Jinsi Waumini wa Parokia ya Mt. Mikaeli Kawe Walivyomzuia Paroko Kusoma Misa

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478
Paroko azuiwa kusoma misa

(Chanzo: Tanzania Daima, Toleo la 07 Oktoba 2019, uk. 5)

Na Janeth Jovin


Ruaichi, Nzigilwa na Kundy.png

Kawe--Jiwe la Msingi-2.png

Sehemu ya sanamu ya Mt. Mikaeli ambaye ndiye msimamizi wa Parokia ya Kawe

Paroko wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mtakatifu Mikaeli, iliyoko eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam, Padre Nicholas Bahati Kundy, amefungiwa nje ya Kanisa na Waumini wake, na hivyo kushindwa kusoma misa ya Jumapili ya tarehe 06 Oktoba 2019, inayoanza saa 12.30 asubuhi.

Waumini hao wanamtuhumu Padre Kundy kwa matumizi mabaya ya fedha za sadaka ya Parokia yake; kushindwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa ujenzi wa Ukumbi wa Kardinali Pengo; kuchakachua chaguzi mbalimbali katika jumuiya kadhaa zilizomo katika Parokia yake; kutoa huduma za kiroho kwa ubaguzi unaotoa upendelea kwa watu wenye fedha nyingi na kuwatelekeza waumini maskini; na kuwanyanyasa mapadre wanaofanya kazi chini yake.

Waumini wanataka paroko aondolewe na Parokia kukabidhiwa kwenye uongozi wa Jimbo. Kwa sasa, Parokia ya Mtakatifu Mikaeli ya Kawe inaongozwa na Shirika la Moyo Mtakatifu wa Mitume wa Yesu kwa niaba ya Uongozi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mwandishi wetu aliwashuhudia waumini wa Parokia ya Kawe wakifurika Kanisani tangu saa 11.45 alfajiri kwa ajili ya kusali rozari takatifu kabla ya ibada kuanza. Rozari ilianza saa 11.55 na kukamilika ndani ya nusu saa, yaani, saa 12.25 alfajiri.


Kawe Malaika Sanamu.png

Sanamu kamili ya Mt. Mikaeli ambaye ndiye msimamizi wa Parokia ya Kawe

Kisha wakaingia wanakwaya kwa ajili ya kuanzisha ibada kwa njia ya nyimbo. Wimbo wa kuanza ibada ya misa ulianza kuimbwa saa 12.30 mpaka saa 12.35 alfajiri bila padre wa kuendesha ibada kujitokeza. Wanakwaya wakasitisha kuimba. Mara akajitokeza muumini mmoja akapanda altareni kwenye kinasasauti na kuwafahamisha waumini kuwepo kwa tatizo.

Samahani ndugu waumini, kuna changamoto ya kiutawala imejitokeza hapo nje. Tunawaomba kuvuta subira wakati tunatafuta msaada wa uongozi wa Jimbo kuishughulikia,” alisikika akisema muumini huyo wa kiume.

Taharuki miongoni mwa waumini ikafuata. Baadhi yao wakaanza kutoke nje ya Kanisa wakielekea kiliko chumba cha sakristia, yaani chumba cha maandalizi kinachotumiwa na mapadre na wasaidizi wao kabla ya kuja altareni kuendesha ibada ya misa.

Mwandishi wetu, aliyekuwa miongoni mwa waumini hao, alisogelea sakristia na kujionea kilichokuwa kinaendela. Waumini kadhaa vijana kwa wazee waliweka kizuizi katika mlango wa kuingia sakristia. Padre aliyejulikana kwa jina la Ntugi Boniventure Kisoka alikuwa ametangulia ili aingie sakristia. Padre Ntugi Boniventure Kisoka akazuiwa.

Katika kujitetea, Padre Ntugi Boniventure Kisoka alisikika akisema kuwa yeye ni mgeni hapo Parokiani na hakuwa na ugomvi na mtu. “Sisi tuna mgogoro na mwenyeji wako ambaye ni Paroko wetu Kundy, nenda umwambie aje,” walisikika waumini wenye hasira wakimwamuru Padre Ntugi. Padre Ntugi alirudi kwenye nyumba ya mapadre kumfuata Padre Kundy.

