike.
 
Back
Top Bottom