Jeshi la Polisi lina Matatizo matatu(3); Yanapelekea Tatizo moja Kubwa!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,478
39,998
CGail-GUQAACtWJ.jpg
Na. M. M. Mwanakijiji

Jeshi la polisi lina matatizo au mapungufu makubwa manne; mapungufu haya yanasababisha au yamekuwa sababu kuu ya tatizo moja kubwa ambalo bado hatujalipatia ufumbuzi wa kudumu. Uhusiano kati ya wananchi na Jeshi lao unategemea sana kutambulika kwa matatizo haya na kutatuliwa kwa kiasi ambacho kitafanya pande zote zione hali imetengamaa sana.

Nimewahi kuandika hili mara kadhaa huko nyuma. Mojawapo ya mada ambazo nilijaribu kuchokozesha ni ile niliyoposti March 18, 2008; karibu miaka kumi nyuma. Mada hii Jeshi la Polisi na mabadiliko yanayohitajika ilikuwa ni miongoni mwa mada ambazo zilikuwa zinajaribu kuangalia jeshi la polisi na nini kifanyike kuliinua na kuliingiza kwenye karne hii ya ishirini na moja. Watu mbalimbali walitoa michango yao. Hivyo, maoni yangu hapa kwa wengine wanaweza kuyaona mageni lakini si mageni kwani ni yale yale ambayo nimeyatoa huko nyuma labda sasa hivi nayatoa tena kwa sababu naamini kuna watu wanaweza kuyafanyia kazi kweli kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Na matatizo nitakayoyaainisha hapa nayo siyo mageni.

Tatizo la Kifikra

Mojawapo ya matatizo makubwa zaidi na labda ndilo linalobeba matatizo mengine ni tatizo la kifikra. Tatizo hili la kifikra (ideological) kimsingi ni tatizo ambalo linatokana na kutokubadilika kifikra. Taasisi zetu nyingi za umma zimebadilika kwa kiasi kikubwa kulinganisha na miaka baada ya uhuru au wakati wa ukoloni. Vyombo vyetu vya usalama kwa kiasi kikubwa havijabadilika sana ukiondoa Jeshi la Wananchi.

Kifikra Jeshi la Polisi ni jeshi la Serikali. Mwaka 2012 katika mada yangu nyingine niliyoanzisha kufuatia mlolongo wa matukio fulani fulani nilisema hivi “Kwa muda wote huu wa Said Mwema na Mkuu wa "Operesheni na Mafunzo" Bw. Chagonja kumekuwepo matukio mengi sana ya uvunjaji wa haki za raia, matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya raia wasio na silaha na kukosekana kwa umakini katika kushughulikia maandamano au mikusanyiko mikubwa ya watu.” Rejea: Said Mwema + Charles Chagonja: Kuparaganyika kwa jeshi la Polisi; Lowassa hapa vipi?

Watu wengi ambao wanazungumzia tukio la kuuawa kwa binti Akwilina na mgongano wa polisi na upinzani wanaangalia kama ni jambo jipya. Hili si jipya na halijabadilika. Hali iliyokuwa hivyo miaka sita nyuma! Jeshi la Polisi bado halijabadilika kifikra.

Katika makala ile nilisema hivi labda hata kwa kuona mbali “Binafsi naamini wakati umefika wa viongozi wa CDM kuitisha maandamano makubwa tu ya kupinga ubovu na uzembe wa Jeshi la POlisi kwani hadi hivi sasa ni wao CDM ndio wanakiona cha moto dhidi ya mkono wa askari wa Mwema.”

Ni fikra gani basi hizi zinazosumbua Jeshi la Polisi na kusababisha hali hii ya kugongana na raia wake?

1. Masalio ya fikra za kikoloni – colonial legacy: Mojawapo ya vitu ambavyo mkoloni alifanikiwa sana kuvifanya ni kutengeneza jeshi la polisi ambalo lilitakiwa kuwa la utii (loyal) na lenye kumtumikia mtawala. Lengo la Jeshi la Polisi lilikuwa ni kuhakikisha kuwa “koloni” linakuwa katika hali ya utulivu na amani; mwananchi hakutakiwa kumsumbua mtawala yaani serikali.

