Mnawezaje kupunguza mzozano katika mazungumzo yenu? Kumbuka kwamba lengo lako kuu, si kumwadhibu mwenzi wako, lakini ni kujifunza kutokana na tatizo lililowapata na kuimarisha ndoa yenu. Kwa mfano, Chul Soo na mke wake, Mi Young, walianza kuchunguza uhusiano wao wakifikiria kilichosababisha Chul Soo afanye uzinzi. "Niligundua kwamba nilikuwa ninajishughulisha sana na mambo yangu ya kibinafsi," anasema Chul Soo. "Pia, nilitaka kuwapendeza wengine na kufanya mambo waliyotaka nifanye. Nilikuwa nikitumia wakati wangu mwingi pamoja nao na kuwapa uangalifu. Jambo hilo lilifanya nisitumie wakati mwingi pamoja na mke wangu." Kufikiria mambo hayo kwa undani kuliwasaidia Chul Soo na Mi Young wafanye marekebisho ambayo, baada ya muda, yaliwasaidia kuimarisha ndoa yao.
JARIBU KUFANYA HIVI: Ikiwa wewe ndiye uliyefanya uzinzi, epuka kutoa udhuru au kumlaumu mwenzi wako. Kubali matokeo ya matendo yako na uchungu uliosababisha. Ikiwa wewe ndiye uliyekosewa, usimpigie kelele mwenzi wako wala kutumia matusi. Ukiepuka kuzungumza kwa njia hiyo, utamtia moyo mwenzi wako aendelee kuongea nawe waziwazi.-
Waefeso 4:32.
2 Shirikianeni. Biblia inasema: "Wawili ni afadhali kuliko mmoja." Kwa nini? "Kwa maana wana thawabu nzuri kwa ajili ya kazi yao ngumu. Kwa maana mmoja wao akianguka, yule mwingine anaweza kumwinua mwenzake." (
Mhubiri 4:9, 10) Kanuni hiyo inafaa hasa mnapojitahidi kuanza kuaminiana tena.
Mkishirikiana, wewe na mwenzi wako, mnaweza kufanikiwa kuaminiana tena. Hata hivyo, nyote
wawili mnahitaji kujitolea kabisa kuokoa ndoa yenu. Ikiwa utajaribu kurekebisha jambo hilo ukiwa peke yako, utakuwa unajiletea matatizo mengi hata zaidi. Unahitaji kumwona mwenzi wako kuwa mshirika wako.
Steve na Jodi waligundua jambo hilo. Jodi anasema "Ilituchukua muda fulani, lakini mimi na Steve tulishirikiana na kuimarisha ndoa yetu. Niliazimia kwamba sitawahi kumuumiza hivyo tena. Ingawa Steve aliumia sana kihisia, aliazimia kutoruhusu ndoa yetu ivunjike. Kila siku, nilijaribu kumhakikishia kwamba mimi ni mwaminifu, naye aliendelea kunionyesha upendo. Kwa sababu hiyo, nitaendelea kumshukuru kila wakati."
JARIBUNI KUFANYA HIVI: Pamoja, azimieni kushirikiana katika kufanya mwaminiane tena.
3 Acha Tabia za Zamani. Baada ya kuwaonya wasikilizaji wake kuhusu uzinzi, Yesu aliwashauri hivi: "Ikiwa, sasa, hilo jicho lako la kuume linakufanya ukwazike, ling'oe ulitupilie mbali nawe." (
Mathayo 5:27-29) Ikiwa wewe ndiye uliyemkosea mwenzi wako, je, unaweza kufikiri kuhusu matendo au mitazamo unayoweza kung'oa na kutupilia mbali ili kuokoa ndoa yako?
Ni wazi kwamba unahitaji kukata uhusiano na yule mtu uliyefanya naye uzinzi.
* (
Methali 6:32; 1 Wakorintho 15:33) Paul, aliyetajwa hapo mwanzoni, alibadili ratiba yake ya kazi na nambari yake ya simu ili asiweze kuwasiliana na yule mwanamke aliyefanya naye uzinzi. Hata hivyo, juhudi hizo zote hazikumwezesha kuacha kuwasiliana naye kabisa. Paul alikuwa ameazimia kumfanya mke wake aanze kumwamini tena hivi kwamba aliamua kuacha kazi yake. Na akaacha kutumia simu yake akawa akitumia ya mke wake. Je, mambo hayo yote yalikuwa na faida yoyote? Debbie, mke wake, anasema: "Miaka sita imepita sasa, lakini mara kwa mara huwa nina wasiwasi kwamba huenda huyo mwanamke akajaribu kuwasiliana naye tena. Lakini sasa nina uhakika kwamba Paul hawezi kuanguka katika mtego huo."
Ikiwa wewe ndiye uliyefanya makosa, unapaswa pia kubadili utu wako. Kwa mfano, huenda unapenda kuwachezea wengine kimapenzi, au huenda unafurahia kuwazia ukiwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengine. Ikiwa ni hivyo, ‘vua utu wa zamani pamoja na mazoea yake.' Badili tabia za zamani na uwe na mazoea ambayo yatafanya mwezi wako akuamini kabisa. (
Wakolosai 3:9, 10) Je, malezi yako yanafanya iwe vigumu kwako kuonyesha upendo? Ingawa huenda ikawa vigumu mwanzoni, usisite kumwonyesha upendo na kumfanya akuamini. Steve anasema: "Mara kwa mara Jodi alinionyesha upendo kwa kunigusa kwa mkono wake, na mara nyingi alisema ‘nakupenda.'"
