JENEZA LA TAIFA : Riwaya bora ya Kiswahili

Orketeemi

JF-Expert Member
Joined
Feb 12, 2013
Posts
5,514
Reaction score
14,173
Wakuu nimeonelea kushare nanyi riwaya hii Bora kutoka kwa mwandishi mahiri wa maabdishi bunifu aitwaye Maundu Mwingizi.

Mwandishi wa riwaya hii anaisimulia kupitia ukurasa wake wa Facebook uitwao #Maundu Mwingizi.

JENEZA LA TAIFA: [Riwaya iliyoshinda Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu]

Mtunzi: Maundu Mwingizi

Sura ya Kwanza

Ilikuwa ni sauti ya mtu anayejaribu kujizuia kutoa sauti, lakini ilivyosikika masikioni mwangu ni kama sauti ya nyani mtoto mwenye njaa au mchoko.

Ni sauti hii ndiyo iliyonishitua usingizini, japo sikuweza kuitambua kwa haraka ni sauti ya nini–au ya nani. Kama ni sauti ya mtu, niliwaza, vyereje ajizuie kutoa sauti? Na kama ni sauti ya nyani mtoto, amefuata nini nyumbani kwetu usiku wa manane? Niliteremsha miguu sakafuni na kuketi kitandani huku nikipikicha macho kuondoa usingizi.

Chumba changu kilikuwa kidogo kilichosheheni vitu vingi. Awali, chumba hiki kilipaswa kuwa jiko, lakini mama yangu alikifanya stoo ya kuhifadhia vyombo, ndoo za maji, vyakula na vitu vidogo vidogo. Baadaye akaweka kitanda kidogo na kunihamishia humo. Tangu hapo niliacha kulala naye chumbani mwake, na hiki ndiyo kikawa chumba changu.

Nilisimama na kutembea taratibu kuulekea mlango wa chumba huku giza likinifuata kwa nyuma na kunitangulia kwa mbele. Giza halikuwa tatizo kwangu. Niliamini naweza kutembea nyumba nzima nikiwa nimejiziba macho kwa kitambaa cheusi bila kuparamia vitu vilivyosheheni ndani. Hii ndiyo nyumba niliyozaliwa na kukulia, hivyo, nilikuwa nikiijua kuliko kiganja changu cha mkono.

Nilipopiga hatua kadhaa mbele, hesabu zangu ziliniambia kuwa, hapo ndipo mahali ambapo kabati dogo la vyombo huwapo. Nilijaribu kupapasa na kweli nikaligusa. Hatua nyingine tatu mbele, zilinifikisha mahali ambapo ndoo za maji hupangwa. Nilipojaribu kupapasa kwa mkono wa kulia, nikagusa maji kwenye ndoo iliyokuwa wazi.

Nilipojua tayari nimekwisha kuukaribia mlango, nilipiga hatua za mwisho ili kuufikia. Bila kujua kilichopo mbele yangu, niliparamia birika la chai pamoja na masufuria vilivyokuwa sakafuni. Sauti ya vyombo hivyo ikasikika chumba kizima–au tuseme nyumba nzima–na papo hapo ile sauti ya nyani mtoto ikatoweka ghafla.

Niliganda kama mke wa Lutuh alipogeuzwa mwamba wa chumvi. Kimya kilizizima kiasi kwamba hapakusikika sauti ya mtu wala kitu. Isingelikuwa hivi vinyweleo ndani ya matundu ya pua yangu, nisingelisikia hata sauti ya pumzi zangu mwenyewe. Kama uliamini naweza kutembea nyumba nzima hali ya kuwa nimefunga kitambaa cheusi machoni–kabla hata hujajua umri wangu–basi hilo ni tatizo lako, si langu.

Niliendelea kusimama bila kutikisika mpaka nilipoisikia tena sauti ile. Safari hii ilisikika kama sauti ya mtoto mwenye kwikwi. Haikuwa sauti kubwa sana bali kutokana na hali ya utulivu wa usiku, ilikuwa kama iliyochujwa na kukuzwa. Kwa hadhari ya hali ya juu, niliburuza nyayo sakafuni hadi nilipoufikia mlango na kutoka.

Mwanga wa taa uliopenya toka chumbani kwa mama, ulilikimbiza giza sebuleni huku harufu ya mafuta ya taa ikisambaa sebuleni, ishara kwamba chemli ilikuwa imewaka kwa muda mrefu. Hapo ndipo niliisikia vizuri ile sauti. Ilikuwa ikitokea chumbani kwa mama. Mshawasha wa kutaka kujua kitokanacho na sauti ile ulinifanya nipige hatua za haraka kuufikia mlango wa chumbani kwake na kuusukuma.

Nilimkuta mama yangu na mwanaume mmoja wakiwa sakafuni kama walivyozaliwa. Nilipiga kelele za kupagawa mithili ya mjane aliyetokewa na mzimu wa mumewe. Yule mwanaume aliruka toka kifuani kwa mama–mtupu kama alivyokuwa–na kukimbilia karibu na masanduku ya nguo, yaliyokuwa juu ya meza ndogo kwenye kona ya chumba. Alifanya haraka kujiziba sehemu za siri lakini mikono yake ilizidiwa kasi na macho yangu. Alikuwa mfupi, mnene na mweusi. Macho yake ya duara yalikoza njano mithili ya kiini cha yai. Shingo yake ni kama ilimezwa kifuani kiasi cha kufanya kichwa chake kionekane kama kimetengwa katikati ya mabega yake. Na kwa kadri ya ufupi wake, ndevu pamoja na nywele za kifuani vilionekana kukutana kwa pamoja.

Kumwona mama yangu akiwa mtupu halikuwa jambo la ajabu kwangu. Nimepata kumwona mara nyingi akiwa hivyo. Mama yangu, kama walivyo akina mama wengi mtaani, alikuwa na desturi ya kuvua nguo mbele yangu kila alipokuwa akiingia au kutoka bafuni kuoga. Na hata wakati mwingine tulioga pamoja. Alifanya hivyo kwa kudhani umri wangu ungali mdogo kuelewa chochote, na pengine kwa sababu sote jinsi yetu ni moja. Na kwa kuwa mara kadhaa nilipata kuoga na Sandra, mtoto wa mwenye nyumba, hivyo, siku zote nilikuwa nikiamini watu wote duniani tunafanana maumbile. Siku hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kumwona mtu wa jinsi nyingine akiwa mtupu. Hilo lilichangia kunitisha. Na mbaya zaidi, nilipomtambua mwanaume huyu: Baba Kamau.

Baba Kamau pamoja na mkewe, mama Kamau, walijulikana sana na watoto hapo mtaani, kila mmoja kivyake na kwa namna yake.

Mama Kamau alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Buguruni. Alijipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa wanafunzi. Ilikuwa ni kawaida kila aliporejea nyumbani akitokea shuleni, watoto wengi tungesitisha michezo na kumlaki kwa shangwe na sauti kuu: “Shikamoo Mwalimu!”

“Marahaba wanafunzi wangu!” Angelisikika akiitika salamu kila alipoamkiwa. “Hamjambo?”

“Hatujambo Mwalimu!”

Cha kufurahisha, watoto wengi tuliokuwa tukimlaki kwa salamu, hata shule tulikuwa hatujaanza. Hivyo, kumsikia mwalimu maarufu kama yeye akituitikia salamu huku akitutambua kama wanafunzi wake, kulituongezea si tu mahaba juu yake bali pia hamu na shauku ya kuanza shule.

