Janeth Rithe: Wizara ya Maendeleo ya Jamii haipewi kipaumbele

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Janeth Joel Rithe: Wizara ya Maendeleo ya Jamii Haipewi Kipaumbele.

Utangulizi
Leo Alhamisi Mei 18, 2023 Waziri Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum amewasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa fedha 2023/24 ambayo umeanza kujadiliwa na inatazamiwa kupitishwa leo.

Sisi ACT WAZALENDO kupitia Waziri kivuli wa Afya, Tumeisikiliza na kuzichambua bajeti hiyo kwa kuangalia taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2022/23 na Mpango wa Bajeti wa 2023/24 Ili kuona ni kwa namna gani Bajeti ya Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, wanawake na makundi maalum inaakisi Mahitaji, matamanio na matarajio ya wananchi, Bajeti hii ni miongoni mwa bajeti zinazofuatiliwa kwa karibu sana na wananchi kutoka na uhusiano wake wa karibu na maisha ya watu.

Katika uchambuzi wetu tumebainisha hoja (6) kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwenye wizara hii kwa mwaka wa 2023/24.

1. Ufinyu wa bajeti unaifanya wizara kubaki kuwa ni idara.
Pamoja na wadau mbalimbali kupokea kwa furaha hatua za uundwaji wa wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maaalum. Mpango na makadirio ya mapato na matumizi wa 2023/2024 yaliyowasilishwa leo bungeni na Waziri inaonyesha wazi kuwa serikali bado haijajiandaa kuifanya hii ni wizara itakayoweza kukabiliana na changamoto ambazo hapo awali zilishindikana.

Ni wazi kuwa bajeti ni nguzo muhimu sana katika kuhakikisha vipaumbele na mipango iliyowekwa inatekelezwa.

Mwaka huu bajeti iliyoidhinishwa na bunge ni shilingi Bilioni 74.2 ambapo Fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za Maendeleo ni Bilioni 30.5 tu licha ya uhaba wa Watumishi wa Maendeleo ya jamii na watumishi wa Ustawi wa jamii, changamoto lukuki za Wamachinga, wanawake, wazee na makundi maalum.

Fedha ndogo kiasi hiki haiendani na majukumu ya Wizara, kiasi zaidi ya hicho hutolewa kwa ajili ya Idara katika Wizara nyengine.

Hivyo basi, ufinyu huu wa bajeti unaipotezea Serikali uhalali wa kuifanya hii ni wizara inayojitegemea ikiwa mpango wake, vipaumbele na utengaji wa bajeti unafuata mwenendo ule ule kama ilivyokuwa ni idara kuu kwenye wizara.

ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo kwenye wizara hii ambayo inashughulikia mafunzo ya uanagenzi, uhamasishaji wa Maendeleo na uratibu wa fedha za mikopo ya vijana, wanawake na walemavu.

2. Uhaba mkubwa wa maafisa ustawi na Maendeleo ya jamii
Uhaba wa rasilimali watu kwenye sekta hii muhimu unapelekea kushusha ufanisi wa utendaji na kukwamisha utekelezaji wa mipango na majukumu.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara kupitia hotuba ya bajeti mwaka 2023/24, Waziri anaonyesha upungufu mkubwa wa maafisa wa ustawi na maafisa wa maendeleo ya jamii hususani katika ngazi ya vijiji na kata.

Taarifa zinaonyesha kuwa mahitaji ya maafisa Maendeleo ya jamii ni watumishi 5,296 idadi ya maafisa waliopo kwa sasa ni 3,003, kwa hiyo kuna upungufu wa maafisa wa Maendeleo ya jamii 2,293 sawa na asilimia 43.3 Kwa upande wa maafisa wa ustawi wa jamii wanaohitajika ni 21,082 waliopo ni 996 sawa na Asilimia 4.7 na kufanya upungufu wa watumishi 20,057 sawa na asilimia 95.3 ya upungufu.

Katika bajeti ya mwaka hakuna kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kuajiri maafisa wa ustawi na Maendeleo ya jamii ili kukabiliana na upungufu huu. Waziri, Dkt. Gwajima ameishia tu kutaja changamoto na kutaka Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa ajira hususani katika ngazi za kata. Wizara haikutenga fedha kukabiliana na changamoto yenyewe.

ACT Wazalendo, tunaishauri Serikali kuweka mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo kwa awamu ya miaka minne kwa kuhakikisha inatoa ajira kwa wastani wa watumishi 6,169 kila mwaka.