Kwa muda fulani, huenda itakuwa jambo lenye busara kumwambia mwenzi wako kila kitu unachofanya kila siku. Mi Young, aliyetajwa mwanzoni anasema: "Chul Soo alihakikisha kwamba aliniambia kila kitu kilichotokea kila siku, hata mambo ambayo hayakuwa muhimu kabisa, ili kuthibitisha kwamba hafichi jambo lolote."
JARIBU KUFANYA HIVI: Zungumzieni mambo ambayo yanaweza kuwasaidia muanze kuaminiana tena. Andikeni mambo hayo na mjitahidi kuyatimiza. Pia, katika ratiba yenu ongezeni mambo ambayo mnaweza kufurahia kufanya pamoja.
4 Tambueni Wakati wa Kusonga Mbele. Msiamue haraka kwamba wakati umefika wa kuanza kuishi kana kwamba mmerudia hali ya kawaida. Andiko la
Methali 21:5 linaonya hivi: "Kila mtu anayetenda haraka-haraka bila shaka huuelekea uhitaji." Itawachukua muda mrefu-labda miaka kadhaa-ili muweze kuaminiana kabisa.
Ikiwa wewe ndiye mwenzi uliyekosewa, jipe muda wa kusamehe kabisa. Mi Young anasema: "Nilifikiri kwamba mke alipaswa kumsamehe mume wake aliyefanya uzinzi. Sikuelewa kwa nini mke angeendelea kumkasirikia mume wake kwa muda mrefu. Hata hivyo, mume wangu alipofanya uzinzi, nilielewa kwa nini ni vigumu kusamehe." Kuaminiana na kusamehe ni mambo yatakayokuja polepole.
Andiko la
Mhubiri 3:1-3 linasema kwamba kuna "wakati wa kuponya." Huenda mwanzoni ukahisi kwamba njia nzuri ni kutomweleza mwenzi wako kuhusu hisia zako. Hata hivyo, kunyamaza kabisa hakutasaidia uanze kumwamini mwenzi wako tena. Ili kurekebisha uhusiano wenu, msamehe mwenzi wako na uonyeshe kwamba umemsamehe kwa kumweleza maoni na hisia zako za ndani. Pia, mtie moyo akueleze mambo anayofurahia na wasiwasi wake.
Usiwe na kinyongo. Jitahidi sana kushinda hisia hizo. (
Waefeso 4:32) Huenda ukafaidika ukitafakari mfano wa Mungu mwenyewe. Waisraeli wa kale walipogeuka na kuacha kumwabudu, Mungu aliumia sana. Yehova alijifananisha na mwenzi wa ndoa ambaye mwenzi wake alikuwa amefanya uzinzi. (
Yeremia 3:8, 9; 9:2) Lakini hakuendelea "kufungia kinyongo mpaka wakati usio na kipimo." (
Yeremia 3:12) Watu wake walipomrudia wakiwa wametubu kikweli, aliwasamehe.
Mwishowe, nyote wawili mkiridhika kwamba mmefanya marekebisho yanayohitajika katika uhusiano wenu, mtaanza kuhisi mkiwa salama. Kisha, badala ya kuanza kufikiri wakati wote kuhusu kuokoa ndoa yenu tu, mnaweza kukazia fikira miradi mingine. Hata hivyo, tengeni wakati wa kuchanganua maendeleo ambayo mmefanya. Msiridhike tu na mambo ambayo mmetimiza. Shughulikieni mambo madogo-madogo ambayo huenda yakawazuia msifanye maendeleo, na mwendelee kuhakikishiana uwajibikaji wenu.-
Wagalatia 6:9.
JARIBU KUFANYA HIVI: Badala ya kujaribu kurudisha ndoa yenu vile ilivyokuwa mwanzoni, jiwazieni ni kana kwamba mnajenga uhusiano mpya na ulio imara zaidi.
Mnaweza Kufaulu
Mnapohisi kwamba hamtafaulu kumbukeni: Mungu ndiye mwanzilishi wa mpango wa ndoa. (
Mathayo 19:4-6) Hivyo, kupitia msaada wake mnaweza kufanya ndoa yenu ifaulu. Wenzi wote waliotajwa hapo juu walifuata mashauri ya Biblia yenye hekima na wakafaulu kuokoa ndoa zao.
Miaka 20 imepita tangu Steve na Jodi walipopatwa na tatizo katika uhusiano wao. Steve anaeleza hivi kuhusu juhudi za kuokoa ndoa yao: "Tulifanya mabadiliko muhimu tulipoanza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. Msaada tuliopata ulikuwa wenye thamani sana na ulitusaidia kukabiliana vyema na wakati huo mgumu." Jodi anasema: "Nahisi kwamba tumebarikiwa sana kwa kuweza kuvumilia wakati huo mgumu. Kwa kujifunza Biblia pamoja na mume wangu, na kujitahidi sana, sasa tuna ndoa nzuri."