Siku moja, mimi na Sandra tukiwa tunacheza nje ya nyumba yetu, tulimwona Kamau akitokea shuleni. Alikuwa darasa la kwanza wakati huo. Alivalia shati jeupe la mikono mifupi, alilolichomekea kwenye kaptula ya buluu. Alivaa viatu vyeusi vya kamba, pamoja na soksi zilizopanda mpaka magotini. Mgongoni, alibeba begi la madaftari, na mkononi alishika ufagio wa chelewa. Chambilecho wahenga, mbwa wa Mfalme ni Mfalme wa mbwa wote. Tulimpenda na kumheshimu Kamau kama ilivyokuwa kwa mama yake. Kila alipopita mtaani, tulimwuliza mambo kadhaa waliyojifunza shuleni. Alituonesha madaftari yake, akituimbia nyimbo, na mengine mengi yahusuyo shule.

Siku hiyo, tulimwomba atupeleke nyumbani kwao ili tukamsalimu mama yake. Ilikuwa ni raha kufuatana naye kana kwamba sote ni wanafunzi. Sandra na Kamau walizoeana zaidi yangu, kwa sababu ya wazazi wao; Mama Sandra na Mama Kamau walikuwa marafiki. Na mara kadhaa Mama Kamau aliingia nyumbani kwetu. Kwa hivyo, Kamau hakuwa na pingamizi. Kiasi cha dakika kumi kwa mwendo wa miguu, zilitufikisha kwa akina Kamau. Hii ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumwona Baba Kamau kwa karibu. Alikuwa kifua wazi huku mkononi ameshika upanga akikata majani ya miti iliyostawi kuzunguka nyumba yao.

Moja kati ya simulizi mashushuri miongoni mwa watoto kumhusu Baba Kamau, ni kwamba alikuwa akila watu. Pengine simulizi hii ilishajiishwa na kimo chake pamoja na maeneo aliyokuwa akifanya kazi. Alikuwa ni dereva wa magari makubwa yaendayo nchini Kongo. Siku hizo, palikuwa na uvumi kwamba nchini Kongo watu wafupi walikuwa wakiliwa. Cha ajabu, yeye ndiye alikuwa mfupi, lakini tuliamini ni yeye ndiye anakula watu. Nilipogeuka kumtazama Sandra, tukakutanisha macho na papo hapo tukageuza na kutimua mbio kurudi nyumbani, tukimwacha Kamau akitushangaa.

Kumwona Baba Kamau chumbani kwa mama yangu, akiwa kama alivyozaliwa, tena usiku wa manane, kulinifanya nihisi huenda siku ile tulipomkimbia nyumbani kwake alituona, na kwamba amekuja kutukamata ili kututafuna. Hivyo ndivyo ubongo wangu mchanga ulivyochakata tukio lile. Kwa kunitazama ungedhani nina umri wa miaka saba, ingawaje mimi mwenyewe nilijiona na miaka kumi, lakini kiuhalisia nilikuwa na miaka minne–kuelekea mitano.

Usingeamini kuwa nina miaka minne mpaka pale ambapo ungeshuhudia matendo yatokanayo na akili zangu. Hili la kudhani Baba Kamau anataka kumla nyama mama yangu ni moja tu, yako mengine. Mfano, mama yangu alipenda sana kuniambia kuwa ninakua kwa haraka kama mgomba–na kwamba, kila siku usiku nyumba inapokuwa kimya wakati tumelala, huwa akiisikia mifupa yangu ya mwili ikitanuka na kujinyoosha. Tangu hapo, kila niliposhituka usiku, nilikuwa nikiganda kimya ili kusikiliza kama nitaisikia hiyo mifupa yangu inavyotanuka. Japo sikuwahi kuisikia hata mara moja, lakini bado niliendelea kumwamini hekaya zake.

“Haya nenda chumbani ukalale, niko na mgeni,” mama alisema huku akijigeuza pale sakafuni na kujilaza kiubavu; mguu wa kushoto akiuweka juu ya ule wa kulia ilhali kiwiko cha mkono wa kulia kikibaki sakafuni na kufanya mbavu zake zisiguse chini. “Hebu angalia ni muda gani sasa.” Aliitazama saa ya ukutani, nami nikaitazama ingawaje sikuwa nikijua kusoma.

“Naogopa,” nilijibu huku nikifuta machozi kwa sehemu ya nyuma ya kiganja.

Mama alinyanyuka sakafuni, akajifunga kanga chini ya makwapa na kunisogelea mlangoni nilipokuwa nimesimama. Alinishika mkono akisema, “Haya twende chumbani ukalale. Usiogope. Niko na mgeni.”
*****

Asubuhi ya siku iliyofuata niliamka kama kawaida. Nilitoka nje na kumwona mama yangu akichota maji bombani na kwenda kuyajaza kwenye majaba yaliyokuwa pembezoni mwa ukuta wa uzio wa nyumba. Pembeni ya ndoo alikusanya rundo la nguo za kufua.

“Shikamoo mama!” nilimsabahi, baada ya kumfikia hapo bombani.

“Marahaba mtoto wangu,” alijibu huku akinishika kichwani na kunipapasa kama vile ananikuna nywele. “Umeamka salama?”

Nilitikisa kichwa kuafiki.

Japo nilikuwa mdogo mno kuweza kuelewa kile nilichoshuhudia usiku, lakini sikuwa mdogo wa kushindwa kukumbuka nilichokiona. Kila nilipomtaza, taswira ya Baba Kamau akiwa juu yake ilijirudia kichwani mwangu kama sinema. Baada ya ubongo wangu kushindwa kuchakata taswira ya tukio lile na kupata tafsiri ya kilichokuwa kikifanyika, nilifikia hitimisho kuwa pengine ilikuwa ni ndoto tu, na kwamba Baba Kamau hakuwemo chumbani kwa mama usiku.

“Haya ukamsalimie na ma’mkubwa,” alisema huku macho yake akiyaelekeza nyumba kubwa.

Niligeuza uso na kumwona Mama Baruti akifagia mlangoni kwake. Alikuwa amevaa gauni la rangi ya samawati. Kichwani alijifunga kilemba cha kijani na njano. Nilimfahamu Mama Baruti kama mama yangu mkubwa – na watoto wake wawili; Baruti na Sandra kama ndugu zangu. Mara kadhaa nililala kwao na mara chache Sandra alilala kwetu.

“Shikamoo, ma’mkubwa,” nilimsabahi baada ya kumfikia.

“Marahaba, Chiku,” alijibu huku akiinua kichwa na kunitazama. “Hujambo?”

Alikuwa mnene kiasi na mrefu kuliko mama yangu. Sugu nyeusi kwenye maungio ya vidole vyake zilionekana kwa haraka kutokana na mkorogo kushindwa kumng’arisha baadhi ya maeneo. Sehemu ya juu ya mashavu yake alikuwa mwekundu kama aliyevilia damu.

“Sijambo,” nilimjibu huku nikirejea kwa mama yangu.

Japo sikuwahi kumwona mama yangu, hata siku moja, akilipa kodi ya nyumba wala bili ya maji, lakini kila lilipotokea jambo linalomhitaji mwenye nyumba, Mama Baruti ndiye alifuatwa na kutoa maelekezo. Hata mpangilio wa nyumba ulidhihirisha hilo. Yeye aliishi nyumba kubwa yenye vyumba vitatu vya kulala, sebule, stoo, jiko na choo cha ndani–iliyokuwa ikitazama barabarani. Mimi na mama tulikuwa tukikaa kwenye banda la kushoto huku banda la kulia likiwa na mpangaji aliyeitwa Sheila. Kila banda lilikuwa na chumba kimoja, sebule, na stoo. Japo nyumba haikuwa na umeme lakini ilikuwa na bomba la maji.