Kabla ya Padre Kundy kujitokeza kulizuka zogo kati ya waumini wanaotuhumu kwa makossa mbalimbali na waumini wanaomtetea. Majibizano na masutano yakaanza kati ya pande hizi mbili.

“Tunataka arudishe fedha za sadaka ya Parokia yetu milioni nne alizofuja pamoja na mpenzi wake,” sauti ilisikika akilalamika.

“Hapana kama ni madai hayo subiri baada ya misa, sisi tumekuja kusali,” sauti ya majibu ilitokeza upande wa kambi inayomuunga mkono Paroko Kundy.

“Hatukubaliano na hilo. Tunataka tupewe taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa ujenzi wa Ukumbi wa Kardinali Pengo, pamoja na fedha za vifaa vya ujenzi vilivyouzwa kinyemela na Paroko,” mmoja wa watu walio katika kambi ya kumkosoa Paroko Kundy alisikika akisema kwa ukali.

“Jamani, sisi wakatoliki hatujazoea utaratibu huo wa kutatua migogoro kwa mabavu,” sauti nyingine ya kike ilichomoza kutoka kwa kambi ya watu wanaomuunga mkono Paroko Kundy.

“Nawashangaa nyie mnaomtetea Paroko huyu. Tumechoshwa na tabia yake ya kuchakachua chaguzi mbalimbali katika Parokia yetu. Tena hana mamlaka ya kuteua Katibu wa Prokia lakini anafanya hivyo kwa kupora madaraka ya Kamati ya Utendaji,” mzee mmoja katika kambi ya kumkosoa Paroko Kundy alitamka kwa msisitizo.

Pia, kuna muumini mwingine aliyelalamikia huduma za kibaguzi. “Hatukubaliani na utaratibu wa kutoa huduma za kiroho kwa ubaguzi unaozalisha upendelea kwa watu wenye fedha nyingi na utelekezaji wa waumini maskini,” alisema muumini huyo.

“Kama ni hivyo, Parokia yetu irudishwe mikononi mwa Jimbo. Hawa Mapadre wa Shirika la Moyo Mtakatifu Mitume wa Yesu wanatuletea mgawanyiko kwa sababu ya kuwanyanyasana wao kwa wao,” alieleza muumini mwingine wa kiume.
Kadiri mzozo huu ulivyozidi kukolea waumini zaidi waliongezeka nje ya Kanisa.

Katika mazingira hayo, watetezi wa Paroko Kundy wakafanikiwa kumrudisha yule Padre mgeni, Padre Ntugi Boniventure Kisoka na kumwingiza katika chumba cha sakristia, lakini bila kuongozana na Paroko Kundy.

Kwa haraka, muumini mmoja wa kiume, alikimbilia altareni kwenye kinasasauti na kutoa tangazo la kuwaita waumini kurudi Kanisani.

“Tunaomba waumini wote kurudi ndani ya kanisa kusudi ibada iendelee, hali imetulia. Tusali kwanza, mengine baadaye. Tumedhibiti hali,” alisikika akiwapa matumaini waumini waliokuwa wametaharuki.

Baadaye, mwandishi wetu aliambiwa na muumini mmoja kwamba, yule mtangazaji mpya alikuwa ni Mwenyekiti wa Parokia ya Kawe, Charles Lupiya. Waumini waliitikia wito wake, wakarudi ndani, ibada ikaendelea, na wale waumini wenye hasira wakatoka nje ya boma la parokia.

Baada ya matangazo na kabla ya kutolewa kwa baraka ya kufunga ibada ya misa, Paroko Kundy alijitokeza mbele ya waumini akitokea chumba cha sakristia.

“Nawapa pole sana waumini wote kwa yaliyotokea. Ni changamoto za Imani. Mambo haya tulizoea kuyasikia kwa wenzetu lakini sio kwetu Wakatoliki. Nawaahidi kwamba jambo hili litashughulikiwa kupitia ngazi za utawala za Kanisa letu,” alimalizia Paroko Kundy bila kuingia kwa undani katika tuhuma zilizoelekezwa kwake na waumini.

