IGP: Makamanda msigombane na waandishi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali , Saidi Mwema, aliwataka makamanda wa polisi wasigombane na waandishi wa habari.

Mwema amewataka makakanda hao wahakikishe wanashirikiana na wanahabari kwa kuwapa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka.

Aidha, Makamanda wa Polisi wa mikoa na vikosi nchini, wameagizwa kutoa ushirikiano na kujenga ubia na waandishi wa habari, ili kutekeleza wajibu wao kama wadau muhimu wa kiutendaji kitaifa.

Makamishna wa Polisi wametoa agizo hilo kwenye mkutano wa maofisa waandamizi wa Jeshi hilo mjini Dodoma. Wametoa maagizo hayo wakati wa mjadala kuhusu mpango wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna Robert Manumba, amesema, kila Kamanda wa Polisi nchini, ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anatoa ushirikiano unaostahili kwa waandishi wa habari.

Manumba amesema, ushirikiano huo utawawezesha waandishi wa habari kutimiza wajibu wao wa kuelimisha wananchi kuhusu yanayotokea kila siku.

Mkurugenzi wa Operesheni wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, amesema, kwa kuwa kuna waandishi bandia ‘makanjanja’, ipo haja kwa waandishi wa habari kuwa na vitambulisho vya vyombo wanavyofanyia kazi pamoja na kitambulisho cha uandishi wa habari - Press Card, ili kuondoa utata.

Chagonja amesema, utaratibu huo ukifuatwa, utapunguza uwezekano wa kuwepo waandishi bandia ambao wamekuwa wakichafua uhusiano baina ya Polisi na vyombo vya habari kwa waandishi wasiowajibika kuandika habari za uchochezi au zinazochafua watu.

Mkuu wa Mipango na Bajeti wa Jeshi hilo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, John Masawe, amesema, ipo haja ya waandishi wa habari nao kupewa mafunzo ya mpango wa Polisi Jamii, ili wafikishe ujumbe kwa wananchi.

Kamanda Masawe alisema waandishi wakielimishwa, itakuwa ni msaada mkubwa kwa Polisi katika kueneza mpango huo kwa wananchi.
 
"Mkurugenzi wa Operesheni wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Paul Chagonja, amesema, kwa kuwa kuna waandishi bandia ‘makanjanja', ipo haja kwa waandishi wa habari kuwa na vitambulisho vya vyombo wanavyofanyia kazi pamoja na kitambulisho cha uandishi wa habari - Press Card, ili kuondoa utata".
Kauli kama hizi ni upotoshaji wa mambo, kwani wewe kama polisi ukitoa taarifa sahihi kwa hao mnaowaona kama Makanjanja kuna tatizo gani. Kwa kushindwa kwenu na urasimu katika utoaji habari ndio inayopelekea kusambazwa kwa taarifa zisizo sahihi. Kitambulisho pekee hakiwezi kumbadilisha mzushi kuwa muadilifu kwa kuwa uzushi ni tabia ya mtu na haiwezi kuzuiwa na kitambulisho.
 
Back
Top Bottom