Usiku wa siku iliyofuata, nakumbuka Sheila na Mama Baruti walikuwa uani wakichota maji kwa muda mrefu. Mama yangu alikuwa juu juu kama ngoma ya daku. Alizunguka sebuleni kisha akatoka uani. Aliporudi sebuleni alikaa na kuinuka ndani ya dakika moja. Alitazama saa ya ukutani, kisha akachungulia uani na kusonya. Aliendelea na zoezi hilo hadi akina Mama Baruti walipomaliza kuchota maji na kuingia ndani. Na hapo ndipo alipopata utulivu. Akatoka nje na kufungua geti, na punde Baba Kamau aliingia na kunipita sebuleni kama mshale–akipitiliza moja kwa moja chumbani kwa mama.

Kwa sababu nilikuwa nimeshakula na kuoga, mama alinichukua na kunipeleka chumbani kwangu kulala. Alinitandikia kitanda na kuniwekea chandarua kama ilivyo kawaida. Akanifunika shuka miguuni kisha akatoka na kwenda chumbani kwake. Haikuchukua muda mrefu nilianza kuisikia tena ile sauti ya nyani mtoto.

Unaweza kumwona mama yangu ni shetani, lakini mimi nikamwona ni malaika. Uzuri ni kwamba sote hatuko sawa. Mama yangu si shetani wala malaika. Ni mwanadamu kama mama yako…kama bado hujapata kumsikia sauti yake usiku, hilo si kosa langu. Ni kosa lako kulala kama pono.

Kila siku ya Jumapili, mama alikuwa na utaratibu wa kunipeleka saluni. Na ilitokea mara kadhaa alipokosa pesa, alipitisha hata mwezi mzima bila kunipeleka saluni. Siku hiyo, mama aliamka mapema na kufanya usafi wa nyumba pamoja na kuniogesha. Alinivisha viatu vya Kimasai pamoja na gauni la waridi lenye maua kwenye pindo la shingo na mikononi. Yeye alivalia sketi fupi ya kaki pamoja na blauzi ya rangi ya malai. Miguuni alivaa mokasini nyeusi zenye soli fupi bila soksi. Hereni pamoja bangili alizovaa vilirandana rangi pamoja na ukubwa. Kwa namna mwili wake ulivyokuwa, haikujalisha angevaa nini, lazima angependeza tu. Alikuwa mwembaba lakini si kimbaumbau. Umbo namba nane lililofunikwa na ngozi nyeusi na laini, vilifanya vijana wengi kugeuka kila alipokatiza.

Kutokana na jua kali la Dar es Salaam, mama yangu hakudiriki kutembea bila mwamvuli. Alidai kuwa, jua kali husababisha ngozi kubabuka na kukaribisha makunyanzi. Siku hiyo pia, alibeba mwamvuli mkubwa ambao aliukunjua tulipoingia tu barabarani. Saluni haikuwa mbali kwa kutokea nyumbani kwetu. Ni kituo kama cha tano hivi kwa usafiri wa Daladala.

Karume ni mahali penye watu wengi na msongamano wa magari licha ya kuwa na barabara pana. Nje ya maduka, bidhaa anuai zilining’inizwa kwenye milango. Vinyago vya watu vilivyovishwa mavazi ya mitindo mbali mbali vilipamba milango ya maduka ya nguo yaliyotazama barabarani.

Amanda aliyekuwa nje ya saluni yake, mkabala na Uwanja wa Karume, akimwosha nywele msichana mmoja mwembamba, alituona tukifika. “Oh, Maya. Karibu shoga yangu,” alisema, akimlaki mama yangu. Alivalia dera la rangi ya njano na weusi, pamoja kilemba cha rangi hiyo hiyo.

“Asante shoga yangu,” mama alijibu, akisimama mlangoni karibu na Amanda.

“Shikamoo,” nilimsabahi nikiwa nimesimama nyuma ya mama.

“Marahaba, Chiku. Eer jamani gauni limekupendeza!”

Nilitabasamu na kumtazama mama. “Asante,” nilisema.

Nilimzoea na kumpenda sana Amanda, si tu kwa sababu ndiye msusi wangu bali kwa sababu alipenda kusifia nguo zangu, nywele zangu na kila kitu changu. Alijua kucheza vema na akili yangu, na pengine akili ya kila mtoto, kwa sababu watoto wote hupenda kushajiishwa kwa maneno mazuri na kupambiwa.

Miongoni mwa mambo yaliyozitafuna pesa za mama yangu ni pamoja na nywele zangu. Alizipenda na kuzitunza kama madini. Pamoja na kunipeleka saluni kila alipopata pesa, bado alihakikisha makopo ya mafuta ya nywele hayakauki nyumbani. Alikuwa tayari kuongeza mafuta ya nywele ndani hata kama yaliyopo bado hayajaisha, badala ya kuninunulia vitabu vya kujifunza kusoma na kuandika. Ni kama alithamini zaidi nywele kuliko ubongo.

Tulimwacha Amanda akiendelea kumwosha nywele yule msichana. Tulipoingia saluni tulimkuta mwanamke mmoja mweusi na mfupi, akijitazama kwenye kioo. Matiti yake makubwa yalituna ndani ya fulana yake nyeupe. Hakuwa mzuri sana lakini alikuwa na mvuto. Na kwa namna alivyojibidiisha kujiremba, angeweza kukamata nadhari ya mwanaume yeyote.

“Aah Bupe,” mama alimsemesha, “mambo vipi!”

“Poa Maya, karibu,” Bupe alijibu huku akiendelea kujitumbua chunusi kwenye kioo. Sikuipenda sauti yake hata kidogo. Ilijaa mawimbi na mitetemo mfano wa mtu anayejiandaa kulia–na ilikwaruza mithili ya punda mwenye pumu.

“Asante,” mama alisema, akienda kuketi kwenye kochi. Nami nikaketi pembeni yake. “Habari za kupoteana!”

“Nzuri shoga’angu, japo we ndo umepotea,” alijibu huku akigeuka kututazama. Chunusi zilimchachamaa kwenye paji la uso kama nyota ziuzungukavyo mwezi mwandamo. “Sisi wenziyo hazipiti siku mbili tuko hapa.”

“Pilika tu ndugu yangu. Lakini maadamu tunakutana tukiwa wazima kama hivi tunamshukuru Mungu.”

“Jamani una mtoto mzuri, Mayasa,” Bupe alisema, akitabasamu na kuniangalia. Meno yake ya mbele yalituna na kutaka kutokeza nje ya kinywa chake. Kila alipoufumba mdomo ulikuwa kama pochi iliyojaa vitu–na kila alipouacha wazi alionekana kama mwenye uchu wa nyama. “Ni mtoto wako huyu?”

Mama alijibu hali ametabasamu. “Ndiyo. Ni wangu. Anaitwa Chiku.”

“Shikamoo,” nilimsalimu kabla sijaambiwa.

“Oh, kumbe we’ ni mama Chiku,” Bupe alimwambia mama. “Marahaba mtoto mzuri,” aliniitikia salamu, akigeuza uso kunitazama. “Jamani watoto wa kike hadi raha. Natamani sana mtoto wa kike.”

“Mtoto ni mtoto tu bwana,” mama alijibu. “Watoto wote ni sawa.”

“Watoto wa kike ni watulivu zaidi. Hawana makeke mengi kama wa kiume. Si unaona tangu umefika yuko ubavuni tu,” Bupe alisema. “Lakini wa kwangu sasa.. yaani tulipofika tu, hakumaliza hata dakika tano akatoka nje kwenda kucheza.”

