Jaji Warioba: Siioni Katiba Mpya

lidoda

JF-Expert Member
Apr 27, 2008
641
574

Awasubiri wabunge mitaani,

Prof. Maina aonya nguvu ya FFU

Jaji Joseph WariobaMWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hali ya mambo yanayoendelea bungeni mjini Dodoma, haoni matumaini ya kupatikana Katiba mpya na hali hiyo imemkatisha tamaa.

Wakati Jaji Warioba akikatishwa tamaa na uwezekano wa kupatikana Katiba mpya, Mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini, Prof. Chris Maina, ameeleza kuwa watu wanaotaka kuzuia historia kuandikwa kwa kutumia askari wa kutuliza ghasia, hawatafanikiwa kwani historia itawaumbua.

Jaji Warioba na Prof. Maina, walitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa Dk. Sengondo Mvungi, pamoja na hafla ya kutimiza miaka 19 ya kuanzishwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Katika matukio hayo mawili yaliyoendana na uzinduzi wa kitabu cha historia ya maisha ya Dk. Mvungi, Jaji Warioba alisema, tangu mwanzo matumaini yalikuwa ni nchi kupata Katiba mpya kwa maridhiano na kwamba baada ya mchakato huo kutekwa na wanasiasa, matumaini hayo yametoweka.

Alisema, badala yake wanasiasa hao wameacha kuangalia maslahi ya taifa na kutegemea uamuzi wa kura badala ya nafasi ya maridhiano kupewa kipaumbele.

"Sina hakika kama tutapata Katiba mpya, kwani rasimu itakayopendekezwa na Bunge Maalum haitapigiwa kura hadi mwaka 2016, kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake," alisema na kuongeza.

Kampeni ya uchaguzi mwakani, Katiba mpya itakuwa ajenda inayoweza kuigawa nchi.

Akizungumzia rasimu iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba, Jaji Warioba alisema limecha maoni yaliyotolewa na wananchi na kuweka yak wake, jambo ambalo ni hatari.

Jaji Warioba, alisema licha ya baadhi ya mambo kuonekana kukubaliwa katika rasimu hiyo, bado yako mengi ya msingi yamewekwa pembeni na kwamba, wabunge waliopitisha uamuzi huo wanapaswa kutoa maelezo ya kutosha kwa wananchi.

Aliyataja baadhi ya mambo ambayo mwelekeo wake ni kukataliwa na wananchi, ni pamoja maadili ya viongozi.

"Katika maadili ya viongozi, wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi, kwa kuwa wanachukizwa na kuporomoka kwa maadili," alisema.

Kutokana na maoni ya wananchi, Jaji Warioba alisema Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika utangulizi wa rasimu, ambako misingi katika Katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani, lakini kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa nayo ni pamoja na utu, usawa, umoja na mshikamamo.

Aliongeza kuwa, wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye Katiba, ambazo ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa ya Kiswahili.

Hata hivyo, Jaji Warioba alisema ni jambo la kusikitisha Bunge Maalum limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora na kuongeza kuwa, kila mtanzania anapaswa awe na tunu hizo.

Madaraka ya wananchi

Kuhusu madaraka ya wananchi, alisema Katiba inatungwa na wananchi na kwa maoni yao, wanataka wawe na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhiki na uwakilishi wake.

Akilifafanua hilo, alisema ni kweli siyo jambo la kawaida kumwondoa mbunge katikati ya kipindi au kumwekea ukomo, lakini kwa sababu ya rushwa katika uchaguzi, wananchi wanaona ni vema watumie madaraka yao kuwajibisha wabunge wao.

Katika hilo, alisema inawekana kwa kuwa tayari Bunge lina kanuni za kuwajibisha wabunge, vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa, vivyo hivyo wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo.

Mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili

Jaji Warioba, alisema pendekezo la kumwondoa Rais na Mawaziri kutoka kwenye Bunge, limekataliwa kwa sababu kumezoeleka mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi za Jumuiya ya Madola.

"Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge, kwani kwenye mfumo wa kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji bali madaraka hayo yako mikononi mwa Waziri Mkuu, ambaye ni mbunge na hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India, Canada, Australia na New Zealand.

"Ikumbukwe kwamba, Tanzania ina mfumo wa urais, ambapo Rais ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu, Amiri Jeshi Mkuu, hivyo Rais na Mawaziri wake kuwa sehemu ya Bunge ni kuchanganya mamlaka, ambapo hali hii ndio inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya Bunge na pia Bunge kuingilia mamlaka ya Serikali," alisema na kuongeza.

Tumeona wakati mchakato huu wa Katiba jinsi madaraka yanavyoingiliana, ambapo wakati wa kutunga sheria ya mabadiliko ya Katiba, tuliona jinsi Bunge lilivyokuwa linafanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kutunga sheria.

