Houseboy' ahukumiwa kunyongwa kwa kumuua bosi wake

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
428
996
Arusha. Mfanyakazi wa ndani wa kiume (house boy), Ismail Sang'wa (28), amehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumuua kwa kumkata shingo na panga aliyekuwa mwajiri wake Emily Kisamo (52) Kisamo alikuwa Ofisa wa Intelijensia wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa).

Hukumu hiyo imetolewa jana Machi 3, 2023 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji Joachim Tiganga aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 70/2022, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wa Serikali wandamizi Janeth Sekule, Grace Madikenya na Charles Kagirwa huku mtuhumiwa huyo akitetewa na Wakili Victor Benard.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Tiganga, ameeleza mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo baada ya kuthibitika alimuua kwa makusudi Kisamo ambaye alikuwa mwajiri wake kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.

Jaji ameeleza kuwa upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha pasipo na shaka kosa la mauaji lililokuwa likimkabili mtuhumiwa huyo baada ya kusikiliza mashahidi 10 na vielelezo 24 vilivyotolewa.

Jaji Tiganga ameeleza mahakama ilitilia shaka utetezi wa mshitakiwa huyo kwa kuwa hakuwasilisha kielelezo wala shahidi wa kuithibitishia mahakama kuwa hakuwa eneo la tukio siku mauaji hayo yalipotokea huku katika maelezo ya onyo akikiri kutenda kosa hilo.

Ameeleza kuwa kupitia ushahidi wa jamhuri, umeweza kuthibitisha mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Desemba 18, 2015 nyumbani kwa marehemu eneo la Uzunguni jijini Arusha majira ya asubuhi.

Jaji ameeleza kuwa kupitia mashahidi hao na maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo iliweza kuthibitika mahakamani kuwa siku ya tukio marehemu alikuwa nyumbani kwake sebuleni akiwa anakunywa uji, ndipo mtuhumiwa ambaye ni mfanyakazi wake wa ndani na alimvizia na kumkata shingo (kwa nyuma) na panga.

Kupitia mashahidi hao, ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo aliuchukua mwili wa marehemu na kuuweka kwenye buti la gari la marehemu aina ya Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY na kuupeleka hadi eneo la Kikwakwaru “B” kata ya Lemara ambapo alilitelekeza hapo na kisha kuondoka.

Imeelezwa kuwa baada ya gari hilo kukaa katika eneo hilo hadi saa mbili usiku, baadhi ya wananchi wa eneo hilo walitoa taarifa polisi na askari wa doria walikwenda na kulichukua gari hilo kwa kulivuta mpaka kituoni na baada ya mshitakiwa kukamatwa alikiri kuhusika na mauaji hayo.

Awali imeelezwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo baada ya kukiri kuhusika na mauaji hayo, alionyesha mahali alipokuwa amefukia taulo, shuka zilizokuwa na damu pamoja na panga alilokuwa ameficha stoo.

Vitu vingine alivyokuwa ameficha kwenye migomba iliyopo nyumbani kwa marehemu pamoja na fedha zaidi ya Sh4.2 milioni, vocha za mtandao wa Vodacom zilizokuwa na thamani ya Sh70,000 na simu nne, alivyokuwa ameficha chini ya banda la kuku.

Credit: Mwananchi

Pia soma

 
Back
Top Bottom