Jenerali: Msekwa umeajiri wahuni wa kutosha, usifanye uhuni




Msekwa ameajiri wahuni wa kutosha, asifanye uhuni



Jenerali Ulimwengu
Agosti 11, 2010


KATIKA hali tuliyoishuhudia wakati wa kura za maoni ndani ya chama - tawala si rahisi kwa ye yote anayefuatilia masuala ya siasa za nchi hii kupuuza masuala yaliyojitokeza. Masuala haya ni mengi, na bila shaka tutaendelea kuyajadili kwa muda mrefu, lakini wiki tunaweza kuyagusia baadhi yake kabla hayajapoa.
Kwanza, kama nilivyosema wiki jana, siasa za chama-tawala kunyata. Mambo tuliyoyashuhudia katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM yanakifu, yanachusha, yanatia kinyaa.
Lakini ni zaidi ya hayo. Kuchusha pekee, ama kutia kinyaa, si jambo jema na wala si hali ya kupendeza. Mtu anaposema anaona kinyaa, labda athari kubwa inayoweza kumtokea ni kupata kichefuchefu na hatimaye kutapika. Kwa yale tuliyoyaona mwaka huu, si uongo kusema kwamba kama kuna watu miongoni mwetu ambao bado wana chembe za uungwana, wamepata kichefuchefu, na wengine labda walijisikia kutapika.
Lakini kichefuchefu si sawa na kifo, na hutokea mtu aliyekolewa na kichefuchefu akafikia hata hatua ya kutapika na bado asife iwapo kutapika kwake hakutokani na maradhi yaliyo mwilini mwake bali ni kutokana na kichefuchefu kinachotokana na hali ya kuudhiwa na kuwa na kinyaa. Binadamu wanao uwezo mkubwa wa kushuhudia mambo ya kuudhi na bado wasife kutokana nayo.
Hata hivyo, mambo hayo yanaudhi, yanakera. Isitoshe, baadhi ya yale tuliyoyashuhudia siyo tu yanaudhi, ila pia yanatisha. Yanatishia usalama wetu kama Taifa kwa sababu yanao uwezo wa kutupeleka mahali ambako hatukutarajia kwenda, mahali pa kutuhilikisha.
Niliwahi kueleza kwamba tumeanza kutumia lugha nyepesi kuelezea dhana nzito. Nimekuwa nikijaribu kueleza kwamba kile tunachokiita ‘kero’ mara nyingi si kero bali ni janga, ni hatari, ni saratani, ni ukoma. Rushwa, kama rushwa, ndani ya jamii haiwezi kuwa kero; ni janga kwa sababu inao uwezo wa kuua jamii nzima.
Lakini, pia, rushwa ni kielelezo kimojawapo cha uoza, na vielelezo vipo vingi. Katika michakato ya uchaguzi, ni kweli, tumeshuhudia vitendo vya rushwa, kwa maana ya watu kugawa fedha na wengine kupokea fedha hizo kwa madhumuni ya kuathiri matokeo ya uchaguzi. Hiyo ni rushwa kama ile anayotoa mtu mwenye shauri mahakamani kumpa hakimu, au mtu mwenye tatizo la kiusalama kumpa askari polisi.
Uoza wa aina hiyo umetokea sana katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama-tawala, na ni vyema kuukemea kwa nguvu zetu zote, na ni lazima kukataa na kutupilia mbali kauli za kipuuzi za watu kama wasemaji wa chama-tawala niliowasikia. Upuuzi ukisikika, tujifunze kuutaja kama upuuzi, na huu ni upuuzi.
Sasa, ndani ya chama-tawala wametokea wahuni waliohamia huko na kisha wakapewa kibarua cha kutoa matamko ya kipuuzi mara kwa mara, maneno yenye mantiki iliyopinda na isiyoweza kumshawishi hata mgonjwa wa Mirembe. Hawa wanajulikana, asili yao inaeleweka, na kwa maana hiyo hawashangazi wanapotoa matamko yasiyokuwa na mantiki yo yote ila tu kujaza nafasi katika vyombo vya habari kwa sababu ni muhimu kwa wanajamii kujua kwamba chama-tawala kimejibu shutuma hii au ile.
Lakini kwa kuwaendekeza wapuuzi kama hawa, na kuwazoea kama wasemaji wa mara kwa mara wa chama-tawala, ipo hatari kwamba hata watu wasiotarajiwa kutamka maneno ya kihuni kuingia katika mkumbo huo na kujisemea tu, alimradi wamesema. Mazoea huzaa hulka, na hulka huzaa utamaduni.