Bupe alitoka nje kumfuata huyo mtoto wake, akituacha tunamtazama sehemu ya nyuma. Ama kweli Mungu hakunyimi vyote. Licha ya meno yake pamoja na chunusi kumpunguzia alama katika urembo, lakini umbo lake lilikuwa ni habari nyingine. Alikuwa na tumbo jembamba mithili ya nyoka, kiuno kilichojibinua kama dondora, huku sehemu ya nyuma ikijiviringa Kibantu.

Yule msichana aliyekuwa akioshwa nywele nje alirejea ndani na kuketi. Alikuwa na nywele nyingi na macho makubwa kama Kangaroo. Kama kuna mtu mwembamba nimepata kumwona duniani basi ni huyu. Wanasema alikuwa akijikondesha kwa ajili ya maandalizi ya kuwania taji la Miss Tanzania. Kama Miss Tanzania anatakiwa kuwa mwembamba kiasi hiki, nilijisemea mwenyewe, basi huyo Miss World atakuwa kama unyoya wa ndege tausi.

Bupe alirejea na mwanaye. Alikuwa amevaa fulana nyeusi na jinzi ya buluu. Hakuwa mweusi kama mama yake japo hakuwa mweupe kama baba yangu. Na laiti isingelikuwa yale matege yake, bila shaka angelikuwa mrefu kunipita hata mimi. Nilichoshukuru Mungu hakuwa na sauti mbaya kama ya mama yake.

“Huoni hata aibu kufika tu na kuzurura nje! Angalia mwenzako alivyotulia pale. Haya kamsalimie ma’mkubwa kisha ukakae pale na mwenzako utulie,” Bupe alimwambia mwanaye.

“Shikamoo ma’mkubwa,” alimsalimu mama.

“Marahaba mwanangu,” mama alijibu huku akimshika mkono. “Unaitwa nani?”

“Naitwa Dakota Alfred Kolikoli.”

Amanda na yule kimbaumbau mwenye macho ya Kangaroo walicheka kwa pamoja. Ni kama walishajua namna Dakota atakavyojitambulisha.

“Wacha we! Ni mwendo wa full name kabisa,” mama alisema huku akimpapasa kichwani. “Safi sana. Haya kaa hapo na Chiku.”

“Mwenyewe anajivunia mno umaarufu wa baba yake,” Bupe alisema huku akitabasamu. Dakota alikuja kuketi karibu yangu, tukaangaliana na kutabasamiana kisha akainamisha kichwa chini. Alionekana mpole na mwenye aibu.

“Kwani baba yake ni Alfred Kolikoli huyu aliyekuwa mcheza mpira wa timu ya Milambo?”

“Ndiye huyo huyo,” Bupe alijibu huku ametabasamu. Ilivyoonekana yeye pia alikuwa akijivunia kuzaa na huyo mcheza mpira. “Kumbe nawe ni mfuatiliaji wa mpira?”

“Aah, si sana. Ni kwa vile tu Milambo ni timu ya mkoani kwetu ndo maana nawajua baadhi ya wachezaji wake.”

“Kwani nawe ni mtu wa Tabora?”

“Ndiyo, japo si Tabora Mjini. Natokea wilayani Urambo.”

“Miye nimekulia Tabora mjini, maeneo ya Minazi Mikinda, ingawaje hata Urambo nimeishi pia. Nilikuwa nakwenda kumtembelea mjomba wangu.”

“Basi hapo mmeshakutana watoto wa Tabora,” Amanda alisema. “Mtaanza kututeta Kinyamwezi humu ndani.”

“Mbona mtajuta,” Bupe alisema.

Wote wakacheka.

“Halafu unajua kama Maya anaishi Buguruni pia?” Amanda alimwambia Bupe.

“We usiniambie,” Bupe alisema akimtazama Amanda kabla ya kurudisha macho kwa mama. “Mimi pia naishi Buguruni.”

Mama alimwelekeza Bupe nyumba tunayoishi na Bupe akaahidi kuja kututembelea. Amanda alipomaliza kumhudumia yule msichana, nikaingia mimi kusuka.

“Hivi Alfred Kolikoli yuko wapi siku hizi?” mama alimwuliza Bupe. “Bado anacheza mpira tu?”

“Na pombe amwachie nani?” Bupe alijibu huku akibetua mdomo juu. “Yuko kwao huko Mara.”
*****

Karibu kila siku Baba Kamau alikuja nyumbani. Japo sikuweza kumzoea kwa sababu kila alipokuja alipitiliza moja kwa moja chumbani kwa mama – na baada ya saa chache za kujifungia chumbani angelitoka na kuondoka. Mara kadhaa alipokuwa akitoka safarini usiku angeanzia nyumbani kwetu, akituletea vitu vya ndani kama mchele, maharage, mikungu ya ndizi, mkaa, nk. Na wakati mwingine angelala hadi alfajiri ambapo angechomoka kimya kimya na kurejea nyumbani kwake kana kwamba ndiyo ameingia asubuhi hiyo toka safarini. Tangu baba Kamau alipoingia maishani mwetu, njaa iligeuka na kuwa ni msamiati wa Kichina. Hata ile sura yake niliyodhani ni mbaya, taratibu nikaanza kuhisi kuwa ni nzuri.

Siku moja, mimi na Sandra tukiwa tunacheza nje ya geti, tulimwona Mama Kamau akitoka shuleni. Kama ilivyo ada tulijiandaa kumsalimu kwa bashasha. Kwa bahati, alipotukaribia akahamia upande wa pili wa barabara, akiwa na mwelekeo wa kuja nyumbani kwetu. Aghalabu, alikuwa akija nyumbani kwetu siku ya Jumapili atokapo kanisani na mara chache Jumamosi, lakini siku hiyo, alikuja katikati ya siku za kazi.

“Shikamoo Mwalimu!” Tulimsalimu kwa pamoja.

“Marahaba, Sandra, hujambo?” alijibu huku akifungua geti na kuingia ndani.

Nilijihisi unyonge kuona sote tumemsalimu lakini amemwitikia Sandra peke yake. Si kwamba hakunifahamu, la hasha. Alinifahamu kwa sura na jina. Na si kwamba hakunisikia, nina hakika alinisikia kwa sababu sauti yangu ilikuwa juu zaidi kuliko ya Sandra. Sikukubali kushindwa, nikarudia tena, “Shikamoo Mwalimu!”

Sikujua kama masikio yake yaliamua kutokunisikia au ni mdomo wake ndiyo ulichagua kutokunijibu. Aligeuka kana kwamba alitaka kumjua aliyesalimia. Kisha akasema, “Sandra, mama yako yupo ndani?”

“Ndiyo, yupo.”

Bila kuongeza neno, aliendelea kutembea na kupotelea ndani. Sandra alirukaruka kwa furaha ya kuongea na mama Kamau. Mimi nilikwenda kuchutama pembezoni mwa geti na kuanza kulia. Kwangu lile lilikuwa ni shambulio la fedheha. Sandra akanifuata na kunibembeleza. Raha yote iliniisha. Tukabaki tumeketi chini bila kucheza wala kuzungumza. Baada ya muda mrefu kupita, bila mama Kamau kutoka, Sandra akaniambia tumfuate ndani nikamsalimu tena. Nikaafiki.

