JESSICA COX Rubani aliyezaliwa bila mikono

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,906
22,049
JESSICA COX Rubani aliyezaliwa bila mikono




Jessica Cox




Kuna mambo ambayo kwa uwezo wa kawaida wa mwanadamu tunaweza kudhani hatuwezi kufanya na endapo tutathubutu lazima tutumie nguvu zisizo za kawaida za uchawi au kutegemea miujiza ya Mungu. Anayefikiria hivyo hayuko sahihi kwani maisha ya Jessica Cox (25) ambaye alizaliwa bila mikono ni mfano hai wa fikra juu ya uwezo mkubwa wa mwanadamu katika mambo mengi yanayomzunguka. Madaktari hawafahamu kwa nini alizaliwa bila mikono, na hata vipimo vya masuala ya uzazi kikiwamo cha Sonograms, havikuonyesha chanzo cha ulemavu huo.

Tangu utoto alipata hisia kwamba hakuhitaji mikono ya bandia na hivyo badala ya kutumia muda mrefu kutafuta namna ya kufanana na wanadamu wengine, aliona ni vyema afurahie kuwa tofauti nao. Aliazimia kukabiliana na changamoto za kutokuwa na mikono kwa kutafuta viungo vingine mwilini kwake kuwa mbadala wa mikono ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya kimwili na kimaisha na akafanikiwa ambapo hadi leo anaitumia miguu kufanya kazi ambazo zingefanywa na mikono na hivyo kuonyesha kwamba kikwazo kikubwa katika maisha si kukosa viungo bali kukosa ujasiri wa kuthubutu na ubunifu.

Alitumia mikono bandia kwa muda na alipotimiza miaka 14 akaiacha, wakati huo familia yake ilihama kutoka Jiji la Sierra Vista katika jimbo la Arizona Marekani kwenda Jiji lingine la Tucson jimboni huko. Kwa mujibu wa Cox, mara nyingi anapovaa koti au sweta ya mikono mirefu wengi huwa wanashindwa kuelewa kuwa hana mikono.

Kama ilivyo kwa wanadamu wengine, alipitia hatua mbalimbali za kukua, akajifunza kula na kuandika kwa kutumia miguu na alishiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo michezo. Kwa mfano wakati akiwa na umri wa miaka 10, alianza kushiriki mchezo wa tae- kwondo (Aina ya mchezo wa kujihami). Ili kuendelea kuwa mkakamavu, msichana huyo pia hufanya mazoezi ya kuogelea, kutembea na pia amekuwa akicheza muziki.

Anasema ana jukumu la kuhakikisha kwamba miguu yake ina nguvu na kuwa na wepesi wa kufanya kazi yoyote. Pamoja na kutokuwa na mikono, Cox ana mkanda mweusi wa kimataifa unaotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Tae-Kwondo (WTF) na alipokwenda kusoma chuoni alijiunga na chama cha mchezo huo cha Marekani akapata mkanda mwingine mweusi.

Inaaminika kwamba Cox ni mtu wa kwanza asiye na mikono aliyepata mkanda wa Tae-Kwondo nchini Marekani na ni mwanamke wa kwanza katika historia ya usafiri wa anga ambaye ameweza kuendesha ndege kwa kutumia miguu. Ana leseni ya urubani inayomruhusu kuendesha ndege ndogo na anaruhusiwa kuruka hadi urefu wa futi 10,000 kutoka usawa wa bahari. Alifundishwa urubani na wakufunzi watatu kwa miaka mitatu kwenye majimbo ya Florida, California na Arizona.

Alikabidhiwa leseni hiyo ya urubani baada ya kumaliza mafunzo katika Kampuni ya Able Flight inayojihusisha na mafunzo ya urubani kwa watu wenye ulemavu iliyopo North Carolina nchini Marekani. Machi mwaka jana alipata nafasi ya kusomeshwa na chuo hicho na akafanya mafunzo kwa vitendo bure kwa kuongozwa na Mkufunzi, Parrish Traweek (42). Cox anasema alikuwa na woga wa mambo mengi maishani kwake lakini siku alipoendesha ndege yenye injini moja ndipo aliposhinda woga mkubwa zaidi katika maisha yake.

Wakati wa kujifunza kuendesha ndege alilazimika kuwa mbunifu kila alipoingia ndani ya ndege na kutoa mfano wa changamoto ya kwanza kuipata wakati wa mafunzo hayo kuwa ni namna ya kufunga mkanda. Anasema, ukiwa mbunifu unapata zaidi ya namna moja ya kufanya jambo fulani, na kwa kufanya utundu alitambua kuwa angeweza kufunga mkanda kabla hajakaa kwenye kiti baada kuulegeza kwa kutumia miguu. Anajivunia kuwa rubani na kueleza uzoefu wake kuwa hakuna kitu kilichompa nguvu kama mazoezi bila ya kuongozwa na mwalimu.

Anasema alipokuwa angani akiendesha ndege wakati huo wa mazoezi binafsi, alilazimika kukubali ukweli kwamba yeye ndiye mwenye jukumu la kuendesha ndege hasa baada ya kujitambua kuwa yuko peke yake bila mwalimu. "Saa 74 za kujifunza urubani kwa mazoezi, nilipokuwa juu ya Jiji la San Manuel kwa mara ya kwanza peke yangu nilitimiza ndoto zangu za tangu utotoni za kuwa Superwoman (Mwanamke jasiri)!" anasema msichana huyo ambaye mara nyingi alijifunza kwa vitendo katika anga la jangwa la Arizona.