Ndivyo ninavyomwangalia Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa chama-tawala, na jinsi anavyozungumzia janga kubwa la uoza ndani ya chama chake. Msekwa anasema kwamba, na anataka tuamini kwamba tatizo la rushwa haliwezi kuwekwa mlangoni kwa chama chake, kwa sababu ni tatizo la Taifa zima.
Hapa kama kuna mtu amemwelea Msekwa, naomba anisaidie. Ni kweli tatizo la rushwa ni la Taifa zima, lakini kwa nini liseelekezwe kwa chama-tawala, chama ambacho, kama wanavyotamba wasemaji wake, ndicho kilichopewa dhamana ya kuongoza Taifa letu? Ni chama hicho kilichoomba, tena kwa nguvu za fedha na jeuri za aina nyingine, kipewe madaraka ya kuongoza nchi yetu, na hiyo dhamama kikapewa.
Sasa, kama nchi nzima imejaa rushwa, kama alivyoeleza Msekwa kwa ufasaha mkubwa, sisi tumwulize nani kama si chama hicho? Lakini labda Msekwa, kwa kuathirika kutokana na ule upuuzi ulioingizwa ndani ya chama chake na wale wahuni niliowataja mapema, alisahau kwamba alikuwa anaulizwa swali kuhusu chama chake.
Ni kweli, kama anavyosema Msekwa, rushwa iko polisi, iko mahakamani, iko hospitalini, iko vyuoni, iko kila mahali. Lakini ukweli huo hauwezi kuwafanya wadadisi wasimuulize Mkuu wa Polisi kuhusu rushwa katika jeshi lake, au wasimuulize Jaji Mkuu kuhusu rushwa katika mahakama zake, na kadhalika. Sijui Msekwa alitaka nani aulizwe kuhusu rushwa ya kutia kinyaa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chake. Tumwulize Waziri wa Afya?
Watu kama Msekwa wanatakiwa waache upuuzi kwani dhamana waliyo nayo ni kubwa mno, wakiendelea na upuuzi wao sote tutaathirika. Hii ndiyo sababu sichelei kumwambia Msekwa kwamba umri wake, uzoefu wake, historia yake, elimu yake na hadhi yake.. vyote hivi havimpi ruksa ya kuzungumza kihuni. Chama chake kimewapa ajira wahuni wengi ambao wanatosha kabisa kutuchekesha huku tukilia machozi.
Hata hivyo, najua kwamba uhuni huu ukiachiwa ukaendelea, siku moja hata hicho kicheko katikati ya machozi kitakatika, na kilio kitakuwa ni cha moja kwa moja. Msekwa anataka kutuambia kwamba hata udanganyifu wa viongozi na watumishi wa chama chake si tatizo la chama chake?
Kama Msekwa na wakuu wengine wa chama-tawala hawaoni kwamba uingizaji wa kadi bandia za uanachama katika michakato ya ndani ya chama hicho si tatizo la chama, ni nini wanachokiona? Hujuma kama hii ingefanywa na chama kingine kinachotaka kukidhoofisha chama-tawala, ingeeleweka. Kwamba watu ndani ya chama hicho wanakihujumu kwa makusudi kabisa halafu wakubwa wake hawaoni kwamba kuna tatizo, ni uthibitisho kamili kwamba nchi hii imo mikononi mwa watu wa kutisha.
Kumbukumbu zangu zinaniarifu kwamba mwaka 1977, katikati ya sherehe zilizotangulia muungano wa TANU na ASP kuunda CCM, Pius Msekwa alikuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM. Katika hafla mojawapo ya maadhimisho hayo, Msekwa alitoa tamko lililosema kwamba jina ‘Chama Cha Mapinduzi’ halikuwa na maana kwamba kila mwanachama wake angetakiwa kuwa mwanamapinduzi.
Hii bila shaka ilikuwa na maana kwamba mtu hakuhitaji kuamini itikadi yo yote ili kuwa mwananchama wa CCM. Lakini aliyekuwa rais wa ASP, Aboud Jumbe, alimkosoa Msekwa kwa kubainisha kwamba ili kuwa mwanachama wa chama kinachoitwa cha mapinduzi ni mantiki ya kawaida kwamba lazima mtu awe mwanamapinduzi. Leo nadhani kwamba mshindi katika ubishi huo wa miaka thelathini na tatu iliyopita ni Msekwa. Naamini ndiyo maana bado anakiongoza chama chake cha mapinduzi kisichokuwa na wanamapinduzi.
Hata kama tutakubali kwamba sisi sote tu vipofu, si tumsikilize Bwana Issa bin Maryam, aliyetufundisha kwa kuuliza swali hili: Je, kipofu anaweza kumwomgoza kipofu mwenziwe? Si wote watatumbukia katika shimo?
Itaendeelea.