3. Ukatili dhidi ya wanawake, wazee na watoto
Vitendo vinavyosababisha athari za kimwili, kingono, kisaikolojia au mateso kwa wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na kutishiwa maisha, kunyimwa uhuru, iwe hadharani au kwa kificho vinazidi kuongezeka nchini kwetu. Ukatili dhidi ya wanawake kupitia mitandao ya kijamii, ubakaji, ukeketaji, vipigo kwa wanandoa, mauaji ya wanawake na watoto imekuwa ni jambo linaloonekana kuzoeleka nchini. Pia, matukio ya ulawiti na ubakaji kwa watoto vinazidi kushamiri tena vitendo hivyo vinafanywa na watu wao wa karibu kabisa, baba mzazi, baba wa kambo na ndugu wa karibu (walezi wao).

Utafiti ulifanywa mwaka 2021 wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF – Tanzania) na Shirika la ECPAT International na INTERPOL unaonyesha kuwa silimia 4 ya watumiaji wa mtandao wenye umri wa miaka 12 – 17 nchini Tanzania ni manusura wa ukatili wa mtandaoni; Watoto wengi hufanyiwa vitendo vya ukatili kupitia mitandao ya kijamii kama vileWhatsApp, Instagram, Facebook, Tik Tok, wanaofanya vitendo vya ukatili ni watu wanaofahamika na watoto wakiwemo ndugu wa karibu na marafiki.Aidha watoto wanaofanyiwa ukatili hawajui namna na sehemu ya kutoa taarifa ili wapate msaada.

Katika kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Machi 2023 jumla ya matukio ya ukatili 15,901 yameripotiwa Polisi ambapo ni kesi 671 tu ndio zilifikishwa mahakamani.

Pamoja na takwimu za Jeshi la Polisi kuhusu hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani kuonesha kupungua kwa matukio ya ukatili yaliyoripotiwa mwaka 2021 ikilinganishwa na miaka iliyopita, bado tumeendelea kushuhudia matukio ya vitendo vya ukatili mara kwa mara kwenye vyombo vya habari hususani kupitia mitandao ya kijamii.

Aidha, ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini.

ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hasa ukatili wa kingono, kimwili na udhalilishaji kwenye mitandao kwa kuboresha madawati ya jinsia, kuweka mifumo rahisi ya kuripoti na kudhibiti ukatili. Pia, tunaishauri Serikali kuunda tume maalumu ya kudhibiti ukatili wa kijinsia na kuhakikisha vyombo vya mahakama vinawezeshwa kimafunzo na kimfumo ili kusimamia kesi za ukatili kwa haraka na uhakika.

4. Kuongezeka kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Ni jambo linalosikitisha kuona kasi kubwa ya kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kila mwaka. Serikali haionekani kustushwa na ongezeko hili lisilo la kawaida na kuchukua hatua stahiki kuondokana na tatizo lenyewe.

Tanzania imeridhia kutekeleza Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto (UNCRC). UNCRC ni chombo cha kisheria ambacho kinaelekeza na kinasisitiza haki za msingi za watoto duniani pote na hii inahusisha, haki ya kuishi, kujiendeleza/kuendelezwa kwa kadiri ya uwezo wa mtoto, kulindwa dhidi ya madhara na mazingira yanayoweza kumdhuru, kumnyanyasa na kutumiwa kwa njia ya kudhulumiwa; kushiriki kikamilifu katika maisha ya kifamilia, kitamaduni na kijamii.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi imefikia jumla ya watoto 218,369 (Me 85,699 na Ke 132,670) hawa ni wale tu waliotambuliwa na wizara kati ya 2,398,354 wanaoishi katika mazingira magumu nchini.

Katika mwaka huu bajeti iliyotengwa na wizara kiasi cha Bilioni 3.6 kwa ajili ya kukabiliana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na ukarabati wa mahabusu za magereza ya watoto mahabusu ya Upanga, Arusha, Mbeya, Moshi na Tanga, Kufuatilia utoaji wa huduma katika makao ya watoto, kukarabati shule ya maadilishi ya Irambo. Utengwaji wa bajeti hauzingatii kiini kinachosababisha kuwepo kwa watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Tunaishauri serikali kuja na mpango wa kumaliza migogoro ya wanandoa, kukabiliana na umaskini na kusimamia huduma bure za afya, lishe na makaazi bora.