Mama Baruti aliketi sakafuni huku ameegemea kochi kubwa lililokuwa upande wa kushoto. Mama Kamau aliketi kwenye kochi dogo lilokuwa upande wa kulia. Japo walikuwa wamezama kwenye mazungumzo lakini tulipotokeza tu, wote waligeuka mlangoni. Sandra ndiye alianza kuingia na kwenda kuketi kwenye meza ya chakula. “Chiku, haya nenda kwanza kwa mama, mtacheza baadaye,” Mama Baruti aliniambia kabla sijaingia. Alinifukuza kwa lugha laini.

*****Nini kinafukuta baina ya Mama Kamau na Mama Chiku? Je, Umejifunza chochote kuhusu maisha ya mtaani kwa wazazi wa kipato cha chini yanavyoathiri malezi ya watoto? TUKUTANE TENA KESHO, saa kumi na mbili na nusu jioni ili kuona hilo Jeneza la Taifa litakwenda kutumika kumzika nani?
 
JENEZA LA TAIFA: Sura ya pili

*****TULIPOISHIA JANA…
Mama Baruti aliketi sakafuni huku ameegemea kochi kubwa lililokuwa upande wa kushoto. Mama Kamau aliketi kwenye kochi dogo lilokuwa upande wa kulia. Japo walikuwa wamezama kwenye mazungumzo lakini tulipotokeza tu, wote waligeuka mlangoni. Sandra ndiye alianza kuingia na kwenda kuketi kwenye meza ya chakula. “Chiku, haya nenda kwanza kwa mama, mtacheza baadaye,” Mama Baruti aliniambia kabla sijaingia. Alinifukuza kwa lugha laini.

ENDELEA...

Niliondoka kichwa chini mikono nyuma. Moja kwa moja nikaingia ndani kwetu na kumkuta mama yangu amelala sakafuni. Nikalala pembeni yake bila kumwamsha. Sikutoka tena nje kucheza. Sikumbuki Mama Kamau aliondoka muda gani, lakini nachokumbuka, kuanzia siku hiyo, ukaribu wa Mama Baruti na mama yangu ulianza kupungua. Sandra akakata mguu ndani mwetu. Yumkini alikatazwa na mama yake. Siku kadhaa mbele, mama yangu naye akanikataza kuingia ndani kwa Mama Baruti.

Tangu kutokea kwa sintofahamu hiyo, Baba Kamau alikuja nyumbani mara moja tu. Baada ya hapo naye alikwenda kama zilivyokwenda nzige. Haikuchukua muda mrefu, pengo lake likaanza kuonekana. Suala la kunywa chai bila vitafunwa na wakati mwingine kulala bila kula likawa la kawaida mno. Maisha yakaanza kutupiga kila aina ya mpigo. Tulipoelemewa zaidi, mama alikimbilia dukani kwa Mangi kukopa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya chakula, lakini sikumbuki kumwona akienda kulipa madeni hata mara moja.

Siku moja usiku, Mangi alikuja nyumbani na kumkuta mama ameketi nje ya mlango wa kuingilia ndani. Mama alipomwona alitahayari. “Karibu, Mangi,” alisema.

“Nimekuja kuchukua pesa yangu.”

“Mmh Mangi… hata salamu kaka yangu!” mama alisema, akiangaza huku na kule kuhakiki kama kuna mtu anayewaona.

“Nimefuata pesa yangu, sikufuata salamu. Nakuheshimu sana Mama Chiku. Tafadhali usitake nikudhalilishe mbele za watu.”

“Mbona huwa nakulipa bila usumbufu, Mangi,” mama alisema akiwa ameshasawajika uso. “Nimekwama kidogo tu siku mbili-tatu hizi. Kuna pesa nategemea kupata kesho. Nitakulipa kaka yangu.”

Mangi alimtazama mama bila kupepesa macho. “Ikifika mpaka kesho saa nne usiku sijapata pesa yangu,” alisema huku akianza kuondoka, “usitegemee kama nitarudi tena kistaarabu hapa.” Akaondoka bila kuaga. Japo hapakuwa na mtu mwingine hapo uwani kushuhudia sintofahamu hiyo, lakini uso wa mama ulifadhaika mno. Aliganda pale kwenye kigoda kama anayesubiri kung’olewa jino.

Mangi alikuja tena nyumbani ikiwa ni siku ya tatu tangu alipokuja mara ya mwisho. Ilikuwa ni majira ya saa nne usiku. Nakumbuka mama alikuwa nje muda mrefu wakati mimi nikiwa sebuleni. Ghafla alirejea akiwa na Mangi na moja kwa moja wakaelekea chumbani. “Haya ukalale mama, nina mazungumzo na mgeni chumbani,” mama aliniambia baada ya kutoka chumbani.
*****

Bupe alikuja nyumbani takribani wiki mbili tangu tulipoona kule saluni. Mama alimlaki na kumkaribisha ndani. Samani zetu zilikuwa chache lakini zilionekana nyingi kutokana na ufinyu wa sebule. Upande wa kulia, mkabala na chumba changu, palikuwa na kochi la watu watatu; upande wa kushoto, palikuwa na makochi madogo mawili ya mtu mmoja mmoja. Makochi yote matatu yalikuwa na mito iliyovishwa foronya za rangi ya kahawia; katikati palikuwa na meza ndogo ya mbao iliyofunikwa kitambaa cha kufuma kwa mkono; mwishoni kabisa mwa sebule, mlango wa chumba cha mama ulikuwa ukitazama sebuleni – pembeni ya mlango huo, palikuwa na kabati refu la mninga kwa ajili ya vyombo. Juu hapakuwa na dari lakini chini palisakafiwa kwa saruji ya kuteleza.

Bupe na mama waliketi kwenye kochi kubwa, wakati mimi nikijilaza kwenye kochi dogo. Mama alimwelezea Bupe hali ngumu ya kiuchumi anayopitia. “Suala la kukosa hata chakula limekuwa kawaida kwangu. Kuna wakati niliamua kufanya biashara ya kuuza maandazi. Nikawa napika na kuyaweka hapo getini. Biashara ilianza kuchanganya vizuri kabla ya siku moja asubuhi, nikiwa nimeacha nje dumu la maandazi na kwenda ndani kuchukua magazeti ya kufungia, wajanja wakapita na dumu lote.”

Bupe aliangua kicheko, akisema, “Naona siku hiyo walifanya Sikukuu ya Maandazi.”

“Yaani badala unipe hata pole, we unanicheka!” mama alisema. “Yaani siku hiyo nililia kama mtoto. Tangu hapo sikuweza tena kupata mtaji mwingine wa maandazi.”

“Ndo ukubwa huo ndugu yangu,” Bupe alisema. “Kwahiyo sasa unaishi vipi na mtoto?”

“Nabangaiza tu mwenzangu. Kuna wakati nilipata bwana, ni dereva wa magari makubwa, sijui kama unamjua, anaitwa Baba Kamau.”

“Baba Kamau,” Bupe alisema na kuangua kicheko kingine cha haja. “Yule Mkongomani mla watu?”

“Siyo Mkongomani bwana. Anaendesha tu magari yaendayo Kongo. Ni Mtanzania japo nasikia ana asili ya Kenya.”

“Wanasema huwa anafadhili vikundi vya vibaka na majambazi. Kuwa naye makini.”

“Kwani hata niko naye tena? Alishakata Kamba,” mama alisema. “Nahisi kuna siku Mama Baruti alimwona akiingia humu kwangu, akaenda kumwambia mkewe. Tangu hapo yule bwana akanipiga kadi nyekundu.”

“Hata hivyo una moyo. Mimi nisingeweza kulala kitanda kimoja na mwanaume wa namna ile? Yale mapua yake, yale macho yake, kile kitambi, Mungu wangu ningetapika. Sasa inabidi usimame mwenyewe kujipambania.”

