Je ukweli unafichwa Ripoti ya Jaji Chande

Je ukweli unafichwa Ripoti ya Jaji Chande

Nicolas J Clinton Gabone

JF-Expert Member
Joined
Mar 13, 2014
Posts
897
Reaction score
559
RIPOTI YA JAJI OTHMAN CHANDE NA DAMU YA TAIFA

JE, UKWELI UNAFICHWA?

Ninaona kuna juhudi za kuuficha ukweli, jambo linaloibua mashaka kwamba huenda lengo ni kulinda maslahi ya watu wachache pamoja na kuimarisha taswira ya uhalali wa serikali iliyoshika madaraka katika mazingira yenye utata.

Imeandaliwa na,
Nicolas Jovin Clinton Gabone
Kiongozi wa zamani wa Jumuiya ya Vijana ya NCCR-Mageuzi.

Well, Ripoti ya Tume ya Jaji Othman Chande haiwezi kutazamwa kama waraka wa kawaida wa utawala, bali ni nyaraka inayogusa moyo wa Taifa, uhalali wa serikali ya sasa na dhamira ya mfumo wetu wa demokrasia. Ndiyo maana kauli ya Rais kwamba ripoti hiyo ni “yake” inapaswa kuchunguzwa kwa darubini ya taaluma, kisheria, kisiasa na hata kimaadili, au kauli yake ilikuwa ya kusudi kuhamisha mjadala wa ripoti yenyewe.

Kisheria, ni kweli kuwa Tume iliyoundwa na mamlaka ya Rais huwasilisha ripoti kwa mamlaka hiyo, na kwa mantiki hiyo Rais anaweza kuwa na nafasi ya kwanza ya kuipokea na kuifanyia kazi. Hata hivyo, ukweli wa kisheria haupaswi kutumiwa kama pazia la kufunika ukweli wa kitaifa. Ripoti inayohusu maisha ya wananchi, damu iliyomwagika na majeraha ya kisiasa ya Taifa zima haiwezi kuelekezwa kuwa mali ya ofisi au ya mtu mmoja. Mara tu ripoti inapogusa maslahi ya umma, haki ya wananchi kujua inakuwa kubwa kuliko haki ya mamlaka kuihodhi.

Hapo ndipo mjadala unapoingia katika eneo la fikra pana na hisia mseto. Kwa upande mmoja, wapo watakaoona kuwa Rais ana mamlaka ya Katiba na utawala ya kusimamia nyaraka hiyo, kuamua muda wa kuichapisha, au namna ya kuitekeleza. Lakini kwa upande mwingine, jamii ya kisiasa, wanazuoni wa sheria na makundi ya haki za binadamu na mimi Gabone watahoji kwa nguvu, ikiwa ripoti hii inahusu vifo vya mamia ya watu, maelfu ya majeruhi, na matumizi ya nguvu ya Dola, ni kwa msingi upi ukweli huo unabaki chini ya milki ya mamlaka moja?

Hapa suala si umiliki wa karatasi, bali umiliki wa ukweli wa kihistoria. Ukweli unapozuiwa kufikishwa kwa umma, hata kwa muda mfupi, mashaka yanaanza kuzaliwa je, kuna sehemu ya ukweli inayolindwa? je, kuna majina, maelezo au maelekezo ambayo yanaweza kuibua uwajibikaji wa kisiasa au wa kisheria yanayozuiwa kuonekana?

Hoja hii inakuwa nzito zaidi tunapounganisha na mawanda ya uchunguzi yenyewe. Ripoti imejikita sana katika matukio ya tarehe 29 Oktoba 2026, siku ya uchaguzi. Lakini mjadala wa kitaaluma hauwezi kuishia hapo, kwa sababu hoja kubwa inayosukumwa na ushuhuda wa waathirika na wachambuzi ni kwamba mauaji na matumizi ya nguvu yaliendelea hata baada ya siku hiyo, katika mazingira ambayo hakukuwa tena na maandamano wala vurugu za wazi. Hapo ndipo kuna swali la msingi je, ripoti imefupisha mgogoro mpana wa kitaifa na kuubana ndani ya fremu ya siku moja? Ikiwa mauaji yaliendelea baada ya maandamano kusambaratika, basi kuyahusisha yote na simulizi ya “ghasia za uchaguzi” kunaweza kuonekana kama upunguzaji wa ukweli na ujenzi wa simulizi inayonufaisha upande mmoja wa mamlaka.


Kisheria, hili ni eneo hatari sana. Matumizi ya nguvu ya Dola yanahalalishwa tu pale ambapo kuna ulazima wa moja kwa moja, tishio linaloonekana, na uwiano kati ya nguvu iliyotumika na tishio lenyewe. Ikiwa baada ya tarehe 29 Oktoba hakukuwa na maandamano wala uvunjifu wa amani, lakini vifo viliendelea kuripotiwa, basi hoja ya “kudhibiti hali” inapoteza nguvu ya kisheria na kuibua maswali ya uwezekano wa matumizi ya nguvu kupita kiasi au hata mauaji yasiyo na msingi wa sheria. Swali la kisheria hapa si tu nani alifyatua risasi, bali nani alitoa amri, chini ya mazingira gani, na kwa msingi upi wa sheria. Haya ni maswali ambayo jamii ya watu wenye bongo kama wewe msomaji huwezi kuyapuuza.

Kwa maadili, kauli ya kuhodhi ripoti inazua hisia kali zaidi. Taifa haliwezi kujenga uponyaji wa kisiasa juu ya ukweli uliofichwa, kwa style ya usomaji wa mtoa ripoti ni kama hakujiandaa wakati yeye ndiye mkuu wa Tume au alikuwa amepewa maelekezo zaidi ya hapo, ukweli anajua yeye au ipo siku na sisi tutajua tu. Kaya zilizopoteza wapendwa wao hazitafuti tu takwimu, zinatafuta ukweli, haki na uwajibikaji. Hivyo, kuzuia ripoti kuwa ya umma kunaweza kutafsiriwa kama kukataa kaya hizo haki ya kujua kilichotokea. Katika maadili ya utawala bora, uwazi si hisani ya serikali kwa wananchi ni wajibu wa msingi wa Dola kwa walioweka mamlaka hayo mikononi mwake.

Sasa ndugu Watanzania, suala hili lina uwezo mkubwa wa kuchochea mjadala wa kitaifa na kuumba mitazamo inayokinzana. Kwa wanaoitetea serikali, hatua ya Rais inaweza kuonekana kama njia ya kuhakikisha taarifa zinachujwa kwa umakini kabla ya kuachiwa kwa umma, siyo mbaya. Lakini kwa upande wa wananchi, wanazuoni na wanaharakati, inaweza kuonekana kama jaribio la kudhibiti simulizi za hadithi na kupunguza uzito wa uwajibikaji wa Dola, au watu wachache. Hii ndiyo sababu mjadala huu haupaswi kuonekana kama mjadala wa utawala pekee, bali ni mjadala unaogusa uhalali wa serikali ya sasa, imani ya wananchi kwa taasisi za Dola na mustakabali wa maridhiano ya kitaifa.

Nachomekea hapa kidogo, Comrade Steven Wasira anapaswa kuepuka kauli za kiburi, kejeli na majigambo, na kuelewa kuwa Taifa hili litaendelea kuwepo hata bila uwepo wake binafsi. Ni vyema akajiepusha na lugha au mienendo ya dharau isiyoendana na misingi ya heshima ya uongozi na majadiliano ya kitaifa.

Tuendelee, kwa kifupi, suala la Rais kuhodhi ripoti ya Jaji Chande haliwezi kutenganishwa na mjadala wa mawanda ya uchunguzi wa matukio ya baada ya tarehe 29 Oktoba. Hapa ndipo nguvu ya hoja ilipo, kama ripoti imejikita katika siku ya uchaguzi huku ukweli wa mauaji ya siku zilizofuata ukiwa bado una maswali, na wakati huo huo umma ukinyimwa fursa ya kuisoma na kuichambua, basi Taifa linaingia katika eneo la mashaka makubwa ya kisiasa, kisheria, taaluma na maadili. Mjadala wa kweli unapaswa kuuliza si tu “ripoti ni ya nani,” bali zaidi, “ukweli ni wa nani?” Na katika Taifa la (demokrasia), jibu la swali hilo haliwezi kuwa la mtu mmoja, ukweli ni wa umma, historia ni ya Taifa, na haki ni ya wananchi.
 
Uchambuzi mzuri sana

Bi Samia Suluhu Hassan anaficha ukweli akidhani kuwa ukweli ni mali yake

Samia yeye na afiche makaratasi, hatuna shida nayo sisi...

Lakini akumbuke hili, kuwa, DAIMA UKWELI HUWA HAUFICHIKI kwani UKWELI ni kama kaa la moto ambalo mtu kalificha ktk mfuko wa suruali, lakini mara linapoanza kumuunguza atalia na kulitoa yeye mwenyewe iwe anapenda au hapendi..!

Muda (time) ni mwamuzi mzuri sana..
 
Comrade Steven Wasira anapaswa kuepuka kauli za kiburi, kejeli na majigambo, na kuelewa kuwa Taifa hili litaendelea kuwepo hata bila uwepo wake binafsi. Ni vyema akajiepusha na lugha au mienendo ya dharau isiyoendana na misingi ya heshima ya uongozi na majadiliano ya kitaifa. 📌📌📌🔨🔨🔨
 
Ndg zangu, hv kweli kbs mlitegemea ile tume itoe ripoti ya kumkandamiza boss wao??.
Hivi kwanza mmeshajua ni maposho mangapi wameshalipwa hadi leo plus ASANTE ya kukamilisha ripoti nzuri???.
Mmechelewa kufahamu ukweli, hii ilikuwa ni tume maalum ya kumsafisha samuya juu ya mauaji ya kabla na baada ya 29 oktoba!!.
 
Back
Top Bottom