5. Kasi ndogo ya Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi
Waziri ametoa Takwimu kuwa jitihada za serikali za kuwezesha wanawake kiuchumi. Wizara inaendelea kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya wanawake (WDF) ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi April 2023 ni Mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 664.5 ilitolewa kwa wanawake wajasiriamali 104 tu. Kwa Mujibu wa Sensa ya Watu na makaazi ya mwaka 2022 Tanzania ina jumla ya wanawake Milioni 31.6 idadi hiyo ya uwezeshwaji inayofanywa kwa wanawake kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya wanawake ni ndogo mno.

Kwa mwenendo huu Serikali inaweza kuchukua zaidi ya miaka mia moja kukamilisha malengo ya kuwainua wanawake wote.
Ni muhimu suala la uratibu wa uwezeshwaji wa wanawake nchini utengenezewe mwongozo na utaratibu utakaotumika ili kila mwanamke anapohitaji msaada ajue utaratibu utakaomwezesha kupata msaada kwa haraka na uhakika.

Pili, Tunaitaka Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake (WDF) Ili iweze kuwawezesha wanawake wengi zaidi nchini.

6. Huduma bora za afya na uzazi salama kwa wajawazito na mama na watoto.
Mazingira rafiki ya huduma za uzazi ni haki ya kila mwanamke na mtoto. Sera ya kutoa huduma za afya bure kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano (5) na wazee, ni kiini macho tu yaani haitekelezwi kwa ufanisi. Kutotekelezwa kwa ufanisi unachangia pia kutokana na uhaba wa miundombinu ya msingi katika vituo vya afya (zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za rufaa za mikoa).

Aidha ukosefu wa vituo vya afya kwenye baadhi ya vijiji vinafanya umbali mrefu kufikia huduma ya afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungulia njiani, kukosa huduma bora na salama za uzazi na vifo vya mama wajawazito. Takwimu za MTUHA zinaonesha kuwa katika kipindi cha April 2022 hadi kufikia Machi 2023 kuna jumla ya Vifo 943 vya wanawake waliojifungua katika vituo vya afya na hii, haijumuishi vifo zinavyotokea kwa ngazi ya jamii.

Pamoja na hali hiyo, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wenye miaka zaidi ya 60 wana haki ya kupata matibabu bure kwa mujibu wa sera ya matibabu bure kutoka katika vituo vya afya vya serikali.

Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa na changamoto kubwa, tathmini yetu inaonyesha kuwa wastani wa asilimia 40 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanalazimika kulipia matibabu. Vilevile, kwa wajawazito wanalipishwa matibabu na inatokea hivyo kwa watu wenye miaka zaidi ya 60 hulazimika kulipia huduma hizo tofauti na utaratibu uliopo.

Tunaitaka Serikali ifuatilie kwa makini utekelezwaji wa sera hii ili kuhakikisha kuwa walengwa – ambao ni watoto, wajawazito na wazee wanapata haki zao za msingi.

7. Kuongezeka kwa matukio ya mauaji na vifo vya wanandoa na wanajamii.
Hali ya usalama ya wananchi hususani wanandoa na watu wenye mahusiano ya kimapenzi imezidi kuwa katika hali mbaya kwa takribani miaka ya hivi karibuni kumeripotiwa zaidi ya matukio makubwa 5 ya mauaji ya wapenzi au wanandoa ama wanafamilia kwa sababu za wivu wa kimapenzi au kukosa maelewano katika ndoa/familia.

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2021 watu 15,131 walifanyiwa ukatili wa kijinsia huku ripoti hiyo ikionyesha ongezeko la mauaji kwa wanawake walio katika ndoa.

Ripoti iliyotolewa Septemba 2021 na jarida la Afrika kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia Tanzania miongoni mwa wanandoa, imeonyesha kuwa, asilimia 46 ya wanandoa hufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambapo asilimia 36 walifanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 32 walifanyiwa ukatili wa kisaikolojia na asilimia 13 walifanyiwa ukatili wa kingono.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2022 inaonesha kuwa zaidi ya Asilimia 35 ya vifo vya wanawake husababishwa na wenza wao. hata hivyo Utafiti uliofanywa na TDHS umeonesha kuwa katika kila wanawake 10 wanawake 3 wamewahi kufanyiwa vitendo vya ukatili.

ACT Wazalendo tunaishauri serikali kupitia jeshi la polisi kuimarisha uwezo wa kubaini matukio ya uhalifu na kuweka mazingira rafiki ya wahanga kutoa taarifa na taarifa kufanyiwa kazi.

