Jeshi Misri, taasisi iliogeuka Dola

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
From: Mohamed Abdulrahman Mohamed

Kusafishwa Mubarak kwa dhihirisha jeshi ni dola ndani ya dola


NA MOHAMMED ABDURAHMAN

Jeshi nchini Misri ndio chimbuko na misingi wa Misri ya leo baada ya mapinduzi ya 1952 yaliomn´goa Mfalme Farouk bin Ahmed Fuad . Kikundi cha wanajeshi walioitwa maafisa huru wakiongozwa na Gamal Abdel Nasser wakaitangaza nchi hiyo kuwa Jamhuri.

Mapinduzi ya Misri yalikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa katika ulimwengu wa kiarabu. Nasser akageuka kiongozi wa umajumui wa Kiarabu na haiba katika siasa za mashariki ya kati na ulimwengu kwa Jumla. Alikuwa akizungumza ulimwengu mzima wa kiarabu kutoka Iraq hadi Syria unatega sikio kumsikiliza.

Mataifa hayo mawili pamoja na Sudan na Libya yaliungana na Misri katika azma ya kuwa na Umoja wa Kijamaa wa mataifa ya Kiarabu, licha ya mivutano iliozuka baadaye, kati ya Iraq na Syria na Sudan na Libya.

Binafsi Abdel Nasser au kama wafuasi wake wengine walivyopenda kumwita kwa jina lake la kwanza “ Gamal”, alijinasabisha sio tu na Uarabu lakini pia Uafrika akitambua umuhimu wa taifa lake kijografia. Aliunga mkono harakati za ukombozi barani Afrika na Misri kuwa nchi ya kwanza barani humo kuwa na Idhaa ya matangazo ya kiswahili ya harakati za ukombozi kupigania uhuru, “ Sauti ya Afrika”, kutoka mjini Cairo. Pia akayaunga mkono makundi ya wapigaji nchini Yemen na Oman.

Jeshi wakati wote limekuwa nguzo ya kisiasa, uchumi na mhimili wa utawala. Lakini baada ya kifo cha Abdel Nasser 1970, mrithi wake Anwar Sadat haraka akabadili dira, hatua ambayo wafuasi wa Nasser ndani na nje ya Misri waliiona ni usaliti.

Misri ilianza kufuata mkondo mwengine. Sadat kuifuta sura ya kimapinduzi na kijamaa na kuijongelea kwa karibu Marekani. Msimamo wa Misri katika Mashariki ya kati ukabadilika.

Oktoba 1973 Sadat akafanikiwa kulikomboa sehemu ya Sinai iliotekwa na Israel katika vita vya Juni 1967, katika shambulio la kushtukizia dhidi ya adui yake Israel. Ushindi huo wa Oktoba ulimpa nguvu zaidi kudhibiti mamlaka yake na kuchukua maamuzi ya peke yake. Akasaini mkataba wa amani na Israel, miezi 16 baada ya hatua yake ya kijasiri ya kuizuru Israel 1977,akiwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kiarabu , kuitambua rasmi dola ya Kiyahudi na wa kwanza kuitembelea rasmi Israel na kulihutubia bunge lake la Knesset.

Maandamano ndani na nje havikumrudisha nyuma Sadat, lakini vile vile yalimuongezea maadui nyumbani na miongoni mwa mataifa mengine ya Kiarabu. Ni Kiongozi wa Sudan Jaffar el-Nimeiri pekee aliyeonesha mshikamano na Sadat. Hata hivyo kusaini mkataba wa amani 1979 na Waziri mkuu wa Israel Menachem Begin , makubaliano yaliopewa jina la Camp David , mahala yalikosainiwa nchini Marekani ukayagharimu maisha yake.

Sadat aliuwawa Oktoba 6 mwaka 1981 katika shambulio la risasi lililofanywa na maafisa vijana wa jeshi wakati wa sherehe ya gwaride kuadhimisha ushindi wa ukombozi wa sehemu ya Sinai. Ndipo hatamu za kumrithi zilipomuangukia Makamu wake Mohamed Hosni Mubarak.

