Huwezi kufuturu pesa ya ufisadi, swaumu ikawa safi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Huwezi kufuturu pesa ya ufisadi, swaumu ikawa safi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Aug 25, 2010.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Aug 25, 2010
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,466
  Likes Received: 5,708
  Trophy Points: 280
  Huwezi kufuturu pesa ya ufisadi, swaumu ikawa safi


  Mpayukaji wa Msemahovyo

  [​IMG] Assalaam Alaykum Wallahmatullillahi Wabarakatu mliofunga na ambao hamkufunga.
  Baada ya kuwaamkia sasa naomba nieleze somo la leo. Amma badu, Wallahi, natamani jambo ambalo wengi, naamini, wanatamani pia ili kujikomboa na kuutokomeza uzandiki na ubaramaki unaoendelea miongoni mwetu.
  Kwanza tukubaliane. Kaya yetu iko pabaya na mikononi mwa wabaya wanaoweza kujifanyia lolote wasichelee kitu kutokana kudhani kila mmoja ni mlevi kama wao wasijue wengine ni waumini wa kweli!
  Kutokana hali hii na kujua kuwa mwezi wa Oktoba tuna uchafuzi uitwao uchaguzi au uchakachuaji, najitahidi kusaka majibu kama nabii wa Mungu kwa Wadanganyika.
  Mwenzenu natamani mwezi mtukufu wa Ramadhan ungejiri Oktoba badala ya mwenzi huu. Nisijeeleweka vibaya na kufanya baadhi waanze kunuia kuninyofoa shingo.
  Natamani hivyo si kwa ajili ya ujuha, jeuri, kufru wala utwahuti. Naamini kwa dhati. Hii ingetuwezesha kuswafi nia zetu na kunuia kupata mahakama ya Kadhi na kupiga teke mfumo mbovu unaotusababishia kuishi kidhambi dhambi unaoongozwa na mafisadi wanaotaka kutufisidi tusipate mahakama yetu ili tujihukumu wa sharia za mola wetu Subhanna wataala.
  Kwanini wana nambari wahedi wahukumiane kwa sheria zao za kitakukukuru na waislamu tusihukumiane kwa sheria za Allah Subhanna wataala? Hivi unadhani watu wangenusurika kunyea debe kama sheria za kaya zingetumika?
  Mtu anakuja na nyaraka za kughushi badala ya kumpeleka lupango unamwambia nyaraka zako si sahihi! Je, kipofu anapomuongoza kipofu unategemea nini? Je fisadi anaposhika kani unategemea nini?
  Hata mtume aliusia kuwa binadamu anapambana na maadui wakuu watatu wanaoweza kumuingiza kwenye ukafiri kirahisi- ufakiri, upenzi wa kuzidi kipimo na ujinga. Situkani.
  Hivi vitu vitatu tunavyo na vinazidi kuongeza namba ya makafiri kwenye kaya. Wanakaya wengi ni wajinga kiasi cha kutojua maadui zao wala haki zao za msingi.
  Wapo wapo wanaliwa mchana kweupe na hawafanyi kitu kutokana na ujinga na ujuha waliopandikizwa chini ya dhana chafu za uwenzetu na upuuzi mwingine kama huu.
  Kutokana na kaya kuendeshwa kifisadi ufakiri unazidi kuumka huku ujinga ukicheza ngoma kwenye vichwa vya wanakaya kutokana na elimu kuwa bidhaa aghali na feki. Ajabu bado wanakaya hawa waathirika wanawapenda watesi wao kupita kiasi hadi kuwapa kula!
  Wengine huiita kura ya kuliwa yaani kumpa mamlaka yule anayekuguguna na kukuchuuza kufanya hivyo kisheria. Wale waliosoma fikhi wananielewa vizuri.
  Hivi ni ukafiri kiasi gani waumini wazima kudanganywa kuwa mnasonga mbele wakati mnavutwa nyuma kilometa milioni moja nanyi mkaamini huku mkijua ni uongo? Je huu siyo sawa na ulevi wa walevi wa kijiweni kwangu ambao kila mwaka hunipa kura ili niwale?
  Kama Ramadhan ingewadia mwezi huu nina hakika: tungetumia swaumu zetu vizuri na vilivyo kuwashikisha adabu vidhabu wanaotuhadaa kutunyonya na kututesa wakati Maulana alituumbia hii dunia tuifaidi wote si wote wao.
  Tungeondokana na yale mambo matatu niliyotaja hapo juu na kuwa waumini na wanakaya safi. Nani kakwambia dini na ukombozi vinagomba?
