Hukumu ya Lema kwa kiswahili

Isango

R I P
Jul 23, 2008
295
450
Nimejaribu kuitafsiri Hukumu ya Mahakama ya Rufaa, iliomrejeshea Godbless Lema Ubunge, ili angalau watoaji wa maoni tuwe wengi, kuna sehemu nimekosa kiswahili fasaha, wengine wanaweza kuongeza, kupunguza au kuboresha na kurekebisha. Ipo katika attachment

Nimezingatia mahitaji ya Watanzania wengi, nimejaribu kuweka hukumu ya Lema katika Kiswahili, ili wote wanaochangia katika
mitandao wanufaike. Nilipokosa tafsiri sahihi mwingine anaruhusiwa kuongeza/kufafanua/ama kurekebisha.

HUKUMU ILIYOTOLEWA MAHAKAMA YA RUFAA:

KATI GODBLESS JONATHAN LEMA DHIDI YA MUSSA HAMIS MKANGA, AGNESS GIDION MOLLEL NA HAPPYNESS KIVUYO

Mwaka 2010, taifa letu lilishudia tena uchaguzi Mkuu mwingine ulioshirikisha vyama vingi. Katika Jimbo la Arusha Mjini, Bw. Godbless Jonathan Lema (ambaye hapa ni mwomba rufaa katika kesi hii) kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alishinda baada kupata kura 56,196, dhidi ya mpinzani wake wa Chama cha mapinduzi, Dr. Batilda Salha Buriani wa Chama cha Mapinduzi CCM aliyepata kura 37,460.

Wajibu rufaa waliotajwa hapo juu walijulikana kama wapiga kura waliosajiliwa na ambao walikuwa ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi ambao pia hawakuridhishwa na matokeo, hivyo walifungua kesi ya kupinga matokeo katika Mahakama Kuu ya Arusha, waliwawasilisha ushahidi na kweli matokeo ya Uchaguzi yalibatilishwa.

Hoja yao ya msingi [locus stand] iliyowasababisha wafungue kesi ilikuwa kwamba, Mwomba rufaa (Godbless Lema) alitamka maneno yasiyo ya kistaarabu wakati wa kampeni, ambapo maneno hayo yanaweza kutafsiriwa kuwa ni ya kufedhehesha, na ya kibaguzi yakiwa na lengo la kuleta ubaguzi wa kidini, kijinsia na ubaguzi wa kimakaazi mambo ambayo yalisababisha wapiga kura wasimchague Dr. Batilda Salha Burian. Wajibu rufaa katika kesi hiyo walileta mashahidi 14, pamoja na waleta maombi ya kesi, wakati Mwomba Rufaa (Lema) alikuwa na mashahidi wanne akiwemo yeye. Mwanasheria Mkuu wa serikali aliyeunganishwa katika kesi ya kupinga matokeo kama sehemu muhimu, hakuwa na shahidi yeyote.

Baada ya kusikiliza pande zote kupitia kwa Mawakili wao, Jaji wa Mahakam Kuu (Arusha), aliona kuwa Mwomba rufaa alitenda mambo yaliyolalamikiwa. Jaji wa Mahakama kuu hakujielekeza vizuri kuhusu sheria za uchaguzi na gharama zake pamoja na uwajibikaji wa wajibu rufaa na hivyo alimwelekeza msajili wa mahakama kuu ya Arusha kumwandikia Mkurugenziwa Uchaguzi wa taifa kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi kifungu cha 114(1)-(7), na kifungu cha 343 (kama kilivyorekebishwa mwaka 2002, ili Mwomba rufaa awekewe vikwazo vya kukosa sifa za kugombea baada ya matokeo kubatilishwa. Mwomba rufaa (Lema) hakukubali, hivyo alikata rufaa.

Katika Rufaa hii, Mawakili Alute Mughwai na Moldest Akida, walikuwepo hapa katika Mahakama ya rufaa kama mawakili wa wawajibu rufaa, huku Method Kimomogoro na Bw. Tundu Lissu wakiwa mawakili wa mwomba rufaa (Lema) . Mwanasheria Mkuu wa serikali aliwakilishwa na mwanasheria Timon Vitalis.