Mubarak ndiye aliyeongoza ndege za kikosi cha anga wakati wa vita hivyo vya Oktoba, tukio liloufanya utawala wa Rais Abdelfatah al-Sisi umtambuwe kuwa shujaa wa taifa na kuelezwa kuwa sababu ya kutunukiwa mazishi ya kitaifa Jumatano wiki iliopita, siku moja baada ya kuiaga dunia akiwa na umri wa miaka 91.

Utawala wa Jenerali mwenzake na Rais wa dola ulijiepusha kumtaja Mubarak kuwa Rais wa zamani. Hata hivyo kuzikwa kwake kitaifa kumewaacha Wamisri wengi vinywa wazi. Sababu ni kwamba Mubarak alitawala kwa mkono wa chuma na hakuwa na simile kwa wapinzani wake ambao wengi waliishia magerezani.

Mubarak alifedheheka akafunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya raia wakati wa vuguvugu la upinzani dhidi ya utawala wake na akahukumiwa kifungo cha maisha, hukumu iliobatilishwa alipokata rufaa, kutokana na kile mahakama ya rufaa ilichodai ni ukosefu wa ushahidi. Pia alishtakiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na wanawawe wawili wa kiume, Gamal na Alaa na kupanda tena kizimbani wakiwa kwenye magwanda ya wafungwa. Mubarak alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela lakini yeye na wanawe , wote wakaachiwa huru baadaye. Hilo nalo liliwashangaza raia wa kawaida ambao hali zao za maisha zilizifi kuwa duni.

Yaliomkuta Rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasi Mohamed Morsi, aliyepinduliwa na Jenerali al-Sisi hata hivyo yalikuwa mengine. Yeye aliwekwa gerezani na kufunguliwa mashtaka. Alipandishwa kizimbani kesi ilioendelea akibakia gerezani hadi alipofariki Juni 2019 baada ya kuanguka na kuziraia mahakamani. Alikuwa na umri wa miaka 67. Utawala wa al- Sisi ulikatalia ruhusa familia kumzika kwenye kiunga chao na akazikwa katika eneo moja la wilaya ya Nasser na watu wachache tu chini ya ulinzi mkali. Hata vyombo vya habari havikuruhusiwa.

Morsi hakudumu madarakani muda mrefu kama Mubarak, ni mwaka mmoja tu. Sababu ya yeye kupinguliwa hsikufanana hata kidogo na ya utawala wa Mubarak. Walichofanana labda ni kwamba wote walipinduliwa kutokana na maandamano ya upinzani wa umma. Raia walivunjwa moyo na Morsi kwa kushindwa kuwatatulia mzigo wa matatizo sugu, ikiwemo hali mbaya uchumi na ukosefu wa umeme.

Lakini kuna sababu nyengine. Wakati Morsi alikuwa kwa baadhi ni alama ya demokrasia nchini Misri tangu alipochaguliwa 2012, kwa wengine alikuwa kitisho wakiwa na hofu taratibu alikuwa akianza kuwa mtawala wa kihafidhina aliyetanguliza ajenda ya chama chake cha Udugu wa Kiislamu, badala ya masilahi mapana ya taifa hilo. Wadadisi wanasema miongoni mwa makosa yake makubwa ni pamoja na kuchukua hatua za mabadiliko katika mfumo wa mahakama na uteuzi ambao haukuzingatia utaratibu jambo ambalo lilisababisha mvutano na vyombo vya sheria.

Hilo la ajenda ya chama chake liliwatia hofu pia majemedari wa kijeshi na mataifa ya kihafidhina ya Kiiarabu yakiongozwa na Saudi Arabia. Haikushangaza kwa hivyo al-Sisi kuungwa mkono na sehemu kubwa ya raia alipoamua kutwaa madaraka. Alipoona amejizatiti, akavua sare za jeshi, akaibadili katiba na kugombea tena. Alihakikisha hakuna mpinzani na akashinda kwa kishindo.

