Je alikuwa ni mama...?

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,395
peeking.gif


Nina uhakika kuhusu watoto wanaoteswa na wazazi wao, wanavyojisikia. Nina uhakika kwa sababu, niliwahi kutokea kuwa mmoja kati ya hao. Lakini pia najua kuhusu watoto wanaoteswa na hata kudhuriwa na kimaisha na mama zao wa kambo. Hapa kwenye hili sitaki kusema chochote kwa sasa.

Nilizaliwa Kilosa mwaka 1960 ambako baba yangu alikuwa mwalimu wa shule ya msingi. Nikiwa na miaka minne hapo hapo Kilosa kwenye kitongoji cha Ulaya, mama yangu mzazi alifariki wakati akijifungua. Bahati mbaya zaidi ni kwamba alifariki yeye na mtoto wake, ambaye angekuwa ndiye mdogo wangu pekee. Baada ya mama kufariki, baba aliomba uhamisho kwa imani kwamba, kifo cha mkewe kiliwa ni mkono wa mtu. Alipewa uhamisho na kupelekwa sehemu inayoitwa Wami Dakawa humohumo mkoani Morogoro. Nikiwa na miaka minane, baba aliamua kuacha kazi. Wakati huo, kwa mujibu wa kumbukumbu zangu alikuwa kama amechanganyikiwa kidogo.

Nasema alikuwa kama amechanganyikiwa kwa sababu alikuwa ni mkali sana, mkatili, na anayeonesha kabisa kwamba, hakuwa na amani na nafsi yake. Pamoja na kwamba alikuwa ni mwalimu {Kabla hajaamua kuacha kazi} mimi mwanaye nilianza shule nikiwa na miaka minane baada ya kuhamia Dakawa. Tena huko kuanza shule kulitokana na shinikizo la wenzake. Ukweli ni kwamba tangu kifo cha mama yangu, baba yangu alikuwa kama adui yangu. Nikiwa na miaka mitano alikuwa akiniachia kazi kama kupika mboga, hasa maharage na nyingine zenye kuhitaji kukagua maji tu. Nilifanya kazi hizo na kuna wakati nilikuwa nakosea.

Nikiwa na miaka mitano nilikuwa napigwa sana kwa makosa ambayo hata mtu wa miaka 15 asingekwepa kuyatenda. Nilikuwa nashinda na kulala na njaa wakati mwingine. Kuna wakati baba alikuwa anaondoka na kwenda kushinda kwenye kaduka kake kalikokuwa karibu na eneo la sabasaba, bila kuacha chochote. Sisi tulikuwa tukiishi mji mpya. Nilikuwa nashinda na njaa au kulala na njaa kwa sababu alikuwa akiondoka asubuhi akiwa amesahau au kufanya kusudi bila kuacha chochote na alikuwa akichelewa sana kurudi. Hakuwa mlevi, lakini sijui alikuwa akipotelea wapi.

Kulikuwa na watoto jirani tuliokuwa tukisoma wote, ambao nadhani walikuwa wamewaambia wazazi wao kuhusu maisha yangu. Kwani wazazi wao waliwaambia waniambie niwe naenda kule nyumbani kwao kama kujisomea kidogo. Lakini nilijua walikuwa wakitaka niende hapo kwa ajili ya kula. Hii ilinisaidai kidogo kwa sababu, hata kama nisingekunywa chai asubuhi, kwa kuwa shule tulikuwa tukila buruga {aina ya uji wa njano}, nilijua jioni ningepata chakula cha kwa rafiki zangu. Sijui hata hivyo ilitokeaje, kwani baba alijua nakula ile nyumba ya jirani. Kwa kweli nilipigwa sana siku hiyo na alikwenda pale kuwatukana wale wasamaria wema.

Nilianza tena maisha ya mateso na shida. Lakini wale wenzangu walikuwa wakiniambia kwamba, nivumilie kwani nitakuwa mkubwa na nitalipiza kwa baba.
Wakati nikiwa darasa la tatu walikuja ndugu zake baba wawili kuishi nasi. Mmoja binamu yake na mwingine ndugu wa huyo binamu. Walikuwa bado vijana wadogo tu, hawakuwa wanazidi miaka 20. Sasa hapo mateso yalikuwa makubwa sana. Hawa jamaa walikuwa wanafanya makosa na kunisingizia mimi. Walikuwa wakiiba fedha za baba, walikuwa wakiharibu vitu na nilikuwa nasingiziwa mimi. Nilikuwa napigwa sana. Hawa ndugu zake baba nao walikuwa wakinipiga sana bila makosa.

Walikuwa wakijitahidi sana kuninyima chakula na mambo ya namna hiyo. Nikiwa hilohilo darasa la tatu niliamua kuacha shule. Sikuona sababu ya kusoma, na nilijua nisingemudu tena. Nilikuwa nikienda karibu na kiwanda cha tumbaku, eneo ambalo linaitwa Tumbaku kufanya vibarua. Kwa mwaka mzima sikuhudhuria shule na nilianza kweli kuwa mtundu. Huko nilianza hata kujifunza kuvuta bangi, ingawa mara chachechache. Nilijifunza kuchungulia wanawake wanaooga hapo karibu na kiwanda, kama walivyokuwa wakifanya wakubwa. Baba hakuwa akijua kwamba nilikuwa siendi shule na pengine hata angejua asingejali, kama angejali ingekuwa ni kwa kunitimua hapo nyumbani tu labda.


Asubuhi nilikuwa na sare za shule na huku nikiwa na nguo za kazi kwenye mfuko wangu wa madaftari. Jioni, nilikuwa narudi kama vile nimetoka shule. Wale ndugu zake baba waligundua kwamba, nilikuwa sijali kuhusu chakula chao na nilikuwa nawajibu hovyo, hivyo walinikomoa. Walimwambia baba kuwa nakula kwa jirani na eti nimesema baba anamalizia fedha zake kwa wanawake. Nadhani ujumbe waliotaka kumpa ndugu yao, yaani baba, bali wakaona ingekuwa salama kwao kuupitishia kwangu. Siku hiyo nilipigwa hadi jirani ikabidi waingilie kati. Baba alinitukana sana, hasa kwa kunisimanga kuhusu mama yangu kufa.

Nilitahayari sana na ilibidi nimwambie kwamba, kama yeye ana akili mbona ni masikini. Sijui hata nilifikiria nini kusema hivyo. Niliamua sasa kwamba sijali. Nilikuwa natoka asubuhi bila sare za shule bali na nguo zangu za kawaida na kwenda kibaruani. Nilikuwa nimekata tamaa bila shaka.
Mwaka ukakatika na wenzangu walifunga na kufungua shule wakaingia darasa jipya, mwaka 1973. Nilitakiwa niwe darasa la tano, lakini badala yake nilishaanza kuzoea maisha ya mitaani. Mwaka huo huo, Februari ndipo ambapo baba aliamua kuoa. Nilisikia akiwaambia wale ndugu zake habari hizo. Mmoja kati yao, yule ndugu wa binamu yake aliyekuwa akiitwa Hamadi ambaye alikuwa akinichukia sana, alimwambia baba kwamba, ningemsumbua sana huyo mkewe. Baba alisema kwamba, kama ninataka kufa, hapo ndipo palikuwa pahala pazuri pa kufia. Aliongeza kuwambia kwamba, angemtahadharisha sana huyo mke wake mpya kuhusu mimi.

Kweli alioa kwa sherehe ndogo ambayo ilifanyika pale pale nyumbani. Baba alikuwa amepanga nyumba nzima ya vyumba vitatu, tulimokuwa tukiishi. Nilikwambia nilikuwa nikilala sebuleni, unaweza kuhisi kwamba, labda ninajaribu kuongopa. Nitakwambia ni kwa nini baba yangu alikuwa akinichukia. Baada ya sherehe ile ya ndoa, ambayo ilihusisha ndugu zake yule mama wanne na wale binamu wa baba na mimi ambaye pale nilikuwa kama kijana wa kutumwa, ulifika muda wa mke wa baba kutambulishwa kwa familia. Baba aliwatambulisha wale ndugu zake wawili kwa yule mama mpya. Halafu alimwambia yule mkewe ambaye nilishamchukia hata kabla hajaolewa, ‘huyu ndiye yule mtoto niliyekwambia. Kama akikukera muda wowote naomba nipate taarifaharaka ili nimfunze adabu. Na vitu vyako uviweke vizuri, maana……'

Yule mama yangu mpya wa kambo aliingilia kati. ‘Sawa nimekuelewa, lakini kwa nini usiniache mwenyewe nikaona kama kweli ni mkorofi?' Huyu mama ambaye naye alikuwa mtu mzima kidogo, akiwa ni mwalimu aliyewahi kufundisha na baba wakati baba anaanza kazi, alisema huku nikiona wazi kwamba, kauli za baba hazikumshawishi. Wale ndugu zake baba walicheka na kusema, ‘kwani shemeji tangu uje hujaona kwamba huyu ni mtoto wa mtaani huj….' Yule mama mpya alimwambia binamu yangu. ‘Nikiwa humu ndani, nisikusikie tena unasema hayo maneno. Nimesema mniache nione mwenyewe, mnanifundisha nini sasa!' Mama alionekana wazi kwamba alikuwa amekasirika.

Nilihisi kama vile nataka kucheka au kuruka kwa furaha au kulia au sijui kufanyaje, sikujua tu. Hajawahi kuja mgeni pale nyumbani na kuambiwa mambo yangu na kuacha kuwaunga mkono baba na ndugu zake. Yule alikuwa ni mtu wa kwanza. Halafu kumbuka alikuwa ni mama wa kambo ambaye nilitegemea angekuwa katili kuliko baba. Lakini kumbe bado nilikuwa sijagundua jambo kubwa zaidi. Jioni ile baba na ndugu zake na mkewe ilikuwa watoke kwenda kutembea mjini kukamilisha ile sherehe ya ndoa. Baba alitoka kwenda kwanza dukani na ndugu zake walitoka nao sijui kwenda wapi. Tulibaki mimi na mama yule mgeni.

Kwenye saa 10.30 jioni yule mama alipokuwa ametoka kuswali aliniita na kuingia nami chumbani kwa baba. Nilisita kuingia kwa sababu nilikuwa nimepigwa marufuku hata kusogelea mlango wa chumba hicho, kwani binamu zake baba walikuwa wakiiba fedha za baba na kudai ni mimi. ‘Ingia Almasi, usiogope mimi ni mama.'

Niliingia na mama aliniambia nikae kitandani. 'Unasikia mwanangu, usikubali kuwa wewe ni mtundu.' Yule mama alianza kusema akiwa amenishika mkono. 'Wewe ni mtoto mzuri, mwenye akili na huruma. Nimekuona ile asubuhi nilipokuja, kwamba, huna tatizo hata kidogo.'Alinyamaza na kuendelea kusema, 'najua unafahamu kwamba, mama yako alikwishafariki, lakini akina mama wanapofariki, hurudi kwa njia nyingine, kuja kuwapenda tena watoto wao. Nimerudi kuja kukupenda ili usome na kufika mbali sana. Lakini usimwambie mtu. Mimi ni mama yako, nataka nikuone ukiwa shujaa kama wakati ule ulipokuwa mdogo….' Alitulia kidogo, alikuwa akilia.

‘Unajua ulipokuwa mdogo ulitambaa na kutembea haraka sana kuliko watoto wengine pale mtaani, hadi watu wakashangaa. Nataka uendelee kuwa mtoto mzuri na mwenye bidii kama wakati ule. Kumbuka kwamba, mimi ni mama nimekuja kukulea.' Akiwa anafuta machozi aliniambia. ‘Tafuta zile nguo zako nzuri, nikuandalie, jioni tutaenda wote na baba kutembea mjini.' Nilihisi kitu ambacho hadi leo wala sikijui kilikuwa ni nini. Nilijiona kama siko duniani au sijijui. Nilibubujikwa na machozi na nilisema kwa kunong'ona, ‘sina nguo nzuri.'

Yule mama alisimama na kusema, ‘usijali mwanangu.'
Alikwenda kwenye sanduku lake na alilokuwa amekuja nalo asubuhi ile na kulifungua. Alitoa suruali, shati na viatu, vyote vipya. Aliniambia nikaoge, halafu nivae nguo zile. Nikiwa na kichwa chepesi hadi kufikia kuyumba, bila kujua sababu, nilikwenda kuoga. Nilimwacha mama huku nyuma akiwa bado anafuta machozi yake. Nilirudi bafuni na kuvaa nguo zile. Ilikuwani mara ya kwanza kwangu kuvaa nguo mpya nikiwa na akili ya kukumbuka, ukiacha sare za shule. Mama alinisifia sana na nilihisi ile hali ambayo sikuwa ninaijua. Hali ngeni kabisa.

Saa 11.30, baba na wale ndugu zake walirudi na awali hakuna aliyenitambua. Waliponitambua, binamu yake baba alisema, ‘umeiba wapi nguo hizo?' Nilimtazama mama ambaye nilikuwa naye pale sebuleni, naye kama kuonyesha kunilinda kama alivyoahidi alisema. ‘Ni mimi nimeiba, Unasemaje?' Palizuka ukimya. Halafu mama alisema maneno ambayo siwezi kuyasahau. 'Huyu ni mwanangu. Hana tabia mbaya na wala sio mjinga kama mnavyotaka aamini. Huyu ni mtoto mjanja na mwenye uwezo mkubwa wa ufahamu. Nataka niseme hivi. Huyu ndiye atakayeniweka au kuniondoa katika nyumba hii. Akionewa tu, nafunga kilicho changu, naondoka na sioni aibu kusema kwamba nitaondoka naye. Nimemaliza.' Hakuna aliyejibu labda kwa sababu hakuna aliyeamini.

Ni kweli hakuna aliyesema neno na sikusikia neno kwa siku ile wala zilizofuata. Wiki ile ile nilianza masomo na wale ndugu zake baba waliondoka miezi miwili tu baadae baada ya kushindwa kuishi na mama ambaye alikuwa ni mtu mnyoofu, anayesema kile ambacho kipo na kinachopaswa kusemwa. Hata baba aliwachukia sana. Huyu mama ndiye ambaye alimbadili kabisa baba na kumfanya kuwa mtu tofauti kwangu. Nikiwa na umri wa miaka 13 ndipo nilipoanza kujua upendo wa baba na mama.

KWA NINI BABA ALIKUWA ANANICHUKIA?

Niligundua kwamba baba katika kuhangaika kwake kwa waganga, aliambiwa kwamba mimi nilizaliwa na mkosi, hivyo kifo cha mama kilikuwa kimepitishwa mikononi mwangu na wachawi na kwamba kama ningekuwa mtu mzima nikiwa kwake, ningesababisha mikosi kwa familia yake. Kwa hiyo baba hakutaka niwe mtu mzima nikiwa kwake. Mama yangu wa kambo ambaye ndiye mama yangu mzazi kwa ninavyoamini kutokana na upendo wake, ndiye aliyebadili mawazo ya baba ya kishirikina na kumfanya kuanza kufikiri vizuri zaidi kuhusu mimi na maisha kwa ujumla.

Leo hii baba yangu amefariki, lakini mama yangu ninaye, nikiwa na mdogo wangu wa kike ambaye ameolewa na ana shughuli zake. Huyu mdogo wangu hakuzaliwa na baba yangu, kwani huyu mama mwema alipokuja kuolewa na baba tayari alishaolewa na kuachana na mumewe na walikuwa na mtoto huyo. Huyu mama ndiye ambaye ameniwezesha kuishi maisha haya ya uadilifu na amani niliyo nayo leo. Ndiye ambaye aliniwezesha kusoma hadi chuo kikuu na kupata ajira na baadae kuanza maisha ya kujitegemea. Ni kweli alikuwa ni mama yangu aliyekuja kunilinda.

Najaribu kufikiria, kuna akina mama wangapi wanaoweza kumkubali mtoto wa mwanamke mwingine kama alivyo? Ni wachache kupindukia. Wengi juhudi yao siku zote ni kuona watoto wa kambo wanakorofishana na baba zao, wanateswa na kutupwa nje ya familia. Lakini ni kwa faida ya nani? Siku zote ni kwa hasara zao. Huja kugundua wamepata hasara wakiwa wamechelewa uzeeni. Ninampenda na nitampenda kuliko mtu mwingine yeyote, mama yangu ambaye amenionesha maana ya kweli kuhusu maisha. Amenifundisha kwamba, suala siyo mama wa kambo, bali ubinadamu, kujua kupenda.

Alikuwa ni mama………………
 
Duuh..nimetoka machozi kidogo I don't know why. Ni story nzuri sana hii kwenye hii jamii yetu ambayo leo kutesa watoto wa wengine imekuwa kitu cha kawaida tu.
 
Mtambuzi babu yangu, kwanza asalam aleykum! pili napenda kusema am soooo touched na hii story ya huyu kaka na upendo wa huyu mama! kwa kweli alikuja at the right tym to save him, wamama wenye roho hiyo are soooo few, ila wababa wapo na nimeona, wanalea watoto wa kambo vizuri tu! fellow women we need to change!
 
Last edited by a moderator:

Yaani hii story imenifanya nitoe machozi na kunikumbusha mbali sana

Shebesha





Mtambuzi babu yangu, kwanza asalam aleykum! pili napenda kusema am soooo touched na hii story ya huyu kaka na upendo wa huyu mama! kwa kweli alikuja at the right tym to save him, wamama wenye roho hiyo are soooo few, ila wababa wapo na nimeona, wanalea watoto wa kambo vizuri tu! fellow women we need to change!
 
Kwa dunia ya leo,ni watu wachache sema wenye roho nzr kama ya huyo mama.ni roho mbovu tu tulizonazo wanawake kwann ucmpende mtoto wa mwanamke mwenzio? Unamjua atakae kufaa ni nani? Hebu tujiulize.mana unaweza kuzaa watoto wengi na asikufae hata mmoja.nakumbuka mama yangu alinambia KUZAA SI KUPATA,KUPATA MAJAALIWA.
 
Mtambuzi babu yangu, kwanza asalam aleykum! pili napenda kusema am soooo touched na hii story ya huyu kaka na upendo wa huyu mama! kwa kweli alikuja at the right tym to save him, wamama wenye roho hiyo are soooo few, ila wababa wapo na nimeona, wanalea watoto wa kambo vizuri tu! fellow women we need to change!
cacico hii ni simulizi ya kweli na inaonyesha upande wa pili wa shilingi.............
 
Last edited by a moderator:
Jamani Mtambuzi umeniacha nabubujikwa na machozi
Mwenyezi mungu ampe maisha mema na marefu huyo mama alieamua kumtunza na kumlinda mtoto wa mwanamke mwenzi kwa upendo wa hali ya juu na usio na kikomo
Ni upendo adimu kutokea
Ni upendo wa Agape
You made my day Mtambuzi nimejifunza kitu kupitia hii habari
God bless
 
Kwa dunia ya leo,ni watu wachache sema wenye roho nzr kama ya huyo mama.ni roho mbovu tu tulizonazo wanawake kwann ucmpende mtoto wa mwanamke mwenzio? Unamjua atakae kufaa ni nani? Hebu tujiulize.mana unaweza kuzaa watoto wengi na asikufae hata mmoja.nakumbuka mama yangu alinambia KUZAA SI KUPATA,KUPATA MAJAALIWA.

Ahsante farkhina kwa maoni yako mazuri.............................
Hili ni soma kwa wazazi wote bila kujali jinsia kwani hata baba alikuwa na yake................
 
Last edited by a moderator:
Hadithi zako ndefu lakini ni mzuri saaana, leo nimebahatika kuisoma yote. Asante kwa somo, kwakweli ni wamama wachache sana wenye moyo kama huo, ila mimi nipo kama huyo mama kwani na mie pia nina mtoto wa 12yrs anafurahia maisha vizuri
 
Mtambuzi! Hii ni zao la Jitambue?

Nieipenda hii, kuonesha upande wa kushoto wa kadhia ya Mama wa kambo. Hili ni tatizo langu kwa baadhi ya wanaJF kwenye "comment" zangu nyingi KUONESHA UPANDE WA KUSHOTO WA KADHIA lakini wanajamvii hunishambulia sana.

Bazazi!
 
Huyo mwanamama ni 'A true Legend' na 'Visionary' mtu anayeona potential ya mtu na kumuinua...

Now this is the true love. Kama mtu alikuwa hajui definition ya true love basi aje asome.

Again more power to you Mkuu Mtambuzi
!
 
Last edited by a moderator:
cacico hii ni simulizi ya kweli na inaonyesha upande wa pili wa shilingi.............
nimeona babu, na laiti leo ningekuwa na mtoto wa kambo hapo nyumbani, ningebadilika leo, imenigusa sana, nimeona kumbe hata mimi naweza kufa kesho, na mwingine akawalea watoto wangu vizuri tu, then why not me doing that to my follow woman??? yaani imenigusa sana!
 
Thanks Gustavo kwa kweli, ni zaidi ya shule..
Ushirikina mbaya sana, yaani waAfrica ni hii dhana yetu ya hakuna natural death ni mbaya sana.

Ndugu nao huwa wanakuwa nyoka ili tu waweze kujinufaisha, sijawapenda hata kidogo...!

Mama wa kambos inabidi wa jifunze hapa kuwa mtoto wa mwenzio ni wako unatakiwa kumlea ipasavyo kwani wewe pia waweza kuacha mwanao akalelewa na watu wengine.

Inasikitisha sana, kwani kijana hakuwahi hata kusifiwa wala kuonekana anaweza kufika alipofika.
Thanks kwa mamama wenye tabia ya upendo na msimamo kama huyu mama!
K
 
Goku wabhe'ja sana, nimesoma huku nikibubujikwa na machozi ya uchungu uliochangayika na furaha. Nimejifunza kitu kikubwa sana si kina mama tu wanaopaswa kutenda mema kwa watoto bali hata watoto pia tunatakiwa kuwapenda na kuwaheshimu mama au baba ambao si wetu. Asante sana Babu Mtambuzi.
 
Last edited by a moderator:
daaah hadi namaliza kusoma hii hadithi ya kweli macho yangu mekundu kwa kufuta machozi... Ni mungu amemleta huyu mama ambaye amekua ni guardian angel kwako! Ni wachache sana wa design yake mungu amzidishie umri ili nae afaidi upendo wa mtoto kwa *****, daaah bigup sana kwake umenifundisha kitu hapa... Asante kwa kupost kitu yenye msaada kwa wengi.
 
Mtambuzi umeniliza mchana wa leo.

Ila piaa umenifanya nireflect true life, ngoja nkwambie wapo wamama wenye roho mbaya ambao hata cacico katuambia tubadilike lakin pia wapo wababa wenye roho mbaya sana nao pia wabadilike. Ila ishu kubwa naiona kwa mtoto husika hasa anapokuwa ni mtu ambaye tayari ameshaanza kujitambua.

Jamani kuna watoto wa kambo wengine hata uwaishishe vipi kwa upendo gani hawakubali wanapenda kuishishwa "maisha ya "mtoto wakambo mke wa baba au mume wa mama" hawa na wenyewe waweza kukutia doa weye baba au mama na kuonekana kuwa unamtesa.

Binafsi nafikiri wote wanapaswa kujitathmini na kuishi kama binadamu kwa upendo na amani.Jamani unachopewa kna maisha ndicho halali yako lazima ukipende na kukithamini ukipewa mzazi wa kambo au mtoto wa kambo ndiyo halali yako yakupasa ukipende tu. Kwa bahati mbaya sana hali zote zweza kubadilika lakini ya ukambo kamwe haiwez kubadilika ikisha kuwa imekuwa tu hata ufanyeje manake hata kifo bado hakitosh kufuta uhalisia huu.
 
Last edited by a moderator:
The devil is always a liar!
Asante sana kwa ujumbe touching na wenye mafunzo makubwa. Duh, shetani kweli ana nguvu lakini Mungu ni wa Ushindi siku zote.

Je ni true story au?
 
Back
Top Bottom