Hotuba ya JK Siku ya Sheria | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hotuba ya JK Siku ya Sheria

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by Mpita Njia, Feb 2, 2011.

 1. Mpita Njia

  Mpita Njia JF-Expert Member

  #1
  Feb 2, 2011
  Joined: Mar 3, 2008
  Messages: 7,012
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
  TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
  WAKATI WA KUADHIMISHA SIKU YA SHERIA
  NCHINI, TAREHE 2 FEBRUARI, 2011
  Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
  Muungano wa Tanzania;
  Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
  Muungano wa Tanzania;
  Mheshimiwa Celina Kombani, Waziri wa Katiba na Sheria;
  Waheshimiwa Majaji Wakuu Wastaaafu;
  Waheshimiwa Majaji wa Rufani;
  Mheshimiwa Jaji Kiongozi;
  Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu;
  Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
  Rais wa Chama cha Mawakili Tanzania Bara;
  Wageni Waalikwa Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

  Nakushukuru sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kushiriki katika sherehe za mwaka huu za kuadhimisha Siku ya Sheria nchini. Ninaungana nawe na viongozi wa dini kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya na kutuwezesha kukutana kwa mara nyingine tena katika siku hii adhimu. Kwa vile ni mara ya kwanza tunakutana katika sherehe hizi tangu uwe Jaji Mkuu wa Tanzania, niruhusu nikupongeze na kukutakia kila la heri katika kutekeleza jukumu lako kubwa la kuongoza mhimili huu muhimu wa kutoa haki nchini. Nakuahidi ushirikiano wangu na wa wenzangu wote Serikalini katika kutimiza majukumu yako. Niruhusuni pia nitoe pongezi za dhati kwa Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Augustino Ramadhani kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha uongozi wake. Lakini pia nampongeza kwa utumishi wa muda mrefu na uliotukuka katika mahakama nchini. Tunamtakia maisha mema katika ustaafu wake.
  Elimu ya Sheria kwa Umma
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Nakupongeza sana wewe na Majaji wenzako kwa kuamua kuwa katika maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka huu, Elimu kwa Umma Kuhusu Mahakama iwe ndiyo ujumbe mkuu. Ni uamuzi sahihi kabisa. Katiba ya nchi imeeleza kinaga ubaga katika ibara ya 107A, kuwa “Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama”. Kwa sababu hiyo, watu hawana budi kuifahamu vyema Mahakama nchini hasa mfumo wake, jinsi inavyofanya kazi na namna gani wanavyoweza kunufaika nayo.
  Nakubaliana nawe, Jaji Mkuu, kuwa elimu kwa umma ndiyo njia pekee ya kuwaongezea wananchi ufahamu wao kuhusu chombo hiki muhimu katika maisha yao. Nawapongeza kwa juhudi muifanyayo hivi sasa ya kutoa elimu ya Mahakama kwa umma. Nakubaliana nawe kuwa bado juhudi zaidi ziongezwe kwa upande wenu na ule wa wadau wengine mbalimbali wakiwemo wale uliowataja katika hotuba yako. Vyombo vya habari vinayo nafasi maalum. Nawaomba mvitumie kwa ukamilifu kuelimisha umma na wao wenyewe niwaombe pia wajitolee kufanya hivyo kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake.
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Nami, nalisisitiza suala la elimu kwa wananchi kuhusu Mahakama kwa sababu ya manufaa yake. Kwanza kabisa, wananchi wanaotambua vyema mfumo wa kupata haki zao ni tofauti na wale wasioujua kabisa. Wasiojua ni rahisi kuonewa au kunyimwa haki zao wakati wanaojua watadai na kupata haki zao. Pili, Mahakama zipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kwamba wananchi ndiyo wadau wakubwa na walengwa. Hivyo basi, lazima wakielewe vyema chombo chao hiki, wawe na imani nacho kuwa kipo kwa ajili yao na waamini kwamba wakifika mbele yake watapata haki wanayostahili.
