Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,997
Na. M. M. Mwanakijiji
Huwezi kuamini kuwa haya niliwahi kuyaona pale mtaani kwetu. Wazazi wawili ambao walikutana ujanani baada ya kila mmoja kupoteza mtoto wa kuzaa. Walipofunga ndoa Mungu akawajalia kupata mtoto mwingine, ambaye wote walimpenda na waliona fahari na baraka kuwa naye. Kwa muda mrefu wazazi wale walikuwa wakifanya kumbukumbu ya watoto wao waliopoteza lakini walifanya sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa mtoto wao yule mmoja mpendwa. Walifanya hivyo kwa muda mrefu lakini baadaye wazazi wale waliacha kumfanyia sherehe ya kuzaliwa yule mtoto wao aliye hai; walianza kufanya sherehe za kuzaliwa kwa watoto wao marehemu.
Jambo hili lilikuwa linatushangaza sana pale mtaani. Hatukuelewa kwanini walikuwa wanafanya vile. Siku moja hata hivyo wazee pale mtaani waliamua kuwaendea wale wazazi na kuzungumza nao. Wazazi wale walisema tu kuwa ilikuwa ni gharama sana kufanya sherehe ya mtoto aliye hai; lakini kwa vile kila mmoja aliwahi kuwa na mtoto wake aliyempenda sana kabla ya kukutana basi kila mmoja aliona kila inapofika kumbukumbu ya kuzaliwa kwa watoto marehemu basi washirikiane kuadhimisha siku hiyo. Wazee waliwaambia kuwa ule ulikuwa ni mwiko; walikuwa wanamchulia mtoto wao aliye hai.
Wale wazazi walisikiliza kwa makini na kuyapa uzito maneno ya wazee wa mtaa wetu (mimi nikiwa mmoja wapo). Wakaamua kuanzia mwaka unaofuatia kutokufanya tena sherehe za kumbukumbu za watoto marehemu na kuanza mara moja kufanya sherehe kubwa ya kuzaliwa kwa mtoto wao yule aliye hai. Wale marehemu walibakia kwenyey picha na kwenye mioyo yao; na kama wakitaka kuadhamisha basi waliadhimisha bila kufanya sherehe yoyote kubwa. Ila siku ya kuzaliwa kwa mtoto wao waliamua kuifanya sherehe kubwa, ya furaha na mtaani pote tulikuwa tukialikwa na tuliungana nao katika furaha yao.
Nilipotafakari tukio hili pale mtaani; likanikumbusha tukio jingine nimewahi kulisikia la watu waliokuwa wanafanya kitu kama hiki… Nitawasimulia siku nyingine.
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com