Hotuba ya Mhe. B. Mkapa Mei Mosi 2001

Mkandara

JF-Expert Member
Mar 3, 2006
15,772
8,958
Wakuu zangu nimeipitia upya ile hotuba ya Mh. benjamin Mkapa siku ya sikukuu ya wafanyakazi mei mosi 2001 kisha nikajiuliza maswali mengi sana..Hivi kweli siasa Ni UONGO UNAOKUBALIKA?..
Ebu nanyi ipitieni Hotuba hiyo kisha nambieni kulikoni?.


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE SIKUKUU YA WAFANYAKAZI, DAR ES SALAAM, MEI MOSI, 2001

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Ndugu Margaret Sitta;
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Ndugu Nestory Ngula;
Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, Mhe. Prof. Juma A. Kapuya, Mb.;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Yusufu Makamba;
Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani, ILO;
Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali;
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi; Mabibi na Mabwana.


Ninayo furaha kubwa kuungana nanyi wafanyakazi wote katika kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi. Nawashukuruni sana viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kwa kunialika kwa mara nyingine kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei Mosi. Mwaliko huu ni kielelezo cha dhamira yenu kushirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya wafanyakazi, na ya nchi yetu. Ahsanteni sana.


Ndugu Wafanyakazi,

Baadhi yenu mlisimamia Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Kwa sehemu kubwa sana uchaguzi ulikwenda vizuri; na ninawapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wote waliohusika. Najua kura za wafanyakazi nazo zilichangia ushindi wangu mkubwa. Walionipigia kura nawashukuru sana; na waliowapigia wagombea wengine nao nawashukuru kwa kuleta uhai katika demokrasia yetu ya vyama vingi ambayo bado tuna kazi kubwa ya kuirutubisha, kuilea na kuikomaza.

Naushukuru uongozi wa vyama vya wafanyakazi uliopita chini ya Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (TFTU), na wafanyakazi wote, kwa mahusiano mazuri tuliyokuwa nayo. Hata pale tulipohitilafiana, tulizungumza, kwa uwazi na ukweli, kisha tukaendelea kujenga nchi, si kuibomoa. Mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na Serikali, na utendaji wa wafanyakazi mbalimbali, ni moja ya mambo muhimu yaliyochangia mafanikio makubwa tuliyopata katika kurekebisha mfumo wa uchumi wetu hadi tukasifiwa duniani kote. Leo napenda katika hadhara hii, na kupitia vyombo vya habari, niwashukuru sana wafanyakazi wa Tanzania. Naomba tuendelee kushirikiana hivyo, kwa manufaa ya taifa na wananchi wote.

Aidha, uvumilivu na utulivu wenu ulitupa fursa ya kushughulikia matatizo makubwa ya uchumi yanayoikabili nchi yetu. Siku zote nimekuwa muwazi na mkweli kwenu na kwa wananchi wote. Nashukuru mmenielewa kuwa nia yangu ni njema, na kwamba kuzungumza matatizo ya taifa letu kwa uwazi na ukweli ndiyo mwanzo wa kukubaliana juu ya ufumbuzi endelevu.

Namshukuru Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa salamu zake na kwa misaada na ushirikiano wao kwa Vyama vya Wafanyakazi na vya Waajiri, na katika kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali, waajiri na wafanyakazi. Nazishukuru pia Serikali za Denmark na Marekani wanaotusaidia kuboresha utendaji katika sekta hii ya kazi.

Natoa shukrani vile vile kwa Mwakilishi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kwa hotuba yake nzuri na kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na Serikali, na Vyama vya Wafanyakazi.

Hivi punde nimetoa zawadi kwa wafanyakazi bora. Naungana nanyi katika kuwapongeza sana, na kuwaomba waendelee na kazi yao nzuri ili wengine wajifunze kutoka kwao.

Pongezi na shukrani zangu za mwisho ni kwa viongozi na wananchi wa Dar es Salaam kwa kuubeba vizuri sana mzigo wa kuwa wenyeji wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu. Nakipongeza pia Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU) kilichosimamia na kuratibu maandalizi ya Mei Mosi hii. Wamefanya kazi nzuri, na ninawashukuru sana.

Vyama Huru vya Wafanyakazi


Ndugu Mwenyekiti,

Mei Mosi ya mwaka huu ni ya kihistoria, iliyoandaliwa na kusimamiwa na uongozi mpya, wa vyama vipya vya wafanyakazi, vilivyo huru kabisa. Vyama huru vya wafanyakazi ni sehemu muhimu sana ya demokrasia, na vikifanikiwa vitachangia sana kuimarisha uelewa, uwajibikaji, na utekelezaji wa haki za wafanyakazi.

Nawapongezeni nyote kwa kuunda vyama vyenu vya wafanyakazi, na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania, (Trade Unions Congress of Tanzania) na kuchagua viongozi wake. Natoa pongezi za dhati kabisa kwako Mama Margaret Sitta kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Shirikisho, na kwa imani kubwa wenzako waliyoionyesha kwako. Hongera sana, na ninakuhakikishia ushirikiano wa dhati unapoanza kutekeleza majukumu yako.

Nakupongeza pia Katibu Mkuu mpya, Ndugu Nestory Ngula, pamoja na nyote mlioaminiwa na wenzenu na kupewa uongozi. Hongereni sana, na ninawahakikishieni ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini.
Hata hivyo napenda kuwatanabahisha kuwa mwisho wa kuundwa kwa vyama, na kuchagua viongozi, ndio mwanzo wa kazi yenyewe, katika mazingira magumu na matatizo mengi ambayo hamuwezi kuyamaliza yote kwa mara moja. Nimepokea malalamiko yenu kuwa Sheria iliyoanzisha vyama huru vya wafanyakazi ina mapungufu. Iwapo hoja ya marekebisho itathibiti, tutakuwa tayari kukaa nanyi, pamoja na washika dau wengine, ili kuirekebisha sheria hiyo kwa namna itakayozingatia maslahi ya kila upande. Maana, Serikali lazima pia ijali maslahi ya washikadau wengine, wakiwemo waajiri, wawekezaji, na wananchi kwa ujumla.

Ndugu Viongozi Wapya,
Katika mazingira haya mapya, na kwa kuzingatia ushindani mkali unaoletwa na utandawazi, ninayo mambo matatu ya kushauri vyama vipya na huru vya wafanyakazi.

Kwanza, hakikisheni mikataba iliyopo sehemu za kazi, na sheria za nchi, inafuatwa na waajiri wenu. Maana hakuna faida kutafuta haki mpya na maslahi mapya, kama hata yale ya awali hayajatekelezwa kwa ukamilifu. Nitatoa mfano. Serikali imeweka kima cha chini cha mshahara kisheria, lakini nasikia bado wapo wafanyakazi wanaolipwa chini ya kiwango hicho. Ninyi mkiwa viongozi wao mnalo jukumu la kuwatetea.

Ninaambiwa pia wapo wafanyakazi ambao hawana barua na mikataba rasmi ya ajira. Hilo nalo inabidi vyama vya wafanyakazi vilichunguze na kuchukua hatua. Nasikia waajiri wengine wamegeuza ajira karibu yote iwe ya vibarua tu. Hoja ya vibarua inaeleweka, lakini ina kikomo chake. Haiwezekani wafanyakazi karibu wote wawe vibarua. Fanyeni utafiti wa kutosha na kisha kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa kushirikiana na Serikali na waajiri.

