Isome hii kuhusu Mwigulu Nchemba

SOEN

JF-Expert Member
Mar 8, 2023
407
179
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba(Mb), ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhakikisha inaunganisha Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) na Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki katika Utoaji wa Huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GIMIS) ili kurahisisha mchakato wa ununuzi Serikalini.

Waziri Nchemba akitoa maelekezo hayo wakati akizindua wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki katika Utoaji wa Huduma za Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini ujulikanao kama GIMIS (GPSA Intergrated Management Informationm System), uliofanyika katika katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina Jijini Dodoma.

Alisema PPRA iunganishe mifumo hiyo haraka iwezekanavyo kwa kuwa Mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala, Ofisi za mikoa na Halmashauri za Wilaya nchini katika kupata huduma za GPSA.

“Mhe. Rais – Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mifumo ya Serikali isomane hivyo ni muhimu mifumo mingine ihakikishe inaunganishwa na GIMIS ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini” alibainisha Mhe. Nchemba.

Alisema kuwa Mfumo wa GIMIS utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini kwa kuwa majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa ndani ya mfumo huo.

Aidha, Dkt. Nchemba alitoa wito kwa Taasisi nunuzi kuhakikisha wanatumia huduma za GPSA kwa kuwa Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake inazitaka kupata huduma na vifaa mtambuka kupita GPSA.

Aliipongeza GPSA kwa kukamilisha ujenzi wa mfumo huo na majengo ya ofisi na vituo vipya vya mafuta vya Songwe, Simiyu, Pwani na Dodoma pamoja na kufanya ukarabati katika ofisi za mikoa 17 na kusimika matenki ya mafuta katika mikoa 12, kwa kuwa hatua hiyo itaongeza mapato na morali ya utendaji kazi kwa watumishi.

Mhe. Nchemba pia aliipongeza GPSA kwa kuendelea kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo katika kipindi cha miaka mitano mpaka kufikia mwaka 2022/2023 imechangia kiasi cha Sh. bilioni 11.9.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alisema mfumo huo umeshaunganishwa na Mfumo Mkuu wa Serikali ambao unaiwezesha mifumo kubadilishana taarifa na umeshaanza kubadilishana taarifa na baadhi ya mifumo ya taasisi za umma ikiwemo Mfumo wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG) na Mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Serikali.

Aliongeza kuwa jitihada zinaendelea kuunganisha Mfumo huo na mifumo mingine ya Serikali kulingana na mahitaji ya ubadilishaji wa taarifa na kubainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria yatawezesha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kusimamia masuala ya Serikali Mtandao kwa ufanisi.

Aidha, aliziasa taasisi nyengine za umma ambazo bado zinakiwango kidogo cha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kuongeza juhudi katika matumizi ya tehama katika utekelezaji majukumu yao kama Sheria ya Serikali Mtandao inavyoelekeza.

“Ni wajibu wa kila taasisi kuweka jitihada za makusudi ili kuhakikisha zinafaidika na fursa zinazotokana na matumizi ya tehama ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kutimiza adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuelekea katika Serikali ya Kidigitali”, alibainisha Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri GPSA, Bi. Dorothy Mwanyika alisema kuwa mfumo huo utatoa huduma katika ununuzi wa vifaa vya ofisi, mafuta katika vyombo vya moto, huduma ya ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali katika maeneo ya bandarini, viwanja vya ndege na mipakani.

Alibanisha kuwa mfumo huu utatumika katika huduma ya ununuzi wa magari ya Serikali ikijumuisha kuanzia maombi ya vigezo, kibali cha ununuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, utoaji wa hati za madai ya ununuzi wa chombo husika pamoja na kuwezesha uombaji wa kibali cha usajili kutoka Wizara ya Fedha na usajili wa chombo cha moto husika utakaofanywa na Wizara ya ujenzi.
 
Back
Top Bottom