na Lucy Ngowi
IMEBAINIKA kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ndiyo chanzo cha kufunguliwa kwa jengo la Machinga Complex lililopo eneo la Ilala.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana, Meneja Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume, alisema ucheleweshaji wa kufunguliwa kwa jengo hilo, unasababishwa na uongozi wa Halmashauri ya Jiji.
Kwa mujibu wa Chiume, NSSF ipo tayari wakati wowote kukabidhi jengo hilo, lakini uongozi wa halmashauri wameomba wasubiri kwa kuwa bado hawajakamilisha ujenzi wa vioski vya wafanyabiashara.
Meneja huyo alisema, awali NSSF ndiyo ilitakiwa ikamilishe ujenzi wa vioski hivyo, lakini halmashauri iliomba ishughulikie suala hilo kwa kuhofia gharama za ujenzi kuzidi kuongezeka.
"Halmashauri wenyewe wanamalizia kujenga vioski, tarehe watakayomaliza haijulikani. Wanajenga vioski hivyo kwa kuwa waliona shirika likijenga gharama itaongezeka baada ya kubadilisha kutoka vioski vitatu hadi sita.
"NSSF wanataka kukabidhi ila halmashauri hawapo tayari, wanasema mpaka vioski viishe. Sasa liishe lini wakati wao ndio wanamalizia kujenga?" alihoji meneja huyo.
Alisema ucheleweshwaji wa jengo hilo, unachelewesha ujenzi mwingine wa jengo la wamachinga katika Wilaya ya Temeke na Kinondoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bakari Kigoba, alisema ucheleweshaji wa kuanza kwa jengo hilo unasababishwa na NSSF, kwani hawajawakabidhi. "Bado sijakabidhiwa jengo na NSSF, ninangoja wakinikabidhi niendelee na yale niliyoyapanga katika jengo hili," alisema mkurugenzi huyo. NSSF imetoa mkopo wa sh bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la Machinga Complex.
Chanzo: Tanzania Daima
Hoja Zangu
Kwa mwendo huu hivi kweli Serikali ya CCM ina dhamira ya dhati ya kumuinua mfanyabiashara mdogo?au wanafanya siasa tu?