Pili, jijengeeni uwezo na utaalam wa kujua hali halisi ya uzalishaji katika kila sehemu ya kazi, undani wa uzalishaji na biashara mnayoifanya, au huduma mnayoitoa, na kuelewa mwenendo wake katika ulimwengu wa ushindani. Ujuzi huo utawawezesha kujiamini mnapokaa na waajiri kuzungumzia mbinu za kuongeza uzalishaji na tija, na kuongeza uwezo wenu wa ushindani katika soko huru, na baada ya kuongezeka kwa uzalishaji na tija, kupata nguvu, haki na msingi wa kudai maslahi bora zaidi. Maana kama uzalishaji na tija haviongezeki, na kama faida haiongezeki, madai ya maslahi bora zaidi yatahimiliwa na nini?

Tatu, zingatieni wajibu wa kujadiliana na waajiri juu ya hali bora za kazi. Mnapaswa kujiimarisha kitaaluma kabla ya kukabiliana na waajiri ili muweze kujenga nguvu za hoja, si kutumia tu hoja ya nguvu itokanayo na wingi wenu. Sheria ya Mahakama ya Kazi imeweka utaratibu wa majadiliano ya pamoja kati ya waajiri na waajiriwa kupitia vyama vyao, ili kufunga mikataba ya hiari ya hali bora za kazi. Sheria hii itaangaliwa upya wakati wa kurekebisha sheria zote za kazi. Lakini ni muhimu mikataba mtakayoifunga isaidie kuchochea uzalishaji, tija na faida ili uwezo wa kuitekeleza mikataba hiyo upatikane.

Kamwe msisahau kuwa Serikali, na sekta ya umma kwa ujumla, sasa si mwajiri mkubwa kama ilivyokuwa zamani. Wanachama wenu wengi sasa watakuwa kwenye sekta binafsi. Na kwa kadri sekta binafsi inavyotwaa majukumu mengi zaidi ya kiuchumi na utoaji wa nafasi za ajira, ndivyo wajibu na kazi za vyama vya wafanyakazi zinavyoongezeka. Jiandaeni vizuri kuubeba mzigo huo, na Serikali itawasaidieni kwa dhati.


Amani na Utulivu


Ndugu Mwenyekiti,

Tukumbushane umuhimu wa amani na utulivu kwetu sisi wafanyakazi. Maana ni rahisi kudhani kuwa anayehusika na amani na utulivu ni Serikali na wanasiasa tu. Lakini ukweli ni kuwa maslahi yenu kama wafanyakazi yanategemea sana hali ya amani na utulivu. Kwa sababu hiyo, kila mfanyakazi ni mshika-dau katika kuhifadhi na kutetea sifa yetu kama kisiwa cha amani na utulivu.

Tunaishi katika dunia ya ushindani kwenye kila jambo, ikiwemo ushindani katika kuvutia mitaji na vitegauchumi, ushindani wa ajira, na ushindani wa biashara. Sifa moja inayotuongezea uwezo wa ushindani katika Bara la Afrika ni hali yetu ya amani na utulivu. Mwekezaji binafsi, ambaye sasa ndiye tunayemtegemea atoe nafasi za ajira, hawezi kuja kuwekeza Tanzania tukipoteza sifa hiyo. Watalii tunaowategemea sana kwa ajira na mapato nao wataikwepa nchi yetu.

Hivyo wafanyakazi wawe wakereketwa wa amani na utulivu. Kwanza, wao wenyewe wasishiriki au kufumbia macho vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani na utulivu. Na pili, washirikiane na Serikali katika kukemea tabia inayoanza kuota mizizi ya kutoheshimu sheria au maelekezo mengine halali ya Serikali yenye lengo la kudumisha amani na utulivu.

Inawezekana wapo wanasiasa wanaofikiri kuwa ghasia, fujo na vurugu kwao ni mtaji wa kisiasa; lakini kwako mfanyakazi wa Tanzania ujiulize utapata faida gani nchi hii ikianza kukwepwa na wawekezaji na watalii.

Umaskini na Maendeleo


Ndugu Mwenyekiti,

Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani, na sasa tumeazimia kuondokana na aibu hiyo. Tumebuni Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayokusudia kutufanya tuwe taifa ambalo watu wake walio wengi watakuwa na maisha bora; taifa lenye amani, utulivu, na umoja; taifa linaloongozwa kwa misingi ya utawala bora, utawala wa sheria; taifa lenye watu walioelimika na wanaoendelea kujielimisha; na taifa lenye uchumi unaohimili ushindani, uchumi unaokua na kutoa ajira na mapato, uchumi endelevu usioharibu mazingira yetu, na uchumi utakaonufaisha washika-dau wote, na kuhimili matumaini yetu ya maisha ya kisasa.

Hayo ni malengo, lakini utekelezaji wake unategemea sana jasho na maarifa ya kila Mtanzania, kila mfanyakazi, kila mkulima, kila mfugaji, kila mvuvi, na kila mfanyabiashara, wa kike na wa kiume. Nchi yetu itaendelea kwa kazi, si kwa maneno matupu au tamaa ya maisha bora. Hatuwezi kuendelea kwa kutegemea fadhila za mataifa mengine. Wao si ndugu zetu, na wakati mwingine wanaweza kuwa na agenda zao ambazo si lazima zishabihiane na malengo yetu. Na hata kama wangekuwa ndugu zetu, wahenga walishatuambia, "Mtegemea cha ndugu hufa maskini".

Haki za binadamu zinazungumzwa sana, lakini jambo ambalo halizungumzwi sana ni ukweli kuwa adui mkubwa wa haki za binadamu ni umaskini. Kwa mtu ambaye hana uhakika wa chakula, haki yake ya msingi ni chakula. Kwa mtu ambaye hana nguo, haki yake ya msingi ni nguo. Na kwa yule ambaye hana mahali pa kuishi haki yake ya kwanza ni kujiwezesha kupata makazi.

Umaskini, na unyonge unaotokana na umaskini na utegemezi, ndiye adui mkubwa sana wa nchi yetu. Tusipokuwa waangalifu, tunaweza kuondolewa kwenye mkazo unaostahili kwenye umaskini, tukang'ang'ania mambo yapitayo ambayo hayampi shibe mwenye njaa, hayamvishi aliye uchi, na hayampi makazi asiye na mahali pa kuishi, sisemi kumpeleka mwanae shule au kumtibu akiugua.

Hivyo ni muhimu sana kwa wanasiasa wote – katika Chama Tawala na katika Upinzani – kuwajali zaidi wananchi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwenye vita dhidi ya umaskini. Mwanasiasa katika nchi maskini kama yetu, iwapo anao uadilifu wowote wa kisiasa ndani yake, ataona uchungu juu ya umaskini wa watu wetu, na ataunga mkono jitihada zote za Serikali kupiga vita umaskini.

Lakini kama wapo wanaofikiri kuwa bidii ya kuandaa maandamano na mikutano ya kudai mimi na Rais Karume tuwapishe Ikulu ndiyo njia sahihi ya kupiga vita umaskini, wanaota ndoto za mchana. Mimi, na nina hakika Rais Karume, tutaendelea kuweka mkazo sahihi na unaostahili katika kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wote, ikiwemo kukuza ajira, kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kuboresha huduma za jamii, na hatimaye kufikia malengo yetu ya kuondosha umaskini kwa faida ya wananchi wote.

Matokeo na Athari za Utandawazi


Ndugu Wafanyakazi,

Dunia yetu ya leo ina sifa mbili kubwa. Moja ni kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia, na ya pili ni mageuzi makubwa katika mifumo ya kijamii na kiuchumi. Mabadiliko na mageuzi hayo yanachochewa na utandawazi, ambao ni wimbi kubwa. Tunakabiliwa na chaguo ama kuacha kubadilika tusombwe na wimbi hilo, na kuendelea kuserereka pembezoni mwa maendeleo ya dunia ya karne ya 21; au tubadilike haraka kisera, kiutendaji, na kimtazamo, na kutafuta mbinu za kuhakikisha nasi tunafaidika katika mfumo huu mpya wa mahusiano duniani, na hivyo kuwahami wafanyakazi wetu.

Utandawazi huu unafuta mipaka baina ya nchi na nchi, bara na bara. Mipaka ya kijiografia haiwezi tena kuzuia maingiliano ya fikra, teknolojia, ujuzi, biashara na mitaji. Katika hali hiyo ushindani unakuwa mkali sana, kwenye kila kitu; ushindani ambao sisi tunauingia tukiwa dhaifu kuliko wenzetu.

Katika mazingira haya, uwekezaji mitaji ndio njia pekee ya kukuza uchumi, kupatikana kwa nafasi za ajira, na kuboresha maisha ya wananchi. Ndiyo maana nchi zote, kubwa na ndogo, tajiri na maskini, zinashindana kuvutia wawekezaji mitaji, kwa kushindana kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kisera, kiutendaji, kisheria - ikiwemo sheria za kazi - na kwa kuboresha miundo mbinu.

Iwapo sisi hatutabadilika, tutajipunguzia mvuto wetu kwa wawekezaji, wakati ambapo sisi wenyewe ndani ya nchi hatuna uwezo wa mitaji na ujuzi kuzalisha bidhaa na kutoa huduma za kushindana kwenye soko la kimataifa. Ni kweli baadhi ya hatua tunazolazimika kuzichukua zinaweza kuathiri baadhi ya wafanyakazi, hasa kwa siku za mwanzo. Lakini, ingawa dawa siku zote ni chungu, hatima yake ni kupona. Kinyume chake ni kukaribisha maradhi, na hata kifo.

Hata hivyo, napenda niwahakikishieni kuwa tunachukua, na tutaendelea kuchukua, kila tahadhari ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa letu, maslahi ya wafanyakazi na maslahi ya wananchi. Hatufanyi mageuzi, na hatuchukui hatua za kuvutia wawekezaji, kwa mtindo wa "bendera fuata upepo". Tunakuwa makini, na kuona hoja ipi inakubalika, na ipi haikubaliki.

Kwa upande wa ushindani wa kibiashara tunayo kazi kubwa mbele yetu inayohitaji ushirikiano mkubwa kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi. Kwanza, lazima tuongeze uzalishaji na tija. Lazima tubadili mtazamo wetu kuhusu kazi, na tupende kufanya kazi kwa kujituma zaidi kuliko kungoja kutumwa, tufanye kazi kwa bidii, kwa ubunifu na kwa maarifa. Pili, lazima tuongeze ubora wa bidhaa tunazotengeneza na kuzifunga vizuri kama washindani wetu katika soko la dunia wafanyavyo. Tatu, lazima tupunguze gharama za uzalishaji na uendeshaji ili bei ya bidhaa zetu iweze kushindana katika masoko ya dunia. Nne, lazima tupunguze gharama za kufanyia biashara. Na tano lazima tuwe hodari zaidi katika kujitangaza na kutafuta masoko mapya, ikiwemo masoko yaliyo jirani nasi.

Na hapa napenda nirudie tena mwito wa kuwa na ushirikiano wa karibu sana kati ya Serikali, waajiri, na wafanyakazi. Tusipokuwa kitu kimoja, na badala yake kuendekeza malumbano na mivutano, hatutafanikiwa. Tuazimie kuanzia leo kuvuta pamoja, si kuvutana.

Upo pia ushindani wa ujuzi na maarifa. Tanzania tuna maliasili nyingi, lakini dunia ya leo, na hasa dunia ijayo, itatawaliwa na wenye maarifa, kwa maana ya sayansi, teknolojia, elimu na ujuzi. Kuwa na maliasili peke yake haitoshi. Hatuna budi tujinoe kwa elimu na ujuzi, na hasa elimu inayomfanya mtu aajirike au ajiajiri.

Yapo malalamiko kuwa wawekezaji kutoka nje wanaajiri sana wageni. Tatizo hili linakuzwa mno kuliko hali halisi ilivyo. Ukiacha sekta kama vile madini ambapo hatuna wataalamu wa Kitanzania wa kutosha, kwenye sekta nyingine nyingi wawekezaji hao hawaruhusiwi kuajiri zaidi ya wageni 5. Utafiti tulioufanya kwenye baadhi ya miradi unaonyesha kuwa kwenye sekta ya viwanda, wageni walioajiriwa ni chini ya asilimia moja ya wafanyakazi wote; kwenye utalii ni zaidi kidogo ya asilimia moja; kwenye madini ni karibu asilimia 15, na kwenye huduma ni asilimia moja. Hivyo hali si mbaya sana, na itazidi kuwa nzuri siku zijazo.

Changamoto kwetu Watanzania ni kuhakikisha tunao wataalamu wa kiwango kinachoweza kushindana na wataalamu wengine duniani, tukianzia na soko la ajira la Afrika Mashariki.

Ndugu Mwenyekiti,
Tutaendelea kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani usiokuwa wa haki kutoka bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizaji wa bidhaa kwa njia ya magendo. Lakini katika dunia ya utandawazi, hoja ya kulinda viwanda vya ndani ni hoja ya mpito tu wakati nchi changa zinajenga uwezo wa kuhimili ushindani. Hivyo utaratibu wa kulinda viwanda lazima uende sambamba na juhudi za makusudi kuongeza uwezo wa ushindani. Na hilo halitawezekana iwapo tutavilinda mno viwanda vyetu.

Kazi na Ajira


Ndugu Wafanyakazi,

Leo napenda pia nizungumzie dhana ya kazi kwa upande mmoja, na dhana ya ajira kwa upande mwingine. Lazima tujifunze kubadili uelewa wetu wa kazi, na uelewa wetu wa ajira. Maana si lazima kila penye kazi pawe na ajira, na si lazima kila penye ajira kuwe na kazi.

Mfano mzuri wa kazi bila ajira ni kina mama. Wanafanya kazi kubwa na muhimu katika familia. Lakini hawana ajira, wala hawalipwi mshahara. Kwa upande mwingine, na hasa kwenye sekta ya umma, wapo watu wana ajira, lakini hawana kazi, au wanagawana kazi ambayo ingeweza kufanywa na mtu mmoja tu. Wapo wanaolipwa mshahara kamili kwa nusu kazi, au robo kazi, na wapo hata wanaolipwa kwa vile tu wameajiriwa, hata kama hawakufanya kazi yoyote.

Tatizo la baadhi ya watu kupenda kulipwa bila kufanya kazi inayolingana na malipo si letu peke yetu. Ipo hadithi ya bwana mmoja kutoka nchi tajiri mojawapo ambaye alikuwa na tabia hiyo. Yeye alikuwa amepunguzwa kazi na akawa analipwa fedha za kujikimu kwa vile alikuwa hana kazi. Ikafika wakati utaratibu huo wa kulipwa bila kazi ukafutwa, akalazimika kutafuta kazi. Akamwendea mwenye nyumba mmoja na kumwomba kazi ya kufyeka majani kwenye bustani yake.

Mwenye nyumba akamwambia, "Kwa kawaida anakuja kijana wa jirani yangu kufanya kazi hiyo, na ninamlipa sh.20,000/=. Lakini kwa vile nakuona una shida ya kazi, wewe nitakulipa sh.25,000/=."
Yule bwana akamjibu, "Tafadhali mwache kijana aendelee na kazi yake; wewe nipe tu hizo sh.5,000/=."

Ndugu Wafanyakazi,
Mengine haya yanachekesha, lakini kujenga uchumi wa kisasa, unaohimili ajira kubwa, na maslahi bora zaidi, si jambo la lelemama, au jambo la kuchekesha. Tupende tusipende, tunakabiliwa na ushindani mkubwa sana, na tukiendelea na tabia hii hatutaweza kuuhimili ushindani huo; viwanda vitafungwa; na ajira ama itahamia nchi za nje, ikiwemo nchi jirani, au wao watakuja nchini kuchukua kazi zetu.

Katika uchumi unaohimiliwa na sekta binafsi ajira na maslahi ya wafanyakazi havipatikani kwa amri ya Serikali, bali kwa uwezo wa kuzalisha, kushindana, na kupata faida. Kama tunataka uchumi ukue, uweze kushindana na kuvutia wawekezaji wengi zaidi, lazima tujenge ushirikiano na kuaminiana zaidi kati ya Serikali, wawekezaji, wananchi na wafanyakazi. Tuunde ubia wa kuhakikisha taifa linafanikiwa, wawekezaji wanafanikiwa, na wafanyakazi nao wanafanikiwa.

Mwaka hadi mwaka tunalalamika kuwa wapo vijana 600,000 – 700,000 wanaoingia katika soko la ajira, wakati sekta rasmi inaweza kuajiri kiasi cha 25,000 tu kwa mwaka. Lakini pia tujiulize hao vijana 600,000 wanaweza kufanya kazi gani ya kuajiriwa? Wana ujuzi gani wenye soko katika hali halisi ya uzalishaji na utoaji huduma nchini? Ukweli ni kuwa wengi wao hawaajiriki kwa urahisi.
Lazima tukubali pia kuwa tunaposema uti wa mgongo wa uchumi wetu ni kilimo, ufugaji na uvuvi, maana yake ni kuwa uti wa mgongo wa uhakika wa ajira ni kilimo, ufugaji na uvuvi, pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya sekta hizo. Tunasema hakuna ajira, lakini tunayo ardhi tele inayofaa kwa kilimo na ufugaji, na tunayo bahari, mito na maziwa yenye samaki. Kwa vyovyote vile haitawezekana kwa sekta rasmi kuajiri wote watafutao kazi. Kwa Watanzania wengi, ajira maana yake ni kujiajiri katika kilimo, ufugaji na uvuvi. Huo ni ukweli ambao hatuna budi sote kuukubali.

Ndugu Wafanyakazi,
Ni kweli Serikali ina wajibu wa kufuatilia wawekezaji ili kuhakikisha wanatekeleza masharti ya mikataba na maelewano yetu, na kufuata sheria za nchi. Tutaendelea kutekeleza jukumu hilo, na kuongeza uwezo wa ukaguzi. Vyama vya wafanyakazi navyo viwe macho. Kwa upande wake, Serikali imeamua kukifanya Kitengo cha Afya na Usalama wa Wafanyakazi kuwa Wakala wa Serikali ili kiweze kujiendesha kwa ufanisi na kutoa huduma bora zaidi kwa wafanyakazi na waajiri.

Ipo pia mipango mingi ya kuimarisha uwezo wa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, kwa msaada wa wahisani mbalimbali. Tunao mradi wa kuimarisha Idara ya Kazi unaofadhiliwa na Serikali ya Denmark. Lengo ni kuweka mazingira bora zaidi ya kisera na kisheria katika mahusiano ya kikazi, kuwa na sheria za kazi zinazoenda na wakati na kuvutia uwekezaji zaidi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, kuongeza uzalishaji na tija za wafanyakazi, na kujenga maelewano mazuri sehemu za kazi.

Mradi mwingine, ambao huu unafadhiliwa na Serikali ya Marekani, ni wa kuanzisha Soko la Ajira. Kazi iliyoanza Aprili mwaka jana ya kukusanya takwimu za msingi kuhusu ajira inatazamiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu. Kituo cha kwanza cha Soko la Ajira (Employment Exchange Centre) kitaanzishwa hapa Dar es Salaam, na baadaye mikoani. Miongoni mwa majukumu ya vituo hivyo itakuwa kutoa ushauri nasaha kwa wanaotafuta kazi, kusaidia kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri, na kukusanya na kutoa takwimu za hali ya soko la ajira kwa ujumla. Huduma hii itawarahisishia waajiri kutafuta wafanyakazi, na wanaotafuta ajira kujua kazi ambazo wana ujuzi nazo zinapatikana wapi.

Ndugu Wafanyakazi,
Tunalo pia bado tatizo la unyanyasaji na ubaguzi wa wanawake katika jamii zetu, katika shule na vyuo, na katika ajira. Kutokana na jitihada zinazochukuliwa na Serikali tatizo linapungua, lakini halijakwisha. Natoa tena wito kwetu sote kufuta aibu hii ya kunyanyasa au kubagua wanawake.

Serikali pamoja na wabia-jamii, kwa msaada wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), tumetekeleza mradi wa kuangalia upya hali ya ajira kwa wanawake katika mazingira ya mageuzi ya uchumi. Tayari ripoti imekamilika na imetupa mahali pa kuanzia katika kutetea na kulinda maslahi ya wanawake. Ikibidi tutabadili sheria na taratibu. Lakini, kazi kubwa zaidi ni kubadili fikra, mazoea, mila na desturi zinazokwamisha ukombozi wa kweli wa wanawake. Kazi hiyo si ya Serikali peke yake; ni ya jamii nzima. Na hapa tena navipongeza vyama huru vya wafanyakazi kwa kuonyesha njia, na kumchagua Mama Sitta awe Mwenyekiti wa kwanza wa Shirikisho lao. Hiyo ni ishara kuwa tutashirikiana vizuri kutetea haki na maslahi ya wanawake sehemu za kazi.