Japo tulipata uhuru na jeshi la polisi kuundwa kama la raia wa Tanzania bado mwelekeo wake (orientation) ni kutumikia serikali iliyoko madarakani na hata chama kilichoko madarakani.



2. Masalio ya Mfumo wa chama kimoja: Wakati wa mfumo wa chama kimoja, majeshi yalikuwa ni kama Jumuiya ya chama. Hata kwenye mikutano ya chama viongozi wa majeshi na vyombo vya usalama waliingia wakiwa na kadi zao na wao wenyewe katika kambi zao walikuwa na matawi ya CCM. Majeshi yalitakiwa kutoa makada wa chama na wengi watakumbuka kuwa viongozi kadhaa wa vyombo hivi vya usalama walikuwa ni makamisaa wa siasa (political commissar) katika jeshi; yaani wakisimamia shughuli za siasa katika sehemu zao hizo.

Kutokana na kuingiliana huku, mfumo wetu uliruhusu watu kutoka jeshini kwenda kwenye nafasi za serikali na watu wa serikali kwenda jeshini na kupanda vyeo n.k. Ndio maana watu kama Rais Kikwete na Edward Lowassa wote walitoka majeshini na kupelekwa kwenye nafasi za kisiasa na wengine wengi walifuata njia hiyo. Matokeo yake, kulikuwa na madeni mengi sana ya wanajeshi waliotaka kuingia kwenye siasa.

Leo hii bado kuna aina fulani ya kuwiwa ambako kuko jeshini ambapo kwenye Jeshi la Polisi kama ilivyo JWTZ bado kuna watu wanaamini na kutegemea kuwa wakimaliza nafasi zao wanaweza kuingia kwenye siasa au kupata nafasi katika siasa. Hili limeendelea kufanyika ambapo viongozi mbalimbali wa majeshi wamejikuta wakiingizwa kwenye siasa. Hakuna mfumo mzuri wa kuhakikisha muda fulani umepita kabla mtu hajaingia kwenye nafasi za serikali. Hili linafanya watu wawe na maswali juu ya maamuzi ambayo yanaweza kutolewa na viongozi wa polisi hasa kama yanaweza kuharibu nafasi zao huko mbeleni.

Tatizo la Kimafunzo

Tatizo la pili kubwa ni tatizo la kimafunzo. Katika ile makala yangu niliyojadili kuparaganyika kwa utendaji wa jeshi la polisi nilielekeza maswali yangu kwa aliyekuwa Kamishinda wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi hilo Kamishna Paul Chagonja. Binafsi nilikuwa na tatizo naye kwa sababu utendaji kazi wa jeshi chini yake ulikuwa unahoji kama askari wetu walikuwa wanapewa mafunzo sahihi ya kutumikia wananchi katika nchi ya kidemokrasia.

Tatizo hili la mafunzo limekuwa likionekana mara kwa mara kiasi kwamba inaweza kuhojiwa kwa haki kabisa kama polisi wetu hasa ngazi za chini wanafundishwa nini wanapojiunga na jeshi hilo na kama wanapewa nafasi ya kujiendeleza kimafunzo katika nadharia na mbinu za jeshi la polisi. Nitatoa mfano mmoja ambao si mgeni; mara kadhaa inapotokea mgongano kati ya Jeshi la Polisi na waandamanaji au kundi kubwa la watu ni kana kwamba polisi hawajui wafanye nini na badala yake njia yao rahisi ni kuanza kushambulia raia bila kubagua (indiscriminately).

Tumeliona hili majuzi wakati jeshi la polisi lilipojaribu kuzuia kundi la waandamanaji waliotaka kuweka shinikizo kwa Msimamizi wa Uchaguzi Kinondoni. Ukiangalia video na picha mbalimbali ni rahisi kuona ni jinsi gani polisi wanakuwa kama mbwa walioachiwa kiasi kwamba hakuna mtu anayewaongoza namna ya kushughulikia makundi ya raia bila kulazimika kutumia silaha za moto hasa kama kundi hilo halina hostility dhidi ya jeshi au watu wengine. Kama watu wanatembea tu kwenda kuulizia hata kama ni wengi kiasi gani, badala ya kuwatawanya kuna ugumu gani kuhakikisha wanakwenda wanakokwenda kwa njia ya amani na kuhakikisha wakimaliza wanachotaka wanaondoka kwa amani? Je, ni lazima kila watu wanapoandamana ni lazima watawanywe kwa nguvu?