8. Mazingira magumu ya wafanyabiashara wadogo na ushirikishwaji katika utungaji wa sheria ya Wamachinga.
Tumesikiliza hotuba ya waziri, tumeona mikakati iliyowekwa kuhusu wamachinga ni kwa ajili ya kuimarisha ofisi za viongozi wa wamachinga na sio katika kuboresha mazingira ya Wafanyabiashara wadogo (wamachinga, mamalishe, na wajasiriamali wengine) bado hayajawekewa mkakati wa kuondoa changamoto zao.

Sekta ya biashara ndogo ambayo ina mchango mkubwa sana nchini kwenye pato la taifa wastani wa asilimia 22 na mchango wake kwenye sekta ya ajira ni wastani wa asilimia 14 ya nguvu kazi nchini zinapatikana kwenye biashara ndogo.

katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Wizara ilitengewa shilingi Bilioni 22.92 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) lakini hadi kufikia mwezi Aprili 2023 fedha hizo hazijatolewa kabisa kwenda kwa wafanya biashara wadogo (Machinga) katika bajeti ya wizara 2023/24 wizara imetenga Bilioni 18.5 ambayo ni pungufu ya Bilioni 4.4 ya kiwango kilichotengwa mwaka jana.

Mwezi Mei 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tanzania aliahidi kutoa Shilingi milioni 10 kila mkoa kwa ajili ya kujenga Ofisi za wamachinga nchi nzima, katika hotuba ya wizara Bungeni waziri Ndg. Dorothi Gwajima ameliambia Bunge kuwa Fedha hizo Milioni 260 zimetolea ila hakuliambia bunge ni Ofisi ngapi zimeshajengwa na zimejengwa katika mikoa gani na hajaonesha ni kwa namna gani Wafanyabiashara wadogo wenyewe wameshirikishwa katika hilo.

Hali ya sasa wafanyabiashara hawaonekani wakilindwa kisheria au shughuli zao kutambulika kama halali kwenye mchango wa uchumi wetu. Kwa, kifupi Wafanyabiashara wadogo hawachukuliwi kama injini ya maendeleo ya miji na majiji. Uamuzi wa kuwapanga Wafanyabiashara wadogo umetikisa uaminifu wao kwa taasisi za kifedha.

Matukio ya kuungua moto kwa masoko ya Wafanyabiashara wadogo yamesababisha hasara kubwa sana kwa Wafanyabiashara.
Tafiti nyingi, zinaonyesha uhusiano uliopo katika shughuli za Wafanyabiashara wadogo na ukuaji na uendelezaji wa viwanda vidogo nchini. Asilimia 47 ya biashara ndogo zinahusisha bidhaa za kilimo ambazo zinaongezwa thamani.

ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Serikali kwa kuziweka pamoja na Wizara ya Maendeleo ya jamii, Viwanda na uwekezaji na TAMISEMI kusikiliza na kuondoa vikwazo kwa wafanyabioashara wadogo. Pia, katika mchakato wa kutunga kwa sheria ya wamachinga nchini, ushirikishwaji wa wamachinga uwe wa hali ya juu.

Hitimisho.
Bajeti ni chombo muhimu sana katika kupima vipaumbele vya matumizi ya fedha za umma katika kukabiliana na changamoto za wananchi. Katika kutazama bajeti ya mwaka huu haiakisi uhalisia wa mahitaji ya wizara. Wizara imetenga bajeti kama vile ni idara tu ya wizara kama ilivyokuwa mwaka juzi ilipokua Idara chini ya Wizara ya Afya.

Ni muhimu kwa Serikali kuona mikakati yake inatafsiriwa kwenye ugharamiaji wa mikakati hiyo kupitia bajeti. Aidha, changamoto za mauaji, ukatili dhidi ya wanawake, wazee na watoto ni muhimu zopewe kipaumbele kama tulivyoshauri.

Serikali lazima iweke mkazo maalum katika kudhughulika na masuala ya wamachinga, kushindwa kushughulikia kiini Cha changamoto wanazokabiliana nazo nazo wafanyabiashara wadogo ni kiashiria kuwa kundi hili kubwa lenye mchango mkubwa kwa Taifa linapuuzwa.

Ndg. Janeth Joel Rithe
Msemaji wa Sekta ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto
ACT Wazalendo
18 Mei, 2023.

IMG-20220905-WA0020.jpg
 
Back
Top Bottom