Sheria na Mikataba


Ndugu Mwenyekiti,

Serikali inatambua umuhimu wa kuridhia Mikataba ya ILO kuhusu malipo sawa kwa kazi sawa, kuondosha ubaguzi katika ajira, na kupiga marufuku ajira mbaya sana ya watoto. Mikataba hiyo pia inahusu haki za msingi za binadamu ambazo zimo ndani ya Katiba yetu. Hivyo tatizo si nia ya kuridhia, bali utaratibu tu wa kufanya hivyo. Na hivi sasa hatua za kuridhia mikataba hiyo karibu zitakamilika.

Kuhusu ajira ya watoto, tangu mwaka 1994 Tanzania imetekeleza Mpango wa Kimataifa wa Kuondosha Ajira ya Watoto kwa kushirikiana na waajiri na wafanyakazi. Juhudi hizo ziliipelekea Tanzania kuwa kati ya nchi tatu duniani zitakazotekeleza mpango wa muda maalum kumaliza ajira mbaya sana ya watoto. Tunatambua pia kuwa umaskini ndicho chanzo na kishawishi kikubwa cha ajira ya watoto. Hivyo juhudi zote za Serikali za kuondosha umaskini zinalenga pia kuondosha tatizo la ajira ya watoto.

Nia ya Serikali ni kuwa na sera na mfumo wa sheria za kazi zinazolinda maslahi ya wafanyakazi, na maslahi ya waajiri, ili mahusiano mema kazini yawe yale ambayo msingi wake ni kuheshimu haki na maslahi ya wafanyakazi na waajiri, yenye tija katika uzalishaji, yanayowezesha ushindani, na kwa hiyo kuleta maendeleo na maisha bora.

Mikopo ya Nyumba kwa Wafanyakazi


Ndugu Mwenyekiti,

Mojawapo ya matatizo ya wafanyakazi wengi ni kukosa uhakika wa nyumba za kuishi wakiwa kazini, lakini hasa baada ya kustaafu. Kumiliki nyumba kunatosheleza hitaji muhimu la mwanadamu; na kumpa heshima na utulivu wa fikra na maisha.

Katika miaka 10 ya kwanza baada ya uhuru, kulikuwa na mfuko wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa umma. Mfuko huo uliwasaidia watumishi wa umma wakati huo kujijengea nyumba. Leo hakuna mfuko kama huo wenye uwezo wa kutosheleza kujenga nyumba za watumishi kwa mkopo. Matokeo yake, na kwa vile mfumo wa ukopeshaji fedha kwa ajili ya kujenga nyumba kwenye benki zetu bado haujaimarika, inabidi wananchi walio wengi wajenge nyumba kwa fedha kutoka mifukoni mwao.

Ujenzi wa namna hiyo ni ishara ya kuwa nyuma sana kimaendeleo, na kwa watumishi wa umma ni chanzo, kichocheo na kishawishi kikubwa sana cha rushwa. Dunia ya leo watu hawajengi hivyo; na ni matumizi mabaya ya fedha hata kwa wale ambao wanazo. Kwa vile nyumba ni mali isiyohamishika, hakuna sababu ya kujenga kwa fedha kutoka mfukoni; na wala hakuna sababu kwa benki zetu kutaka mkopaji arejeshe mkopo katika muda mfupi. Kwenye nchi zilizoendelea mikopo ya nyumba inalipwa kwa hata zaidi ya miaka 25.

Kwa sababu hiyo nimeamua, kwa kuzingatia sera ya Chama changu, kuwa tuanzishe mfumo ulio wazi wa mikopo ya nyumba na uwekaji nyumba rehani kwa jumla; na pia kuwa na utaratibu mwingine maalum kwa watumishi wa umma.

Hivi sasa Serikali inashauriana na washika-dau mbalimbali, pamoja na benki zetu, kuona namna bora ya kutekeleza jambo hili kwa haraka, lakini kwa makini sana, maana hatutaki yale yaliyoisibu Benki ya Nyumba yarudiwe tena. Lazima nitoe tahadhari. Mkopo ni mkopo, na lazima urejeshwe kulingana na makubaliano kati ya mkopaji na mkopeshaji. Ujanja wa kukwepa wajibu wa kulipa hauwezi kupewa mwanya tena kwenye sheria zetu.

Maandalizi ya kisera na kisheria yanaendelea. Karibu tunakamilisha Kanuni za Sheria ya Ardhi ya mwaka jana kwa kushirikiana na washika dau wengine ili kuvutia benki kukopesha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Serikali pia itaendeleza sera za jumla za uchumi zitakazosaidia kuweka mazingira bora kwa ukopeshaji wa muda mrefu, kama vile kuendelea kushusha mfumuko wa bei, na riba za benki.

Nawaombeni viongozi wa vyama vya wafanyakazi nanyi mhamasishe wafanyakazi kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa, na kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, muanzishe ushirika wa nyumba. Tatizo la nyumba ni kubwa, na ufumbuzi wake lazima utuhusishe na kutushirikisha wote.

Rushwa na Ubadhirifu


Ndugu Wafanyakazi,

Nizungumzie kidogo kuhusu rushwa na ubadhirifu. Wote wawili hawa ni maadui wakubwa wa maendeleo na ustawi wetu. Ipo rushwa inayopotosha haki, na kuifanya iwe bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa. Na ipo rushwa inayopotosha maamuzi ya kiutendaji na kuliingizia taifa au taasisi yoyote ile hasara kubwa. Mfano ni pale ambapo barabara ambayo ingeweza kujengwa kwa sh.5 bilioni, inaishia kujengwa kwa sh.10 bilioni, na mzigo huo unabebwa na uchumi wa taifa, na hatimaye wananchi. Dhahiri rushwa ni kitu kibaya sana katika jamii na lazima tupigane nayo bila kuchoka au kukata tamaa.

Na rushwa si janga la Tanzania peke yake. Hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuthubutu kusema kuwa wao ni watakatifu kabisa katika suala hili. Tofauti zilizopo ni aina ya rushwa baina ya nchi na nchi, kiwango cha rushwa, na uwazi uliopo katika kujadili uwepo wa rushwa katika jamii na taifa.

Tanzania tumekuwa wazi sana kuhusu rushwa. Sijui ni nchi ngapi zimeunda Tume kama niliyounda mimi chini ya Jaji Warioba kutafiti rushwa kwa undani katika nchi yetu, kubainisha chanzo chake, na kuweka mpango maalum na mkakati wa kuipiga vita rushwa. Na utekelezaji unaendelea kwa kuziba mianya ya rushwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kuongeza uwezo wetu wa kupokea, kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kuhusu tuhuma zote za rushwa. Upo mkakati wa kitaifa, na upo mkakati kwa kila sekta na kila Wizara.

Kazi ya kupiga vita rushwa ni ngumu sana, hasa ikijipenyeza pia kwenye vyombo vinavyosimamia sheria na haki. Nyote ni mashahidi kuwa kesi za rushwa zinachukua muda mrefu mno. Wakati mwingine ni vigumu kupata ushahidi utakaothibiti mahakamani, hasa pale wale wenye taarifa za ndani na ushahidi hawako tayari kushirikiana na Serikali.

Siwezi kuwalaumu wananchi wanapoishiwa na subira. Wakati mwingine hata mimi natamani ningekuwa na uwezo wa kutia watu ndani pale tuhuma nzito dhidi yao zinaponifikia. Lakini zama hizo zimepita. Leo dhana inayoshamiri ni ya utawala wa sheria, ambapo mtuhumiwa anahesabika hana hatia hadi mahakama itakapoamua kesi inayomkabili.

Hali hiyo inaiweka Serikali katika hali ngumu sana. Vyombo vya habari vinaandika tuhuma za rushwa, na kuifanya jamii iamini kuwa yanayotajwa ni kweli, na hivyo wanataka wasikie kesho yake mtuhumiwa kafungwa au kafilisiwa. Hata marafiki zetu kutoka nchi za nje nao wanakosa subira. Lakini hao hao, na waandishi wa habari hao hao, ndio wa kwanza kutupa darasa juu ya haki za binadamu, utawala bora, na utawala wa sheria!!

Napenda niwahakikishieni, Ndugu Wafanyakazi, kuwa dhamira na utashi wa kisiasa wa kupiga vita rushwa sio tu upo pale pale, bali unaongezeka. Ambacho nina uhakika hakiongezeki ni ushirikiano wa wafanyakazi katika kupiga vita rushwa na ubadhirifu. Mimi ninaelewa wananchi wa kawaida wakinyoshea kidole Serikali na taasisi zake. Lakini napata taabu nikiambiwa wafanyakazi wanalalamikia rushwa. Maana, hakuna mtu anayeitwa Serikali anayepokea rushwa. Mpokea rushwa si Serikali; ni mfanyakazi mwenzetu, tunamjua, lakini tunaoneana haya. Huo ndio ukweli, na unafanya kazi yetu iwe ngumu sana.

Huko mikoani niliwahi kuwataka wananchi wafanye mikutano ya hadhara na kupiga kura ya maoni kuhusu wanaowatuhumu kula rushwa. Najua huu si utaratibu mzuri sana, lakini ulitupa pa kuanzia kwa kuwajua wanaotuhumiwa, na kuanza kuwachunguza.

Sasa niambieni. Ni mara ngapi mmesikia kuwa katika Wizara au Taasisi fulani wameitisha mkutano wa wafanyakazi wote kwa lengo la kupiga kura ya maoni, ya siri, ya kuwafichua wenzao wanaowajua kuwa ni wala rushwa? Maana haiwezekani awepo muuguzi katika hospitali anayedai rushwa kutoka kwa wagonjwa, halafu wenziwe wasimjue. Vivyo hivyo kwenye Jeshi la Polisi, Mahakama, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Elimu, na kadhalika.

Nakubali wito wenu kuwa vita dhidi ya rushwa izidi kuongezwa nguvu na kasi. Lakini nasema nafasi bado ipo kubwa kwa wafanyakazi kusaidia vita hivyo pale walipo, kwa wenyewe kuacha rushwa na ubadhirifu, na kwa kutoa taarifa za wenzao wanaochafua jina la mahali pao pa kazi kwa kupanukisha rushwa. Zama za ukimya wa kulindana sasa ziishe. Na wakati mwingine kunyosheana vidole baina ya sekta na sekta, wizara na wizara, idara na idara, haisaidii sana kama watu wasipoanza kusafisha rushwa pale walipo. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yupo hapa. Yeye hupenda kusema, "Mkia wa mbuzi ni mfupi; unasafisha pale alipolala."

Na sisi sawia. Mfanyakazi wa Wizara ya Elimu anakuwa mwepesi kulaumu rushwa aliyopambana nayo alipoenda mahakamani, lakini ile rushwa mtumishi wa mahakama aliyopambana nayo katika kumwandikisha mtoto wake shule haioni.

Natoa wito kwa vyama vipya vya wafanyakazi vione kuwa mojawapo ya kazi zao ni kusafisha jina la sehemu yao ya kazi, na jina la taaluma zao. Vyama vya wafanyakazi vione haya, na kuchukua hatua, pale jamii inapowanyooshea vidole kuwa ni wala rushwa au wabadhirifu. Vibuni mikakati ya kujisafisha, na ikibidi viombe msaada wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa katika kupanga na kutekeleza mikakati hiyo. Lazima pia, wote kwa pamoja, kujenga utamaduni wa kuona rushwa na ubadhirifu kuwa ni jambo la aibu, na kuwa mali isiyotokana na jasho, mali inayonuka rushwa, ubadhirifu na wizi, ni aibu na fedheha kubwa!

UKIMWI


Ndugu Wafanyakazi,

Nimefarijika kusikia risala yenu ikieleza kutambua kwenu kuwa janga la UKIMWI linahitaji elimu kwa jamii yote pamoja na waajiri ili kufanikisha mapambano dhidi yake. Mmetoa mwito pia kuwa wafanyakazi walioathirika wasitengwe au kunyanyaswa mahali pa kazi. Nakubali na ninaungana nanyi kabisa katika hoja yenu hiyo.

Ningependa sote tujiulize tena maswali magumu bila aibu na tuchukue hatua bila ajizi. Je, tangu mwaka huu uanze tumeshiriki kiasi gani kuzuia kuenea kwa UKIMWI? Je, wewe umekwisharekebisha mwenendo wako na kuacha tabia zinazochangia kuenea kwa UKIMWI? Je, hapo kazini pamekuwa na mwamko mpya wa kupambana na UKIMWI? Wewe mfanyakazi unashiriki vipi?
Ndugu Wafanyakazi,

Kila mmoja atafakari kwa dhati moyoni mwake na achukue hatua. Nawaomba pia waajiri wawe mstari wa mbele katika vita hivi na wawasaidie wafanyakazi wao kwa kila hali kuweza kujikinga, na kwa walioathirika tayari kuwatendea haki bila ubaguzi. Kila sehemu ya kazi sasa iwe na utaratibu wa kukumbushana mara kwa mara juu ya UKIMWI, na mkakati mahususi wa kuzuia kuenea kwa virusi vya UKIMWI.

Hitimisho:


Ndugu Wafanyakazi,
Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuwakumbusha kuwa njia ya maendeleo imejaa jasho na vumbi. Tuzingatie utamaduni wa kupenda kufanya kazi kwa bidii, maarifa, ubunifu na kujituma. Lawama ni tamu ikitoka mdomoni, lakini peke yake haitapeleka mkono kinywani. Na katika kujituma kila mfanyakazi akumbuke kuwa la muhimu si muda anaotumia kufanya kazi, bali kiasi cha kazi anayoweza kuifanya katika muda aliopewa.

Wenzetu majirani na duniani kote wanajishughulisha, usiku na mchana, kuongeza uzalishaji na kunoa uwezo wao wa tija na ushindani. Na sisi tuamke. Nina matumaini makubwa nanyi viongozi wapya wa vyama huru vya wafanyakazi kwamba mtashirikiana vizuri na Serikali na waajiri ili nchi yetu ijikomboe kiuchumi na kuleta ustawi kwa wananchi wake. Hakuna njia ya mkato, isiyo na machungu. Tuwaongoze wafanyakazi kujua na kuzingatia jambo hilo. Na tuwashirikishe kama tunataka kushinda vita hivi.