Kihistoria Wafuasi wa Udugu wa Kiislamu wamekuwa kitisho kwa viongozi takriban wote wa Kiarabu. Misri ilianza kulikandamiza kundi hilo tangu enzi ya Gamal Abdel Nasser aliyewatia ndani viongozi wake kadhaa na wengine kukimbilia uhamishoni. Hali hiyo ilijirudia baada ya Morsi kuangushwa na sasa kundi hilo linazingatiwa na utawala wa al-Sisi kuwa la kigaidi.

Wakosoaji wa al-Sisi wanasema kumsafisha Mubarak ni pigo kwa wahanga waliopoteza maisha yao kupigania demokrasia, ambayo Mubarak aliikandamiza kwa sheria kali ya hali ya hatari na mahakama za usalama wa taifa kuwafunga mamia ya ya waliodiriki kumpinga. Alifuata nyayo za Sadat na sasa al-Sisi anafuata nyayo za wenzake waliomtangulia, kutovumilia aina yoyote ya upinzani.

Jeshi la Misri limedhihirisha kuwa sio taasisi tu bali ni dola. Linamiliki biashara zote kubwa. Mtindo huo ulianza baada ya Sadat kuwafungulia milango wawekezaji wa kigeni. Majemedari ni miongoni mwa matajiri wakubwa, hali iliokithiri katika utawala wa Mubarak. Kwa upande mwengine rushwa na ufisadi umechangia hali mbaya ya kiuchumi kiasi ya kwamba Misri inategemea msaada wa fedha kutoka mataifa ya kiarabu ya ghuba, yakiongozwa na mfadhili mkubwa, Saudi Arabia.

Marekani ni mfadhili mwengine wa kijeshi na kiuchumi. 2018 utawala wa Donald Trump uliamua Kuruhusu msaada wa kijeshi wa dola 195 milioni, ambao ulikuwa umezuiliwa kwa sababu ya ukiukaji wa haki za binadamu. Marekani inadai kuendelea na msaada wake wa kijeshi kwa Misri ni muhimu ili kuwepo na uwiano wa usalama na utulivu katika Mashariki ya kati.

Umasikini umegeuka udhaifu na Fedha ndio yenye kuzungumza. Katika hali hiyo, Saudi Arabia sasa ndiyo inayoshika nafasi ya usoni na kuwa msemaji wa mataifa ya kiarabu , nafasi iliokuwa ikishikiliwa na Misri. Ndoto ya Gamal Abdel Nasser imezikwa. Watawala hujiepusha kumtaja na kutukuza mchango wake, katika ujenzi wa taifa hilo. Miongoni mwa yaliozikwa pamoja na Nasser ni suala la haki za Wapalestina waliokimbilia Misri 1948 . Wao na vizazi vyao walihakikishiwa haki sawa kama Wamisri, ikiwa ni pamoja na elimu , matibabu na ajira. Yote yaliondolewa alipoingia madarakani Sadat na Leo hali yao haikubadilika.

Wachambuzi wanaziona hatua zote za kuachana na sera za Gamal Abdel Nasser ni sehemu ya watawala wa kijeshi aliofuata kuhakikisha wanabakia madarakani kwa kuridhia wanachokioni ni mabadiliko ya hali ya kisiasa duniani , lakini kutokuwa tayari kuridhia mabadiliko yoyote ndani ya Misri kwenyewe. Kutwaa madaraka Abdelfatah al-Sisi 2012 na kumuangusha Mohamed Morsi, pamoja na tukio la kumtangaza Hosni Mubarak kuwa shujaa na kumpa mazishi ya kitaifa, kunadhihirisha Jeshi nchini Misri sio tu ni taasisi bali ni Dola.

Nakumbuka maneno ya jirani yangu mmoja kutoka Misri, aliyenambia, "My brother for Sisi, the word democracy is not in his dictionary”( Ndugu yangu kwake Sisi, neno demokrasia halimo katika kamusi lake).

Inaelekea Wamisri wataendelea kuwa katika hali hiyo kwa kipindi kingine kirefu.

Chanzo:Raiamwema

Baruapepe:,mamohamed55@hotmail.com





Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom