Yanga yafungiwa CAF
na Khadija Kalili
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
SIKU moja baada ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuifungia Yanga katika mashindano yake, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nalo limeipiga ‘stop' kucheza mashindano ya kimataifa kwa miaka miwili.
Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema jana kuwa huo ni uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo, iliyoketi juzi na kutoa adhabu hiyo kwa kitendo kilichofanywa na Yanga.
Mbali ya adhabu hiyo kwa Yanga, pia Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega na Katibu Mwenezi wake, Francis Lucas, wamepewa siku saba kuthibitisha madai kuwa kulikuwa na makubaliano ya Simba na Yanga kupewa sh mil 50 kila moja.
Mwakalebela, alisema Mwakalebela alisema Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Jumatatu na Rais wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga, imetoa adhabu hiyo ili kuwa funzo kutokana na timu hiyo kuwakacha Simba katika mechi ya Jumapili.
Hiyo ilikuwa mechi ya kusaka nafasi ya mshindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Kagame, iliyoanza Julai 12 na kufikia tamati Julai 27.
Alisema kuanzia jana ni marufuku Yanga kucheza mechi za kimataifa - iwe za kirafiki au za ushindani - hali inayoifanya Yanga kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga ilipata nafasi hiyo baada ya kumaliza nafasi ya kwanza katika Ligi Kuu iliyofikia tamati Aprili 27, huku Prisons ikimaliza ya pili na Simba nafasi ya tatu.
Alisema kuwa adhabu hiyo imetolewa na Kamati hiyo kwa mujibu wa mamlaka ya kikatiba iliyopewa kutokana na makosa yaliyofanywa na Yanga yaliyoitia nchi aibu.
"Ni kinyume kabisa cha dhana ya ‘fair play' (uungwana wa michezo). Zaidi ya hapo, kitendo cha Yanga kimeiweka katika nafasi mbaya TFF na wadhamini waliowekeza mamilioni ya shilingi katika mashindano hayo," alisema Mwakalebela.
Mwakalebela alisema kitendo cha Yanga kimeidhalilisha TFF kama mwenyeji wa mshindano ya Cecafa, kwani kingeweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao na kurudisha nyuma jitihada za maendeleo ya soka nchini.
Mbali ya adhabu hiyo, Kamati ya Utendaji, ikitumia ibara ya 34 kifungu 1(q), Madega na Lucas wametakiwa kuwasilisha utetezi wao kuhusu kila klabu kupewa sh mil 50.
Alisema hiyo ni kutokana na kauli ya Katibu Mwenezi wa klabu hiyo, Lucas, aliyotoa muda mfupi baada ya kufutwa kwa mechi ya Simba na Yanga, kwamba Yanga ilifanya hivyo baada ya TFF na Cecafa kukiuka makubaliano ya kila klabu kupewa mil 50.
Mwakalebela alisema Jumapili jioni Julai 27, Mwenyekiti wa Yanga, Madega, alikutana na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Lamada na kusisitiza madai yaliyokuwa yametolewa na katibu mwenezi wake, kwamba walizuia timu baada ya kubaini unafiki na ubabaishaji katika uendeshaji wa soka.
Mwakalebela alisema kilichotokea ni viongozi wa klabu hizo kuomba kupewa fedha za kulipia gharama za kambi, hivyo kila timu kupatiwa sh mil 5.
Katika kuleta ufanisi zaidi, TFF ilifanya mazungumzo na wadhamini wa michuano hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), waliotoa sh mil 3 kwa Yanga, Simba na Miembeni.
Alisema baada ya kutekelezwa hayo, suala la fedha lilikuwa limekwisha, hivyo kupisha taratibu nyingine za mechi ya Jumapili ambako saa nne subuhi ya siku ya mechi, kulikuwa na mkutano na kuhudhuriwa na viongozi wa klabu zote mbili.
Kwa mantiki hiyo, hakukua na makubaliano yoyote kuhusu Simba na Yanga kupewa fedha kiasi cha sh mil 50 kabla ya mechi.
Katika hatua nyingine, Rais wa Cecafa, Leodegar Tenga, amesema hana budi kuwaangukia kwa maandishi wadhamini wote na mlezi wa Kombe hilo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kwa kitendo kilichotokea.
Wadhamini wa Kombe hilo, TBL kupitia bia yake ya Castle na Shiririka la Utangazaji Tanzania (TBC) na mashabiki wote wa soka wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.