Bwana mmoja aliwahi kusema, "Mtu akikwambia ametajirika kutokana na kazi nzito, muulize, kazi hiyo nzito ameifanya nani?"

Na sisi sote tunatamani maisha bora, ya kisasa. Tunajua pia kuwa utajiri na maisha bora chanzo chake ni kazi nzito. Swali. Kazi hiyo nzito aifanye nani?

Nawatakieni Sikukuu njema.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.
 
Duh, jamaa anauwezo mkubwa wa kuongea. Ni hotuba nzuri na yenye kusema ukweli halisi wa nchi kama yetu. Inatia mkazo kwa watu wafanye kazi, inaonyesha namna kiongozi wa nchi anavyotakiwa, inatoa dira lakini weekness zake ni kuwa alifanikiwa kutufunika macho tusione yanayotendeka serikalini.
Jamaa alikuwa anaongea vizuri sana, kiasi cha kuaminika kirahisi kwa wananchi, lakini nyuma ya pazia anauma ile mbaya.
But anyway, Big up Mr Ex president BWM.
 
jamaa hakuwahi kuwatukana wafanyakazi wazandiki,wafitini wala wanafiki hotuba nzuri japo kuna uongo ila kidogo,mkapa angekuwa na mke mzuri wa kumshauri angekuwa sasa anahesabika kama shujaa na angekuwa amezoa tuzo ya MO IBRAHIM
 
BMW ameponzwa sana na mkewe otherwise we would have a president to remember and not to forget!
 
BMW ameponzwa sana na mkewe otherwise we would have a president to remember and not to forget!

Mimi sikubaliani na hili, tatizo ni kwamba watu hawakumfahamu vyema Mkapa kabla hajawa Rais. Waulizeni watu waliofanya kazi Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, na hasa watu wa Idara ya Uhasibu, wao ndio wanaweza kukupa ukweli halisi wa madudu ya Mkapa. Je, na kipindi hicho ilikuwa ni kwa sababu ya mkewe?

Anna Mkapa alikuja ku-take opportunity baada ya kuona uozo ulivyokuwa unakwenda. Uvundo wa Mkapa ulianzia kwenye kuuza NBC na yaliyofauata wote tunayajua. Kwa hiyo mnataka kusema ununuzi wa Radar nao ni Mama Mkapa? Ununuzi wa ndege ya rais, Meremeta, Mwananchi, EPA, Twin Towers, na mikataba mibovu ya madini.

Kuna projects ambazo Mama Mkapa alikuwa na uhusiano nazo moja kwa moja, kwa mfano dili la TANESCO, KIWIRA, na hiyo miradi yake mingine ya kukopesha walimu, dili za kununua nyumba na mengineyo. Lakini ukichunguza sana, asimilia kubwa ya ufisadi aliofanya Mkapa ni kwa kushirikiana na mafisadi wenzake ambao leo hii bado wako madarakani na wanaendelea kumlinda kwa nguvu zote.
 
BMW ameponzwa sana na mkewe otherwise we would have a president to remember and not to forget!
Katika biblia Adamu alipokosa na kutoa utetezi kuwa ni kwa sababu ya mkewe hilo halikumpa Mungu excuse ya kutomuadhibu. Tena alipewa bonge la adhabu maana yeye ndiye alipewa maagizo asiguse yale matunda.

Ben inabidi abebe lawama maana yeye ndiye alikuja kwetu kuomba tumuamini na kumpa kura awe rais wetu na wala si Anna. Isitoshe ni yeye Ben aliyeapa kuwa atalinda katiba na kutawala akifuata sheria. Kwa hili anawajibika bila kujali habari zozote za kuhurumiwa.

Kwa kikwete yeye na mkewe wote wanaomba kura hivyo anaweza kusema yule mke wangu aliyeniombea kura ndiye alinifanya nionekane nina makosa.
 
Asante Mkandara kwa kutukumbusha. Kwa hali ya mambo ilivyo inawezekana kabisa bado Mkapa akawa hero kwa kipindi kirefu.
 
Kwa kikwete yeye na mkewe wote wanaomba kura hivyo anaweza kusema yule mke wangu aliyeniombea kura ndiye alinifanya nionekane nina makosa.

lol ... Mchukia Fisadi umeniacha hoi. Maana naona Mama Kikwete naye yuko kwenye kampeni za kitanda kwa kitanda akimuombea kura mumewe. Hii inaashiria kitu kibaya sana, JK akipata urais tena lazima mama nae adai mafao yake ya kupiga kampeni, so tujiandae kufisadiwa zaidi kuliko ufisadi wa Anna Mkapa.
 
Asante Mkandara kwa kutukumbusha. Kwa hali ya mambo ilivyo inawezekana kabisa bado Mkapa akawa hero kwa kipindi kirefu.

Hotuba nzuri haimfanyi awe HERO, to me Mkapa ni ZERO. Ni mzuri sana wa kujenga hoja, lakini utekelezaji wa hotuba hizo ndo mgogoro unapoanzia.

Labda nianze kwa kukumbusha machache: Wakati anapiga kampeni za kwanza kabisa 1995, alisema kwamba mtu AKITUHUMIWA kuwa fisadi ama mla rushwa, atamuwajibisha mara moja, au ni sababu tosha ya kumuondoa madarakani. Kauli hiyo ilikuwa ikirejewa sana ile Radio ya Ujirani ya pale St. Joseph. Fr. Francois aliiweka hiyo kwa makusudi. Baadaye Mkapa alikuja kusema huwezi kumshughulikia mtu kwa tuhuma za majungu. Je, ina maana tuhuma zote zilizokuwa zikipigiwa kelele zilikuwa majungu wakati akiwa madarakani na alipokuja kuondoka na ukweli kuwekwa wazi, bado tutamwita HERO?

Mkapa anasema wananchi ndio tunajua wala rushwa na hatuwataji kwa kuwa tunaoneana haya, lakini huyo huyo alipoanza kupelekewa wala rushwa na mafisadi, alikuwa wa kwanza kulalamika kwamba kuna tuhuma za majungu. Sasa wananchi tufanye nini?

Ni nani anatakiwa kufuatilia tuhuma? Mwananchi au Vyombo vya dola? Hivi wakati Radar inanunuliwa hakujua kwamba lilikuwa bomu? Kila kitu kilikuwa kwenye file mpaka Clare Short akasafiri kutoka UK kuja Dar, na baadaye akaamua kujizulu, bado Mkapa amekomaa na radar yake.

Net Group Solution wakati inakuja waliingizwa TANESCO kwa usimamizi wa FFU kwa maagizo toka Ikulu, kelele zote hizo hakusikia? Hiyo dili ilimuondoka Maokola Majogo kutoka Wizara ya Nishati na Madini, akapelekwa kule kwa Makamu wa Rais akapumzike, maana alikuwa anaweza uzibe wa Kaburu kuingia. Watu walishaandika mpaka wamiliki wa kampuni ya wazawa ambayo ndio ilikuwa inashirikiana na Kaburu. Bado mtu anasema tuhuma za majungu, na bado tutamwita Hero.