“Kwa namna shida zilivyonifika hapa,” mama alisema, akijigusa shingoni kwa ncha za vidole, “niko tayari kuuza chochote–hata damu yangu, ikiwa utakubali kuinunua.”

“Kama kweli uko tayari kuuza chochote, usikae tena kizembe. Pambana huku na kule. Mwenye mashavu mawili haunguzwi na uji,” Bupe alisema, huku akitingisha kichwa na kuzungusha macho mithili ya mtoto mwenye degedege, kiasi kwamba ilimchukua muda mama yangu kuling’amua fumbo lile.

“Unamaanisha nini?”

“Uji ukianza kukuunguza shavu la kushoto unauhamishia shavu la kulia. Na la kulia likichemka unaurudisha kushoto, mpaka unaumeza.”

Mama yangu alimtazama Bupe lile jicho la unataka kusema nini?

“Asiyejua maana haambiwi maana,” Bupe alisema na kucheka tena. “Hivi kwanza una umri gani, Maya?”

Mama aliguna na kusema, “Miaka ishirini na moja.”

“Uuwi!” Bupe alipiga ukunga. Akanigeukia kwenye kochi nilipokuwa nimejilaza. “Chiku mwanangu, kuanzia leo usiwe unaniita mama mdogo, sawa? Ni mama mkubwa. Umesikia?”

Nikatikisa kichwa kukubali.

Mama alicheka huku akitikisa kichwa.

Bupe akasema, “Mimi nina miaka ishirini na tatu.”

“Kwa namna ulivyojifaragua nidhani umenizidi hata miaka tisa, kumbe miwili tu.”

“Hata kama ni siku moja tu, Maya. Unakuwa mdogo wangu,” alisema akicheka. “Haya sasa nisikilize kwa makini, mdogo’angu. Hata nisipokwambia leo, iko siku utajua tu. Hiyo hali yako unayosema ni mbaya kiuchumi, si mbaya kuliko ilivyokuwa ya kwangu. Tofauti yetu ni moja tu; unachokitoa wewe kwa wanaume ili wakupatie msaada wa pesa, mimi nakitoa kwa makubaliano ya malipo rasmi. Kwa nini? Kwa sababu siwezi kusubiri fadhila za mtu kwenye mwili wangu.”

“Malipo rasmi?” mama aliuliza. “Kwamba unajiuza? Unafanya ukahaba?”

“Ukahaba ni neno gumu mno. Tuseme ni huduma ya kimwili. Analipa pesa, namhudumia.”

“Mungu wangu,” mama alisema. “Hapana, Bupe. Kujiuza ni Big No kwangu.”

“Mbona hapo ulipo tayari unajiuza, Maya. Hao wanaume wanaokusaidia pesa huwa unawapa nini?” Bupe alisema kwa sauti ya chini huku ametabasamu. “Nd’o maana nilikuuliza umri wako. Bado una utoto mwingi, Maya.”

“Kujiuza? Hiyo biashara ni kosa kisheria. Na ukikamat...”

“Kosa ni lipi hapo? Kuupa raha mwili wangu kwa kutumia mwili wa mtu mwingine au kumpa raha mtu mwingine kwa kutumia mwili wangu? Hiyo Serikali inateseka nini mimi nikitumia mwili wangu kutatua shida zangu?”

“Ni makosa kisheria kwa sababu inahatarisha afya yako na ya hao wateja wako juu ya magonjwa ya zinaa. Pia, unash…”

“Unadhani hayo magonjwa ya zinaa yanajua kutofautisha kati yenu nyie mnaofanya kwa kutegemea malipo ya hisani na siye tulioji-rasimisha? Tena basi nikwambie, sisi mnaotuita makahaba ndiyo tunazingatia mno kanuni za afya kuliko ninyi. Sisi kwetu hakuna tendo bila kinga. Upo hapo?”

“Bupe,” mama alisema kwa upole. “Ukahaba unashusha heshima. Ni kinyume cha maadili na utamaduni wetu.”

“Utamaduni wenu akina nani? Sikiliza Maya, jamii zote za kale zilizoturithisha ustaarabu na maadili, hazikukichukulia kitendo hiki kuwa ni jinai au utovu wa maadili, bali walikiheshimu kama ni kitendo cha burudani. Ni mchakato wa kimwili kama vile kushikana mikono au kusukana nywele.”

“Achana na hizo jamii zako za kale, Bupe. Sheria za hapa kwetu haiziruhusu. Na ukikamatwa utakwenda kuozea jela.”

“Nikamatwe na nani? Ingekuwa rahisi kihivyo basi shughuli hizi zingeshatoweka. Ngoja nikwambie kitu, Maya. Ukahaba ulikuwepo duniani tangu mwanadamu alivyoanza kuwepo, na kwa hivyo utaendelea kuwepo kadri mwanadamu atakavyokuwepo. Kama mitume, wakoloni, na kila aina ya watawala wa dunia walishindwa kuutokomeza, usitegemee kuna siku hao maaskari wako watautokomeza. Kwanza hao maaskari ndo wateja wetu wakubwa.”

“Pamoja na yote, lakini hiyo si kazi ya heshima, mpenzi. Ni kuuza utu wako tu.”

“Si kazi ya heshima, ndiyo. Ni kuuza utu wangu, ndiyo. Lakini je, wewe una kazi gani hapo ulipo? Hujui kuwa kazi ndiyo kipimo cha utu? Nani atakuheshimu kama huna hata hela ya kula? Uko wapi huo utu wako kama unadhalilishwa mpaka na akina Mangi kwa sababu ya madeni? Amka shoga yangu. Hata mimi sifanyi kazi hii kwa kupenda bali nafanya ili niishi. Nawe pia unaweza kufanya kwa malengo–na si kama kazi rasmi. Mara moja moja unapokwama kiuchumi na kukosa nyenzo ya kukukwamua ndipo unajiongeza.”

Kilipita kimya cha sekunde kadhaa kabla mama hajafungua tena kinywa chake. “Bupe, hivi uliishia kidato cha ngapi?”

“Cha nne.”

“Nikuombe jambo moja,” mama alisema. “Achana na ukahaba na urudi shule.”

“Sasa hayo ni maombi mawili. Kurudi shule na kuacha ukahaba, huoni kama hayo ni maombi mawili tofauti?” Bupe alijibu na kucheka. “Ningekubali kurudi shule endapo kungekuwa na kozi ya kusomea ukahaba.”

Mama alicheka na kutikisa kichwa. “Hauko mbali sana na pendekezo langu. Kasomee sheria ili uje kuwa wakili. Kwa kuwa una uwezo mkubwa wa kujieleza na kujitetea, ukiwa mwanasheria, makahaba watakuwa wanakulipa ukawatetee mahakamani. Hapo utakuwa unakula hela za ukahaba bila kufanya ukahaba.”

Ikawa zamu ya Bupe kucheka.

“Sasa Maya, mimi nakukimbia shoga yangu,” Bupe alisema, akisimama na kufungua pochi yake. Akatoa noti mbili na kumpatia mama. “Hizi utamnunulia Chiku chochote kitu – asilale na njaa.”

“Asante sana, Bupe. Nashukuru sana,” mama yangu alisema huku akisimama na kupokea pesa. “Mungu akubariki. Umenifaa mno leo.”