Mwomba rufaa (kupitia mawakili wake) alitoa sababu kumi na nane kupinga hukumu ya Arusha. Tulisoma kwa uangalifu na kwa umakini sababu za wajibu rufaa wa kuleta kesi hii (maombi haya). Hatukuona kama ni suala la msingi kwa kuwa suala lenyewe halikuwa wazi zaidi, hii ni kwa sababu msingi wa hoja ya kesi [locus standi] ni wa muhimu katika kuanzisha kesi zozote za kisheria katika mahakama.[Kwamba kuna kesi ya kujibu au hakuna kesi ya kujibu kisheria].

Kwa kuwa suala la hoja ya msingi wa uwepo wa kesi (locus standi) ni la umuhimu katika uendeshaji wa kesi kama hizi, tuna mtazamo sahihi kuwa tunawajibika kupitia kumbukumbu hizi ili tuweze kubaini kama waleta maombi (walioshtaki) walikuwa na hoja ya msingi kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo au hapana. Swali hili lilianzishwa na Mawakili Timon Vitalis na Methos Kimomogoro kama pingamizi la msingi. Katika kujibu suala hilo, Wakili wa wajibu rufaa Alute Mugahwai alijielekeza katika kifungu cha 5.111(1) ya sheria kuwa wajibu rufaa walikuwa kweli ni wapiga kura walioandikishwa kihalali.

Aya ya pili ya Malalamiko inasemeka :- "walalamikaji ni wapiga kura walioandikishwa kupiga kura katika uchaguzi ambao matokeo yake yanalalamikiwa, vivuli vya vitambulisho vyao vya kupigia kura vimewekewa alama A( l-J)". Ni kweli kwamba Wakili Alute Mughwai aliwasilisha vitambulisho vya kupigia kura kuthibitisha kuwa walalamikaji walikuwa ni wapiga kura walioandikishwa, hayo yalijiri mahakamani tarehe 06/09/2011.

Bahati mbaya sana vitambulisho vya wapiga kura havikutolewa na kukubaliwa na mahakama kama ushahidi kwa kanuni za kimahakama na taraibu zake. Jaji Mjuluzi aliridhika tu kwakuonyeshwa vitambulisho vya wapiga kura, na kujiridhidha kwa mujibu wa kifungu cha 111(1) (a) ya sheria za maamuzi za mahakama ya rufaa katika kesi ya Wiliam Bakari na wenzake dhidi ya Chediel Yohane Mgonja na Mwanasheria Mkuu, katika Kesi ya Madai namba 84 ya mwaka 1980, kwa uamuzi uliojikita katika kifungu cha 126 (a).
Lakini katika kesi hii hakuna ushahidi kwenye kumbukumbu za mahakama kuonyesha kuwa wajibu rufaa walikuwa kweli ni wapiga kura walioandikishwa kihalali. Kumbukumbu zina viambatanisho, na kisheria viambatanisho sio ushahidi ambao Mahakama inapaswa kuugemea pasipo kutiliwa shaka.

Katika kesi ya Sabry Hafidhi Khalfan dhidi ya Zanzibar Telecom Ltd (Zantel) Zanzibar Kesi ya madai Na. 47 ya 2009 haijaripotiwa mahakaka ilisema:-

"Tunapaswa kujua kwamba, viambatanisho vilivyoletwa na Mlalamikaji au vilivyotolewa katika maelezo ya Mlalamikiwa sio ushahidi. Labda kwa faida ya sasa tutamke kwamba, lengo lote la kuambatanisha viambatanisho kwenye kesi,ni kuwezesha pande zote kujua kesi inayowakabili. Kwa hiyo wazo la kuzungumzia viambatanisho katika kesi visichukuliwe kama ni ushahidi.