Mkuu wangu Mkandara, nakubaliana na wewe, SIASA ni UONGO UNAOKUBALIKA. Maana kilichotamkwa na Mkapa, si kile alichokuwa akifanya nyuma ya pazia, na alikuwa akiandamwa na magazeti utamuona anaongea kwa kufoka mpaka povu linamtoka na kumbe anatetea ufisadi tu.
 
Hotuba nzuri haimfanyi awe HERO, to me Mkapa ni ZERO. Ni mzuri sana wa kujenga hoja, lakini utekelezaji wa hotuba hizo ndo mgogoro unapoanzia.

Labda nianze kwa kukumbusha machache: Wakati anapiga kampeni za kwanza kabisa 1995, alisema kwamba mtu AKITUHUMIWA kuwa fisadi ama mla rushwa, atamuwajibisha mara moja, au ni sababu tosha ya kumuondoa madarakani. Kauli hiyo ilikuwa ikirejewa sana ile Radio ya Ujirani ya pale St. Joseph. Fr. Francois aliiweka hiyo kwa makusudi. Baadaye Mkapa alikuja kusema huwezi kumshughulikia mtu kwa tuhuma za majungu. Je, ina maana tuhuma zote zilizokuwa zikipigiwa kelele zilikuwa majungu wakati akiwa madarakani na alipokuja kuondoka na ukweli kuwekwa wazi, bado tutamwita HERO?

Mkapa anasema wananchi ndio tunajua wala rushwa na hatuwataji kwa kuwa tunaoneana haya, lakini huyo huyo alipoanza kupelekewa wala rushwa na mafisadi, alikuwa wa kwanza kulalamika kwamba kuna tuhuma za majungu. Sasa wananchi tufanye nini?

Ni nani anatakiwa kufuatilia tuhuma? Mwananchi au Vyombo vya dola? Hivi wakati Radar inanunuliwa hakujua kwamba lilikuwa bomu? Kila kitu kilikuwa kwenye file mpaka Clare Short akasafiri kutoka UK kuja Dar, na baadaye akaamua kujizulu, bado Mkapa amekomaa na radar yake.

Net Group Solution wakati inakuja waliingizwa TANESCO kwa usimamizi wa FFU kwa maagizo toka Ikulu, kelele zote hizo hakusikia? Hiyo dili ilimuondoka Maokola Majogo kutoka Wizara ya Nishati na Madini, akapelekwa kule kwa Makamu wa Rais akapumzike, maana alikuwa anaweza uzibe wa Kaburu kuingia. Watu walishaandika mpaka wamiliki wa kampuni ya wazawa ambayo ndio ilikuwa inashirikiana na Kaburu. Bado mtu anasema tuhuma za majungu, na bado tutamwita Hero.

Mkuu wangu Mkandara, nakubaliana na wewe, SIASA ni UONGO UNAOKUBALIKA. Maana kilichotamkwa na Mkapa, si kile alichokuwa akifanya nyuma ya pazia, na alikuwa akiandamwa na magazeti utamuona anaongea kwa kufoka mpaka povu linamtoka na kumbe anatetea ufisadi tu.

Keil, nashukuru kwa kuraise hoja zako. Nafahamu fika Mkapa alifanya mambo mengi ambayo yanautata kwa Taifa letu. Lakini ukisoma vizuri thread yangu nimesema kwa jinsi hali ya mambo ilivyo, huyu bwana sikumoja tutamuona ni hero. Time will tell au pengine naota tu maana ni kama naona giza tu mbele yangu.
 
Mimi sikubaliani na hili, tatizo ni kwamba watu hawakumfahamu vyema Mkapa kabla hajawa Rais. Waulizeni watu waliofanya kazi Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, na hasa watu wa Idara ya Uhasibu, wao ndio wanaweza kukupa ukweli halisi wa madudu ya Mkapa. Je, na kipindi hicho ilikuwa ni kwa sababu ya mkewe?

Anna Mkapa alikuja ku-take opportunity baada ya kuona uozo ulivyokuwa unakwenda. Uvundo wa Mkapa ulianzia kwenye kuuza NBC na yaliyofauata wote tunayajua. Kwa hiyo mnataka kusema ununuzi wa Radar nao ni Mama Mkapa? Ununuzi wa ndege ya rais, Meremeta, Mwananchi, EPA, Twin Towers, na mikataba mibovu ya madini.

Kuna projects ambazo Mama Mkapa alikuwa na uhusiano nazo moja kwa moja, kwa mfano dili la TANESCO, KIWIRA, na hiyo miradi yake mingine ya kukopesha walimu, dili za kununua nyumba na mengineyo. Lakini ukichunguza sana, asimilia kubwa ya ufisadi aliofanya Mkapa ni kwa kushirikiana na mafisadi wenzake ambao leo hii bado wako madarakani na wanaendelea kumlinda kwa nguvu zote.

Watu wanaosema Mkapa kashawishiwa na mkewe hawamjui Mkapa.

Mkapa mzee yule ndio wale wazee wanaomfanya mke anakuwa kama mtoto, Mama Anna hakuweza kufurukuta kwa Ben Mkapa let alone kumpangia ajenda.

Mkapa kawadindishia kina Tony Blair and company akimtetea Mugabe mkutano wa Commonwealth Australia, mpaka Tony Blair akaomba undugu kutokana na kuona resolve yake, leo mnataka kusema huyu ni mtu wa kushawishiwa kirahisi na mkewe ?

Huyu mama Anna Mkapa anaweza kabisa kuwa na makosa, lakini hili la kwamba yeye ndiye aliyemshawishi Mkapa afanye madudu ni kumuonea. Kama mtu anawajua the Mkapas on a personal level anaweza kukuambia mpaka wanaingia Ikulu yule mama alikuwa muoga kama mtawa, na Mkapa jeuri kama firauni, ndiyo maana hata wakataka kuachana kabla ya uchaguzi 1995, Nyerere alipoona habari ya urais akawapatanisha, kama si urais wangekuwa wameshatalikiana.

Sasa huyu ni mtu wa kushawishiwa na mkewe ?
 
Wakuu zangu mimi nimejaribu kumsoma na kurudisha fikra zangu mwaka 2001, kisha narusha mbele kuja mwaka 2005 alipoondoka madarakani yaani hotuba yake na matendo yake yeye mwenyewe ni Tofauti kubwa kama Mbingu na Ardhi.

Je, Kiongozi bora ni yule anayeweza kuandika vizuri hotuba na kusema sana majukwaani au Uzalendo wake yeye mwenyewe?.. ndipo narudi ktk CV ya kiongozi hasa tunapojua kesha fanya madudu huko nyuma sidhani kama ni jambo la Busara wananchi kumchagua mtu kwa sababu tu anajua kuongea vizuri.

Yaani nilipofika kwenye Rushwa na jinsi alivyolipiga vita nashindwa hata kuelewa huyu mtu alikuwa na akili za aina gani kama sii TAPELI kubwa kupita kiasi..samahani sikukusudia kutukana ila nashindwa kabisa kuelewa kilimkuta kipi hata akapinduka.
 
Back
Top Bottom