Padre Kundy Kawe.jpg

Padre Nicholas Bahati Kundy

Baada ya kauli hii kutoka kwa Padre Kundy, Padre Ntugi Boniventure Kisoka alitoa Baraka ya kufunga ibada ya misa mnamo saa 2.50 asubuhi.

Inadaiwa kwamba, tarehe 23 Juni 2019, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Nzigirwa, alitembelea parokia ya Kawe na kuendesha ibada ya Misa. Alitumia mahubiri ya siku hiyo kutuliza hali ya hewa kwa kuzitaka pande zinazovutana kumaliza tofauti zao.

Aidha inadaiwa kwamba tarehe 22 Julai 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe walionana na Katibu wa Askofu, Padre Mtavango. Baada ya maongezi mafupi Padre Mtavango aliwambia kuwa suala lao litawasilishwa kwa Askofu Mkuu kwa hatua zaidi.

NYONGEZA


Siku nzima ya tukio, mwandishi alifanya jitihada za kuwasiliana kwa simu na mtuhumiwa pamoja na watawala wa kanisa wanaohusika na sakata zima lakini hawakuwa tayari kupokea simu ili kueleza mtazamo wao juu ya tuhuma zilizoibuliwa katika tukio lile.

Watu waliopigiwa simu na mwandishi, namba za simu zao zikiwa kwenye mabano, ni wafuatao:

Padre Kasembo, Mkurugenzi wa Walei Jimbo (0787188501); Padre Kundy, Paroko wa Kawe (0754372616), Charles Lupilya, Mwenyekiti wa Parokia ya Kawe (0713237963), Robert Sehewa, Katibu wa Parokia ya Kawe (0687166549 na 0713264458); na Padre Mtavango, Katibu wa Askofu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam (0765189300).

Simu hizi zote zilikuwa hewani lakini hazipokelewi. Simu pekee iliyokuwa haipo hewani siku hiyo ni simu ya Dekano wa Dekania ta Mt. Petro, Padre Benedict, ambaye ni Parokia wa Mwananyamala (0766274870).

Kwa sababu hii, wahusika katika upande wa mtuhumiwa walipoteza fursa muhimu kwa ajili ya kufafanua tuhuma zilizoelekezwa kwa Paroko kutoka kwa waumini wenye hasira. Jambo hili liliwanyima waumini taarifa zenye ulinganifu kuhusu tuhumza dhidi ya Paroko wao.

Katika hatua nyingine, utafiti umesaidia kupatikana kwa kumbukumbu za kimaandishi zenye kuthibitisha kwamba, mgogoro huu ni wa muda mrefu, na tayari umekwishafika katika uongozi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Kwa mfano, tarehe 7 Juni 2019 Kamati ya Waumini wanne kutoka Parokiani Kawe walipeleka barua rasmi ya malalamiko kwa Askofu Mkuu wa Dar es Salaam, kwa wakati huo akiwa Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo. Barua hiyo ilisainiwa na waumini 300 kutoka Kanda zote 17 za Parokia ya Kawe (Kiambatanisho A).

Na wajumbe walioiwasilisha kwa mkono barua hiyo Jimboni ni Francis Katambi, Samwel Mgila, Leonard Joseph na David Kulwa.

Katika barua hiyo, waumini hao walimtuhumu Padre Kundy kwa matumizi mabaya ya fedha za sadaka ya Parokia yake; kushindwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa ujenzi wa Ukumbi wa Kardinali Pengo; kuchakachua chaguzi mbalimbali katika jumuiya kadhaa zilizomo katika Parokia yake; kutoa huduma za kiroho kwa ubaguzi unaotoa upendelea kwa watu wenye fedha nyini na kuwatelekeza waumini maskini; na kuwanyanyasa mapadre wanaofanya kazi chini yake.

Tarehe 8 Juni 2019 na 11 Juni 2019, Kardinali Pengo alimtuma Paroko wa Mwananyamala, kuongea na waumini wenye manung’uniko, Kamati ya Utendaji ya Parokia pamoja na Paroko.

Tarehe 23 Juni 2019, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Nzigirwa, alitembelea parokia ya Kawe na kuendesha ibada ya Misa. Alitumia mahubiri ya siku hiyo kutuliza hali ya hewa kwa kuzitaka pande zinazovutana kumaliza tofauti zao.