Sikujua ni kiasi gani alichopewa, lakini kwa namna alivyoshukuru ni dhahiri kama hakikuwa kikubwa sana basi mama alikuwa ameishiwa hadi senti ya mwisho.
_____

*****ITAENDELEA kesho saa 12:30 jioni. Mtunzi ni Maundu Mwingizi.
 
JENEZA LA TAIFA (Sura ya tatu)
Mtunzi: Maundu Mwingizi

Dar es Salaam ni moja kati ya miji yenye joto kali mno nchini Tanzania. Ni kawaida kukuta watu wametandika mikeka na kuketi nje ya nyumba zao wakati wa mchana utadhani kuna shughuli maalumu. Mama yangu hakupendelea sana kukaa nje licha ya joto kali, lakini siku hiyo, nasi tulitoka nje si tu kwa ajili ya kupunga upepo, bali pia kuaangalia makundi ya wananchi yakipita kuelekea viwanjani kushangilia–si kusikiliza–hotuba ya Mgombea Urais. Hiyo ilikuwa ni takribani miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 1995.

Majira ya saa kumi na mbili jioni, tukiwa tumeketi kibarazani, ilikuja teksi na kuegesha nje ya nyumba yetu. Mama akasema, “Enhe rafiki yako huyo.”

Nilifuata uelekeo wa macho ya mama yaliyokuwa yamekita kwenye teksi. Baruti alifungua mlango na kushuka akiwa amebeba begi mkononi. Alivalia traki suti ya buluu na raba nyeupe. Nilimgeukia mama hali ya kuwa nimetabasamu kisha nikarudisha tena macho kwa Baruti.

Nilimpenda sana Baruti, naye alinipenda pia. Nilipokuwa mdogo ni Baruti ndiye aliyekuwa akinibeba na kunibembeleza nilipokuwa nikilia. Hata katika nyakati ngumu kiuchumi, alikuwa akinifuata kila unapotimu muda wa chakula ndani kwao ili nikale pamoja nao, na wakati mwingine alinibebea chakula na kuniletea ndani kwetu.

Awali tulikuwa tukiishi na Baruti nyumba moja hadi baba yake mzazi alipomchukua na kumhamishia Arusha. Kuhamishiwa kwake Arusha kulisababishwa na utundu pamoja na utukutu wake kufurutu ada. Hakukaukiwa matukio hata siku moja. Mfano, siku moja yeye na marafiki zake, walichukua upupu na kwenda kuupakaza kwenye nguo za ndani za akina mama maeneo ya Buguruni Malapa, zilizokuwa zimeanikwa kambani. Usiniulize kuhusu kizaazaa kilichojiri hapo, jaribu tu kutafakari kiwango hicho cha utundu wake. Majirani walishukuru alipohamishwa. Tangu hapo, kumwona ikawa ni mpaka wakati wa likizo–mara mbili au tatu kwa mwaka.

Teksi ilipoondoka, Baruti alivuka na kuja usawa wetu. Nilimkimbilia kwenda kumpokea. Wakati huo alikuwa darasa la tano. Miaka yake 12 kama si 13; mfupi, maji ya kunde, na mwenye nywele nadhifu zilizokatwa kwa usawa. Alisogea hadi mahali alipoketi mama yangu na kumsalimu, “Shikamoo, mama Chiku.”

“Marahaba, Baruti. Habari za safari?”

“Nzuri.”

“Haya karibu,” mama alisema huku akinitazama. “Naona rafiki yako amefurahi.”

Baruti akiwa ametabasamu, alizungusha yale macho yake makubwa ya duara toka kwa mama hadi kwangu. “Asante,” alisema.

Bupe aliwasili punde baada ya Baruti kuingia ndani. Alivaa gauni refu la kahawia lililomkamata vilivyo maungoni. Kichwani alijifunga kitambaa cha rangi ya kijani na njano chenye picha ya mgombea Urais. “Unatoka wapi na jua lote hili, mtoto wa kike,” mama alisema.

“Mwezangu,” Bupe alijibu na kujibwaga kibarazani. “Leo tangu asubuhi tumeshinda Ofisi ya Mtendaji Kata, kuna dili la mawakala kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Nasikia wanalipa vizuri sana japo kupata hiyo nafasi ndiyo patashika.”

“Miye mwenzenu hayo mambo ya siasa…sijui ni uchaguzi huwa hata siyaelewi. Hebu nami unipachike huko kwenye hu uwakala nipate chochote.”

“Kama mambo ya siasa huyawezi, utauwezaje uwakala?” Bupe alisema. Kabla mama hajajibu, akapita bwana mmoja anaendesha baiskeli na Bupe akapaza sauti kumwita, “Kasongo! Kasongo! Ina maana hutuoni au dharau?”

“Aah, sikukuona, Bupe,” Kasongo alijibu baada ya kugeka na kututazama.

“Aah sio vizuri hivyo.” Sauti ya Bupe alikwangua mithili ya kuku aliyemeza chura. “Njoo kwanza nikutambulishe kwa mtu wa kwenu hapa.”

Kasongo aligeuza baiskeli na kutufuata hadi tulipokuwa tumeketi. Shati lake la mikono mirefu alilichomekea kwenye suruali na kuipandisha mpaka juu ya kitovu. Namna alivyozichonga ndevu zake mduara – kuzunguka mdomo, pamoja na namna miwani mikubwa ilivyofunika macho yake alikuwa mfano wa mwanamuziki wa bolingo.

“Jamani hamjambo?” alisalimia huku akiiweka vizuri kamera yake aliyokuwa ameining’iniza shingoni.

“Salama. Karibu,” mama alijibu.

“Sijui kama mnafahamaniana,” Bupe alisema, akimtazama mama yangu. Alipoona mama hana dalili ya kumfahamu, akamgeukia Kasongo. “Huyu anaitwa Mayasa, ni mtu kutoka Urambo pia.”

“Oh, nashukuru kukufahamu,” Kasongo alijibu, akimtazama mama kwa bashasha. “Urambo sehemu gani?”

“Sehemu moja wanapaita Boma Village.”

“Boma Village kubwa. Ni maeneo gani pale?”

“Maeneo ya Tarafani pale. Nyumba kama ya pili toka kwenye kile kiji ghorofa cha Kapuya.”

“Nyumba ya pili unamaanisha kwa yule bi mkubwa mrefu mweusi–nadhani huwa anafanya kazi ya kufua?”

Bupe na mama walitazamana na kucheka kwa pamoja. “We kweli mwenyeji Urambo. Ndiyo hapo hapo. Na huyo bi mkubwa ndiye mama’angu.”

“Urambo iko kiganjani mwangu,” alisema kwa majigambo. “Hiyo mitaa nimepiga sana picha.”

Baada ya mawili-matatu, Kasongo aliaga na kuondoka, akiahidi kurejea siku nyingine kumsalimu mama. Kabla Kasongo hajafika mbali, Bupe naye alisimama na kuaga.

“Sasa unaniachaje shoga yangu? Tangu asubuhi sijauma kitu,” mama alisema kwa sauti ya chini.

“Kama nilivyokwambia, leo muda wangu wote umeteketea huko kwa Mtendaji,” Bupe alijibu. “Kama vipi uniibukie kwangu mishale ya saa mbili hivi, pengine nitakuwa nimeshadaka vichwa viwili-vitatu.”

Ilikuwa imeshatimu kumi na mbili jioni. Bupe alipoondoka nasi tuliingia ndani. Ilikuwa ni kawaida kila siku jioni, mama huwahi kufunga madirisha na kuwasha taa kabla mbu wa magharibi hawajavamia ndani.