  Kwanza, sijui kama wanaharamu hawa hufunga. Kama wanafunga basi wanajifunga na kuchuma dhambi kwa kumhadaa Allah ambaye haadahiki hata kidogo. Maana huwezi kufuturu pesa ya ufisadi au itokanayo na kuiba na kununua kura swaumu yako ikaswhihi. Never. It can't swihi hata kidogo.
  Naanini kama Ramadhan ingewadia mwezi wa kumi, hata madhambi yanayotendwa na hawa wanaowania ulaji wa dezo kwa kumwaga pesa chafu na safi yangepungua.
  Wananchi wapenda dezo hasa waliofunga, wangejiepusha na wezi hawa wanaowanunua ili wawauze kwa bei mbaya kwa mabwana zao.
  Naamini pia hata hawa wanaosia uongo wangepunguza ingawa hawana dini zaidi ya mamlaka na ufisadi. Unakuta jitu linakariri mistari ya Qur'an na Biblia kila liendako. Lakini nyuma ya pazia jitu hili hili gendaeka ndilo fadhili kuu la mafisadi.
  Linatumia madaraka yake kupitisha watoto wake na maswahiba zake kwenye kugombea ulaji huku likiwapendekeza mabwana zake wa nyuma ya pazia wagombee ubunge.
  Hebu jiulize. Kwanini siku hizi ubunge umekuwa kivutio cha wafanyabiashara mabilionea wenye kutia kila shaka? Jibu ni rahisi. Wananunua kaya kwa matumizi yao machafu hapo baadaye.
  Msipoangalia hata Al-Qaeda na Al Shabaab watakuja chomeka watu wao. Mtastukia mnaambiwa kaya yenu iko chini ya makundi haya bila nyinyi kujua. Shauri yenu endeleeni kujiuza kama vyangu. Kwanini kura yako iwe kula ya mtu mwingine? Bila shaka anayefanya hivi anakuona ***** ndiyo maana anakuhadaa na kukuhonga upuuzi.
  Pia natamani Kwaresima nayo ingejiri mwezi Oktoba ili jamaa zangu wa ufisadi na kulindana wageuzwe majivu hasa Jumatano ya majivu. Natamani Kwaresima na Ramadhan zingefika mwezi wa kumi ili hawa wanaohonga ulevi na uongo wakose wakuhonga.
  Maana walevi wangeadimika na nafasi yao kuchukuliwa na waumini ambao bila shaka kwa nguvu ya imani zao wangepinga dhambi ya kuhongwa kwa nguvu na akili zao zote.
  Hata wale wanaopenda kuomba rushwa ya ngono kama yule ticha wa pale nonihino aliyebambwa juzi wangekoma na kukosa wateja kama si kupungua ingawa wanaharamu hawa hawana dini.
  Juzi nilicheka nusu kufa ingawa nilikuwa nimeudhika nikafikia kucheka kwa maudhi. Nilimsikia mgosi Machungi wa Makambale akiongopa kuhusu uraia wa Bwashee.
  Ukiangalia msijida wake wa kulazimisha na anavyopenda kukwoti vitabu vitakatifu unaweza kuhadaika kuwa ana dini. Kwa taarifa yenu mgosi ni rafiki yangu na mpambe wangu. Hana dini hata kidogo. Dini yake ni ulaji na mamlaka.
  Hii ndiyo maana kwa sasa anazunguka kwa wajina wake na swahiba yake Mainjiii kumtoa upepo wa kuhongea wanuka njaa kwa kisingizio cha kufuturisha.
  Kesho mtamsikia yule jambazi wa Kagoda naye akifuturisha kabla ya kuhani mkuu baba yao naye kutoa futari. Mie japo nimepigika kiuchumi, kwa imani yangu ya kweli, siwezi kufuturu futari ya wizi hasa itolewayo na hawa sharmutah wal habithi hata kama wanajiona ni watukufu.
  Mie najua wazi kuwa aliye bora mbele ya Allah ni yule amuaminiye na kumuogopa Allah. Hata uwe na mipesa kama wauza unga au madaraka kama firauni mie hunitishi na ndiyo maana huwa napayuka bila kujali ukubwa wa kacheo ka mtu.
  Hebu jiulize. Wangekuwa waislamu wa kweli kama mimi kweli wangehujumu uchumi hadi futari inapanda bei na wasifanye kitu? Loh! Kumbe saa ya kufuturu imetimu! Acha niwahi kufuturu halali mie. Wabillahi tawfiq.


  [​IMG]
   
 2. Ringo Edmund

  Ringo Edmund JF-Expert Member

  #2
  Aug 25, 2010
  Joined: May 10, 2010
  Messages: 4,895
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 0
  Na walaaniwe milele.aaamin
   
 3. Anyisile Obheli

  Anyisile Obheli JF-Expert Member

  #3
  Aug 25, 2010
  Joined: Dec 13, 2009
  Messages: 3,304
  Likes Received: 19
  Trophy Points: 135
  Mungu awaunguze kwa Moto ulao, na aibu yao iwakute wangali hai
   
Loading...