Anapenda baadaye awe mkufunzi wa watu wenye ulemavu wanaojifunza kuendesha ndege na ameanza kufuatilia mchakato huo ili atimize lengo lake. Kazi anayoifanya leo ni matokeo ya swali aliloulizwa mwaka 2005 na rubani wa ndege za kivita, Robin Stoddard. Alimuuliza kama anapenda kuwa rubani na hakuwa na jibu lakini pia hakupuuza swali hilo akalifanyia kazi, akaanza kujifunza katika Chuo cha Wright Flight. Kabla ya swali hilo hakuwahi kuwa na ndoto za kuwa rubani na tangu alipokuwa mdogo aliogopa kuendesha ndege za abiria.

Traweek ambaye ni Mkufunzi wa Cox anamsifia binti huyo kuwa ni rubani mzuri, na imefahamika kwamba mkufunzi huyo amewafundisha marubani wengi, na baadhi yao hawana uwezo wa kuendesha ndege kama msichana huyo anayepanga kuandika kitabu kuhusu maisha yake. Cox anasema wanaosita kujifunza urubani wanakosa kumbukumbu ya kudumu katika maisha yao.

“Alipokuja hapa akitaka kuendesha ndege nilijua asingeshindwa kuendesha ndege,” anasema Traweek. Anasema ilikuwa kazi ngumu kupata ndege anayoweza kuitumia, hatimaye wakapata ndege aina ya Ercoupe ambayo ilitengenezwa kwenye miaka ya 1940. Cox aliitafuta ndege hiyo Florida na California lakini hatimaye akaipata San Manuel jimboni Arizona.

"Ukiwa na Cox kwa dakika 20 huwezi kufahamu kwamba hana mikono, anawaonyesha watu kwamba hakuna kikwazo maishani, ni wa aina yake," anasema Traweek. Msichana huyo amekuwa akitoa ushuhuda kwa mamia ya watu katika mikutano mbalimbali ya kimataifa. "Nawashauri sana watu wenye ulemavu wafikirie kuwa marubani," anasema Cox na kueleza kwamba inasaidia kuondoa mtazamo potofu kwamba watu wenye ulemavu hawana uwezo, na anavyoona yeye wanaweza kujiwekea malengo makubwa na kuyafikia.

Aliwahi kukumbana na mazingira yaliyosababisha akate tamaa ya kutofikia lengo lake, alijipa moyo na sasa ana leseni iitwayo ‘Sport Pilot License’ inayomruhusu kuendesha ndege za Ercoupe kwa kutumia miguu, aliipata baada ya kufanikiwa kurusha ndege akiwa peke yake Mei mwaka juzi.

Oktoba 10 mwaka jana alipata mtihani mwingine ambapo Mkufunzi wa Marubani, Terry Brandt, alimtaka arushe ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa San Manuel nje kidogo ya Tucson na baada tu ya kuruka, mwelekeo wa upepo ukabadilika, wakakumbana na misukosuko lakini akaweza kukabiliana nayo na kutua salama katika eneo lenye sehemu ndogo ya kutua. 'Nilimwonyesha ubora wa uwezo wangu," anasema Cox na kubainisha kwamba alipotua mkufunzi huyo alimweleza kuwa ametua vizuri.

Alipoanza kujifunza kuendesha gari, alishawishiwa atumie gari lililotengenezwa maalumu kwa ajili yake, likatengenezwa hivyo na baada ya muda akaviondoa vifaa vilivyowekwa kumsaidia akawa anaendesha kama madareva wengine, na sasa ana leseni halali ya udereva.

Ili kuthibitisha ulemavu si kikwazo kwake, amesoma Shahada ya Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Arizona na kwa sasa anaandika kwa kutumia mguu. Ana uwezo wa kuchapa maneno 25 kwa dakika kwenye kompyuta. Cox ana uwezo pia wa kuosha vyombo, kuchana nywele zake na kufanya kazi nyingine za kila siku pamoja na kujiremba.

Rubani huyo anasema changamoto kubwa kwake si ulemavu ila kuikubali hali hiyo na kujisikia mtu aliyekamilika, kuwa huru na mwenye nguvu ili jamii imkubali na ajisikie kwa namna alivyo, msichana huyo ana uwezo mkubwa wa kujieleza, ni mtoa mada mwenye ushawishi kwenye mikutano ya kimataifa. Anatoa somo kwa wengine kwamba, maisha ya wanadamu yanaathiriwa zaidi na namna wanavyofikiri kuliko upungufu wao wa kimaumbile na anafundisha namna ya kukabili changamoto za kimaumbile na kuitafsiri upya dhana ya inawezekana.

Si hivyo tu anashawishika kuamini kwamba, ulemavu na mafanikio aliyopata hadi sasa vitawasaidia wengine kutafakari zaidi na kutathmini uwezo wao wa ndani kuliko ule unaoonekana na kubadili mtazamo wao kuhusu wao na maisha kwa ujumla. Msichana huyo anaishukuru familia yake wakiwamo wazazi wake, mama yake mzazi, Inez (58), baba yake mzazi, William (68), kaka yake, Jason (28) na mdogo wake Jackie (23) kwa kumwezesha kufikia mafanikio hayo.
 
Back
Top Bottom