Baada sasa ya kujiridhisha na tafsiri hiyo kuhusu hadhi ya viambatanisho vinavyoletwa,na utaratibu unaotumika kuvifikisha Mahkamani kisheria, tunapaswa tuangalie Mpiga kura aliyeandikishwa ni yupi? Jibu linatolewa chini ya kifungu cha 13,19, na 20 vikisomwa pamoja. Mpiga kura halali aliyeandikishwa ni raia yeyote wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 anayekidhi mahitaji ya kisheria. Kwa kuzingatia hayo mtu anaandikishwa kuwa mpiga kura endapo tu msimamizi wa uchaguzi au msaididi wake au afisa yeyote aliyepewa jukumu la kuandikisha katika eneo husika atakuwa ameridhika na vigezo na Afisa anayetajwa atampa kitambulisho cha mpiga kura. Mtu huyo baada ya kujiandikisha na kupewa kitambulisho anakuwa mpiga kura halali. Kwa hiyo kisheria kitambulisho cha mpiga kura kilichotolewa kihalali na maafisa waliotajwa ni uthibitisho wa halali wa mpiga kura aliyeandikishwa. Kitambulisho hicho ni Uthibitisho kwa mwenye na nacho kuwa ni Mpiga kura halali.

Katika kesi hii, tumeonyesha kuwa Wakili Alute amejaribu kuonyeyesha kuwa wajibu rufaa walikuwa ni wapiga kura halali kwa kuleta vitambulisho vyao vya kupigia kura kwa Jaji. Kwanza haisemwi wazi kwanini Wakili Alute "yeye mwenyewe" alipeleka vitambulisho vya kupigia kura kwa Jaji, Pili, hata utaratibu wa "upelekaji" vitambulisho hivyo ni kinyume na taratibu zinazojulikana za kupeleka viambatanisho na/au kumbukumbu Mahakamani. Kawaida ushahidi kama huo (katika kesi hii Kitambulisho cha Mpiga kura) kilipaswa kuwasilishwa na mpiga kura mwenyewe ambaye ndio mmiliki halali. Tunataka kuweka wazi kiujumla kuwa, sheria ya ushahidi lengo lake ni kutoa ulinzi (au maelekezo yafaayo) ni kwa namna gani (ipi) na ni vipi ushahidi unavyopaswa kuchukuliwa na kupelekwa mahakamani ili kuondoa au kupunguza mianya ya kutotenda haki.

Bila kuzingatia misingi hiyo ya kuulinda ushahidi, Kiurahisi sana Mahakama inaweza kuangukia katika kile kinachoitwa mahakama ya Kangaroo (angalia Herman Henjewele dhidi ya Kesi ya Jinai NA.. 164/2005 (haijaripotiwa) Hata hivyo, Kumbukumbu za mahakama hazionyeshi kama wajibu rufaa walipatia fursa ya kuzungumzia kitu chochote chenye uhusiano na kuvipeleka vitambulisho vya kupigia kura vinavyozungumzwa hapa kwa utaratibu tuliouzoea.

Zaidi ya hayo yote vitambulisho hivyo vilirudishwa kwa Wakili wao siku ile ile, kwa hiyo haviwezi kuzingatiwa kuwa ni sehemu muhimu ya kumbukumbu za Mahakama katika kesi hii ukizingatia pamoja na njia iliyotumika kuviwasilisha mahakamani. Kwa mtiririko huu wa
kisheria tunajiridhisha kuwa hakukuwa na ushahidi au kumbukumbu kuonyesha kuwa wajibu rufaa hawa walikuwa wapiga kura halali kwa makusudi ya kifungu cha 111(1)( a) cha sheria.

Potelea mbali tuchukulie kuwa wajibu rufaa walikuwa ni wapiga kura halali, tujiulize je walikuwa na haki ya msingi wa kusimamia (au hadhi yao kisheria) ili kuweza kupinga matokeo ya uchaguzi kwa misingi ya maneno yasiyo ya kistaarabu ambayo Mwomba Rufaa (Lema) inasemekana aliyatamka wakati wa kampeni?

Tumeonyesha dhahiri kuwa Wakili Alute alikubaliana na utafiti wa Mujuluzi J kuhusiana na hukumu ya ya kesi ya Mgonja, lakini kwa Upande Mwingine Wakili Timon Vitalis, Method Kimomogoro, na Tundu Lissu walipinga kwa nguvu zote hapa kwenye Mahakama ya rufaa, na hoja yao ya msingi ilikuwa "suala hili lipo kinyume cha sheria".

