IGP Sirro afunguka sakata la Mtwara

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema haikuwa kazi rahisi kuchunguza, kuwakamata na kufikishwa kortini maofisa saba wa jeshi hilo mkoani Mtwara kwa tuhuma za kumuua mfanyabiashara wa madini na kumpora mamilioni ya fedha.

Alisema ugumu wa suala hilo ulitokana na kuwahusisha maofisa wa jeshi hilo hivyo uchunguzi wake kuhitaji muda na umakini mkubwa.

IGP Sirro alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu aliyofanya na Mwananchi, ambapo alisema sakata hilo lilianza Oktoba mwaka jana lakini lilifika mezani kwake Januari 17 mwaka huu.

Januari 26, mwaka huu Gazeti la Mwananchi ndilo lililokuwa la kwanza kuandika taarifa za sakata hilo kuwa inadaiwa maofisa hao walimpora mfanyabiashara wa madini, Hamis Mussa Sh70 milioni na kisha kudaiwa kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na kuutupa mwili wake baharini.

Advertisement
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi vililidokeza Mwananchi kuwa mauaji hayo yalifanyika katika hospitali ya Jeshi la Polisi mjini Mtwara Oktoba mwaka jana, lakini taarifa za mauaji hayo zikavuja mwezi uliopita.

Lilikuwa suala gumu
Jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Sirro alisema baada ya kupata taarifa za tuhuma hizo zinazowahusu maofisa wa jeshi hilo walianza kufanya uchunguzi uliowezesha wahusika kufikishwa mahakamani.

“Ukweli hili jambo lilikuwa na ugumu kwa kuwa liliwahusisha maofisa wa polisi, hivyo hata namna ya kwenda nalo lilihitaji weledi na umakini, lakini sisi tumefanya kazi kubwa ambayo nilitarajia ingechukuliwa kwa mtazamo chanya lakini hali ilikuwa tofauti,” alisema.

“Sisi ndiyo tuliochunguza na baadaye tukawa wazi kwa kutangaza kwa umma hatua tulizozichukua dhidi ya maofisa wale, hatuna kitu cha kuficha kwa kuwa anayefanya uhalifu hatumwi na taasisi yetu bali ni tabia yake,” alisema.

Sirro alisema si sahihi watu kulihusisha Jeshi la Polisi na matukio au tabia za ukiukaji wa maadili, haki za binadamu, uhalifu, sheria, taratibu na miongozo ya taasisi hiyo zinazofanywa na baadhi ya waajiriwa.

“Unajua tunaajiri askari si kutoka Marekani au taifa jingine lolote, tunaajiri kutoka kwenye jamii, hivyo kama kuna wahalifu tusitarajie watakosekana kwenye taasisi yetu, la msingi tunalolifanya ni kuwawajibisha wale wote wanaokwenda kinyume” alisema

Akiongea kwa tahadhari, IGP Sirro alisema suala la maofisa hao lilifanyika kwa kificho ndiyo maana lilichukua muda kubainika na kuanza kwa uchunguzi.

Alisema kwa kuwa jambo hilo lilikuwa likiwahusu maofisa ambao walikuwa eneo la tukio, hivyo haikuwa rahisi kwa watu wengine kubaini kilichofanyika lakini kwa kuwa Jeshi la Polisi lina watu wenye weledi wanaoijua kazi yao, walifanikiwa kujua nini kilifanyika

“Asilimia 90 ya tuhuma za mauaji zinazotokea hapa nchini Jeshi la Polisi tunafanikiwa kuwatia mbaroni wahusika ndiyo maana huwa nashangaa ninaposikia malalamiko ya watu yanayoonyesha jeshi letu ni la kulinda wasiofuata maadili ya kazi waliyopewa,” alisema.

Kuhusu kukithiri kwa matukio ya uhalifu, mkuu huyo wa polisi alisema si kazi ya taasisi yake pekee katika kuyazuia, bali kunahitajika ushirikiano wa wadau mbalimbali kwa kuwa nchi inapokuwa na amani shughuli mbalimbali zinafanyika kwa uhuru na ufanisi zaidi.

Sakata lilivyoanza
Taarifa zilizolifikia Mwananchi zilidai kuwa Oktoba mwaka jana, mmoja wa watuhumiwa kati ya saba waliofikishwa mahakamani alikwenda kwa kaimu mkuu wa upelelezi mkoa na kumjulisha kuwa huko Nachingwea kuna mfanyabiashara ameuza madini.

“Huyo mkaguzi alimfuata bosi wake na kumweleza hayo kwamba huyo jamaa (marehemu) ana pesa nyingi inaonekana ameuza madini. Walitengeneza mazingira kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine na kumkamata,” kilidai chanzo kimoja.

Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya kumkamata polisi walifanya upekuzi katika nyumba yake na kumkuta na Sh70 milioni na kumchukua pamoja na fedha hizo na kwenda naye Mtwara mjini ambako walimweka mahabusu kwa siku tatu.

“Baada ya siku tatu walimwachia bila masharti lakini wakawa wamebaki na zile pesa zake na alipotoka akakutana na ndugu yake, akamwelezea sakata zina, ndipo huyo ndugu akasema twende ukadai vitu vyako,” ilielezwa.

Inadaiwa kuwa alivyofika polisi wakamkamata tena na kumshikilia huku ndugu aliyemsindikiza akibaki nje.

“Huyo ndugu yake baada ya kuona jamaa hatoki alienda kumwangalia kule ndani polisi akakuta kama wanahojiwa, akarudi nje lakini baada ya muda alipata SMS (ujumbe mfupi) kutoka kwa ndugu yake akimjulisha kuwa ameachiwa.”

Hata hivyo, tangu siku hiyo mfanyabiashara huyo hakuonekana tena hivyo ndugu wakawa wanaendelea kufuatilia kwa kuwa mara ya mwisho alikuwa mikononi mwa polisi, hivyo wakawa wanashuku huenda kuna jambo limemtokea.

Tangu Oktoba mwishoni mwa Januari fununu zikaanza kwamba polisi walimuua na ndipo uchunguzi ukaanza hadi kuwalenga hao maofisa wa polisi,” kilieleza chanzo chetu.

Wasimamishwa
Februari 4, mwaka huu akiwa Magu njiani kwenda Mara kuhudhuria kilele za maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM Rais Samia Suluhu Hassan alimuagiza Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kuunda kamati kuchunguza tuhuma za mauaji hayo akisema haikuwa sahihi polisi kujichunguza.

Saa chache baada ya agizo hilo, Waziri Mkuu aliunda kamati maalumu ya watu tisa ya kuchunguza mauaji hayo na mengine ya Kilindi mkoani Tanga ambayo ilianza kazi Februari 5, 2022 na ingekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14.

Kamati hiyo ina maofisa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, Takukuru, Ofisi ya Mwanansheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Pia alimuagiza Sirro awasimamishe kazi Kamanda wa Polisi Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa mkoa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara.

Mwananchi

Pia soma:

1. SIMULIZI: Mauaji ya Mfanyabiashara Musa Hamis Mtwara, Machozi na Damu
2. Mtwara: Maafisa Saba(7) wa Polisi wafikishwa Mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Kijana aliyekuwa akiwadai zaidi ya Tsh milioni 33.7
Ngo'mbe akianza kufwariki lazima alushelushe miguu!
 
Back
Top Bottom