 
Duuuuh

Hili liko wazi kabisa kuwa Ethics zima ya kura za maoni ni viongozi wa ngazi za juu CCM ndio kwa 100% walivuluga uchaguzi huu na lawama ziende kwao bira ubishi.

Kama Bilal alitoa mapendekezo na yakapelekwa NEC na sikuchache kabla ya uchaguzi makamba akabadili mpangilio wa uchaguzi na kujitamkia yake hapa si ndipo unapo pima elimu,uzefu wake katika siasa muda wote huo anashindwa soma alama za nyakati duuuh mbona haibu hiii

Nipelekeni chuo cha kuwa mwanamapinduzi na kuwa mzalendo, sijui ndio kile kilichokuwa kule UKEREWE Mrutunguru Chuo cha siasa, ambacho sasa kimekuwa secondary kweli CCM walianza poteza umapinduzi toka 90's
 
Asante sana jenerali unajua kutumia kalamu yako!

Ni kweli akitaka kutumia kalamu yake huitumia pale panapomhusu TingaTinga na huyu mwingine kwa sababu za kihistoria, lakini anapohusiswa EL kalamu ya Jenerali Twaha Ulimwengu huwa inakuwa butu!! Huu ni mtazamo wangu TU!!
 
Hivi nyinyi fundamentalists mkoje! Huo mwenendo wa Ulimwengu kumkashifu Yesu umeuona wapi? Na wapi aliposema amenukuu Biblia au Kuran Tukufu? Akikwambia huyo Bwana anayemzungumzia ni jirani yake utasema nini? Tusiwe defensive kupita kiasi. Hakuna baya alilolizungumza.

Amandla......
Ndugu Amandla, mimi naheshimu uhuru wa kutoa mawazo. Vilevile, naheshimu uhuru wako wa kupinga, kuunga mkono au kufafanua hoja mbalimbali. Lakini kushambulia mtu sio haki...hapo napingana. Umemshambulia Ntambaswala kwa kumwita fundamentalist... kwani yeye hana haki kama ya kwako ya kukosoa, kupinga au kufafanua?

Ukweli Jenerali kaandika hoja yake nzuri kwa hoja na mtiririko ili kila msomaji aweze kufuatana naye bila kujikwaa. Ntambaswala amejikwaa katika nukuu iliyotolewa. Kazi ya kusoma na kumfuatilia ikatibuka na aliyesababisha ni mwandishi mwenyewe. Ulimwengu amefeli katika sehemu hiyo ya nukuu. Sheria ya kunukuu inataka mwandishi yeyote kutumia jina sahihi na chanzo halisi (name and source of quotation should be indisputable) katika kufikisha hoja au ujumbe wake. Huwezi ku-justify kosa la mwandishi eti kwa vile kaandika mada nzuri lakini kakosea nukuu. Ile nukuu ina haki miliki na unaweza kudaiwa kisheria. Bahati mbaya nukuu iliyotumika ni jina linalogusa imani za watu...usiwalazimishe watu wote waneglect makosa ya nukuu ya jina la nabii wao. Hapo tusilete ubishi Generali arekebishe, vinginevyo ujumbe wake hautafika kwa baadhi ya wasomaji wake. Amefanya vizuri kulalamikia hali ya udhaifu unaojionesha kwa vingozi wetu, hilo ni vema. Sasa awe mwangalifu na yeye katika nukuu ya kazi za watu wengine na pia awatendee haki wasomaji wake wote.
 
Msekwa mtu ovyo kabisa, hii trick ya kusema "mbona fulani naye amefanya" is the oldest in the book. Two wrongs do not make a right.

Traffic cop akikusimamisha kwa sababu una speed (or for any other offence for that matter) huwezi kumwambia "mbona yule naye ana speed ?"

Swala si yule, swala ni wewe, sheria inaweza kushindwa kuwakamata wahalifu wote, lakini ikikukamata wewe, hata kama ni kwa ajili ya kutoa mfano tu, swali pekee lenye maana ni "umefanya hilo kosa au hujafanya ?". Hizo habari za "yule naye kafanya" hazikusaidii, pengine zitaonyesha tu kwamba unakubali kwamba umekosea.
Tatizo kama alivyotangulia kusema Jenerali Ulimwengu, chama tawala kinaongozwa na watu wasio na uwezo kiutawala, hata kama ufahamu wa nini kinachotokea wakati huu wanao. Maamuzi ya wafanye nini ili kuyakabilia ama kuyadhibiti yasiendelee hawana hata kidogo, azia kwa mkuu wa chama hicho hadi chini.
Hii ni kwa sababu wamechaguana/kupeana nafasi hizo si kwa vigezo vilivyowekwa kwa misingi ya chama cha wakati huo wa Nyerere bali kwa vigezo vinavyoendana na kuendelea kunufaishana kama kundi. Haya yote yanadhihirishwa na matamshi na hata vitendo vinavyoendelea kufanya wa wao, yakiwemo la Rais na TUCTA, Msekwa katika kusemea rushwa, Tabwe kutetea kauli ya JK, na mengine mengi. Hata hivyo, wote wanatutisha zaidi kuonyeshwa kwamba, wanaamini watanzania bado tu wajinga kiasi hicho cha kutofanya uchambuzi juu ya kauli zao na kuuona ukweli ama uongo ndani yake kirahisi zaidi. Ndiyo maana, pamoja na kukosema mara ya kwanza, mfano, rais alivyotishia TUCTA, bado watu kama Tambwe wanajitokeza kwa mara ya pili, na hata kesho bado watajitokeza kutetea makosa yaliyorudiwa zaidi ya mara mbili.

Hii, ndiyo sababu hasa ya sisi kama wananchi tunatiwa kinyaa na hatimaye inapelekea tufikie kutapika kirashisi tu kwa sababu ya hali ya mazingira tuliyomo kuchafuliwa kwa makusudi kabisa na kundi/genge hili la wafuja mali za umma.
 
Back
Top Bottom