"Lakini baadaye Rais anafanya mazungumzo na watu nje ya Bunge na baadaye Bunge linalazimika kubadili maamuzi ambako hata Bunge Maalum la Katiba limetendewa hivyo… kwa maana hiyo, Bunge halina madaraka kamili na Rais anaweza kuingilia wakati wowote," alisema.

Alisema, katika Bunge la kawaida mawaziri wanawabana wabunge kupitisha mambo ya Serikali na wabunge mara nyingine wanaingilia kazi za Serikali, kwa mfano Kamati za Bunge kwenda moja kwa moja kwenye taasisi za Serikali kutoa maagizo au maazimio kwenye maeneo ya utendaji.

Hivyo, anachoona dhana ya kutenganisha madaraka ya mhimili ni jambo la msingi sana katika mfumo wa demokrasia na nchi nyingi zimebadili Katiba ili kufanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.

Muundo wa Muungano


Katika suala la Muungano ambalo ndilo limeteka nafasi kubwa ya majadiliano tangu mchakato huo uanze, Warioba alisema pamoja na Tume kuorodhesha kero zaidi ya 40, baada ya uchambuzi wa kina ilionekana kero nyingi ama zimepatiwa ufumbuzi au zinaweza kurekebishwa na tume ilichambua tu zile ambazo zilionekana ni nzito.

Alibainisha kuwa, lalamiko kubwa kwa upande wa Tanzania Bara ni Zanzibar kuvunja Katiba ya Muungano, ambako alihoji kuwa kutokana na yale yaliyopitishwa na Bunge la sasa ni kweli Zanzibar itakubali sheria zinazotungwa na Bunge kutumika nchi nzima bila masharti.

"Swali lingine ni kama kweli Zanzibar imekubali Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu ziwe mamlaka nchi nzima bila masharti, itakubali kuondoa mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2010 na suala la Bunge kupendekeza kwamba raia awe na haki kupata ardhi. Je Zanzibar wamekubali raia wote wawe na haki hiyo kwa upande wa Zanzibar," alihoji.

Awasubiri wabunge mitaani

Kuhusu shutuma mbalimbali zilizoelekezwa na wajumbe wa Bunge Maalum kwa wajumbe wa Tume ya iliyokuwa ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema baada ya wajumbe hao kumaliza kuongea katika vipaza sauti vya Bunge, wanapaswa kutambua kuwa wanawasubiri mitaani.

"Wao wanasema Jaji Warioba na wajumbe wenzake ni ‘Shiidaah' tena wanasema Warioba ni shida kubwa, mimi nawaambia wanakaribia kuacha vipaza sauti vya Bunge waje huku mitaani wawaeleze wananchi yale waliyopitisha na sisi tutabaki katika msimamo wa kutetea maoni ya wananchi, hapo ndipo watakapojua kama walio na shida ni sisi au wao," alisema.

Maina aonya nguvu za FFU

Kwa upande wake, Prof. Maina, alisema kwa jinsi nchi inavyoshuhudia vioja vya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ndiyo umuhimu wa tume iliyoongozwa na Jaji Warioba unavyoendelea kujidhihirisha.

Alisema, wanaoipinga rasimu ya pili ya Katiba wanaushangaza umma wa Watanzania kwa kueleza kuwa wabunge 75 ni mzigo kwa serikali huku wakishindwa kuainisha wingi wa kuwa na wabunge 360 na gharama zake.

"Leo wanaposema wabunge 75 ni gharama kuliko 360 hauwezi kuwaelewa, wanaposema mawaziri 15 ni gharama zaidi ya 60 pia hatuwaelewi na hawa wanataka kuficha historia na katika hili… wanadiriki kutumia FFU lakini hawajui kuwa historia haifichwi na ina kawaida ya kuumbua na itawaumbua hata wakiwa bado hai," alisema Profesa Maina.

Chanzo:Tanzania Daima
 
Ahsante sana Mkuu kwa kuiweka hii hapa. Ahsante sana Warioba kwa kuamua kuingia mtaani kupambana na hawa Mapanya na Mafisi wanaojali maslahi yao na si yale ya Tanzania na Watanzania. Paragraph ya mwisho katika article hii inaonyesha jinsi ambavyo Serikali tatu zitakuwa na gharama nafuu kwa Tanzania ukilinganisha na Serikali mbili kwa kuwa na idadi ndogo ya Wabunge na Mawaziri kitu ambacho kitapunguza gharama za uendeshaji kwa kiwango kikubwa.
 