Saa mbili juu ya alama tulikuwa njiani kuelekea kwa Bupe. Ni mtaa wa tatu, kusini magharibi mwa nyumbani kwetu, maarufu kama Buguruni Danguroni. Shughuli za eneo hilo ndizo zilitengeneza jina la Danguroni. Tuliingia mtaa wa kwanza kushoto. Ni kiji-mtaa chembamba kama uchochoro lakini kirefu kama barabara. Karibu nyumba zote za upande wa kushoto ziligeukia upande wa mtaa wa pili, hivyo hapakuwa na milango kwa nyuma. Upande wa kulia ndipo nyumba zilitazama mbele ya mtaa.

Baadhi ya milango ilikuwa imefungwa huku mingine ikiwa wazi. Milango iliyokuwa wazi Ilifunikwa pazia nyepesi zenye kuonesha ndani. Mwanga wa rangi nyekundu au kijani ulitoka kwenye kila chumba kama ishara ya kazi zifanyikazo humo. Wanawake wa namna mbalimbali waliketi nyuma ya mapazia na wengine kwa pembezoni mwa milango ya vyumba hivyo wakichungula nje kama ndege tunduni.

“Oya, niaje,” mwanamke mmoja mweupe na mnene, aliyekuwa ameketi mlangoni kwake, alimsemesha kijana aliyekuwa akipita mbele ya chumba chake. “Pita ndani, mwanaume.”

Yule kijana aliangaza huku na kule, kisha akakunja kona ya ghafla na kuingia moja kwa moja chumbani alikokaribishwa. Yule mwanamke mnene akasimama taratibu kama vile hakuna kilichotokea. Akanyanyua kistuli alichokuwa amekalia na kuingia nacho chumbani kisha akafunga mlango.

Tulipita eneo hilo taratibu na kusonga mbele. Karibu kila chumba kilikuwa kikifukizwa udi na kufanya moshi hafifu kuchomoza milangoni na madirishani, huku mtaa mzima ukinukia. Sikujua siri ya sayansi ile ya udi pamoja na taa za rangi, lakini nilihisi pengine ni ishara au kivutio kwa wateja.

Nyumba kama ya tano mbele, tukamwona Bupe ameketi kwenye kistuli nje ya chumba chake. Alivalia shimizi ya rangi ya pinki, iliyomwacha wazi karibu sehemu yote ya mabega na mgongo, na kuishia juu ya magoti. “Ningeshangaa kama mngepotea,” Bupe alisema baada ya kutuona.

“Hata kama ndo ushamba, si wa kupotea Buguruni,” mama alisema, huku akiketi kibarazani pembezoni mwa chumba cha Bupe. Nami nikaketi pembeni yake. Tukawa tumeuweka kati mlango wa chumba; Bupe kushoto, mimi na mama kulia.

Baada ya kujuliana hali, mama akasema, “Dakota yuko wapi?”

“Yuko hapo mbele tu, kuna duka la rejareja kwenye ile kona mliyoingilia, humo ndo huwa analala. Kuna rafiki yangu amepanga humo.”

Mtaa wa Danguroni ulikuwa mdogo na umejificha mno, lakini haukukaukiwa watu. Palikuwa na mchanganyiko wa pilika za wapita njia wa kawaida na wateja mahususi. Kwa mbele kidogo, upande wa kushoto, palikuwa na kundi la vijana wakicheza kamari. “Kwa hiyo hao vijana wote wanajua kuwa mnajiuza hapa?” mama aliuliza.

Bupe aliwatazama vijana wale na kucheka. “Mbona hata sisi tunajua kuwa wanacheza kamari japo ni makosa? Tena baadhi yao tunawaombea washinde kila siku kwa sababu ni wateja wetu, na hatuna noma nao.”

“Oh, Mungu wangu!” mama alisema, akishindwa kudhibiti mshangao wake. “Wateja wenu halafu asubuhi mnatazamanaje usoni?”

“Hapa mjini, Maya. Kila mmoja anafanya mambo yake bila kumwangalia mwenzake,” Bupe alijibu. “Japo ni kweli, ukitaka kufanya vizuri biashara hii, jiepushe kumhudumia mtu unayejuana naye au yeyote wa maeneo haya. Ni vizuri zaidi kama ukiwa unaishi maeneo mengine ili chumba cha huku kiwe ni kwa ajili ya kazi tu.”

“Kwani kwenye mtaa huu kila nyumba–au tuseme kila chumba–watu wanajiuza?”

“Hapana. Kuna wanaoishi na familia zao kawaida.”

“Wanawachukuliaje nyie mnaofanya kazi hii?”

“Kwa nini wajihusishe na mambo yasiyowahusu? Wao siyo wanaojiuza na wala siyo wanaonunua. Kila mmoja ana malengo yake kimaisha tofauti na mwingine, kwa hivyo, vyovyote watakavyotuchukulia ni juu yao. Maya, usifanye kitu kwa kuogopa watu watakuchuliaje. Hakuna atakayekuletea ugali nyumbani kw…”

Kabla hajafikisha neno lake mwisho, akatokea bwana mmoja mwembamba na mrefu. Alivalia suruali ya kitambaa na shati la mikono mirefu. Mkononi alishika gazeti. Alikuwa anatembea kwa kunyata kama paka, akigeuka huku na kule kama anayeoga nje. Bupe aliacha kuzungumza na kumtazama kwa uchu kama mvuvi aliyenasa samaki kwenye ndoano. “Pita ndani, mwanaume,” Bupe alimsemesha.

Mkono wa kulia alishika gazeti alilokuwa akijipigapiga nalo kwenye kiganja cha mkono wa kushoto huku akiangaza kulia na kushoto. Alipokunja kona ya ghafla, bila kusita wala kugeuka, alipita chumbani moja kwa moja. Bupe aliachia tabasamu la ushindi wakati mama yangu akiweka kiganja cha mkono mdomoni akijizuia kucheka. Walitazamana kama watoto waliotenda jambo lililokatazwa na wazazi.

“Kamalizane naye,” Bupe alisema na kumtazama mama usoni bila ya chembe ya mzaha, akimaanisha alichosema.

Mama alipigwa butwaa kana kwamba hakutegemea kukabidhiwa jukumu lile. Ni kweli hakuwa na dhamira ya kujiuza–au tuseme walau hakuwa amejiandaa kwa siku hiyo–lakini alikuwa amejiandaa kuchukua pesa toka kwa mtu anayejiuza. Ni kama alitegemea kupatiwa samaki na badala yake akapatiwa ndoano. Kukataa kwenda chumbani ilikuwa ni sawa na kumtusi Bupe. Kwamba, Bupe ndiye akawajibike kisha pesa aletewe yeye. Ulikuwa ni mtego uliomshinda kuutegua. Hivyo, akanyanyuka na kuingia chumbani, huku akiuvuta mlango nyuma yake.

Haikuchukua muda mama alifungua mlango na kujitokeza sehemu ya kiwiliwili chake. Akasema neno kwa sauti ya chini, sikuweza kulinasa. Bupe akamjibu, “Zimo humo kwenye droo ya kitanda. Hakikisha anavaa. Na akulipe pesa kwanza.”

Mama alirejea chumbani na kufunga mlango. Kwa mbali nilimsikia yule bwana akimwuliza mama, “Wewe ni mgeni eeh?”

Mama akasikika akijibu, “Nina kamba mguuni?”

Bupe alinitazama akitabasamu. Akanyanyuka na kunishika mkono. “Twende zetu dukani, mwanangu. Unapenda pipi eeh?”

Kuna mtoto asiyependa pipi? Kama yupo shauri yake. Mimi napenda pipi kuliko watoto wote duniani. Nikanyanyuka na kumfuata dukani.
_____

*****ITAENDELEA kesho saa 12:30 jioni. Kama kuna lolote ulilojifunza au kuburudishwa nalo usisite kuniandikia…
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…