*Makada wake wakamatwa kwa kuchoma bendera za Chadema
*Mukama awaangukia wananchi, adai ametumwa na Kikwete
*Prof. Safari awajibu wanazuoni wa kiislamu kuhusu DC
*Nyumba ya Katibu Kata wa CUF Nyandekwe yachomwa moto
Na Waandishi Wetu, Igunga, Dar
JESHI la Polisi Wilayani Igunga mkoani Tabora, linawashikilia kiongozi mmoja na kada mwingine wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kosa kuchoma mabango ya picha ya mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kushusha bendera za chama hicho.
Waliotiwa mbaroni juzi jioni ni Katibu wa Msaidizi wa CCM ambaye pia ni Mhasibu wa CCM Wilaya ya Sikonge, Bw. Bakari Luasa na Bw. Rajabu Said ambao walikamatwa katika kijiji cha Chagana Kata ya Itumba.
Viongozi hao, walikamatwa saa 5:00 asubuhi juzi muda mfupi kabla ya msafara wa mgombea wa CCM, Dkt. Dalaly Kafumu na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Wilson Mukama na viongozi wengine kuwasili eneo hilo.
Bw. Mukama na msafara wake walikuta tafrani baada ya wafuasi wa Chadema kuwashikilia viongozi hao na kuwadhiti hadi walipowakabidhi kwa polisi.
Makada hao wa CCM walipandishwa kwenye gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili PT 1946 hadi Kituo cha Polisi mjini Igunga ambako walikabidhiwa kwa Mkuu wa
Kitengo cha Tathmini, Ufuatiliaji na Upelelezi wa Makosa ya
Jinai katika uchaguzi huu, Bw. Isaya Mngulu.
Wakazi wa kijiji hicho wakiwamo wafuasi wa Chadema walikuwa na marungu, mapanga na mikuki ili kuwashughulikia, lakini jitihada zilizofanywa na kiongozi mmoja wa Chadema, Bw. Kibende Mwangombe ziliwatuliza.
Mwangombe aliiambia Majira kuwa waliokamatwa walifika katika
eneo hilo kufanya uhalifu wakiwa na mtu mwingine ambaye jina lake halikufamika mara moja, lakini alikimbia baada ya ugomvi kuanza.
Siku zote CCM wemekuwa mabingwa wa kueneza siasa za
propaganda kwamba Chadema tunafanya fujo, nadhani ninyi
wenyewe mmejionea. Jambo lililonifurahisha ni kwamba viongozi waandamizi wa CCM wamejionea wenyewe, alisema Mwangombe.
Mwenyekiti wa Wazazi CCM Wilaya ya Igunga, Bw. Selemani Majilanga, aliwaomba wananchi na wafuasi wa Chadema wasiwafanyie fujo wahalifu hao.
Nawaomba ndugu zangu wananchi msifanye fujo kwa watu hao, wako
mikononi mwa polisi, basi acheni sheria ichukue mkondo wake, watashughulikiwa kwa taratibu zote zinazostahili, alisema Majilanga.
Baada ya watuhumiwa kuondolewa, mkutano huo, uliendelea huku, Bw. Mukama akijinadi kwa wananchi kuwa ametumwa na Rais Jakata Kikwete kuwaomba wananchi hao kumpa kura za ndiyo mgombea
wa CCM, Dkt. Kafumu ili awe mbunge wao.
Kwa upende wake, Mratibu wa Kampeni wa CCM ambaye pia ni
Katibu wa Fedha na Uchumi, Bw. Mwigulu Nchemba aliwataka
wananchi kutokuchagua wapinzani kwa sababu hawana serikali.
Katika mkutano huo, mwananchi mmoja alilipandisha dumu la
maji machafu lita 20 na kumuuliza mgombea wa CCM, Dkt. Kafumu atachukua hatua gani kuondoa adha ya kukosa maji iliyodumu miaka mingi.
Nimekuletea maji haya unayoone mwenyewe, sisi tunakunywa
maji machafua kiasi hiki, je, ukipata ubunge utafanyaje ili
tuondokane na aibu hii ambayo sasa imeonekana kuwa ya
kawaida kila kukicha, alihoji mwananchi huyo.
Madai ya wanazuoni wa kiislamu
Chadema kimesema kuwa hakiko tayari kujibizana na wanazuoni wa kiislamu bali kinasubiri uamuzi wa mahakama utakaoamua iwapo Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatma Kimario alivuliwa hijabu kwa makusudi alipokamatwa na wafuasi wa chama hicho.
Hatua hiyo ya Chadema imekuja siku moja baada ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini (HAY AT) kukitaka chama hicho kulaani na kumuomba radhi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatma Kimario kwa kumvua sitaha yake na hivyo kumdhalilisha.
Akizungumza na wandishi wa habari Makao Makuu ya Chama hicho, Mjumbe Kamati Kuu ya CHADEMA Prof. Abdallah Safari alisema kuwa chama hicho hakiko tayari kujibizana na wanazuoni hao.
"Si vizuri kuzungumzia mambo ambayo yako mahakamani lakini mahakama itaamua kama DC Fatma alivuliwa hijabu na kama alivuliwa ni kwa makusudi gani, ni uamuzi wa mahakama pekee ndio utaokaomua," alisema Prof Safari.
Alisema kuwa Chadema haina sera ya udini kwa hiyo hakiwezi kushabikia mtu kuvuliwa hijabu kwa makusudi huku akionya viongozi wa dini kuacha kutoa taarifa zinazopotosha ukweli na zinazolenga kuvuruga mshikamano wa Watanzania.
Prof. Safari ambaye ni mwanasheria na mwanazuoni wa kiisalamu, alisema kauli hizo zina lengo la kufarakanisha umma wa waislamu na chama hicho ambacho kinalengo la kuwaondoa madarakani viongozi wanaodaiwa kunuka ufisadi wa CCM
Helkopta kukata anga
Wakati huo huo Chadema kinategemewa kuanza kutumia helkopta kurudia kampeni katika Kata zote 26, lengo likiwa ni kuwakumbusha wananchi na kuwahamasisha kukichagua chama hicho zikiwa zimebaki siku tisa kufika uchaguzi.
Nyumba ya Katibu CUF yachomwa
Nyumba ya Katibu Kata wa Kata ya Nyandekwa, Bw. Hamisi Makala imeteketea kwa moto na vitu vyote vilivyokuwemo ndani.
Mratibu wa CUF Kata ya Nyandekwa, Bw. Emmanuel Ezekiel alisema wakati akifungua mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea wa chama hicho kuwa tukio linahusishwa na mambo ya kisiasa.
Kutoka na matukio ya kihalifu yanayoendelea katika jimbo la Igunga ambako kampeni za uchaguzi mdogo zikiendelea kushika kasi, CUF imewataka wananchi kuacha kujiingiza kwenye siasa za chuki.
Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa wa CUF, Bw. Mbarara Maharagande akimwombea kura mgombea Ubunge wa chama hicho, Bw. Leopold Mahona alisema siasa za kumwaga damu zisipewe nafasi kwani zinajenga uhasama kwa wana Igunga wakati waliosababisha hayo wakitanua Dar es Salaam na familia zao.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga alithibitisha kutokea tukio hilo la moto na kumwagiza Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya kufanya upelelezi haraka.