  Jambo la tatu, ni kuwa itanipunguzia taabu ninayoipata ya kuwaambia watu kuwa jambo lililoamuliwa Mahakamani, Rais hana mamlaka nalo. Mara kadhaa, watu huja kwangu kunilalamikia kuwa hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama. Ninapowajibu kuwa lililoamuliwa na Mahakama sina uwezo wa kulitengua hawaamini, wananishangaa na kuona kama vile ninakwepa wajibu wangu. Naamini elimu kuhusu Mahakama ikielezwa na kueleweka vizuri itasaidia wananchi kutambua mgawanyo wa madaraka ipasavyo.
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Katika hotuba yako umeeleza kwa ufasaha mafanikio makubwa ambayo Mahakama ya Tanzania imepata na changamoto zilizopo ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi. Nimekuelewa vizuri na bila ya shaka wenzangu katika “bureaucracy” nao wameelewa, hasa msisitizo wako wa kutaka changamoto zishughulikiwe kwa ukamilifu ili ufanisi uongezeke katika Mahakama zetu na haki itendeke na kuonekana inatendeka kwa wakati.
  Napenda kukuhakikishia wewe, Waheshimiwa Majaji, Mahakimu na watumishi wa kada mbalimbali katika Mahakama ya Tanzania kuwa tutaendeleza juhudi tulizozianza na ambazo tunaendelea nazo hivi sasa za kuimarisha Makahama Tanzania. Dhamira yetu ya kuendelea kuujengea uwezo wa mhimili wa Mahakama iko pale pale. Hakuna mabadiliko.
  Katika miaka mitano iliyopita tumefanya mambo mengi mazuri na nawaahidi kufanya vizuri zaidi katika miaka ijayo. Tumejenga majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kagera na Shinyanga. Tutaendelea kutenga fedha ili ujenzi ufanyike katika mikoa iliyobakia hatua kwa hatua mpaka kila mkoa uwe na Mahakama Kuu yake. Sina kipingamizi kwa upande wa kuongeza Majaji ili mmalize kiu yenu. Nileteeni mapendekezo yenu nitafanya uteuzi kama nilivyofanya miaka iliyopita.
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Tutaendelea kuimarisha Mahakama za Hakimu Mkazi za Mikoa na Wilaya kwa maana ya ujenzi wa majengo na ajira ya Mahakimu. Katika miaka mitano iliyopita tulijenga jengo la Mahakama ya Mkoa wa Manyara na kufanya ukarabati mkubwa wa majengo ya Mahakama za Mikoa 5, na kuajiri Mahakimu Wakazi 256.
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Nimeona jinsi ulivyozungumza kwa uchungu kuhusu hali ya Mahakama za Mwanzo. Nakubaliana nawe kuwa kazi kubwa inahitaji kufanyika kuboresha mambo katika Mahakama hizi. Nakuhakikishia kuwa tuko tayari kufanya zaidi ya tufanyavyo sasa. Kama mjuavyo, katika miaka mitano iliyopita Mahakama za Mwanzo 34 zilijengwa. Nawaahidi kuwa tutaongeza mgao wa fedha ili kasi iongezeke ya kupunguza pengo la Mahakama 131 zilizobakia. Katika kipindi hicho Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo 394 waliajiriwa. Tutalishughulikia tatizo la kuchelewa kupata kibali cha ajira kwa Mamlaka husika.
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Napenda kuwashauri, kuwa mtengeneze mpango maalum wa uendelezaji wa Mahakama za Mwanzo nchini. Mpango huo ujumuishe ujenzi wa majengo mapya ya Mahakama, nyumba za Mahakimu na ukarabati wa majengo yaliyochakaa ili kurejesha na kudumisha heshima ya mhimili huu muhimu wa kutoa haki. Gharama za mpango huo zikishajulikana tutapanga mpango wa kibajeti na kuutekeleza.
  Bajeti na Mfuko wa Mahakama
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Ni kweli kama ulivyonukuu niliyoyasema Bungeni tarehe 18 Novemba, 2010 wakati wa kuzindua Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu dhamira ya kuongeza bajeti ya Mahakama na kuanzishwa kwa Mfuko wa Mahakama. Tumeanza utekelezaji wa yote hayo mawili. Mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Mahakama umefikia hatua ya juu kabisa. Matarajio yetu ni kupeleka muswada wa sheria utakaowezesha kuanzishwa Mfuko huo katika Bunge la Aprili, 2011 na kwamba utaanza rasmi katika mwaka wa fedha 2011/2012.
