BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 699
- 1,697
Mambo mazito Yanayosubiri Majibu
Baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atazungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuliutubia Taifa, mijadala mikubwa imeibuka kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi wanatarajia hotuba itakayofungua ukurasa mpya wa matumaini, huku wengine wakitabiri kuwa huenda kusiwe na jipya linakokuja.
Matarajio haya yamechochewa zaidi na taarifa zinazozagaa mtandaoni kuhusu uwezekano wa kufanyika maandamano tarehe 9 Desemba 2025. Pamoja na hilo, Jeshi la Polisi na viongozi mbalimbali wa serikali wamekuwa wakitoa onyo kwa wanaohamasisha maandamano hayo, wakisisitiza kulinda amani ya nchi na kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Kwa muktadha huo, macho na masikio yameelekezwa kwa Rais Samia wakitarajia ujumbe utakaoweza kurejesha tumaini na kuondoa taharuki inayojitokeza, hasa katika miji mikubwa.
Tayari baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine makubwa wameanza kufanya manunuzi ya akiba kana kwamba wanajiandaa kujifungia ndani (lockdown) kufuatia hofu iliyojengeka. Hali hii inahusishwa na kumbukumbu mbaya ya tukio la ghafla la lockdown wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, lililoambatana na matukio mbalimbali yaliyowaacha wananchi wakiwa na hofu nzito.
Macho na Masikio Yanataka Kusikia Nini?
Huenda ikawa mojawapo ya hotuba inayosubiriwa kwa hamu zaidi tangu Rais Samia achukue madaraka, kutokana na mazingira ya kisiasa na kijamii yanayoendelea. Ingawa tayari amewahi kuhutubia Taifa na kutoa maelekezo kadhaa, bado maswali mengi yameendelea kuibuka kuhusu masuala mazito yanayogusa mustakabali wa nchi.
Rais Samia alishaunda Tume ya kuchunguza matukio ya kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ikiwa na jukumu la kubaini chanzo, athari na masuala mengine yanayohusiana na yaliyotokea. Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwake, Tume hiyo imekumbwa na ukosoaji kuhusu muundo wake na uhalali wa utekelezaji wa majukumu yake. Wapo wanasheria ambao hata wamefikisha malalamiko yao Mahakamani wakipinga uhalali wake.
Nini Kinangojea?
1. Uwajibikaji
Neno “uwajibikaji” limeendelea kuwa kitendawili kigumu. Pamoja na malalamiko ya matukio mbalimbali yanayodaiwa kutokea, hakuna uwazi kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika. Baadhi ya watu wanasisitiza kuwa kuna watendaji ambao walipaswa ama wajiuzulu au wawajibishwe rasmi. Taasisi kama Baraza la Maaskofu (TEC) na wadau wengine wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa kweli.
Hivyo, jicho linamwangalia Rais Samia ili kuona kama ataweza kutoa mwanga mpya katika eneo hili linaloonekana kuwakera wananchi wengi.
2. Kukiri Matumizi ya Nguvu Kupita Kiasi na Uzembe
Baadhi ya watendaji wa serikali wamekiri kuwepo kwa athari ikiwemo vifo wakati wa uchaguzi, lakini bado hakuna tamko la wazi linalokiri matumizi ya nguvu kupita kiasi katika kudhibiti matukio. Pia, kumekuwepo na madai ya watu kushambuliwa nje ya maeneo ya maandamano, hata wakiwa majumbani mwao. Wananchi wanahoji ni kwanini hakuna aliyewajibishwa au kukiri uzembe uliosababisha vifo na majeraha kama inavyodaiwa.
3. Hatma ya Washtakiwa Waliohusishwa na Uchaguzi
Wakati akihutubia Bunge baada ya kuapishwa, Rais Samia alimwelekeza DPP kuwaachia baadhi ya watuhumiwa aliowaita “waliokwenda kwa mkumbo.” Baadhi tayari wameachiwa. Hata hivyo, yapo makundi ya watuhumiwa wanaokabiliwa na mashtaka mazito yanayohusishwa na uchaguzi na bado wako gerezani bila mwelekeo wa mustakabali wao. Jambo hili linatarajiwa kuhitaji ufafanuzi.
4. Kulaani na Kukemea Utekaji na Mauaji
TEC, Chadema, asasi za kiraia, wananchi na wadau wengine wameendelea kulalamikia vitendo vya utekaji na mauaji yanayodaiwa kutokea katika kipindi cha uchaguzi. Hata hivyo, yamekosa sauti ya wazi ya kukemewa na hatua madhubuti dhidi ya wahusika. Katika mitandao ya kijamii, malalamiko mengi yanayahusisha moja kwa moja na vyombo vya dola au watawala. Wananchi wanataka kufahamu: je, waliodaiwa kutekwa wataonekana? Waliowajibika watachukuliwa hatua?
5. Hatma ya Lissu na Chadema
Kumekuwepo na mvutano kati ya Chadema na serikali, na baadhi kuona kama chama hicho kinadhibiwa kwa njia zisizo za haki. Mwenyekiti wake yuko gerezani kwa miezi takribani nane akishitakiwa kwa makosa yasiyo na dhamana ya uhaini. Wadau wanasema hakuna maridhiano ya kweli yanayoweza kupatikana wakati chama kikuu cha upinzani kiko katika hali hiyo. Suala hili linangojewa kwa hamu.
6. Mwelekeo wa Taifa Kidiplomasia, Kisiasa na Kiuchumi
Athari za uchaguzi zinatajwa kuikosesha Tanzania mvuto wa kidiplomasia, ikiwemo kutajwa katika ripoti hasi, hatari ya kupoteza misaada, mikopo na uwekezaji. Kwenye uchumi, sekta kama utalii ambayo hutegemea utulivu—imetajwa kufifia. Kisiasa, kuna nyufa kubwa kati ya wafuasi wa vyama na hili linahitaji tiba ya kitaifa.
Wapo wanaotamani kuona uhuru wa kujieleza ukirejeshwa kikamilifu, ikiwemo kufunguliwa kwa jukwaa la JamiiForums lenye historia ya kuchochea uwajibikaji na mijadala huru nchini.
7. Waliopotea au Miili Isiyopatikana
Kumekuwepo na taarifa za watu kutafuta ndugu zao bila mafanikio. Hili limeacha majonzi na maswali mazito kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Wanahitaji majibu na faraja ili kuponya majeraha ya muda mrefu.
Hitimisho
Macho na masikio ya Watanzania sasa yanaelekezwa kwa Rais Samia kuona kama hotuba yake italeta mwanga mpya wa matumaini au kama kivuli cha hofu kitaendelea kutawala. Ni vizuri kukumbuka kuwa alipochukua uongozi kwa mara ya kwanza alijenga matumaini ya siasa, diplomasia na uchumi unaotazama mbele kabla ya hali hiyo kuyumba. Swali linalobaki ni:Je, ataweza kutoa majawabu ya masuala haya mazito na kurejesha mwelekeo wa Taifa?