"Kusikia kwa kenge mpaka damu imtoke masikioni...! " Muache Sitta na genge lake wamalizie wizi wao huo wa pesa zetu halafu wakione cha mtemakuni...Hawa ni kama viwavi ndani ya shamba la mahindi. Tutalipiga shamba zima dawa tuone kama kuna kiwavi atakaesalimika.....
 
Naona hao wabunge hawatathubutu kuja mitaani kwa wananchi bali wataingia mitini.
 
nimeamini ccm wanatumia akili ndogo kwenye mambo mazito katika nchi hii hasa katika mradi wa ccm wa bunge la katiba unaoendelea mjini dodoma ni dhahiri kuwa watanzania karibia wote wanapinga mradi huu kwani ni uwiz na ujambazi wa pesa za umma unaofanywa mchana kweupe ukiongozwa na wakuu wa nchi na wananchi wanapotaka kupinga ujambazi huu ccm mnatumia FFU kulinda ujambazi kaeni mkijua wananchi wametambua kuwa mnajivunia hao ffu kwahyo wanatafuta mbinu za kutatua tatizo *miaka kumi ijayo mtavuna mnacho panda kwa ubabe kwa akili ndogo nchi haitatawalika
 
Hili bandiko linazidi kufufua matumaini ya watanzania ya kwamba; kuna siku katiba yao itapatikana! Samweli Sitta na genge lake la kihuni wameteka mchakato kulinda ufisadi wao, lakini nguvu ya umma 2015 itawasambaratisha ccm.
 
Warioba kaongea kama mwanaume ,sio yule mwenyekiti ambaye kila kikao yeye ni cdm mara ukawa na msg 50 za matusi per day.
 
MKUU kwa tafsiri nyingine ni kwamba warioba atakuwa upande wa NDIZI na Sitta atakuwa Upande wa chungwa
 
Warioba sasa atulie. Amebwata mno! Katiba tayari atake asitake

Mkuu hata hili la katiba na umuhimu wake bado haujajua na unaongea bila wasi wasi kama katiba tayari?

1.Sitta akimaliza kazi yake atamkabidhi Rais JK

2.Rais JK atampa Rais ajaye ili aamue kama ataendelea na rasimu ya Sitta au la

3.Bunge la JMT ka November litafanya marekebisho kuhusu kuingiza kipengele cha Tume huru ya Uchaguzi;Rais apate asilimia zaidi ya 50+1 na matokeo yalalamikiwe Mahakamani

4.Uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa na uchaguzi wa Rais na Wabunge mwakani utatumia katiba ya sasa

5.Rais ajaye akikubali kuendelea na katiba ya Sitta ndipo itapelekwa Bungeni kupitishwa then kwa wananchi kwa referendum kuanzia mwaka 2016

6.Wananchi wakiipitisha inarudi tena kwa Rais kusainiwa kuwa katiba kamili

7.Rais ajaye asipo kuwa interested ina maana Sitta alitumia tu hela zetu

8.Rais akikubali mchakato uendelee lkn wananchi wakiikataa kwenye kura za maoni hamna katiba!!

Kwa maelezo haya marefu bado unamuunga mkono Sitta kuendelea na vikao Dodoma?
 
Bunge ndiyo central pivot kwenye maamuzi yote hapa nchini. Hadi siku tutakapokuwa na bunge huru ndipo tutaweza kutengeneza katiba...
 
..."wao wanasema Jaji Warioba na
wajumbe wenzake ni ‘Shiidaah’ tena
wanasema Warioba ni shida kubwa,
mimi nawaambia wanakaribia kuacha
vipaza sauti vya Bunge waje huku
mitaani wawaeleze wananchi yale
waliyopitisha na sisi tutabaki katika
msimamo wa kutetea maoni ya
wananchi, hapo ndipo watakapojua
kama walio na shida ni sisi au wao,”
alisema...

ALIYEYAKOROGA LAZIMA AYANYWE
 
kibaraka/ umekuwa mbwa koko wa kihindi

Kwa jina la Mungu wewe sio mzima au upeo wako ni sawa na ubungo wa kuku! kama hujui manufaa ya katiba na ni kwa ajili ya nani bac aidha elimu yako utata, hupendi kusoma, au uliwahi kuugua ugonjwa wa kimirembe mirembe!:angry:
 
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.

Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na muungano. “Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na rasimu iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.

“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda Katiba iliyoboreshwa. Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge Maalumu haitapigiwa kura hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,” alisema.

Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka kesho Katiba Mpya itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato ukaanza upya.”

Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati yake imefuta ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha ibara 47, kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.

Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa kuwa si mambo ya muungano.

Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili kama ilivyo sasa na kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia saa 1:02 kufafanua umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu iliyotolewa na Bunge la Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la Katiba wana msemo wao kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa watakapomaliza vikao vya Bunge hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea mtaani walipo wananchi ndiyo watajua nani ni ‘shida’, kati yake na wao.

Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili kanuni ili kuruhusu wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo kwa baruapepe (e-mail) na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba alisema, “Utaratibu huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata mimi nimeanza kukata tamaa.”

Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu waliohudhuria kongamano hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila mjumbe wa tume hiyo alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini waliweka kando mawazo yao baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya Katiba wanayoitaka.

Katika maadhimisho hayo, Jaji Warioba pia alizindua kitabu cha marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi anapumua Katiba’. Dk Mvungi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja wa waanzilishi wa LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini alikopelekwa kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani kwake.
Maadili ya Viongozi wa umma

Kuhusu maadili ya viongozi wa umma alisema, “Wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi. Kutokana na maoni ya wananchi Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani.”

Alisema kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa ambayo ni; utu, usawa, umoja na mshikamano na kwamba wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye katiba ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa (Kiswahili ).

“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe mzalendo, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania anatakiwa aenzi umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alihoji.

Alisema tunu za taifa ndiyo msingi wa utamaduni na maadili ya taifa, kwamba mwelekeo wa taifa utategemea jinsi wananchi wanavyoenzi misingi mikuu na tunu.

Aliponda kitendo cha Bunge la Katiba kutoweka miiko ya uongozi kwenye Katiba wakati kila siku viongozi wanalalamika juu ya rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi.

“Katika bara la Afrika, nchi kama Afrika Kusini, Namibia na Kenya zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba. Hapa kwetu sheria tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi. Sijui kwa nini Bunge la Katiba wameondoa hili,” alisema.

Madaraka ya Wananchi

Jaji Warioba alipinga kitendo cha Bunge la Katiba kuondoa kipengele cha wananchi kuwa na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhishwi na uwakilishi wake bungeni, mbunge kutokuwa waziri ili aweze kuwawakilisha vizuri na ukomo wa mbunge kuwa vipindi vitatu .

“Bunge lina kanuni za kuwawajibisha wabunge na wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo. Vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa wabunge wao katikati ya kipindi. Wananchi nao wanataka watumie madaraka yao,” alisema.

Mgawanyo wa madaraka

Akizungumzia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya Bunge, Serikali na Mahakama, alisema pendekezo lao la kumwondoa rais na mawaziri kutoka kwenye Bunge linakataliwa kwa sababu nchi imezoea mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi nyingi za jumuiya ya madola.

“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge. Kwenye mfumo wa kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji. Madaraka hayo yako mikononi mwa Waziri Mkuu ambaye ni mbunge. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India, Canada, Australia, New Zealand,” alisema.

Akitolea mfano mwingiliano huo alisema wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bunge lilitunga sheria lakini baadaye Rais alifanya mazungumzo na watu nje ya bunge na baadaye bunge likalazimika kubadili uamuzi.

“Tanzania ina mfumo wa urais ambapo rais ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu na amiri jeshi mkuu. Rais na mawaziri wake kuwa sehemu ya bunge ni kuchanganya mamlaka. Hali hii inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya bunge na pia bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,” alisema.

Aliongeza, “Nchi nyingi zimebadili Katiba zao ili kutenganisha madaraka ya mihimili. Jirani zetu wa Msumbiji na Kenya wamefanya hivyo. Kenya imefanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.”

Muungano

Huku akitaja kero 20 za muungano, 11 za Zanzibar na 10 za Tanzania Bara zilizotajwa na wananchi wakati wa kukusanya maoni, Jaji Warioba alisema, “Ingawa Rasimu ya Bunge Maalumu limerudisha madaraka ya rais kuigawa nchi hiyo peke yake haitoshi. Mambo haya ni magumu kubadilika kwa upande wa Zanzibar.”

Aliongeza kuwa ili kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ni lazima mabadiliko yapitishwe kwa theluthi mbili au zaidi ya Wawakilishi.
chanzo mwananchi





 
Hapa ndipo watanzania wajue kuwa ccm haina shida na wananchi kujua wanataka nini,kikundi kidogo kinaamua wananchi waufyate.
Bila kuiondoa ccm madarakani tusitarajie jipya,watu wanaoingia madarakani kwa kuhonga wapiga kura za maoni,wapiga kura uchaguzi mkuu watawezaje kukujali?
Hata bunge la katiba kazi kubwa ilikuwa kutafuta fedha za kukampeni 2015 ndio maana walikataa kusitisha bunge la katiba ili wapate za kazi ya kuhonga!
Wabunge wa ccm na madiwani wao ndio kazi inayosumbua halmashauri zetu!
 
Back
Top Bottom