Tarehe 11 Julai 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe walikwenda Makao Makuu ya Jimbo na kuomba miadi ya kuonana na Katibu wa Askofu, Padre Mtavango.

Tarehe 22 Julai 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe walionana na Katibu wa Askofu, Padre Mtavango. Baada ya maongezi mafupi Padre Mtavango aliwambia kuwa suala lao “litawasilishwa kwa Askofu Mkuu kwa hatua zaidi.”

Hata hivyo, kulingana na maongezi yaliyofanyika hawakuwa na imani na Padre Mtavango. Hivyo, siku hiyo ya tarehe 22 Julai 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe waliomba miadi ya kuonana na Askofu Mkuu kupitia wahudumu wa mapokezi. Walielekezwa kuonana na Askofu Mkuu tarehe 29 Julai 2019.

Tarehe 27 Juai 2019, Kamati Maalum iliyoundwa na Askofu Mkuu, Kardinali Pengo ilifika Parokiani kawe kuzihoji pand zinazosigana. Wajumbe wa Kamati hiyo ni Padre Vitalis Kasembo (Mkrugenzi wa Walei Jimboni), Mzee Sirro, na Balozi Nicolas Kuhanga.

Watu waliohojiwa ni Mzee Makwabe, Mzee Magila, David Joseph Kulwa na Uongozi wa Parokia ya Kawe. Mahojiano yalifanyika siku moja na kukamilika.

Baadaye, Mwenyekiti wa Kamati ya Askofu, Padre Vitalis Kasembo aliandika kimemo kilichotoa maelekezo ya maandishi kwa waumini wa Kawe akiwataka kuandaa ushahidi kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma zao mbele ya Kamati.

Kwa mujibu wa kimemo hicho, kilichoandikwa na Padre Vitalis Kasembo, waumini wa Kawe walitakiwa kuthibitisha tuhuma zifuatazo:


  • Kwamba, Parokiani Kawe kuna “wizi wa [sadaka ya] milioni nne” uliofanywa kwa Baraka za Paroko ambapo zilitolewa kwa “mhusika kwa ajili ya kuanzia maisha,” ambapo mhusika alikuwa Katibu muhtasi wa Paroko.
  • Kwamba, kuna watu “waliodaiwa pesa TZS 250,000/= na 370,000/= kwa ajili ya kufunga ndoa,” jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu wa Kanisa Katoliki.
  • Kwamba, kuna “wanandoa waliofunga jioni” kwa sababu ya kipato chao kuwa bora na wanandoa wengine “waliolazimishwa kufunga ndoa asubuhi kwa sababu ya kipato chao” kuwa duni.
  • Kwamba, Paroko wa Kawe anavuruga “uchaguzi” kwa kutoa maagizo ya kuzuia baadhi ya waumini asiowapenda kuchaguliwa na wakati mwingine kutumia “bastola” kuwatisha waumini.
  • Kwamba, Paroko Kundy anamiliki kwa siri “duka la vifaa vya ujenzi na pharmacy.” Kunahitajika “vibali vya maduka hayo.”
  • Kwamba, Paroko anayo tabia ya kupokea “rushwa” kutoka kwa waumini tofauti. Jambo hili linapaswa kuthibitishwa kwa kuonyesha “rushwa” hiyo “ilitolewa kwa nani,” lini na wapi?
  • Kwamba, Padre Kundy alikodisha “gari lililobeba nondo na cement” ya Parokia iliyokuwa imenunuliwa kwa ajili ya kujenga ukumbi wa parokia, ambapo vitu hivyo vinadaiwa kuchukuliwa kama mali ya “wizi” kwa Baraka za Paroko. Namba ya gari hilo inahitajika.
  • Kwamba, Padre Kundy anasoma misa akiwa amebeba "bastola" kiunoni na hivyo kuwatia hofu waumini.
  • Na kwamba, Paroko Kundy anazusha tuhuma za "ushoga" dhidi ya mapadre wenzake wa Shirika la Mitume wa Yesu ili waondoke na kutoa mwanya kwa ajili ya yeye kuendelea na ufujaji wa fedha za Parokia.
Kawe--Kimemo.png

Kimemo kilichoandikwa na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Kardinali Pengo kikiwa kinakwenda kwa Waumini Kawe kuwataka wathibitishe tuhuma dhidi ya Paroko Kundy.