Haya yote yanahoji, Je, Kamishna Nsato Marijani anayesimamia Operesheni na Mafunzo anaweza kusema nini juu ya weledi wa askari wake? Je, anaridhika na jinsi wanakutana (engage) raia? Je, ni lazima wakati wowote raia ambao ni wanachama wa upinzani wanapokutana na polisi iwe ni katika uadui (hostility)? Je, polisi wetu wanafundishwa nini jinsi ya kutuliza hali ambayo inachemka na kuwafanya watu watulie badala ya kuanza piga piga? Je, hivi ndivyo wanawafundisha vijana wetu?

Tatizo la Kimuundo

Bado jeshi letu kimuundo bado halijakaa sawasawa hasa linapokuja katika kufanya kazi katika mazingira ya vyama vingi. Sidhani kama polisi wameshakaa na kujiuliza ni jinsi gani wanaweza kusimamia haki za raia mbalimbali katika nchi yetu katika mazingira ambayo yana pande mbili ambazo wakati mwingine kisiasa zinakuwa mbali sana (polarized public). Hivi ni kweli kabisa, polisi wao kazi yao ni kukamata wapinzani, kuwesweka ndani, kuwanyanyasa kila inapowezekana ili kuhakikisha wajue kuwa hawako serikalini?

Hili pia linaweza kuonekana katika kushughulikia mambo yanayowakuta wapinzani. Mojawapo ya mambo ya hatari sana ambayo yanaweza kuja kutokea mbeleni – na bahati mbaya sioni ni namna gani hili litaepukika – ni kuwa yale ambayo yanawakuta wapinzani yanaweza kuja kuwakuta watu wa chama tawala. Tunapopuuzia au kufanya siyo jambo zito la kushtua kiongozi wa upinzani anapouawa au kujaribiwa kuuawa na badala yake kuchukulia kama ni “linaweza kumpata yeyote” tunatengeneza mazoea ya hatari. Ikumbukwe kuwa historia ni mwalimu mzuri sana, lakini ni mnyapara mbaya sana wa kumbukumbu; mauaji ya kisiasa au yanayoonekana kuwa ni ya kisiasa mara zote hatima yake ni kujibiwa kwa mauaji ya kisiasa vile vile.

Leo hii, tunaweza kuona kuwa haya yanayowakuta viongozi wa Chadema au wanachama wake ni ya kawaida; na tunaweza kusema “wakome”. Lakini tusije kushtukia siku moja yanaanza kuwakuta viongozi na wanachama wa CCM na kuanza kwa mauaji na vitendo vya kulipizana visasi. Hakuna kitu kibaya sana kama roho ya kisasi kwani huwa inapita kwenye damu hadi vizazi vingine. Leo hii tunaweza kukaa kimya na kudhani kuwa hili limekwisha lakini watakuja kutendewa wengine na sote tutaanza kuona hili limefikaje.

Tunatokaje hapa:

Kuna mambo mengi yanaweza kufanyika kuanzia sasa ili kujenga uhusiano mwema kati ya Jeshi la Polisi na raia wanaowatumikia. Binafsi nina mapendekezo machache tu.

1. Jeshi la Polisi liheshimu uhai. Mojawapo ya mambo yamenishangaza zaidi ni mwitikio wa watu mbalimbali kufuatia kuuawa kwa binti Akwilina. Watu wengi wameonekana kuumizwa, kushtushwa na kuguswa na mauaji ya binti yule na bila ya shaka kwa haki kabisa. Lakini pia imenifanya nihoji kama watu wameguswa kwa sababu binti mzuri, mwanafunzi, na ambaye picha yake imemuonesha kama binti ya mtu fulani, dada, rafiki na hata ndugu. Kwamba, watu wameguswa kwa sababu wameona picha na kujua kuwa binti yule hakuwa kwenye maandamano na tena alikuwa kwenye shughuli zake. Hizi ndizo sababu watu wameumizwa?