Sheria inasema, Suala hili sio kwa manufaa ya umma kwa mwenendo wa kesi kisheria chini ya kifungu cha 26 (6) cha Katiba, kwa hiyo haki ya msingi ya kusimamia kimahakama mtu anayopaswa kuonyesha ni kuwa haki zake ziliingiliwa au maslahi yake yalikiukwa na matokeo yake yanapaswa yaonekane (athari ionekane), kwa hiyo mpiga kura hana haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwa kuwa haki zake na maslahi yake hayakukiukwa au kuingiliwa. (haki za mpiga kura ni kuandikishwa, kupiga kura na kuhakikisha kura yake ilihesabiwa, je wajibu rufaa kati ya hizo haki zao ipi ilikiukwa?) Kifungu cha 111(1) kinasomeka:
111(1) Matokeo ya uchaguzi yanaweza kupingwa na mmojawapo kati ya hawa wafuatao, (a)Mpiga kura aliyepiga kura kihalali, au alikuwa na haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi unaobishaniwa.

Kwanza tunaomba kueleza pasipo shaka kuwa, sheria ya msingi wa kusimamia hoja (locus standi) ipo katika sheria za kawaida,
na inatumika katika mahakama zetu kwa mujibu wa kifungu cha 2(3) ya Ulazima wa kisheria na Matumizi ya Sheria kifungu cha
358 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ili kuweza kuendana na sheria ya misingi ya kuwa na hoja katika hali kama hii inapojitokeza. Soma Lujuna Shubi Ballonzi, Senior dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Mapinduzi (1996) (tlr 203)

Kwa sasa katika Tanzania imepanuliwa zaidi ili iweze kuendana na matashi ya jamii kifungu 26 (2) cha katiba, kwa hiyo raia wa nchi hii ana hoja ya msingi kusimamia anaposhtaki kwa masuala yenye manufaa kijamii. Na ulazima wa kisheria unategemeana haki inayotafutwa na taathira yake (madhara) yake kijamii. Katika Kesi ya Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali [1995] TLR 31 Lugakingira J, alizingatia ulazima wa kufuata sheria katika suala hilo na manufaa ya kijamii, akasema: Pamoja na ulazima wa kuzingatia sheria kwa manufaa ya Umma, mahakama hii haikatai ukweli kuwa mlalamikaji ana manufaa binafsi na kesi hii,

Alienda mbali zaidi akasema:- Ulazima wa kisheria katika kesi hii sio kuonyesha/kuridhisha udadisi wa watu, lakini Sheria zimewekwa ili kuisadia mahakama iweze kutoa nafuu kwenye jamii yote au kikundi fulani cha jamii.

Katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali dhidi ya Chama cha Congress cha Malawi, Kesi ya madai Na.22 ya Mwaka 1996, Mahakama ya Rufaa ya Malawi ilionyesha msingi wa kusimamia haki kisheria na ilisema hivi:-

Suala la hoja ya msingi wa kesi, ni suala la kisheria, na itakuwa ni masuala ya utawala bora tukizingatia kuwa sio kila mtu anaweza kufungua kesi kama yeye sio sehemu ya suala linalobishaniwa. Hii ni kusema kuwa ni lazima awe sehemu ya jambo linalobishaniwa kisheria.

Katika kesi hii na maamuzi; kwamba iwe wajibu rufaa walikuwa au hawakuwa wapiga kura halali kwa mujibu wa kifungu cha 111 (1)( a) cha sheria kinachompa mtu haki ya kupinga matokeo ya Uchaguzi hata kama haki zake hazikukiukwa na maslahi yake kuingiliwa. Tumelitafakari sana suala hilo na hivyo tunapenda kusema: Kwanza masuala ya kesi za Uchaguzi sio manufaa kwa umma, ingawa yana umuhimu mkubwa sana kwa umma. Hii ni kwa sababu pengine haki inayotafutwa haiwezi kunufaiha jamii yote kwa ujumla
wake. Pili, Kesi ilifunguliwa chini ya kifungu cha sheria na 26 (2) cha Katiba kinachoruhusu kila raia kuleta malalamiko kisheria kwa manufaa ya Umma. Kifungu hicho cha Katiba kinasomeka kwamba: Kila mtu kwa mujibu wa sheria anaweza kufungua kesi kulinda katiba.

Kwa kuwa kesi ya uchaguzi sio kwa manufaa ua Umma, kisheria hatusomi kifungu hicho kwani tutakuwa tumekiuka kifungu kinachohusu ‘haki ya msingi ya kusimamia hoja' [locus standi]. Tunaona kwa mtanzamo wetu, kifungu cha 111(1) (a) cha sheria
kinachotoa haki kwa mpiga kura ambaye haki zake zimekiukwa au maslahi yake kuingiliwa.

Kwa hiyo kwa kesi hii; Kama Ukiukwaji ulifanyika, basi mlalamikaji wa kwanza anapaswa awe Mgombea Mwenyewe ambaye haki zake
zilikiukwa. Na ili kukipatia kifungu hiki tafsiri pana, yeye ndio ana haki zaidi hata kama haki zake hazikukiukwa angetetea vizuri
kanuni na hoja ya kusimamia Misingi ya uwepo wa kesi ya kujibu [locus stand]. Hatuko tayari kukiuka kanuni hii. Hivyo, tunakubaliana na hoja za Timon Vitalis, Method Kimomogoro na Tundu Lissu kwenye suala la "wapiga kura halali".

Kwa mtazamo huo huo, tunathibitisha pasipo shaka kuwa Kesi ya Mgonja ilihukumiwa kinyume, ilitoa tafsiri potofu ya ‘hoja ya msingi ya uwepo wa kesi ya kujibu.

Tunasema hivyo kwa kuwa hatufikirii kwamba Mahakama iliruhusu kila mpiga kura yeyote bila kuzingatia mahali alipojindikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo ya uchaguzi wowote, wa jimbo lolote mahakamani katika nchi hii.
Utakuwa ni ujinga.

Katika kesi ya Grey dhidi ya Pearson (1857) 6 HLC 61 ilieleweka kuwa:-
"Kama tafsiri ya maneno inaweza kupelekea ujinga na/au upumbavu wa aina fulani au uhusiano wa maneno yanayopingana au tabia ya kubadilika badilika,kukosa msimamo hali hiyo inaweza kuepukwa ili kutojiweka kajika ujinga/upumbavu na kuonekana hatuna msimamo.

Kwa mtazamo huo, kwa utulivu kabisa tunasema kuwa wajibu rufaa hawakuwa na hoja ya kusimamia Misingi ya uwepo wa kesi ya
kujibu [locus stand] katika kesi iliyoletwa katika Mahakama ya rufaa. Hiyo peke yake inatosha na kumpa Mwomba rufaa haki. Rufaa imeshinda na tunatengua hukumu ya Mahakama Kuu kwa amri ya Mahakama ya rufaa, tunamtangaza Mwomba rufaa kuwa Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini. Wajibu rufaa watapaswa kulipa gharama za Mwomba rufaa pamoja na mawakili wake wote wawili.

Imetolewa Dar es Salaam, tarehe 19, Decemba, 2012. Mbele ya Jaji,
N.P Kimaro, B.M Luanda na S.A. MASATTI. Having
 

Attachments

  • HUKUMU YA LEMA, KWA KISWAHILI..pdf
    142.7 KB · Views: 319
Nimejaribu kuitafsiri Hukumu
ya Mahakama ya Rufaa, iliomrejeshea Godbless Lema Ubunge, ili angalau
watoaji wa maoni tuwe wengi, kuna sehemu nimekosa kiswahili fasaha,
wengine wanaweza kuongeza, kupunguza au kuboresha na kurekebisha. Ipo
katika attachment

Mnyapaa wengine tunatumia cm hebu iweke tuweze kuisoma wole waang.
 
Isango asante kwa contribution yako! sijadownload bado but ingependeza utuwekee version zote manake wengine hatujaona hata hiyo ya kingereza!
 
Back
Top Bottom