Wajumbe wa Kamati ya kumwona Askofu wanasema kuwa, waliandaa ushahidi husika kipengele kwa kipengele (Kiambatanisho B).

Hata hivyo, waumini wa Kawe wanasema kuwa, mpaka leo Padre Vitalis Kasembo hajaja kuuchukua wala hajawaita waupeleke.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, tarehe 29 Julai 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe walikwenda kumwona Askofu Mkuu, Kardinali Pengo. Waliongea naye kwa dakika kumi. “Nimeteua Kamati kushughulikia tatizo lenu na sijapokea taarifa yao. Hivyo subirini,” aliwambia Kardinali Pengo.

Mwezi mmoja baadaye, hakukuwa na majibu yoyote kutoka kwa Kardinali Pengo. Hivyo, tarehe 29 Agosti 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe, walikwenda tena Jimboni kuomba miadi ya kuonana na Askofu Mwandamizi, Juda Thadeus Ruaichi.

Tarehe 30 Agosti 2019, Kamati ya wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe ilifanikiwa kuonana na Askofu Mwandamizi Ruaichi. Katika maongezi yake wajumbe wakagundua kuwa Askofu Ruachi alikuwa hajapelekewa barua ya malalamiko kutoka Parokiani Kawe, iliyoandkwa tarehe 7 Juni 2019. Hivyo, Askofu Ruachi akaomba wajumbe wampe nakala. Kikao kilichukua masaa mawili.

“Nimewaelewa na ninawaahidi kwamba nitalishughulikia suala lenu kwa ukamilifu,” Askofu Ruachi aliwaahidi wajumbe wanne kutoka Parokia ya Kawe.

Kabla Askofu Ruaichi hajapata fursa ya kutekeleza ahadi yake, Parokia ya Kawe iliingia katika chaguzi za Jumuiya Ndogo Ndogo.

Chaguzi hizi zinasimamiwa na wajumbe kutoka Parokiani wakiwa na ujumbe maalum "kutoka ngazi za juu" kwenye ofisi ya Paroko.

Ujumbe unasema kwamba fulani na fulani wasichaguliwe. Walengwa ni wale waumini waliosaini barua iliyokwenda kwa Askofu Ruaichi.

Tabia hii ya kuingilia uchaguzi wa Jumuiya ndogo ndogo ndiyo ilitonesha kidonda na kuamsha hasira za waumini mpaka wakafikia hatua ya kumfungia nje ya Kanisa Paroko wao.

Kwa ujumla, waumini wa Kawe waliotoa maoni yao wanaona kuwa, Paroko Kundi anafanya matendo yanayochafua wasifu wake wa kikazi kama padre na kwamba, kwa njia ya mzunguko, matendo hayo yanachafua wasifu wa kitume wa Kanisa Katoliki, linalopaswa kutimiza mapenzi ya Mungu kwa mujibu wa kanuni za kikanisa zinazowaongoza mahalifa wa Kristo.

Parokia ya Mtakatifu Mikaeli ya Kawe inaongozwa na mapdre wa shirika la Mitume wa Yesu ambao wanahudumia parokia sehemu mbalimbali duniani, mojawapo ikiwa ni Parokia ya Kawe. Ni wamisionari wenye makao makuu Nairobi Kenya. Viongozi wa shirika hili huingia mkataba na majimbo ili kuendesha Parokia kwa mujibu wa miongozi ya shirika.

Parokia ya Mt. Mikaeli Kawe inayo miradi mingi ya kibishara ikiwemo Ukumbi wa Mikutano wa Kardinali Pengo, Mafunzo ya ushonaji, mafunzo ya kompyuta, na kozi ya wanafunzi wanaojiandaa kwenda kidato cha kwanza (pre-form one).


Kawe--Ukumbi-1.png

Kawe--Jiwe la Msingi.png

Mradi wa ukumbi wa Parokia ya Kawe

Kawe-Training Program.png

Tangazo la mafunzo, ambao ni mradi mmojawapo Parokiani Kawe

VIAMBATANISHO


Kiambatanisho A: Barua ya waumini wa Kawe Kwenda Jimboni, nakala ilipelekwa kwa Paroko Kawe, Kardinali Pengo, na Mkuu wa Dekano. Imebeba tuhuma nzito dhidi ya Paroko.

Barua--Pg1.png

Barua--Pg2.png

Barua--Pg3.png

Barua--Pg4.png
 

Attachments

  • 1570463267567.png
    1570463267567.png
    36.7 KB · Views: 20
  • 1570463327186.png
    1570463327186.png
    33.9 KB · Views: 19
  • Kawe--Paroko.png
    Kawe--Paroko.png
    64.5 KB · Views: 17
  • Padre Kundy Kawe2.jpg
    Padre Kundy Kawe2.jpg
    24.5 KB · Views: 20
Milioni nne ndio wanasema ufujaji?
Mahesabu ya RC hayakaguliwi na hatuna utaratibu wa kuhoji mapato na matumizi
Huwa yanasomwa tu ....
Come on guys.....
By the way Unazuia watu kupata baraka zao kwa kisingizio eti anapendelea matajiri. .. wapi duniani hakuna uendeleo. ...
Tujifunze kuvumiliana tu.
 
Mhhh! Mambo haya tuliyazoea kutokea kwa Waanglikan, Walutheri, Wamoroviani, nk. Sasa kama na Wakatoliki na sisi tumeamua kuunga tela, basi kazi ipo.

Ila kama huyo Paroko naye anazingua, ni bora akahamishwa mapema ili kutuliza hali ya hewa.
Ulizoea kuona kwa wenzio sio? Ona na kwako sasa na kuanzia leo acha kudhani nyinyi ni tofauti! Waroma mnajionaga tofauti sana sijui kwanini
 
Naamini jimboni watamshughulikia ili kuweka hili jambo sawa,Kanisa Catholic huu ujinga wa kukunja makabrasha haujakuwepo nimesali Magomeni pale Mashahidi wa Uganda kabla sijahimia Mbezi tangia akiwepo Fr Benno Kikudo,akaja Fr Dismas na Fr Joseph akaja Fr Likoko hakuna siku hatukusomewa mapato na matumizi.

Jana Parokia nayosali Mbezi Makabe tumesomewa matumizi hasa wakati huu ujenzi unapofanyika aina hii ya viongozi haitakiwi huyu apewe onyo kali asiwavuruge waumini
 
RC mapadri Wana mamlaka makubwa Sana hasa icho kipengele cha mapato na matumizi ,ishu kama Hz zipo parokia nyingi sema waumini Wana vumilia na ni maswala ya kiimani.
Rwaichi najua ataweka mambo Sawa kwenye kipengele hicho.
 
[QUOTE="Mama Amon, post: 33061401, member:]

“Tunataka arudishe fedha za sadaka ya Parokia yetu milioni nne alizofuja pamoja na mpenzi wake,” sauti ilisikika akilalamika.

[/FONT][/SIZE]



[/QUOTE]

Kwani mapadre wana wapenzi au wanamzushia tu
 
Naamini jimboni watamshughulikia ili kuweka hili jambo sawa,Kanisa Catholic huu ujinga wa kukunja makabrasha haujakuwepo nimesali Magomeni pale Mashahidi wa Uganda kabla sijahimia Mbezi tangia akiwepo Fr Benno Kikudo,akaja Fr Dismas na Fr Joseph akaja Fr Likoko hakuna siku hatukusomewa mapato na matumizi.

Jana Parokia nayosali Mbezi Makabe tumesomewa matumizi hasa wakati huu ujenzi unapofanyika aina hii ya viongozi haitakiwi huyu apewe onyo kali asiwavuruge waumini
Huyo ni padri wa shirika LA mitume wa yesu na sio jimbo
 
Inasikitisha sana!

Kuna tatizo la husuda na inferiority complex muongoni mwa waumini!

Kipimo cha kujua kama anapendeleaga wenye fedha ni kipi kama wakiulizwa hao walalamikaji kwa mfano?!
 
Back
Top Bottom