Binafsi nimeumizwa kwa sababu moja tu; uhai wa mwanadamu mwenzetu umekatishwa bila sababu ya msingi na nje kabisa ya utaratibu wa kisheria. Sijajali sana kama aliyeuawa ni binti, ana picha Facebook, alikuwa anaenda chuo, alikuwa kwenye basi n.k Haya yote yanaweza kugusa lakini kubwa ni kwamba amepoteza uhai! Hakuna haki ya msingi ya mwanadamu kuliko haki ya kuwa hai!

Polisi wameonekana mwanzoni kupuuzia jambo hili na hata kulaumu upinzani na hata kuonekana kama hawajalipa uzito wake. Hili ni kweli kwenye matukio mengine. Ndugu zangu, haijalishi nani ameuawa ni lazima tuoneshe tunajali uhai! Kama aliyeuawa angekuwa ni muuza machungwa katika shughuli zake tungeguswa hivi; mawaziri na viongozi wangejitahidi kwenda kutoa pole nyumbani kwao? Je, angeuawa mzee mmoja hivi ambaye alikuwa anajipitia tu kwenye shughuli zake bado tungeitikia vile vile? Na hata kama angeuawa kijana katika maandamano yale bado tungechukulia kuwa ni makosa ya Chadema?

Jeshi la polisi NI LAZIMA lioneshe linajali usalama WA RAIA NA MALI ZAO. Na hawa raia ni Watanzania wote! Haijalishi vyama vyao, haijalishi dini zao, haijalishi ukwasi wao, uzuri wao, urembo, fedha au hali yoyote waliyo nayo; kwamba wao ni raia inatosha kuwa sababu ya kushtushwa wanapopoteza uhai, na polisi wasiwe wa kwanza kutoa roho za watu au kuonekana kupuuzia wanaposikia mtu kauawa. Ni lazima jeshi lioneshe linaheshimu uhai wa raia wake.




2. Kurejesha Makamisaa wa Polisi:
Tujenge uhusiano mpya kati ya siasa na jeshi la polisi. Mojawapo ya mapendekezo yangu ni kuona jinsi gani jeshi la polisi linajipanga upya (new alignment) kutumia wadau mbalimbali wa kisiasa bila kuonekana lina upande. Njia mojawapo napendekeza ni kurejesha wadhifa wa Makamisaa wa Polisi katika Jeshi la Polisi. Maafisa hawa wajuu wawe wa mikoa na wenye vyeo kuanzia Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) na kuendelea na wawe na jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za kisiasa katika mikoa yao. Kinyume na makamisaa wakati wa mfumo wa chama kimoja katika mfumo huu makamisaa watakuwa na majukumu angalau yafuatayo:

· Kuwa kiunganisha kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa (political liaison)

· Kuhakikisha shughuli za kisiasa zinafanyika kwa amani

· Kuidhinisha maandamano na kutoa ulinzi kwenye maandamano hayo

· Kutoa ulinzi kwa vyama na viongozi wa kisiasa inapohitajika

· Kuwa wa kwanza kutuliza mihemko ya kisiasa na kutafuta suluhishi inapotokea migongano

· n.k

Jambo la muhimu hapa ni kuwa chini ya makamisaa wa polisi, vurugu na mauaji yenye mazingira ya kisiasa yawe ni mambo ya zamani. Kusiwe na hisia hisia tena. Kamisaa wa polisi alitakiwa afuatilie madai ya CHADEMA kuhusu shahada za mawakala na kuhakikisha zinapatikana mapema na hivyo kuondoa ulazima wa maandamano. Chadema wangelalamikia kwake. Maslahi ya huyu ni kuhakikisha kuwa shughuli za kisiasa ikiwemo uchaguzi wowote ule vinafanyika kwa amani na utulivu lakini pia katika haki ya kuaminika na isiyoonesha upendeleo wa aina yoyote. Bila ya shaka hapa nazungumzia upande wa kiusalama tu kwani kuna taasisi nyingine nazo zinahitaji kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Matatizo haya yote yanachangia katika tatizo letu moja kubwa; nalo ni watu kuona kuwa jeshi la polisi ni la chama tawala, linamtumikia Rais na liko dhidi ya upinzani. Hii si lazima iwe hivyo.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
 
umesomeka vema, changamoto inabaki kuwa police political commissar mwenye cheo cha SSP anawajibika kwa RPC mwenye cheo cha ACP au SACP na kwa muundo wa jeshi la polisi atawajibika kupokea amri za bosi wake na ambao wengi wao akili zao wanazijua wenyewe
 
Siku Watanzania na hasa upinzani wakimtambua adui wao wa kweli ndio itakuwa chanzo cha ukombozi wa kweli. Rais aliye madarakani ndio amekuwa chambo na dodoki la lawama.