  Natumai baada ya mfuko kuanza Mahakama ya Tanzania itaanza maisha mapya kuhusu uendeshaji wa mambo yake. Kuhusu bajeti, napenda kuwahakikishia kuwa ahadi yangu iko pale pale. Tutaongeza fedha katika bajeti ya Mahakama kama tulivyofanya miaka mitano iliyopita. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa bajeti ya Mahakama tumeiongeza kutoka shilingi bilioni 36 (2006/7) hadi shilingi bilioni 63 (2010/11). Nia tunayo na tutatimiza ahadi. Kuhusu baadhi ya stahili za Majaji ambazo bado hazijatekelezwa, napenda kuwahakikishia kuwa yatatekelezwa kwa ukamilifu katika mwaka ujao wa fedha yaani 2011/2012. Mfuko wa Mahakama utakapoanza masuala ya watumishi wa kada nyingine katika Mahakama itakuwa rahisi zaidi kuboresha maslahi yao kuliko ilivyo sasa.
  Mageuzi ya Sekta ya Sheria
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Kabla ya kumaliza hotuba yangu nataka nitoe maombi mawili kwako ili kwa pamoja na wenzako myafanyie kazi. La kwanza linahusu Maboresho ya Sekta ya Sheria (Legal Sector Reform). Nawaomba muongeze kasi ya utekelezaji wa program hii muhimu. Kasi ya sasa inaelekea kuwa ndogo. Nimeambiwa inalalamikiwa hata na wabia wetu wa maendeleo. Baadhi yao wanasema wamelazimika kukaa muda mrefu au hata kuzirudisha pesa walizokuwa wamezitenga kwa ajili ya kuendeleza Mahakama nchini. Wanalaumu kasi yetu ndogo ya utekelezaji wa program kwa mambo hayo kutokea.
  Mhehimiwa Jaji Mkuu;
  Pengine baadhi ya matatizo tunayohangaika nayo sasa yasingekuwapo kwani inawezekana pesa yake ipo inasubiri kutumika au tumeikosa kutokana na kukawia kwetu. Naomba tuongeze kasi ili tunufaike na rasilimali nyingi zilizopo katika program hiyo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika Mahakama nchini.
  Maadili ya kazi
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Jambo la pili ninalopenda kuwaomba au kulizungumzia si geni. Nimeshalisemea siku za nyuma lakini kwa sababu bado linalalamikiwa sina budi kulitaja tena. Nalo linahusu uadilifu katika utoaji haki. Bado kuna hisia na madai kuhusu uadilifu mdogo wa baadhi ya watoa haki katika mfumo wa Mahakama. Kwa sababu hiyo zipo hisia na imani kuwa wasiokuwa na uwezo wa kifedha ni vigumu kupata haki katika Mahakama zetu. Uwezo wa kuondoa hisia na imani hiyo uko mikononi mwenu.
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Natambua si Majaji au Mahakimu wote ambao uadilifu wao unatiliwa shaka. Natambua pia kwamba mnafanya juhudi kubwa za kupambana na wale wasiokuwa waadilifu miongoni mwenu. Nafahamu kuwa wapo waliokwisha wajibishwa kwa ajili hiyo. Nawaomba muongeze bidii na maarifa katika mapambano haya. Kama hapana budi kubuni maarifa mapya mfanye haya. Mafanikio yenu katika mapambano hayo, yataboresha sana taswira ya Mahakama yetu mbele ya umma wa Watanzania. Ni sifa na heshima kubwa kwetu sote.
  Mwisho
  Mheshimiwa Jaji Mkuu;
  Nimesema maneno mengi kuliko nilivyokusudia, sasa naomba nimalizie kwa kurudia kukupongeza wewe binafsi, Majaji, Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo. Nafarijika kuona moyo wenu wa kujituma na dhamira yenu ya kuboresha mambo katika mfumo wa utoaji haki nchini. Nawaomba muendelee na msimamo na moyo wenu huo, nami nawaaahidi ushirikiano wangu na ule wa wenzangu Serikalini. Tuko pamoja. Na kwa pamoja tutafika tuendako. Ninawatakia kila la heri katika kuadhimisha Siku ya Sheria mwaka huu.
  Asanteni kwa kunisikiliza
   
Loading...