Hata kama leo aondoke JPM madarakani ....si chadema wataoshika nchi ....wanaweza kumuondoa CCM wenyewe na wakabaki madarakani ....cha moto kipo pale pale ....Polisi na vyombo vya dola ni matokeo tu ...
 
Umeishia kuwalaumu polisi ambao mwisho wa siku wanafanya kazi kwa orders tu. Vipi hao wanaotoa order kwa jeshi la polisi huoni nalo ni tatizo tena kubwa zaidi?
 
Tatizo kubwa la polic ni kuwa uongozi wao umekuwa compromised na viongozi wa chama tawala ambao ni wanasiasa.

Today ni rahisi sana mwanachama wa chama tawala akaamuru polic kwenda kufanya jambo fulani na wakaenda tu kichwa kichwa.

polic inahitaji reform kwenye uongozi, ile access ambayo chama tawala wanayo juu ya polic ikatwe ili polic wasilalie upande wowote
 
Iliripotiwa kwamba askari walipofika karibu na waandamanaji walitoa onyo kua waandamanaji watawanyike na kua hiyo ni amri ya amiri jeshi mkuu na wao walikua wanatii amri ya amiri jeshi.

Ikiwa walipiga risasi usawa wa vichwa na mapaja ya watu ni kusema kua ama amiri jeshi mkuu alisema nendeni mkapige risasi au hakusema ila ni manual yao askari ndivyo inavyowaelekeza.

Hoja yangu ni kua huu uzi ungegusa mahala pake kama amiri jeshi mkuu angeuona na akaufanyia kazi. Siro au Mambosasa wakiuona wanaweza kukubali kua ni kweli uzi una hoja lakini wanatakiwa kumtii aliyewateua.
 
Ndiyo kusema kutibu mgonjwa lazima ujue anasumbuliwa na nini!

Restructuring the Police Force at this point is the only way forward- Jitihada za kubadili jina toka wizara ya ----- kwenda ya Usalama wa Raia haisaidii kitu.

Tunafaa tuende mbele. Mfumo,Sheria ,Sera na Majukumu ya jeshi la Police yanafaa yafanyiwe mapitio- Vikwazo vingine vya Maendeleo huwa havionekani.
 
SIASA ndio chanzo cha matatizo yoote ndani ya jeshi la Polisi, unapotaka kutatua tatizo lolote lazima kwanza ujue chanzo cha tatizo lenyewe, Chanzo cha matatizo yote ndani ya jeshi la Polisi ni SIASA..

CCM wanalitumia jeshi la polisi kama moja ya ngao yao ya kuendelea kuwepo, hali hii imelifanya jeshi la polisi kujikita zaidi na majukumu haya na kuacha majukumu yake ya msingi..
 
Ili kuondoa masalia ya fikra, maudhui, muundo na utendaji wa kikoloni katika zama hizi za kujitawala Serikali ya JMT haina budi kutengeneza upya Katiba na sheria zetu, hilo haliepukiki iwe katika muda mfupi au mrefu.

Kuna mgongano, mwingiliano, mchanganyo (confusion) na uchafu mwingi wa sheria na utendaji ambao unaotokana na msingi mbovu; na chanzo cha hayo ni Katiba (mbovu/dhaifu) ya Nchi. Viraka vimekuwa vingi mpaka vazi halijulikani ni la aina gani au rangi gani tena (huwezi kujua ni joho, kanzu, gauni au overcoat). Na kama sio udhaifu wa upinzani na ujinga wa wananchi naamini Watawala wangeshalazimishwa kuona wanachokataa kukiona kwa miongo kadhaa.
 
Back
Top Bottom